Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 8—Luther Mbele ya Baraza

  Mfalme mpya, Charles V, alikuwa ndiyo tu amesimikwa rasmi katika kiti cha enzi cha Ujerumani, na wawakilishi wa Roma waliharakisha kumpelekea salamu zao za pongezi na kumshawishi mfalme atumie madaraka yake kukomesha Matengenezo. Kwa upande mwingine, elekta wa Saxony, ambaye kwa sehemu kubwa, alikuwa amechangia katika kumweka Charles madarakani, alimsihi asichukue hatua yo yote dhidi ya Luther bila kumpa nafasi ya kumsikiliza. Kwa sababu hiyo mfalme aliwekwa katika mtanziko na usumbufu mkubwa. Wawakilishi wa papa wasingeridhishwa na kitu cho chote pungufu ya amri ya kumhukumu kifo Luther. Elekta wa Saxony alikuwa ametangaza kwa nguvu kuwa “siyo ofisi ya mfalme mkuu wala mtu ye yote alikuwa ameonesha kuwa maandishi ya Luther yalikuwa yamekanushwa;” hivyo basi aliomba “kuwa Dkt. Luther apewe hakikisho la usalama, ili aweze kufika mbele ya mahakama ya majaji wasomi, wacha Mungu, na wasio na upendeleo.”—D'Aubigne, b. 6, ch. 11.PKSw 107.1

  Macho na masikio ya wahusika wote sasa yalielekezwa kwa mkutano wa viongozi wa majimbo ya Ujerumani ulioitishwa kukaa katika jiji la Worms mara tu baada ya Charles kutawazwa na kuwa mfalme ya dola ya Ujerumani. Kulikuwepo masuala na maslahi muhimu ya kisiasa yaliyokusudiwa kujadiliwa katika baraza lile kuu la kitaifa; kwa mara ya kwanza wakuu wa Ujerumani walikuwa wanakutana na mfalme wao kijana katika mkutano wa mashauriano. Kutoka katika nchi zote zilizoko chini ya Uroma walikuja viongozi wa kanisa na wa serikali. Viongozi wa serikali, watu wa vyeo vya juu, wenye mamlaka makubwa, wakiwa na wivu wa kutetea madaraka yao na nafasi zao za kurithishwa; viongozi wa juu wa kanisa, wakiwa na utambuzi wa ukuu wao na nguvu zao; viongozi wakuu wa mhimili wa mahakama na walinzi wao wenye silaha; na mabalozi kutoka nchi za kigeni na za mbali,-wote walikusanyika katika jiji la Worms. Pamoja na kusanyiko hilo kubwa, shauku yao kubwa ilikuwa juu ya kazi ya Mwanamatengenezo wa Saxony.PKSw 107.2

  Awali, Charles alikuwa amemwagiza kiongozi wa Saxony amlete Luther mbele ya Baraza la Kitaifa, akimhakikishia ulinzi, na akiahidi mjadala huru, mbele ya watu wenye uwezo, juu ya masuala yanayobishaniwa. Luther alikuwa na shauku ya kufika mbele ya mfalme. Afya yake wakati huu ilikuwa dhaifu zaidi; hata hivyo alimwandikia kiongozi wa Saxony: “Ikiwa siwezi kwenda Worms nikiwa na afya njema, nitabebwa kwenda huko, nikiwa mgonjwa hivi hivi. Kwa kuwa ikiwa mfalme ameniita, siwezi kuwa na mashaka kuwa ni wito wa Mungu Mwenyewe. Ikiwa wana nia ya kunifanyia ukatili, na jambo hilo linawezekana kabisa (kwa kuwa siyo kwa maagizo yao wenyewe ambayo kwayo wananiamuru niende mbele yao), ninaweka jambo hilo mikononi mwa Bwana. Yeye bado Yu hai na bado anatawala, Yeye aliyehifadhi vijana watatu wasiungue katika tanuru la moto. Ikiwa hataniokoa, maisha yangu yana umuhimu mdogo sana. Hebu tusiruhusu injili kuaibishwa mbele ya watu waovu, na hebu tumwage damu yetu kwa ajili ya injili, ili tusitoe nafasi ya wao kushinda. Siyo juu yangu kuamua ikiwa maisha yangu au kifo changu vitachangia zaidi katika wokovu wa wote.... Unaweza kutarajia yote kutoka kwangu... isipokuwa kukimbia na kukana. Kukimbia siwezi, na kukana haiwezekani kabisa.”—Ibid., b. 7, ch. 1.PKSw 107.3

  Baada ya habari kusambaa jijini Worms kuwa Luther alikuwa anakuja kusimama mbele ya Baraza Kuu la Kitaifa, msisimko mkubwa uliibuka. Aleanda, mwakilishi wa papa ambaye kesi hiyo ilikuwa imewekwa chini yake hasa, alishtuka na kukasirishwa sana. Aliona kuwa matokeo yangekuwa ya hatari kwa maslahi ya upapa. Kuanzisha uchunguzi kuhusiana na kesi ambayo papa alikuwa tayari ameshatangaza hukumu ya adhabu ingekuwa ni kuonesha dharau kwa mamlaka ya papa mkuu. Zaidi ya hapo, aliogopa kuwa hoja fasaha na zenye nguvu za mtu huyu zingeweza kugeuza viongozi wengi mbali na maslahi ya papa. Hivyo basi, kwa mkazo mkubwa alimsihi Charles asimlete Luther mbele ya Baraza Kuu la Worms. Karibu na wakati huu barua iliyotangaza kuwa Luther ameshatengwa na Kanisa ilichapishwa; na hili, likijumuishwa na maneno ya mwakilishi wa papa, vilimshawishi mfalme kukubali. Alimwandikia kiongozi wa Saxony kuwa ikiwa Luther hawezi kukana, inampasa abakie Wittenberg.PKSw 108.1

  Kwa kutokuridhishwa na ushindi huu, Aleanda alifanya kazi kwa nguvu zake zote na hila zote alizoweza kuwezesha adhabu ya Luther. Kwa juhudi kubwa ambayo ingestahili kwa kazi bora zaidi kuliko hiyo, alishikiniza suala hilo lifanyiwe kazi na viongozi wa serikali, maaskofu, na wajumbe wengine wa baraza kuu la kitaifa, akimshitaki Mwanamatengenezo kwa kosa la“ushawishi, uasi, ufisadi, na kufuru.” Lakini ukali na hasira vilivyooneshwa na mwakilishi wa papa vilifunua roho iliyokuwa ikimwendesha. “Anasukumwa na chuki na kisasi,” yalikuwa ndiyo maoni ya jumla, “zaidi kuliko imani na kicho.”—Ibid., b. 7, ch. 1. Wengi wa wajumbe wa Baraza Kuu la Kitaifa waliazimia kuwa upande wa Luther zaidi kuliko hata kabla ya wakati huo.PKSw 108.2

  Kwa juhudi zilizoongezwa mara dufu Aleanda alimbana mfalme atekeleze amri za papa. Lakini kwa sheria za Ujerumani hili lisingeweza kufanyika bila ridhaa ya viongozi wengine wote wa majimbo; na, kwa kuzidiwa na juhudi za mwakilishi wa papa, Charles alimwamuru Aleanda alete madai yake mbele ya Baraza Kuu la Kitaifa. “Ilikuwa siku ya kujivunia kwa mjumbe wa papa, ... mama na bimkubwa wa makanisa yote.” Alipaswa kuthibitisha ukuu wa Petro mbele ya wenye mamlaka na wakuu wa ulimwengu wa Kikristo. “ Alikuwa na karama ya ufasaha, na alikuwa na uwezo uliokidhi hitaji la tukio la siku hiyo. Uongozi wa Mungu ulipanga kuwa Roma itangulie kwa njia ya waongeaji wake mahiri mbele ya mkutano mkuu wa majaji, kabla kanisa halijahukumiwa.”—Wylie, b. 6, ch. 4. Kwa shingo upande wale waliokuwa upande wa Mwanamatengenezo walijiandaa kusikiliza hotuba ya Aleanda. Kiongozi wa Saxony hakuhudhuria katika kikao hicho, lakini kwa maelekezo yake baadhi ya wajumbe wake walihudhuria ili kuandika maelezo ya hotuba ya mjumbe wa papa.PKSw 108.3

  Kwa nguvu zote za usomi na ufasaha, Aleanda alijipanga kuushinda ukweli. Shitaka baada ya shitaka lilirushwa dhidi ya Luther kuonesha kuwa Luther ni adui wa kanisa na serikali, na adui wa watu walio hai na walio kufa, adui wa viongozi wa kanisa na walei, adui wa mabaraza na Wakristo binafsi. “Katika makosa ya Luther kuna mambo ya kutosha” alitangaza, kusababisha kuchomwa moto kwa “wazushi laki moja.” Kwa kumalizia alijaribu kuonesha dharau dhidi ya wafuasi wa imani ya matengenezo: “Hawa wafuasi wa Luther ni kitu gani? Ni kikundi cha waalimu waasi, makasisi fisadi, watawa wasio waadilifu, wanasheria wasiojua kitu, na viongozi walioharibikiwa, wakijumuisha watu wa kawaida ambao wamepotoshwa na kudanganywa na hawa viongozi. Ni kwa kiasi gani jumuia ya Wakatoliki iko juu zaidi katika idadi, uwezo, na nguvu! Amri ya pamoja itakayotolewa na mkutano huu makini itaelimisha watu wa kawaida, itawaonya watu wenye busara, itawapa msimamo watu wanaotatanishwa, na itawapa nguvu watu walio dhaifu.”— D'Aubigne, b. 7, ch. 3.PKSw 109.1

  Kwa silaha kama hizo hizo watetezi wa ukweli katika zama zote wamekuwa wakishambuliwa. Hoja hizo hizo zimetolewa dhidi ya watu wote wanaojaribu kuwasilisha, dhidi ya makosa yaliyozoeleka, neno la wazi na la moja kwa moja la mafundisho ya neno la Mungu. “Hawa wanaohubiri mafundisho mapya ni akina nani?” Wanasema wale wanaotamani dini inayopendwa na wengi. “Ni watu wasio na elimu, idadi yao ni ndogo, na watu wa tabaka la watu walio maskini sana. Na bado wanadai kuwa wanao ukweli, na kwamba wao ni watu ambao wamechaguliwa na Mungu. Ni wajinga na wamedanganyika. Kanisa letu ni kubwa na lina idadi kubwa na mvuto mkubwa kiasi gani! Ni watu wangapi wana uwezo mkubwa na elimu ya juu miongoni mwetu! Ni nguvu kubwa kiasi gani iko upande wetu!” Hizi ndizo hoja ambazo zina mvuto mkubwa ulimwenguni; lakini peke yake hazitoshi sasa kuliko zilivyokuwa siku za Mwanamatengenezo.PKSw 109.2

  Matengenezo hayakuishia kwa Luther kama wengi wanavyodhani. Yanapaswa kuendelea mpaka mwisho wa historia ya ulimwengu huu. Luther alikuwa na kazi kubwa ya kufanya katika kuwaakisia wengine nuru ambayo Mungu aliruhusu imwangazie; hata hivyo hakupokea nuru yote ambayo ilipaswa itolewe kwa ulimwengu. Tangu wakati ule mpaka wakati huu, nuru mpya imeendelea kuangazia katika Maandiko, na kweli zimekuwa daima zikifunuliwa.PKSw 109.3

  Hotuba ya mjumbe wa papa ilikuwa na mguso mkubwa kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Kitaifa. Luther hakuwepo mkutanoni, akiwa na kweli za wazi na zinazoshawishi za neno la Mungu, kumzima shujaa wa upapa. Hakuna jaribio lo lote lililofanywa la kumtetea Mwanamatengenezo. Kulikuwepo na mwelekeo wa wazi siyo tu wa kumhukumu yeye na mafundisho aliyoyafundisha, lakini ikiwezekana kung'oa mizizi ya uzushi. Roma ilikuwa na fursa kubwa ya kutetea msimamo wake. Yote ambayo Kanisa lingeweza kusema katika kuthibitisha msimamo wake yalikuwa yamesemwa. Lakini kile kilichoonekana kama ushindi kwa Kanisa kiliashiria kushindwa kwake. Tangu wakati huo tofauti kati ya ukweli na uongo ilionekana waziwazi, kwa sababu wangepanua wigo wa mgogoro na kuuanika hadharani. Tangu siku hiyo Roma isingekuwa salama kama ilivyosimama kabla ya hapo.PKSw 110.1

  Wakati wajumbe wengi wa Baraza Kuu la Kitaifa wasingesita kumtoa Luther kwa kisasi cha Roma, wengi wao waliona na walichukia uovu uliokuwemo kanisani, na walitamani kuondolewa kwa mabaya yaliyowapata watu wa Ujerumani kama matokeo ya ufisadi na tamaa ya viongozi wa kanisa. Mjumbe wa papa aliwasilisha utawala wa papa kwa kupendelea upapa kwa kiwango cha juu kabisa. Sasa Bwana alimsukuma mjumbe mmoja wa Baraza kutoa maelezo ya kweli kuhusu madhara ya ukatili wa upapa. Kwa ujasiri wa kitawala, Mtoto wa Mfalme wa Saxony alisimama katika kusanyiko lile la watawala na kutaja kwa usahihi wa kutisha uongo na machukizo ya upapa, na matokeo yake mabaya. Katika kufunga alisema:PKSw 110.2

  “Haya ndiyo maudhi yanayopiga kelele dhidi ya Roma. Aibu yote imewekwa pembeni, na lengo lao pekee ni ... pesa, pesa, pesa, ... kiasi kwamba wahubiri ambao wangefundisha ukweli, hawasemi kitu zaidi ya uwongo, na siyo tu kuwa wanavumiliwa, bali pia wanapewa zawadi, kwa sababu kwa kadiri uongo wao unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo mapato yao yanavyokuwa makubwa zaidi. Ni kutoka katika chemchemi hii chafu ndiko maji haya machafu hutiririka. Ufisadi hunyosha mkono hadi ubadhirifu.... Kwa namna ya ajabu sana, ni kashifa inayosababishwa na viongozi wa dini inayorushia watu wengi walio maskini katika hukumu ya milele. Matengenezo makubwa inapaswa yafanyike.”—Ibid., b. 7, ch. 4.PKSw 110.3

  Ukosoaji wenye nguvu na makini dhidi ya maovu ya upapa usingeweza kuwasilishwa na Luther binafsi; na ukweli kuwa msemaji alikuwa adui mkubwa wa Mwana matengenezo uliyapa maneno yake mvuto mkubwa.PKSw 110.4

  Kama macho ya wajumbe wa mkutano yangefumbuliwa, wangeweza kuwaona malaika wa Mungu kati kati yao, wakimulika nuru dhidi ya giza la makosa na kufungua akili na mioyo ya watu ili waupokee ukweli. Ilikuwa nguvu ya Mungu wa ukweli na hekima iliyowaongoza hata maadui wa matengenezo, na hivyo iliandaa njia kwa ajili ya kazi kubwa iliyokuwa karibu kufanyika. Martin Luther hakuwepo; lakini sauti ya Yule aliyekuwa mkubwa zaidi kuliko Luther ilisikika katika mkutano ule.PKSw 110.5

  Kamati iliundwa mara moja na Baraza kuandaa orodha ya manyanyaso ya upapa yaliyowalemea watu wa Ujerumani. Orodha hii, iliyokuwa na vipengele mahususi mia moja na moja, iliwakilishwa kwa mfalme, ikiwa na ombi kuwa achukue hatua za haraka kuondoa manyanyaso hayo. “Ni hasara kubwa kiasi gani kwa kupotea roho za Wakristo,” waombaji walisema, “ni vitisho vingapi, unyang'anyi mkubwa kiasi gani vinawakabili watu, kwa sababu ya tamaa ya kiongozi wa kiroho wa Ukristo! Ni wajibu wetu kuzuia maumivu na kudhalilishwa kwa watu wetu. Kwa sababu hiyo kwa unyenyekevu mkubwa lakini kwa msisitizo mkubwa tunakusihi uamuru matengenezo ya hali ya juu, na uhakikishe kuwa yanatekelezwa.”—Ibid., b. 7, ch. 4.PKSw 111.1

  Sasa Baraza lilidai Mwanamatengenezo atokee mbele yao. Pamoja na kusihi, mapingamizi, na vitisho vya Aleanda, mwisho wake mfalme aliafiki, na Luther aliitwa aje mbele ya Baraza. Pamoja na samasi kilitolewa pia cheti cha hakikisho la usalama wake, ili kuhakikisha kuwa atarudi nyumbani salama. Nyaraka hizi zilipelekwa Wittenberg na mjumbe, aliyeagizwa kumleta katika jiji la Worms.PKSw 111.2

  Marafiki wa Luther waliingiwa na hofu na kusumbuka sana. Wakitambua chuki na uadui dhidi yake, waliogopa kuwa hata cheti cha hakikisho la usalama kisingeheshimiwa, na walimsihi asihatarishe maisha yake. Alijibu: “Wafuasi wa papa hawataki niende Worms, bali wanatamani nihukumiwe na kuuawa. Hilo siyo tatizo. Msiniombee mimi, bali ombeeni neno la Mungu.... Kristo atanipa Roho Wake niwashinde hawa watumishi wa uovu. Nitawadhihaki katika uhai wangu; nitawashinda kwa kifo changu. Wanajishughulisha jijini Worms ili wanilazimishe kukana; na huku ndiko kutakuwa kukana kwangu: Nilisema awali kuwa papa ni mwakilishi wa Kristo; sasa ninasema kuwa yeye ni adui mkubwa wa Bwana wetu, na mtume wa Shetani.”—Ibid., b. 7,ch. 6.PKSw 111.3

  Luther hakuwa peke yake katika safari hii ya kuhatarisha maisha. Kando ya mjumbe wa mfalme, watu watatu miongoni mwa marafiki zake wa karibu waliazimia kusafiri naye. Melanchthon alitamani sana kumsindikiza. Moyo wake ulikuwa umeshikamana na ule wa Luther, na alikuwa na hamu ya kuaandamana naye, ikiwa lazima, hadi gerezani au mautini. Lakini maombi yake yalikataliwa. Ikiwa Luther angeangamia, matumaini ya Matengenezo yangebaki kwa huyu mtendakzi mwenzake kijana. Mwanamatengenezo alisema alipokuwa akitengana na Melanchthon: “Ikiwa sitarudi, na maadui zangu wakaniua, endelea kufundisha, na simama imara katika ukweli. Fanya kazi badala yangu.... Ikiwa wewe utabaki ukiwa hai, kifo changu kitakuwa matokeo madogo sana.”— Ibid., b. 7, ch. 7. Wanafunzi na raia waliokuwa wamekusanyika kushuhudia kuondoka kwa Luther waliguswa sana. Watu wengi ambao mioyo yao ilikuwa imeguswa na injili, walimuaga kwa machozi. Hivyo Mwanamatengenezo na wenzake walioondoka Wittenberg.PKSw 111.4

  Wakiwa safarini waliona kuwa mawazo ya watu yalikuwa na hisia za hofu na kukata tamaa. Katika baadhi ya miji hakupewa heshima yo yote. Walipopumzika ili kulala usiku, kasisi mmoja rafiki yake Luther, alieleza hofu zake kuonesha mbele ya Luther picha ya mwanamatenegezo wa Italia ambaye alikuwa ameuawa kwa ajili ya kutetea imani yake. Siku iliyofuata waligundua kuwa maandishi ya Luther yalikuwa yamepigwa marufuku jijini Worms. Wajumbe wa mfalme walikuwa wakitangaza amri ya mfalme na kuwataka watu walete maandishi yote yaliyopigwa marufuku kwa mahakimu.PKSw 112.1

  Mjumbe, kwa kuhofia usalama wa Luther Barazani, na akifikiri kuwa msimamo wake unaweza kuyumbishwa, aliuliza ikiwa bado alitamani kuendelea na safari. Alijibu: “Ingawa nimepigwa marufuku kila mji, nitaendelea na safari.”—Ibid., b. 7, ch. 7.PKSw 112.2

  Mjini Erfurt, Luther alipokelewa kwa heshima. Akiwa amezungukwa na kundi la watu wenye shauku, alipita katika mitaa ambayo mara nyingi aliitembelea akiwa na mkoba wa omba omba. Alitembelea chumba chake katika nyumba ya watawa, na akatafakari kuhusu mapambano ambayo kwayo nuru sasa iliyofurika Ujerumani ilimwagwa katika roho yake. Aliombwa kuhubiri. Jambo hili alikuwa amekataza kulifanya, lakini mjumbe wa mfalme alimpa ruhusa, na mtawa ambaye awali alikuwa mfagiaji wa jumba la watawa, sasa alipanda mimbarani kuhubiri.PKSw 112.3

  Kwa mkutano uliohudhuriwa na watu wengi alihubiri kutoka maneno ya Kristo, “Amani iwe kwenu.” “Wanafalsafa, wasomi, na waandishi,” alisema, “wamejaribu kuwafundisha watu jinsi ya kupata uzima wa milele, na hawajafanikiwa. Sasa nitawaambia: ... Mungu amemfufua Mtu mmoja kutoka katika wafu, Bwana Yesu Kristo, ili kuangamiza kifo, kukomesha dhambi, na kufunga milango ya kuzimu. Hii ni kazi ya wokovu.... Kristo ameshinda! Hii ni habari ya furaha; na tumeokolewa kutokana na kazi Yake, na siyo kutokana na kazi yetu, na siyo kwa uwezo wetu wenyewe.... Bwana wetu Yesu Kristo alisema, ‘Amani iwe kwenu; angalieni mikono yangu;’ maana yake ni kuwa, Angalia, wee mwanadamu! Ni mimi, Mimi peke Yangu, ambaye nimeichukua dhambi yenu, na nimewakomboa; na sasa ninyi mnayo amani, asema Bwana.”PKSw 112.4

  Aliendelea, akionesha kuwa imani ya kweli itadhihirishwa na maisha matakatifu. “Kwa kuwa Mungu ametuokoa, hebu tupange kazi zetu ili ziweze kukubalika Kwake. Je, wewe ni tajiri? Hebu utajiri wako utumiwe kuwasaidia maskini. Je, wewe ni maskini? Hebu huduma zako zikubalike mbele ya matajiri. Ikiwa kazi zako zinakubalika mbele yako peke yake, huduma unayojifanya kumfanyia Mungu ni uongo.”—Ibid., b. 7, ch. 7.PKSw 112.5

  Watu walisikiliza kana kwamba waliotekewa. Mkate wa uzima ulikuwa ukigawiwa kwa roho zilizokuwa zikifa kwa njaa. Kristo alikuwa akiinuliwa juu kuliko mapapa, wakuu wa madola, na wafalme. Luther hakugusia kabisa hatari iliyokuwa ikimkabili. Hakutaka wamfikirie yeye binafsi au kuwafanya wamwonee huruma binafsi. Katika kumtafakari Kristo alisahau nafsi yake. Alijificha nyuma ya Mtu wa Kalwari, akitafuta kumwasilisha Yesu kama Mkombozi pekee wa mwenye dhambi.PKSw 113.1

  Wakati Mwanamatengenezo alipokuwa akiendelea na safari yake, kila mahali aliangaliwa kwa shauku kubwa. Umati mkubwa wa watu walimzunguka, na sauti za marafiki zilimwonya juu ya kusudi la viongozi wa Kanisa la Kirumi. Baadhi wakasema, “watakuchoma moto,” na kukuunguza mwili wako uwe majivu, kama walivyomfanya John Huss.” Luther alijibu, “Hata kama wangewasha moto njia nzima kuanzia jiji la Worms hadi jiji la Wittenberg, ndimi za moto ziende juu hadi mbinguni, ningetembea katikati yake katika jina la Bwana; ningetokea mbele yao, ningeingia katika mataya ya kiboko huyu, na kuvunja meno yake, nikimkiri Bwana Yesu Kristo.”—Ibid., b. 7, ch. 7.PKSw 113.2

  Habari za kukaribia kwake Worms zilisababisha vurumai. Marafiki zake walitetemeka kwa kuhofia usalama wake; maadui zake walikuwa na hofu ya mafanikio ya kazi yao. Juhudi kubwa zilifanywa kumshawishi asiingie jijini. Kwa uchochezi wa watetezi wa upapa aliombwa apumzike katika jengo la rafiki yake mmoja nje ya jiji, ambapo, ilitangazwa kuwa matatizo yote yangerekebishwa kwa mapatano. Marafiki zake walijitahidi kuamsha hofu zake kwa kueleza hatari zilizomkabili. Juhudi zao zote zilishindwa. Luther, akiwa bado hajatetereka, alitoa msimamo wake: “Hata kama kuna mashetani wengi katika jiji la Worms kama vigae kwenye papa la nyumba, bado nitaingia tu ndani.”—Ibid., b. 7, ch. 7.PKSw 113.3

  Alipofika Worms, kundi kubwa la watu lilikuja malangoni kumkaribisha. Mkusanyiko mkubwa kama huo ulikuwa haujawahi kutokea hata kumpokea mfalme mwenyewe. Msisimko ulikuwa wa kiwango cha juu, na kutoka katikati ya mkusanyiko sauti ya juu na ya huzuni iliimba wimbo wa mazishi kama onyo kwa Luther juu ya hatari iliyokuwa ikimsubiri. “Mungu atakuwa mlinzi wangu,” alisema, alipokuwa akishuka kutoka katika gari lake la kukokotwa na farasi.PKSw 113.4

  Watetezi wa upapa hawakuamini kuwa Luther angethubutu kutokea jijini Worms, na kufika kwake kuliwafanya waogope sana. Mfalme aliwaita wanabaraza haraka sana kutafakari juu ya hatua inayopaswa kuchukuliwa. Mmoja wa maaskofu, mtetezi wa upapa mwenye msimamo mkali, akasema: “Tumejadili sana juu ya suala hili. Tunakuomba wewe mfalme umwangamize mtu huyu mara moja. Je, Sigismund hakuwezesha John Huss achomwe moto? Hatulazimiki kutoa wala kuheshimu cheti cha usalama cha mzushi.” “Hapana,” mfalme alisema, “tunapaswa kutunza ahadi yetu.”—Ibid., b. 7, ch. 8. Hivyo iliamuriwa kuwa Mwanamatengenezo asikilizwe.PKSw 113.5

  Jiji lote lilikuwa na shauku ya kumwona mtu huyu wa ajabu, na kundi kubwa la wageni lilijaza nyumba za wageni mara moja. Luther alikuwa amepona kidogo ugonjwa wake wa siku za karibuni; alikuwa amechoshwa na safari, ambayo ilikuwa imechukua majuma mawili kamili; ilimpasa ajiandae kukutana na matukio makubwa kesho yake, hivyo alihitaji ukimya na pumziko. Lakini shauku ya kumwona ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba alifaulu kupumzika kwa saa chache tu ambapo malodi, mashujaa, makasisi, na raia walikusanyika kwa shauku na kumzunguka. Miongoni mwao walikuwemo waheshimiwa ambao kwa ujasiri walikuwa wamemwomba mfalme asimamie matengenezo ya uovu miongoni mwa viongozi wa kanisa na wale ambao, Luther alisema, “waliokuwa wamewekwa huru na injili yangu.”—Martyn, uk. 393. Maadui, na marafiki, wote kwa pamoja walikuja kumwona huyu mtawa asiye na woga; lakini aliwapokea kwa utulivu usiotetereka, akiwajibu wote kwa heshima na hekima. Mwonekano wake ulikuwa wenye uimara na ujasiri. Uso wake mweupe, mwembamba, ukiwa na viashiria vya kazi ngumu na kuugua, ulivaa mwonekano wa ukarimu na furaha. Umakini na udhati wa kina wa maneno yake ulimpa nguvu ambayo hata maadui zake hawakuweza kuistahimili. Marafiki na maadui kwa pamoja walijazwa na mshangao. Baadhi walishawishika kuwa mvuto wa Kimungu ulikuwa ndani yake; wengine walisema, kama Mafarisayo walivyosema kuhusiana na Kristo: “Ana pepo.”PKSw 114.1

  Siku iliyofuata Luther aliitwa kufika mbele ya Baraza Kuu. Afisa kutoka ikulu ya mfalme aliteuliwa kwenda kumleta na kumwongoza ukumbini; hata hivyo alifika mahali pale kwa shida sana. Kila njia ilikuwa imefurika watu wenye shauku ya kumwona huyu mtawa aliyethubutu kupinga mamlaka ya papa.PKSw 114.2

  Alipokuwa karibu kuingia mbele ya majaji wake, jenerali mkongwe, shujaa wa vita vingi, aliongea naye kwa upole: “Maskini mtawa, maskini mtawa, sasa unakwenda kuweka msimamo ulio bora zaidi kuliko mimi au kapteni mwingine ye yote alivyoweza kufanya katika vita iliyomwaga damu nyingi zaidi kuliko vita zote. Lakini, ikiwa kazi yako ni ya haki, na wewe una uhakika nayo, songa mbele katika jina la Mungu, na usiogope kitu chochote. Mungu hatakuacha.”—D'Aubigne, b. 7, ch. 8. Hatimaye Luther alisimama mbele ya Baraza. Mfalme alikalia kiti cha enzi. Alizungukwa na maofisa wa ngazi za juu kabisa katika ufalme. Ilikuwa haijawahi kutokea mtu ye yote kusimama mbele ya mkutano unaovutia kuliko ule ambao Martin Luther alitakiwa kutetea imani yake mbele yake. “ Mwonekano huu tu peke yake ulikuwa ishara ya ushindi dhidi ya upapa. Papa alikuwa ameshamhukumu yule mtu, na sasa alikuwa amesimama mbele ya mahakama, ambayo, kwa tendo hili tu peke yake, ilikuwa imejiweka juu ya papa. Papa alikuwa ameshamweka chini ya amri ya kutengwa, na alikuwa amekata mahusiano yake na jamii yote ya watu; na bado alikuwa ameitwa kwa lugha ya heshima, na kupokelewa mbele ya mkutano mkubwa kuliko mikutano yote duniani.PKSw 114.3

  Papa alikuwa ameshamhukumu kuwa kimya siku zote, na sasa alikuwa karibu kuhutubia maelfu ya wasikilizaji makini waliokusanyika pamoja kutoka kona zote za ulimwengu wa Ukristo. Mapinduzi makubwa yalikuwa yametekelezeka kupitia kwa Martin Luther. Roma ilikuwa tayari inashuka kutoka katika kiti chake cha enzi, na ilikuwa sauti ya mtawa iliyomshusha chini.”—Ibid., b. 7, ch. 8.PKSw 115.1

  Mbele ya mkutano wa waheshimiwa wenye vyeo vya juu, Mwanamatengenezo aliyezaliwa katika umaskini, alionekana kunyenyekeshwa na kunyanyasika. Baadhi ya wakuu, walipogundua hisia zake, walimwendea, na mmoja wao alimnong'onezea: “Usiwaogope wao wanaoua mwili, bali mwogope Yeye anayeweza kuua roho.” Mwingine alisema: “Watakapowapeleka mbele ya watawala na wafalme kwa ajili Yangu, mtapewa, na Roho wa Baba, cha kusema.” Hivyo maneno ya Kristo yaliletwa na watu wakuu ulimwenguni kumtia nguvu mtumishi Wake katika saa ya kujaribiwa.PKSw 116.1

  Luther aliongozwa hadi sehemu iliyoangaliana moja kwa moja na kiti cha enzi cha mfalme. Ukimya mkuu uliushika umati wa watu waliokusanyika. Ndipo ofisa kutoka ikulu ya mfalme alisimama na, akinyosha kidole kuelekea mkusanyiko wa maandishi ya Luther, alimtaka Mwanamatengenezo ajibu maswali mawili—ikiwa alikiri kuwa ni maandishi yake, na ikiwa alikuwa tayari kukana maoni aliyoyaweka katika maandishi yale. Majina ya vitabu yaliposomwa, Luther alijibu kuwa kwa swali la kwanza, alikiri kuwa vitabu vile ni vyake. “Kwa swali la pili,” alisema, “kwa kuwa ni swali linalohusiana na imani na wokovu wa roho, na kwa kuwa neno la Mungu, hazina kuu na ya thamani kubwa kuliko zote iwe mbinguni au duniani, linahusika, itakuwa siyo busara kujibu haraka haraka bila kutafakari. Kuna uwezekano nikathibitisha kidogo zaidi kuliko uhalisia unavyodai, au nikathibitisha kwa nguvu zaidi kuliko ukweli unavyohitaji, na kwa sababu hiyo nikatenda dhambi dhidi ya kauli hii ya Kristo: ‘Atakayenikana mbele za watu, nitamkana mbele ya Baba Yangu wa mbinguni’ [Mathayo 10:33.] Kwa sababu hiyo ninakusihi, ee mfalme mkuu, kwa unyenyekevu wote, unipe muda, ili niweze kujibu bila kulikosea neno la Mungu.”—D'Aubigne, b. 7, ch. 8.PKSw 116.2

  Kwa kutoa ombi hili, Luther alichukua hatua muafaka. Mwelekeo huu uliwashawishi wajumbe wa mkutano kuwa hakutoa majibu kwa jaziba au kukurupuka. Utulivu huo na kujitawala, ambako hakukutarajiwa kwa mtu ambaye alikuwa amejionesha kuwa jasiri na mwenye msimamo usioyumba, ulimwongezea nguvu, na kumwezesha baadaye kujibu kwa busara, uamuzi, hekima, na heshima iliyowashangaza watu wengi na kuwakatisha tamaa maadui zake, na ulikemea ufedhuli na kiburi. Siku iliyofuata alipaswa kutokea ili kutoa jibu lake la mwisho. Kwa muda fulani moyo wake ulisinyaa ndani yake alipotafakari juu ya mamlaka zilizoungana dhidi ya ukweli. Imani yake ilitetereka; hofu na kutetemeka vilimjia, na kihoro kilimgubika. Hatari ziliongezeka mbele yake; maadui zake walioonekana kushangilia, na nguvu za giza kushinda. Mawingu yalijikusanya na kumzunguka na yalionekana kama yalimtenga na Mungu. Alitamani kupata uhakikisho kuwa Bwana wa majeshi atakuwa pamoja naye. Akiwa na kilio moyoni alijitupa chini akalala kifudi-fudi na kumwaga vilio vya moyo uliopondeka na kuvunjika-vilio ambavyo hakuna mtu ye yote anayeweza kuvielewa isipokuwa Mungu peke yake.PKSw 116.3

  “Ee Mungu Mwenyezi wa milele,” alisihi, “ulimwengu huu unatisha kiasi gani! Tazama, umefunua mdomo ili unimeze, na mimi nina tumaini kidogo sana Kwako.... Ikiwa inanipasa kutumainia nguvu ya huu ulimwengu peke yake, huu ndio mwisho wangu.... Saa yangu ya mwisho imefika, hukumu yangu imeshatangazwa.... Ee Mungu, nisaidie dhidi ya hekima ya ulimwengu. Fanya hivyo, ... Wewe peke Yako; ... kwa kuwa kazi hii siyo yangu, bali ya Kwako. Sina lo lote la kufanya hapa, sina la kubishania na hawa wakuu wa ulimwengu.... Lakini kazi hii ni Yako, ... na kazi ya haki na ya milele. Ee Bwana, nisaidie! Mungu mwaminifu usiyebadilika, sina mtu mwingine ninayemtumainia.... Cho chote kinachotokana na mwanadamu hakina uhakika; yote yaayotokana na mwanadamu yanaangusha.... Wewe umenichagua kwa ajli ya kazi hii.... Simama kando yangu, kwa ajili ya mpendwa Wako Yesu Kristo, ambaye ni mlinzi wangu, ngao yangu, na ngome yangu imara.”—Ibid., b. 7, ch. 8.PKSw 116.4

  Uongozi wa Mungu wenye hekima uliruhusu Luther agundue hatari iliyokuwa mbele yake, ili asitegemee nguvu zake mwenyewe na asikimbilie kwa kiburi hatarini. Hata hivyo hofu yake haikuwa kwa ajili ya mateso binafsi, hofu ya maumivu au kifo, kilichoonekana kuwa karibu sana, ambacho kilimtisha. Alikuwa amefikia kilele cha mgogoro, na alihisi kutotosha kukabiliana na kilele hicho. Kwa sababu ya udhaifu wake kazi ya ukweli ingeshindwa. Alishindana na Mungu siyo kwa ajili ya usalama wake, bali kwa ajili ya ushindi wa injili. Kama ilivyokuwa kwa Israeli, katika pambano lile la usiku kando ya kijito cha upweke, ndivyo maumivu na mapambano ya roho yake yalivyokuwa. Kama ilivyokuwa kwa Israeli, alimshinda Mungu. Katika hali yake isiyokuwa na msaada kabisa imani yake ilimshikilia Kristo, Mkombozi mwenye nguvu. Aliimarishwa kwa uhakikisho kuwa asingekwenda mbele ya baraza akiwa peke yake. Amani ilirudi moyoni mwake, na alifurahi kuwa aliruhusiwa kuliinua neno la Mungu mbele ya watawala wa mataifa.PKSw 116.5

  Akili yake ikiwa imetulizwa kwa Mungu, Luther alijiandaa kwa ajili ya mapambano yaliyokuwa mbele yake. Alifikiria juu ya mpangilio wa jibu lake, alichunguza aya katika maandishi yake, na alichota kutoka katika Maandiko uthibitisho stahiki kutetea misimamo yake. Ndipo, akiwa ameweka mkono wake wa kushoto juu Kitabu Kitakatifu, ambacho kilikuwa wazi mbele yake, aliinua mkono wake wa kulia kuelekea mbinguni na aliapa “kubaki akiwa mwaminifu kwa injili, na kukiri imani yake kwa uhuru, hata kama ingebidi kuthibitisha ushuhuda wake kwa damu yake.”—Ibid., b. 7, ch. 8.PKSw 117.1

  Alipopelekwa tena mbele ya Baraza, sura yake haikuwa na kiashiria chochote cha hofu wala aibu. Akiwa mtulivu na mwenye amani, lakini jasiri na muungwana sana, alisimama kama shahidi wa Mungu miongoni mwa wakuu wa dunia. Yule afisa mteule wa mfalme alimwamuru atoe uamuzi wake ikiwa alikusudia kukana mafundisho yake. Luther alijibu kwa sauti tulivu na ya unyenyekevu, bila ukali wala mhemko. Mwonekano wake ulikuwa wa heshima na adabu; na bado alionesha ujasiri na furaha iliyoushangaza mkutano. “Mfalme mtulivu sana, waheshimiwa wana wa wafalme, watawala wakuu wenye neema,” alisema Luther, “Nimekuja mbele yenu siku ya leo, kwa amri niliyopewa jana, na kwa rehema za Mungu ninakuomba mheshimiwa mfalme na viongozi wakuu mliopo hapa msikilize kwa neema utetezi wa kazi ambayo nina hakika ni ya haki na ya kweli. Ikiwa, kwa kutokujua, nitakosea taratibu na itifaki za baraza, ninawasihi sana mnisamehe; kwa kuwa sikulelewa katika ikulu za wafalme, bali katika upweke wa nyumba ya watawa.”—Ibid., b. 7, ch. 8.PKSw 117.2

  Ndipo, akijielekeza kujibu swali, alisema kuwa vitabu vyake havikuwa vya aina moja. Katika baadhi ya vitabu aliandika juu ya imani na matendo mema, na hata maadui zake walisema kuhusu hivyo vitabu kuwa licha ya kutokuwa na madhara yo yote vilikuwa na manufaa sana. Kuvikana vitabu hivi ingekuwa ni kuukataa ukweli ambao pande zote zinaukiri. Kundi la pili la vitabu lilikuwa na maandishi yaliyofunua ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka ya upapa. Kuvikana vitabu hivi kungeimarisha ukatili wa Roma na kufungua zaidi milango kwa ajili ya uovu mkubwa zaidi. Katika kundi la tatu la vitabu vyake alishambulia watu binafsi waliotetea maovu yaliyokuwepo. Kuhusiana na vitabu alikiri wazi kuwa alitumia lugha kali kuliko ilivyostahili. Hakudai kuwa hakuwa na makosa kabisa; lakini hata hivi vitabu asingevikana kwa sababu kufanya hivyo kungewapa nguvu maadui wa ukweli, na wangetumia fursa hiyo kuwakandamiza watu wa Mungu kwa ukatili mkubwa zaidi.PKSw 117.3

  “Hata hivyo mimi ni mwanadamu tu, na siyo Mungu,” aliendelea; “Kwa hiyo nitajitetea kama Kristo alivyojitetea: ‘Ikiwa nimesema vibaya, toeni ushahidi dhidi ya ubaya huo.’ ... Kwa rehema za Mungu, ninakuomba, mfalme mtulivu sana, na ninyi, waheshimiwa sana wana wa wafalme, na watu wote wa kila ngazi, mthibitishe kutoka katika maandiko ya manabii, na mitume kuwa nimekosea. Na mara tu nikishawishika kuwa vina makosa, nitakana kila kosa, na nitakuwa wa kwanza kushika vitabu vyangu na kuvitupa motoni.PKSw 118.1

  “Mambo ambayo nimeyasema wazi hivi punde yanaonesha, natumaini, kuwa nimepima na kufikria kwa uangalifu hatari zinazonikabili; lakini licha ya kutokukatishwa tamaa, ninafurahi kuona kuwa injili sasa, kama ilivyokuwa nyakati za awali, imekuwa chanzo cha taabu na mpasuko. Hii ni tabia, hii ni hatima, ya neno la Mungu. ‘Sikuja kuleta amani duniani, bali upanga,’ alisema Yesu Kristo. Mungu ni wa ajabu na anatisha katika mashauri Yake; angalia isije ikawa, kwa kujaribu kuepuka mipasuko, ukalitesa neno la Mungu, na kujimwagia mafuriko ya kutisha ya hatari zisizokoma, za maafa ya sasa, na ukiwa wa milele.... Ninaweza kunukuu mifano mingi kutoka katika Neno la Mungu. Ninaweza kuzungumzia habari za Farao, wafalme wa Babeli, na wale wa Israeli, ambao kazi zao hazikuwahi kuchangia kwa kiwango kikubwa kwa uhabirifu wao wenyewe kuliko wakati walipofuata mashauri, ambayo kwa mtazamo wa juu juu, yalionekana kuwa ya busara katika kuimarisha utawala wao. ‘Mungu anaondoa milima, na hawalijui hilo.'”—Ibid., b. 7, ch. 8.PKSw 118.2

  Luther alikuwa ameongea katika lugha ya Kijerumani; aliombwa arudie maneno yale yale kwa lugha ya Kilatini. Ingawa alikuwa amechoshwa na juhudi za awali, alitii, na alihutubia tena, kwa uwazi ule ule na nguvu ile ile kama alivyofanya mara ya kwanza. Uongozi wa Mungu ulielekeza jambo hilo. Akili za viongozi wengi zilikuwa zimepofushwa kwa makosa na ushirikina kiasi kwamba katika hotuba ya kwanza hawakuona nguvu ya hoja za Luther; lakini kurudia kuliwawezesha kuelewa vizuri zaidi hoja zilizotolewa.PKSw 118.3

  Wale ambao walifumba macho ili wasiione nuru kwa ugumu wa moyo tu na waliazimia kutoshawishiwa na ukweli, walikasirishwa na nguvu ya maneno ya Luther. Alipomaliza kusema, msemaji wa Baraza alisema kwa hasira: “Hukujibu swali uliloulizwa.... Unatakiwa kutoa jibu la wazi na fupi.... Unakana, au hukani?” Mwanamatengenezo alijibu: “Kwa kuwa mfalme mtulivu na waheshimiwa viongozi mnataka kwangu jibu la wazi, sahili, na fupi, nitawapa jibu hilo, nalo ni hili: siwezi kusalimisha imani yangu ama kwa papa au kwa mabaraza, kwa sababu ni wazi kama ulivyo mchana kuwa wamekosea mara nyingi na wanapingana wao kwa wao. Isipokuwa, hivyo basi, nishawishiwe kwa ushuhuda wa Maandiko au kwa hoja madhubuti, isipokuwa tu pale nitakaposhawishiwa kwa njia ya aya nilizozinukuu, na isipokuwa tu pale watakapoifanya dhamiri yangu ishikamane na neno la Mungu, siwezi na sitaweza kukana, kwa kuwa siyo salama kwangu kusema jambo lolote dhidi ya dhamiri yangu. Hapa nasimama, siwezi kufanya jambo lolote jingine; ee Mungu nisaidie. Amina.”—Ibid., b. 7, ch. 8.PKSw 118.4

  Hivyo alisimama mtu huyu mwenye haki juu ya msingi wa hakika wa neno la Mungu. Nuru ya mbinguni iliangazia uso wake. Ukuu wake na usafi wa tabia yake, haki na furaha ya moyo wake, vilionekana kwa wote aliposhuhudia dhidi ya nguvu ya makosa na wao walivyoshuhudia nguvu ya imani ishindayo ulimwengu.PKSw 119.1

  Mkutano wote kwa muda walibaki kimya wakiwa wameshikwa na mshangao. Wakati kujibu swali lake la kwanza Luther aliongea kwa sauti ya chini, katika hali ya heshima, na akiwa katika hali kama ya kujisalimisha. Watetezi wa kanisa la Roma walikuwa wametafsiri hali hii kama ushahidi kuwa ujasiri wake ulikuwa unaelekea kwisha. Walichukulia ombi lake la kupewa muda kama utangulizi wa yeye kukana mafundisho yake. Charles mwenyewe, akizingatia, nusu akionesha dharau, umbo dhaifu la mtawa, nguo zake za kimaskini, na usahili wa hotuba yake, alisema: “Mtawa huyu hatanifanya niwe mzushi.” Ujasiri na uimara ambao sasa aliuonesha, pamoja na nguvu na uwazi wa hoja zake, uliwajaza wajumbe wa baraza kwa mshangao. Mfalme, baada ya kuguswa, alisema kwa hisia: “Mtawa huyu anaongea kwa moyo mkuu na ujasiri usio na mashaka.” Wengi wa viongozi wa Ujerumani walimwangalia kwa kujivunia huyu mwakilishi wa taifa lao.PKSw 119.2

  Wafuasi wa Roma walikuwa wameshindwa; hoja yao ilionekana kuwa dhaifu na isiyoungwa mkono na wajumbe wengi. Walitafuta kudumisha mamlaka yao, siyo kwa kutumia Maandiko, bali kwa kujielekeza kutumia hoja ya vitisho, hoja ya Roma isiyoshindwa. Alisema msemaji wa Baraza: “Usipokanusha, mfalme na majimbo ya ufalme watajadili hatua ya kuchukua dhidi ya mzushi mkorofi.”PKSw 119.3

  Rafiki wa Luther, aliyefurahi sana aliposikiliza utetezi wake mzuri, alitetemeshwa na maneno haya; lakini daktari mwenyewe alisema katika hali ya utulivu: “Ee Mungu uwe msaada wangu, kwa kuwa siwezi kukana cho chote.”—Ibid., b. 7, ch. 8.PKSw 119.4

  Aliambiwa aondoke katika ukumbi wa Baraza wakati viongozi wakijadiliana. Ilihisiwa kuwa tatizo kubwa lilikuwa limefika. Kukataa kwa daima kwa Luther kujisalimisaha kungeweza kubalidi historia ya kanisa kwa zama zijazo. Iliamuriwa kumpa nafasi nyingine tena ili akanushe. Kwa mara ya mwisho aliletwa katika mkutano. Kwa mara nyingine swali lilitolewa, ikiwa angekanusha mafundisho yake. “Sina jibu jingine la kutoa,” alisema, “zaidi ya lile nililokwisha kulitoa.” Ilikuwa wazi kuwa asingeweza kushawishika, ama kwa ahadi au vitisho, kujisalimisha kwa mamlaka ya Roma.PKSw 119.5

  Viongozi wawakilishi wa upapa walichukizwa kuwa mamlaka yao, ambayo iliwafanya wafalme na wakuu watetemeke, ingeweza kudhihakiwa na mtawa maskini; walitamani kumfanya ahisi hasira yao kwa kutesa maisha yake. Lakini Luther, akielewa hatari iliyomkabili, alikuwa ameongea nao wote kwa adabu na utulivu. Maneno yake hayakuwa na kiburi, hasira, na kumsingizia mtu. Alijisahau mwenyewe binafsi, na wakuu waliokuwa wamemzunguka, na alihisi kuwa alikuwa katika uwepo wa Yule aliye juu sana zaidi ya mapapa, maaskofu, wafalme, na wafalme wakuu. Kristo alikuwa amezungumza kupitia ushuhuda wa Luther kwa nguvu na utukufu ambao kwa muda fulani uliwavutia marafiki na maadui kwa kicho na mshangao. Roho wa Mungu alikuwepo katika Baraza lile, akigusa mioyo ya viongozi wakuu wa dola. Baadhi ya wana wa wafalme walikiri kwa ujasiri uhalali wa kazi za Luther. Wengi walishawishiwa na ukweli; lakini kwa baadhi miguso iliyopokelewa haikuwa ya muda mrefu. Kulikuwepo na kundi la watu ambao hawakueleza kushawishika kwao, lakini ambao, baada ya kuchunguza Maandiko wao wenyewe, katika wakati uliofuata wakawa waungaji mkono wasio na hofu wa Matengenezo.PKSw 120.1

  Elekta Frederick alikuwa ametarajia kwa hamu kubwa ujio wa Luther mbele ya Baraza, na kwa msisimko mkubwa alisikiliza hotuba yake. Kwa furaha na kujisikia vizuri alishuhudia ujasiri, uimara, na kujitawala, na aliazimia kusimama imara zaidi kumtetea. Alitofautisha wahusika katika pambano, na aliona kuwa hekima ya mapapa, wafalme, na maaskofu ilikuwa imeoneshwa kuwa siyo kitu kwa nguvu ya ukweli. Upapa ulikuwa umepata anguko ambalo lingehisiwa miongoni mwa mataifa yote na katika zama zote.PKSw 120.2

  Wakati mjumbe wa papa alipopokea madhara yaliyosababishwa na hotuba ya Luther, aliogopa, kuliko hapo awali, kwa ajili ya usalama wa nguvu ya Kiroma, na alidhamiria kutumia kila njia iliyokuwa katika uwezo wake kufanikisha ushindi wa Roma dhidi ya Mwanamatengenezo. Kwa kutumia ufasaha na stadi za kidiplomasia vitu ambavyo alikuwa akivimudu kwa kiwango cha juu, aliwasilisha kwa mfalme kijana upumbavu na hatari ya kuvunja urafiki na kupoteza msaada wa kiongozi wa Roma mwenye nguvu nyingi, kwa sababu ya mafundisho ya mtawa asiye na maana.PKSw 120.3

  Maneno yake hayakupita bila madhara. Siku iliyofuata baada ya jibu la Luther, Charles aliagiza ujumbe upelekwe katika Baraza Kuu la Kitaifa, akitangaza azimio lake la kutekeleza sera ya watangulizi wake ya kusimamia na kulinda dini ya Kikatoliki. Kwa kuwa Luther alikuwa amekataa kukana makosa yake, hatua kali zinapaswa zichukuliwe dhidi yake na uzushi alioufundisha. “Mtawa mmoja, aliyepotoshwa na upumbavu wake mwenyewe, ameinuka dhidi ya imani ya Kikristo. Ili kudhibiti kufuru hii, nitatoa kafara falme zangu, hazina zangu, rafiki zangu, mwili wangu, damu yangu, roho yangu, na maisha yangu. Nitamfukuza Agustino Luther, na kumpiga marufuku asisababishe vurugu hata kidogo miongoni mwa watu; halafu nitawashughulikia yeye mwenyewe na wafuasi wake kama wazushi wakaidi, kwa kuwatenga na kanisa, kwa kuwatenga na watu, na kwa kila njia inayoweza kuwaangamiza. Ninatoa wito kwa nchi wanachama kuishi kama Wakristo waaminifu.”—Ibid., b. 7, ch. 9. Hata hivyo mfalme alitangaza kuwa cheti cha uhakikisho wa usalama wa Luther kilipaswa kiheshimiwe, na kuwa kabla ya hatua yo yote ile kuchukuliwa dhidi yake, alipaswa kuruhusiwa kufika nyumbani kwake salama.PKSw 120.4

  Maoni mawili yanayopingana sasa yalitolewa na kusisitizwa na wajumbe wa Baraza. Wajumbe na wawakilishi wa papa walidai tena kuwa cheti cha uhakikisho wa usalama wa Mwanamatengenezo ilipaswa kipuuzwe. “Mto Rhine,” walisema, “inapasa upokee majivu yake, kama ulivyopokea majivu ya John Huss karne moja iliyopita.”—Ibid., b. 7, ch. 9. Lakini viongozi wakuu wa ufalme wa Ujerumani, ingawa wao wenyewe walikuwa wafuasi wa papa na maadui wakuu wa Luther, walipinga ukiukwaji wa hadharani wa uaminifu wao kwa umma, kama doa kwa heshima ya taifa. Walitolea mfano wa majanga yaliyofuata baada ya kifo cha Huss, na walisema kuwa wasingethubutu kusababisha kurudiwa kwa majanga yale ya kutisha yaangukie tena juu ya nchi ya Ujerumani, na juu ya kichwa cha mfalme wao kijana.PKSw 121.1

  Charles mwenyewe, akijibu hilo pendekezo baya, alisema: “Ingawa heshima na imani vinapaswa kupigwa marufuku kutoka ulimwenguni mwote, vinapaswa kuhifadhiwa katika mioyo ya viongozi wakuu.”—Ibid., b. 7, ch. 9. Aliendelea kusihiwa zaidi na maadui wakuu wafuasi wa upapa kumshughulikia Mwanamatengenezo kama Sigismund alivyomshughulikia Huss—kumwachia kanisa limshughulikie; lakini akikumbuka mandhari wakati Huss katika mkutano wa hadhara alipoonesha minyororo yake na kumkumbusha mfalme juu ya imani yake iliyopotoka, Charles V alisema: “Nisingependa kufanya kama Sigismund alivyofanya.”—Lenfant, vol. 1, p. 422.PKSw 121.2

  Hata hivyo Charles aliamua kwa makusudi kuukataa ukweli uliowasilishwa na Luther. “Nimedhamiria kwa nguvu zangu zote kuwaiga wazee wangu,” aliandika mfalme.—D'Aubigne, b. 7, ch. 9. Aliamua kuwa asingeondoa mguu wake katika njia ya mila na desturi, ili atembee katika njia za ukweli na haki. Kwa kuwa baba zake walifanya, angeunga mkono upapa, ikiwa ni pamoja na ukatili na ufisadi wake wote. Hivyo aliweka msimamo wake, akikataa kila nuru iliyo tofauti na ile baba zake waliyoipokea, au kufanya wajibu wowote ambao hawakuufanya.PKSw 121.3

  Kuna wengi leo wanaong'ang'ania mila na desturi za baba zao. Wakati Bwana anapowatumia nuru ya nyongeza, wanakataa kuipokea, kwa sababu, kwa kuwa haikutolewa kwa baba zao, isingepokelewa na wao. Hatuwekwi katika nafasi ambazo baba zetu walikuwa; matokeo yake wajibu na majukumu yetu siyo sawa na yao. Hatutakubaliwa na Mungu kwa kuangalia mfano wa baba zetu kuamua wajibu wetu badala ya kuchunguza neno la ukweli sisi wenyewe. Wajibu wetu ni mkubwa zaidi kuliko ule wa wazee wetu. Tunawajibika kwa nuru waliyoipokea, na ambayo ililetwa kwetu kama urithi wetu, na tunawajibika pia kwa nuru ya nyongeza ambayo sasa inang'aa juu yetu kutoka katika neno la Mungu.PKSw 122.1

  Alisema Kristo kuhusu Wayahudi wasioamini: “Kama nisingalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi yao” (Yohana 15:22). Nguvu ya Mungu ile ile ilikuwa imesema kupitia kwa Luther na kuongea na wakuu wa Ujerumani. Na kama nuru ilivyomulika kutoka katika neno la Mungu, Roho Wake aliwasihi kwa mara ya mwisho watu wengi katika mkutano ule. Kama vile Pilato, karne nyingi zilizopita, alivyoruhusu kiburi na kutaka kupendwa na watu, vifunge moyo wake dhidi ya Mkombozi wa ulimwengu; kama vile Festo alivyomuaga mjumbe wa ukweli, “Sasa enenda zako, nami nikipata nafasi nitakuita;” kama vile Agripa mwenye kiburi alivyokiri, “Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo” (Matendo 24:25; 26:28), lakini aligeuka na kuukataa ujumbe uliotumwa na Mbingu—ndivyo Charles V, akijisalimisha kwa shinikizo la kiburi na sera za ulimwengu, aliamua kuikataa nuru ya ukweli.PKSw 122.2

  Minong'ono na mipango dhidi ya Luther ilienea kila mahali, ikasababisha taharuki kubwa katika jiji lote. Mwanamatengenezo alikuwa na marafiki wengi, ambao, wakijua ukatili na hila ya Roma kwa wote waliojaribu kufichua ufisadi wake, waliazimia kuwa hatatolewa kafara. Mamia ya watu wenye vyeo vya juu waliahidi kumlinda. Siyo watu wachache walioupinga ujumbe wa mfalme wa kujisalimisha kwa mamlaka ya utawala wa Roma. Kwenye malango ya nyumba na katika maeneo ya mikusanyiko ya watu, mabango yalibandikwa, baadhi yakimlaumu na mengine yakimpongeza Luther. Kwenye moja ya mabango haya yalikuwa yamendikwa tu maneno ya maana ya mtu mwenye hekima: “Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana” (Mhubiri 10:16). Mwamko mkubwa wa jumla uliomwunga mkono Luther katika nchi yote ya Ujerumani ulimshawishi mfalme na Baraza kuwa dhuluma yo yote ambayo ingefanywa dhidi yake ingehatarisha amani ya ufalme na hata uimara wa kiti cha enzi.PKSw 122.3

  Mfalme Frederick wa Saxony alibaki kimya, na kwa uangalifu alificha hisia zake halisi dhidi ya Mwanamatengenezo, wakati huo huo akimlinda wakati wote kwa bidii bila kuchoka, akifuatilia mienendo yake yote na ile ya maadui zake. Lakini walikuwepo watu wengi ambao hawakuficha huruma zao kwa Luther. Alitembelewa na watoto wa mfalme, malodi, mabaroni, na watu wengi wenye heshima, viongozi wa kiraia na viongozi wa kikanisa. “ Chumba kidogo cha daktari,” aliandika Spalatin, “hakikuwatosha wageni wote waliomtembelea.”— Martyn 1:404. Watu walimwona kana kamba ni zaidi ya mwanadamu. Hata watu ambao hawakuyaamini mafundisho yake walihusudu uadilifu wake mkubwa uliomwezesha kukabiliana na kifo kwa ujasiri badala ya kukiuka dhamiri yake.PKSw 122.4

  Juhudi nyingi zilifanywa kupata ukubali wa Luther wa kupatana na Roma. Malodi na wana wa wafalme walimwambia kuwa ikiwa atashikilia msimamo wake wa kujiwekea hukumu yake dhidi ya ile ya kanisa na ya baraza siyo muda mrefu angefukuzwa atoke katika ufalme na asingekuwa na ulinzi. Kwa tishio hili Luther alijibu: “Injili ya Kristo haiwezi kuhubiriwa bila kuamsha chuki.... Kwa nini sasa hofu au woga wa hatari unitenge na Bwana, na unitenge na neno la Mungu ambalo peke yake ni ukweli? Hapana; afadhali nitoe mwili wangu, damu yangu, na maisha yangu.”—D'Aubigne, b. 7, ch. 10.PKSw 123.1

  Kwa mara nyingine tena alisihiwa ajisalimishe kwa hukumu ya mfalme, na ndipo asingekuwa na jambo la kuogopa. “Ninakubali,” alijibu, “kwa moyo wangu wote, kuwa mfalme, wana wa mfalme, na hata Mkristo wa kawaida kabisa, achunguze na ahukumu kazi zangu; lakini kwa sharti moja, watumie neno la Mungu kama kiwango chao. Wanadamu hawana cha kufanya kingine isipokuwa tu kulitii. Msiifanyie ukatili dhamiri yangu, ambayo imeshikamana na imefungwa pamoja na Maandiko Matakatifu kwa mnyororo.”—Ibid., b. 7, ch. 10.PKSw 123.2

  Kwa kitisho kingine alisema: “Ninakubali kuachana na cheti cha hakikisho la usalama. Ninaweka nafsi yangu katika mikono ya mfalme, lakini neno la Mungu—kamwe!”—Ibid., b. 7, ch. 10. Alieleza utayari wake kujisalimisha kwa uamuzi wa baraza kuu, lakini kwa sharti moja kuwa baraza litakiwe kuamua kulingana na Maandiko. “Katika masuala yahusuyo neno la Mungu na imani,” aliongeza, “kila Mkristo ni jaji mzuri kama alivyo papa, hata kama anaungwa mkono na mabaraza milioni moja, laweza kuwa upande wake.”—Martyn 1:410. Hatimaye marafiki na maadui walishawishika kuwa juhudi zaidi kwa ajili ya upatanisho zisingefua dafu.PKSw 123.3

  Kama Mwanamatengenezo angesalimu amri katika pointi moja tu, Shetani na majeshi yake wangekuwa wamepata ushindi. Lakini uimara wake usioyumba ulikuwa njia ya kulikomboa kanisa, na mwanzo wa zama mpya na bora zaidi. Mvuto wa mtu huyu mmoja, aliyethubutu kufikiri na kutenda tofauti na wengine katika mambo ya dini, ulibadili kanisa na ulimwengu, siyo tu katika wakati wake, lakini pia katika vizazi vya baadaye. Uimara na uaminifu wake ungewaimarisha wote, hadi mwisho wa wakati, ambao wangepitia katika uzoefu unaofanana na huo. Nguvu na utukufu wa Mungu vilisimama juu ya mashauri ya wanadamu, juu ya nguvu nyingi za Shetani.PKSw 123.4

  Luther aliamurishwa mara moja na mamlaka ya mfalme arudi nyumbani, na alijua kuwa tangazo hili lingefuatwa haraka na hukumu yake. Mawingo ya vitisho yalielea juu ya njia yake; lakini alipokuwa akiondoka Worms, moyo wake ulikuwa umejaa furaha na sifa. “Shetani mwenyewe,” alisema, “alilinda ngome ya papa; lakini Kristo alikuwa ameweka ufa mpana katika ngome hiyo, na Shetani alikuwa amelazimishwa kukiri kuwa Bwana ana nguvu zaidi kuliko yeye.”—D'Aubigne, b. 7, ch. 11.PKSw 124.1

  Baada ya kuondoka kwake, bado akitamani kuwa uimara wake usitafsiriwe kuwa uasi, Luther alimwandikia mfalme. “Mungu, ambaye ni mchunguzi wa mioyo,” alisema, “kuwa niko tayari kwa juhudi zangu zote kumtii mfalme mtukufu, katika heshima au pasipokuwa na heshima, katika uzima au mauti, na pasipo kubagua cho chote isipokuwa tu neno la Mungu, ambalo kwalo mwanadamu anaishi. Katika mambo yote ya maisha haya ya sasa, uaminifu wangu hautatikisika, kwani hapa kupoteza au kupata siyo suala la msingi katika masuala ya wokovu. Lakini wakati masuala ya umilele yanapohusika, Mungu hapendi kuwa mwanadamu ajisalimishe kwa mwanadamu. Kwa sababu kujisalimisha kama huko katika masuala ya kiroho ni ibada halisi, na ibada inapaswa kufanywa kwa Muumbaji pekee.”—Ibid., b. 7, ch. 11.PKSw 124.2

  Akiwa safarini kutoka Worms, mapokezi ya Luther yalikuwa mazuri zaidi kuliko wakati alipokuwa akisafiri kuelekea huko. Viongozi wa kuu wa kanisa walimkaribisha mtawa aliyekwa ametengwa na kanisa, na watakawala wa kiraia walimheshimu mtu ambaye mfalme alikuwa amemhukumu. Alibembelezwa ahubiri, na, licha ya marufuku ya mfalme, alipanda tena kibwetani. “Sikuwahi kuahidi kulifunga minyororo neno la Mungu,” alisema, “wala sitafanya hivyo.”—Martyn 1:420.PKSw 124.3

  Muda mfupi baada ya kuondoka Worms, wafuasi wa papa walimzidi nguvu mfalme naye alitoa amri dhidi ya Luther. Katika amri hii Luther alitangazwa kuwa “Shetani mwenyewe katika umbo la mwanadamu na aliyevaa vazi la kitawa.”—D'Aubigne, b. 7, ch. 11. Iliagizwa kuwa mara tu cheti chake cha hakikisho la usalama kikiisha muda wake, hatua stahiki zichukuliwe kusitisha kazi yake. Watu wote walikatazwa kumtunza, kumpa chakula wala maji ya kunywa, au kwa njia ya neno au tendo, iwe hadharani au faraghani, kumsaidia au kumwunga mkono. Alitakiwa kukamatwa mahali popote ambapo angepatikana, na kukabidhiwa kwenye vyombo vya dola. Wafuasi wake pia walitakiwa kufungwa gerezani na mali zao kufilisiwa. Maandishi yake yalipaswa kuteketezwa, na, hatimaye, wote ambao wangethubutu kukaidi amri hii waliunganishwa katika hukumu ile. Elekta wa Saxony na viongozi katika ufalme waliokuwa marafiki wa Luther walikuwa wameondoka Worms mara tu baada yay eye kuondoka, na amri ya mfalme ilipata idhini ya Baraza Kuu. Sasa wafuasi wa Roma walifurahi sana. Walidhani hatima ya Matengenezo ilikuwa imetiwa muhuri.PKSw 124.4

  Mungu alitengeneza mlango wa kutokea kwa ajili ya mtumishi Wake katika saa hii ya hatari. Jicho lisilosinzia lilimfuata Luther katika safari zake zote, na moyo wa kweli na safi ulikuwa umedhamiria kumwokoa. Ilionekana wazi kuwa Roama isingetulia na kuridhika bila kumwua Luther; kumficha ndiko peke yake kumwokoa na makanwa ya simba. Mungu alimpa hekima Frederick wa Saxony ya kubuni mpango wa kumhifadhi Mwanamatengenezo. Kwa ushirikiano na marafiki wa kweli kusudi la Fredrick lilitekelezwa, na Luther kweli alifichwa mahali ambapo marafiki na maadui wake hawakuweza kumfikia. Alipokuwa njiani kuelekea nyumbani alikamatwa, akatengwa na wasaidizi wake, na kwa haraka alipitishwa mstuni hadi katika jumba lililoko Wartburg, katika ngome iliyotelekezwa mlimani. Kukamatwa kwake na kufichwa kwake kulifanywa kwa siri sana kiasi kwamba hata Frederick mwenyewe kwa muda mrefu hakujua ni wapi alikopelekwa. Kutojua huku hakukuwa kwa bahati mbaya; kwa kadiri Fredrick alivyokuwa hajui mahali Luther alipo, asingeweza kusema chochote juu yake. Alijiridhisha kuwa Mwanamatengenezo yuko salama, na kwake kujua hilo kulimfanya aridhike.PKSw 125.1

  Masika, kiangazi, na wakati wa joto ulipita, na wakati wa baridi ulifika, na Luther bado alibaki kuwa mfungwa. Aleanda na wafuasi wake walishangilia kwa kuwa nuru ya injili ilionekana kuzimika. Lakini badala yake, Mwanamatengenezo alikuwa anajaza taa yake mafuta kutoka katika ghala la ukweli; na nuru yake ilikuwa inaenda kuangaza kwa mng'aro mkubwa zaidi.PKSw 125.2

  Katika usalama wa kirafiki wa ngome ya Wartburg, Luther kwa muda alifurahia kuwa mbali na joto na vurugu za vita. Lakini hakuridhika kuishi kwa muda mrefu katika ukimya na mapumziko. Kama mtu aliyezoea maisha ya shughuli na misuguano mikali, asingeweza kuishi maisha ya kukaa tu. Katika siku zile za kujitenga hali ya kanisa iliinuka mbele yake, na alilia katika hali ya kukata tamaa: “Hivi kweli! Hakuna mtu katika siku za hivi karibuni wa hasira Yake, wa kusimama kama ukuta mbele ya Bwana, na aokoe Israeli!”— Ibid., b. 9, ch. 2. Kwa mara nyingine tena, mawazo yake yalirudi kwake yeye mwenyewe, na aliingiwa na hofu ya kushtakiwa kwa woga kwa kukimbia mapambano. Ndipo alijidharau yeye mwenyewe kwa uvivu wake na kupenda kwake kufurahisha nafsi yake. Lakini wakati huo huo alikuwa kila siku akifanya kazi nyingi zaidi ya zile ambazo mtu mmoja angeweza kufanya. Kalamu yake haikukaa kivivu. Wakati maadui zake wakijidanganya kuwa alikuwa amenyamazishwa, walishangaa na kuchanganyikiwa walipopata ushahidi mbashara kuwa alikuwa bado kazini. Idadi kubwa ya vijizuu, vilivyotokana na kalamu yake, vilikuwa vimesambaa katika nchi nzima ya Ujerumani. Alifanya pia huduma muhimu kuliko zote kwa watu wake wa Ujerumani kwa kutafsiri Agano Jipya katika lugha ya Kijerumani. Kutoka katika Patmo yake ya miamba aliendelea kwa karibu mwaka mzima kuhubiri injili na kukemea dhambi na makosa ya wakati wake.PKSw 125.3

  Lakini ilikuwa siyo tu kumhifadhi Luther dhidi ya hasira za maadui zake, wala kumwezesha kuwa na wakati wa ukimya kwa ajili ya kazi hizi, kuwa ndiyo sababu pekee za Mungu kumwondoa mtumishi Wake kwenye jukwaa la maisha ya hadharani. Kulikuwepo na matokeo yenye thamani kubwa zaidi kuliko haya ambayo yangeweza kupatikana. Katika upweke na maficho ya mapumziko yake ya mlimani, Luther alikuwa ametengwa na misaada ya kidunia na kufungiwa mbali na sifa za kibinadamu. Kwa hiyo aliokolewa kutoka katika hatari ya kuwa na kiburi na kujitumainia, vitu ambavyo mara nyingi husababishwa na mafanikio. Kwa njia ya mateso na kunyenyekeshwa alikuwa ameandaliwa tena kutembea kwa usalama juu ya vilele smbavyo alikuwa ameinuliwa kwa ghafla.PKSw 126.1

  Watu wanapofurahia uhuru ambao huletwa kwao kwa njia ya ukweli, wanakuwa na mwelekeo wa kuwasifu walee ambao Mungu anawatumia kuvunja minyororo ya makosa na ushirikina. Shetani hutafuta kuondoa mawazo na mapenzi kutoka kwa Mungu, na kuyaelekeza kwa mawakala wa kibinadamu; huongoza watu kuheshimu chombo na kupuuza Mkono unaoelekeza matukio ya uongozi wa Mungu. Mara nyingi viongozi wa dini wanaosifiwa na kuheshimiwa hivyo hupoteza hitaji la kumtegemea Mungu na huongozwa kujitumainia wenyewe. Matokeo yake wanatafuta kutawala akili na dhamiri za watu, walio na mwelekeo wa kutafuta uongozi wao badala ya kutafuta uongozi wa neno la Mungu. Kazi ya matengenezo mara nyingi imedumaa kwa sababu ya roho hii ambayo inatawala ndani ya wale wanaounga mkono matengenezo. Mungu analinda kazi ya Matengenezo dhidi ya hatari hii. Alitamani kazi ile isipokee chapa ya mwanadamu bali chapa ya Mungu. Macho ya watu yalikuwa yameelekezwa kwa Luther kama mfafanuzi wa ukweli; aliondolewa ili macho yote yaelekezwe kwa Mwasisi wa milele wa ukweli.PKSw 126.2

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents