Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    21—Siku Za Mwisho Wa Kazi Ya Elisha

    Tangu Elisha alipoitwa kuwa nabii katika siku za utawala wa mfalme Ahabu, aliishi na kuona mabadiliko mengi yakitokea katika Israeli. Hukumu za adhabu mbalimbali zimewaangukia Waisraeli wakati wa utawala wa Hazaeli, Mshami, ambaye alitiwa mafuta kutawala apate kuwaadhibu Waisraeli, ambao ni taifa kaidi lenye kuasi. Mpango mzito wa Yehu wa kuleta mapinduzi nchini, umewafutilia mbali watu wote wa nyumba ya Ahabu. Baada ya Yehu, Yehoahazi aliyetawala alioteza miji mingi, ambayo ilikuwa upande wa mashariki wa Yordani, iliyotekwa na Washami. Mara nyingine ilionekana kana kwamba Washami wataitawala nchi nzima ya Israeli. Lakini matengenezo yaliyoanzishwa na Eliya, na kuendelezwa na Elisha, yaliwashtua watu mara kwa mara na kuwaelekeza kwa Mungu. Madhabahu za Baali zilikuwa zimeachwa, na makusudi ya Mungu yalikuwa yanawaingia pole pole, hasa wale waliomtafuta kwa mioyo yao yote.MwI 213.1

    Upendo wa Mungu kwa watu wake wapotevu ndio uliosababisha Washami wawaadhibu. Kwa ajili ya huruma zake tu ndiyo akamwinua Yehu ili awaondolee mbali watu waovu wasiwe kikwazo kwa watu wanyofu Alimwangamiza Yezebeli, mwovu pamoja na nyumba yote ya Ahabu. Mara moja tena kwa fadhili za Mungu, manabii wa Baali na Ashtorethi waliachwa, na madhabahu zao zikabomolewa. Mungu alijua kuwa, kama mitego na majaribu vikiondolewa, baadhi ya watu wema watazitupilia mbali njia za kimizimu, na kutafuta njia za mbinguni zenye uzima, na hii ndiyo sababu aliruhusu misiba ya kila aina iwapate ili wapate kumrudia. Hukumu zake zilikuwa za huruma, na zilipowashtua na kumtafuta aliziondoa.MwI 213.2

    Wakati mashindano baina ya wema na uovu yalipokuwa yakiendelea miongoni mwa taifa hilo, na wakati shetani alipokuwa akijitahidi kukamilisha kazi yake ya kuliangamiza taifa, ambayo aliianzisha wakati wa utawala wa Ahabu na Yezebeli. Elisha aliendelea kutoa ushuhuda wake wa kweli ya Mungu. Alikabiliana na mapingamizi, lakini hakuna mtu aliyekanusha maneno yake. Aliheshimiwa na watu wote, katika ufalme mzima. Watu wengi walimjia ili kupata mashauri kwake. Wakati Yezebeli alipokuwa angali hai, Yoramu, mfalme wa Israeli alikuja kwa nabii ili kupata mashauri; na mara moja alipokuwa Dameski, alitembelewa na wajumbe kutoka kwa Benhadadi, mfale wa Shamu, waliotaka kujua kama ugonjwa uliomshika mfalme utapona au utamwua. Kwa jumla nabii alifanya kazi yake wakati wa uasi mkuu, ambapo ukweli wa mbinguni ulidharauliwa kabisa na kutojaliwa. Taifa zima lilikuwa katika uasi wa dhahiri.MwI 214.1

    Na Mungu hamtupi kamwe mtumishi wake. Wakati mmoja, hapo jeshi la Syria lilipokuwa likivamia nchi ya Israeli, mfalme wa Shamu alitaka sana kumwangamiza nabii Elisha kwa sababu ya shughuli aliyokuwa nayo ya kumwonya mfalme wa Israeli kuhusu mipango ya adui. Mfalme wa Shamu alishauriana na watu wake, akasema, “Kituo changu kitakuwapo mahali fulani.” Mpango huo ulifunuliwa kwa Elisha na Bwana, naye “akapeleka habari kwa mfalme kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili.”MwI 214.2

    “Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; aka vaita watumishi wake, akawaambia, Je! hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwetu aliye upande wa mfalme wa Israeli? Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, Yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala.”MwI 214.3

    Ili kusudi kulichukulia hatua jambo hili la nabii Elisha, mfalme wa Shamu aliamuru, akasema, “Enendeni, mkamwangalie aliko, nipate kupeleka watu, kwenda kumchukua.” Nabii alikuwa Dothani. Mfalme alipofahamu kuwa yuko Dothani, “akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, akauzingira mji ule pande zote. Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka na kwenda nje, kumbe! pana jeshi la watu, na farasi, na magari, wameuzingira mji ule.MwI 215.1

    Kwa hofu na mshangao, mtumishi wa Elisha, alimrudia na habari hizi: “Ole wetu, bwana wangu, tufanyeje?” Nabii akamjibu, “Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”MwI 215.2

    Ili kusudi mtumishi apate hakika ya mambo hayo, “Elisha akaomba, akasema, Ee, Bwana nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona, na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.”MwI 215.3

    Kati ya mtumishi wa Mungu na jeshi la Shamu lenye silaha, palikuwa na jeshi la mbinguni, yaani malaika, wakiwazunguka. Wameshuka chini kwa nguvu, si kuja kuangamiza wala kuabudiwa, bali kuzungukia na kumhudumia mtumishi wa Bwana, ambaye ni dhaifu, wala hana uwezo wa kujisaidia.MwI 215.4

    Wakati watu wa Mungu wanapofikishwa mahali pafinyu sana, na inaonekana kwamba hakuna njia ya kuponea, Bwana mwenyewe huwa tegemeo lao.MwI 215.5

    Majeshi ya Shamu yalivyokuwa yakisonga mbele bila kufahamu kuwa kuna majeshi ya mbinguni, “Elisha akamwomba Bwana, akasema, Uwapige nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha. Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria. Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha akasema, Bwana wafumbue macho watu hawa, wapate kuona Bwana akawafumbua macho, wakaona kumbe! walikua katikati ya Samaria. Naye mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee, baba yangu, niwapige? niwapige? Akajibu, Usiwapige; Je, ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa bwana wao. Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao.” Soma 2 Wafalme 6.MwI 215.6

    Baada ya jambo hili, Waisraeli walikaa kwa amani bila kupata mashambulio ya Washami, kwa muda. Lakini baadaye, katika utawala wa mfalme shujaa Hazaeli, Washami waliuzingira Samaria na kuuhusuru. Waisraeli walikuwa bado kubanwa kabisa, kama walivyobanwa wakati huu. Maovu ya baba, kwa kweli, yalikuwa yanapatilizwa kwa watoto na wajukuu. Utisho wa njaa ulimkabili mfalme wa Israeli, wakati Elisha alipotabiri juu ya ukombozi kesho yake.MwI 216.1

    Mapambazuko ya kesho hiyo yalipokaribia, “Bwana” akawasikizisha Washami sauti za magari na farasi, kama jeshi kubwa linalowajia. Wakaingiwa na hofu,” Wakaondoka, wakakimbia, kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kituo chao vile vile kama kilivyokua wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. Hawakusimama mpaka ng'ambo ya Yordani.MwI 216.2

    Usiku uliotangulia, wenye ukoma wanne waliokuwa langoni pa Samaria, ambao walishikwa na njaa kiasi cha kutojizuia tena, waliazimu kwenda katika matuo ya Washami, na kujisalimisha mikononi mwa majeshi, ili wapatiwe chakula. Walishangaa mno, walipoingia kituoni, “kumbe! hapana mtu.” Waliingia katika “hema moja bila kuzuiwa na mtu, wakala na kunywa, na kuchukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu wakaenda wakavificha. Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema, leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza.” Mara wakarudi mjini kuwaambia habari hizi njema.MwI 216.3

    Nyara zilizotekwa siku hiyo zilikuwa nyingi sana, mpaka “vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, na kipimo cha unga mzuri kwa shekeli,” kama nabii Elisha alivyotabiri jana yake. Mara moja tena jina la Mungu lilitukuzwa mbele ya mataifa sawasawa na neno la Bwana, kwa kinywa cha nabii wake katika Israeli. Soma 2 Wafalme 7:5-16.MwI 217.1

    Hivyo mtu wa Mungu aliendelea kufanya kazi mwaka kwa mwaka, akishirikiana na watu, na wakati wa hatari akisimama kando ya wafalme kama mshauri wao. Uasi wa muda mrefu, na ibada ya sanamu, vimewaletea watu misiba mingi na huzuni kuu. Giza la uasi lilikuwa bado limeenea pote katika nchi, lakini hapa na pale palikuwako watu waliosimama imara kwa Mungu, wakipinga kabisa ibada ya Baali. Jinsi Elisha alivyoendeleza kazi ya matengenezo ya dini bila kuchoka, kulipatikana watu wengi waliouvua umizimu kabisa, na kujiunga na kundi la Mungu. Kazi ya nabii ilitiwa nguvu na miujiza ya neema aliyoifanya, naye alitamani kueneza imani hii kwa watu wote. Po pote alipokwenda alikuwa mwalimu wa haki.MwI 217.2

    Kwa hali ya kibinadamu, hali ya kiroho ya Waisraeli ilionekana ya kukatisha tamaa, sawasawa na hali iliyomo ulimwenguni leo inavyowakatisha tamaa wajumbe wa Mungu. Lakini ni kanisa la Kristo ni chombo cha Mungu cha kutangazia ukweli wake ulimwenguni. Limepewa mamlaka ili kutenda kazi maalum; na kama likidumu kuwa aminifu kwa Mungu, likiitii sheria yake, uwezo wa mbinguni utakaa ndani yake. Likitimiza wajibu wake kwa uaminifu, hapatakuwako na uwezo wa aina yo yote utakaopingana nalo. Majeshi ya Shetani hayatafua dafu kwake, kama vile makapi yasivyofua dafu kwa tufani.MwI 217.3

    Mbele ya kanisa liko pambazuko lenye heri, siku tukufu, iwapo litavaa vazi la haki ya Kristo, na kuondoa uhusiano wo wote na ulimwengu.MwI 217.4

    Mungu anawaita watu wake waaminifu, wanaomwamini, wawazungumzie wasioamini kwa ushujaa na matumaini. Mgeukieni Bwana, enyi wafungwa wa tumaini. Tafuteni nguvu kutoka kwa Mungu aliye hai. Onyesheni imani halisi bila kuyumbayumba, mkikubali kumtumikia katika uwezo wake. Tukitwaa uwezo wake kwa imani, atatubadili kwa njia ya ajabu, sisi tusio na tumaini, wala uwezo wo wote, wenye hali ya kukatisha tamaa. Hayo yote yatabadilika. Atatenda hivyo kwa ajili ya utukufu wa jina lake.MwI 217.5

    Hivyo wakati wote Elisha alipokuwa akizunguka huko na huko katika nchi, alijitahidi kuendeleza shule za manabii. Po pote alipokuwa Mungu alikuwa pamoja naye, akimpa maneno ya kusema, na uwezo wa kufanya miujiza. Wakati mmoja “Wana wa manabii wakamwambia Elisha, Angalia basi, mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu. Basi twende mpaka Yordani, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili tujifanyie huko mahali pa kukaa.” 2 Wafalme 6:1, 2. Elisha alifuatana nao mpaka Yordani, ili kuwako kwake kuwatie ushujaa, na kuatolea mafundisho, hata kufanya miujiza ya kuwasisimua, katika kazi. “Mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini, akalia, akasema, Ole wangu! bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile. Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali. Akakata kijiti, akakitupa pale pale, chuma kikaelea. Akasema , Kiokote, Basi akanyosha mkono, akakitwaa.” Mafungu 5-7.MwI 218.1

    Hivyo kazi yake ilikuwa ya maana sana, kiasi cha kueneza sifa zake, hata alipokuwa katika kufa, mfalme Yoashi, mwabudu wa sanamu, ambaye hakumjali Mungu, alimkiri Elisha kwamba ni baba katika Israeli, na tena, anayo manufaa makubwa kwake kuliko majeshi ya askari yenye magari ya vita. Habari inasomwa, hivi, “Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! gari la Israeli na wapanda farasi wake! 2 Wafalme 13:14.MwI 218.2

    Kwa watu wengi wenye matatizo, Elisha aliwawia kama baba mwenye huruma Na katika kisa hiki hakumwacha mfalme kijana huyu vivi hivi, ingawa si mwaminifu, wala hakustahili kuwa mfalme, alihitaji mashauri. Kwa maandao ya Mungu, alikuwa anamsogeza kijana huyu katika nafasi nzuri ya kurekebisha mambo yake ya wakati uliopita, na kuandama njia bora ya kuuimarisha ufalme wake. Washami walikuwa wameteka sehemu yote ya mashariki ya Yordani. Lazima wafukuzwe, na kutolewa hapo. Mungu ataonyesha uwezo wake mara moja tena kwa taifa lililoasi, la Israeli.MwI 218.3

    Nabii aliyekuwa katika kufa alimwagiza mfalme: “Twaa uta na mishale.” Yoashi alitii. Nabii akasema, “Weka mkono wako katika uta.” Yoashi akaweka mkono wake juu ya uta. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya Yoashi. Kisha akasema, “Lifungue dirisha linaloelekea mashariki,” kuelekea miji ile iliyotekwa na Washami. Mfalme alipofungua dirisha, Elisha akamwambia apige mshale. Alipotupa mshale, nabii alitamka kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, “Mshale wa ukombozi wa Bwana, kutokana na Washami, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki, hata utakapowaangamiza.”MwI 219.1

    Sasa nabii aliijaribu imani ya mfalme. Akimwagiza Yoashi achukue mishale, alisema, “Piga chini.” Mfalme alipiga chini mara tatu, halafu akaacha. Elisha akasema, huku amekasirika, “Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita,” ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza, bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu.” 2 Wafalme 13:15-19.MwI 219.2

    Fundisho hili lawahusu watu wote wenye kukabidhiwa madaraka. Mungu anapofungua njia ili kazi fulani ifanyike, naye akahakikisha kwamba ataifanikisha, yule aliyekabidhiwa kazi hiyo lazima aifanye kwa nguvu zake zote, ili aikamilishe. Ule uwiano wa juhudi na uvumilivu, kufaulu hutegemea, yaani kufaulu kunategemea juhudi na kudumua kuendelea bila kuacha.MwI 219.3

    Mungu hutenda miujiza kwa watu wake tu wakati wanapofanya sehemu yao kwa bidii bila kukata tamaa na kuacha. Anawaita watu wenye kufanya kazi yake kwa nia moja, watu wajasiri wenye kupenda kuokoa watu, wenye juhudi isiyoyumbayumba. Watenda kazi wa namna hiyo hawataogopa kazi kwamba ni ngumu, wala hawataona kuwa jambo fulani la mbele ni bure, halina faida; wataendelea tu na kazi bila hofu yo yote, mpaka mambo yaliyoonekana kuwa hayawezekani, yawezekane. Hakuna kitu kitakachowazuia kufanya kazi pamoja na Mungu, hata gereza, au kifo kikiwakabili, hakiwezi kuwatisha na kuwageuza waache kusudi lao.MwI 219.4

    Kazi ya Elisha ilifungwa kwa mashauri aliyompa mfalme kijana, Yoashi. Elisha, ambaye roho ya Eliya ilimjaza alidumu kuwa mtenda kazi mwaminifu mpaka mwisho. Hakuweza kuwa kigeugeu hata kidogo, wala hakujaribu kusahau mwungano wake na Mwenyezi Mungu. Kila mara njia ilipoonekana kuwa imeziba, aliendelea mbele tu katika imani, na Mungu alimheshimu kwa kufungua njia.MwI 219.5

    Elisha hakumfuata bwana wake Eliya katika gari la moto, ila Mungu alimruhusu augue tu akiwa duniani Wakati mrefu wa ugonjwa wake na maumivu yake, imani yake ilikuwa imara naye alifarijika kwa kuongea na wajumbe wa mbinguni. Jinsi alivyoona majeshi huko Dothani yenye magari ya moto na farasi, hali kadhalika sasa anafarijika kwa wajumbe wa mbinguni, ambao ni malaika wema. Katika maisha yake yote amejizoeza kuwa na imani kuu, na kadiri alivyomjua Mungu na ahadi zake, na fadhili zake, imani yake imekomaa sana, na wakati alipokabili mauti, alikuwa tayari kupumzika kwa amani, kutokana na kazi yake. Ina thamani machoni pa Bwana, mauti ya wacha Mungu wake.” Zaburi 116:15. “Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake.” Mithali 14:32.MwI 220.1

    Elisha aliweza kusema kama Daudi katika Zaburi: “Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha.” Zaburi 49:15. Atashangilia kwa maneno haya: “Lakini mimi najua Mkombozi wangu yu hai, na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.” Ayubu 19:25. “Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, niamkapo nishibishwe kwa sura yako.” Zaburi 17.15.MwI 220.2

    Tokea wakati wa mafanikio ya Sulemani na kuendelea katika historia za watu wa Mungu tunawakuta hawa— mashujaa wa imani, watu waliokuwa imara upande wa kweli walioamini kuwa sawa; watu ambao, wakati wa mateso na hata kifo, walitoa ujumbe wa Mungu wa kuwaonya watu ambao walikuwa wakifuata tamaa zao.MwI 221.1

    Kitabu hiki, kwa miaka mingi kimekuwa kikiuzwa kuliko vingine vyote ulimwenguni, kimetafsiriwa kwa lugha nyingi. Ni imani ya watoa vitabu kwamba Mashujaa wa Imani kitawafunuliwa watu mambo mapya ya kupendeza katika wakati huu wa msukosuko wa historia, na kumwacha msomaji na mambo mengi ambayo anaweza kuyafanya yanayohusu siku zetu.MwI 221.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents