Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 2—Mateso katika Karne za Kwanza

  Yesu alipowafunulia hatima ya Yerusalemu na matukio ya ujio wa pili, alitabiri pia uzoefu wa watu Wake tangu wakati ambao angechukuliwa kutoka kwao, hadi kurudi Kwake katika nguvu na utukufu kwa ajili ya ukombozi wao. Kutokea kwenye Mlima wa Mizeituni Mwokozi aliziona dhoruba ambazo zingelikabili kanisa la mitume; na akipenya zaidi katika wakati ujao, jicho Lake lilibaini pepo kali, zinazotisha ambazo zingewapiga wafuasi Wake katika zama zilizokuwa zinakuja za giza na mateso. Katika matamko machache ya maana na ya kutisha alitabiri kiwango ambacho watawala wa ulimwengu huu wangechangia katika kulitesa kanisa la Mungu (Mathayo 24:9, 21, 22). Iliwapasa wafuasi wa Kristo kupita katika njia ile ile ya unyenyekevu, aibu, na mateso aliyopitia Bwana wao. Uadui uliomkabili Mkombozi wa ulimwengu ungedhihirishwa dhidi ya wote ambao wangeliamini jina Lake.PKSw 28.1

  Historia ya kanisa la awali ilishuhudia utimizo wa maneno ya Mwokozi. Nguvu za dunia na za kuzimu zilijipanga dhidi ya Kristo kwa kupinga kazi ya wafuasi Wake. Upagani ulibaini mapema kuwa ikiwa injili ingefanikiwa, mahekalu yao na madhabahu zao zingefutiliwa mbali; kwa hiyo ulikusanya majeshi yake yote kuharibu Ukristo. Mioto ya mateso iliwashwa. Wakristo walinyang'anywa mali zao na kufukuzwa kutoka katika nyumba zao. Walistahimili “mashindano makubwa ya maumivu” (Waebrania 10:32). Wengine “walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani” (Waebrania 11:36). Idadi kubwa miongoni mwao walitia muhuri ushuhuda wao kwa damu yao. Mtu huru kwa mtumwa, tajiri na maskini, wasomi na wasiokuwa wasomi, wote pamoja waliuawa bila rehema.PKSw 28.2

  Mateso haya, yakianzia chini ya Nero karibu na wakati wa kuuawa kwa Paulo, yaliendelea kwa kiwango kikubwa au kidogo kwa karne kadhaa. Wakristo walishitakiwa kwa uongo wakihusishwa na uhalifu wa kutisha sana na kutangazwa kuwa chanzo cha majanga makubwa—njaa, magonjwa, na matetemeko ya ardhi. Walipofanywa kuwa walengwa wa chuki mashaka ya kila mtu, watoa taarifa walisimama tayari, kwa ajili ya mapato, kuwasaliti watu wasio na hatia. Walihukumiwa kama waasi dhidi ya dola, kama maadui wa dini, na chukizo kwa jamii. Idadi kubwa miongoni mwao walitupwa kwa wanyama wakali au waliunguzwa moto katika viwanja vya maonesho. Baadhi walisulubishwa; wengine walifunikwa kwa ngozi za wanyama pori na kusukumiwa katika viwanja vya michezo ili wararuliwe na mbwa. Adhabu yao ilifanywa kuwa burudani katika sherehe za umma. Umati mkubwa wa watu ulihudhuria kufurahia mateso yao na watazamaji waliangua vicheko na nderemo walipowaona wahanga wa mateso wakifa kwa uchungu mkubwa.PKSw 28.3

  Popote walipotafuta makimbilio, hawa wafuasi wa Kristo walisakwa kama wanyama wa mawindo. Walilazimika kujificha katika maeneo ya ukiwa na upweke. “Walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi” (Aya ya 37, 38). Mapango yalitumiwa na maelfu kama maficho. Chini ya milima nje ya mji wa Rumi, mahandaki marefu yalikuwa yamechorongwa katika ardhi na miamba; mtandao wenye giza na tata wa njia za mahandaki ulienea umbali wa maili kadhaa mbali na kuta za mji. Katika maficho haya ya chini ya ardhi wafuasi wa Kristo waliwazika wenzao waliokufa; na hapa pia, waliposhukiwa na kupigwa marufuku, walikuja kuishi hapa kama nyumbani kwao. Wakati Mpaji wa uzima atakapowaamsha wale waliopigana vita vizuri, wafia dini wengi kwa ajili ya Kristo watatoka katika hayo mahandaki yenye giza.PKSw 29.1

  Katika mateso makali sana hawa mashahidi wa Yesu waliihifadhi imani yao bila kuichafua. Pamoja na kuwa walinyang'anywa kila aina ya utulivu, wakiwa mahali pasipokuwa na mwanga wa jua, wakiishi gizani lakini katika kifua cha ardhi, hawakutamka neno lo lote la lawama. Kwa maneno ya imani, uvumilivu, na tumaini walitiana moyo kuvumilia umaskini na maumivu. Hasara ya baraka za duniani haikuweza kuwalazimisha kuikana imani yao kwa Kristo. Majaribu na mateso yalikuwa ngazi ya kuwaleta karibu zaidi na pumziko lao na zawadi yao.PKSw 29.2

  Kama watumishi wa zamani wa Mungu, wengi wao “waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora” (Aya ya 35). Haya yaliwakumbusha maneno ya Bwana wao, kuwa wanapoteswa kwa ajili ya Kristo walipaswa kufurahi kwa furaha kuu, kwa kuwa thawabu yao ingekuwa kubwa mbinguni; kwa kuwa ndivyo manabii walivyoteswa kabla yao. Walifurahi kwa sababu walihesabiwa kustahimili mateso kwa ajili ya ukweli, na nyimbo za shangwe zilipanda juu kutoka katikati ya chakarika ya ndimi za moto. Wakitazama juu kwa imani, walimwona Kristo na malaika wakiwa wameinama juu ya kuta za mbinguni, wakiwaangalia kwa shauku kubwa na wakiafiki msimamo wao imara. Sauti iliwaijia kutoka katika kiti cha enzi cha Mungu: “Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima” (Ufunuo 2:10).PKSw 29.3

  Ilikuwa juhudi za bure kwa Shetani kujaribu kuliharibu kanisa la Kristo kwa nguvu. Pambano kuu ambamo wanafunzi wa Yesu walisalimisha maisha yao halikwisha wakati hawa wabeba bendera waamanifu walipofia kwenye lindo lao. Kwa kushindwa kwao walishinda. Watenda kazi wa Mungu walichinjwa, lakini kazi Yake ilisonga mbele daima. Injili iliendelea kusambaa na idadi ya wafuasi wake ilizidi kuongezeka. Ilipenya katika maeneo yaliyokuwa hayafikiwi na majeshi ya Kirumi. Mkristo mmoja alisema, akibishana na watawala wa kipagani waliokuwa wakihamasisha mateso ya Wakristo: Mnaweza “kutuua, kututesa, kutuhukumu.... Uonevu wenu ni ushahidi kuwa sisi hatuna hatia.... Wala ukatili wenu ... hautawasaidia.” Huu ulikuwa mwaliko wenye nguvu zaidi wa kuwaleta wengine katika Ukristo. “Kwa kadiri mnavyotuchinja, ndivyo idadi yetu inavyozidi kuongezeka; damu ya Wakristo ni mbegu.”—Tertullian, Apology, paragraph 50.PKSw 29.4

  Maelfu walifungwa na kuchinjwa, lakini wengine waliibuka na kujaza nafasi zao. Na wale waliouawa kwa ajili ya imani yao walikufa katika Kristo na kuhesabiwa kuwa washindi. Walipiga vita vizuri, na wanatazamia kupokea taji ya utukufu wakati Kristo akija mara ya pili. Mateso waliyoyapata yaliwaleta karibu wao kwa wao na wote kwa pamoja karibu na Mwokozi wao. Mfano wao wa maisha na ushuhuda wa kifo chao vilikuwa ushuhuda wa daima wa ukweli; na wakati ilipotarajiwa kidogo sana, wafuasi wa Shetani waliachana na utumishi wa Shetani na kuja kutumika chini ya bendera ya Kristo.PKSw 30.1

  Shetani, hivyo basi, aliweka mipango kupigana vita kwa mafanikio zaidi dhidi ya serikali ya Mungu kwa kusimika bendera yake katika kanisa la Kikristo. Ikiwa wafuasi wa Kristo wangedanganywa na kuongozwa kumkosea Mungu, ndipo nguvu yao, ujasiri wao, na uimara wao vingehafifishwa, na wangekuwa mawindo rahisi ya Shetani.PKSw 30.2

  Adui mkuu sasa alijielekeza kupata kwa njia ya udanganyifu alichoshindwa kukipata kwa nguvu. Mateso yalikoma, na badala yake viliingizwa vishawishi vya hatari vya mafanikio ya muda na heshima ya dunia. Waabudu sanamu waliongozwa kupokea sehemu ya imani ya Kikristo, huku wakitupilia mbali kweli zingine muhimu. Walidai kumkiri Yesu kuwa Mwana wa Mungu na kuamini mauti na ufufuo Wake, lakini hawakushawishika kuwa ni wenye dhambi wala kuhisi haja ya toba au ya badiliko la moyo. Kwa wao kupunguza mambo fulani katika imani zao walipendekeza kuwa Wakristo nao wapunguze baadhi ya mambo, ili wote waungane kwenye jukwaa la imani ya Kikristo.PKSw 30.3

  Sasa kanisa lilikuwa katika hatari ya kutisha. Gereza, maumivu, moto, na upanga vilikuwa baraka ukilinganisha na mwelekeo huu. Baadhi ya Wakristo walisimama imara, wakisema kuwa wasingekubali kulegeza masharti. Baadhi yao waliunga mkono wazo la kulegeza masharti au kurekebisha baadhi ya vipengele vya imani yao na kuungana na waliokubali sehemu ya Ukristo, wakidai kuwa kufanya hivyo kungekuwa njia ya uongofu wao kamili. Huo ulikuwa wakati wa kilio kikuu kwa wafuasi wa Kristo waaminifu. Katika vazi la Ukristo bandia, Shetani alikuwa akijipenyeza katika kanisa, ili achafue imani yao na kugeuza akili zao kutoka kwenye neno la ukweli.PKSw 30.4

  Hatimaye Wakristo walio wengi walikubali kushusha viwango vyao, na muungano uliundwa kati ya Ukristo na upagani. Ingawa waabudu sanamu walidai kuwa wameongoka na kujiunga na kanisa, bado waliendelea kung'ang'ania ibada zao za sanamu, wakibadilisha tu vitu vya kuabudu kuwa sanamu za Yesu, Mariamu, na watakatifu. Chachu mbaya ya sanamu, iliyoingizwa kanisani kwa njia hiyo, iliendeleza kazi yake ya uharibifu. Mafundisho potofu, kaida za kishirikina, na sherehe za ibada ya sanamu zilijumuishwa katika imani na ibada ya kanisa. Wafuasi wa Kristo walipoungana na waabudu sanamu, dini ya Kikristo ilinajisiwa, na kanisa lilipoteza usafi na nguvu yake. Walikuwepo baadhi, hata hivyo, ambao hawakupotoshwa na makosa haya. Bado walidumisha uaminifu wao kwa Mwasisi wa ukweli na walimwabudu Mungu pekee.PKSw 30.5

  Kumekuwepo daima matabaka mawili miongoni mwa watu wanaodai kuwa wafuasi wa Kristo. Wakati tabaka moja linajifunza maisha ya Mwokozi na kwa dhati hutafuta kusahihisha kasoro zao na kufuata mfano wa Kristo, tabaka jingine hujiepusha na ukweli wa wazi, unaohusu maisha ya kila siku, ambao hufunua dosari zao. Hata wakati wa usafi wake wa juu kabisa, kanisa halikuundwa na watu ambao wote ni wa kweli, safi, na wa dhati. Mwokozi wetu alifundisha kuwa wale ambao kwa kuchagua waliendekeza dhambi hawakupaswa kupokelewa ndani ya kanisa; lakini alijihusisha na watu waliokuwa na kasoro katika tabia, na aliwapa msaada wa mafundisho na mfano Wake, ili wapate fursa ya kuona kasoro zao na kuzisahihisha. Miongoni mwa wale kumi na wawili alikuwemo msaliti. Yuda alipokelewa, siyo kwa sababu ya dosari zake za tabia, bali alipokelewa pamoja na kwamba alikuwa nazo. Aliunganishwa na wanafunzi, ili, kwa njia ya mafundisho ya mfano wa Kristo, aweze kujifunza mambo yanayounda tabia ya Kikristo, na hivyo aweze kuongozwa kuona dosari zake, atubu, na, kwa msaada wa neema ya Mungu, asafishe roho yake “kwa kuitii kweli.” Lakini Yuda hakutembea katika nuru ambayo kwa neema ya Mungu iliruhusiwa imwangazie. Kwa kuendekeza dhambi aliyaalika majaribu ya Shetani. Mazoea mabaya ya tabia yaliruhusiwa kutawala. Alisalimisha akili yake chini ya utawala wa nguvu za giza, alikasirika wakati makosa yake yalipokemewa, na hivyo aliongozwa kutenda uhalifu wa kutisha wa kumsaliti Bwana wake. Kadhalika, watu wote wanaolea uovu chini ya mwavuli wa utaua huwachukia wale wanaosumbua amani yao kwa kukemea njia yao ya dhambi. Fursa inayofaa ikijitokeza, kama Yuda, wanawasaliti wale ambao kwa faida yao, wanajaribu kuwakosoa.PKSw 31.1

  Mitume walikutana na watu kanisani waliodai kuwa wacha Mungu wakati kwa siri walilea uovu. Anania na Safira walisema uongo, wakijifanya kuwa wametoa vyote kwa Mungu, wakati kwa uchoyo walizuia sehemu kwa ajili yao wenyewe. Roho wa ukweli aliwafunulia mitume tabia halisi ya hawa wanaojifanya, na hukumu za Mungu zilifuta doa hili la uchafu kutoka katika kanisa lililokuwa safi. Ushuhuda huu wa wazi wa utambuzi wa Roho wa Kristo katika kanisa ulikuwa ni tishio kwa wanafiki na watenda maovu. Wasingedumu kushikamana kwa muda mrefu na wale ambao, kwa tabia na mwenendo, walikuwa wawakilishi wa kudumu wa Kristo; na majaribu na mateso yalipowajia wafuasi Wake, wale tu ambao waolikuwa tayari kuacha kila kitu kwa ajili ya ukweli ndio waliobaki kuwa wanafunzi Wake. Kwa hiyo, kwa kadiri mateso yalivyoendelea kuwepo, kanisa lilibaki kwa kiasi kikubwa likiwa safi. Lakini mateso yalipokoma, waongofu waliongezeka ambao baadhi yao hawakuwa waliojitoa kikamilifu, na njia ilifunguliwa kwa Shetani kukita mizizi ndani ya kanisa.PKSw 31.2

  Lakini hakuna muungano kati ya Mfalme wa nuru na mfalme wa giza, na haiwezekani kukawepo muungano kati ya wafuasi wao. Wakristo walipokubali kuungana na wale waliokuwa wameongoka nusu kutoka katika upagani, walifuata njia ambayo iliwapeleka mbali na ukweli zaidi na zaidi. Shetani alifurahia kwa kufanikiwa kudanganya idadi kubwa ya wafuasi wa Kristo. Ndipo alipotumia nguvu zake zaidi kuwabana hawa, na kuwafanya wawatese waliobaki wakiwa waaminifu kwa Mungu. Hakuna aliyejua vizuri zaidi kupinga imani ya kweli ya Kikristo kuliko wale ambao awali walikuwa watetezi wake; na hawa Wakristo waasi, wakiungana na wenzao ambao ni nusu wapagani, walielekeza vita yao dhidi ya vipengele muhimu sana vya mafundisho ya Kristo.PKSw 32.1

  Ilihitaji jitihada kubwa sana kwa wale ambao wangekuwa waaminifu kusimama imara dhidi ya udanganyifu na machukizo yaliyofichwa katika mavazi ya kikuhani na kuingizwa katika kanisa. Biblia haikukubaliwa kama kiwango cha imani. Fundisho la uhuru wa dini liliitwa fundisho la uongo na waliolitetea walichukiwa na kutengwa.PKSw 32.2

  Baada ya pambano la muda mrefu na kali, waaminifu wachache waliamua kuvunja uhusiano na kanisa lililoasi ikiwa lingeendelea kukataa kukumbatia uongo na ibada ya sanamu. Waliona kuwa kujitenga lilikuwa suala lisiloepukika ili waweze kutii neno la Mungu. Wasingeweza kuvumilia makosa ambayo yaliua roho zao, na kuonesha mfano ambao ungehatarisha imani ya watoto na wajukuu wao. Ili kupata amani na umoja walikuwa tayari kufanya na jambo lo lote ambalo lilikubaliana na uaminifu kwa Mungu; lakini waliamini kuwa amani isingeweza kununuliwa kwa kuvunja kanuni. Ikiwa umoja ulimaanisha kulegeza masharti ya ukweli na utakatifu, ni afadhali kuwepo tofauti, na hata vita.PKSw 32.3

  Ingekuwa vema kwa kanisa na ulimwengu ikiwa kanuni zilizowaongoza watu wale wenye msimamo zingeamshwa katika mioyo ya watu wanaodai kuwa watu wa Mungu. Kuna usingizi wa kutisha kuhusiana na mafundisho ambazo ni nguzo za imani ya Kikristo. Maoni yalikuwa yakinzidi kupata nguvu, kuwa, hata hivyo, haya siyo ya muhimu sana. Uozo huu unaoimarisha zaidi mikono ya mawakala wa Shetani, yaani nadharia potofu na uongo unaofisha ambao ulihatarisha maisha ya waaminifu walipoupinga na kuufunua katika zama zilizopita, sasa unakubaliwa na maelfu ya watu wanaodai kuwa wafuasi wa Kristo.PKSw 32.4

  Wakristo wa awali walikuwa kweli watu wa pekee sana. Tabia zao zisizo na doa na imani yao isiyoyumba vilikuwa ni kemeo la daima lililosumbua amani ya mwenye dhambi. Japokuwa walikuwa wachache kwa idadi, bila mali, cheo, au majina yenye heshima, walikuwa tishio kwa waovu mahali popote ambapo tabia na mafundisho yao vilijulikana. Kwa hiyo walichukiwa na watu waovu, sawa na jinsi Habili alivyochukiwa na Kaini mwovu. Kwa sababu ile ile ambayo kwayo Kaini alimwua Habili, waliotupilia mbali udhibiti wa Roho Mtakatifu, waliwaua watu wa Mungu. Ilikuwa ni kwa sababu hiyo hiyo Wayahudi walimkataa na kumsulibisha Mwokozi—kwa sababu usafi na utakatifu wa tabia Yake ulikuwa kemeo la kudumu kwa uchoyo na ufisadi wao. Tangu siku za Kristo mpaka sasa wanafunzi Wake waaminifu wameamsha chuki na upinzani wa wale wanaopenda na kufuata njia za dhambi.PKSw 33.1

  Hivyo basi, ni kwa jinsi gani injili inaweza kuitwa ujumbe wa amani? Isaya alipotabiri juu ya kuzaliwa kwa Masihi, alimpa jina,“Mfalme wa Amani.” Wakati malaika walipowatangazia wachungaji kuwa Kristo amezaliwa, waliimba juu ya mbuga za Bethlehemu: “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” (Luka 2:14). Kama vile kuna hali ya kukinzana kati ya matamko ya unabii na maneno ya Kristo: “Sikuja kuleta amani, bali upanga” (Mathayo 10:34). Lakini, zikieleweka vizuri, aya hizo mbili zinapatana kabisa. Injili ni ujumbe wa amani. Ukristo ni mfumo ambao, ukipokelewa na kutiiwa, unaweza kueneza amani, mapatano, na furaha duniani. Dini ya Kristo inawaunganisha wote wanaoyapokea mafundisho yake na kuwafanya kuwa ndugu wa karibu. Ilikuwa utume wa Yesu kuwapatanisha wanadamu na Mungu, na hivyo kumpatanisha mwanadamu na mwenzake. Lakni sehemu kubwa ya ulimwengu iko chini ya utawala wa Shetani, adui mkuu wa Kristo. Injili inawasilisha kwao kanuni za maisha ambazo zinakinzana na mazoea na shauku zao, na wanainuka dhidi yake. Wanachukia usafi unaofunua na kuhukumu dhambi zao, na wanatesa na kuharibu wale wanaotetea madai yake halali na matakatifu. Ni kwa maana hii—kwa sababu ya ukweli wake ulio juu injili inasababisha chuki na migogoro—ndiyo maana injili inaitwa upanga.PKSw 33.2

  Hekima ya Mungu isiyokuwa na maelezo inayoruhusu wenye haki wateswe na waovu imekuwa chanzo cha mashaka makubwa kwa wengi walio na imani dhaifu. Baadhi wanafikia hatua ya kupoteza tumaini kwa Mungu kwa sababu anaruhusu watu waovu kabisa wafanikiwe, wakati watu wazuri na walio safi kabisa wanaumia na kuteswa kwa nguvu zao za kikatili. Kwa jinsi gani, watu wanauliza, inawezekanaje Mungu ambaye ni mwenye haki na rehema, na ambaye hana nguvu katika nguvu zake, avumilie dhuluma na uonevu kama huo? Hili ni swali ambalo hatuna cho chote cha kufanya. Mungu ametupatia ushahidi wa kutosha wa upendo Wake, na hatuna mashaka kuhusu wema Wake kwa sababu hatuwezi kuelewa utaratibu wa hekma Yake. Mwokozi aliwaambia wanafunzi Wake, kwa kutarajia mashaka ambayo yangesonga roho zao nyakati za majaribu na giza: “Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi” (Yohana 15:20). Yesu aliteseka kwa ajili yetu zaidi kuliko ye yote miongoni mwa wafuasi Wake anavyoweza kuteseka kwa sababu ya ukatili wa wanadamu waovu. Wale ambao wameitwa kuteseka na kufa kwa ajili ya Kristo wanafuta nyayo za Mwana mpendwa wa Mungu.PKSw 33.3

  “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake” (2 Petro 3:9). Hasahau au kuwatelekeza watoto Wake; bali anawaruhusu waovu waoneshe tabia yao halisi, ili ye yote aliye na shauku ya kutenda mapenzi ya Mungu asidanganyike kuhusiana nao. Kadhalika, wenye haki wanawekwa katika tanuru ya mateso ili watakaswe; ili kwamba mfano wao uwashawishi wengine kuhusiana na uhalisia wa imani na utaua; na ili kwamba mwenendo wao usioyumba uwahukumu wasiomcha Mungu na wasioamini.PKSw 34.1

  Mungu anaruhusu watu waovu wafanikiwe na wadhihirishe uadui wao dhidi Yake, ili wakati watakapokuwa wamejaza kipimo cha uovu wao watu wote waweze kuona haki na rehema Yake wakati anapowaangamiza kabisa. Siku ya kisasi chake inakuja upesi, wakati wale wote ambao wamevunja sheria Yake na kuwakandamiza watu Wake watapokea zawadi stahiki ya matendo yao; wakati kila tendo la ukatili na uonevu kwa waaminifu wa Mungu litaadhibiwa kana kwamba ni Kristo Mwenyewe aliyetendewa.PKSw 34.2

  Kuna swali lingine muhimu ambalo lapaswa kujibiwa na makanisa ya leo. Mtume Paulo alisema “na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa” (2 Timotheo 3:12). Kwanini, sasa, mateso yanaonekana kwa kiasi kikubwa kusinzia? Sababu pekee ni kuwa kanisa limekubaliana na kiwango cha dunia na kwa hiyo haliamshi upinzani. Dini ambayo ipo katika siku zetu haina tabia iliyo safi na takatifu kama dini ya siku za Kristo na mitume. Ni kwa sababu tu ya roho ya mapatano na dhambi, ni kwa sababu kweli kuu za neno la Mungu hazitiliwi manani ipasavyo, ni kwa sababu kuna utaua kidogo katika kanisa, ni kana kwamba Ukristo unapendwa na ulimwengu. Hebu na kuwepo uamsho wa imani na nguvu ya kanisa la awali, na roho ya mateso itaamshwa, na mioto ya mateso makali itawashwa upya.PKSw 34.3

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents