Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura 12—Yatupasayo Kufanya Tukiwa na Mashaka Moyoni

  WATU wengi, hasa walio Wakristo wapya, siku zingine huwa na mashaka moyoni juu ya mambo mengine katika Biblia ambayo hawawezi kuyaeleza ama kuyafahamu. Naye Shetani huyatumia mambo yale kwa kuwapunguzia imani yao katika kukubali kwamba Biblia ni ufunuo wa Mungu. Wanasema, “Nawezaje kujua njia iliyo ya haki? Kama kweli Biblia ni Neno la Mungu, nawezaje kuondolewa mashaka haya moyoni, nisije nikashikwa na fadhaa?”KY 110.1

  Kila jambo atakalo Mungu tulisadiki, hakosi kutubainishia sababu ya kuwa na imani juu ya jambo lile. Jinsi Mungu mwenyewe alivyo hai, namna ya tabia zake, na ukweli wa Neno lake, mambo haya yote yamehakikishwa kwetu kwa namna nyingi. Hata hivyo Mungu haoni ni afadhali kutuondolea nafasi ya kuwa na shaka. Imetupasa kumwamini Mungu kwa vile tunavyobainishiwa mioyoni mwetu juu ya mambo yasiyoonekana, siyo kwa ajili ya mambo yaliyo dhahiri katika macho yetu ya kibinadamu.KY 110.2

  Haiyamkiniki kwa nia ya kibinadamu kufahamu kabisa namna ya tabia za Mungu wala kazi yake. “Kwa kutafuta utampata Mungu? Utampata Mwenyiezi Mungu alivyo bora? Juu kama mbingu; utafanyaje? Chini kupita ahera; utajuaje?” Ayub 11:7, 8.KY 111.1

  Mtume Paulo alisema, “Ee ajabu ya utajiri na hekima na maarifa ya Mungu; hazina hata kiasi! hukumu zake hazichunguziki, na njia zake hazitafutikani!” Warumi 11:33. Na hata “mawingu na giza yamemzunguka,” “haki na hukumu maweko ya kiti chake.” Zab. 97:2. Katika matendo yake juu yetu twaweza kufahamu makusudi yake kwa kutosha kuona upendo wake na huruma yake isiyo na kiasi, na jinsi uwezo wake ulivyo mkuu kupita cheo. Twaweza kutambua makusudi yake kwa kadiri inavyotufaa; zaidi ya hayo imetulazimu kumtawakali Mwenyiezi Mungu, ambaye moyo wake umejaa upendo.KY 111.2

  Katika Neno la Mungu, vile vile katika sifa yake, kuna mambo ya siri wasiyoweza wanadamu kuyafahamu. Jinsi dhambi ilivyoingia ulimwenguni, jinsi Kristo alivyojifanya kuwa na umbo halisi la binadamu, uzazi wa pili jinsi ulivyo, ufufuo, na mengineyo katika Biblia, ni mafumbo makubwa sana kushinda akili za kibinadamu kuyaeleza, wala kufahamu maana yake vizuri. Lakini hatuna sababu ya kuwa na shaka juu ya Neno la Mungu kwa ajili ya kutofahamu mafumbo ya uongozi wake na majaliwa yake. Hata katika mambo ya ulimwengu na viumbe vyake twaona mafumbo mengi tusiyoweza kuyafahamu. Wenye akili sana wameshindwa kueleza habari za uhai jinsi ulivyo, hata uhai wa vidudu vidogo. M.ahali pote pana maajabu tusiyoweza kuyafahamu. Kwa hivyo mbona tunastaajabu tukiambia kuwa kuna mambo ya kiroho yasiyowaza kufahamiwa na kuelezwa na binadamu? Shinda imekuwa kwa ajili ya udhaifu na akili chache za binadamu. Katika Maandiko yenyewe Mungu ametuhakikishia jinsi Maandiko haya yalivyo yake, tusione shaka moyoni juu ya Neno lake kwa sababu ya kutofahamu mafumbo yake yote.KY 111.3

  Mtume Petro amesema kwamba katika Maandiko “yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa . . . kwa upotevu wao wenyewe.” 2 Pet. 3:16. Wengine husema ya kwamba mafumbo ya Biblia ni sababu ya kutosadiki maneno yake: lakini kwa kweli mafumbo haya ni ushahidi mkuu kuwa yametoka kwa Mungu. Kama ingekuwa Biblia haina habari za Mungu ila tu mambo yawezavo kuelezwa kwa urahisi na kufahamiwa na binadamu, Biblia isingekuwa na hakika kwamba ni ya Mungu kweli.KY 112.1

  Mafundisho ya Biblia juu ya wokovu, yametolewa kwa namna ifaayo kwa mahitaji na matakwa ya moyo wa binadamu; watu wastaarabu na wenye elimu nyingi wamevutwa na uzuri wa maneno yake; na hata watu duni waweza kuelewa na kufahamu njia ya wokovu. Hata hivyo twaweza kuyasadiki hivi tu, kwa kuwa Mungu ndiye anayetujulisha mambo hayo. Mpango wa Mungu juu ya ukombozi wa wanadamu umebainishwa vizuri kwetu, ili mtu ye yote ajue la kufanya katika kutubu kwa Mungu, na kuwa na imani kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ili apate kuokoka kwa njia aliyoiweka Mungu. Walakini ndani ya mambo haya kuna mafumbo ya Mungu yasiyofunuliwa ila kwa yule anayeyachunguza kwa moyo na bidii. Na kwa jinsi anavyozidi kuyachunguza maneno ya Biblia, ndivyo anavyozidi kusadikishwa kwamba ni Neno la Mungu aliye hai.KY 113.1

  Wenye kumkana Mungu hutupilia mbali Neno lake kwa sababu hawawezi kufahamu mafumbo yake yote. Hata na wengine wanaojidai kuwa wanasadiki Biblia, huona mashaka moyoni juu ya jambo hilo. Mtume amesema, “Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Waeb. 3:12. Ni vizuri kujifunza mafundisho ya Biblia, na kuchunguza “hata mafumbo ya Mungu,” (1 Wakor. 2:10 ), kwa kadiri yana- vyofunuliwa katika Maandiko. Ingawa ni “kwa Bwana Mungu wetu yaliyo ya siri,” ni kwetu sisi “yaliyofunuliwa,” Kumbu. 29:29. Lakini ni kusudi la Shetani kuipotoa njia ya binadamu kama anataka kuyachunguza mambo. Kwa ajili ya ufundi wanaojiona kuwa nao katika kuchunguza mafundisho ya Biblia, watu wengine huwa wepesi wa kuchukizwa wasipoweza kueleza maana ya kila sehemu ya Maandiko kwa namna ya kutosheleza nafsi zao wenyewe. Ni aibu kwao kukiri ya kwamba hawayafahamu vizuri. Hawataki kumngojea Mungu hata atakapowafunulia maana ya hakika. Huona kwamba akili za kibinadamu zimetosha kuwafahamisha Maneno ya Mungu; nao wakishindwa kufanya hivi, basi huyakana kuwa si ya Mungu. Kuna maelezo na mafundisho mengi ya dini yanayodhaniwa tu ya kuwa asili yake ni maneno ya Biblia, lakini maana yake ni kinyume cha ukweli wa Biblia. Kwa ajili ya mambo hayo watu wengi hushikwa na fadhaa na kuona shaka mioyoni mwao. Lakin imekuwa hivyo si kwa ajili ya Neno la Mungu hasa, ila kwa kuwa wanadamu wamepotoa maneno yake.KY 113.2

  Kama wanadamu wangeweza kupata kufahamu jinsi Mungu alivyo hasa, pamoja na matendo yake, basi, wasingekuwa na jambo jipya la kuvumbua, wasingezidi kuelimishwa tena, wasingepata kuzidisha maendeleo yao ya kiroho. Hapo Mungu asingekuwa Mwenye enzi; tena kwa vile ambavyo binadamu angekuwa amefika mwisho wa elimu na maarifa yote, asingepata maendeleo yo yote tena. Tumshukuru Mungu kwa kuwa si hivyo. Mungu ni mewnye uwezo wote, mwenye kujua yote; “ndani yake zimo hazina zote za hekima na maarifa.” Wakol. 2:3. Maisha ya milele wanadamu watakuwa wanachunguza na kuendelea kufahamu akili za Mungu, wema wake, na enzi yake, bila mwisho.KY 114.1

  Kuna njia moja tu kwa kupata kuelimishwa na kuendelea kufahamu Neno la Mungu,— kama Roho ya Mungu inang’aa mioyoni mwetu na kutumuliki. “Mambo ya Mungu hakuna ayajuaye ila Roho ya Mungu;” “maana Roho huyachunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.” 1 Wakor. 2:11,10. Tena Mwokozi aliwaahidia wafuasi wake hivi: “Ajapo yeye, Roho ya kweli, atawaongozeni katika yote iliyo kweli; . . . atatwaa katika iliyo yangu, atawapasheni habari.” Yoh. 16:13, 14.KY 115.1

  Mungu ataka binadamu atumie akili zake. Kuchunguza na kujifunza Biblia kunaimarisha roho zetu kwa jinsi isivyowezekana katika kujifunza mambo yo yote mengine. Ili tupate Kufahamu Maandiko, na mioyo yetu isifadhaisnwe, imetupasa kuwa na imani na moyo mmoja kama watoto, tuwe tayari kufundishwa ua kumwomba Roho Mtakatifu msaada wake. Tukiona uwezo wa Mungu na akili zake jinsi vilivyo kuu zaidi pasipo kiasi, na kuelewa hali yetu ya kutoweza kufahamu namna ya utukufu wake, hapo basi imetupasa kunyenyekea; na tunapofunua katabu cha Neno lake, imetupasa kuwa na heshima na unyenyekevu moyoni kama tupo mbele yake hasa.KY 115.2

  Kuna mambo mengi ya fumbo, ambayo Mungu atawadhihirishia wale watakao kweli kuyafahamu. Lakini bila uongozi wa Roho Mtakatifu binadamu huelekea kupotoa maneno ya Biblia na kueleza maana isiyo ya kweli. Masomo mengi ya wanadamu katika Biblia yamekuwa bure bila faida. Kama kitabu cha Neno la Mungu kinafunuliwa bila heshima na maombi: mtu asipomkazia Mungu fikara zake na upendo wake na kufanya mapenzi ya Mungu, bila shaka atashikwa na fadhaa. Ndipo Shetani atayatawala mawazo yake, na kumtilia moyoni mwake maelezo ya Biblia ya yasiyo ya kweli. Kila mara wanadamu wasipopatana na Mungu katika maneno na matendo yao, ingawa ni wenye maarifa ya namna gani, bila shaka watakosa kufahamu Maandiko, tena haifai kuyaamini maelezo yao. Wengi wao walio na mashaka moyoni, asili ya kushuku kwao ni kupenda dhambi. Masharti na vizuizi vya Neno la Mungu havipendezi wenye moyo wa kujisifu; na wale wasiokubali kufanya matakwa ya Biblia yake huwa wepesi kutosadiki kuwa ni Neno la Mungu halisi. Bali, wote watakao kwa moyo kujua matakwa ya Mungu na huyafanya, hao nao watabainishiwa kuwa Biblia na Maneno ya Mungu yawezayo kuwapa hekima hata wapate wokovu.KY 116.1

  Kristo asema, “Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya elimu hii kwamba yatoka kwa Mungu.” Yoh. 7:17. Badala ya kubishana bure juu ya mambo msiyoweza kuyafahamu, ni heri mfanye kila wajibu wenu kwa vile mnavyofahamu na kuelewa nao, ndipo mtasaidiwa kuyafahamu na kuyafanya yale ambayo sasa mnayaonea mashaka.KY 117.1

  Mungu ataka tujihakikishie ukweli wa Neno lake na ahadi zake. Asema, “Onjeni mwone BWANA ndiye mwema.” Zab. 34:8. Tusitegemee neno la wengine, ila tuonje sisi wenyewe na kuona wema wake. Asema tena, “Ombeni, na mtapata,” Yoh. 16:24. Ahadi zake zitatimia. Haziwezi kuwa na upungufu. Na kwa vile tunavyomkaribia Yesu, na kufurahishwa na upendo wake, ndivyo nuru yake itakavyong’aa mioyoni mwetu, tena mashaka na giza vitaondolewa. Mtume Paulo asema ya kwamba Mungu alituokoa “na nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake.” Wakol. 1:13. Kila ambaye “amepita toka mauti hata uzima” anaweza kutia “muhuri wake kwamba Mungu ni wa kweli.” Yoh. 5:24; 3: 33. Awe- za kushuhudia, “Nimepata msaada kwake Yesu; naye ameniruzuku mahitaji yangu yote, nimeshibishwa njaa ya moyo wangu; tena sasa Biblia inakuwa kwangu ufuno wa Yesu Kristo. Waniuliza mbona namwamini Yesu?—Kwa kuwa ni Mwokozi wangu. Kwa nini nasadiki Biblia? Kwa sababu nimeona kuwa ni sauti ya Mungu moyoni mwangu.” Twaweza kuwa na ushuhuda ndani yetu kuwa neno la Biblia ni kweli, tena Kristo ni Mwana wa Mnngu. Twajua kwamba hatufuati hadithi zilizotungwa kwa werevu. 2 Petro 1:16.KY 117.2

  Petro awaamuru Wakristo walio ndugu zake, “Kaeni katika neema, na katika kumjua Bwaua wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo.” 2 Pet. 3:18. Watu wa Mungu wakikaa katika neema yake, watazidi kudhihirishiwa Neno lake. “Matembezi yao wenye haki kama nuru nyeupe, iangazayo ikizidi hata mchana utimiapo.” Methali 4:18.KY 118.1

  Kwa imani twaweza kutazama mbele hata mpaka ufalme wa Mungu, na kutumaini ahadi ya Mungu juu ya kutuzidisha akili, na jinsi uwezo wetu wote utakavyoungamana na uwezo wa Mungu. Twaweza kufurahi kwa kuwa yote ambayo sasa tumeshikwa na fadhaa nayo, hapo ndipo yatadhihirishwa kwetu; mambo yanayokuwa magumu kufahamiwa, wakati huo yataelezwa dhahiri. “Wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana jinsi ninavyojuliwa na mimi sana.” 1 Wakor 13:12.KY 118.2

  Kumtegemea Mwokozi,
  Kwangu tamu kabisa;
  Kukubali Neno lake
  Nina raha moyoni.

  Kumtegemea Mwokozi,
  Kwangu tamu kabisa;
  Kuamini damu yake
  Nimeoshwa kamili.

  Kumtegemea Mwokozi,
  Kwangu tamu kabisa;
  Kwake daima napata
  Uzima na amani.

  Nafurahi kwa sababu
  Nimekutegemea;
  Yesu, Mpendwa na Rafiki
  Uwe nami dawamu.
  KY 119.1

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents