Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 5—John Wycliffe

  Kabla ya Matengenezo, kulikuwa na nyakati ambazo nakala za Biblia zilikuwa chache sana, lakini Mungu hakuruhusu neno Lake liharibiwe kabisa. Kweli zake hazikupaswa kufichwa milele. Aliweza kuvunja kirahisi minyororo iliyofunga maneno ya uzima kama alivyoweza kufungua milango ya chuma ya magereza ili kuwaacha watumishi wake huru. Katika nchi tofauti za Ulaya watu walisukumwa na Roho wa Mungu kuutafuta ukweli kama kutafuta hazina iliyositirika. Kwa uongozi wa Mungu wakiyapata Maandiko Matakatifu, walipekua kurasa zake kwa shauku kubwa. Walikuwa tayari kuikubali nuru kwa gharama yo yote dhidi yao. Japokuwa hawakuweza kuona mambo yote kwa uwazi, waliwezeshwa kuelewa kweli nyingi zilizozikwa kwa muda mrefu. Wakiwa wajumbe waliotumwa na mbingu walisonga mbele, wakivunjavunja minyororo ya makosa na ushirikina, na kuwaita wale ambao kwa muda mrefu walikuwa utumwani, waamke na kupata uhuru wao.PKSw 57.1

  Isipokuwa tu miongoni mwa Wawaldensia, neno la Mungu lilifungiwa kwa zama nyingi katika lugha iliyoeleweka kwa wasomi tu; lakini wakati ulikuwa umewadia kwa Maandiko kutafsiriwa na kusambazwa kwa watu wa nchi zingine katika lugha zao za asili. Ulimwengu ulikuwa umepita katika usiku wake wa manane. Saa za giza zilikuwa zinaishia, na katika nchi nyingi kulitokea ishara za kuwadia kwa mapambazuko.PKSw 57.2

  Katika karne ya kumi na nne katika nchi ya Uingereza ilitokea “nyota ya asubuhi ya Matengenezo.” John Wycliffe alikuwa mjumbe wa matengenezo, siyo tu kwa ajili ya Uingereza peke yake, bali pia kwa ajili ya ulimwengu wote wa Ukristo. Upinzani mkuu dhidi ya Rumi ambao aliruhusiwa kuzungumzia haukuwa rahisi kamwe kunyamazishwa. Upinzani huo ulifungua pambano ambalo liliwezesha uwekwaji huru wa watu binafsi, wa makanisa, na wa mataifa.PKSw 57.3

  Wycliffe alipata elimu kubwa, na kwake kumcha Bwana kulikuwa chanzo cha hekima. Alijulikana chuoni kwa kicho chake na kwa talanta zake za ajabu na uwezo wake wa elimu. Kwa sababu ya kiu chake kwa ajili ya maarifa alijitahidi kupata ujuzi katika nyanja zote za elimu. Alipata elimu falsafa ya ualimu, sheria za kanisa, katika sheria za madai, hususani za nchi yake. Katika muda baada ya shughuli zake thamani ya mafunzo haya ya awali iliweza kuonekana. Uelewa wake wa kina wa falsafa na nadharia za wakati wake ulimwezesha kubaini dosari zake; na kwa kujifunza kwake sheria za kitaifa na kikanisa alijiandaa kwa ajili ya pambano kuu la kutafuta uhuru wa kiraia na wa kidini. Wakati ambapo aliweza kupata silaha kutoka katika neno la Mungu, alikuwa na uwezo wa kiakili upatikanao shuleni, na alizijua mbinu za wasomi. Nguvu ya uwezo wake wa kiakili na kiwango na kina cha ujuzi wake vilimpa heshima mbele ya marafiki na maadui zake. Wafuasi wake waliridhika kuwa shujaa wao alikuwa miongoni mwa watu wenye uwezo mkubwa wa kiakili kitaifa; na maadui zake walizuiwa kudharau kazi ya matengenezo kwa kubaini ujinga au udhaifu wa mtu aliyeunga mkono matengenezo.PKSw 57.4

  Wakati Wycliffe alipokuwa bado chuoni, alianza kujifunza Maandiko. Katika nyakati zile za awali, wakati Biblia ilipokuwa katika lugha za awali, wasomi waliweza kuifikia chemchemi ya ukweli, ambayo ilikuwa imefungiwa isifikiwe na matabaka ya watu wasio na elimu. Hivyo njia ilikuwa imeandaliwa kwa ajili ya kazi ya baadaye ya Wycliffe kama Mwanamatengenezo. Wasomi walikuwa wamejifunza neno la Mungu na walikuwa wamepata ukweli mkuu wa neema Yake ya bure ikiwa imefunuliwa humo. Katika mafundisho yao walikuwa wametawanya ukweli huu, na walikuwa wamewaongoza wengine waugeukie ujumbe huu ulio hai.PKSw 58.1

  Wakati Wycliffe alipojielekeza kuchunguza Maandiko, alianza uchunguzi wake kwa bidii ile ile iliyomwezesha kupata elimu ya shuleni. Tangu wakati huo alihisi kuwa na uhitaji mkubwa, ambao siyo masomo yake ya shuleni wala mafundisho ya kanisa yangeweza kuukidhi. Katika neno la Mungu alipata kile ambacho alikuwa akikitafuta kwa muda bila kukipata. Katika Maandiko aliweza kuona mpango wa wokovu ukiwa umefunuliwa na Kristo akiwa ameelezwa kama mtetezi wa mwanadamu. Alijitolea kuwa mtumishi wa Kristo na alidhamiria kutangaza kweli alizozigundua.PKSw 58.2

  Kama wanamatengenezo wengine, Wycliffe hakuweza, mwanzoni mwa kazi yake, kuona mapema kule ambapo matengenezo yangempeleka. Hakuwa na lengo la kuipinga Rumi moja kwa moja. Bali kuupenda ukweli kwa moyo kulimfanya aingie mgogoro dhidi ya uongo. Kwa kadiri alivyogundua kwa wazi makosa ya upapa, ndivyo alivyozidi kufundisha Biblia kwa bidii zaidi. Aliona kuwa Rumi ilikuwa imeacha neno la Mungu na kukumbatia mapokeo ya wanadamu; bila hofu aliwashitaki mapadri kwa kuacha Maandiko, na alidai kuwa Biblia irudishwe kwa watu na kwamba mamlaka yake iimarishwe kanisani. Alikuwa mwalimu mahiri na mhubiri fasaha, na maisha yake ya kila siku yalionesha ukweli aliouhubiri. Ujuzi wake wa Maandiko, nguvu ya hoja zake, na ujasiri na uadilifu wake usioyumba vilimfanya aheshimiwe na kukubaliwa na watu wengi. Watu wengi walikuwa wamechoshwa na imani yao ya awali waliona uovu uliokuwemo katika Kanisa la Kirumi, na walisifia ukweli uliohubiriwa na Wycliffe kwa shangwe ya wazi; lakini viongozi wa upapa walijazwa na hasira walipotambua kuwa huyu Mwanamatengenezo alikuwa akipata ukubali wa wengi zaidi kuliko wao.PKSw 58.3

  Wycliffe alikuwa mgunduzi makini wa makosa, na alikosoa bila hofu matumizi mabaya ya Maandiko yaliyoidhinishwa na mamlaka ya Rumi. Wakati akifanya kazi mchungaji wa mfalme, alisimama imara dhidi ya malipo ya kodi iliyodaiwa na papa kutoka kwa mfalme wa Uingereza na alionesha kuwa upapa kujipatia mamlaka juu ya watawala wa kiraia ilikuwa kinyume na busara ya kawaida na ufunuo wa neno la Mungu. Madai ya papa yalizusha hasira kubwa, na mafundisho ya Wycliffe yalikuwa na mvuto mkubwa katika akili za viongozi wa kitaifa. Mfalme na wasaidizi wake wa karibu waliungana kukataa madai ya mamlaka ya kidunia ya papa kwa kukataa kulipa kodi. Hivyo pigo kubwa liligonga ukuu wa upapa katika nchi ya Uingereza.PKSw 58.4

  Uovu mwingine ambao Mwanamatengenezo alipambana nao kwa muda mrefu na kwa nguvu nyingi ulikuwa uanzishwaji wa makundi ya watawa omba-omba. Watawa hawa walijaa katika nchi ya Uingereza, wakitia doa baya katika ukuu na mafanikio ya taifa. Uzalishaji, elimu, maadili, vyote viliguswa na mvuto unaodhoofisha. Maisha ya kivivu na omba-omba ya watawa siyo tu kuwa yalikuwa unyonyaji wa raslimali za watu, bali ulitia aibu kwa kazi ya uzalishaji. Vijana walikatishwa tamaa na kuharibiwa. Kwa mvuto wa hawa watawa watu wengi walivutwa kuingia nyumba za watawa na kuishi maisha ya kitawa, na walifanya jambo hili siyo tu bila ruhusa ya wazazi, bali pia bila kuwapa taarifa na kinyume na maagizo yao. Mmoja wa Mababa wa Kanisa la Kirumi akikazia madai ya utawa dhidi ya matakwa ya upendo na wajibu wa kidugu, alisema: “Hata kama baba yako angelala mbele ya mlango wako akilia na kuomboleza, na mama yako mzazi akikuonesha mwili uliokubeba na matiti yaliyokunyonyesha, inakupasa kuwakanyaga chini ya nyayo zako, na kwenda zako kwa Kristo.” Kwa “unyama huu wa kutisha,” kama Luther alivyouita baadaye, “ukiwa na sura ya mbwa mwitu na ukatili zaidi kuliko sura ya Ukristo na utu,” ndivyo mioyo ya watoto ilivyofanywa kuwa migumu dhidi ya wazazi wao.—Barnas Sears, The Life of Luther, ukurasa wa 70. Hivyo ndivyo viongozi wa upapa, kama Mafarisayo wa zamani, walivyoifanya amri ya Mungu ilivyovunjwa ili kufuata mapokeo. Kwa njia hiyo, nyumba ziliachwa ukiwa na wazazi walinyang'anywa watoto wao.PKSw 59.1

  Hata wanafunzi katika vyuo vikuu walidanganywa na mwonekano wa hawa watawa walishawishika kujiunga nao. Wengi wao baadaye walijutia hatua hiyo, baada ya kugundua kuwa wameharibu maisha yao na kuwaletea huzuni wazazi wao; lakini mara baada ya kunaswa katika mtego ilikuwa haiwezekani kupata uhuru wao tena. Wazazi wengi, kwa kuhofia mvuto wa watawa, walikataa kuwapeleka watoto wao katika vy vikuu. Kulikuwa na kuporomoka kwa idadi ya wanafunzi waliohudhuria masomo katika vyuo vikuu vya elimu. Shule zilikosa wanafunzi, na ujinga ulishamiri.PKSw 59.2

  Papa aliwapa hawa watawa mamlaka ya kusikiliza maungamo na kutoa msamaha. Jambo hili lilikuwa chanzo cha uovu mkuu. Wakijielekeza kukuza mapato yao, watawa walikuwa tayari kutoa msamaha kwa ye yote kiasi kwamba wahalifu wa kila namna waliwaendea, na, matokeo yake, maovu makubwa kuliko kawaida yaliongezeka kwa kasi kubwa.Wagonjwa na maskini waliachwa wateseke, wakati misaada ambayo ilipaswa kupelekwa kwa wahitaji ilipelekwa kwa watawa, ambao kwa kutumia vitisho, walidai sadaka kwa watu huku wakiwashutumu watu wasiowaletea zawadi watawa kuwa ni waasi. Pamoja na madai yao ya umasikini, utajiri wa watawa uliongeza daima, na majengo yao ya gharama na meza zao za kianasa zilifanya umaskini wa taifa uliokuwa ukiongezeka uonekane wazi zaidi. Na wakati wakitumia muda wao katika anasa na raha, walituma kwa niaba yao watu wajinga, ambao waliweza kusimulia hadithi, hekaya na vichekesho kuwafurahisha watu na kuwafanya wawe wahanga wa watawa. Hata hivyo watawa waliendelea kuwashikilia watu wengi katika ushirikina wao na waliwafanya waamini kuwa wajibu wao wa kidini ilikuwa kukiri ukuu wa papa, kuwaheshimu watakatifu, na kuwapa zawadi watawa, na kwamba kufanya hivyo kulitosha kabisa kuwapa nafasi mbinguni.PKSw 59.3

  Wasomi na wacha Mungu wengi walifanya kazi ya kuleta matengenezo katika makundi haya ya watawa bila mafanikio; lakini Wycliffe, kwa ufafanuzi wa kina zaidi, aligonga kwenye mzizi wa uovu, akitangaza kuwa mfumo wenyewe ulikuwa wa uongo na kuwa ulipaswa kutupiliwa mbali. Mijadala na maswali viliamshwa. Wakati watawa walipozunguka nchi nzima, wakiuza misamaha ya papa, wengi waliongozwa kutilia mashaka juu ya uwezekano wa kununua msamaha kwa pesa, walihoji kwa nini wasitafute msamaha kwa Mungu badala ya kuutafuta kwa papa wa Rumi. (Tazama Kiambatanisho.) Watu wengi walishtushwa na tamaa ya mali ya watawa, ambao uroho wao haukuonekana kuridhishwa. “Watawa na makasisi wa Rumi,” watu walisema, “wanatutafuna kama saratani. Inapasa Mungu atuokoe, vinginevyo watu wataangamia.”—D'Aubigne, b. 17, ch. 7. Kuficha tamaa yao, hawa watawa omba omba walidai walikuwa wakifuata mfano wa Mwokozi, wakisema kuwa Yesu na wanafunzi Wake walitegemezwa kwa ukarimu wa watu. Dai hili liliharibu kazi yao, kwa kuwa liliwafanya watu wasome wenyewe Biblia ili kujitafutia ukweli—jambo ambalo kati ya yote halikupendwa kabisa na Rumi. Akili za watu zilielekezwa kwenye Chanzo cha ukweli, jambo ambalo Rumi ilikusudia kuuficha.PKSw 60.1

  Wycliffe alianza kuandika na kuchapisha vijizuu dhidi ya watawa, siyo, hata hivyo, kwa lengo la kufanya malumbano nao, bali kuvuta akili za watu zielekee kwenye mafundisho ya Biblia na kwa Mtunzi wa Biblia. Alitangaza kuwa mamlaka ya kusamehe au kuondoa ushirika wa muumini ni ya papa na ya makasisi, na kuwa mtu hawezi kiuhalisia kuondolewa ushirika wake kanisani bila kwanza kuhukumiwa na Mungu. Hakuna njia bora zaidi kupita hii angeweza kuangusha mfumo mkubwa wa kiroho na kiutawala ambao papa alikuwa ameujenga ambamo roho na miili ilikuwa imeshikwa mateka.PKSw 60.2

  Tena Wycliffe alitakiwa kutetea haki za utawala wa Kiingereza dhidi ya ukandamizaji wa Rumi; na baada ya kuteuliwa kuwa mwakilishi wa mfalme, alitumia miaka miwili katika nchi ya Netherlands, kufanya mijadala na wawakalishi wa papa. Hapa alikutanishwa na viongozi wa kanisa kutoka Ufaransa, Italia na Uhispania, na alipata fursa ya kuona nyuma ya pazia na kujipatia ufahamu wa mambo mengi ambayo yangebaki kuwa siri kwake kama angekaa tu Uingereza. Alijifunza mengi ambayo yangeongeza hoja katika hotuba zake baada ya kazi ile. Kutoka kwa hawa wawakilishi wa utawala wa papa alijifunza kikamilifu uhalisia na malengo ya upapa. Alirudi Uingereza kuyarudia mafundisho yake ya awali kwa uwazi zaidi na kwa juhudi kubwa zaidi, akitangaza kuwa tamaa, kiburi na udanganyifu vilikuwa miungu ya Rumi.PKSw 60.3

  Katika moja ya vijizuu vyake alisema, akiongelea juu ya papa na wakusanyaji wake wa mapato:“Wanapora riziki za watu maskini wa nchi yetu, na wanachota hazina kubwa, kila mwaka, kutoka katika pesa ya mfalme, kwa ajili ya sakramenti na mambo ya kiroho, ambyo ni mafundisho ya uongo yaliyolaaniwa na rushwa ili kutoa vyeo kanisani, na wanawafanya Wakristo wakubaliane na wadumishe mafundisho ya uongo. Na kwa hakika ingawa nchi yetu ilikuwa na akiba kubwa ya dhahabu, na kwa kuwa hakuna mtu mwingine aliyeichukua isipokuwa huyu mkusanyaji wa kasisi wa ulimwengu, kwa mchakato wa kadiri muda unavyokwenda akiba hii lazima itaisha; kwa kuwa daima anaichukua kutoka katika nchi yetu, na hairudishi hata kidogo isipokuwa laana ya Mungu kwa sababu ya rushwa yake.”—John Lewis, History of the Life and Sufferings of J. Wiclif, ukurasa wa 37.PKSw 61.1

  Mara tu baada ya Wycliffe kurudi Uingereza, mfalme alimteua kuwa paroko wa Lutterworth. Huu ulikuwa uhakikisho kuwa mfalme angalau hakuwa amechukizwa na hotuba zake za uwazi na ukweli. Mvuto wa Wycliffe ulihisiwa katika uongozi na utendaji wa nyumba ya mfalme, kadhalika katika kuumba imani ya Taifa.PKSw 61.2

  Radi na ngurumo za upapa zilianza kurindima dhidi yake. Barua tatu za matamko ya kipapa zilitumwa Uingereza,—kwa chuo kikuu, kwa mfalme, na maaskofu,—zote zikiamrisha uchukuliwaji wa hatua za haraka na stahiki kumnyamazisha mwalimu wa uongo. (Augustus Neander, General History of the Christian Religion and Church, period 6, sec. 2, pt. 1, par. 8. Tazama pia Kiambatanisho). Kabla ya kuwasili kwa barua hizo, hata hivyo, maaskofu, kwa juhudi zao, walikuwa wamemwita Wycliffe mbele ya hao kwa ajili ya mashtaka. Lakini wawili miongoni mwa viongozi wakuu katika ufalme waliambatana naye mahakamani; na watu waliolizunguka jengo na kuingia ndani, waliwatisha sana majaji kiasi kwamba mashtaka yaliahirishwa kwa muda, na aliachiliwa aondoke kwa amani. Muda mfupi baadaye, Edward III, ambaye katika uzee wake maaskofu walikuwa wakitafuta kumshawishi awe kinyume cha Mwanamatengezo, alifariki dunia, na mlinzi wa zamani wa Wycliffe akawa kaimu mfalme.PKSw 61.3

  Lakini kuwasili kwa barua za papa kuliilazimisha Uingereza yote kumkamata na kumfunga Wycliffe. Hatua hizi zilielekeza moja kwa moja kuwa auawe kwa kuchomekwa juu ya mti wenye ncha kali. Ilionekana kana kwamba ilimpasa Wycliffe awe mawindo ya kisasi cha Rumi. Lakini Yeye alisema kwa mtu mmoja wa zamani, “Usiogope: ... Mimi ni ngao yako” (Mwanzo 15:1), alinyosha tena mkono Wake kumlinda mtumishi Wake. Mauti ilikuja, lakini siyo kwa Wycliffe, bali kwa papa aliyeamrisha kuangazwa kwa Wyclifee. Gregori XI alikufa, na viongozi wa kanisa waliokuwa wamekusanyika kuendesha mashtaka ya Wycliffe, walitawanyika.PKSw 62.1

  Uwezo wa Mungu ulidhibiti matukio kutoa fursa ya ukuaji wa Matengenezo. Kifo cha Gregori kilifuatiwa na uchaguzi wa mapapa wawili walio hasimu. Mamlaka mbili zinazozozana, kila moja ikidai kutokukosea, sasa zilidai utii. (Tazama Kiambatanisho.) Kila mmoja aliwaalika waaminifu kumuunga mkono kupambana na mwingine, akishinikiza madai yake kwa laana nzito dhidi ya maadui zake, na ahadi za zawadi mbinguni kwa wanaomwunga mkono. Tukio hili lilidhoofisha sana nguvu ya upapa. Makundi yanayopingana yalikuwa na kila kitu walichokihitaji kushambuliana wao kwa wao, na Wycliffe kwa muda fulani alipumzika. Matamko ya laana na lawama yaliruka kutoka kwa papa na kwenda kwa papa, na mito ya damu ilimwagwa kuunga mkono madai yao yanayopingana. Uhalifu na kashfa vilifurika kanisani. Wakati huo Mwanamatengenezo, katika ukimya wa mapumziko katika parokia yake ya Lutterworth, alikuwa akifanya kazi kwa bidii kuwaelekeza watu kwa Yesu Kristo, Mfalme wa Amani badala ya kuwaelekeza kwa mapapa waliokuwa wakigombana.PKSw 62.2

  Utengano, pamoja na mapambano na ufisadi uliotokana na utengano huo, viliandaa njia kwa ajili ya Matengenezo kwa kuwawezesha watu kuona upapa ulivyokuwa katika uhalisia wake. Katika kijizuu alichokichapisha, Kuhusu Utengano wa Mapapa, Wycliffe aliwaalika watu waamue ikiwa wenyewe hawa makasisi wawili hawakuwa wakisema ukweli kwa kulaumiana kuwa kila mmoja wao alikuwa mpinga Kristo. “Mungu,” alisema, “hawezi kuendelea kumruhusu shetani atawale kupitia kasisi mmoja tu, bali ... alileta utengano miongoni mwa hao wawili, ili kwamba watu, katika jina la Kristo, waweze kuwashinda kwa urahisi zaidi wote wawili.”—R. Vaughan, Life and Opinions of John de Wycliffe, vol. 2, uk. 6. Wycliffe, kama Bwana wake, alihubiri injili kwa maskini. Kwa kutokuridhishwa na usambazaji wa nuru katika nyumba zao za hali ya chini katika parokia yake ya Lutterworth, alidhamiria kuwa injili ipelekwe kila mahali katika nchi ya Uingereza. Kutekeleza jambo hili aliunda kikundi cha wahubiri, sahili, wacha Mungu, walioupenda ukweli na hawakupenda jambo lo lote zaidi ya kueneza injili. Watu hawa walienda kila mahali, wakifundisha katika masoko, katika mitaa ya miji mikubwa, na katika njia za vijijini. Waliwatafuta wazee, wagonjwa, na maskini, na waliwasimulia kwa furaha habari njema ya neema ya Mungu.PKSw 62.3

  Kama pprofesa wa eliungu wa Oxford, Wycliffe alihubiri neno la Mungu katika kumbi za chuo kikuu. Aliwasilisha kwa uaminifu sana ukweli kwa wanafunzi wake, kiasi kwamba walimpa cheo cha“daktari wa injili.” Lakini kazi kubwa kabisa kuliko zote katika maisha yake ilikuja kuwa tafsiri ya Maandiko katika lugha ya Kiingereza. Katika kitabu, On the Truth and Meaning of Scripture, alidokeza kusudio lake la kutafsiri Biblia, ili kwamba kila mtu katika nchi ya Uingereza aweze kusoma, katika lugha aliyozaliwa nayo, matendo makuu ya Mungu.PKSw 63.1

  Lakini kwa ghafla kazi zake zilikatizwa. Ingawa alikuwa bado hajafika umri wa miaka sitini, kazi nyingi bila kupumzika, kusoma, na mashambulizi ya adui zake vilidhoofisha nguvu zake na kumfanya azeeke mapema. Alishambuliwa na ugonjwa wa hatari. Habari hizi ziliwafurahisha sana watawa. Sasa walidhani atatubu kwa uchungu uovu alioufanyia kanisa, na waliharakisha kwenda katika chumba chake kusikiliza ungamo lake. Wawakilishi kutoka makundi manne ya kidini, wakiwa na viongozi wanne wa kiraia, walikusanyika kumzunguka mtu waliyedhani anaenda kufa. “Kifo kipo mdomoni mwako,” walisema; “hebu guswa na makosa yako, na kanusha mbele yetu yote uliyoyasema dhidi yetu.” Mwanamatengenezo aliwasikiliza akiwa kimya; halafu alimwambia mhudumu wake amwinue na kumkalisha kitandani, na, akiwakazia macho wakiwa wamesimama wakisubiri kanusho lake, alisema, kwa sauti imara, yenye nguvu ambayo mara nyingi iliwafanya watetemeke: “Sifi, bali nitaishi; na nitatangaza tena matendo maovu ya watawa.”—D'Aubigne, b. 17, ch. 7. Kwa mshangao, watawa walikimbia kutoka chumbani.PKSw 63.2

  Maneno ya Wycliffe yalitimia. Aliishi na kuweka katika mikono ya watu wa nchi yake silaha yenye nguvu nyingi kuliko silaha nyingine yo yote dhidi ya Rumi— aliwapa Biblia, silaha ya mbinguni ya kukombolea, kuangazia, na kuhubiria habari njema kwa watu. Vilikuwepo vikwazo vingi vya kushinda ili kutekeleza kazi hii. Wycliffe alilemewa na madhaifu mengi; alijua kuwa alikuwa na miaka michache iliyobaki ya yeye kufanya kazi; aliona upinzani ambao alipaswa kukabiliana nao; lakini, kwa kutiwa moyo na ahadi za neno la Mungu, alisonga mbele bila kukatishwa tamaa na kitu cho chote. Akiwa na nguvu kamili za kiakili, uzoefu mwingi, alihifadhiwa na kuandaliwa na Mungu kwa namna ya pekee sana kwa ajili ya kazi hii, kazi iliyokuwa kubwa zaidi kuliko kazi zingnine zote. Wakati ulimwengu wote wa Kikristo ulikuwa umegubikwa na taharuki, Mwanamatengenezo katika parokia yake ya Lutterworth, bila kusikia tufani iliyokuwa ikivuma huko nje, alikuwa akiendelea na kazi aliyochaguliwa kuifanya.PKSw 63.3

  Hatimaye kazi ilikamilika—tafsiri ya kwanza kabisa ya Biblia katika lugha ya Kiingereza ilipatikana. Neno la Mungu lilifunguliwa Uingereza. Mwanamatengenezo hakuogopa sasa gereza au mti wenye ncha kali. Alikuwa ameweka katika mikono ya Waingereza nuru ambayo isingeweza kuzimwa kamwe. Kwa kuwapa Biblia watu wa nchi yake, alikuwa amefanya kazi kubwa zaidi ya kukata minyororo ya ujinga na uovu, zaidi kuikomboa na kuiinua nchi yake, kuliko mafanikio mengine yo yote yaliyowahi kupatikana kwa njia ya vita.PKSw 63.4

  Sanaa ya kuchapisha vitabu ikiwa bado haijajulikana, ilikuwa kwa njia ya kazi iliyofanywa polepole na kwa uchovu mwingi nakala za Biblia ziliweza kuongezeka. Hamu ya kukipata kitabu hicho ilikuwa kubwa sana kiasi ambacho wengi walijitolea kuingia katika kazi ya kuinakili, lakini ilikuwa kwa shida sana waliofanya kazi ya kunakili waliweza kukidhi mahitaji. Baadhi ya wanunuzi waliokuwa na uwezo mkubwa wa kipesa walitaka Biblia nzima. Wengine walinunua sehemu tu. Katika matukio mengi, familia kadhaa ziliungana kununua nakala moja. Ni kwa njia hiyo Biblia ya Wycliffe ilifika katika nyumba za watu.PKSw 64.1

  Wito kwa watu kuwa watumie busara uliwaamsha kutoka katika utii usio na maswali kwa mafundisho yasiyohojiwa ya kipapa. Wycliffe sasa alifundisha mafundisho bainifu ya Uprotestanti—wokovu kwa njia ya imani katika Kristo, na kuwa Maandiko pekee ndiyo hayakosei. Wahubiri aliokuwa amewatuma walisambaza Biblia, pamoja na maandishi yake mwenyewe, kwa mafanikio makubwa kiasi kwamba imani hii mpya ilipokelewa na takribani nusu ya watu wa Uingereza.PKSw 64.2

  Kuonekana kwa Maandiko kulileta fadhaa kwa mamlaka za kanisa. Iliwapasa sasa kukabiliana na mamlaka iliyo na nguvu nyingi zaidi kuliko ya Wycliffe—mamlaka ambayo dhidi yake silaha zao zisingefua dafu. Kwa wakati huu hakukuwa na Sheria Uingereza iliyokataza Biblia, kwa kuwa kabla ya hapo ilikuwa haijachapishwa katika lugha ya Kiingereza. Sheria kama hizo zilitungwa baadaye na kutekelezwa kwa nguvu nyingi. Kwa muda fulani, pamoja na juhudi za makasisi, kulikuwepo na kipindi chenye fursa ya kusambaza neno la Mungu.PKSw 64.3

  Kwa mara nyingine tena viongozi wa upapa walipanga kunyamazisha sauti ya Mwanamatengenezo. Mbele ya mabaraza matatu aliitwa mfululizo kujibu mashitaka, lakini bila mafanikio. Kwanza kamati ya maaskofu iliyatangaza maandishi yake kuwa ya uzushi, na, wakimwongoa mfalme kijana, Richard II, upande wao, walipata amri ya mfalme ya kuwatupa gerezani wale wote ambao walishikilia mafundisho yaliyopigwa marufuku.PKSw 64.4

  Wycliffe alitoa wito kwa kamati ya maaskofu hadi kwa bunge; bila hofu alilishitaki kanisa kwa baraza la kitaifa akidai kanisa lifanye matengenezo kwa kuacha unyanyasaji na ufisadi ambao kanisa lilikuwa linaufanya. Kwa ushawishi mkubwa alionesha uporaji wa madaraka na ufisadi wa uongozi wa kipapa. Maadui zake walichanganywa. Marafiki na waungaji mkono wa Wycliffe walikuwa wamelazimishwa kujisalimisha, na ilikuwa imetarajiwa kwa ujasiri kuwa Mwanamatengenezo mwenyewe, katika uzee wake, akiwa peke yake na bila rafiki, angesujudia mamlaka ya muungano wa ufalme na upapa. Lakini badala ya matarajio hayo papa na wafuasi wake walijishuhdia wakishindwa. Bunge, likiwa limeamshwa na miito yenye nguvu ya Wycliffe, lilifuta amri ya mateso, na Mwanamatengenezo aliwekwa huru tena.PKSw 64.5

  Kwa mara ya tatu alishitakiwa, na sasa alishtakiwa mbele ya mahakama ya juu kabisa ya kanisa katika ufalme. Hapa hakuna upendeleo wo wote ambao ingeoneshwa kwa uzushi. Hapa hatimaye Rumi ingeshinda, na kazi ya Mwanamatengenezo ingekomeshwa. Hivyo ndivyo walivyofikiri viongozi wa upapa. Ikiwa wangefanikiwa kutimiza kusudi lao, Wycliffe angelazimika kukana mafundisho yake, au angeondoka mahakamani kwenda kuliwa na ndimi za moto.PKSw 65.1

  Lakini Wycliffe hakukana mafundisho yake; asingeweza kujifanya kukana. Bila hofu yo yote alidumu kusimamia mafundisho yake na alitupilia mbali mashtaka ya watesi wake. Akiacha kujiangalia mwenyewe, nafasi yake, na tukio lenyewe, aliwaita wasikilizaji wake mbele ya mahakama ya Mungu, na alipima nadharia zao na udanganyifu wao katika mizani ya ukweli wa milele. Nguvu ya Roho Mtakatifu ilihisiwa katika chumba cha baraza. Mguso wa Mungu ulikuwa juu ya wasikilizaji. Walionekana kana kwamba hawana nguvu ya kuondoka mahali pale. Kama mishale kutoka katika podo la Bwana, maneno ya Mwanamatengenezo yalichoma mioyo yao. Shtaka la uzushi, walilokuwa wamelileta dhidi yake, yeye kwa ushawishi wenye nguvu aliirusha kwao wenyewe. Kwa nini, alidai, walidiriki kueneza makosa? Kwa ajili ya mapato, mkafanyia biashara neema ya Mungu?PKSw 65.2

  “Mnafikiri mnapambana na nani?” aliwauliza hatimaye. Je, mnapambana na mzee aliyekuwa akichungulia kaburi? Hapana! Mnapambana na ukweli— Ukweli ulio na nguvu kubwa zaidi, na utawashinda ninyi.”—Wylie, b. 2, ch. 13. Baada ya kusema hayo, aliondoka mkutanoni, na hakuna hata mmoja wa maadui zake aliyejaribu kumzuia.PKSw 65.3

  Kazi ya Wycliffe ilikuwa kama imekwisha; bendera ya ukweli aliokuwa ameubeba kwa muda mrefu ulikuwa karibu kudondoka kutoka mkononi mwake; lakini kwa mara nyingine tena alipaswa kutoa ushuhuda kwa ajili ya injili. Ukweli ulikuwa utangazwe ukitokea katika ngome ya makosa. Wycliffe aliitwa kujibu mashtaka dhidi yake mbele ya mahakama ya kipapa mjini Roma, ambapo mara nyingi palimwaga damu ya watakatifu. Hakuwa kipofu kiasi cha kutoona hatari iliyotishia maisha yake, hata hivyo alikuwa tayari kutii wito wa mahakama kama isingekuwa kwa sababu ya kiharusi kilichomfanya ashindwe kusafiri. Lakini, ingawa sauti yake isingeweza kusikilizwa mjini Roma, aliweza kusema kwa njia ya barua, na alidhamiria kulifanya hili. Kutokea katika parokia yake Mwanamatengenezo alimwambia papa barua, ambayo, wakati ikiwa na heshima na roho ya Kikristo katika uandishi wake, ilikemea majivuno na kiburi cha papa.PKSw 65.4

  “Kwa hakika ninayo furaha,” alisema, “kufungua na kutangaza kwa kila mtu imani yangu, na hususani kwa askofu wa Roma: ambaye, kwa kadiri ninavyoamini kuwa sahihi na kweli, atakuwa tayari kuthibitisha imani yangu tajwa, au ikiwa itakuwa na makosa, basi ataiboresha. “Kwanza, ninachukulia kuwa injili ya Kristo ni mwili wote wa sheria ya Mungu.... Ninamwona na kumchukulia askofu wa Roma, yeye akiwa mwakilishi wa Kristo hapa duniani, kuwa amefungwa zaidi kuliko wengine wote, kwa sheria ya injili. Kwa kuwa ukuu miongoni mwa wanafunzi wa Kristo haukutokana na hadhi au heshima za kidunia, bali ulitokana na kuwa karibu na sahihi katika kumfuata Kristo katika maisha na tabia Yake.... Kristo, kwa muda wa uwepo Wake hapa, alikuwa maskini kuliko wote, na aliepuka na kutupilia mbali kabisa utawala na heshima za kidunia ..PKSw 66.1

  “Hakuna mtu mwaminifu ambaye atathubutu kumfuata papa mwenyewe au mtu mwingine ye yote mtakatifu miongoni mwa watu watakatifu, lakini katika mambo kama hayo kwa kadiri ambavyo amemfuata Bwana Yesu Kristo; kwa kuwa Petro na wana wa zebedayo, kwa kutamani heshima ya kidunia, kinyume na kufuata hatua za Kristo, alikosea, na hivyo katika makosa hayo hawapaswi kufuatwa....PKSw 66.2

  “Papa anapaswa kuachana na mamlaka ya kidunia na himaya na utawala wa kilimwengu, na hivyo kwa ufanisi kuelekeza nguvu zake zote katika kazi ya kichungaji; kwa kuwa hivyo ndivyo Kristo alivyofanya, na hususani mitume Wake. Hivyo basi, ikiwa nimekosea katika vipengele hivi, kwa unyenyekevu mkubwa najisalimisha kukosolewa, hata kama kwa kifo, ikiwa kuna haja ya kufanya hivyo; na ikiwa ningefanya kazi kulingana na mapenzi yangu au shauku ya nafsi yangu, ningetokea mbele ya askofu wa Roma; lakini Bwana ameniamuru kufanya kinyume chake, na amenifundisha kumtii Mungu kuliko mwanadamu.”PKSw 66.3

  Katika hitimisho alisema: “Hebu tumwombe Mungu, ili amwongoze Papa wetu Urban VI, kama alivyoanza, kwamba pamoja na viongozi wenzake wa kanisa wamfuate Bwana Yesu Kristo katika maisha na tabia; na kwamba waweze kuwafundisha watu kwa ufanisi, na kwamba wao, kadhalika, waweze kuwafuata katika hayo.”—John Foxe, Acts and Monuments, vol. 3, uk. 49, 50.PKSw 66.4

  Hivyo Wycliffe aliwasilisha kwa papa na makadinali wake unyenyekevu na upole wa Kristo, akionesha siyo tu kwao peke yao bali kwa Wakristo wote, tofauti kati yao na Bwana ambaye walidai kumwakilisha.PKSw 66.5

  Wycliffe alitarajia kuwa maisha yake yangekuwa gharama ya uaminifu wake. Mfalme, papa, na maaskofu waliungana kufanikisha kifo chake, na ilionekana kwa hakika kuwa miezi michache ilibaki kabla ya kutundikwa kwake kwenye mti wenye ncha kali. Lakini ujasiri wake haukutetereka. “Kwa nini unatafuta mbali taji ya kifo cha mfia dini?” alisema. “Hubiri injili ya Kristo kwa maaskofu wenye kiburi, na kifo cha mfia dini hutakikosa. Nini! Je, niwe hai halafu nikae kimya? ... Kamwe! Acha pigo lianguke, ninasubiria ujio wake.”—D'Aubigne, b. 17, ch. 8.PKSw 66.6

  Lakini ulinzi wa Mungu ulimkinga mtumishi Wake. Mtu ambaye kwa maisha yake yote amesimama kwa ujasiri akiutetea ukweli, katika hatari za maisha yake, haikutokea kwake kuwa mhanga wa chuki ya maadui zake. Wycliffe hakutafuta kujikinga mwenyewe, lakini Bwana alikuwa mlinzi wake; na sasa, maadui zake walipohisi uhakika wa mawindo yao, mkono wa Mungu ulimweka mbali nao. Katika kanisa lake la Lutterworth, alipokuwa akiendesha huduma ya meza ya Bwana, alianguka, kwa kupigwa na kiharusi, na kwa muda mfupi alisalimisha uhai wake.PKSw 67.1

  Mungu alikuwa amemchagulia Wycliffe kazi yake. Aliweka neno la kweli katika mdomo wake, na aliweka mlinzi kando yake ili neno hili liwaendee watu. Maisha yake yalilindwa, na kazi zake zilirefushwa, mpaka msingi ulipowekwa kwa ajili ya kazi kubwa ya Matengenezo.PKSw 67.2

  Wycliffe alitokea katika uficho wa Zama za Giza. Hakukuwa na ye yote kabla yake aliyetokea ambaye kutokana na kazi yake angejenga mfumo wake wa matengenezo. Akiwa amelelewa na kukuzwa kama Yohana Mbatizaji kutimiza utume mahsusi, alikuwa mtangulizi wa zama mpya. Pamoja na hayo katika mfumo wa ukweli aliouwasilisha kulikuwepo umoja na ukamilifu ambao Wanamatengenezo waliofuata baadaye hawakuupita, na ambao hawakuweza kuufikia, hata miaka mia moja baadaye. Kwa hiyo, msingi mpana na wa kina ulikuwa umekwisha kuwekwa, muundo ulikuwa imara na wa kweli, kiasi kwamba haukuhitaji kujengwa upya na wale waliokuja baadaye.PKSw 67.3

  Vuguvugu kubwa ambalo Wycliffe alilizindua, ambalo lililenga kukomboa dhamiri na akili, na lililoyaweka huru mataifa yaliyokuwa yamefungwa kwa muda mrefu katika gari la ushindi wa Rumi, lilitokana na Biblia. Hapa ndipo kulikuwepo na chanzo cha mkondo wa baraka, ambazo, kama maji ya uzima, yametiririka tangu karne ya kumi na nne. Wycliffe aliyakubali Maandiko Matakatifu kwa imani thabiti kama ufunuo uliovuviwa wa mapenzi ya Mungu, kanuni toshelevu la imani na utendaji. Alielimishwa kuchukulia Kanisa la Rumi kama mamlaka ya Kimungu, isiyokosea, na kulikubali kwa uchaji usio na maswali mafundisho na desturi za miaka elfu moja; lakini aligeuka na kuyaacha hayo yote na kulisikiliza neno takatifu la Mungu. Hii ilikuwa mamlaka aliyohimiza watu waitambue. Badala ya kanisa kusema kupitia kwa papa, alitangaza mamlaka pekee ya kweli ni sauti ya Mungu akisema kupitia neno Lake. Na hakufundisha siyo tu kuwa Biblia ni ufunuo kamili wa mapenzi ya Mungu, lakini kwamba Roho Mtakatifu ni mtafsiri pekee wa Maandiko, na kwamba kila mtu ni, kwa njia ya kujifunza mafundisho yake, kujifunza wajibu wake kwa ajili yake. Hivyo aligeuza akili za watu kutoka kwa papa na kanisa la Rumi na kuzipeleka kwa neno la Mungu.PKSw 67.4

  Wycliffe alikuwa mmoja wa Wanamatengenezo wakuu sana. Katika upana wa akili, na uwazi wa fikra, katika uimara wa kudumisha ukweli, na katika ujasiri wa kuulinda ukweli, alilingana na watu wachache waliotokea baada yake. Usafi wa maisha, juhudi isiyochoshwa katika kujifunza na kazi, uadilifu usiochafuliwa, na upendo kama wa Kristo na uaminifu katika huduma yake, zilikuwa sifa za Mwanamatengenezo wa kwanza. Na jambo hili lilikuwa hivyo licha ya giza la kiakili na ufisadi wa kimaadili wa zama alizozaliwa na kuishi.PKSw 68.1

  Tabia ya Wycliffe ni ushuhuda wa nguvu inayoelimisha, na kubadilisha ya Maandiko Matakatifu. Biblia ndiyo ilimfanya awe vile alivyokuwa. Juhudi ya kuzishika kweli kuu za ufunuo wa neno la Mungu hutoa upya na nguvu kwa talanta zingine zote. Inapanua akili, hunoa uwezo wa ufahamu, na hukomaza maamuzi. Kujifunza Biblia kunawezesha kila wazo, hisia, na matumaini zaidi kuliko vyanzo vingine vyote vya mafunzo vinavyoweza kufanywa. Inatoa uimara wa nia, uvumilivu, ujasiri, na ustahimilivu; inalainisha tabia na kutakasa roho. Mafundisho ya dhati, yenye kicho, ya Maandiko, hukutanisha akili ya mwanafunzi na akili isiyokuwa na mipaka, inaweza kuupatia ulimwengu watu wenye nguvu zaidi za kiakili na za kiutendaji, hali kadhalika inatoa kanuni za juu zaidi, kuliko zile zinazotolewa na falsafa ya kibinadamu. “Kufafanusha maneno yako,” anasema mtunga zaburi, “kwatia nuru; Na kumfahamisha mjinga” (Zaburi 119:130).PKSw 68.2

  Mafundisho makuu yaliyofundishwa na Wycliffe yaliendelea kuenea kwa muda mrefu; wafuasi wake, waliojulikana kama Wawiklifiti as “Wycliffites” na “Lollards,” siyo tu kuwa walifika kila sehemu ya nchi ya Uingereza, bali walitawanyika pia katika nchi zingine wakichukua ujumbe wa injili. Sasa kwa kuwa kiongozi wao alikuwa ameondolewa, wahubiri walifanya kazi kwa bidii kubwa zaidi kuliko hapo mwanzo, na watu wengi walifurika kusikiliza mafundisho yao. Baadhi ya waheshimiwa, na hata mke wa mfalme, walikuwa miongoni mwa waongofu. Katika sehemu nyingi kulikuwepo na matengenezo ya dhahiri katika mienendo ya watu, na alama za ibada ya sanamu ya Urumi ziliondolewa makanisani. Lakini dhoruba isiyokuwa na huruma ya mateso ilipasuka juu ya wale wote waliodiriki kuikubali Biblia kama mwongozo wao. Wafalme wa Kiingereza, wakitamani kuimarisha nguvu zao kwa kupata msaada wa Roma, hawakusita kuwatoa kafara Wanamatengenezo. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Uingereza mti wenye ncha kali uliamriwa dhidi ta wanafunzi wa injili. Kufia dini kulifuata kufia dini. Watetezi wa ukweli, wakipigwa marufuku na kuteswa, waliweza tu kumwaga vilio vyao katika masikio ya Bwana wa Sabato. Wakiwindwa kama maadui wa kanisa na wasaliti wa ufalme, waliendelea kuhubiri kisiri siri, wakijificha kwa kadiri walivyoweza katika nyumba za watu maskini, na mara nyingi wakijificha katika mashimo na mapango.PKSw 68.3

  Licha ya moto wa mateso, upinzani wa kimya kimya, kicho, dhati, subira, dhidi ya ufisadi wa kidini uliokuwepo wakati ule uliendelea kusemwa kwa karne nyingi. Wakristo wa siku zile za awali walikuwa na uelewa mdogo tu wa ukweli, lakini walikuwa wamejifunza kulipenda na kulitii neno la Mungu, na kwa uvumilivu mwingi waliteseka kwa ajili ya huo ukweli. Kama wanafunzi katika siku za mitume, wengi walitoa kafara mali zao za kidunia kwa ajili ya kazi ya Kristo. Wale walioruhusiwa kuishi katika nyumba zao kwa furaha waliwahifadhi ndugu zao waliofukuzwa, na wakati na wao waliokimbizwa, kwa furaha, walikubali kuishi maisha ya kukataliwa. Maelfu, ni kweli, kwa kutishwa na hasira ya watesaji, walinunua uhuru wao kwa kafara ya imani yao, na waliotoka katika magereza yao, walivaa majoho ya toba, kutangaza kuikana imani yao. Lakini idadi haikuwa ndogo—miongoni mwao walikuwemo watu wenye hadhi ya juu na watu wa hali ya chini—walioshuhudia bila hofu ukweli katika vyumba vya magereza, katika “Minara ya Lollard,” na katikati ya mateso na ndimi za moto, wakifurahia kuwa walihesabiwa kustahili kujua “ushirika wa mateso Yake.”PKSw 69.1

  Wafuasi wa upapa walishindwa kutekeleza kusudi lao kwa Wycliffe wakati wa uhai wake, na chuki yao haikuridhishwa wakati mwili wake ukiwa umepumzika kimya kaburini. Kwa amri ya Baraza la Constance, zaidi ya miaka arobaini baada ya kifo chake mifupa yake ilifukuliwa na kuchomwa moto hadharani, na majivu yalitupwa katika kijito kilichokuwa jirani. “Kijito,” anasema mwandishi wa zamani, “kimesafirisha majivu yake katika mto wa Avon, Avon utayapeleka katika mto wa Severn, Severn utayapeleka katika bahari nyembamba, na bahari nyembamba zitayapeleka katika bahari kuu. Na hivyo majivu ya Wycliffe ni ishara ya mafundisho yake, ambayo sasa yamesambaa ulimwenguni kote.”—T. Fuller, Church History of Britain, b. 4, sec. 2, par. 54. Maadui zake hawakuelewa maana ya tendo lao ovu. Ilikuwa kwa njia ya maandishi ya John Huss wa Bohemia, alioongozwa kuyakataa mengi ya makosa ya Urumi na kujiunga na kazi ya matengenezo. Hivyo katika nchi hizi mbili, ambazo zimetenganishwa na umbali mkubwa, mbegu ya ukweli ilipandwa. Kutoka Bohemia kazi iliendelea katika nchi zingine. Akili za watu zilielekezwa kwa neno la Mungu lililokuwa limesahauliwa kwa muda mrefu. Mkono wa Mungu ulikuwa ukiandaa njia kwa ajili ya Matengenezo Makuu.PKSw 69.2

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents