Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    4—Matokeo Ya Uasi

    Jambo kubwa miongoni mwa mambo yaliyosababisha upotovu wa Sulemani, hata akawa mkatili vile, ni kule kushindwa kuendeleza roho ya kujikana na kujinyima.MwI 41.1

    Wakati Musa alipowaambia watu juu ya agizo la Mungu huko Sinai kwamba: “Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao,” jibu la Waisraeli liliandamana pamoja na kutoa sadaka “Wakaja kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza, na kila mtu ambaye roho yake ilimfanya kuwa apenda, nao wakaleta sadaka.” Kutoka 25:8; 35:21. Maana ujengaji wa maskani ambayo ni kubwa kiasi kile, kulitakiwa matayarisho hasa; vitu vingi sana vya thamani vilihitajiwa kwa kazi hii, lakini Bwana alikubali kupokea sadaka zilizotolewa kwa hiari tu. Bwana alisisitiza kwa Musa akisema, “Kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwa kwake sadaka yangu.” Kutoka 25:2. Roho ya kumcha Mungu na kujinyima ndiyo iliyotakiwa kwanza katika matayarisho ya maskani ya Mungu Mwenyezi.MwI 41.2

    Mwito huo huo ulitolewa tena wakati Daudi alipomkabidhi Sulemani madaraka ya kujenga hekalu Katika mkutano mkubwa Daudi aliuliza: “Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa Bwana?” 1 Mambo ya Nyakati 29:5. Mwito huu wa kujiweka wakfu na kumtumikia Bwana, ulipaswa kuwa katika nia za watu wote wanaohusika katika ujenzi wa hekalu.MwI 41.3

    Wale waliojiweka wakfu huko jangwani ili kujenga maskani, waliochaguliwa na Mungu kuwa mafundi walipewa akili na hekima ya pekee. “Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli, Angalieni, Bwana amemwita kwa jina lake Bezaleli. . . wa kabila ya Yuda; naye amemjasa roho ya Mungu katika hekima, na akili, na ujusi. Naye amemtilia moyoni mwake ili apate kufundisha, yeye na Oholiabu . . . wa kabila ya Dani. Amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi ya kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza . . . na ya mwenye kufuma nguo, ya hao wafanyao kazi yo yote. . . . Basi Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye Bwana amemtia akili na hekima.” Kutoka 35:30-35; 36:1. Ujuzi wa mbinguni ukashirikiana na watenda kazi ambao wamechaguliwa na Mungu mwenyewe.MwI 42.1

    Wazao wa mafundi hao waliurithi ujuzi huo wa wazee wao kwa sehemu kubwa. Kwa muda watu hawa wa uzao wa Yuda na Dani waliendelea katika hali ya unyofu, bila kujiinua na kujipenda nafsi zao; lakini pole pole, kwa siri sana, walianza kupotoka, kiasi cha kumwacha Mungu na kuacha kumtumikia kwa unyofu wa moyo. Walidai mishahara mikubwa kwa ajili ya ufundi wao mwingi. Mara nyingine madai yao yalikubaliwa; lakini mara nyingi sana walipata kazi kwa mataifa mengine yaliyowazunguka. Badala ya kuwa na roho nyofu za kujikana nafsi zao, kama wazee wao walivyokuwa, wakawa watamanifu, wenye kutaka kuchuma tu zaidi na zaidi. Hivyo basi wakatumia karama ya ufundi waliyopewa na Mungu kutumikia wafalme wa mataifa yasiyomjua Mungu, ili kusudi wakifu tamaa yao ya mali. Wakatumia talanta zao kwa njia isiyomtukuza Muumba wao.MwI 42.2

    Kati ya watu hao, ndimo Sulemani alijipatia mafundisho wa kusimamia ujenzi wa hekalu juu ya mlima, wa Moria. Kila sehemu inayotakiwa katika jengo hili takatifu iliandikwa barabara, na kumkabidhiwa mfalme, laiti! angemtazamia Mungu kwa imani, ili apate wasaidizi waliojiweka wakfu, ambao wamejaliwa kuwa na akili na hekima ya pekee, wapate kufanya kazi kama ilivyokusudiwa. Lakini Sulemani alipoteza nafasi hiyo ya kuonyesha imani yake kwa Mungu. Badala yake akatuma ujumbe kwa mfalme wa Tiro akisema, “Unipelekee basi mtu mstadi wa kazi ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma na ya urujuani, na nyekundu na samawi, mwenye kujua kuchora machoro, pamoja na wastadi walioko Yuda na Verusalemu. . . .”2 Mambo ya Nyakati 2:7.MwI 42.3

    Mfalme wa Wafoiniki alikubali ombi hilo, akamtumia Hiramu, “Mwana wa mwanamke wa binti za Dani, na babaye alikuwa mtu wa Tiro.” Fungu 14. Hiramu alikuwa ametokana na uzao wa umama wa Oholiabu, ambaye alipewa akili za pekee na Mungu apate kutengeneza maskani huko jangwani, zamani za miaka mamia iliyopita.MwI 43.1

    Hivyo, aliyekuwa msimamizi wa wafanya kazi wa Sulemani, alikuwa mtu aliyekuwa akifanya kazi kwa kujitumikia mwenyewe. Hakumtumikia Mungu kwa moyo wa kujinyima. Yeye alitumikia mungu wa dunia hii, yaani mali. Makusudi ya maisha yake yote yaliongozwa na kanuni za kukipenda nafsi.MwI 43.2

    Kwa ajili ya ufundi wake mkubwa, Hiramu alidai mshahara mkubwa sana. Mwishowe hali yake ya uroho wa fedha iliwaambukiza wenzake pia. Kwa vile walivyokuwa wakifanya kazi pamoja kila siku, na kulinganisha mshahara wake na mishahara yao, mwisho hata wao wakapotoka, wala hawakuihesabu kazi yao kuwa ni kazi takatifu. Roho ya kujinyima ikawatoka, na badala yake wakawa na roho ya uroho wa fedha. Matokeo yakawa kudai mishahara mikubwa, ambayo walipewa.MwI 43.3

    Hivyo basi mvuto mbaya huo ulienea katika sehemu zote za kazi ya Bwana, hata kuenea po pote katika ufalme wake. Mishahara mikubwa iliyodaiwa na kupeana, iliwafanya watu wengi waishi maisha ya anasa sana na starehe. Watu maskini walionewa na matajiri; na roho ya kujinyima ilitoweka kabisa. Hali hii ya upotovu, iliyoenea pengi sana; mtu ambaye hapo mwanzo alikuwa miongoni mwa wenye hekima ya kutisha, aliyewapita wote, na sasa amekuwa mwasi.MwI 43.4

    Tofauti kubwa kati ya roho ya watu waliotengeneza maskani jangwani na wale waliojenga hekalu la Sulemani, inatufundisha fundisho muhimu. Watu waliojenga hekalu ambao walikuwa wakitafuta faida yao wenyewe walikuwa na tabia iliyo na watu wengi leo, ambao hujipenda nafsi zao tu, wenye kutafuta vyeo na mishahara mikubwa. Roho ya kujitolea kwa hiari kufanya kazi, kama ile iliyoonekana wakati wa kutengeneza maskani, imeadimika mno sasa. Lakini roho ya namna hiyo ndiyo inayotakiwa wafuasi wa Kristo kuwa nayo. Bwana wetu ametuonyesha mfano wa jinsi iwapasavyo wanafunzi wake kufanya kazi. Kwa wale anaowaita na kusema kwamba: “Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu”, (Mathayo 4:19) hakuwaahidi mshahara wa aina yo yote kwa ajili ya kazi yao. Yawapasa kushiriki kujikana kwake na kujinyima.MwI 44.1

    Haitupasi kufanya kazi kwa ajili ya mishahara tunayopokea. Nia inayotusukuma kazini mwa Mungu isiam- batane na kitu cho chote cha kujitumikia binafsi. Kazi inayokubalika mbele za Mungu ni ile inayofanywa kwa roho ya kujitoa, bila kujifikiria binafsi. Bwana wetu amepanga kwamba, katika kumfanyia kazi, ubinafsi wote uondolewe. Pasiweko hata na uzi mmoja wa kujipenda nafsi unaochanganywa katika kazi yake. Katika kazi zetu hatuna budi kutumia werevu na akili na hekima vile ambavyo Mungu aliwataka waliotengeneza maskani ya zamani kuwa navyo. Hata hivyo katika kazi zetu zote hatuna budi kukumbuka daima kuwa huduma kuu ambayo ni maarufu sana hukubaliwa na Mungu tu, ikiwa haikufanywa kwa roho ya kujiinua, ya ubinafsi, ila ubinafsi uliwekwa kwenye madhabahu ya kuteketezea kafara.MwI 44.2

    Upotovu mwingine uliosababisha kuanguka kwa mfalme wa Israeli ni kule kushindwa na jaribu la kujitwalia utukufu ambao ni stahili ya Mungu peke yake. Tangu siku ile Sulemani alipokabidhiwa kazi ya kujenga hekalu mpaka kumalizika kwake, nia yake iliyokua dhahiri ni “kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli.” 2 Mambo ya Nyakati 6:7. Nia hii ilikubalika katika mkutano mkuu wa wana wa Israeli wakati wa kuzinduliwa kwa hekalu. Katika maombi yake, mfalme alikiri kuwa Yehova alikuwa amesema, “Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu.” 1 Wafalme 8:29.MwI 44.3

    Sehemu mojawapo miongoni mwa mambo ya maana sana Sulemani aliyotaja katika sala yake ya kuzindua hekalu, ilihusu wageni ambao watakuja kutoka nchi za mbali ili kujifunza habari za Mungu, ambaye jina lake limetukuka kati ya mataifa. Mfalme alisema, “Maana watasikia habari za jina lako kuu, na za mkono wako ulio hodari, na za mkono wako ulionyoshwa.” Badala ya wageni hao watakaokuja kuabudu Sulemani alisihi akisema: “Basi, usikie . . . ukatende kwa kadiri ya yote atakayokuomba mgeni huyo; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako.” 1 Wafalme 8:42, 23.MwI 45.1

    Mwisho wa huduma Sulemani aliwasihi watu wawe waaminifu kwa Mungu ili kusudi “Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa Bwana ndiye Mungu; hakuna mwingine.” Fungu la 60.MwI 45.2

    Mkuu zaidi ya Sulemani alikuwa yule aliyebuni hekalu, hekima ya Mungu na utukufu wake vilisimama pale dhahiri. Watu ambao hawakufahamu ukweli huu, kwamba Mungu ndiye aliyebuni jengo hili, walimsifu na kumtukuza Sulemani; lakini yeye alikataa heshima ya kuibuni na kuijenga hekalu.MwI 45.3

    Mambo yalikuwa hivyo wakati Malkia wa Sheba alipomtembelea Sulemani. Aliposikia habari ya hekima yake Pamoja na hekalu mashuhuri alilojenga, alikusudia kuja “ili amjaribu kwa maswali ya fumbo,” na kujionea mwenyewe kazi zake za ajabu Akifuatana na msafara mkubwa wa watumishi, na ngamia waliochukua “manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani”, alisafiri mpaka Yerusalemu. “Alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni.” Aliongea naye mambo ya ajabu ya viumbe; na Sulemani akamfundisha habari za Mungu aliyeumba viumbe vyote, ambaye hukaa juu sana huko mbinguni na kutawala mahali po pote. “Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asim- wambie.” 1 Wafalme 10:1-3; 2 Nyakati 9:1, 2.MwI 45.4

    “Naye Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga. . . roho yake ilizimia.” Akakiri na kusema, “Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako.” 1 Wafalme 10:4-8; 2 Mambo ya Nyakati 9:3-6.MwI 45.5

    Wakati ugeni wake ulipokwisha, Malkia wa Sheba alikuwa amefundishwa kamili na Sulemani juu ya asili ya hekima yake na ufanisi wake, hata hakuweza kujizuia, kumtukusa si mtu bali Mungu, “Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki.” 1 Wafalme 10:9. Hiyo ndiyo hali ambayo Mungu alikusudia ionyeshwe kwa watu wote. Na wakati “wafalme wote wa duniani wakamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni” (2 Mambo ya Nyakati 9:23), kwa muda fulani Sulemani alimtukuza Mungu kwa njia ya kuwaelekeza hao wote kwa Muumba wa vyote, mbingu na nchi, Mtawala Mkuu wa ulimwengu, Mwenye hekima yote.MwI 46.1

    Kama Sulemani angaliendelea katika hali hiyo ya unyenyekevu, na kuzidi kuwaelekeza watu kwa Mungu aliyemjalia hekima hiyo na ufanisi huo, wala asijivutie heshima yeye mwenyewe, habari zake zingalikuwa na umaarufu kiasi gani! Lakini, wakati kalamu ya mwandishi wa mbinguni ilipoandika mambo yake mema, iliandika pia juu ya upotovu na maanguko vake. Alipoinuliwa na kufikia kilele cha ukuu, huku akizungukwa na mafanikio ya kila namna, Sulemani alipata kizunguzungu, akatetereka na kuanguka. Akiendelea kusifiwa na watu wa dunia, pole pole, mwisho akashindwa kujizuia asijitukuze. Hekima ile aliyotunukiwa nayo ili amtukuze yeye aliyempa, ikamjaza kiburi na kutakabari. Mwishowe akawaruhusu watu wamnene kama mtu wa ajabu mno, anayestahili sifa kuu kwa ajili ya jengo mashuhuri alilolibuni na kulijenga kwa ajili ya “jina la Bwana, Mungu wa Israeli.”MwI 46.2

    Hivyo basi, hekalu la Yehova, likajulikana katika mataifa yote kuwa “hekalu la Sulemani”. Binadamu akajitwalia heshima inayomstahili “Aliye juu kuliko walio juu,” Mhubiri 5:8. Mpaka leo, hekalu ambalo Sulemani alilinena kuwa, “nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa jina lako” (2 Mambo ya Nyakati 6:33), hutajwa mara nyingi kuwa hekalu la Sulemani, wala si hekalu la Yehova.MwI 46.3

    Mtu hawezi kuonyesha upotovu zaidi kuliko kukubali watu wamsifu kwa ajili ya karama za mbinguni alizotunukiwa. Mkirsto wa kweli atamtanguliza Mungu katika mambo yote. Nia ya kutakabari haitaruhusiwa kuuzima upendo wake kwa Mungu;, daima, kwa bidii atapeleka sifa zote kwa Baba wa mbinguni. Wakati ule tunapolitukuza jina la Mungu kwa uaminifu, ndipo nguvu ya msukumo wetu huwa chini ya usimamizi wa mbinguni, na sisi huwezeshwa kuendeleza uwezo wa kiroho na akili.MwI 47.1

    Yesu ambaye ni Bwana Mungu, siku zote alilitukuza jina la Baba vake wa mbinguni. Aliwafundisha wanafunzi wake kuomba hivi: “Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe.” Mathayo 6:9. Na haikuwapasa wasahau kutaja kwamba: “Kwa kuwa wako ni . . . utukufu.” Fungu 13. Hivyo ndivyo mponyaji mkuu alivyokuwa akiyaelekeza mawazo ya makutano yam- welekee Mungu aliye asili ya nguvu zote, wala yasimwelekee yeye mwenyewe. Basi makutano walipostaajabu wakati “Walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona,“. . .hawakumtukuza yeye, bali “wakamtukuza Mungu wa Israeli.” Mathayo 15:31. Katika sala ya ajabu ambayo Kristo aliomba kabla hajasulibiwa, alisema, “Mimi nimekutukuza duniani.” Tena aliomba, “Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe.” “Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.” Yohana 17:4, 25, 26.MwI 47.2

    “Bwana asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu Ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana.” Yeremia 9:23, 24.MwI 47.3

    “Nitalisifu jina la Mungu. . . .
    Nami nitamtukuza kwa shukrani.”
    “Umestahili wewe, Bwana, . . . kuupokea utukufu na
    heshima'na uweza.”
    “Nitakusifu wewe, Bwana, Mungu wangu,
    Kwa moyo wangu wote,
    Nitalitukuza jina lako milele.”
    “Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
    Na tuliadhimishe jina lake pamoja.”
    MwI 48.1

    Zaburi 69:30; Ufunuo 4:11; Zaburi 86:12; 34:3.

    Kule kuanzisha kawaida zinazoondoa roho ya kujinyima na kuingiza roho ya choyo, ya tamaa, kuliambatana na upotovu mwingine mkubwa wa kupotosha kusudi la Mungu kwa ajili ya Israeli. Mungu alikuwa amekusudia kwamba watu wake wawe nuru ya ulimwengu na utukufu wa sheria yake udhihirishwe katika maisha yao. Kwa ajili ya kuendeleza kusudi hilo, ndiyo sababu Mungu akiwapa watu wake wateule mahali pa kufaa katika kusudi lake ya mataifa ya dunia.MwI 48.2

    Siku za utawala wa Sulemani, ufalme wa Israeli ulienea tangu Hamathi, upande wa kaskazini, mpaka Misri, upande wa kusini; na kutoka Bahari ya Kati mpaka mto wa Efrati. Kutoka katika nchi hii, njia nyingi zilitawanyika kila upande za kufanyia biashara, na misafara ya wafanyi biashara ilikuwa ikipitapita nchini daima. Hivyo, Sulemani na watu wake walipewa nafasi ya kumdhihirisha Mfalme wa Wafalme kwa watu wa mataifa yote, na kuwafundisha kumheshimu na kumtii. Elimu hii ya Mungu ilipasa itolewe kwa ulimwengu wote. Kwa njia ya kafara za kuteketezwa Kristo ainuliwe kwa watu wote wa mataifa yote, ili watakaoamini wapate kuishi.MwI 48.3

    Sulemani, ambaye amewekwa kuwa kichwa cha taifa lililoteuliwa kuwa mionzi ya nuru ya ulimwengu, alipaswa kutumia hekima aliyopewa na Mungu na uwezo wa mvuto wake kuwaletea mataifa yote habari ya Mungu wa kweli, maana hawakuwa na habari hizo. Kwa njia hiyo makutano makubwa yangaliletwa kwa Mungu na kutii sheria yake, na Waisraeli wangalilindwa na uharibifu wa matendo ya kimataifa, na Bwana wa mbingu na nchi angalitukuzwa vikubwa. Lakini Sulemani alipoteza njozi yake kuhusu kusudi hilo la Mungu. Alishindwa kutimiza wajibu wake wa kuwaonyesha wasafiri waliokuwa wakipitapita katika nchi yake, Mungu wa kweli.MwI 48.4

    Roho ya ujumbe wa Injili ambayo Mungu alikuwa amemtunukia Sulemani pamoja na Waisraeli wengine waliokuwa waaminifu, ilidhoofishwa na tamaa ya biashara, na mwisho ikatoweka kabisa. Ile nafasi Mungu aliyotoa ya kuleta watu wa mataifa karibu nao, ilitumiwa kwa ajili ya kuchuma mali na kujifaidia binafsi. Sulemani alitafuta tu kuimarisha hali yake kwa njia ya kujenga miji yenye maboma imara kwenye milango ya kuingilia kutoka nchi nyingine, ili kufanya biashara. Aliujenga tena mji wa Gezeri karibu na Yopa, ambao uko kwenye njia kati ya Misri na Syria na akajenga Bethoroni, ulio upande wa magharibi wa Yerusalemu, ambao ni ngome ya kulinda njia kuu itokayo katika nchi ya Yuda kwenda Gezeri na njia ya pwani ya bahari; akajenga Megiddo, uliopo kwenye njia kuu ya kutoka Dameski kwenda Misri, na kutoka Yerusalemu kwenda pande za kaskazini; na “Tadmori, wa nyikani” (2 Mambo ya Nyakati 8:4), kwenye njia kuu itokayo mashariki. Miji hii yote iliimarishwa sana. Biashara ya pwani ya Bahari ya Shamu ilifanikiwa na kuimarishwa kwa njia ya kuunda “merikebu huko Ezion-geberi,. . .pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu.” Wanamaji wa Tiro “pamoja na watumishi wa Sulemani,” waliviendesha vyombo hivi, “wakafika Ofiri, wakachukua toka huko dhahabu,” na “miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani.” 1 Wafalme 9:26, 28; 10:11. 2 Mambo ya Nyakati 8:18.MwI 49.1

    Hazina ya mfalme na ya watu wake wengi iliongezeka sana, ingawa ni kwa njia isiyofaa. Kwa ajili ya uroho wa mali na upofu wa watu wale waliokabidhiwa mausia ya Mungu, watu wengi, makundi kwa makundi waliopitia katika njia kuu hizo wakifanya biashara, walidumu kuwa katika hali ya kutom- tambua Mungu kwa sababu, hapakuwako na mtu wa kuwaambia habari za Mungu. Mwenendo wa Sulemani ni kinyume kabisa cha njia Kristo aliyofuata alipokuwa duniani. Mwokozi wetu ijapokuwa alikuwa na “uwezo wote,” kamwe hakuutumia kwa kujifaidi mwenyewe. Kazi yake kamilifu ya kuwahudumia wanadamu haikuharibiwa na hali mbaya ya kutamani cheo, au ukuu na utukufu wa ulimwengu huu. Kristo hakutafuta vitu hivyo. Yeye alisema, “Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake.” Mathayo 8:20. Watu ambao wameusikia mwito wa wakati huu, na kuingia kazini mwa Bwana wajifunze sana njia zake. Hakupoteza nafasi yo yote iliyopatikana, hata kama ni barabarani.MwI 49.2

    Wakati ambapo Yesu hakuwa na safari, alikaa Kaper- naumu, mji uliojulikana kuwa ni wa “kwao”. Mathayo 9:1. Mji huo ambao ulikuwa umejengwa kwenye njia kuu itokayo Dameski kwenda Yerusalemu na pwani ya Bahari ya Kati, ndipo palipokuwa kitovu cha kazi ya Yesu. Watu kutoka katika nchi mbali mbali walipitia mjini huko na kupanga humo. Hapa Yesu alikutana na watu wa mataifa yote na hali zote. Hivyo mafundisho aliyofundisha yalienezwa pande zote na wale walioyasikia, na kwa hiyo watu waliamka na kuchunguza unabii unaohusu kuja kwa Mwokozi na kazi yake. Na kwa njia hii habari njema hiyo ilienezwa ulimwenguni.MwI 50.1

    Wakati wetu huu, nafasi ya kukutana na watu wa mataifa mbali mbali na wa hali mbali mbali ni kubwa sana kuliko nafasi ya wakati wa Waisraeli. Njia za kusafiria zimeongezeka mara elfu.MwI 50.2

    Wajumbe wa Mungu Mkuu aliye juu leo, inawabidi kuchukua nafasi hizo za usafiri na kuzitumia kuenezea ujumbe huu, kama Kristo alivyofanya hapo zamani, po pote wanapokutana na wasafiri hawa. Inawapasa kupanda mbegu ya injili kama Kristo alivyopanda, huku wakificha ubinafsi katika Mungu. Yawapasa kueleza ukweli wa maandiko matakatifu, ili upate kuota mioyoni mwao, na kukua mpaka kwenye uzima wa milele.MwI 50.3

    Mafundisho tunayopata kutokana na kushindwa kwa Waisraeli kwa muda wa miaka mingi, ni ya kuogofya sana. Wafalme na raia zao waligeuka, wakaacha makusudi makuu waliyoitiwa na Mungu, wakafuatana mambo mengine. Hata hivyo, ingawa walikuwa dhaifu hivyo na kushindwa Waisraeli wa leo, wanaomwakilisha Mungu wa mbinguni ambao ndio wanaohesabika katika kanisa halisi la Kristo yawapasa kuwa hodari; maana wamekabidhiwa kazi iliyotolewa kwa wanadamu ili waimalize, na kufikia siku ya kutoa thawabu. Ingawa ni hivyo, mivuto ya hatari iliyokuwako siku za Sulemani itakuwako pia wakati huo. Majeshi ya adui wa haki yote yako, yamejiimarisha kabisa; na ni kwa nguvu ya Mungu tu, ushindi unaweza kupatikana. Mashindano yaliyo mbele yetu yanahitaji nia ya kujinyima kabisa na roho ya kujitolea, bila kujitegemea mwenyewe bali kujikabidhi na kumtegemea Mungu kamili, na kutumia kila nafasi ipatikanayo kwa hekima ili kuongoa watu. Baraka za Bwana zitaandamana na kanisa lake, kwa kadiri linavyosonga mbele katika umoja, Suku likiudhihirishia ulimwengu wenye giza uzuri wa utakatifu unaoonekana katika hali yake ya kikristo, yenye kujitolea kabisa, ambayo humtukuza Mungu peke yake wala si wanadamu, wenye nia ya kuwahudumia wote wenye haja ya kupata mibaraka iletwayo na injiliMwI 50.4

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents