Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura 11—Kuomba ni Faradhi Yetu

  MUNGU hutumia njia nyingi kwa kusema nasi, yaani kwa viumbe vyake, kwa kuwafunulia wanadamu mambo yajayo, kwa maongozi yake, na kwa mvuto wa Roho yake Mtakatifu. Lakini hata njia hizi zote hazitoshi; hata na sisi pia imetupasa kumtolea Mungu yote yaliyomo mioyoni mwetu. Imetulazimu kuongea na Baba yetu aliye m binguni, ili tupate uzima na nguvu za kiroho. Na kama twataka kuongea na Mungu, sharti tuwe na mambo ya kumwambia, hasa juu ya maisha yetu.KY 98.1

  Katika kuomba tunamfunulia Mungu mioyo yetu na kuongea naye kama tunavyoongea na rafiki wa kweli. Si lazima kufanya hivyo ili kumjulisha Mungu hali yetu ilivyo, bali kuongea naye kunatuwezesha kumpokea mioyoni mwetu. Sala hazimlazimishi Mungu kushuka kwetu, bali ni sisi ambao tunainuliwa mpaka kufika kwake.KY 98.2

  Yesu alipokuwa hapa duniani, aliwafundisha wanafunzi wake kusali. Aliwaagiza waweke mbele ya Mungu upungufu wao na mahitaji yao ya kila siku, na kumtupia mashaka yao na mahangaiko yao yote. Tena kama alivyowaahidi wanafunzi wake ya kwamba maombi yao yatakubaliwa, basi ahadi ile imekuwa yetu pia; yaani anatuahidi ya kuwa sala zetu zitakubaliwa.KY 98.3

  Yesu mwenyewe, alipokaa na wanadamu, aliomba kwa kawaida. Mwokozi wetu alijishirikisha mahitaji yetu na udhaifu wetu; kwa hivi akawa mhitaji na mwombaji, akimwomba Baba yake ili apate nguvu za kufanya kazi yake na kuyashinda majaribu yatakayompata. Yeye ndiye mfano wetu katika mambo yote. Ni ndugu yetu ashirikiye udhaifu wetu, “alijaribiwa sawa sawa na sisi katika mambo yote;” lakini kwa sababu alikuwa safi bila dhambi, akayaepuka maovu nafsini mwake. Katika hali yake ya kibinadamu, kuomba kulikuwa ni faradhi yake iliyomhusu, naye tena akapata faraja na furaha katika kuongea na Baba yake. Na ikiwa Mwokozi wetu, aliye Mwana wa Mungu, aliona ya kwamba anahitaji kuomba, basi sisi, tulio wanadamu dhaifu wenye dhambi, tunahitaji zaidi kufanya bidii katika maombi ya kawaida. Baba yetu aliye mbinguni huwa anangoja kutubariki. Mungu yu tayari kusikiliza maombi ya kweli ya kila mtoto wake, walakini sisi hatuna moyo sana wa kumwambia Mungu haja zetu.KY 99.1

  Giza ya Shetani huzunguka wale wasiofanya bidii katika kuomba. Adui wao, Shetani, huwashawishi ili wafanye maovu, nao kwa sababu ya kuacha kuomba hawana nguvu za kushindana naye. Mbona watu wa Mungu hutupilia mbali faradhi yao ya kuomba, ijapokuwa kuomba ni kama ufunguo mikononi mwa waaminifu wa Mungu wa kuwafungulia msaada wote na mibaraka yote ya Mungu isiyo na kiasi. Tusipoomba siku zote na kukesha kwa uangalifu, tutajitia katika hatari ya kuwa walegevu wa mambo ya kiroho na kupotewa na njia ya haki.KY 100.1

  Kuna masharti mengine juu yetu ambayo ni wajibu wetu, ili tuweze kutumaini ya kuwa Mungu atatusikia na kutujibu maombi yetu. Shart moja ni hili; lazima tufahamu jinsi tunavyohitaji msaada wake. Ameahidi, “Nitamimina maji juu yake mwenye kiu, na mito juu ya pakavu.” Isa. 44:3. Wale wenye njaa na kiu ya haki, wamtakao Mungu sana, watashiba. Lakini baraka za Mungu haziwezi kupatikana ila kwanza moyo uwe umefunguliwa na Roho Mtakatifu kuingia. Bwana wetu hujua haja zetu, lakini imetupasa kutambua haja zetu sisi wenyewe na kumwomba Mungu mambo hayo. Asema, “Ombeni na mtapewa.” Mattayo 7:7. Tena “Yeye asiyemwachilia Mwana wake yeye, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. atakosaje kutukarimia na vitu vyote pamoja naye?” Warumi 8:32.KY 100.2

  Tukiwa tunaangalia maovu moyoni na kuyashikilia, Mungu hawezi kusikia maombi yetu; lakini mwenye kutubia kosa lake, maombi yake yanakubaliwa mara moja. Hatuwezi sisi kujistahilisha machoni pa Mungu kwa matendo yetu mema; ustahilifu wa Yesu ndio utakaotuokoa, na damu yake ndiyo itakayotutakasa; hata hivyo kuna masharti juu yetu pia ili tukubaliwe na Mungu.KY 101.1

  Sharti jingine juu yetu ni kuwa na imani. “Pasipo imani haiwezekani kumpendeza (Mungu): kwa maana mtu ampendezaye Mungu lazima aamini kwamba yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Waeb. 11:6. Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Marko 11:24. Je, twayasadiki maneno yake?KY 101.2

  Kama tunakosa kupata mambo yale yale tuliyoyaomba, kwa wakati ule ule tuombao, hata hivyo tukubali ya kwamba Mungu hutusikia, tena atatujibu maombi yetu. Kwa ajili ya ujinga wetu, pengine twamwuliza Mungu mambo yasiyotufaa, naye Baba yetu wa mbinguni hutujibu na kutupa mambo yale yanayokuwa bora kwetu,—ambayo sisi wenyewe tungeyataka kama tungeweza kuona mambo yote jinsi yalivyo kama Mungu aonavyo. Hata kama inaonekana kwamba maombi yetu hayajibiwi, tutazidi kuendelea kutumaini ahadi yake; kwa kuwa bila shaka atatujibu baadaye, nasi, tutapata mbaraka ule ule unaotupasa. Lakini kusema ya kwamba Mungu hana budi kutujibu maombi tunayoomba na kutupa sisi yale yale tunayoyataka,—ni kama kujidai bila haki na kumfanyia Mungu kiburi. Mungu ni mwenye busara asiyeweza kufanya kosa, tena yu mwema; kwa hivyo hawanyimi waaminifu wake jambo jema lo lote. Ni heri tutegemee ahadi yake ya kweli, “Ombeni na mtapewa.”KY 101.3

  Tunapomwendea Mungu na kumwomba msamaha na mbaraka wake, imetupasa kuwa na moyo wa upendo na kusamehe wengine. Twawezaje kuomba hivi, “Utusamehe makosa yetu, kama sisi tunavyowasamehe waliotukosea.” Na sisi katika roho zetu tungali hatujakubali kuwasamehe wengine? Tukitumaini kujibiwa maombi yetu, sharti tuwe na roho ya kuwasamehe wengine kama vile sisi tunavyotarajia kusamehewa.KY 102.1

  Kudumu katika kuomba ni sharti jingine juu ya kujibiwa maombi. Kama tunataka kuongeza imani na kuwa watu wazima katika Kristo, imetupasa kuomba siku zote; “katika kusali, mkidumu;” “dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani.” Warumi 12:12; Wakol. 4:2. Petro awausia Wakristo, “Mwe na akili, mkakeshe katika sala.” 1 Petro 4:7. Mtume Paulo awaagiza hivi, “Katika kila neno kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru, haja zenu zijulike kwa Mungu.” Wafil. 4:6. Na Yuda pia asema, “Ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu, na kuomba katika Roho Mtakatifu, jilindeni katika upendo wa Mungu.” Yuda 20, 21. Tukidumu katika kuomba, roho zetu zitafungamana kuwa moja na Mungu, ili tupate uzima utokao kwake; na maisha yetu yatakuwa safi machoni pake.KY 102.2

  Sharti tufanye bidii katika kuomba; tusikubali kitu cho chote kutuzuia kuomba. Shika kila nafasi ya kwenda mahali ambapo watu huzoea kuomba. Wale watakao kushirikiana na Mungu kweli, wataonekana kila mara kwenye mkutano wa kusali; watakuwa waaminifu katika kufanya iliyo wajibu wao, pia watakaza mioyo yao kupata msaada wote wa Mungu unaowahusu.KY 103.1

  Sharti tuombe pamoja na watu wa nyumbani; na zaidi ya yote tusiwe wavivu katika kuomba faraghani peke yetu, maana kufanya hivyo ndio asili ya uzima wa roho. Kusali hadhara ya watu peke yake hakutoshi. Yatupasa kumfunulia Mungu mioyo yetu katika faragha, ambapo maombi yetu yatasikiwa na Mungu bila shaka; maana hapo tuna nafasi kumwonyesha mambo yetu yote. Katika sala ya upweke roho zetu hupata nguvu ya kustahimili katika kushindana na Shetani. Mungu ndiye nguvu zetu.KY 103.2

  Omba faraghani; tena katika kufanya kazi yako, umwinulie Mungu moyo wako. Hivyo ndivyo Enok alivyopata kuendelea pamoja na Mungu. Shetani hawezi kamwe kumshinda yule ambaye moyo wake humtegemea Mungu hivi.KY 104.1

  Hakuna wakati wala mahali pasipofaa kumwombea Mungu. Hakuna kinachoweza kutuzuia tusimwinulie mioyo yetu katika kusali. Kati ya watu njiani, hata katika kufanya kazi yetu, twaweza kumwomba Mungu msaada wake na uongozi wake, kama alivyofanya Nehemia alipomtolea mfalme Artashashta haja yake. Ni heri tumkaribishe Yesu aje akae mioyoni mwetu daima. Wale ambao mioyo yao i wazi kwa kupata msaada na mbaraka wa Mungu, hao wamo ulimwenguni kweli, lakini si watu wa ulimwengu kwa sababu hawapendi kufuata mambo na anasa za dunia. Hao nao hupatana na mambo ya mbinguni na kushirikiana na Mungu.KY 104.2

  Mwonyeshe Mungu mahitaji yako, furaha yako, uzito wako, mashaka yako na hofu zako. Huwezi kumwudhi Mungu wala kumchosha. Yeye ambaye huhesabu nywele za kichwa chako, hawezi kuwa na kutojali kwa mahitaji ya watoto wake. “Bwana ni mwenye rehema nyingi, mwenye huruma.” Yak. 5:11. Moyo wake wa upendo huingiwa na huruma kwa ajili ya huzuni na uzito wetu. Mwambie mambo yote yanayofadhaisha moyo. Hakuna msiba uwezao kumpata hata mtoto wake aliye mdogo, wala jambo linalomhangaisha au kumfurahisha, wala hakuna maombi yatokayo moyoni mwa mmojawapo wa watu wake, bila Baba yetu aliye mbinguni kuyaona yote na kusikia mara moja. Huyaangalia na kuyajali mambo yote yanayohusika na watu wake. “Huwaponya waliopondeka moyo, huziganga jeraha zao.” Zab. 147:3. Mungu humfikiria na kumwangalia kila mtu kana kwamba hakuna mtu mwingine wa kumshughulikia ila yeye tu ambaye Mwana wake Mpendwa alikufa kwa ajili yake.KY 104.3

  Yesu alisema, “Mtaomba kwa jina langu: wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea Baba: kwa maana Baba mwenyewe awapenda ninyi.” Yoh. 16:26, 27. “Mimi niliyewachagua ninyi, . . . ili lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu, awapeni.” Yoh. 15:16. Na kuomba kwa jina la Yesu, maana yake siyo kulitaja tu jina lake katika mwanzo na mwisho wa sala. Maana yake ni hivi: katika kuomba kwetu tuwe na nia na roho ndani yetu iliyokuwamo ndani ya Yesu na kuziamini ahadi zake, kutegemea neema yake, na kutenda matendo ya namna yake.KY 105.1

  Maisha yetu lazima kufanana na maisha ya Kristo, kwa kuomba na kufanya kazi pia. Yeye aombaye tu kila mara bila kufanya kazi yo yote, hatimaye maombi yake yatakuwa yasiyo na maana. Wale wasiomtumikia Yesu aliyewatumikia wao sana, hawana mambo yafaayo kuombwa, wala hawana sababu ya kusali. Watu kama hao hujifikiria nafsi zao wenyewe tu. Hawawezi kuwaombea wengine na kufikiri mahitaji yao, wala kuendesha ufalme wa Kristo na kupata nguvu za kumtendea kazi yake ya Injili.KY 105.2

  Tunaona hasara tukikosa kushirikiana kwa kuimarishiana katika kumtumikia Mungu. Katika kushirikiana na kuongea kwetu sisi Wakristo twapata upungufu mkuwa sana kwa ajili ya kutokuwa na huruma sisi kwa sisi kama inavyotupasa. Lakini tukiandamana na watu na kufanya urafiki wa kweli nao, na kujua mambo yao, tunapata kuwahurumia wengine katika haja zao na misiba yao; pia ni njia ya kusitawisha mambo ya kiroho na kupata nguvu sisi wenyewe kwa kumtumikia Mungu.KY 106.1

  Kama Wakristo wangekuwa wanashirikiana sawa sawa, na kuongea juu ya upendo wa Mungu na mambo yanayohusiana na ukombozi, mioyo yao wenyewe ingeburundika, pia wangewaburudisha wengine mioyo yao. Kama tungezidi kumfikiria Yesu na kuongea juu yake, na kutojifikiria sana nafsi zetu, Yesu angezidi kuwapo pamoja nasi.KY 106.2

  Kama tungemwaza Mungu kila mara kama vile Mungu anavyotuonyesha uangalifu wake kwetu, angekuwa katika fikara zetu milele. Twazoea kuongea juu ya mambo ya dunia hii kwa kuwa tunahusika nayo na kupendezwa nayo. Twaongea juu ya rafiki zetu kwa sababu twawapenda. Tunafikiri sana juu ya mambo ya maisha ya kila siku, kama ni ya furaha au ya huzuni. Lakini imekuwa wajibu wetu kumpenda Mungu zaidi, kwa kuwa ametufanyia mema mno; ingefaa kuwa desturi na kawaida yetu kumfikiria Mungu zaidi ya wengine wote, na kuongea juu ya wema wake na uwezo wake.KY 106.3

  Ni wajibu wetu kumshukuru Mungu zaidi kwa ajili ya “rehema zake na miujiza yake kwa wanadamu.” Zab. 107:8. Asili ya kumwabudu Mungu si kutaka na kupata mahitaji yetu hasa. Tusifikiri juu ya haja zetu tu, bila kufikiri mibaraka tunayoipata. Sisi hatuombi zaidi kupita kiasi, lakini tunakosa kumtolea Mungu shukrani kwa kiasi kipasacho. Twapata rehema zake daima, walakini tunamshukuru kwa machache tu katika yote ambayo ametutendea.KY 107.1

  Katika siku za zamani, Waisraeli walipokutanika katika mkutano wa dini, Mungu aliwaagiza hivi: “Ndipo mtakapokula mbele ya Bwana Mungu wenu, nanyi mtafurahia kila mtakazotia mikono, ninyi na nyumba zenu, alizokubarikia Bwana Mungu wako.” Kumbu. 12: 7. Yote yatendwayo kwa kumtukuza Mungu yafaa kutendwa kwa furaha, na shangwe, na shukrani, siyo kwa huzuni na moyo mzito.KY 107.2

  Mungu wetu ndiye Baba mwenye huruma na rehema. Imewapasa watu wake kumfurahia katika kumwabudu na kumtumikia. Yeye ambaye amewawekea watoto wake wokovu mkuu, hataki wamtumikie kama vile angalitaka msimamizi wa watumwa aliye mkali, na asiye na huruma. Mungu ndiye rafiki yao aliye bora zaidi; na wanapomwabudu naye hutumaini kuwa pamoja nao, kusudi awabariki na kuwafariji, akijaza mioyo yao furaha na upendo. Mungu ataka watoto wake waburudike moyo katika huduma yake, tena wasione kazi yake kuwa ni ngumu sana, bali wapate kupendezewa katika kumtumikia. Hata na wale wanaokutanika kumwabudu, Mungu hutaka wapate kufikiri juu ya uangalifu na upendo wake, ili wachangamshwe moyo katika mambo yote ya maisha yao, na kufanya yote kwa haki na uaminifu.KY 108.1

  Kristo naye amesulubiwa, na hili ni jambo la kufikiriwa sana, lipasalo kuwa jambo kubwa katika maongezi yetu. Imetupasa kukumbuka mibaraka yote tunayoipata mkononi mwa Mungu; na kama tunafahamu upendo wake mkubwa usio na kifani, basi tukubali kumwekea amana mambo yetu yote, yule aliyesulubiwa kwa ajili yetu.KY 108.2

  Huko mbinguni Mungu husujudiwa kwa nyimbo na shangwe. Nasi tunapomtolea Mungu shukrani yetu, tunamtukuza kama vile anavyotukuzwa na majeshi ya mbinguni. “Atoaye za kushukuru, ndiye anitukuzaye.” Zab. 50:23. Hivyo tufike mbele zake “kwa zaburi na tenzi na nyimbo za roho, mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; mkimshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote.” Soma Isa. 51:3; Waef 5:19.KY 109.1

  Tafuta daima utakatifu;
  Fanya urafiki na Wakristo tu;
  Nena siku zote na Bwana wako:
  Baraka uombe kwa kila jambo.

  Tafuta daima utakatifu;
  Uwe peke yako ukimwabudu;
  Ukimwangalia Mwokozi wako,
  Utabadilishwa kama alivyo.

  Tafuta daima utakatifu;
  Kiongozi wako awe Yesu tu;
  Katika furaha au huzuni
  Dumu kumafuata Yesu Mwokozi.

  Tafuta daima utakatifu;
  Umtawaze Roho moyoni mwako;
  Akikuongoza katika haki,
  Hufanywa tayari kwa kazi yake.
  KY 109.2

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents