Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura 8—Kukua Katika Kristo na Kuwa Watu Wake Wakamilifu

  KULE kuongoka moyo ambako kunatufanya tupate kuwa watoto wa Mungu, kumenenwa katika Biblia kama ni kuzaliwa. Pengine tena kumelinganishwa na kuota kwa mbegu njema zilizopandwa na mlimaji. Vivyo hivyo wale ambao wameongoka moyo na kuanza kumfuata Kristo ni kama “watoto wachanga,” ( 1 Petro 2:2 ), tena lazima wakue hata wawe kama watu wazima katika Kristo Yesu. Kadiri zinavyotakiwa mbegu njema kwa mimea mizuri, basi pia imewapasa watu wawe na mbegu njema moyoni ili watoe matunda mema ya kiroho. Isaya asema juu yao, “Wapate kuitwa miti ya haki, miche ya BWANA, atukuzwe.” Isa. 61:3.KY 72.1

  Akili zote na ustadi wote wa binadamu haviwezi kamwe kuhuisha kitu cho chote ulimwenguni. Hata wanyama wala mimea, vyote hupata kuhuishwa na Mungu tu. Hivyo wanadamu hawapati kuzaliwa mara pili na kupata uzima mpya wa kiroho ila katika uzima utokao kwa Mungu. Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kushiriki uzima ule ambao hutolewa na Kristo.KY 72.2

  Na jinsi ilivyo katika kupata uzima, ndivyo ilivyo katika kuendelea kukua. Mimea haipati maua na matunda yake ila kwa uwezo wa Mungu tu. Yeye ndiye anayeziotesha na kukuza mbegu, “kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke,” Marko 4:28. Mimea haikui kwa kuhangaika kujitahidi yenyewe, ila kwa kuvipokea vile inavyopewa na Mungu kwa kuendesha uzima wake. Hivyo pia mtoto hawezi kuongeza urefu wake kwa kujitahidi mwenyewe. Na wewe pia, kwa kujishughulisha na kuhangaika kwako huwezi kuendelea kukua katika mambo ya kiroho. Mmea au mtoto hupata kukua wakipokea vile vinavyoweza kusaidia na kuendesha uzima wao,—hewa, na chakula. Na kwa kadiri vitu vile vinavyosaidia kwa kuendesha uzima wa sasa, ndivyo alivyo Kristo kwa wale waaminifu wake. Yeye ndiye “nuru ya milele” kwao, “ndiye jua na ngao.” (Isa. 60:19; Zab. 84:11). “Atakuwa kama umande kwa Israel.” “Atashuka kama mvua juu ya majani yaliyokatwa.” ( Hosea 15:5, Zab. 72:6 ). Yeye ndiye maji ya uzima, “mkate wa Mungu . . . ushukao kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Yoh. 4:14; 6:35,33.KY 73.1

  Yesu mwenyewe hufundisha mambo haya haya anaposema, “Kaeni ndani yangu na mimi ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu, kadhalika na ninyi, msipokaa ndani yangu . . . Maana pasipo mimi hamwezi kufanya neno.” Yoh. 15:4,5. Tawi lazima lifungamane na mti wenyewe ili lipate kukua na kuzaa matunda; basi, wewe pia imekulazimu kumtegemea Kristo ili upate kuishi maisha safi. Pasipo yeye huna uzima kabisa. Peke yako huwezikuyakinga majaribu, wala kukua kwa namna ya kiroho na kuwa mtu mwenye usafi. Unapokaa ndani yake utasitawi. Kama unaishi kwake, huwezi kunyauka wala kutozaa matunda. Bali utakuwa kama mti uliopandwa mtoni penye maji.KY 73.2

  Wengi hudhani kwamba ni wajibu wao kufanya sehemu ya kazi ile wenyewe. Wamemtumainia Kristo kwa kusamehewa dhambi, lakini sasa wanaona ya kwamba ni heri wajitahidi wenyewe ili waishi maisha yaliyo sawa. Kujitahidi hivyo hakutafaulu kamwe. Yesu asema, “Pasipo mimi hamwezi kufanya neno.” Tena ni kwa njia ya kushiriki naye na kuongea naye, kwa kukaa ndani yake kila siku saa zote, tunavyopata kukua kwa namna ya kiroho. Yeye si mwanzo tu wa imani yetu, ila mwisho wake pia; yaani, imetupasa kumtumainia Kristo tangu mwanzo mpaka mwisho. Imetupasa ili Kristo akae nasi, siyo tu kwa siku zile tuanzapo kumjua na siku za mwisho wa maisha yetu, ilakini kwa mwenendo wetu wote katika maisha yetu yote. Daudi alisema, “Nimeweka BWANA siku zote mbele yangu: kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika.” Zab. 16: 8.KY 74.1

  Pengine unauliza, Nawezaje kukaa ndani ya Kristo?” Kama vile ulivyompokea moyoni mara ya kwanza. “Kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye.” “Mwenye haki ataishi kwa imani.” Wakol. 2:6; Waeb. 10:38. Ulijitoa kwa Mungu kuwa mtu wake kabisa, kumtii na kumtumikia tena ulimtumaini Kristo kama Mwokozi wako. Wewe mwenyewe hukuweza kujiondolea dhambi zako na kugeuza moyo wako; lakini ulipokuwa umejitoa kuwa wa Mungu, ndipo uliposadiki kama Mungu ndiye aliyekutendea haya yote kwa ajili ya Kristo. Kwa njia ya kumwamini Kristo, ulikuwa wake; tena kwa kumwamini hivyo utazidi kukua naye—kwa kujitoa na kumpokea. Lazima ujitoe kwake kabisa,—moyo wako, nia yako, na utumishi wako; jitoe kwake na kuzishika amri zake na matakwa yake yote. Hivyo pia imekupasa kuvipokea vyote vinavyotoka kwa Kristo, ili akuwezeshe kumtii sawa sawa; umkubali Kristo mwenye mibaraka yote akae moyoni mwako, awe uwezo wako, na haki yako, na msaidizi wako daima.KY 75.1

  Jitoe kwake Mungu kila asubuhi, kabla hujafanya kitu cho chote. Omba hivi: “Bwana wangu, unichukue, niwe wako kamili. Nia yangu na maazimio yangu yote nayaweka mbele yako. Unitumie leo, niwe mtumishi wako. Ukae nami ili kazi yangu yote itendeke kwa uwezo.” Hili ni jambo lipasalo kwa kila asubuhi, kujitoa kuwa wa Mungu kwa siku ile. Makusudi yote na miradi yako yote uweke mbele yake ili kuyafanya au kutofaya kwajinsi atakavyokuonyesha. Hivyo ndivyo maisha yako yatakavyokuwa mkononi mwa Mungu kila siku, na maisha yako yatazidi kuwa kwa mfano wa Kristo.KY 75.2

  Kukaa ndani ya Kristo ni kukaa raha mustarehe moyoni, na kutulizwa roho. Matumaini yako si juu yako mwenyewe, ila kwa Kristo. Udhaifu wako umefungamana na ujinga wako na kutojua kwako hufungamana na akili zake, na nguvu zake, uhafifu wako umefungamana na uwezo wake. Hivyo haifai kujiangalia nafsi na kujiwazia sana; yapasa kumwangalia Kristo tu, na kufikiri sana juu ya upendo wake na sifa yake jinsi ilivyo njema na timilifu. Jinsi Kristo alivyojinyima, na udhilifu wake jinsi alivyoaibishwa, jinsi alivyo safi na mtakatifu, upendo wake usio na kifani,—hayo ndiyo mambo vafaayo kufikiriwa moyoni. Kwa njia ya kumpenda Yesu, kumfuatisha kwa namna ya matendo yake na tabia zake, kumtegemea na kumtumainia kabisa, utapata kugeuka kuwa katika mfano wake.KY 76.1

  Yesu asema, “Kaeni ndani yangu.” Maneno haya yatufikirisha juu ya kukaa mustarehe na imara, na kuwa na matumaini. Asema tena, “Njooni kwangu, nami nitawapumzisha.” Mattayo 11:28,29. Mtunga Zaburi alisema hivi: “Umnyamalie BWANA, ukamngoje.” Zab. 37:7. Na Isaya pia hutuambia, “Kwa kunyamaza na kutumaini zitakuwa nguvu zenu.” Isaya. 30:15. Kustarehe huku hakupatikani kwa kukaa bure katika hali ya kutofanya kazi; kwa kuwa katika maneno yale ya Mwokozi wetu, ahadi ya kupata raha imeungamana na wito wa kufanya kazi. “Jitieni nira yangu, . . . nanyi mtapata raha.” Mattayo 11:29. Yule anayemtegemea Kristo zaidi na kukaa raha kwake moyoni, ndiye atakayekuwa mtu wa moyo na juhudi kwa kumtumikia Mungu.KY 77.1

  Kama mtu anajifikiria nafsi na kujipendeza mwenyewe tu, roho yake hugeuka na kutoka kwa Kristo ambaye ni uwezo na uzima wake. Kwa hivyo Shetani huwa anafanya bidii kuvuta watu na kuwapotosha, ili kuwazuia wasimshiriki Kristo. Anasa za dunia, fadhaa na mashaka, na ama huzuni, makosa ya wengine, makosa na upungufu wako mwenyewe—Shetani hutumia hayo yote kwa kupotosha fikara za watu. Tujiangalie tusidanganywe na hila zake. Wengi wanaotaka kufanya yapasayo na kuishi maisha safi machoni pa Mungu, mara nyingi huvutwa kwa Shetani katika kufikiri sana juu ya makosa yao na udhaifu wao mpaka wamejitenga mbali na Kristo. Tusifikiri nafsi zetu sana, na kuhangaika na mashaka moyoni kama tutaokoka au sivyo. Mambo kama hayo hugeuza moyo kutoka kwa Kristo aliye asili ya nguvu zetu. Weka roho yako mkononi mwa Mungu kama amana, na kumtumainia. Mazungumzo yako na fikara zako ziwe juu ya Yesu. Usiwe na shaka wala hofu moyoni. Serna kama alivyosema mtume Paulo: “Ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu aliyenipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Wagal. 2:20. Ukae na kustarehe kwa Mungu, ukasadiki kwamba aweza kukilinda kile ulichokiweka amana kwake. Kama unajiweka mkononi mwake, atakuwezesha kushinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyekupenda. ( Soma Warumi 8:37).KY 77.2

  Kristo alipoutwaa mwili wa kibinadamu, alijifungia mioyo ya wanadamu kwake kwa upendo wake, na kufungamana huku hakuwezi kuharibika ila kwa hiari ya mwanadamu mwenyewe. Shetani hufanya bidii siku zote kuvuta roho zetu na kutushawishi ili tujitenge mbali na Kristo. Kwa hivyo imetupasa kujilinda, na kuomba kwa bidii ili tusishawishiwe na jambo lo lote na kuchagua kutawaliwa na Shetani. Tumkazie Kristo macho yetu, yeye awezaye kutulinda. Tukimtazama Yesu, tutakuwa salama; wala hakuna awezaye kutupokonya katika mkono wake. Tukimwangalia Yesu na utukufu wake daima, “tunabadilishwa na kufananishwa na mfano huo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana aliye Roho.” 2 Wakor. 3:18.KY 78.1

  Hivyo ndivyo wanafunzi wake wa zamani walivyopata kufanana naye. Walikuwa naye wakafundishwa kwake. Wakamwangalia, kama watumishi wanavyomwangalia bwana wao, ili wapate kujua yaliyo wajibu wao. Walikuwa wanadamu wenye “tabia moja na sisi.” Yak. 5:17. Wakawa wakishindana na maovu sawa na sisi. Iliwapasa kusaidiwa kama sisi, ili wapate kuishi maisha yaliyo safi na matakatifu.KY 79.1

  Na hata Yohana, mwanafunzi mpendwa wa Yesu, aliyefanana naye zaidi ya wengine, hakuwa na sifa njema kwa desturi. Alikuwa mtu wa kujitokeza mbele na kutaka makuu. Naye alipozidi kufahamu namna ya sifa ya Yesu jinsi ilivyo bora, alizidi kuona upungufu wake mwenyewe na kushushwa moyo. Siku kwa siku moyo wake ukazidi kuvutwa kwa Yesu Kristo, na kujisahau nafsi yake mwenyewe. Moyo wake ulitengenezwa kuwa mpya kwa Roho Mtakatifu, na hata tabia zake hasa ziligeuka kufanana na Kristo. Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa kila ashirikianaye naYesu. Kristo akaapo ndani ya moyo, na kuutawala, ndipo yule mwanadamu anapogeuzwa tabia zake hasa; sasa fikara zake na tamaa zake ni juu ya Mungu na mambo ya mbinguni.KY 79.2

  Siku ya kupaa kwake mbinguni, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata mwisho wa dunia.” Mattayo 28:20. Akapaa mbinguni na umbo la kibinadamu. Walijua ya kwamba alikwenda kuwaandalia makao, na kurudi tena baadaye, kuwapeleka kwake alipo.KY 80.1

  Walipokutana walikumbuka ahadi yake jinsi alivyosema, “Mkimwomba Baba neno kwa jina langu atawapeni. Mpaka leo hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, na mtapata, furaha yenu iwe timilifu.” Yoh. 16:23,24. Pia walitumaini ya kwamba “Kristo ndiye aliyekufa, naam, na zaidi ya haya, amefufuka, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu, tena ndiye anayetuombea.” Warumi 8:34. Na siku ya Pentekote wakapata kujazwa Roho Mtakatifu, yule Mfariji ambaye Kristo ailsema juu yake, “Naye atakaa ndani yenu.” Alisema pia, “Yawafaa ninyi niondoke; kwa maana nisipoondoka, Mfariji hatakuja kwenu; bali nikienda zangu, nitampeleka kwenu.” Yoh. 14:17; 16:7. Tangu siku hiyo, kwa njia ya Roho Mtakatifu, Kristo amekuwa anaweza kukaa mioyoni mwa watu wake siku zote, Sasa waweza kumshiriki Kristo zaidi kuliko walivyomshiriki siku zile alipokuwa nao katika umbo la kibinadamu. Upendo na uwezo wa Kristo vikaonekana kwao, hata wengine walipotambua hivyo, “wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.” Matendo 4:13.KY 80.2

  Kwa kadiri Kristo alivyowasaidia wanafunzi wake wa zamani, ndivyo apendavyo kuwasaidia watu wake wa sasa; kwa kuwa katika kuomba kwake alisem. “Wala si hao tu ninaowaombea, bali na wao watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.” Yoh. 17:20.KY 81.1

  Yesu alituombea sisi, ili tuwe katika umoja ndani yake, kama Yeye na Baba yake walivyo katika umoja. Huo ni umoja wa namna gani! Mwokozi alisema juu yake mwenyewe, “Mwana hawezi kutenda neno kwa nafsi yake, ila lile amwonalo Baba analitenda;” akasema tena, “Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake.” Yoh. 5:19; 14:10. Ikiwa Kristo anakaa mioyoni mwetu, atatenda kazi yake ndani yetu, ili kutaka kwetu na kutenda kwetu kupatane na kusudi lake jema.Wafil. 2:13. Tutafanya kama alivyofanya yeye; tutakuwa na nia ndani yetu iliyokuwamo ndani yake; hivyo kwa kumpenda Yesu na kukaa ndani yake, tutakua “mpaka tumfikie yeye katika yote, aliye kichwa, ndiye Kristo. Waef. 4:15.KY 81.2

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents