Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 17—Wajumbe wa Asubuhi

  Moja ya vipengele vya ukweli uliofunuliwa katika Biblia ambavyo ni vya muhimu sana na vyenye utukufu mwingi ni kile kinachohusu ujio wa pili wa Kristo anapokuja kumalizia kazi kubwa ya ukombozi. Kwa wasafiri watu wa Mungu, waliokwisha kuondoka muda mrefu uliopita wakaenda katika “nchi na uvuli wa mauti,” tumaini lenye baraka, linaloleta furaha limetolewa tena katika ahadi ya kutokea Kwake, Yeye aliye “ufufuo na uzima,” “kuwarudisha nyumbani watu Wake waliofukuzwa.” Fundisho la ujio wa pili wa Kristo ni ufunguo muhimu wa Maandiko Matakatifu. Tangu siku ile ambayo watu wawili wa kwanza walipogeuza hatua zao za huzuni na kuondoka kutoka katika Bustani ya Edeni, watoto wa imani wameendelea kusubiri ujio wa Yeye Aliyeahidiwa kuvunja nguvu ya mharibifu na kuwarudisha tena katika Paradiso iliyopotea. Watakatifu wa zamani walitazamia ujio wa Masihi katika utukufu, kama kilele cha tumaini lao. Heneko, mtu wa saba katika mfululizo wa ukoo wa wale walioishi katika Bustani ya Edeni, mtu ambaye kwa karne tatu duniani alitembea na Mungu, aliruhusiwa kumwona kutokea mbali Mkombozi anayekuja. “Angalia,” alisema, “Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote” (Yuda 14, 15). Mzee Ayubu katika usiku wa mateso yake alisema kwa msisimko na kwa tumaini lisilo na shaka: “Najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.... Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine” (Ayubu 19:25-27).PKSw 228.1

  Ujio wa Kristo kuleta utawala wa haki uliwahamasisha waandishi wa Maandiko Matakatifu kuandika maneno mazuri sana na yanayosisimua. Waandishi wa mashairi na manabii wa Biblia waliandika habari ya ujio wa Kristo kwa maneno yanayong'ara kwa moto wa mbinguni. Mwandishi wa zaburi aliimba kuhusu nguvu na ukuu wa Mfalme wa Israeli: “Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika. Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza.... Ataziita mbingu zilizo juu, Na nchi pia awahukumu watu wake” (Zaburi 50:2-4). “Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie, Bahari na ivume na vyote viijazavyo, Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo, Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha; Mbele za Bwana, kwa maana anakuja, Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa uaminifu wake” (Zaburi 96:11-13).PKSw 228.2

  Alisema nabii Isaya: “Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa.” “Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo. Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake” (Isaya 26:19; 25:8, 9).PKSw 228.3

  Na Habakuki, akiwa katika njozi takatifu, aliuona ujio Wake. “Mungu alikuja kutoka Temani, Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani. Utukufu wake ukazifunika mbingu, Nayo dunia ikajaa sifa yake. Mwangaza wake ulikuwa kama nuru” “Akasimama, akaitetemesha dunia; Akatazama, akawasitusha mataifa; Na milima ya zamani ikatawanyika; Vilima vya kale vikainama; Miendo yake ilikuwa kama siku za kale” “Ukapanda farasi zako, Katika magari yako ya wokovu” “Milima ilikuona, ikaogopa; Gharika ya maji ikapita; Vilindi vikatoa sauti yake, Vikainua juu mikono yake. Jua na mwezi vikasimama makaoni mwao; Mbele ya nuru ya mishale yako ilipotapakaa, Mbele ya mwangaza wa mkuki wako umeremetao.” “Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako, Kwa ajili ya wokovu wa masihi wako; Ukakiponda kichwa cha nyumba ya waovu, Ukiuweka wazi msingi hata mwambani” (Habakuki 3:3, 4, 6, 8, 10, 11, 13).PKSw 229.1

  Mwokozi alipokuwa karibu kutengana na wanafunzi Wake, aliwafariji katika huzuni zao kwa kuwahakikishia kuwa angerudi tena: “Msifadhaike mioyoni mwenu.... Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi.... Mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo” (Yohana 14:1-3). “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye,” “ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake: na mataifa yote watakusanyika mbele zake” (Mathayo 25:31, 32).PKSw 229.2

  Malaika waliobaki kwenye Mlima wa Mizetuini baada ya Kristo kupaa mbinguni walirudia ahadi ya kurudi kwa Kristo kwa wanafunzi: “Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni” (Matendo 1:11). Na mtume Paulo, akizungumza kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, alishuhudia: “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu” (1 Wathesalonike 4:16). Anasema nabii wa Patmo: “Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma” (Ufunuo 1:7).PKSw 229.3

  Ujio wake umezungukwa na habari za ule utukufu wa“kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu” (Matendo 3:21). Ndipo utawala ambao umedumu kwa muda mrefu wa uovu utavunjwa; “Falme za dunia” zimekwisha kuwa “falme za Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele” (Ufunuo 11:15). “Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, Na wote wenye mwili watauona pamoja” “Ndivyo Bwana MUNGU atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote” Atakuwa “taji ya fahari, na kilemba cha uzuri, kwa mabaki ya watu wake” (Isaya 40:5; 61:11; Isaya 28:5).PKSw 229.4

  Wakati huo ndipo ufalme wa amani wa Masihi uliotamaniwa kwa muda mrefu utakaposimikwa chini ya mbingu yote. “Maana Bwana ameufariji Sayuni; amepafariji mahali pake palipokuwa ukiwa; amefanya jangwa lake kuwa kama bustani ya Edeni, na nyika yake kama bustani ya Bwana.” “Litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni” “Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa furaha yangu; na nchi yako Beula.” “Kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe” (Isaya 51:3; 35:2; 62:4, 5).PKSw 230.1

  Ujio wa Bwana umekuwa katika zama zote tumaini la wafuasi Wake wa kweli. Ahadi ya Mwokozi wakati akiwaaga kwenye Mlima wa Mizeituni, kuwa atakuja tena, ilitoa mwangaza kwa mustakabali wa wanafunzi Wake, ukijaza mioyo yao furaha na tumani ambalo huzuni isingeweza kulizima wala majaribu yasingeweza kulihafifisha. Katikati ya mateso na majaribu, “kutokea kwa Mungu wetu mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo” lilikuwa “tumaini lenye baraka” Wakristo wa Thesalonike walipojawa na huzuni kwa kuwazika wapendwa wao, waliokuwa wametumaini kuishi na kushuhudia ujio wa Bwana, Paulo mwalimu wao, aliwaeleza juu ya ufufuo, utakaotokea wakati wa ujio wa pili wa Mwokozi. Ndipo waliokufa katika Kristo watafufuka kwanza, na pamoja na walio hai tutanyakuliwa kumlaki Bwana hewani. “Na hivyo,” alisema, “tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo” (1 Wathesalonike 4:16-18).PKSw 230.2

  Kwenye kisiwa cha miamba cha Patmo mwanafunzi mpendwa alisikia ahadi, “Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi,” na sauti yake yenye shauku inatoa ombi la kanisa katika safari yake yote, “Amina; na uje, Bwana Yesu” (Ufunuo 22:20).PKSw 230.3

  Kutoka katika gereza, nguzo ya kuchomea watu moto, jukwaa la kukatia vichwa vya watu, ambapo watakatifu na wafia dini walishuhudia kwa ajili ya ukweli, inakuja baada ya karne nyingi sauti ya imani na tumaini. Ikiwa “imehakikishiwa juu ya ufufuo Wake binafsi, na hatimaye ufufuo wa kwao wakati wa ujio Wake, kwa ajili ya kazi hiyo,” alisema mmoja wa Wakristo hao, “walidhihaki mauti, na walionekana kuwa juu ya mauti.”—Daniel T. Taylor, The Reign of Christ on Earth: or, The Voice of the Church in All Ages, ukurasa wa 33. Walikuwa tayari kushuka makaburini mwao, ili “wafufuke wakiwa huru.”—Ibid., ukurasa wa 54. Walitarajia kumwona “Bwana akishuka kutoka mbinguni katika mawingu akiwa na utukufu wa Baba Yake,” “kuwaletea wenye haki nyakati za ufalme” Wawaldensia walikuwa na imani hiyo hiyo.— Ibid., ukurasa wa 129-132. Wycliffe alitazamia kutokea kwa Mkombozi kama tumaini lenye baraka la kanisa.—Ibid., ukurasa wa 132-134.PKSw 230.4

  Luther alisema: “Ninashawika kwa hakika kuwa, siku ya hukumu haiwezi kukosa kuwepo ndani ya miaka mia tatu kamili. Mungu hataweza, hawezi, kuruhusu huu ulimwengu mwovu uendelee kwa muda mrefu zaidi.” “Siku kuu inakaribia ambapo ufalme wa machukizo utapinduliwa.”—Ibid., ukurasa wa 158, 134.PKSw 231.1

  “Ulimwengu huu uliozeeka hauko mbali na mwisho wake,“Melanchthon alisema. Calvin aliwahimiza Wakristo “wasisite-site, wakitarajia kwa shauku kubwa siku ya ujio wa Kristo kama tukio kubwa kuliko matukio mengine yote;” na alitangaza kuwa “familia yote ya waaminifu itadumu kuitazamia siku hiyo.” “Inatupasa kuwa na njaa kwa ajili ya Kristo, inatupasa kutafuta, kutafakari,” alisema, “mpaka kupambazuka kwa siku ile kuu, ambapo Bwana wetu ataonesha kikamilifu utukufu wa ufalme Wake.”—Ibid., ukurasa wa 158, 134.PKSw 231.2

  “Je, sio kuwa Bwana wetu Yesu amepeleka miili yetu mbinguni?” alisema Knox, Mwanamatengenezo wa Scotch, “na si atarudi? Tunajua kuwa atarudi, na tena haraka.” Ridley na Latimer, waliosalimisha maisha yao kwa ajili ya ukweli, walitazamia kwa imani kwa ajili ya ujio wa Bwana. Ridley aliandika: “Ulimwengu usio na mashaka—ninaamini jambo hili, na kwa hiyo ninalisema—unakaribia. Hebu sisi wote pamoja na Yohana, mtumishi wa Mungu, tumlilie katika mioyo yetu Mwokozi wetu Kristo, Njoo, Bwana Yesu, njoo.”—Ibid., ukurasa wa 151, 145.PKSw 231.3

  “Mawazo ya ujio wa Bwana,” alisema Baxter, “ni matamu na yananipa furaha kubwa sana.”—Richard Baxter, Works, vol. 17, uk. 555. “Ni kazi ya imani na tabia ya watakatifu Wake kupenda kutokea Kwake na kulitazamia tumaini lile lenye baraka.” “Ikiwa mauti ni adui atakayeangamizwa wakati wa ufufuo, tunaweza kujifunza jinsi waumini wanavyopaswa kutamani na kuomba kwa ajili ya ujio wa pili wa Kristo, wakati ushindi huu mkamilifu utakapopatikana.”—Ibid., vol. 17, uk. 500. “Hii ni siku ambayo waumini wote wanapaswa kuitamani, kuingoja, kama ukamifu wa kazi yote ya ukombozi wao, na shauku na juhudi zote za roho zao.” “Harakisha, Ee Bwana, siku hii yenye baraka!”—Ibid., vol. 17, uk. 182, 183. Hili ndilo lililokuwa tumaini la kanisa la mitume, la “kanisa nyikani,” na la Wanamatengenezo.PKSw 231.4

  Unabii hauelezi tu namna na kusudi la ujio wa Kristo, bali hueleza pia ishara ambazo kwazo watu watajua kukaribia kwa ujio Wake. Yesu alisema: “Kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota” (Luka 21:25). “Jua litatiwa giza, na mwezi hatautoa mwanga wake. na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu” (Marko 13:24-26). Mwandishi wa kitabu cha Ufunuo anaeleza ishara za kwanza zinazotangulia Ujio Wake wa Pili: “Palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu” (Ufunuo 6:12).PKSw 231.5

  Ishara hizi zilishuhudiwa kabla ya kuanza kwa karne ya kumi na tisa. Katika utimizo wa unabii huu kulitokea, mwaka 1755, tetemeko la kutisha kuliko yote yaliyowahi kutokea na kuwekwa katika kumbukumbu ya maandishi. Ingawa linajulikana sana kama tetemeko la Lisbon, lilienea na kufika eneo kubwa la Ulaya, Afrika, na Amerika. Lilifika hadi Greenland, katika maeneo ya India ya Magharibi, katika kisiwa cha Madeira, katika nchi za Norwe na Uswidi, Uingereza Kuu na Ireland. Lilighubika kiasi cha eneo lisilopungua maili za mraba milioni nne. Katika bara la Afrika mtikisiko ulikuwa mkubwa sana kama ulivyokuwa katika bara la Ulaya. Sehemu kubwa ya Algiers iliharibiwa; na umbali mfupi kutoka Morocco, kijiji chenye wakazi kati ya elfu nane na elfu kumi kilimezwa chote. Wimbi kubwa lilifagia pwani ya Uhispania na Afrika na kumeza miji na kusababisha uharibifu mkubwa.PKSw 232.1

  Ilikuwa katika nchi za Uhispania na Ureno ambapo mtikisiko ulisababisha uharibifu mkubwa kuliko maeneo mengine yote. Katika maeneo ya Cadiz wimbi lililopitia hapo lilikuwa limeinuka kwa takribani futi sitini kwenda juu. Milima, “mirefu sana katika nchi ya Ureno, ilitikiswa sana, kama ilivyopaswa kuwa, kuanzia kwenye misingi hasa, na baadhi yake ilifunguka kwenye vilele vyake, iliyopasuka na kuachana kwa namna ya ajabu sana, mabonge makubwa ya vipande vyake yakitupwa chini katika mabonde yaliyo karibu. Ndimi za moto zilitoka katika mipasuko hiyo.”— Sir Charles Lyell, Principles of Geology, ukurasa 495.PKSw 232.2

  Katika jiji la Lisbon “sauti ya radi ilisikika chini ya ardhi, na muda mfupi baadaye mtikisiko mkubwa sana uliangusha chini sehemu kubwa ya jiji lile. Katika kipindi cha takribani dakika sita watu sitini elfu waliangamia. Bahari ilirudi nyuma kwanza, na kuicha sakafu ya bahari ikiwa kavu; halafu bahari ilirudi, maji yake yakiwa yameinuka kwa kiasi cha futi hamsini au zaidi juu ya usawa wake wa kawaida.” “Miongoni mwa matukio mengine ambayo hayakuwa ya kawaida yaliyosimuliwa kuwa yalitokea katika jiji la Lisbon wakati wa janga hilo, ilikuwa kuzama kwa gati mpya, iliyojengwa kwa marumaru tupu, kwa gharama kubwa. Kundi kubwa la watu lilikuwa limejikusanya pale kwa ajili ya usalama, kama sehemu ambayo wangeweza kuwa mbali na majengo yaliyokuwa yakianguka chini; lakini muda mfupi gati lilianza kuzama chini na watu wate waliokuwa juu yake, na hakuna mwili hata mmoja wa waliokufa ulioelea juu ya uso wa bahari.”—Ibid., ukurasa wa 495.PKSw 232.3

  “Mtikisiko” uliosababishwa na tetemeko “ulifuatiwa ghafla na anguko la kila kanisa na kila nyumba ya watawa, karibu majengo makubwa yote ya serikali, na zaidi ya robo ya nyumba zote za makazi ya watu. Kama saa mbili baada ya mtikisiko, moto ulilipuka katika maeneo mbali mbali, na moto uliwaka kwa ukali mwingi kwa muda wa karibu siku tatu mfululizo, kiasi kwamba jiji lote liliteketezwa kabisa. Tetemeko lilitokea siku takatifu, wakati makanisa na nyumba za watawa zilipokuwa zimejaa watu, ni watu wachache sana waliookoka.”—Encyclopedia Americana, art. “Lisbon,” note (ed. 1831). “Hofu ya watu isingeweza kuelezeka. Hakuna mtu aliyelia na kutoa machozi; tukio lile lilitisha mno kiasi kwamba hakuna aliyeweza kutoa machozi. Watu walikimbia huko na huko, wakiwa wamechanganyikiwa kwa ajili ya hofu, wakipiga-piga nyuso zao na vifua vyao, wakipiga kelele, ‘Tuhurumie! Ulimwengu umekwisha!’ Akina mama waliwasahau watoto wao, na kukikimbia huku na huko wakiwa wamevaa sanamu za Yesu akiwa amewambwa msalabani. Kwa bahati mbaya, wengi walikimbilia makanisani ili kupata ulinzi; lakini hawakupata msaada wowote na ibada za sakramenti ziliumbuka; viumbe hawa maskini walijaribu kukamata mimbari; sanamu, mapadri, na watu wote walizikwa pamoja katika maangamizi ya pamoja.” Imekadiriwa kuwa watu wapatao tisini elfu walipoteza maisha yao siku ile ya maangamizi.PKSw 233.1

  Miaka ishirini na tano baadaye ilitokea ishara ya pili iliyotajwa katika unabii—kutiwa giza kwa jua na mwenzi. Kilichoshangaza kuhusu ishara hii ilikuwa ukweli kuwa wakati wa kutimizwa kwake ulibainishwa waziwazi. Katika maongezi ya Mwokozi na wanafunzi Wake juu ya mlima wa Mizeituni, baada ya kuelezea kipindi kirefu cha kujaribiwa kwa kanisa,—miaka 1260 ya mateso ya upapa, ambacho aliahidi kuwa mateso yatafupishwa,— alitaja matukio kadhaa ambayo yatatangulia ujio Wake, na aliweka wakati maalumu ambapo moja ya ishara hizi ingeshuhudiwa: “Lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake” (Marko 13:24). Siku 1260, au miaka 1260, iliishia mwaka 1798. Robo ya karne kabla, mateso yalikuwa yamekwisha kwa kiwango kikubwa. Baada ya mateso haya, kwa mujibu wa maneno ya Kristo, jua lilipaswa kutiwa giza. Siku ya tarehe 19 Mei 1780, unabii huu ulitimizwa.PKSw 233.2

  “Karibu, kama siyo tukio la pekee kabisa, laweza kuwa tukio ambalo ni siri kubwa kuliko yote na ambalo halina maelezo,...ni siku hii ya giza ya Mei 19, 1780,—la kutiwa giza la ajabu na lisiloelezeka la mbingu na angahewa katika Uingereza Mpya.” R. M. Devens, Our First Century, ukurasa wa 89.PKSw 233.3

  Shuhuda wa tukio hili aliyeishi katika mji wa Massachusetts anaelezea tukio kama ifuatavyo: “Asubuhi jua lilichomoza likiwa safi, lakini ghafla lilifunikwa. Mawingu yaliteremka chini na kuwa karibu na ardhi, na kutoka katika mawingu hayo, ambayo yalikuwa meusi na ya kutisha, kama yalivyokuja kuonekana muda mfupi uliofuata, radi ilimulika, ngurumo za radi zikarindima, na mvua ya rasha-rasha ilinyesha. Kuelekea saa tatu asubuhi, mawingu yalipungua, na rangi yake iligeuka na kuwa ya shaba katika mwonekano wake, na ardhi, miamba, miti, majengo, maji, na watu walibadilishwa na mwanga huu wa ajabu, usiokuwa wa dunia hii. Dakika chache baadaye, wingu jeusi lilitanda kote angani isipokuwa tu ukingo mwembamba katika upeo wa macho, na kulikuwa na giza ambalo kwa kawaida hutokea saa tatu usiku muda wa jioni wa wakati wa joto....PKSw 233.4

  “Hofu, wasiwasi, na kicho, pole pole vilianza kujaza akili za watu. Wanawake walisimama milangoni, wakiangalia nje gizani; wanaume walirudi nyumbani kutoka mashambani; seremala aliacha zana zake, mhunzi aliacha karakana yake yenye kalibu, mfanya biashara aliacha kaunta yake. Shule zilifungwa, na wanafunzi walikimbia wakitetemeka kuelekea nyumbani. Wasafiri walikatisha safari zao na kutafuta hifadhi katika nyumba zilizokuwa karibu yao. ‘Ni nini kinakuja?’ kila mdomo na kila moyo uliuliza. Ilionekana kana kwamba kimbunga kilikuwa karibu kupita katika nchi, au kana kwamba ilikuwa siku ya kilele cha mambo yote.PKSw 234.1

  “Mishumaa ilitumika; na mioto ya nyumbani ilitoa mwanga mkali kama unavyooenekana katika usiku usiokuwa na mbalamwezi wakati wa majira ya kupukutika kwa majani.... Kuku walirudi katika vibanda vyao na kusinzia, ng'ombe walirudi katika mazizi yao na kulala, vyura walitoa macho, ndege waliimba nyimbo zao za jioni, na popo waliruka-ruka huku na huko. Lakini mwanadamu alijua kuwa usiku ulikuwa bado haujawadia....PKSw 234.2

  “Dkt. Nathanael Whittaker, mchungaji wa kanisa la Tabernacle katika mji wa Salem, aliendesha huduma za kidini katika nyumba ya mikutano, na alitoa hubiri ambapo alidai kuwa giza lile halikuwa la kawaida. Waumini walikusanyika makanisani katika sehemu zingine mbalimbali pia. Mafungu ya Biblia kwa ajili ya mahubiri ambayo hayakuandaliwa kwa namna tofauti tofauti yalikuwa yale yaliyoelekea kuonesha kuwa giza lile lilipatana na unabii wa Maandiko.... Giza liliongezeka katika uzito mara tu baada ya saa tano asubuhi.”—The Essex Antiquarian, April, 1899, vol. 3, No. 4, uk. 53, 54. “Katika maeneo mengi ya nchi giza lilikuwa nene kiasi kwamba watu wasingeweza kujua wakati kwa kutazama saa ya mkononi au ya ukutani, wala wasingeweza kula chakula, wala kufanya shughuli zao za nyumbani, bila mwanga wa mishumaa PKSw 234.3

  “Kiasi cha giza hili kilikuwa siyo cha kawaida. Giza hili lilionekana hadi mashariki sehemu za Falmouth. Upande wa magharibi lilifika sehemu ya mbali ya Connecticut, hadi Albany. Upande wa kusini, lilionekana katika fukwe za bahari; na kuelekea upande wa kaskazini giza lilifunika eneo lote la makazi ya watu wa Amerika.”—William Gordon, History of the Rise, Progress, and Establishment of the Independence of the U.S.A., vol. 3, uk. 57.PKSw 234.4

  Giza nene la mchana lilifuatiwa, saa moja au mbili kabla ya jioni, na anga lisilokuwa na mawingu, na jua lilitokea na kuonekana, ingawa lilikuwa bado limefunikwa na ukungu mzito na mweusi. “Baada ya jua kuzama, mawingu yalirudi tena juu, na giza likaingia kwa muda mfupi sana.” “Wala siyo kweli kuwa giza la usiku lilikuwa la kawaida bali lilikuwa nene na lilitisha zaidi kuliko hata lile la mchana; pamoja na hayo kulikuwa na mbalamwezi iliyokuwa karibu kukomaa, na hakuna kitu chochote kilichoweza kutambuliwa bila msaada wa mwanga wa mshumaa au chanzo kingine kilichotengenezwa na mwanadamu, ambao, ulipoonekana kutokea kwa nyumba za jirani na kwingineko kote ambako ni mbali, ulionekana kupitia katika giza la Kimisri ambalo lilionekana kama lisiloweza kupenywa na miale ya nuru.”—Isaiah Thomas, Massachusetts Spy; or, American Oracle of Liberty, vol. 10, No. 472 (Mei 25, 1780). Mtu aliyeshuhudia tukio alisema: “Nilishindwa kujizuia kuelewa wakati huo, kuwa ikiwa kila kitu chenye uwezo wa kutoa mwanga katika ulimwengu kilikuwa kimefunikwa na kivuli kisichoweza kupenywa, au kisichoweza kuondosheka, giza lisingeweza kuwa kamilifu zaidi ya pale.”—Letter by Dr. Samuel Tenney, of Exeter, New Hampshire, December, 1785 (in Massachusetts Historical Society Collections, 1792, 1st series, vol. 1, uk. 97). Ingawa ilipofika saa tatu ya usiku ule mwezi ulionekana vizuri kabisa, “haukuweza kuondoa hata kidogo vivuli vya hofu ya kifo.” Baada ya saa sita usiku giza lilitoweka, na mwezi, ulipoonekana kwa mara ya kwanza, ulikuwa na mwonekano wa damu.PKSw 235.1

  Mei 19, 1780, inasimama katika historia kama “Siku ya Giza.” Tangu wakati wa Musa hakuna kipindi kilichokuwa na giza lenye uzito, kiwango, na muda kama huo, lililowahi kuandikwa katika kumbukumbu. Maelezo ya tukio hili, kama yalivyotolewa na shuhuda aliyeona tukio, lilikuwa mwangwi wa maneno ya Bwana, yaliyoandikwa na nabii Yoeli, miaka elfu mbili na mia tano iliyopita kabla ya kutimizwa kwake: “Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya Bwana iliyo kuu na itishayo” (Yoeli 2:31).PKSw 235.2

  Kristo aliwaeleza watu Wake waangalie ishara za ujio Wake na kufurahi kwa kuona viashiria vya ujio wa Mfalme wao. “Basi mambo hayo yaanzapo kutokea,” alisema, “changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.” Aliwaonesha wafuasi Wake miti iliyokuwa ikichipuka, na kusema: “Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu” (Luka 21:28, 30, 31).PKSw 235.3

  Lakini kwa kuwa roho ya unyenyekevu na uaminifu ilikuwa imetoweka kanisani na badala yake kanisa likaingiwa na kiburi na ibada ya kimtindo, upendo kwa Kristo na imani Kwake ulikuwa umepoa. Kwa sababu ya kuipenda dunia na anasa, watu waliodai kuwa wa Mungu walipofushwa hata wakashindwa kukumbuka mafundisho ya Yesu kuhusu ishara za ujio Wake. Fundisho la ujio wa pili lilipuuzwa; mafundisho yanayolihusu yalifichwa na tafsiri potovu, hadi, kwa sehemu kubwa, likapuuzwa na kusahauliwa. Hususani ilikuwa hivyo katika makanisa ya Amerika. Uhuru na raha ambayo matabaka yote ya jamii waliipata, tamaa kubwa ya mali na anasa, iliyozaa matumizi ya muda mwingi katika kutafuta pesa, kukimbilia kutafuta umaarufu na madaraka, mambo ambayo yalionekana kuwa na uwezekano wa kupatikana kwa watu wote, viliwafanya watu kuelekeza nguvu zao na matumaini yao kwa vitu vya ulimwengu huu, na kusukumia mbali katika wakati ujao ile siku kuu ambayo utaratibu wa sasa wa mambo utatoweka.PKSw 236.1

  Mwokozi alipowaeleza wafuasi Wake kuhusu ishara za kurudi Kwake, alitabiri hali ya kurudi nyuma itakayokuwepo muda mfupi kabla ya ujio Wake wa pili. Kungewepo, kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu, shughuli na pilika pilika za mambo ya kidunia na utafutaji wa anasa—kununua, kuuza, kupanda, kujenga, kuoa, na kuolewa—pamoja na kumsahau Mungu na maisha yajayo. Kwa watu wanaoishi wakati huu, maelekezo ya Kristo ni: “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo” “Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu” (Luka 21:34, 36).PKSw 236.2

  Hali ya kanisa wakati huu imeelezwa katika maneno ya Mwokozi katika kitabu cha Ufunuo: “Una jina la kuwa hai, nawe umekufa. Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia” Na wanaokataa kuamka kutoka usingizi wa usalama wa kujidanganya, onyo kali linatolewa: “Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako” (Ufunuo 3:1, 3).PKSw 236.3

  Ilikuwa muhimu watu waamshwe na kujulishwa hatari iliyowakabili; kuwa walipaswa wamshwe ili wajiandae kukabiliana na matukio makubwa yanayoshikamana na kufungwa kwa mlango wa rehema. Nabii wa Mungu anatangaza: “Kwa kuwa siku ya Bwana ni kuu, yenye kitisho sana; naye ni nani awezaye kuistahimili?” Ni nani awezaye kusimama wakati Yeye aliye “na macho safi hata usiweze kuangalia uovu,” na hawezi “kutazama ukaidi”? (Yoeli 2:11; Habakuki 1:13). Kwa watu wanaolia wakisema, “Mungu wangu, sisi Israeli tunakujua,” lakini “wamelihalifu agano langu, wameiasi sheria yangu,” na wameharakisha kumfuata mungu mwingine, huku wakiwa wameficha uovu katika mioyo yao, na wakipenda njia za uasi—kwa watu hawa siku ya Bwana ni “giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga” (Hosea 8:2, 1; Zaburi 16:4; Amosi 5:20). “Kisha itakuwa wakati ule,” asema Bwana, “nitauchunguza Yerusalemu kwa taa, nami nitawaadhibu watu walioganda juu ya sira zao: wasemao katika mioyo yao, Bwana hatatenda mema, wala hatatenda mabaya” (Sefania 1:12). “Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali” (Isaya 13:11). “Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa;” “utajiri wao utakuwa mateka, na nyumba zao zitakuwa ukiwa” (Sefania 1:18, 13).PKSw 236.4

  Nabii Yeremia, akiangalia mbele hadi wakati huu wa kutisha, alisema: “Naumwa katika moyo wangu wa ndani; .... siwezi kunyamaza; kwa sababu umesikia, Ee nafsi yangu, sauti ya tarumbeta, mshindo wa vita” (Yeremia 4:19, 20).PKSw 237.1

  “Siku ile ni siku ya ghadhabu, Siku ya fadhaa na dhiki, Siku ya uharibifu na ukiwa, Siku ya giza na utusitusi, Siku ya mawingu na giza kuu, Siku ya tarumbeta na ya kamsa” (Sefania 1:15, 16). “Tazama, siku ya Bwana inakuja,.... ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake” (Isaya 13:9).PKSw 237.2

  Katika muktadha wa siku ile kuu, neno la Mungu, katika lugha makini na yenye mguso, anawaita watu Wake waamke kutoka katika usingizi wao wa kiroho na kutafuta uso Wake katika hali ya toba na unyenyekevu: “Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Pigeni na kelele katika mlima wangu mtakatifu; Wenyeji wote wa nchi na watetemeke; Kwa maana siku ya Bwana inakuja. Kwa sababu inakaribia.” “Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto,...; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu.” “Nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya” (Yoeli 2:1, 15-17, 12, 13).PKSw 237.3

  Kuwaandaa watu kusimama katika siku ya Mungu, kazi kubwa ya matengenezo inapaswa kufanyika. Mungu aliona kuwa wengi wa watu wanaodai kuwa ni watu Wake walikuwa hawajengi kwa ajili ya umilele, na katika rehema Yake alikuwa karibu kutuma ujumbe wa onyo wa kuwaamsha watoke katika hali yao kuzubaa na kuwaongoza katika maandalizi ya ujio wa Bwana.PKSw 237.4

  Onyo hili limetolewa katika Ufunuo 14. Hapa kuna ujumbe wenye sehemu tatu unaowakilishwa na kutangazwa na malaika wa mbinguni na kufuatiwa kwa haraka na ujio wa Mwana wa Adamu kukusanya “mavuno ya nchi.” Onyo la kwanza, miongoni mwa maonyo haya, linatangaza hukumu inayokaribia. Nabii alimwona malaika akiruka “katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa, akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji” (Ufunuo 14:6, 7). Ujumbe huu unaelezwa kuwa sehemu ya “injii ya milele.”PKSw 238.1

  Kazi ya kuihubiri injili haijawekwa katika mikono ya malaika, bali imewekwa kama dhamana katika mikono ya wanadamu. Malaika watakatifu wanatumika katika kuelekeza kazi hii, wanasimama harakati zote kubwa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu; lakini utangazaji halisi wa injili hufanywa na watumishi wa Kristo duniani.PKSw 238.2

  Watu waaminifu, ambao walitii misukumo ya Roho wa Mungu na mafundisho ya neno Lake, walipaswa kutangaza onyo hili kwa ulimwengu. Watu hawa ni wale waliosikia“neno la unabii lililo imara zaidi,“ambalo ni“taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu” (2 Petro 1:19). Walikuwa wakitafuta kumjua Mungu zaidi kuliko hazina zote zilizositirika, wakiamini kuwa kumjua Mungu ni “bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi” (Mithali 3:14). Na Bwana aliwafunulia mambo makuu ya ufalme. “Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake” (Zaburi 25:14).PKSw 238.3

  Siyo wanateolojia wasomi ambao walikuwa na ufahamu wa huu ukweli, na ambao walijihusisha katika utangazaji wake. Ikiwa watu hawa wangekuwa walinzi waaminifu na wenye kukesha, wakiyachunguza Maandiko kwa bidii kubwa na maombi mengi, wangeweza kuujua wakati wa usiku; unabii ungeweza kuwafunulia matukio yanayokuja karibuni. Lakini hawakufanya hivyo, na ujumbe ulitolewa na watu walio wa kawaida kabisa. Yesu alisema: “Enendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako” (Yohana 12:35). Watu wanaoiacha nuru ambayo Mungu amewapa, au wanaopuuza kuitafuta wakati inapatikana kwa ajili yao, wataachwa gizani. Lakini Mwokozi alisema: “Yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima” (Yohana 8:12). Yeyote aliye na kusudi moja tu la kutafuta kutenda mapenzi ya Mungu, akiifuata kwa bidii nuru aliyonayo tayari, atapokea nuru kubwa zaidi; kwa mtu kama huyo nyota ya nuru ya mbinguni itatumwa kumwongoza katika ukweli wote.PKSw 238.4

  Wakati wa ujio wa kwanza wa Kristo makuhani na waandishi wa Mji Mtakatifu, ambao walikuwa wamepewa dhamana ya maagizo ya Mungu, walipaswa kuzijua dalili za nyakati na kutangaza ujio wa Yule aliyekuwa ameahidiwa. Unabii wa Mika ulitangaza mahali ambapo angezaliwa; Danieli alisema wakati mahsusi wa ujio Wake (Mika 5:2; Danieli 9:25). Mungu alikabidhi unabii huu kwa viongozi wa Kiyahudi; hawakuwa na udhuru wa kutojua na kutangaza kwa watu kuwa ujio wa Masihi ulikuwa karibu. Kutokujua kwao kulikuwa matokeo ya dhambi ya kupuuzia. Wayahudi walikuwa wakijenga minara ya kumbukumbu kwa ajili ya manabii wa Mungu waliouawa, ilhali kwa kutoa heshima yao kwa watu mashuhuri walikuwa wakitoa heshima kwa watumishi wa Shetani. Wakiwa wamezama katika mapambano na tamaa zao kwa ajili ya vyeo na mamlaka miongoni mwa watu, walishindwa kutambua fadhila waliyopewa na Mungu, Mfalme wa mbinguni.PKSw 239.1

  Kwa shauku na kicho kikubwa wazee wa Israeli walipaswa kujifunza na kuelewa mahali, wakati, na muktadha, wa tukio kubwa kuliko matukio yote katika historia ya ulimwengu—ujio wa Mwana wa Mungu kutekeleza ukombozi wa mwanadamu. Watu wote walipaswa kukesha na kungojea ili wawe miongoni mwa watu wa kwanza kumpokea Mkombozi wa ulimwengu. Lakini, kumbe, katika mji wa Bethlehemu wasafiri wawili waliochoka kutoka katika milima ya Nazarethi walitembea urefu wote wa mtaa mwembamba hadi mwisho wa mji upande wa mashariki, wakitafuta bila mafanikio mahali pa kupumzika na kujihifadhi wakati wa usiku. Hakuna milango iliyokuwa tayari kuwapokea. Hatimaye walipata hifadhi katika banda bovu la ng'ombe, na Mwokozi wa ulimwengu alizaliwa humo.PKSw 239.2

  Malaika wa mbinguni walikuwa wameuona utukufu ambao Mwana wa Mungu alishiriki na Baba Yake kabla ulimwengu haujakuwepo, na walitarajia kwa shauku kubwa kuwa kuonekana Kwake duniani kungekuwa tukio ambalo lingeleta furaha kubwa kwa watu wote. Malaika walichaguliwa kupeleka habari ya furaha kwa wale waliokuwa tayari kuipokea na ambao kwa furaha wangeitangaza kwa wakazi wa dunia. Kristo alikuwa amejishusha ili kuchukua asili ya mwanadamu; alipaswa kubeba uzito usio na kikomo wa taabu kwa kutoa nafsi Yake kuwa sadaka kwa ajili ya dhambi; lakini malaika walitamani kuwa hata katika unyenyekevu Wake, Mwana wa Yeye Aliye Juu Sana atokee mbele ya wanadamu akiwa na angalau heshima na utukufu unaolingana na hadhi Yake. Je, wakuu wa dunia wangeweza kukusanyika katika makao makuu ya Israeli kusubiri ujio Wake? Je, majeshi ya malaika wangemtambulisha kwa mkutano mkubwa wa watu walio na shauku ya kumwona?PKSw 239.3

  Malaika alitembelea dunia kuona watu ambao walikuwa wamejiandaa kumpokea Yesu. Lakini hakuona viashiria vya maandalizi ya kumpokea. Hakusikia sauti ya sifa na shangwe kwa sababu ya kukaribia kwa ujio wa Masihi. Malaika anasimama kwa muda juu ya mji mteule na hekalu ambapo uwepo mtakatifu wa Mungu ulikuwa ukidhihirika kwa zama nyingi; lakini hata hapa kuna kutojali kule kule. Makuhani, katika majivuno na kiburi, walikuwa wakitoa kafara zilizo najisi hekaluni. Mafarisayo walikuwa wakiwahutubia watu kwa sauti kubwa au wakiomba sala za kujisifu katika kona za mitaa. Katika ikulu za wafalme, katika mikutano ya wanafalsafa, katika shule za marabi, wote hawakuwa na wazo lo lote kuhusu ukweli wa ajabu ambao ulikuwa umejaza mbingu kwa furaha na sifa—kuwa Mkombozi wa wanadamu alikuwa karibu kutokea duniani.PKSw 240.1

  Hakukuwa na ushahidi wowote kuwa Kristo alitarajiwa, na hakukuwa na matayarisho kwa ajili ya Mkuu wa uzima. Kwa mshangao, mjumbe wa mbinguni alikuwa karibu kurudi mbinguni akiwa na taarifa ya kuaibisha, wakati anapogundua kundi la wachungaji ambao walikuwa wakichunga makundi yao ya kondoo usiku, na, wakiangalia katika mbingu yenye nyota, wakitafakari unabii wa Masihi aliyetarajia kuja duniani, na wakitamani ujio wa Mkombozi wa ulimwengu. Pale palikuwa na kundi la watu ambao walikuwa wakijiandaa kupokea ujumbe wa mbinguni. Na kwa ghafla malaika wa Bwana aliwatokea, akitangaza habari njema yenye furaha kubwa. Utukufu wa mbinguni ulifurika pande zote za uwanda, kundi la malaika wasio na idadi lilifunuliwa, na kana kwamba furaha ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba isingeweza kufaa kuletwa na mjumbe mmoja kutoka mbinguni, sauti nyingi zinapasuka na kuwa wimbo ambao mataifa yote ya waliookolewa watauimba: “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” (Luka 2:14).PKSw 240.2

  Ndiyo, kisa hiki cha Bethlehemu ni somo muhimu kiasi gani! Ni kwa uzito kiasi gani hukemea kukosa imani kwetu, kiburi chetu na kujitosheleza kwetu. Kisa hiki kinatuonya kwa umakini mkubwa kiasi gani ili tukeshe, isije ikawa, kwa kutojali kwetu ambako ni haramu tushindwe kutambua dalili za nyakati, na hivyo tushindwe kujua siku ya kujiliwa kwetu.PKSw 240.3

  Ilikuwa siyo tu juu ya milima ya Yuda, siyo tu miongoni mwa wachungaji maskini peke yao, ambapo malaika waliwakuta wakeshaji kwa ajili ya ujio wa Masihi. Katika nchi za kipagani pia walikuwepo watu waliosubiri ujio Wake; walikuwa watu wenye hekima, matajiri, na waungwana, wanafalsafa wa Mashariki. Wanafunzi wa vitu vya asili, Mamajusi walimwona Mungu katika kazi za mikono Yake. Kutoka katika Maandiko ya Kiebrania walikuwa wamejifunza juu ya Nyota ambayo ingeinuka kutoka katika ukoo wa Yakobo, na wakiwa na shauku kubwa walisubiri ujio Wake, ambaye angekuwa siyo tu “Faraja ya Israeli,” lakini pia “Nuru ya kuwaangazia Mataifa,” na “kwa ajili ya wokovu wa miisho ya dunia” (Luka 2:25, 32; Matendo 13:47). Walikuwa watu waliotafuta nuru, na nuru kutoka katika kiti cha enzi cha Mungu iliangazia njia kwa ajili ya nyayo zao. Wakati makuhani na marabi wa Yerusalemu, watunzaji na wafafanuzi wa ukweli waliochaguliwa na Mungu, walikuwa wamegubikwa katika giza, nyota iliyotumwa na Mbingu iliwaongoza hawa wageni kutoka katika Mataifa tofauti na taifa la Kiyahudi hadi mahali alipozaliwa Mfalme aliyekuwa amezaliwa punde.PKSw 240.4

  Ni “kwa hao wamtazamiao” ambao Kristo “atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa wokovu” (Waebrania 9:28). Kama vile habari ya kuzaliwa kwa Mwokozi ilivyokuwa, ujumbe wa ujio wa pili haukuwekwa mikononi mwa viongozi wa kidini wa watu. Walishindwa kudumisha uhusiano wao na Mungu, na walikataa nuru kutoka mbinguni; kwa hiyo hawakuwa sehemu ya watu wanaoelezwa na mtume Paulo: “Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza” (1 Wathesalonike 5:4, 5).PKSw 241.1

  Walinzi juu ya kuta za Sayuni walipaswa kuwa watu wa kwanza kudaka habari za kwanza za ujio wa Mwokozi, wa kwanza kuinua sauti zao kutangaza ukaribu Wake, wa kwanza kuwaonya watu wajiandae kwa ajili ya ujio Wake. Lakini walikuwa wamebweteka, wakiota amani na usalama, wakati walikuwa wamelala usingizi katika dhambi zao. Yesu aliliona kanisa Lake, kama mtini usiozaa matunda, ukiwa umefunikwa na majani ya kujifanya, lakini bila matunda ya thamani. Kulikuwepo uzingatiaji wa mifumo ya kidini, wakati roho ya unyenyekevu, toba, na imani ya kweli—ambayo ndiyo pekee ingekuwa ibada inayokubalika kwa Mungu—havikuwepo. Badala ya neema za Roho vilionekana kiburi, taratibu za kujirudia za kidini, kujisifu, ubinafsi, na ukandamizaji. Kanisa lililokuwa likirudi nyuma lilifumba macho yake lisione dalili za nyakati. Mungu hakuwaacha, au kuruhusu watu wake waaminifu washindwe; lakini walimwacha, na walijitenga na upendo Wake. Kwa kukataa kutii masharti, ahadi za Mungu hazikutimizwa.PKSw 241.2

  Haya ndiyo matokeo ya hakika ya kutokuona umuhimu wa kuboresha nuru na fursa ambazo Mungu anazozitoa. Kanisa lisipofuatilia milango ya uongozi Wake, likipokea kila mwale wa nuru, likitekeleza kila wajibu ambao unafunuliwa kwao, dini itadidimia na kurudi katika uzingatiaji wa mambo ya kurudia-rudia, na roho ya uchaji wa kweli itaondoka. Ukweli huu umedhihirishwa kwa kurudia - rudia katika historia ya kanisa. Mungu anataka kutoka kwa watu Wake kazi za imani na utii unaolingana na mibaraka na fursa zilizotolewa. Utii unahitaji kafara na unahusisha msalaba; na hii ndiyo sababu wengi wa wafuasi wa Kristo walikataa kupokea nuru kutoka mbinguni, na, kama ilivyokuwa kwa Wayahudi wa zamani, hawakujua wakati wa kujiliwa kwao (Luka 19:44). Kwa sababu ya kiburi chao na kutokuamini kwao Bwana aliwapita na kufunua ukweli kwa wale ambao, kama wachungaji wa Bethlehemu na Mamajusi wa Mashariki, walitii nuru yote waliyoipokea.PKSw 241.3

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents