Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    9—Eliya Mtishbi

    Milimani pa Gileadi, upande wa mashariki wa mto wa Yordani, aliishi huko mtu mwenye imani kuu na maombi mengi, ambaye ilimpasa kurekebisha hali ya uasi wa Israeli, wakati wa utawala wa Ahabu, jina lake Eliya Mtishbi. Hakujulikana kwa sifa yo yote, wala hakuishi katika mji wo wote maarufu, walakini aliingia katika kazi ya Mungu, akiwa na roho nyenyekevu ya kumtegemea Mungu tu, ili amfanikishe. Katika kinywa chake mlitoka neno la imani na nguvu, na alijitoa kwa kazi ya Mungu katika maisha yake yote. Kazi kuu aliyofanya ilikuwa ya matengenezo ya dini. Yeye ndiye aliyekuwa sauti iliayo nyikani, ambayo ilikemea dhambi, na kuzuia mfuriko wa maovu. Na alipotokea kwa watu kama mkemea dhambi, ujumbe wake ulileta faraja ya Gileadi kwa watu wote waliotamani kuponywa majeraha ya dhambi.MwI 89.1

    Eliya alipoona jinsi Waisraeli walivyozidi kuzama maovuni na katika ibada ya sanamu, roho yake ilisikitika mno, na akawa na uchungu mwingi. Mungu alikuwa amewatendea watu wake mambo makuu. Alikuwa amewatoa katika utumwa, “Akawapa nchi za mataifa . . . ili wazishike amri zake, na kuzitii sheria zake.” Zaburi 105:44, 45. Lakini makusudi ya mema ya Yehova juu yao yalisahauliwa kabisa. Kutokuamini kwa taifa hili teule kulikuwa kunawatenga na Mungu wao, aliye nguvu zao. Eliya alipoangalia hali hii ya uasi mkuu, alihuzunika sana, akiwa katika milima ya kwao. Katika hali hii alimsihi Mungu, awaadhibu watu hao, waliokuwa watu wake, kwa ajiii ya njia yao mbovu, ili waweze kutafakari njia zao na kuona jinsi ilivyo vibaya kujitenga na Mungu wa mbinguni. Alitamani kuwaona wakitubu na kumrudia Mungu kabla hajakasirika na kuwafutilia mbali kabisa.MwI 89.2

    Maombi ya Eliya yalijibiwa. maneno ya kusihi, kugombeza, na kuonya, ambayo yalitolewa mara kwa mara kwa Waisraeli, yalikuwa yameshindwa kuwatubisha na kuwarudisha katika njia ya Mungu. Sasa wakati umefika ambapo lazima Mungu awazungumzie kwa njia ya adhabu na hukumu. Kwa kuwa wenye kuabudu Baali walitangaza kuwa, mibaraka yote inayowajia, yaani umande wa mbinguni na mvua, havitoki kwa Mungu, ila hutoka kwa uwezo wa asili. usioonekana, kwamba mungu jua ndiye anayewapatia mafanikio yao na mavuno yaMwI 90.1

    nchi yao; hivyo laana ya Bwana ilipasa iikalie nchi na kuiharibu. Makabila maasi haya ya Israeli yalipaswa kuonyeshwa upumbavu wao wa kutumaini uwezo wa Baali, ili wapate mahitaji yao ya kila siku. Wasipomkiri Mungu kuwa ndiye awapaye vitu vyote wanavyovihitaji, na kumgeukia kabisa kwa toba halisi, umande wala tone la mvua halitaonekana katika nchi.MwI 90.2

    Eliya aliagizwa atoe ujumbe wa hukumu ya mbinguni kwa Ahabu Hakutafuta njia ya kuwa mjumbe wa Bwana; neno la Bwana lilimjia. Na yeye akiwa na wivu kwa ajili ya Bwana hakuchelewa kutii agizo la Bwana. Ingawa kufanya hivyo kulionekana kwamba kutasababisha kuuawa kwake na mfalme mwovu Ahabu. Nabii aliondoka mara moja, akasafiri mchana na usiku, mpaka akafika Samaria, pale kwenye jumba la kifalme, Eliya hakuomba ruhusa ya kuingia ndani, wala hakupoteza muda wa kujijulisha kuwa yeye ni nani. Akiwa amevaa mavazi ya kawaida tu, kama manabii wa siku hizo walivyozoea kuvaa, aliwapita walinzi ambao hawakumwangalia akasimama mbele ya mfalme aliyeshangaa kumwona hivyo.MwI 90.3

    Eliya hakuomba samaha kwa ajili ya kufika kwake ghafula bila taarifa. Mkuu kuliko mfalme wa Israeli amemwagiza kunena; na mara hiyo, akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni, akanena akisisitiza kwamba, hukumu kutoka kwa Mungu Mkuu akaaye mbinguni zitawaangukia Waisraeli. Akatangaza kwa ujasiri, akisema, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.” 1 Wafalme 17:1.MwI 92.1

    Eliya aliutoa ujumbe wake kwa ajili ya imani kamili yenye nguvu, akiliamini neno la Mungu lisiloshindwa. Kama asingekuwa na imani halisi, na kumtegemea Mungu anayemtumikia Eliya, asingeweza kamwe kutoa ujumbe wa namna hiyo mbele ya Ahabu, wala asingeweza kuonekana mbele yake. Aliposafiri kutoka kwao kwenda Samaria, Eliya alivuka vijito vingi vyenye kutiririka daima, vilima vyenye majani mabichi, misitu yenye miti mirefu, ambayo ilionekana kuwa haikauki kamwe kwa vyo vyote. Kila kitu alichoona njiani kilikuwa kizuri sana. Huenda nabii angali hakujua ni namna gani vijito hivi visivyokauka kwa vyo vyote, na vilima na mabonde ambavyo vinanawiri hivyo, vitaharibiwa na ukavu wa nchi. Lakini hata hivyo, aliamini tu neno la Bwana. Aliamini kwamba Mungu atawadhili Waisraeli hawa waasi, na kwa njia ya adhabu, watatubu na kumrudia Mungu wao. Amri ya mbinguni imetolewa tayari, nayo haishindiki; naye Eliya aliitangaza amri hiyo bila kuhofia uhai wake.MwI 92.2

    Maneno ya kutangaza hukumu ya Mungu, yalimwangukia mfalme Ahabu kama ngurumo ya radi, akatiwa bumbuazi; lakini kabla Ahabu hajazindukana katika bumbuazi hiyo, ili naye aseme neno, Eliya alikuwa ametoweka mara kama alivyokuja. Hakungoja kuona matokeo ya maneno yake yenye ujumbe mkali. Bwana alimtangulia ili kumtayarishia njia yake. Nabii aliagizwa, “Geuka. uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha kerithi kinachokabili Yordani. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko.” 1 Wafalme 17:3, 4.MwI 92.3

    Mfalme akamtafuta kwa bidii, lakini nabii hakuonekana. Malkia Yezebeli akikasirika kwa ajili ya ujumbe uliofunga hazina za mbinguni, hakupoteza wakati, ila alishauriana na manabii wa Baali, wote wakapatana kumlaani nabii Eliya na kulaani adhabu ya Mungu iliyotangazwa na Eliya. Lakini bidii yao ya kumtafuta Eliya aliyetamka maneno hayo, haikufaulu. Wala hawakuweza kuficha maneno ya hukumu yaliyotamkwa kwa ajili ya uasi wao, yasijulikane kwa wengine. Maneno ya Eliya ya kuulaani uasi wa Israeli, na kutangazwa kwa adhabu itakayowaangukia, yalienea kwa haraka sana katika nchi yote. Wengine waliogopa sana, lakini kwa ujumla, ujumbe wa mbinguni ulidhihakiwa kabisa.MwI 92.4

    Maneno ya nabii yalifanya kazi mara moja. Wale waliodhihaki ujumbe huo na kudhani kuwa hauwezi kuwa kama ulivyotangazwa, walianza kuona matokeo yake. Maana baada ya kupita miezi michache hivi, waliona nchi imeanza kukauka, kwa kuwa haik upata um ande wala mvua; mimea ikanyauka. Kadiri siku zilivyopita, ndivyo vijito vya maji ambavyo kamwe havijakauka, vilianza kupungua sana, na kukauka. Hata hivyo watu wakihimizwa na wakuu wao, waliambiwa watumaini uwezo wa Baali tu, wayatupilie mbali maneno ya Eliya. Makuhani wao waliendelea kuhubiri kwa nguvu kwamba, baraka za mvua na umande huletwa na Baali peke yake. Wakasema, Msiyaogope matisho ya Mungu wa Eliya, wala msitetemeke kwa maneno yake; maana mafanikio yetu yote, na baraka za mashambani hutokana na Baali,”MwI 93.1

    Ujumbe wa Mungu kwa Ahabu ulimpa Yezebeli na wafuasi wake wote wanaotumikia Baali na Ashtorethi, nafasi ya kupima uwezo wa miungu yao, na kuupambanisha na maneno ya Eliya. Kwa kulinganisha wingi wa manabii, Eliya alikuwa peke yake kati ya manabii mamia ya Baali na Ashtorethi. Lakini basi, ikiwa tangazo la nabii Eliya, kwamba hakutakuwa na mvua, likipinduliwa na uwezo wa Baali, mvua inyeshe na mito na vijito vya maji viendelee kama kawaida, basi, mfalme na watu wote wafuate Baali kuwa ndiye Mungu.MwI 93.2

    Makuhani wa Baali wakaendelea kuwashikilia watu katika udanganyifu kwa njia ya kutoa kafara kwa miungu na kuomba usiku na mchana ili mvua inyeshe juu ya nchi. Makuhani hao walijaribu kuipendeza miungu yao kwa kuitolea kafara kubwa kubwa, ili ifurahi na kuleta mvua. Walidumu kuomba kwa bidii kwenye madhabahu zao za miungu ili mvua inyeshe. Kila usiku, katika nchi nzima yenye dhiki, sauti za kuombea mvua zilisikika zikisihi Baali alete mvua. Lakini hakuna hata wingu lililoonekana mbinguni, ingawa kuzuia miali mikali ya jua. Hakuna hata tone la umande au la mvua lililoanguka juu ya nchi iliyokaukiana. Neno la Yehova linasimama imara bila kugeuzwa na makuhani wa BaaliMwI 93.3

    Mwaka ukapita, bila hata tone moja la mvua. Nchi ikawa kama iliyokaangwa kwa moto. Joto la jua likakaushia mbali mimea iliyobaki na ubichi. Mito na vijito vikakauka, na kilio cha makundi ya ng'ombe na kondoo waliokuwa wakizunguka huko na huko katika dhiki kuu, kilikuwa kikubwa sana. Makonde yaliyokuwa yakistawi sana hapo mwanzo, sasa yaligeuka yakafanana na jangwa lenye mchanga mtupu. Vichaka vilivyokuwa vikiabudiwa na vilivyoheshimiwa kwamba ni makao ya miungu, vilinyauka kabisa, na majani yake yakapukutika yote. Miti minene ya msituni ikawa hafifu sana, wala haikuweza kutoa kivuli. Hewa ikawa kavu sana, yenye kusonga roho: mavumbi yalikuwa mengi kiasi cha kupofusha macho na kuziba pumzi za watu. Miji na vijiji vilivyostawi sana, viligeuka kuwa mahali pa maombolezo. Dalili za njaa na kuu kwa wanadamu na wanyama zilitangaza ajali inayokuja. Njaa ya kutisha ilikuwa inakaribia zaidi na zaidi.MwI 94.1

    Walakini katika mambo haya yote, Israeli hawakutubu, wala kujifunza kitu cho chote ambacho Mungu alitaka wajifunze. Hawakufahamu kuwa yeye aliyeuumba ulimwengu, hutawala kawaida zake, nazo humtii. Wakijivunia ibada yao ya uongo, Israeli hawakuwa tayari kunyenyekea mbele za Mungu, bali walianza kutaja sababu nyingine iliyoleta hali hiyo, ili kujifariji.MwI 94.2

    Hasa Yezebeli, alikataa hata kukubali kuwa ukavu huo wa nchi ulikuwa ni adhabu ya Mungu kwa moyo mgumu wa kumchukiza Mungu, aliungana na Israeli wote kumlaani Eliya, kwamba ndiye amesababisha shida hii. Akasema, “Je, siye Eliya aliyelaumu ibada yetu? Kama akiondolewa mbali, miungu yetu itafurahi, na shida yetu itakoma.”MwI 94.3

    Ahabu akihimizwa na mkewe, malkia Yezebeli, alianzisha mpango wa utafutaji wa nabii Eliya. Alitafutwa kwa bidii kila mahali pawezapo kuwa maficho yake. Alituma watu kumtafuta katika nchi za mataifa yaliyowazunguka, wa karibu na wa mbali. Alimtafuta mtu aliyemchukia mno, na aliyemwogopa pia. Aliwaapisha mataifa hayo yote kwamba hawajui habari zo zote za nabii Eliya. Lakini utafutaji huo wote haukufaulu, ilikuwa kazi bure. Nabii alikuwa salama kutokana na ukorofi wa mfalme, ulioleta kumwagwa kwa ghadhabu ya Mungu juu ya nchi.MwI 94.4

    Yezebeli aliposhindwa kumpata Eliya, alikusudia kulipiza kisasi kwa kuwachinja manabii wote wa Bwana katika Israeli Hakuna hata mmoja atakayeachwa hai. Mwanamke huyo mwenye ghadhabu alitekeleza mpango wake kwa ukamilifu Watumishi wa Bwana Mungu walichin|wa kwa wingi sana. Hata hivyo, sio wote waliouawa. Obadia, msimamizi wa nyumba ya Ahabu, ambaye alikuwa mwaminifu kwa Mungu, “akatwaa manabii mia, akawaficha hamsini hamsini katika pango, akawalisha chakula na kuwapa maji.” 1 Wafalme 18:4. Kufanya hivyo, Obadia alihatarisha maisha yake kweli kweli.MwI 95.1

    Mwaka wa pili wa njaa ukapita, na hata sasa hakukuwa na dalili yo yote ya umande au mvua. Ukavu wa nchi na njaa vikazidi kuendelea katika ufalme wote wa Ahabu. Wazazi wa watoto walilazimika kuona watoto wao wakifa machoni mwao, maana hawana msaada wo wote. Hata hivyo Israeli hawa walifanya shingo zao ngumu, wala hawakujinyenyekeza kwa Bwana Mungu, ila tu walizidi kumlaani Eliya aliyetamka maneno yenye ole. Walionekana kutopambanua mwito wa Mungu ili watubu katika shida yao; hawakuelewa kwamba Mungu anaweza kuingilia kati na kuwaokoa wasipitie mpaka wa usamehe wa mbinguni.MwI 95.2

    Uasi wa Israeli ulikuwa wa kutisha kuliko njaa iliyowakabili. Mungu alikuwa anataka kuwatoa katika udanganyifu walimokuwa, na kuwaelekeza kwake yeye ambaye uzima wao umo mikononi mwake Alikuwa anawasaidia ili wapate imani yao ya kwanza waliyopoteza, hivyo ilipasa awaadhibu.MwI 95.3

    “Je, mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? asema Bwana Mungu; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?” “Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli? Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana Mungu; basi ghairini, mkaishi.” “Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?” Ezekieli 18:23, 31, 32; 33:11.MwI 95.4

    Mungu alikuwa ametuma wajumbe kwa Israeli, ili kuwasihi warudie uhusiano wao na Mungu. Kama wangejali ujumbe huu, na kama wangegeuka kutoka kwa Baali na kumrudia Mungu aliye hai, ujumbe wenye ole uliotolewa na Eliya usingalitolewa kamwe. Lakini maonyo ambayo yangewawia uzima harufu ya uzima, yakawa harufu ya mauti iletayo mauti kwao. Majivuno yao yamepata pigo; ghadhabu yao imechemka kuwaelekea wajumbe, na sasa wanamghadhabikia Eliya vikubwa. Kama wangebahatisha kumpata, wangempeleka kwa Yezebeli haraka sana; ni kana kwamba, kama wakimwua watapata nafuu katika dhiki yao, au maneno aliyosema yatakosa kutimia. Katika taabu yao, wao walidumu kuabudu sanamu tu. Kwa njia hiyo walikuwa wakiongeza dhambi juu ya dhambi, ambazo zimesababisha hukumu ya Mungu kuiangukia nchi.MwI 96.1

    Dawa ya Israeli waliotaabika ilikuwa moja tu, yaani kugeuka na kuacha njia za uovu zilizoleta adhabu ya Mungu juu yao. Lazima wamgeukie Mungu kwa mioyo yao yote. Walikuwa wamepewa hakikisho kamili na Mungu, kwamba: “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” 2 Mambo ya Nyakati 7:13, 14. Mungu alizuia mvua na umande katika nchi yao, ili watu wake wageuke na kuingia katika hali hii bora, yaani wakate shauri kumtafuta Mungu kwa mioyo yao yote.MwI 96.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents