Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Utangulizi

  Kabla ya kuingia kwa dhambi, Adamu alikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Muumbaji wake; lakini tangu mtu alipojitenga na Mungu kwa kuasi, jamii ya wanadamu imenyimwa fursa hii muhimu sana. Kwa njia ya mpango wa wokovu, hata hivyo, njia imefunguliwa ambapo wakazi wa dunia wanaweza tena kuwa na uhusiano na mbingu. Mungu amewasiliana na wanadamu kwa njia ya Roho Wake, na nuru ya Kimungu imetolewa kwa ulimwengu kwa njia ya ufunuo aliowapa watumishi aliowachagua. “Wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu” (2 Petro 1:21).PKSw 4.1

  Katika kipindi cha miaka elfu mbili na mia tano ya kwanza ya historia ya mwanadamu, hakukuwa na ufunuo ulioandikwa. Watu waliofundishwa na Mungu, waliwasilisha maarifa yao kwa wengine, na mawasiliano hayo yalirithishwa kutoka kwa baba kwenda kwa mtoto, kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Matayarisho ya neno lililoandikwa yalianza wakati wa Musa. Ufunuo uliovuviwa ulikusanywa pamoja na kuunda kitabu kilichovuviwa. Kazi hii iliendelea katika kipindi kirefu cha miaka elfu moja na mia sita—kuanzia kwa Musa, mwanahistoria wa uumbaji na sheria, hadi kwa Yohana, mwandishi wa ukweli mzuri wa injili.PKSw 4.2

  Biblia inamtaja Mungu kuwa ndiye mtunzi wa Biblia; lakini Biblia iliandikwa kwa mikono ya wanadamu; na katika mitindo tofauti ya vitabu vyake mbalimbali inadhihirisha tabia mbalimbali za waandishi kadhaa. Ukweli uliofunuliwa wote una “pumzi ya Mungu” (2 Timotheo 3:16); lakini umeelezwa katika maneno ya wanadamu. Yeye Aliye wa Milele kwa njia ya Roho Wake Mtakatifu aliangazia nuru katika akili na mioyo ya watumishi Wake. Aliwapa ndoto na njozi, ishara na mifano; na wale waliofunuliwa ukweli huo waliuweka katika mawazo na lugha ya kibinadamu.PKSw 4.3

  Amri Kumi zilitamkwa na Mungu Mwenyewe, na ziliandikwa kwa mkono Wake Mwenyewe. Zilitoka kwa Mungu, na hazikutokana na utunzi wa kibinadamu. Lakini Biblia, pamoja na ukweli wake wa Kimungu, umeelezwa katika lugha za kibinadamu, huonesha muungano wa Kimungu na kibinadamu. Muungano kama huo ulikuwepo katika asili ya Kristo, ambaye alikuwa Mwana wa Mungu na Mwana wa mtu. Kwa hiyo, huu ni ukweli unaoihusu Biblia, na ni ukweli uliomhusu Kristo, kwamba “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu” (Yohana 1:14).PKSw 4.4

  Ikiwa imeandikwa katika zama tofauti, na watu waliotofautiana katika hadhi na kazi, na katika uwezo wa kiakili na kiroho, vitabu vya Biblia huonesha tofauti kubwa katika mtindo, kadhalika tofauti katika asili ya masomo yanayofunuliwa. Miundo mbalimbali ya tungo imetumiwa na waandishi mbalimbali; mara nyingi ukweli ule ule umeelezwa na waandishi tofauti kila mmoja kwa namna yake. Na waandishi kadhaa wanapowasilisha somo kwa njia ya vipengele na mahusiano tofauti, kunaweza kuwepo, kwa msomaji wa juu juu, asiyekuwa makini, au asiyekuwa tayari kueleweshwa, tofauti au kupingana, ambapo mwanafunzi makini, mwenye kicho, aliye na utambuzi mzuri, anagundua mwafaka uliopo katika maandiko.PKSw 4.5

  Kama ulivyowasilishwa kupitia kwa watu tofauti, ukweli unatolewa kwa njia tofauti. Mwandishi mmoja anavutwa kueleza zaidi sehemu moja ya somo; anashikilia vipengele vinavyopatana na uzoefu wake au vilivyo katika uwezo wake wa ufahamu na uelewa; mwingine anashikilia sehemu tofauti; na kila mmoja, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, huwasilisha kile ambacho kimegusa akili yake kwa nguvu—sehemu tofauti ya ukweli, lakini kuna mwafaka kamili katika sehemu zote. Na kweli zilizofunuliwa hivyo huungana kuunda kitu kimoja kizima kikamilifu, kinachofaa kukidhi mahitaji ya watu katika mazingira na uzoefu wa maisha.PKSw 5.1

  Mungu amependezwa kuwasilisha ukweli Wake kwa ulimwengu kwa njia ya mawakala wa kibinadamu, na Yeye Mwenyewe, kwa njia ya Roho Wake Mtakatifu, aliwapa sifa watu na aliwawezesha kuifanya kazi hii. Aliongoza akili katika kuchagua cha kusema na cha kuandika. Hazina iliwekwa kama dhamana katika vyombo vya udongo, japokuwa ni hazina iliyotoka mbinguni. Ushuhuda umewasilishwa kwa njia ya maneno yasiyokuwa makamilifu ya lugha ya kibinadamu, japokuwa ni ushuhuda wa Mungu; na mtoto wa Mungu mtiifu, anayeamini anaona ndani yake utukufu wa nguvu ya Kimungu, ukiwa umejazwa neema na kweli.PKSw 5.2

  Katika neno Lake, Mungu amewapa watu maarifa muhimu kwa ajili ya wokovu. Maandiko Matakatifu yanapaswa kupokelewa kama ufunuo wenye mamlaka, usiokosea wa mapenzi Yake. Maandiko ni kiwango cha tabia, mfunuaji wa mafundisho, na kipimo cha uzoefu. “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema” (2 Timotheo 3:16, 17).PKSw 5.3

  Hata hivyo, ukweli kuwa Mungu amefunua mapenzi Yake kwa watu kwa njia ya neno Lake, hauondoi hitaji la uwepo na uongozi endelevu wa Roho Mtakatifu. Kinyume chake, Roho Mtakatifu aliahidiwa na Mwokozi wetu, kufunua neno kwa watumishi Wake, kuangazia na kutumia mafundisho yake. Na kwa kuwa ni Roho wa Mungu aliyeongoza katika uandishi wa Biblia, haiwezekani kuwa fundisho la Roho liwe kinyume na fundisho la neno.PKSw 5.4

  Roho hakutolewa—wala hawezi kutolewa—kuizidi Biblia; kwa kuwa Maandiko yanasema wazi kuwa neno la Mungu ni kiwango ambacho kwacho mafundisho yote na uzoefu vinapaswa kupimwa. Alisema mtume Yohana, “Msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani” (1Yohana 4:1). Na Isaya anasema, “Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi” (Isaya 8:20).PKSw 5.5

  Kazi ya Roho Mtakatifu imeaibishwa sana kutokana na makosa ya kundi la watu ambao, wakidai kuangaziwa Naye, wanadai kutokuwa na hitaji la kuongozwa na nenola Mungu. Wanasukumwa na hisia wanazodai kuwa sauti ya Mungu ndani ya roho. Lakini roho inayowatawala siyo Roho wa Mungu. Ufuataji huu wa hisia, huku wakipuuza Maandiko, unaweza kusababisha machafuko tu, udanganyifu na kuangamia. Unachochea zaidi mipango ya yule mwovu. Kwa kuwa huduma ya Roho Mtakatifu ni ya muhimu sana kwa kanisa la Kristo, ni moja ya mbinu za Shetani, kwa njia ya makosa ya wanaharakati na wazushi, kuifanya kazi ya Roho iaibishwe na kuwafanya watu wa Mungu wapuuze chanzo hiki cha nguvu ambacho Bwana wetu amekitoa.PKSw 6.1

  Kwa kupatana na neno la Mungu, Roho Wake alipaswa kuendeleza kazi ya neno la Mungu katika kipindi chote cha kazi ya kutangaza injili. Katika zama ambazo Maandiko ya Agano la Kale na Jipya yalitolewa, Roho Mtakatifu hakukoma kuwasilisha nuru kwa watu, kando ya mafunuo yaliyowekwa pamoja kuunda Biblia Takatifu. Biblia yenyewe inasimulia jinsi ambavyo, kwa njia ya Roho Mtakatifu, watu walipokea maonyo, ushauri, na maelekezo, katika mambo ambayo hayakuhusiana na utoaji wa Maandiko. Sehemu zingine zinataja manabii katika zama tofauti, ambao maneno yao hayakuandikwa popote. Katika hali inayofanana na hiyo, baada ya kukamilisha na kufunga orodha ya vitabu vinavyounda Biblia, Roho Mtakatifu alikuwa bado aendelee na kazi Yake ya kuangazia, kuonya, na kufariji watoto wa Mungu.PKSw 6.2

  Yesu aliwaahidi wanafunzi Wake, “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; ... na mambo yajayo atawapasha habari yake”(Yohana 14:26; 16:13). Maandiko yanafundisha wazi kuwa ahadi hizi, mbali kabisa na kutoishia kwa siku za mitume peke yake, zinaendelea kuwepo kwa ajili ya kanisa la Kristo katika zama zote. Mwokozi anawahakikishia wafuasi Wake, “Mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:20). Na mtume Paulo anaeleza kuwa karama na uongozi wa Roho Mtakatifu umo ndani ya kanisa “kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo” (Waefeso 4:12, 13).PKSw 6.3

  Mtume aliwaombea waumini wa Efeso akisema, “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na ... kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake kwetu sisi tunaoamini” (Waefeso 1:17-19). Huduma ya Roho mtakatifu katika kuangazia ufahamu na ufunguaji wa akili ili kuelewa mambo yenye kina ya neno takatifu la Mungu, ilikuwa ni baraka ambayo Paulo aliitafuta kwa ajili ya kanisa la Waefeso.PKSw 7.1

  Baada ya udhihirisho wa ajabu wa Roho Mtakatifu Siku ya Pentekoste, Petro aliwahimiza watu watubu na kubatizwa kwa jina la Kristo, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zao; na alisema: “Nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie” (Matendo 2:38, 39).PKSw 7.2

  Karibu sana na matukio ya siku kuu ya Mungu, Bwana kupitia kwa nabii Yoeli ameahidi udhihirishwaji maalumu wa utendaji mahsusi wa Roho Wake (Yoeli 2:28). Unabii huu ulitimizwa kwa sehemu kwa kumwagwa kwa Roho Siku ya Pentekoste; lakini utafikia kilele cha utimizwaji wake kwa udhihirishwaji wa neema ya Mungu wakati wa kufungwa kwa kazi ya injili.PKSw 7.3

  Pambano kuu kati ya wema na uovu litaendelea kuwa kubwa zaidi hadi mwisho wa wakati kabisa. Katika vizazi vyote, ghadhabu ya Shetani imeelekezwa kwa kanisa la Kristo; na Mungu ametoa neema Yake na RohoWake kwa watu Wake ili kuwaimarisha waweze kusimama dhidi ya nguvu za mwovu. Wakati mitume wa Kristo walipotakiwa kupeleka injili Yake ulimwenguni na kuiandika kwa ajili ya zama zote zijazo, walipewa mwangaza rasmi wa Roho. Lakini kwa kadiri kanisa linavyokaribia ukombozi wake wa mwisho, Shetani atafanya kazi kwa nguvu kubwa zaidi. Ameshuka kwenu “mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu” (Ufunuo 12:12). Atatenda “kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo” (2 Wathesalonike 2:9). Kwa miaka elfu sita, yule mdanganyifu ambaye wakati fulani aliwahi kuwa katika nafasi ya juu kuliko wote miongoni mwa malaika wa Mungu amejielekeza kikamilifu kufanya kazi ya udanganyifu na uuaji. Na uwezo wote na stadi za kishetani na hila zilizopatikana, ukatili wote uliokuzwa, katika kipindi cha mapambano haya ya zama zote, yatawakabili watu wa Mungu katika pambano la mwisho. Na katika wakati huu wa hatari inawapasa wafuasi wa Kristo kupeleka ulimwenguni onyo la ujio wa pili wa Bwana; na watu wanapaswa kuandaliwa kusimama mbele Yake wakati wa kuja Kwake bila, “mawaa wala aibu mbele yake” (2 Petro 3:14). Wakati huu utolewaji wa neema na nguvu ni wa muhimu zaidi kwa kanisa kuliko hata siku za mitume.PKSw 7.4

  Kwa njia ya mwangaza wa Roho Mtakatifu, matukio ya pambano ambalo limeendelea kwa muda mrefu kati ya wema na uovu yamefunuliwa kwa mwandishi wa kurasa hizi. Nyakati fulani fulani nimeruhusiwa kuangalia utendaji, katika zama tofauti, wa pambano kuu kati ya Kristo, Mfalme wa uzima, Mwasisi wa wokovu wetu, na Shetani, mfalme wa uovu, mwasisi wa dhambi, mwasi dhidi ya sheria takatifu ya Mungu. Uadui wa Shetani dhidi ya Kristo umedhihirishwa kwa wafuasi Wake. Chuki ile ile dhidi ya kanuni za sheria ya Mungu, sera ile ile ya upotoshaji, ambayo kwayo, uongo unapambwa ili uonekane kuwa ni ukweli, ambayo kwayo sheria za kibinadamu zinaheshimiwa badala ya sheria ya Mungu, na watu wanaelekezwa kuabudu kiumbe badala ya Muumbaji, inaonekana katika historia yote ya wakati uliopita. Juhudi za Shetani za kuwakilisha vibaya tabia ya Mungu, ili kuwafanya watu wawe na uelewa potofu kuhusu Muumbaji wao, na kuwafanya wamtazame kwa hofu na chuki badala ya upendo; jitihada zake za kuweka pembeni sheria ya Mungu, na kuwafanya watu wafikiri kuwa hawabanwi na masharti yake; na mateso yake dhidi ya wale wanaothubutu kupinga upotoshaji wake, daima zimetumika katika zama zote. Zinaonekana katika historia ya wazee, manabii, na mitume, wafia dini na wanamatengenezo.PKSw 7.5

  Katika pambano kuu la mwisho, Shetani atatumia sera ile ile, ataonesha roho ile ile, na atafanya kazi kwa lengo lile lile kama lilivyokuwa katika zama zilizotangulia. Kile kilichofanyika, kitafanyika, isipokuwa tu ni kwamba pambano kuu linalokuja litakuwa na ukubwa wa kutisha zaidi kuliko ulimwengu ulivyowahi kushuhudia wakati wowote hapo awali. Upotoshaji wa Shetani utakuwa wa kijanja zaidi, mashambulizi yake yatakuwa ya kudhamiria zaidi. Kama ingewezekana, anatamani awapotoshe hata wateule (Marko 13:22).PKSw 8.1

  Kwa kadiri ambavyo Roho wa Mungu amenifunulia kweli kuu za neno Lake, na matukio yaliyopita na yale yajayo, nimeagizwa kuwaeleza wengine kile ambacho kimefunuliwa—wafuatilie historia ya pambano katika zama zilizopita, na hususani kuyawasilisha ili kutoa mwangaza kuhusiana na pambano linalokuja haraka la wakati ujao. Ili kufikia lengo hili, nimejitahidi kuchagua na kuweka pamoja matukio katika historia ya kanisa kwa njia ambayo inasaidia kufuatilia ufunuo wa kweli kuu zinazopima ambazo katika vipindi tofauti zimetolewa kwa ulimwengu, ambazo zimeamsha hasira ya Shetani, na uadui wa kanisa linalopenda ulimwengu, na ambazo zimedumu kuwepo kwa njia ya wale ambao “hawakuyapenda maisha yao hadi kifo”PKSw 8.2

  Katika kumbukumbu hizi tunaona kielelezo cha pambano lililoko mbele yetu. Tunapozitafakari tukizingatia nuru ya neno la Mungu, na kwa njia ya mwangaza wa Roho Wake, tunaona hila za yule mwovu zikiwa wazi, na hatari zinazopaswa kuepukwa na wale ambao wataonekana kuwa “hawana mawaa” mbele za Bwana wakati wa ujio Wake.PKSw 8.3

  Matukio makuu ambayo yameweka alama katika maendeleo ya matengenezo katika zama zilizopita ni masuala ya kihistoria, ambayo yanajulikana sana na yanayotambuliwa katika ulimwengu wa Kiprotestanti; ni kweli ambazo haziwezi kupingwa na mtu ye yote. Historia hii nimeieleza kwa muhtasari, kulingana na makusudi ya kitabu hiki, na muhtasari ambao ni wa lazima kuzingatiwa, kweli zikiwa zimeelezwa kwa ufupi na kufinywa katika nafasi ndogo kwa kadiri ilivyoonekana kutosheleza uelewa stahiki wa matumizi yake. Katika sehemu zingine ambazo mwanahistoria ameyaweka pamoja matukio na kupata, maelezo mafupi, ya kina kuhusiana na somo husika, au ameeleza kwa muhtasari wa matukio kwa namna inayofaa, maneno yake yamenukuliwa; lakini katika maeneo mengine jina la mwandishi au kitabu kilichonukuliwa havikutajwa, kwa kuwa dondoo hazikunukuliwa kwa kusudi la kumtambua mwandishi kama mamlaka, bali kwa sababu kauli yake inasaidia wasilisho lililo tayari na lenye nguvu kuhusu somo husika. Katika kusimulia uzoefu na mitazamo ya wale wanaofanya kazi ya matengenezo katika nyakati zetu, matumizi kama hayo yamefanywa kuhusiana na kazi zao zilizochapishwa.PKSw 9.1

  Sio kusudi hasa la kitabu hiki kueleza kweli mpya kuhusu mapambano ya nyakati zilizopita ili kuibua kweli na kanuni zinazohusiana na matukio yajayo. Hata hivyo kama sehemu ya pambano kati ya nguvu za nuru na giza, kumbukumbu zote za wakati uliopita zinaonekana kuwa na maana mpya; na kwa njia ya kumbukumbu hizo nuru inaangazia wakati ujao, ikiangazia njia ya wale ambao, kama wanamatengenezo wa zama zilizopita, wataitwa, hata kwa kuhatarisha faida za kidunia, kushuhudia “kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu Kristo.”PKSw 9.2

  Kufunua matukio ya pambano kuu kati ya ukweli na uongo; kuweka wazi hila za Shetani, na mbinu ambazo kwazo anaweza kupingwa kwa mafanikio; kutoa suluhisho toshelevu la tatizo kubwa la uovu, kuangaza nuru juu ya mwanzo na mwisho wa dhambi na kuonesha haki na ukarimu wa Mungu katika kushughulika na viumbe Wake; na kuonesha asili ya sheria Yake takatifu na isiyobadilika, ndiyo kusudi la kitabu hiki. Ili kwa njia ya mvuto wake, roho ziweze kuokolewa kutoka katika nguvu za giza, na kuwa “washirika wa urithi wa watakatifu walio nuruni,” kwa ajili ya utukufu Wake Yeye aliyetupenda, na aliyejitoa kwa ajili yetu, ndiyo ombi la dhati la mwandishi.PKSw 9.3

  E.G.W.

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents