Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 15—Biblia na Mapinduzi ya Ufaransa

  Katika karne ya kumi na sita, Matengenezo yakiwasilisha Biblia iliyofunguliwa kwa watu, yalitaka kuingizwa katika nchi zote za Ulaya. Baadhi ya mataifa yaliikaribisha kwa furaha, kama mjumbe kutoka Mbinguni. Katika nchi zingine upapa ulifanikiwa kwa kiwango kikubwa kuzuia kuingia kwake; na nuru ya maarifa ya Biblia, na mivuto yake inayoinua, kwa kiwango kikubwa iliondolewa. Katika nchi moja, ingawa nuru iliingia, haikutambuliwa na giza. Kwa karne nyingi, ukweli na makosa vilishindana ili kimoja kitawale kingine. Mwishowe uovu ulishinda, na ukweli wa mbinguni ulisukumiwa nje. “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru” (Yohana 3:19). Taifa liliachwa livune matokeo ya uchaguzi wao. Kizuizi cha Roho wa Mungu kiliondolewa kwa watu kudharau karama ya neema Yake. Uovu uliruhusiwa ukomae. Na ulimwengu wote uliona tunda la kuchagua kuikataa nuru.PKSw 201.1

  Vita dhidi ya Biblia, iliyoendelezwa kwa karne nyingi katika nchi ya Ufaransa, iliishia katika matukio ya Mapinduzi. Mlipuko huo wa kutisha ulikuwa matokeo yasiyoepukika ya ukandamizaji wa Maandiko wa Rumi. (Tazama Kiambatanisho.) Uliwasilisha mfano wa wazi kuliko yote ambayo ulimwengu umewahi kushuhudia wa utendaji kazi wa sera ya upapa— kielelezo cha matokeo ambayo kwa zaidi ya miaka elfu moja ya mafundisho ya Kanisa la Rumi yamekuwa yakielekeza kwayo.PKSw 201.2

  Ukandamizaji wa Maandiko wakati wa kipindi cha utawala wa upapa ulitabiriwa na manabii; na mwandishi wa kitabu cha Ufunuo anataja pia matokeo ya kutisha ambayo yangetokea hususani katika nchi ya Ufaransa kutokana na utawala wa “mtu wa dhambi.”PKSw 201.3

  Alisema malaika wa Bwana: “Nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili. Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia.... Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua. Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulibiwa.... Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi. Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama” (Ufunuo 11:2-11).PKSw 201.4

  Vipindi ambavyo vimetajwa hapa—“miezi kumi na miwili,” na “siku elfu moja na mia mbili”—vinahusu kipindi kile kile, vyote vinawakilisha kipindi cha muda ambacho kanisa lingeteswa na Rumi. Miaka 1260 ya utawala wa upapa ilianza B.K. 538, na kiliisha mwaka 1798. (Tazama maelezo ya Kiambatanisho kwa ajili ya ukurasa wa 54.) Wakati huo jeshi la Ufaransa liliingia Rumi na kumfanya papa kuwa mfungwa, na alifia uhamishoni. Ingawa papa mpya alichaguliwa muda mfupi uliofuata, utawala wa upapa haujaweza kamwe tangu wakati huo kuwa na nguvu uliokuwa nayo kabla.PKSw 202.1

  Mateso ya kanisa hayakuendelea kipindi chote cha miaka 1260. Kwa sababu ya rehema kwa ajili ya watu Wake, Mungu aliupunguza muda wa mateso yao makali. Alipokuwa akitabiri “taabu kuu” ambayo ingelipata kanisa, Mwokozi alisema: “Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo” (Mathayo 24:22). Kutokana na nguvu ya Matengenezo mateso yalikomeshwa kabla ya mwaka 1798.PKSw 202.2

  Kuhusu mashahidi wawili nabii anaeleza zaidi: “Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi.” “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu” (Ufunuo 11:4; Zaburi 119:105). Mashaidi wawili huwakilisha Maandiko ya Agano la Kale na Agano Jipya. Yote mawili ni ushuhuda muhimu kuhusu mwanzo na uendelevu wa sheria ya Mungu. Yote mawili ni mashahidi kwa ajili ya mpango wa wokovu. Mifano, kafara, na huelekeza kwa Mwokozi anayekuja. Injili na Nyaraka za Agano Jipya huelezea kuhusu Mwokozi aliyekuja kwa namna sahihi iliyotabiriwa na mifano na unabii.PKSw 202.3

  “Watatoa unabii kwa siku elfu moja na mia mbili na sitini, wakiwa wamevaa nguo za magunia“Katika sehemu kubwa ya kipindi hiki, mashahidi wa Mungu walibaki mafichoni. Mamlaka za kipapa zilijitahidi kuwaficha watu neno la kweli, na waliweka mbele yao mashahidi wa uongo wapinge ushuhuda wao. (Tazama Kiambatisho.) Wakati Biblia ilipopigwa marufuku na mamlaka za kidini na kiraia; wakati ushuhuda wake ulipopindishwa, na kila juhudi ikafanywa ili watu na mapepo wagundue njia ya kubadilisha akili za watu dhidi yake; wakati wale waliojaribu kutangaza ukweli wake mtakatifu walipowindwa, waliposalitiwa, walipoteswa, walipotupwa katika vyumba vya magereza, walipouawa kwa ajili ya imani yao, au walipolazimishwa kukimbilia katika maficho ya milimani, na mashimo na mapango ya ardhini—hapo ndipo mashaidi waaminifu waliposhuhudia wakiwa katika nguo za magunia. Lakini waliendeleza ushuhuda wao katika kipindi chote cha miaka 1260. Katikati ya giza kuu kabisa walikuwepo watu waaminifu waliolipenda neno la Mungu na walikuwa na wivu kwa ajili ya heshima Yake. Kwa hawa watumishi waaminifu ilitolewa hekima, nguvu, na mamlaka ya kutangaza ukweli Wake katika kipindi chote cha wakati huu.PKSw 202.4

  “Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa” (Ufunuo 11:5). Watu hawawezi kukanyaga neno la Mungu bila kuadhibiwa. Maana ya onyo hili la kutisha imeelezwa katika sura ya mwisho ya kitabu cha Ufunuo: “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki” (Ufunuo 22:18, 19).PKSw 203.1

  Hayo ndiyo maonyo ambayo Mungu ameyatoa kuwalinda watu dhidi ya kugeuza kwa namna yoyote ile kile ambacho amekifunua au amekiamuru. Maonyo haya ya kutisha ni kwa ajili ya wale wote ambao kwa sababu ya mvuto wao wanawaongoza wengine kudharau sheria ya Mungu. Walitakiwa wawasaidie wale ambao wanasema kwa kirahisi - rahisi kuwa hakuna madhara yo yote kutii au kutotiii sheria ya Mungu waogope na watetemeke. Wote wanaoinua maoni yao juu ya ufunuo wa Mungu, wote ambao hubadilisha maana ya wazi ya Maandiko ili kukidhi mahitaji yao, au kwa ajili ya kufanana na ulimwengu, wanajitwika wajibu wa kutisha.PKSw 203.2

  Neno lililoandikwa, sheria ya Mungu, itapima tabia ya kila mtu na kuwahukumu wote ambao kipimo hiki kisichokosea kitawatangaza kuwa wamepungua.PKSw 203.3

  “Watakapokuwa wamemaliza [wanamaliza] ushuhuda wao.” Kipindi ambacho mashahidi wawili walitoa unabii wakiwa katika mavazi ya magunia, kiliishia mwaka 1798. Walipokuwa wanakaribia mwisho wa kazi yao mafichoni, vita ilipigwa dhidi yao na mamlaka inayowakilishwa na “mnyama atokaye katika kuzimu.” Katika mataifa mengi ya Ulaya mamlaka zilizotawala katika kanisa na serikali kwa karne nyingi ziliongozwa na Shetani kwa njia ya upapa. Lakini hapa kuna mwonekano mpya wa ufunuo wa nguvu ya kishetani.PKSw 203.4

  Ilikuwa sera ya Rumi, chini ya madai ya kuiheshimu Biblia, kuitunza ikiwa katika lugha isiyoeleweka na ikiwa imefichwa ili isionwe na watu. Chini ya utawala wake mashahidi walitoa unabii “wakiwa katika mavazi ya magunia.” Lakini mamlaka nyingine—mnyama atokaye kuzimu—ilipasa ainuke na kupigana vita vya wazi, vya kudhamiria dhidi ya neno la Mungu. “Mji mkuu” ambao kati kati yake mashahidi wawili wanauawa, na ambapo mizoga yao inalala, ni Misri “kiroho”. Kati ya mataifa yote yaliyosimuliwa katika historia ya Biblia, Misri kwa ujasiri mkubwa ilikana uwepo wa Mungu aliye hai na ilipinga amri zake. Hakuna mfalme aliyediriki kufanya uasi wa wazi na wa kiburi cha hali ya juu dhidi ya mamlaka ya Mbingu zaidi ya alivyofanya mfalme wa Misri. Wakati ujumbe ulipoletwa kwake na Musa, katika jina la Bwana, Faraoh alijibu kwa kiburi: “Bwana ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui Bwana, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao” (Kutoka 5:2). Huu ni ukanamungu, na taifa lililowakilishwa na Misri lingetoa sauti kama ile ile ya kukataa madai ya Mungu aliye hai na lingedhihirisha roho kama ile ile ya kutokuamini na ukaidi. “Mji mkuu” umelinganishwa pia, “kiroho,” na Sodoma. Ufisadi wa Sodoma katika kuvunja amri za Mungu ulionekana hasa katika uasherati na uzinzi. Na dhambi hii ilipaswa kuwa sifa kuu ya taifa ambalo lingetimiza vipengele vya andiko hili.PKSw 203.5

  Kwa mujibu wa maneno ya nabii, hivyo basi, muda mfupi kabla ya 1798 mamlaka fulani ambayo mwasisi wake ni Shetani ingeinuka na kupiga vita Biblia. Na katika nchi ambapo ushuhuda wa mashahidi wawili wa Mungu wangenyamazishwa, kungeoenekana ukanamungu wa Farao na uasherati na uzinzi wa Sodoma.PKSw 204.1

  Unabii huu umepata utimizo sahihi na wa kushangaza katika historia ya Ufaransa. Wakati wa Mapinduzi, mwaka 1793, “ulimwengu kwa mara ya kwanza ulisikia mkutano wa watu, waliozaliwa na kuelimishwa katika ustaarabu, na wakidai kuwa na haki ya kuongoza moja ya mataifa mazuri sana ya Ulaya, wakiinua sauti yao pamoja kuukataa ukweli muhimu sana ambao roho ya mwanadamu hupokea, na kukana kwa umoja wao imani na ibada ya Mungu.”—Sir Walter Scott, Life of Napoleon, vol. 1, ch. 17.” Ufaransa ni taifa pekee duniani ambalo lina rekodi iliyoandikwa na inayoendelea kuwapo, ya kwamba kama taifa iliinua mkono wake kufanya uasi wa wazi dhidi ya Mwumbaji wa Ulimwengu. Waliomkufuru Mungu ni wengi, wakanamugnu ni wengi, wamekuwepo, na wataendelea kuwepo, katika nchi ya Uingereza, Ujerumani, Uhispania, na kwingineko; lakini Ufaransa inasimama peke yake katika historia ya ulimwengu kama taifa moja pekee ambalo, kwa amri ya Bunge, lilitangaza kuwa hakuna Mungu, na ambayo raia wote wa mji mkuu, na raia walio wengi mahali pengine, wanawake kwa wanaume, walicheza na kuimba walipolipokea tangazo hilo.”—Blackwood’s Magazine, November, 1870.PKSw 204.2

  Ufaransa pia ilikuza tabia zilizoifananisha na Sodoma. Wakati wa Mapinduzi kulikuwa na mwonekana wa wazi wa anguko la kimaadili na ufisadi uliofanana na ule uliosababisha kuharibiwa kwa miji ya Sodoma na Gomora. Na mwanahistoria anawasilisha kwa pamoja ukanamungu na ufisadi wa Ufaransa, kama ulivyotolewa katika unabii: “Kwa mshikamano wa karibu sana na sheria hizi zinazoathiri dini, kulikuwa na kile kilichodhoofisha muungano wa ndoa—mshikamano mtakatifu sana ambao wanadamu wanaweza kuufanya, na ambao una uendelevu unaoimarisha sana jamii— na kuifanya ndoa kuwa mkataba tu wa kiraia wenye sura ya mpito, ambapo watu wowote wawili wanaweza kushikamana na kuachana wakati wowote kulingana na matakawa yao.... Ikiwa Shetani na malaika zake walikaa na kufikiria jinsi ya kuharibu kwa mafanikio kila kilicho cha kuheshimiwa, chenye neema, au cha kudumu katika maisha ya nyumbani, na wakati huo huo kupata uhakikisho kuwa tabia mbaya ambayo ilikuwa lengo lao kuanzisha na kuendeleza kutoka kizazi hadi kizazi, wasingeweza kugundua mbinu iliyo na uwezo mkubwa zaidi kuliko kushusha thamani ya ndoa.... Sophie Arnoult, mwigizaji mwanamke ambaye alijulikana sana kwa ajili ya maneno na misemo yake ya kuchekesha katika uigizaji wake, alielezea ndoa ya kiserikali kama ‘sakramenti ya uzinzi.'”—Scott, vol. 1, ch. 17. “Mahali ambapo pia Bwana wetu alisulibiwa.” Kipengele hiki cha unabii nacho kilitimizwa pia na Ufaransa. Hakuna nchi ambapo roho ya uadui dhidi ya Kristo imeoneshwa kwa kiwango kikubwa zaidi ya kile kilichooneshwa katika nchi ya Ufaransa. Hakuna nchi ambako ukweli ulikutana na upinzani mkali na wa kikatili zaidi ya ulivyokutana katika nchi ya Ufaransa. Katika mateso ambayo Ufaransa iliyafanya juu ya watu walioikiri injili, Ufaransa ilimsulubisha Kristo kwa kuwatesa wanafunzi Wake.PKSw 204.3

  Karne baada ya karne damu ya watakatifu ilimwagwa. Wakati Wawaldensia waliposalimisha maisha yao juu ya milima ya Piedmont “kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu Kristo,” ushuhuda kama huo kwa ajili ya ukweli ulitolewa na ndugu zao, Waalbegensia wa Ufaransa. Katika siku za Matengenezo wanafunzi wake waliuawa kwa maumivu ya kutisha. Wafalme na wasaidizi wake, wanawake na wajakazi wa nyumba ya mfalme, maamiri na makamanda wa jeshi la nchi, walilisha macho yao kwa kutazama maumivu ya mashahidi wa Yesu. Wahujenoti jasiri, wakipigania haki za msingi ambazo mioyo ya wanadamu huichukulia kuwa haki zao takatifu sana, walimwaga damu yao katika viwanja vingi vya mapambano. Waprotestanti walihesabiwa kama walihalifu, bei ilipangwa kwa ajili ya vichwa vyao, na waliwindwa kama wanyama wa porini.PKSw 205.1

  “Kanisa jangwani,” wazaliwa wachache wa Wakristo ambao walikuwa bado wapo katika nchi ya Ufaransa katika karne ya kumi na nane, wakiwa wamejificha katika milima ya kusini, bado walidumisha imani ya baba zao. Walipojaribu kukutana usiku kando kando ya mlima katika maeneo ya mbugani yaliyojificha, waliwindwa na askari wapanda farasi na kukokotwa kwenda katika utumwa wa maisha katika manchani. Watu safi, wenye tabia njema, na watu wenye akili sana wa nchi ya Ufaransa walifungwa katika minyororo, waliteswa kwa mateso ya kutisha, na walifungwa pamoja na wanyang'anyi na wauaji. (Tazama Wylie, b. 22, ch. 6.) Wengine, ambao walitendewa kwa huruma kuliko wengine, walipigwa risasi na kufa kikatili, walianguka katika magoti yao wakiomba. Mamia ya wazee, wanawake wasioweza kujilinda, na watoto wasio na hatia waliachwa wakiwa maiti ardhini katika maeneo yao ya mikutano. Katika kuzunguka katika milima au misitu, mahali walipokuwa wamezoea kukutana, halikuwa jambo la ajabu kukuta “kila baada ya hatua nne, maiti zikiwa zimetapakaa katika nyasi, na maiti zingine zikiwa zimening'inizwa juu ya miti.” Ardhi yao, ikiwa imeachwa ukiwa kwa upanga, shoka, kuni, “iligeuzwa kuwa nyika ya huzuni.” “Maovu haya yalitendwa... siyo nyakati za giza, bali katika zama za mwangaza za mfalme Louis XIV. Sayansi wakati huo ilikuwa imekua, wasomi walikuwa wengi, watumishi wa ikulu na mji mkuu walikuwa wasomi tena wenye umbuji, na kwa kiwango kikubwa maendeleo hayo yalikuwa yamekuza huruma na ukarimu.”—Ibid., b. 22, ch. 7.PKSw 205.2

  Lakini matendo mabaya kuliko yote katika orodha ya matendo mabaya ya uhalifu, yalikuwa mauji makuu yaliyotokea eneo la Mtakatifu Bartholomayo. Ulimwengu bado unakumbuka kwa hofu inayotetemesha matukio ya kutisha sana miongoni mwa matendo ya kikatili ya karne zote za kutisha, yalikuwa mauaji ya kuogofya na ya kutisha yaliyofanyikia eneo la Mtakatifu Bartholomayo. Mfalme wa Ufaransa, baada ya kushinikizwa na mapadri na maaskofu wa Kirumi, alitoa idhini kwa ajili ya kazi ya kutisha. Kengele, ilipolia usiku wa manane, ilikuwa ishara ya mauaji. Maelfu ya Waprotestanti, wakiwa wamesinzia katika nyumba zao, wakitumia heshima waliyoahidiwa na mfalme, walikokotwa nje bila onyo na kuuawa kikatili.PKSw 206.1

  Kama vile Kristo alivyokuwa kiongozi asiyeonekena wa watu Wake kutoka katika utumwa wa Misri, hali kadhalika Shetani alikuwa kiongozi asiyeonekana katika kazi hii ya kutisha ya kuzidisha idadi ya wafia dini. Kwa siku saba mauaji ya kinyama yaliendelea katika jiji la Paris, siku tatu za kwanza kwa hasira isiyoweza kueleweka. Na mauaji hayakufanyika jijini peke yake, bali kwa amri maalumu ya mfalme yalienezwa kwa majimbo na miji mingine ambako Waprotestanti waliweza kupatikana. Kulikuwa hakuna kujali umri au jinsia. Hata watoto wachanga wasio na hatia na wazee wakongwe hawakuachwa hai. Muungwana na mkulima, mzee na kijana, mama na mtoto, walikatwa-katwa pamoja. Katika nchi yote ya Ufaransa mauaji yaliendelea kwa miezi miwili. Watu wema kabisa wapatao elfu sabini, nguvu kazi ya Ufaransa, waliuawa.PKSw 206.2

  “Taarifa za mauaji makuu zilipofika Rumi, furaha miongoni mwa viongozi wa kanisa haikuwa na mipaka. Kardinali wa Lorraine alimzawadia mjumbe kwa taji elfu moja; mzinga wa Mtakatifu Angelo ulipigwa kutoa saluti ya furaha; na kengele zilipigwa katika kila mnara; mioto ya sherehe iligeuza usiku kuwa mchana; na papa Gregory XIII, akiwa na makardinali na viongozi wakuu wengine wa kanisa, walikwenda kwa maandamano marefu kuelekea katika kanisa la Mtakatifu Louis, ambapo kardinali wa Lorraine aliimba wimbo wa sifa na shukurani kwa Mungu uitwao kwa Kilatini Te Deum.... Medali ilipigwa kama kumbukizi ya mauaji makuu, na katika jiji la Vatikani bado kunaweza kuonekana picha tatu za kuchora za Vasari, zikielezea shambulio dhidi ya mkuu wa jeshi la wanamaji, mfalme akiwa katika kikao cha baraza wakipanga mauaji, na mauaji yenyewe. Gregory alimtumia Charles Ua la Waridi la Dhahabu; na miezi minne baada ya mauaji makuu, ... alisikiliza kwa kuridhika hubiri la padri wa Kifaransa, ... ambaye alizungumzia juu ya ‘siku ile iliyojaa furaha na shangwe, wakati ambapo baba mtakatifu sana alipopata taarifa, na alionesha moyo wa dhati alipotoa shukurani kwa Mungu na kwa Mtakatifu Louis.'”—Henry White, The Massacre of St. Bartholomew, ch. 14, par. 34.PKSw 206.3

  Roho mbaya ile ile iliyohamasisha Mauaji Makuu yaliyofanyikia katika eneo la Mtakatifu Bartholomayo ilichangia pia katika matukio ya Mapinduzi. Yesu Kristo alihukumiwa kuwa yeye ni mwongo, na sauti ya pamoja ya wakanamungu wa Ufaransa ilikuwa, “Ponda Mhuni,” maana yake Kristo. Kufuru mbaya kabisa na uovu wa kuchukiza vilienda pamoja, na watu wasio na maadili kabisa, watu katili sana na waovu kupindukia, ndio walioheshimiwa na kutukuzwa sana. Katika mambo yote haya, heshima kuu alipewa Shetani; wakati Kristo, katika tabia Yake ya ukweli, usafi, na upendo usiyo na ubinafsi, alisulubiwa.PKSw 207.1

  “Yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua.” Mamlaka ya kikanisa iliyotawala katika nchi ya Ufaransa wakati wa Mapinduzi na Utawala wa Hofu, vilipigana vita dhidi ya Mungu na neno Lake takatifu zaidi kuliko ulimwengu ulivyowahi kushuhudia. Ibada ya Mungu ilipigwa marufuku na Bunge. Biblia zilikusanywa na kuchomwa moto hadharani kwa kila aina ya dhihaka iliyowezekana. Sheria ya Mungu ilikanyagwa-kanyagwa. Taasisi zote za Biblia zilipigwa marufuku. Siku ya mapumziko ya kila juma iliondolewa na badala yake kila siku ya kumi ilitumiwa kwa kejeli na kufuru dhidi ya Mungu. Ubatizo na Meza ya Bwana vilipigwa marufuku. Na matangazo yalibandikwa katika maeneo ya makaburi yakisomeka waziwazi yaliyosema kuwa kifo ni usingizi wa milele.PKSw 207.2

  Kumcha Mungu kulisemwa kuwa mbali kabisa na mwanzo wa hekima na kwamba kumcha Mungu ilikuwa mwanzo wa upumbavu. Aina zote za ibada za kidini zilipigwa marufuku, isipokuwa ibada za uhuru na za nchi. “Askofu wa kikatiba wa Paris aliletwa hadharani afanye jukumu kubwa katika upuuzi wa kijeuri na wa kashfa mbaya sana ambao haujawahi kufanyika mbele ya wawakilishi wa kitaifa.... Aliitwa mbele akiwa na wasaidizi wake katika maandamano kamili, kutangaza kwa Mkutano kuwa dini aliyoifundisha kwa miaka mingi ilikuwa, katika nyanja zake zote, uongo wa kipadri, ambao hauna msingi wowote katika historia na katika ukweli mtakatifu. Alikanusha, kwa uwazi na katika maneno yanayoeleweka kabisa, uwepo wa Mungu ambaye alitoa maisha yake kumwabudu, na aliamua kwa wakati ujao kuabudu uhuru, usawa, mambo mema, na uadilifu. Ndipo alipoweka mezani mapambo ya kiaskofu, na kupewa fursa ya kukumbatiwa na mwenyekiti wa kongamano. Baadhi ya mapadri walioasi walifuata mfano wa askofu huyu.”—Scott, vol. 1, ch. 17.PKSw 207.3

  “Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi.” Ufaransa iliyomkana Mungu ilikuwa imenyamazisha sauti inayotoa maonyo ya mashahidi wawili wa Mungu. Neno la ukweli lililala likiwa limekufa katika mitaa yake, na wale waliochukia makatazo na masharti ya sheria ya Mungu walifurahia. Watu walimtukana hadharani Mfalme wa mbinguni. Sawa na wenye dhambi wa zamani, walipiga kelele: “Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu?” (Zaburi 73:11).PKSw 208.1

  Kwa ujasiri wenye kufuru kuliko inavyoweza kuaminika, mmoja wa mapadri wa shirika jipya alisema: “Mungu, kama kweli upo, lipiza kisasi kwa ajili ya jina Lako lililojeruhiwa. Mimi ninakutukana Wewe! Unakaa kimya; hutumi radi Zako. Ni nani atakayeamini uwepo Wako baada ya tukio hili?”—Lacretelle, History 11:309; in Sir Archibald Alison, History of Europe, vol. 1, ch. 10. Huu ulikuwa mwangwi wa dai la Farao: “Bwana ni nani, hata niitii sauti Yake?” “Mimi simjui Bwana!”PKSw 208.2

  “Mpumbavu amesema moyoni mwake, hakuna Mungu” (Zaburi 14:1). Na Bwana anasema kuhusu watu wanaopotosha ukweli: “Upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote” (2 Timotheo 3:9). Baada ya Ufaransa kupiga marufuku ibada ya Mungu aliye hai, “Yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele,” haikuchukua muda mrefu Ufaransa iliporomoka hadi kuanzisha ibada ya sanamu inayodhalilisha, kwa kuabudu Mungu Mke wa Mantiki, katika utu wa mwanamke fisadi. Na ibada hii ilifanywa katika kongamano lililowakilisha taifa, na mamlaka kuu kabisa za kiraia na kibunge! Anasema mwanahistoria: “Moja ya sherehe za wakati huu wa ukichaa, upuuzi uliounganishwa na uasi dhidi ya Mungu viliwekwa mbele ya watu. Milango ya uwanja ilifunguliwa kuruhusu wanamuziki, kuingia wakiwa wametanguliwa na viongozi wakuu wa jiji, waliingia kwa maandamano makubwa, wakiimba wimbo wa kusifu uhuru, wakisindikiza mtu ambaye baadaye ndiye alikuja kuwa wa kuabudiwa, mwanamke aliyefunikwa, ambaye walimwita Mungu wa Mantiki. Baada ya kuingizwa alifunuliwa, akiwa mrefu, na aliketishwa upande wa kulia wa mwenyekiti wa kongamano, ambapo alitambuliwa kuwa ni binti mchezaji wa muziki wa opera.... Binti huyu, kama mwakilishi stahiki wa mungu hoja waliyemwabudu, Kongamano la Kitaifa la Ufaransa lilifanya ibada kwa ajili yake.PKSw 208.3

  “Mchezo huu wa kipagani na kipuuzi ulifanywa kwa mtindo maalumu; na usimikaji huu wa Mungu Mke wa Mantiki ulifanywa na kuigizwa upya katika taifa zima, katika maeneo ambayo wakazi wake walitamani kujionesha kuwa sehemu ya Mapinduzi.”—Scott, vol. 1, ch. 17.PKSw 209.1

  Alisema msemaji mahiri aliyetambulisha ibada ya Mantiki: “Watunga sheria! Ushikiliaji sana mambo bila akili umeondoka na nafasi yake imechukuliwa na mantiki. Macho yake yasiyoona vizuri yasingeweza kustahimili mwangaza mkali wa nuru. Siku ya leo mkutano mkubwa umekusanyika chini ya matao hayo ya kigothiki, ambayo, kwa mara ya kwanza, yamerudisha mwangwi wa ukweli. PaleWafaransa wamesherehekea ibada pekee ya kweli,—ibada ya Uhuru, ibada ya Mantiki. Hapa tumefanya maombi kwa ajili ya mafanikio ya majeshi ya Jamhuri. Pale tumeachana na sanamu zisizo na uhai na badala yake tumepata mungu Mantiki, sanamu ile iliyo hai, kiumbe aliye mzuri sana katika vitu vya asili.”—M. A. Thiers, History of the French Revolution, vol. 2, uk. 370, 371.PKSw 209.2

  Wakati mungu mke alipoletwa ukumbini, msemaji alimshika mkono, na akiuangalia umati alisema: “Enyi watu mnaokufa, acheni kutetemeka mbele ya radi zisizo na nguvu za Mungu ambaye amesababisha hofu zenu. Tangu sasa msimtambue mungu mwingine zaidi ya Mantiki. Ninawapa sanamu yake iliyo tukufu na safi sana, toeni kafara zenu kwa mungu huyu.... Angukeni mbele ya Seneti kubwa ya Uhuru, O! Kifuniko cha Mantiki!”PKSw 209.3

  “Mungu mke, baada ya kukumbatiwa na mwenyekiti wa kongamano, alipandishwa juu ya gari zuri, na aliendeshwa, katikati ya kundi kubwa la watu, hadi katika kanisa kuu la Notre Dame, kuchukua nafasi ya Mungu. Pale alipandishwa juu hadi katika madhabahu ya juu, na alipokelea hapo heshima za wote waliokuwepo.”—Alison, vol. 1, ch. 10.PKSw 209.4

  Hili lilifuatwa, muda mfupi baadaye, na uchomaji wa Biblia hadharani. Wakati mmoja wanachama wa “Chama Mashuhuri cha Nyumba ya Makumbusho” waliingia katika ukumbi wa manispaa, wakipiga kelele, “Hongera sana Mantiki!” wakiwa wameba juu ya mlingoti mabaki ya vitabu kadhaa vilivyounguzwa moto, miongoni mwake vikiwemo vitabu vya sala, vitabu vya nyimbo, na Agano la Kale na Jipya, “vilivyopatanishwa katika moto mkuu,” alisema mwenyekiti, “upumbavu wote walioubuni wamewaongoza wanadamu kuutekeleza.”—Journal of Paris, 1793, No. 318. Quoted in Buchez-Roux, Collection of Parliamentary History, vol. 30, pp. 200, 201.PKSw 209.5

  Upapa ndio ulioanzisha kazi ambayo ukanamungu ulikuwa ukikamilisha. Sera za Rumi zilitengeneza yale mazingira, ya kijamii, kisiasa, na kidini, ambayo yalikuwa yakiipeleka Ufaransa katika maangamizi. Waandishi, wakizungumzia vitisho vya Mapinduzi, wanasema kuwa huku kuvuka mipaka kunapaswa kuleta lawama kwa kiti cha enzi na kanisa. (Tazama Kiambatisho.) Katika maana halisi ya kutenda haki mashitaka haya yanapaswa kurundikwa juu ya kanisa. Upapa uliweka sumu katika akili za wafalme dhidi ya Matengenezo, kama adui wa ufalme, wazo la uchonganishi ambalo lingekuwa hatarishi kwa amani na utangamano wa taifa. Ilikuwa ushawishi wa Rumi ambao kwa njia hiyo ulihamasisha ukatili wa kutisha na ukandamizaji usio kifani uliofanywa na mfalme.PKSw 210.1

  Roho ya uhuru iliondoka pamoja na Biblia. Popote injili ilipopokelewa, akili za watu ziliamshwa. Walianza kutupilia mbali minyororo ambayo ilikuwa imewafunga katika utumwa wa ujinga, uovu, na ushirikina. Walianza kufikiri na kutenda kama watu. Wafalme walianza kutetemeka kwa ajili ya ukandamizaji wao.PKSw 210.2

  Rumi haikuchelewa kuchochea hofu na wivu wao. Papa alimwambia balozi wa Ufaransa mwaka 1525: “Wazimu [Uprotestanti] huu siyo tu kuwa utashinda na kuharibu dini, bali utashinda na kuharibu tawala zote, utashinda na kuangamiza uungwana, sheria, utaratibu, na mamlaka zote.”—G. de Felice, History of the Protestants of France, b. 1, ch. 2, par. 8. Miaka michache baadaye balozi wa papa alimwonya mfalme: “Mheshimiwa, usidanganyike. Waprotestanti watavuruga utaratibu wote wa kiraia na wa kidini.... Kiti cha enzi na madhabahu vyote kwa pamoja viko hatarini.... Uanzishaji wa dini mpya kwa vyovyote vile utaanzisha serikali mpya.”— D'Aubigne, History of the Reformation in Europe in the Time of Calvin, b. 2, ch. 36. Na wanateolojia waliamsha chuki za watu kwa kutangaza kuwa mafundisho ya Kiprotestanti “yanawashawishi watu kushika mambo mapya ya kipumbavu; yanamnyang'anya mfalme heshima na utii wa raia, na yanavuruga kanisa na serikali” Hivyo ndivyo Rumi ilivyofaulu kuipanga Ufaransa dhidi ya Matengenezo. “Ilikuwa ni kwa kusudi la kudumisha kiti cha enzi, kulinda waungwana, na kudumisha sheria, ndiyo maana upanga wa mateso kwa mara ya kwanza ulichomolewa kutoka katika ala yake katika nchi ya Ufaransa.”—Wylie, b. 13, ch. 4.PKSw 210.3

  Kidogo sana watawala wa nchi walijua mapema matokeo ya sera hiyo hatarishi. Mafundisho ya Biblia yangeweza kujaza akili na mioyo ya watu kanuni za haki, kiasi, ukweli, na ukarimu ambazo ndizo jiwe kuu la pembeni la mafanikio ya taifa. “Haki huinua taifa” Na kwa njia hiyo “kiti cha enzi huimarika” (Mithali 14:34; 16:12). “Kazi ya haki itakuwa amani;” na matokeo yake, “yatakuwa ni utulivu na matumaini daima” (Isaiah 32:17). Anayeitii sheria ya Mungu ataziheshimu na kuzitii kikamilifu sheria za nchi yake. Mtu anayemcha Mungu atamheshimu mfalme katika utekelezaji wa mamlaka yake yote ya haki na halali. Lakini Ufaransa yenye huzuni ilipiga marufuku Biblia na kuwafukuza wafuasi wake. Karne baada ya karne, watu wa kanuni na uadilifu, watu wenye akili makini na nguvu ya kimaadili, waliokuwa na ujasiri wa kusimamia kile walichokiamini na imani yao kiasi cha kuteseka kwa ajili ya ukweli—kwa karne nyingi watu hawa walifanya kazi kwa nguvu nyingi kama watumwa katika vichochoro, waliuawa kwa moto, au waliozea katika vyumba vya magereza. Maelfu kwa maelfu walipata usalama kwa kukimbia na kwenda uhamishoni; na jambo hili liliendela kwa miaka mia mbili hamsini baada ya kuanzishwa kwa Matengenezo.PKSw 210.4

  “Kwa mara chache sana kulikuwepo kizazi cha watu wa Ufaransa wakati wa kipindi kirefu ambacho hakikushuhudia wanafunzi wa injili wakikimbia mbele ya hasira za kichaa za mtesaji, na wakiondoka na akili, sanaa, bidii, na utaratibu, ambapo, kama kanuni, walifanikiwa kwa viwango vya juu sana, kutajirisha nchi ambazo walipata hifadhi. Na kwa uwiano ule ule ambao walizijaza nchi nyingine kwa karama hizi, ndivyo walivyoondoa karama hizo katika nchi ya Ufaransa. Ikiwa wale wote waliofukuzwa wangetunzwa katika nchi ya Ufaransa; ikiwa, katika miaka hii mia tatu, stadi za viwanda za wakimbizi zingekuwa zikilima udongo wake; ikiwa, katika miaka hii mia tatu, ujuzi wao wa sanaa ungekuwa ukitumiwa katika uzalishaji nchini mwao; ikiwa, katika miaka hii mia tatu, akili zao zenye ubunifu na nguvu ya uchambuzi zingetumiwa kuboresha fasihi yake na kuendeleza sayansi yake; ikiwa hekima yake ingetumiwa kuongoza mabaraza yake, mashujaa wake wakipigana vita vyao, haki yao ikitunga sheria zake, na dini ya Biblia ikiimarisha akili na ikiongoza dhamiri za watu, ni utukufu mwingi kiasi gani ungeifunika Ufaransa leo! Ufaransa leo ingekuwa nchi kubwa duniani, yenye mafanikio, na furaha—kielelezo cha kuigwa na mataifa mengine!PKSw 211.1

  “Lakini chuki yenye upofu na isiyoepukika ilimfukuza kutoka katika udongo wake kila mwalimu wa tabia njema, kila shujaa wa utaratibu, kila mlinzi mwaminifu wa kiti cha enzi; iliwaambia watu ambao walikuwa na uwezo wa kuifanya nchi yao ‘ijulikane na itukuke', chagua unachokitaka, kuchomwa moto au kukimbilia uhamishoni. Hatimaye uharibifu wa dola ulikamilika; hakukubaki dhamiri ya kupigwa marufuku; hakuna dini ya kukokotwa kwenda kwenye jukwaa la kuchomea moto watu; hakuna uzalendo wa kufukuzwa uondoke nchini.”—Wylie, b. 13, ch. 20. Na Mapinduzi, na mambo yake ya kutisha, yalikuwa ndiyo matokeo yake na machungu yake.PKSw 211.2

  “Kwa kitendo cha Wahujenoti kuikimbia nchi mdororo wa jumla wa kiuchumi uliikumba nchi ya Ufaransa. Miji iliyokuwa ikistawi kwa viwanda uchumi wake uliporomoka; wilaya zenye rutuba zilirudi katika hali yake ya zamani ya nyika; udumavu wa akili na anguko la uadilifu vilifuata kipindi cha maendeleo yaliyokuwa siyo ya kawaida. Jiji la Paris liligeuka na kuwa nyumba kubwa ya ombaomba, na inakadiriwa kuwa, wakati Mapinduzi yakianza, watu ombaomba laki mbili walikuwa wakitafuta msaada kutoka katika mikono ya mfalme. Majesuti peke yao ndio waliostawi katika taifa lililokuwa likioza, na walitawala kwa ukatili wa kutisha makanisa na shule, magereza na manchani.”PKSw 211.3

  Injili ingekuwa imeiletea Ufaransa suluhisho la yale matatizo ya kisiasa na kijamii ambayo yalishinda stadi za viongozi wake wa kidini, mfalme wake, na wabunge wake, na mwisho wake yakaliweka taifa katika hali isiyotawalika na uharibifu mkubwa. Lakini chini ya madhehebu ya Rumi watu walipoteza masomo ya Mwokozi yenye baraka za kujikana nafsi na upendo usio na ubinafsi. Waliongozwa mbali na matendo ya kujikana nafsi kwa ajili ya wengine. Matajiri hawakukemewa kwa kuwakandamiza maskini, watu maskini hawakuwa na msaada kwa ajili ya utumwa na udhalilishwaji wao. Uchoyo wa watu maskini na wenye nguvu uliongezeka na kuongezeka katika uhalisia ukandamizaji wake. Kwa karne nyingi ulafi na ufisadi wa watu wenye fursa zao ulisababisha unyonyaji kwa wakulima wadogo. Matajiri waliwakosea watu maskini, na watu maskini waliwachukia matajiri.PKSw 212.1

  Katika majimbo mengi ardhi ilimilikiwa na matajiri, na watu waliokuwa katika matabaka ya wafanya kazi walikuwa wapangaji tu; waliishi kwa rehema za wamiliki wa mashamba husika na walilazimishwa kulipa gharama za juu. Mzigo wa kutegemeza kanisa na dola uliwaangukia watu wa daraja la kati na daraja la chini, ambao walitozwa kodi kubwa na mamlaka za kiraia na mamlaka za kidini. “Raha ya matajiri ilichukuliwa kuwa sheria kuu; wakulima wakubwa na wakulima wadogo wangeweza kukosa chakula, ilhali wakandamizaji wao waliendelea kunawiri na kustawi.... Watu walilazimishwa kila mahali kujali maslahi pekee ya mabwana zao. Maisha ya vibarua katika kilimo yalikuwa maisha ya kazi zisizoisha na madhila yasiyopungua; malalamiko yao, ikiwa walidiriki kulalamika, yalijibiwa kwa dharau na matusi. Mahakama za haki ziliwasikiliza siku zote matajiri kuliko wakulima; rushwa zilipokelewa sana na majaji; na mwelekeo mdogo tu wa mtawala ulitosha kupata nguvu ya kisheria, kwa sababu ya mfumo wa rushwa iliyokithiri. Kuhusiana na kodi zilizokamuliwa kutoka kwa watu wa kawaida, kwa njia ya viongozi wa serikali kwa upande mmoja, na viongozi wa kanisa kwa upande mwingine, fedha iliyofika katika hazina ya mfalme au katika hazina ya askofu haikuzidi nusu; sehemu iliyobaki ilitapanywa katika maisha ya ufisadi na anasa. Na watu waliowafanya wenzao kuwa maskini wao wenyewe walikuwa wanasamehewa kodi, na walipewa haki na sheria au desturi kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali serikalini. Idadi ya watu waliokuwa na upendeleo maalumu walikuwa laki moja hamsini elfu, na kwa ajili ya raha zao mamilioni ya watu walilazimishwa kuishi maisha yasiyokuwa na matumaini na ya kudhalilika sana.” (Tazama Kiambatisho.)PKSw 212.2

  Ofisi ya mfalme ilijaa anasa na ubadhirifu. Kulikuwa na imani ndogo sana kati ya raia na watawala. Hatua zote zilizochukuliwa na serikali zilitiliwa mashaka kwa sababu ya ubinafsi na uchoyo uliotawala. Kwa zaidi ya nusu karne kabla ya wakati wa Mapinduzi kiti cha enzi kilikaliwa na Louis XV, ambaye, hata nyakati zile za uovu, alijulikana kama mfalme mvivu, asiyekuwa makini, na mwenye tamaa. Akiwa na tabaka la watawala makabaila katili na tabaka la chini la watu maskini, dola ikiwa na matatizo makubwa ya kifedha na watu wakiwa na hasira, halikuhitajika jicho la nabii kuona mapema bomu lililokuwa karibu kulipuka. Kwa maonyo ya washauri wake mfalme alikuwa na desturi ya kujibu: “Najaribu kufanya mambo yaendelee hivyo kwa kadiri nitakavyoendelea kuishi; baada ya kifo changu mambo yatakuwa yatakavyokuwa.” Mashauri ya kufanya matengenezo yalitolewa lakini aliyaona maovu, lakini hakuwa na ujasiri wala nguvu ya kukabiliana nayo. Uharibifu ulioisubiri Ufaransa ulielezwa kwa lugha ya picha katika jibu lake la kivivu na kibinafsi, “Baada yangu, gharika!”PKSw 213.1

  Kwa kucheza na wivu wa wafalme na wa matabaka ya watawala, Rumi ilipata mamlaka ya kuwafanya wawafanye watu kuwa watumwa wao, Rumi ikijua vema kuwa hatimaye dola itadhoofika, na kwa njia hiyo atapata wepesi wa kuwaweka watawala na watu wao wote kwa pamoja chini kongwa lake la utumwa. Kwa sera iliyoona mbali Roma ilielewa kuwa ili kuwaweka watu katika utumwa kikamilifu, pingu zinapaswa kufungwa kwenye roho zao; na kwamba njia ya hakika kabisa ya kuwazuia watu wasitoke katika utumwa wao ilikuwa kuwafanya wasiweze kuwa huru. Jambo jingine lililoleta zaidi ya maelfu ya mateso ya kutisha kuliko mateso ya kimwili yaliyosababisha kutungwa kwa sera yake, ilikuwa kushuka kwa kiwango cha uadilifu. Wakiwa wamenyang'anywa Biblia, na wakiwa wameachiwa mafundisho ya chuki na ubinafsi, watu walifunikwa na ujinga na ushirikina, na walizama katika uovu, kiasi kwamba walijikuta hawana uwezo wa kujiongoza.PKSw 213.2

  Lakini matokeo ya mambo haya yote yalikuwa tofauti sana na kile Rumi ilichokuwa imekikusudia. Badala ya kuushikilia umma katika utii usio na maswali kwa mafundisho yake yasiyohojiwa, matokeo yake yaliwafanya kuwa makafiri na wanamapinduzi. Waliudhihaki Urumi kama ni usanii wa mapadri. Waliwaona viongozi wa kidini kama kikundi cha kuwakandamiza. Mungu pekee waliyemjua alikuwa mungu wa Roma; mafundisho yake ndiyo yalikuwa dini yao pekee. Walichukulia ulafi na ukatili wako kama matunda halali ya Biblia, na hawakutamani kuwa na mojawapo ya hayo.PKSw 213.3

  Rumi iliwakilisha vibaya tabia ya Mungu na ilipotosha maagizo Yake, na sasa watu walikataa Biblia na Mwasisi wake. Rumi ilitaka imani isiyohoji mafundisho yake, chini ya idhini bandia ya Maandiko. Katika mwitikio kwa hilo, Voltaire na washirika wake walitupilia mbali neno la Mungu kabisa na wakasambaza sumu ya ukanamungu kila mahali. Rumi ilikuwa imekanyaga watu chini ya nyayo zake za chuma; na sasa umma wa watu, wakiwa wamedhalilika na kufanyiwa ukatili mkubwa, katika kujibu mapigo ya mtesaji wao katili, walitupilia mbali kila kizuizi. Wakiwa wamekasirika kwa sababu ya uongo wa wazi ambao kwa muda mrefu walikuwa wakiuabudu, walitupilia mbali ukweli na uongo kwa pamoja; na wakichukulia kuwa uvunjaji wa sheria ndiyo uhuru, watumwa wa uovu walifurahia uhuru wao wa kufikirika.PKSw 214.1

  Wakati wa mwanzo wa Mapinduzi, kwa idhini ya mfalme, watu wa kawaida walipewa fursa ya uwakilishi unaozidi ule wa matajiri na viongozi wa dini wakiwekwa pamoja. Kwa njia hiyo, mzani wa mamlaka ulikwenda katika mikono yao; lakini hawakuwa wamejiandaa kuutumia mzani huo kwa hekima na kiasi. Wakiwa na shauku ya kushughulikia mabaya waliyotendewa, waliazimia kufanya kazi ya kuijenga upya jamii. Raia walioudhiwa, ambao akili zao zilikuwa zimejazwa uchungu na kumbukumbu za muda mrefu za mabaya waliyotendewa, waliazimia kuipindua hali yao ya mateso ambayo yalikuwa yamekuwa makubwa kiasi cha kutoweza kuchukulika na kulipiza kisasi kwa wale ambao waliwachukulia kuwa waasisi wa mateso yao. Waliokandamizwa walitumia somo ambalo walijifunza kutokana na ukatili na wakawa wakandamizaji wa wale waliwakandamiza.PKSw 214.2

  Ufaransa yenye huzuni ilivuna umwagikaji wa damu kama mavuno ya mbegu walizopanda wao wenyewe. Matokeo ya kuutii utawala na mamlaka ya Rumi yalikuwa ya kutisha. Wakati Ufaransa, chini ya usimamizi wa Dini ya Kirumi, ilijenga nguzo ya kwanza ya kuchomea watu moto mwanzoni mwa Matengenezo, hapo ndipo Mapinduzi yalijenga bamba la kwanza la kukatia vichwa vya wahalifu. Mahali pale pale ambapo wafia dini wa kwanza wa imani ya Kiprotestanti walichomewa moto katika karne ya kumi na sita, wahanga wa kwanza wa Mapinduzi walikatwa vichwa katika karne ya kumi na nane. Kwa kitendo cha kuikataa injili, ambayo ingeleta uponyaji wa nchi yao, Ufaransa ilifungua mlango kuruhusu ukanamungu na uharibifu uingie ndani ya nchi. Mara tu baada ya vizuizi vya sheria ya Mungu kuwekwa pembeni, ilionekana wazi kuwa sheria za mwanadamu haziwezi kudhibiti mawimbi yenye nguvu ya mihemko ya kibinadamu; na taifa lilisombwa na kupelekwa katika uasi na kutotawalika. Vita dhidi ya Biblia ilizindua zama ambazo husimama kama zama za Utawala wa Hofu. Amani na furaha viliondolewa katika nyumba na mioyo ya watu. Hakuna mtu aliyekuwa salama. Aliyesherehekea ushindi leo alishukiwa, alihukumiwa, kesho. Ukatili na tamaa vilitawala bila mpinzani.PKSw 214.3

  Mchungaji, viongozi wa kazi, na matajiri walilazimishwa kujisalimisha kwa mauaji ya watu walioingiwa na kichaa. Kiu yao ya kulipiza kisasi iliamshwa tu na mauaji ya mfalme; na watu walioamuru auawe muda si mrefu walimfuata kwenye jukwaa la kunyongea. Mauji ya jumla ya wote walioshukiwa kuwa kinyume na Mapinduzi yalipangwa rasmi. Magereza yalifurika wafungwa, wakati mmoja yakiwa na wafungwa zaidi ya laki mbili. Miji ya ufalme ilijaa matukio ya kutisha. Kikundi kimoja cha wanamapinduzi kilipigana na kikundi kingine, na Ufaransa iligeuka kuwa uwanja mkubwa wa makundi ya watu wanaopingana, wakiongozwa na hasira ya mihemko yao. “Katika jiji la Paris tukio moja la ghasia lilifuata jingine, na raia waligawanyika katika mchanganyiko wa vikundi vinavyopingana, ambavyo vilionekana vilikuwa vimedhamiria kuuana na kumalizana kabisa.” Na kuongezeka kwa matatizo ya jumla ya taifa, Ufaransa iliingia katika vita ya muda mrefu na yenye madhara makubwa dhidi ya mataifa makubwa ya Ulaya. “Nchi ilikuwa karibu kufilisika, wanajeshi walikuwa wakidai malipo ya nyuma ya mishahara yao, wakazi wa jiji la Paris walikuwa wanakaribia kufa kwa njaa, majimbo yalikuwa yamebaki bila kitu kwa sababu ya wanyang'anyi, na ustaarabu ulikaribia kufutika kwa sababu ya nchi kutotawalika na uhalifu usio na mamlaka ya kuudhibiti.”PKSw 215.1

  Kwa kiwango kikubwa watu walikuwa walijifunza masomo kutokana na ukatili na mateso ambayo Rumi ilikuwa imewafundisha kwa juhudi kubwa. Siku ya kupatilizwa ilikuwa imekuja hatimaye. Wakati huu siyo wanafunzi wa Yesu waliotupwa magerezani na walioburuzwa kwenda kwenye nguzo za kuchomea watu moto. Muda mrefu uliopita watu hawa waliangamizwa au walifukuzwa na kwenda kuishi uhamishoni. Roma isiyo na huruma sasa ilihisi nguvu ya mauaji ya wale ambao iliwafundisha kufurahia matendo ya umwagaji damu. “Mfano wa utesaji ambao viongozi wa kanisa la Ufaransa waliuonesha kwa zama nyingi, sasa uliwarudia wao kwa nguvu nyingi zaidi. Majukwaa ya kunyongea watu yalikuwa na wekundu wa damu ya mapadri iliyokuwa ikitiririka. Manchani na magereza, ambayo awali yalijawa na Wahujenoti, sasa yalijawa na watesaji wao. Wakiwa wamefungiwa kwa minyororo kwenye benchi na wakivuja jasho kwenye kasia, viongozi wa kanisa Katoliki la Roma walipata uzoefu wa mateso ambayo kanisa lao liliyafanya sana dhidi ya wazushi wapole” (Tazama Kiambatanisho.)PKSw 215.2

  “Ndipo zilikuja siku ambazo sheria ya kikatili zaidi kuliko sheria zote ilitekelezwa na mahakama katili kuliko mahakama zote; ambapo hakuna mtu ambaye angeweza kusalimia jirani zake au kufanya maombi yake binafsi ... bila hatari ya kutenda kosa linaloadhibiwa kwa kifo; wakati wapelelezi walipotembelea kona zote; wakati bamba la kukatia vichwa vya watu lilikuwa refu na gumu likiwa kazini kila asubuhi; wakati magereza yakijazwa kama meli za watumwa zinavyojazwa; wakati mifereji ilipopitisha damu ikitiririka kuelekea mto.... Wakati magari ya kukokotwa na ng'ombe yaliyobeba wahanga yalipopita katika mitaa ya Paris, yakiwapeleka mahali pa kuuliwa, wawakilishi, ambao kamati ya mfalme ilikuwa imewatuma katika idara mbalimbali, walisherehekea kwa njia ya ukatili mkubwa ambao ulikuwa haujawahi kuonekana katika mji mkuu. Kisu cha mashine ya kuulia kiliinuka na kuanguka kwa kasi ambayo ilikuwa ndogo mno kwa kazi yao ya kuchinja watu. Mistari mirefu ya mateka ilifyekwa kwa mundu wa kukatia vichara vya zabibu. Matundu yaliwekwa katika sakafu ya mtumbwi uliojaa watu. Mji wa Lyons uligeuka kuwa jangwa. Katika mji wa Arras hata rehema ya kikatili ya kifo cha haraka wafungwa walinyimwa. Maeneo yote hadi Loire, tangu Saumur hadi baharini, makundi makubwa ya kunguru na mwewe walikula maiti zilizokuwa uchi, zikiwa zimejisokota pamoja na kukumbatiana katika namna isiyofaa kuonwa. Hakuna huruma iliyooneshwa kwa jinsia au umri. Idadi ya wavulana na wasichana wa miaka kumi na saba waliouliwa na serikali ile inayotisha, inakadiriwa kuwa mamia. Watoto wachanga walionyakuliwa kutoka katika vifua vya mama zao walitupwa kutoka mkuki hadi mkuki kwenye mtaa wa Jacobin” (Tazama Kiambatanisho.) Katika muda mfupi wa miaka kumi, maelfu ya wanadamu waliuawa.PKSw 215.3

  Yote haya yalitendeka kulingana na matakwa ya Shetani. Jambo hili ndilo ambalo kwa zama nyingi amekuwa akilifanyia kazi. Sera yake ni uongo tangu mwanzo hadi mwisho, na kusudi lake ni kuleta maumivu na maafa kwa wanadamu, kuharibu na kuchafua kazi ya Mungu, kutia doa katika makusudi ya Mungu matakatifu ya ukarimu na upendo, na kwa njia hiyo alete huzuni mbinguni. Hivyo basi, kwa sanaa zake za uongo anatia upofu katika akili za watu, na anawaongoza watu kutupa lawama za kazi za Shetani kwa Mungu, kana kwamba maumivu ni matokeo ya mpango wa Muumbaji. Kwa jinsi hiyo hiyo, wakati watu ambao wamedhalilishwa na ambao wameumizwa sana kwa sababu ya nguvu yake ya kikatili wanapopata uhuru wao, anawashawishi waende mbali zaidi katika kuwatesa watesi wao. Ndipo picha ya uovu usio na mipaka unapotumiwa na watu wakatili na watesaji kama kielelezo cha matokeo ya uhuru.PKSw 216.1

  Wakati kosa katika vazi moja linapogunduliwa, Shetani anavalisha kosa hilo hilo katika joho jingine, na watu wengi hulipokea kwa shauku kubwa kama walivyopokea kosa hilo katika vazi la kwanza. Watu walipogundua kuwa dini ya Kirumi ni dini ya uongo, na Shetani akatambua kuwa asingeweza tena kwa kupitia taasisi hii kuwaongoza watu kukiuka sheria ya Mungu, Shetani aliwashawishi watu kuchukulia dini zote kuwa ni udanganyifu, na kuwa Biblia ni hadithi ya uongo; na, wakitupa pembeni amri takatifu, watu walijiachia na kujiingiza katika uovu usio na mipaka.PKSw 216.2

  Kosa kubwa lililoleta madhara makubwa kwa wananchi wa Ufaransa ilikuwa kupuuza ukweli huu mmoja: kuwa uhuru wa kweli unapatikana katika utii wa dhati kwa sheria ya Mungu. “Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari.” “Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya” (Isaya 48:18, 22; Mithali 1:33).PKSw 217.1

  Wakanamungu, wasioamini, na waasi hupinga na hukataa sheria ya Mungu; lakini matokeo ya mvuto wao huthibitisha kuwa ustawi wa mwanadamu umeshikamana na utii wake kwa amri za Mungu. Wasiojifunza somo katika kitabu cha Mungu wanalazimishwa kulipata somo hilo katika historia ya mataifa.PKSw 217.2

  Wakati Shetani alipolitumia Kanisa la Kirumi kuwapeleka watu mbali na utii, mbinu yake ilifichwa, na kazi yake ilikuwa imefunikwa kiasi kwamba udhalilishaji na maumivu yaliyotokana na mbinu hiyo havikuonekana kuwa ni matunda ya uasi dhidi ya sheria ya Mungu. Na nguvu yake kwa kiasi kikubwa ilidhibitiwa na utendaji kazi wa Roho wa Mungu kwa hiyo makusudi yake yalizuiliwa kukomaa na kufika hatua ya kuzaa matunda yaliyotarajiwa. Watu hawakuweza kuunganisha madhara na chanzo chake, na hivyo, hawakuweza kugundua sababu ya taabu zao.PKSw 217.3

  Lakini katika Mapinduzi sheria ya Mungu iliwekwa pembeni waziwazi na Baraza Kuu la Kutunga Sheria. Na katika Utawala wa Hofu uliofuata, utendaji kazi wa chanzo na madhara viliweza kuonekana kwa wote. Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu.PKSw 217.4

  Wakati Ufaransa ilipomkataa Mungu na kuiweka Biblia pembeni, watu waovu na roho za mashetani walifurahia kufikia lengo ambalo walilitamani kwa muda mrefu—ufalme usiothibitiwa na sheria ya Mungu. Kwa kuwa hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, matokeo yake mioyo ya wanadamu ilithibitishwa “ndani yao ili kutenda mabaya” (Mhubiri 8:11). Lakini ukiukwaji wa sheria ya haki na takatifu lazima ulete maumivu na maangamizi kwa vyo vyote vile. Ingawa hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, matendo maovu ya wanadamu yalikuwa yakiratibu utekelezaji wa uharibifu wao. Karne nyingi za uasi na uhalifu zilikuwa zikidunduliza ghadhabu dhidi ya siku ya kupatilizwa; na uovu wao ulipojaa, watu waliokuwa wakimdhihaki Mungu walijifunza kwa kuchelewa kuwa ni jambo linalotisha kuuchosha uvumilivu wa Mungu. Roho wa Mungu anayedhibiti, anayeweka kizuizi dhidi ya nguvu za kikatili za Shetani, alikuwa ameondolewa kwa kiwango kikubwa, na yule ambaye furaha yake ni kuwaona wanadamu wakiwa katika mateso aliruhusiwa kutekeleza mapenzi yake. Wale ambao walikuwa wamechagua huduma ya uasi waliachwa wavune matunda ya uasi mpaka nchi ilijazwa kwa uhalifu wa kutisha kiasi ambacho kalamu haiwezi kuandika. Kutoka katika majimbo yaliyoharibiwa na miji ilivyovunjwa vunjwa kilio cha kutisha kilisikika—kilio cha uchungu mwingi sana. Ufaransa ilitikiswa kama vile tetemeko la ardhi linavyotikisa nchi. Dini, sheria, utulivu wa kijamii, familia, dola, na kanisa— vyote viliharibiwa na mikono ya watu wasiomcha Mungu iliyokuwa imeinuliwa dhidi ya sheria ya Mungu. Mwenye hekima alisema ukweli: “Mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake.” “Ajapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia, akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, wenye kicho mbele zake; walakini haitakuwa heri kwa mwovu” (Mithali 11:5; Mhubiri 8:12, 13). “Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana;” “Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe” (Mithali 1:29, 31).PKSw 217.5

  Mashahidi waaminifu wa Mungu, waliochinjwa na mamlaka yenye makufuru “inayopanda kutoka kuzimu,” hawakubaki kimya kwa muda mrefu. “Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama” (Ufunuo 11:11). Ilikuwa mwaka 1793 ambapo sheria zilizopiga marufuku dini ya Kikristo na kuweka pembeni Biblia zilipitishwa na Bunge la Ufaransa. Miaka mitatu na nusu baadaye, azimio lililotengua sheria hizi, na hivyo kutoa uhuru wa watu kusoma Maandiko, lilipitishwa na Bunge hilo hilo. Ulimwengu ulisimama kwa mshangao na hofu kubwa baada ya kuona ukubwa wa madhara yaliyotokana na kuyakataa Maandiko Matakatifu, na watu wakatambua umuhimu wa kumwamini Mungu na kuliamini neo Lake kama msingi wa matendo mema na uadilifu. Bwana alisema: “Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli,” (Isaya 37:23). “Basi, tazama, nitawajulisha, mara moja hii nitawajulisha, mkono wangu, na nguvu zangu; nao watajua ya kuwa, jina langu ni YEHOVA” (Yeremia 16:21).PKSw 218.1

  Kuhusu mashahidi wawili nabii anaeleza zaidi: “ Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama” (Ufunuo 11:12). Tangu Ufaransa ilipopiga vita dhidi ya mashahidi wawili wa Mungu, mashahidi hao walipewa heshima kubwa mno kuliko kabla ya hapo. Mwaka 1804 shirika la kuchapisha na kusambaza Biblia la British and Foreign Bible Society lilianzishwa. Shirika hilo lilifuatwa na mashirika mengine yanayofanana na hilo, yakiwa na matawi mengi, katika bara la Ulaya. Mwaka 1816 shirika la American Bible Society liliundwa. Wakati shirika la British Society lilipoundwa, Biblia ilikuwa imechapishwa na kusambazwa katika lugha hamsini. Tangu wakati huo Biblia imeshachapishwa katika lugha na lahaja mamia mengi. (Tazama Kiambatanisho.)PKSw 218.2

  Kwa miaka hamsini kabla ya 1792, juhudi kidogo zilifanyika kwa ajili ya kazi ya umishenari katika nchi za kigeni. Hakuna vyama vipya vilivyoundwa, na ni makanisa machache sana yaliyofanya juhudi ya kueneza Ukristo katika nchi za kipagani. Lakini kuelekea mwishoni mwa karne ya kumi na nane badiliko kubwa lilitokea. Watu walianza kutoridhishwa na matokeo ya kutegemea falsafa ya mantiki peke yake na waligundua umuhimu wa ufunuo wa Mungu na dini halisi. Tangu wakati huu kazi ya umishenari katika nchi za kigeni ilifikia ukuaji uliokuwa haujawahi kufikiwa kabla ya hapo. (Tazama Kiambatanisho.)PKSw 219.1

  Maboresho katika uchapishaji ulitoa msukumo katika kazi ya usambazaji wa Biblia. Ongezeko la miundombinu ya mawasiliano kati ya nchi mbalimbali, kuondolewa kwa vizuizi vya zamani vya chuki na ubaguzi kati ya taifa moja na jingine, na upotezaji wa nguvu za kiserikali za kiongozi mkuu wa Kanisa la Roma vilifungua njia kwa ajili ya neno la Mungu kusambaa. Kwa miaka kadhaa Biblia ilikuwa imeshaanza kuuzwa bila kizuizi katika mitaa ya Roma, na sasa ilianza kupelekwa katika kila eneo linalokaliwa watu ulimwenguni kotePKSw 219.2

  Mkanamungu Voltaire aliwahi kusema kwa majivuno: “Nimechoshwa na watu wanaosema kwa kurudia-rudia kuwa watu kumi na mbili walianzisha dini ya Kikristo. Nitathibitisha kuwa mtu mmoja anatosha kuishinda dini ya Kikristo.” Vizazi vingi vimepita tangu kifo chake. Mamilioni ya watu wamejiunga kupigana vita kwa ajili ya Biblia. Lakini dini ya Kikiristo siyo tu kuwa haijaangamizwa, badala yake mahali ambapo palikuwa na Biblia mia moja wakati wa Voltaire, kuna Biblia elfu kumi sasa, ndiyo, nakala laki moja za kitabu cha Mungu. Katika maneno ya Mwanamatengenezo wa awali kuhusu kanisa la Kikristo, “Biblia ni fuawe ambayo imemaliza nyungo nyingi.” Bwana alisema: “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu” (Isaya 54:17).PKSw 219.3

  “Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele.” “Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu, Maagizo yake yote ni amini, Yamethibitika milele na milele, Yamefanywa katika kweli na adili” (Isaya 40:8; Zaburi 111:7, 8). Chochote kitakachojengwa juu ya mamlaka ya mwanadamu kitashindwa; lakini cho chote kitakachojengwa juu ya mwamba wa neno la Mungu lisilobadilika kitasimama milele.PKSw 219.4

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents