Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 3—Zama za Giza la Kiroho

  Mtume Paulo, katika barua yake ya pili kwa Wathesalonike, alitabiri uasi mkuu ambao ungetokana na uanzishwaji wa mamlaka ya upapa. Alitangaza kuwa siku ya Kristo isingekuja, “usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” Na zaidi hapo, mtume Paulo anatahadharisha ndugu zake kuwa “ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa” (2 Wathesalonike 2:3, 4, 7). Hata katika tarehe hizo za awali, aliona, yakiingia polepole kanisani, makosa ambayo yangetayarisha njia kwa ajili ya ukuaji wa upapa.PKSw 35.1

  Kidogo kidogo, mwanzoni kwa siri na katika hali ya ukimya, na hatimaye kwa uwazi zaidi kwa kadiri makosa yalivyozidi kupata nguvu na kutawala akili za watu, “siri ya uasi” iliendeleza kazi yake ya udangayifu na kufuru. Karibu pasipokutambua, mila na desturi za upagani ziliingia ndani ya kanisa. Roho ya kulegeza masharti na kuiga ilidhibitiwa kwa muda kwa mateso makali ambayo kanisa liliyapata chini ya upagani. Lakini mara tu mateso yalipokoma, na Ukristo ukaingia katika mabaraza na nyumba za kifalme, kanisa liliweka pembeni usahili na unyenyekevu wa Kristo na wa mitume Wake na badala yake lilivaa kujionesha na kiburi cha makuhani wa kipagani na watawala; na badala ya matakwa ya Mungu, kanisa liliweka nadharia na desturi za wanadamu. Uongofu wa juu juu wa Konstantini, katika sehemu ya awali ya karne ya nne, ulileta furaha kubwa; na ulimwengu, uliojifunika joho la utakatifu bandia, uliingia kanisani. Upagani, wakati ukionekana kana kwamba umekwisha, ulishinda. Roho yake ilitawala kanisa. Mafundisho yake, sherehe, na ushirikina vilijumuishwa katika imani na ibada ya watu waliodai kuwa wafuasi wa Kristo.PKSw 35.2

  Muungano huu wa upagani na Ukristo uliwezesha kuzaliwa kwa “mtu wa dhambi” aliyetabiriwa katika unabii kuwa atapingana na kujiinua juu ya Mungu. Mfumo huo mkubwa wa dini ya uongo ni chombo maalumu cha nguvu ya Shetani—mnara wa kumbukumbu ya juhudi zake kukaa juu ya kiti cha enzi na kuitawala dunia kulingana na mapenzi yake.PKSw 35.3

  Shetani wakati fulani alijaribu kuunda umoja na Kristo. Alimjia Mwana wa Mungu katika jangwa la majaribu, na akimwonesha falme za ulimwengu na utukufu wa falme hizo, akiahidi kuziweka katika Mikono Yake ikiwa tu atakiri ukuu wa mfalme wa giza. Kristo alimkemea mjaribu mwenye kiburi na kumlazimisha aondoke. Lakini Shetani anafanikiwa sana anapomletea mwanadamu majaribu hayo hayo. Ili kupata mapato na heshima za kidunia, kanisa liliongozwa kutafuta msaada na uungwaji mkono wa watu wakubwa duniani; na baada ya kumwacha Kristo kwa njia hiyo, lilishawishika kujisalimisha chini ya wakala wa Shetani—askofu wa Rumi.PKSw 35.4

  Ni moja ya mafundisho makuu ya Urumi kuwa papa ni kichwa kinachoonekana cha kanisa la ulimwengu la Kristo, aliyekabidhiwa mamlaka kuu juu ya maaskofu na wachungaji katika sehemu zote za dunia. Zaidi ya hayo, papa amepewa majina ya Mungu mwenyewe. Anatambulishwa kuwa yeye ni “Bwana Mungu Papa” (tazama Kiambatanisho), na anatangazwa kuwa yeye hakosei. Anadai aabudiwe na watu wote. Dai lile lile lililotolewa na Shetani katika jangwa la majaribu bado linatolewa naye kupitia kwa Kanisa la Rumi, na kuna idadi kubwa ya watu wanaomwabudu.PKSw 36.1

  Lakini watu wanaomcha na kumheshimu Mungu wanakabiliana na madai haya ya kutisha kama Kristo alivyokabiliana na madai ya adui mkuu: “Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake” (Luka 4:8). Mungu hajadokeza mahali popote katika neno Lake kuwa amemteua mtu ye yote kuwa kichwa cha kanisa. Fundisho la ukuu wa papa linapingana kabisa na mafundisho ya Maandiko. Papa hawezi kuwa na mamlaka juu ya kanisa la Kristo isipokuwa kwa kujichukulia madaraka.PKSw 36.2

  Viongozi wa kanisa la Rumi wanaendelea kuleta mashitaka dhidi ya Waprotestanti kuwa wameleta mafundisho ya uongo na kwa makusudi wakajitenga na kanisa. Lakini mashtaka haya ni yao hasa. Wao ndio walioishusha bendera ya Kristo na kuikana “imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu” (Yuda 3).PKSw 36.3

  Shetani alijua vizuri kuwa Maandiko Matakatifu yangewawezesha watu kutambua udanganyifu na kupinga nguvu zake. Ilikuwa ni kwa njia ya neno hata Mwokozi wa ulimwengu aliweza kuyapinga mashambulizi yake. Kwa kila shambulizi, Kristo alijikinga kwa ngao ya ukweli wa milele, akisema, “Imeandikwa.” Kwa kila pendekezo la adui, aliweka pingamizi la hekima na nguvu ya neno. Ili Shetani adumishe utawala wake juu ya wanadamu, na kustawisha mamlaka ya kipapa, alilazimika kuwafanya watu wasiyajue Maandiko. Biblia inamwinua Mungu na inawaweka wanadamu katika nafasi zao stahiki; kwa hiyo kweli zake takatifu ilipaswa zifichwe na kukandamizwa. Mantiki hii iliigwa na Kanisa la Kirumi. Kwa mamia ya miaka usambazaji wa Biblia ulipigwa marufuku. Watu walikatazwa kuisoma au kuwa nayo katika nyumba zao, na mapadre na maaskofu wasiozingatia kanuni walitafsiri mafundisho yake kuunga mkono mitazamo yao. Kwa njia hiyo papa akatokea kukubaliwa duniani kote kama mwakilishi wa Mungu duniani, aliyepewa mamlaka juu ya kanisa na dola.PKSw 36.4

  Baada ya mtambuzi wa makosa kuondolewa, Shetani alifanya kazi kulingana na mapenzi yake. Unabii ulikwisha tangaza kuwa upapa utafikiri “kubali nyakati na sheria” (Danieli 7:25). Hakuchelewa kuifanya kazi hii. Ili kuwapatia waongofu kutoka katika upagani mbadala wa ibada ya sanamu, na kwa njia hiyo kuhamasisha kuukubali Ukristo kwa jina tu, ibada ya sanamu na mifupa ya watakatifu polepole viliingizwa katika ibada ya Kikristo. Amri ya baraza kuu (Tazama Kiambatisho) hatimaye ilianzisha mfumo huu wa ibada ya sanamu. Kukamilisha kazi ya kufuru, Rumi iliondoa amri ya pili kutoka katika sheria ya Mungu, amri inayokataza ibada ya sanamu, na ikaigawa amri ya kumi kuwa mbili, ili kudumisha idadi ya amri kumi.PKSw 36.5

  Roho ya kuungana na upagani ilifungua njia ya kuhafifisha zaidi mamlaka ya Mungu. Shetani, akifanya kazi kupitia viongozi wa kanisa wasiojiweka wakfu kikamilifu, alichezea amri ya nne pia, na kujaribu kuondoa Sabato ya kale, siku ambayo Mungu aliibariki na kuitakasa (Mwanzo 2:2, 3), na badala yake akainua siku kuu iliyoadhimishwa kama “siku ya heshima ya jua.” Badiliko hili awali halikufanywa kwa uwazi. Katika karne za kwanza Sabato ya kweli ilitunzwa na Wakristo wote. Walikuwa na wivu kwa ajili ya heshima ya Mungu, na, wakiamini kuwa sheria Yake haibadiliki, walilinda kwa bidii utakatifu wa kanuni zake. Lakini kwa hila kubwa Shetani alifanya kazi kupitia mawakala wake kutimiza kusudi lake. Ili kuzifanya akili za watu ziikubali Jumapili kirahisi, Jumapili ilifanywa kuwa siku kuu ya kuheshimu ufufuo wa Kristo. Huduma za kidini zilifanywa siku hiyo; hata hivyo ilichukuliwa kuwa siku ya maburudisho, Sabato ikiwa bado inaadhimishwa kama siku takatifu.PKSw 37.1

  Ili kuandaa njia kwa ajili ya kazi ambayo alikuwa amekusudia kuifanya baadaye, Shetani alikuwa amewaongoza Wayahudi, kabla ya ujio wa Kristo, kuibebesha mizigo Sabato mzigo wa masharti magumu sana, akafanya utunzaji wake kuwa mzigo. Sasa, akinufaishwa na mtazamo hasi ambao alikuwa amesababisha Sabato kutazamwa, aliifanya idharaulike kwa kuiita mila na desturi ya Kiyahudi. Wakati Wakristo walio wengi wakiendelea kuiadhimisha Jumapili kama siku kuu ya furaha, aliwaongoza, ili kuonesha chuki yao kwa dini ya Kiyahudi, kuifanya Sabato kuwa siku ya kufunga, siku ya huzuni na maumivu.PKSw 37.2

  Katika sehemu ya kwanza ya karne ya nne mfalme Konstantini alitoa amri kuifanya Jumapili kuwa siku ya sherehe katika Dola lote la Rumi (Tazama Kiambatanisho). Siku ya jua iliheshimiwa na raia wake wapagani na iliheshimiwa pia na raia wake Wakristo; ilikuwa sera ya mfalme kuunganisha makundi mawili yenye maslahi yanayokinzana ya upagani na Ukristo. Alishawishiwa kufanya hivyo na maaskofu wa kanisa, ambao, kwa kusukumwa na tamaa na kiu ya madaraka, walitambua kuwa ikiwa siku ile ile ingeadhimishwa na Wakristo na wapagani, ingewahamasisha wapagani kuupokea Ukristo kwa jina na hivyo kuongeza nguvu na utukufu wa kanisa. Lakini wakati Wakristo wengi wacha Mungu waliongozwa pole pole kuikubali Jumapili kama siku iliyo na kiasi fulani cha utakatifu, bado waliendelea kuishika Sabato ya kweli kuwa ndiyo siku takatifu ya Bwana na waliiadhimisha ili kuitii amri ya nne.PKSw 37.3

  Mdanganyaji mkuu alikuwa bado hajamaliza kazi yake. Alidhamiria kuukusanya ulimwengu wa Kikristo chini ya bendera yake na kupitishia madaraka yake chini ya mwakilishi wake, papa mwenye kiburi aliyedai kuwa mwakilishi wa Kristo. Kwa kupitia kwa wapagani walioongoka nusu, maaskofu wenye tamaa, na waumini wa kanisa wapenda dunia alifanikisha kusudi lake. Mabaraza makubwa yaliendeshwa mara kwa mara, ambapo viongozi wakubwa wa kansia walikusanywa pamoja kutoka duniani kote. Karibu katika kila baraza Sabato iliyowekwa na Mungu ilikandamizwa chini zaidi, wakati huo huo Jumapili iliinuliwa juu. Kwa njia hiyo sherehe ya kipagani ilikuja hatimaye iliheshimiwa kama agizo takatifu, ilhali Sabato ya Biblia ilitangazwa kuwa mabaki ya dini ya Kiyahudi, na uadhimishaji wake ulitangazwa kuwa umelaaniwa.PKSw 38.1

  Mwasi mkuu akafanikiwa kujiinua “juu ya kila kiitwacho Mungu, au kuabudiwa” (2 Wathesalonike 2:4). Alijaribu kubadili kanuni pekee ya sheria ya Mungu ambayo bila shaka inawaelekeza wanadamu kwa Mungu wa kweli na aliye hai. Katika amri ya nne, Mungu anafunuliwa kuwa ni Muumbaji wa mbingu na nchi, na hapa anatofautishwa na miungu ya uongo. Ilikuwa ni kwa ajili ya kumbukumbu ya kazi ya uumbaji ambapo siku ya saba ilitakaswa kama siku ya mapumziko kwa ajili ya mwanadamu. Sabato ilikusudiwa kumweka Mungu aliye hai mbele ya akili za wanadamu kama chanzo cha uzima na Yeye anayestahili kicho na ibada. Shetani anapambana kuondoa kicho cha wanadamu kwa Mungu, na kuondoa utii wao kwa sheria Yake; hivyo, anaelekeza juhudi zake hususani dhidi ya amri inayoelekeza watu kwa Mungu Muumbaji.PKSw 38.2

  Waprotestanti sasa wanadai kuwa ufufuo wa Kristo uliifanya Jumapili kuwa Sabato ya Wakristo. Lakini hakuna ushahidi wa maandiko. Heshima kama hiyo haikutolewa kwa siku hivyo na Kristo au mitume. Uadhimishaji wa Jumapili kama siku ya ibada ya Wakristo ulitokana na “siri ya uasi” (2 Wathesalonike 2:7) ambayo, hata katika wakati wa Paulo, ilikuwa imeanza kazi yake. Ni wapi na ni lini Bwana aliidhinisha mtoto huyu wa upapa? Ni sababu gani halali inaweza kutolewa kwa ajili ya badiliko ambalo Maandiko hayaliidhinishi?PKSw 38.3

  Katika karne ya sita, upapa ulikuwa umeshajijenga kikamilifu. Kiti chake cha mamlaka kilisimikwa katika mji mkuu wa dola, na askofu wa Rumi alitangazwa kuwa kiongozi wa kanisa lote. Upagani ulisalimisha nafasi yake kwa upapa. Joka alimpa mnyama “nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi” (Ufunuo 13:2). Na sasa ikaanza miaka 1260 ya ukandamizaji wa kipapa uliotabiriwa katika unabii wa Danieli na Ufunuo (Danieli 7:25; Ufunuo 13:5-7; Tazama Kiambatanisho). Wakristo walilazimishwa kuchagua ama kusalimisha uadilifu wao na kukubali sherehe na ibada za kipapa, au kuharibu maisha yao gerezani au kuuawa kwa msumeno, moto, au shoka. Ndipo yalitimizwa maneno ya Yesu: “Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu” (Luka 21:16, 17). Mateso yalifungulia dhidi ya waaminifu kwa hasira kali zaidi kuliko ilivyowahi kutokea hapo awali, na ulimwengu uligeuka kuwa uwanja mkubwa wa vita. Kwa mamia ya miaka, kanisa la Kristo lilikimbilia mafichoni na mahali pa upweke. Nabii anasema: “Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu na mia mbili na sitini” (Ufunuo 12:6).PKSw 38.4

  Kitendo cha Kanisa la Rumi kupata mamlaka kuliashiria kuanza kwa Zama za Giza. Kwa kadiri mamlaka yake yalivyoongezeka, kina cha giza kiliongezeka zaidi. Imani ilihamishwa kutoka kwa Kristo, msingi wa kweli, kwenda kwa papa wa Rumi. Badala ya kumtumaini Mwana wa Mungu ili kupata msamaha wa dhambi na wokovu wa milele, watu walimtazama papa, na mapadri na maaskofu ambao alikasimu madaraka kwao. Walifundishwa kuwa papa alikuwa mpatanishi wao wa kidunia na kuwa hakuna ambaye angeweza kumwendea Mungu isipokuwa kwa kupitia kwake; na, zaidi ya hapo, kwamba alisimama mahali pa Mungu kwao na kwa hiyo alitakiwa kutiiwa bila maswali. Kukiuka matakwa yake ilikuwa sababu tosha ya kustahili adhabu kali iliyotolewa kwenye miili na roho za wakosaji. Hivyo akili za watu ziliondolewa kwa Mungu na kupelekwa kwa wanadamu wanaokosea, wenye mapungufu, na wakatili, zaidi ya hao, akili zao zilielekezwa kwa mfalme wa giza mwenyewe, aliyetumia nguvu zake kupitia kwao. Dhambi ilijificha katika vazi la utakatifu. Maandiko yanapokandamizwa, na mwanadamu aanapojidhania kuwa yuko juu ya wote, tutegemee kuona ulaghai, hila udanganyifu na uovu wa kudhalilisha. Kwa kuziinua sheria na desturi za wanadamu kulijitokeza ufisadi ambao daima hujitokeza kwa sababu ya kuiweka pembeni sheria ya Mungu.PKSw 39.1

  Hizo zilikuwa siku za hatari kwa kanisa la Kristo. Wainua bendera waaminifu walikuwa wachache kweli kweli. Ingawa ukweli haukuachwa bila mashahidi, lakini kwa nyakati fulani ilionekana kuwa makosa na ushirikina vingeshinda kabisa, na dini ya kweli ingefunika kabisa duniani. Injli haikusikika kabisa, badala yake kaida mbalimbali za dini ziliongezwa, na watu walibebeshwa mizigo na shughuli nzito.PKSw 39.2

  Watu walifundishwa siyo tu kumwangalia papa kama mpatanishi wao, bali kutumainia kazi zao wenyewe kuwapatanisha kwa ajili ya dhambi. Safari ndefu za kwenda kuhiji, matendo ya kitubio, na ibada ya mifupa ya wataktifu, ujenzi wa makanisa, na maeneo matakatifu, na madhabahu, malipo ya pesa nyingi kwa kanisa—haya na matendo mengi kama hayo yaliingizwa ili kumfurahisha Mungu au kupata upendeleo Wake; kana kwamba Mungu alikuwa kama wanadamu. Anayekasirishwa kwa mambo madogo madogo, au anayepozwa kwa zawadi na matendo ya kitubio!PKSw 39.3

  Pamoja na hayo uovu huo ulishamiri hata miongoni mwa viongozi wa Kanisa la Kirumi, mvuto wake ulionekana kuongezeka kila kukicha. Karibu na mwisho wa karne ya nane, waumini wa mfumo wa upapa walidai kuwa katika zama za kwanza za kanisa maaskofu wa Rumi walikuwa na nguvu ile ile ya kiroho ambayo wanayo kwa sasa. Kuthibitisha dai hili, mbinu za aina fulani lazima zitumike kulipatia mamlaka; na mbinu hiyo mara moja ilipendekezwa na baba wa uongo. Maandishi ya awali yalighushiwa na watawa. Matamko ya mabaraza ambayo hayakuwahi kusikika yaligunduliwa, yakithibitisha kuwa papa ndiye kiongonzi mkuu duniani tangu nyakati za awali. Na kanisa lililokuwa limetupitilia mbali ukweli kwa tamaa lilikubali mambo hayo ya uongo (Tazama Kiambatanisho).PKSw 39.4

  Wajenzi wachache waaminifu juu ya msingi wa kweli (1 Wakorintho 3:10, 11) walichanganywa na kuzuiwa wakati takataka za mafundisho ya uongo zilipozuia kazi. Kama wajenzi wa kuta za Yerusalemu wakati wa Nehemia baadhi waliposema: “Nguvu zao wachukuao mizigo zimedhoofika, na kifusi tele zipo; tusiweze kuujenga ukuta” (Nehemia 4:10). Wakiwa wamechoshwa na pambano lisiloisha dhidi ya hila, uovu, na kila kikwazo ambacho Shetani aliweza kukibuni kuzuia maendeleo yao, baadhi waliokuwa wajenzi waaminifu walivunjika moyo; na kwa ajili ya amani na usalama wa mali zao na maisha yao, waligeuka na kuuacha msingi wa kweli. Wengine, pasipo kuchoshwa na upinzani wa maadui zao, walitangaza bila hofu: “Msiwaogope; mkumbukeni Bwana, aliye mkuu mwenye kuogofya” (Aya ya 14); na waliendelea na kazi, kila mmoja akiwa na upanga kiunoni mwake (Waefeso 6:17).PKSw 40.1

  Roho ile ile ya chuki na upinzani kwa ukweli imewavuvia maadui wa Mungu katika kila zama, na ukeshaji na uaminifu ule ule umewavuvia watumishi wa Mungu. Maneno ya Kristo kwa mitume wa kwanza yanatumika kwa wanafunzi Wake hadi mwisho wa wakati: “Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni” (Marko 13:37).PKSw 40.2

  Giza lilionekana kuongezeka zaidi. Ibada ya sanamu ikaonekana kuwa jambo la kawaida, na maombi yakatolewa kwa sanamu. Desturi iliyokuwa ya kishirikina kabisa ikastawi. Akili za watu zilitawaliwa kabisa na ushirikina kiasi ambacho busara ilionekana kupoteza mwelekeo wake. Wakati mapadri na maaskofu wenyewe walikuwa wapenda anasa, wenye tamaa, na mafisadi, ilitarajiwa kabisa kuwa watu waliowategemea ili kupata mwongozo kwao walizama katika ujinga na uovu.PKSw 40.3

  Hatua nyingine katika utawala wa upapa ilichukuliwa, wakati, katika karne ya kumi na moja, Papa Gregori VII alipotangaza ukamilifu wa Kanisa la Kirumi. Miongoni mwa mapendekezo aliyoyaleta ni lile linalodai kuwa kanisa halijawahi kukosea, wala halitakosea, kwa mujibu wa Maandiko. Lakini uthibitisho wa Maandiko haukuambatanishwa na dai hilo. Papa mwenye kiburi alidai pia kuwa na mamlaka ya kuwaondoa wafalme, na alitangaza kuwa hakuna hukumu ambayo aliyoitangaza ingeweza kutenguliwa na mtu ye yote yule, bali kwamba alikuwa na mamlaka ya kutengua maamuzi ya wengine wote (Tazama Kiambatanisho).PKSw 40.4

  Mfano wa wazi wa ukatili wa huyu anayedai kuwa hakosei ulionekana katika namna alivyomshughulikia Mfalme wa Ujerumani, Henri IV. Kwa ujasiri wake wa kutotambua mamlaka ya papa, mfalme huyu alitangazwa kuondolewa katika ushirika wa kanisa na kuondolewa madaraka ya ufalme. Kwa hofu ya kuachwa na vitisho vya wasaidizi wake ambao walishawishiwa na agizo la papa dhidi yake, Henri aliona umuhimu wa kufanya amani na Rumi. Akiandamana na mkewe na mtumishi wake mwaminifu walivuka milima ya Alps wakati wa majira ya baridi, ili ajinyenyekeshe mbele ya papa. Alipofika karibu na jengo ambalo Gregori alikuwa amekwenda kupumzika, alipelekwa bila walinzi wake, katika ukumbi wa nje, na pale, katika baridi kali ya majira ya baridi, kichwa chake kikiwa wazi bila kufunikwa cho chote, na miguu iliyo peku, alisubiri kupata ruhusa ya papa ili aende kwake. Mpaka alipoendelea kusubiri kwa siku tatu akifunga na kuungama, ndipo papa alipokubali kumpa msamaha. Hata hivyo ilikuwa kwa sharti kuwa mfalme asubiri kibali cha papa kabla ya kurudi madarakani au kutumia mamlaka ya kifalme. Na Gregori, akifurahia ushindi wake, alitamba kuwa ilikuwa jukumu lake kushusha kiburi cha wafalme.PKSw 40.5

  Tofauti iliyoje kati ya tabia kandamizi ya huyu papa mwenye kiburi na unyenyekevu na upole wa Kristo, anayejitambulisha kama anayesihi kwenye mlango wa moyo ili aingie, ili alete msamaha na amani, na ambaye aliwafundisha wanafunzi Wake: “Na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu” (Mathayo 20:27).PKSw 41.1

  Karne zilizofuata zilishuhudia ongezeko la daima la makosa katika mafundisho yaliyotolewa na Roma. Hata kabla ya kuanzishwa kwa upapa mafundisho ya wanafalsafa wa kipagani yalikuwa yakitumiwa na yalikuwa na mvuto mkubwa kanisani. Wengi wa wale waliodai kuwa wameongoka bado waliendelea kushikilia kanuni za msingi za falsafa zao za kipagani, na siyo tu kuwa waliendelea kujifunza wenyewe peke yao, bali walianza kuzifundisha falsafa hizo kwa wengine kwa madai kuwa ilikuwa njia ya kueneza mvuto wao miongoni mwa wapagani. Makosa makubwa yaliingizwa katika imani ya Kikristo kwa njia hiyo. Mashuhuri miongoni mwa makosa hayo ilikuwa imani ya asili ya kutokufa ya mwanadamu na uendelevu wa ufahamu wa mtu aliyekufa. Fundisho hili liliweka msingi ambao juu yake Rumi ilijenga maombi kwa watakatifu waliokufa na kumtukuza Bikra Maria. Kutokana na fundisho hili pia kulizuka uzushi wa moto wa milele kwa watu wasiotubu, fundisho ambalo liliingizwa mapema kabisa katika imani ya kipapa.PKSw 41.2

  Ndipo njia iliandaliwa kwa ajili ya uingizwaji wa ugunduzi mwingine wa upagani, ambao Rumi iliuita purgatori, uliotumika kuwaogofya watu wengi waliokwishazoezwa kupokea na kuamini kila fundisho na waliokwisha aminishwa ushirikina. Kwa njia ya fundisho hili la uongo inaonesha kuwa kuna mahali pa mateso, mahali ambapo roho za wale ambao hawastahili hukumu ya milele wanapaswa kupata adhabu kwa ajili ya dhambi zao, na ambapo, wakishasafishwa uchafu wao, wanaruhusiwa kuingia mbinguni (Tazama Kiambatanisho).PKSw 41.3

  Bado kulikuwa na uongo mwingine uliohitajika kuwezesha Rumi kunufaika kutokana na hofu na uovu wa waumini. Fursa hii iliwezeshwa na fundisho la msamaha. Ondoleo kamili la dhambi, za wakati uliopita, za wakati huu, na za wakati ujao, na kuachiliwa maumivu au adhabu zo zote zinazomkabili mtu, viliahidiwa kwa wote ambao wangejiorodhesha katika vita vya papa na kupanua mipaka ya utawala wake duniani, kuwaadhibu maadui zake, au kuwaangamiza wale waliodiriki kukataa ukuu wake wa kiroho. Watu pia walifundishwa kuwa kwa kulipa pesa kwa kanisa wanaweza kujinasua kutoka katika dhambi, na pia kunasua roho za rafiki zao waliokufa ambao walikuwa wamefungiwa katika ndimi za moto zitesazo za purgatori. Kwa njia hiyo Rumi ilijaza hazina zake ili kudumisha ukuu, raha, na uovu wa yule aliyejifanya kuwa mwakilishi wa Yule ambaye hakuwa na mahali pa kulaza kichwa Chake (Tazama Kiambatanisho)PKSw 42.1

  Fundisho la Biblia la Meza ya Bwana liliondolewa na badala yake ikawekwa kafara ya ibada ya sanamu ya misa. Makasisi wa kipapa walijifanya, kwa sherehe zisizo na maana, kubadilisha mkate na divai ya kawaida kuwa “mwili na damu ya Kristo” halisi—Cardinal Wiseman, The Real Presence of the Body and Blood of Our Lord Jesus Christ in the Blessed Eucharist, Proved From Scripture, lecture 8, sec. 3, par. 26. Kwa madai ya kiburi na kufuru, walidai hadharani kuwa walikuwa na uwezo wa kumwumba Mungu, Muumbaji wa vitu vyote. Wakristo walitakiwa, kwa tishio la kifo, kuapa kuwa wanaamini fundisho hili la uongo na la kutisha, linalotukana Mbingu. Watu wengi waliokataa waliunguzwa kwa ndimi za moto (Tazama Kiambatanisho).PKSw 42.2

  Katika karne ya kumi na tatu ilianzishwa taasisi ya kutisha kuliko taasisi zote za upapa—Mahakama ya Kanisa Katoliki ya kukomesha uasi. Mfalme wa giza aliwahemsha viongozi wa ngazi mbalimbali za upapa. Katika mabaraza yao ya siri Shetani na malaika zake waliendesha akili za watu waovu, bila kuonekana kati kati yao alisimama malaika wa Mungu akiandika kumbukumbu za kutisha za maamuzi yao na kuandika historia ya matendo ya kutisha sana kiasi cha kutofaa kuonwa na macho ya wanadamu. “Babeli mkuu” alilewa kwa “damu za watakatifu.” Kumbukumbu za mamilioni ya wafia dini zilimlilia Mungu kwa ajili ya kisasi dhidi ya mamlaka asi.PKSw 42.3

  Upapa ulikuwa dikteta wa ulimwengu. Wafalme na wafalme wakuu walipiga magoti kwa papa wa Kirumi. Hatima za watu, za muda mfupi na milele, zilionekana kuwa chini ya utawala wake. Kwa mamia ya miaka mafundisho ya Rumi yalipokelewa na watu wengi na bila maswali, kaida zake zilifanywa kwa kicho, sherehe zake zilisherehekewa na wote. Viongozi wake waliheshimiwa na kutunzwa kwa ukarimu. Hakuna wakati wowote mwingine ambapo Kanisa la Kirumi lilipata heshima, ukuu au mamlaka kama hayo.PKSw 42.4

  Lakini”mchana wa upapa ulikuwa usiku wa manane wa ulimwengu.”—J. A. Wylie, The History of Protestantism, b. 1, ch. 4. Maandiko Matakatifu yalikuwa hayajulikani kwa kiwango kikubwa, siyo tu kwa watu wa kawaida, lakini hata kwa mapadri. Kama Mafarisayo wa zamani, viongozi wa kipapa walichukia nuru iliyofunua dhambi zao. Sheria ya Mungu, kiwango cha utakatifu, ilipoondolewa, walitumia madaraka bila mipaka, na walitenda uovu bila udhibiti. Udanganyifu, tamaa ya mali, ufujaji wa mali vilishamiri. Watu hawakujizuia kutenda uhalifu ambao kwao wangeweza kujipatia mali au cheo. Makazi ya mapapa na maaskofu yalikuwa mazingira ya uovu na ufisadi. Baadhi ya mapapa waliotawala walikuwa na hatia ya uhalifu mkubwa kiasi kwamba baadhi ya watawala wa kidunia walijaribu kuwapindua viongozi hawa wa kanisa kama watu wakatili sana wasiostahili kuvumiliwa. Kwa karne nyingi Ulaya haikupiga hatua yo yote katika elimu, sanaa, au ustaarabu. Udumavu wa kimaadili na kiakili viligubika ulimwengu wa Kikristo.PKSw 43.1

  Hali ya ulimwengu chini ya mamlaka ya Kirumi iliwakilisha utimizo wa kutisha na kuogofya wa maneno ya nabii Hosea: “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe:... kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.” “Hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi. Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu hugusana na damu” (Hosea 4:6, 1, 2). Hayo yalikuwa matokeo ya kutupilia mbali neno la Mungu.PKSw 43.2

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents