Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 27—Uamsho wa Kisasa

    Mahali popote pale ambapo neno la Mungu lilihubiriwa kwa uaminifu, matokeo yalifuata yaliyothibitisha kuwa neno lilitoka kwa Mungu. Roho wa Mungu alifuatana na ujumbe wa watumishi Wake, na neno lilikuwa na nguvu. Wenye dhambi walihisi dhamiri zao zikihuishwa. “Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu” aliangazia katika vyumba vya siri vya mioyo yao, na mambo yaliyofichika ya giza yaliwekwa dhahiri. Walishawishika sana katika akili zao na mioyo yao. Walisadikishwa kuhusu dhambi na haki na hukumu inayokuja. Walipata ufahamu wa haki ya Yehova na walihisi hofu ya kutokea, katika hatia yao na uchafu wao, mbele ya Mchunguzi wa mioyo. Kwa uchungu walilia: “Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” Msalaba wa Kalwari, pamoja na kafara yake isiyo na kikomo kwa ajili ya dhambi za wanadamu, ulipofunuliwa, waliona kuwa hakuna kitu kingine isipokuwa haki ya Kristo pekee ndiyo ingetosha kufanya upatanisho wa dhambi zao; haki ya Kristo pekee ndiyo ingeweza kumpatanisha mwanadamu na Mungu. Kwa imani na uvumilivu walimpokea Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Kwa njia ya damu ya Yesu walipata “ondoleo la dhambi zilizopita.”PKSw 352.1

    Roho hizi zilileta matunda yapasayo toba. Waliamini na kubatizwa, na waliinuka na kutembea katika upya wa uzima—viumbe wapya katika Kristo Yesu; wakiachana na maisha yao ya zamani waliyoishi kwa kufuata tamaa za mwili, bali waishi kwa imani ya Mwana wa Mungu na kufuata nyayo Zake, wakiakisi tabia Yake, na kujitakasa kama Yeye alivyo mtakatifu. Mambo ambayo awali waliyachukia sasa wanayapenda, na mambo ambayo awali waliyapenda sasa wanayachukia. Wenye kiburi na waliojikweza waligeuka na kuwa wapole na wanyenyekevu wa moyo. Watu wa ovyo na wenye majivuno walibadilika na kuwa watu makini na wasiojitanguliza mbele. Watu waliokuwa wakimkufuru Munngu walibadilika wakawa wacha Mungu, walevi wa pombe waliacha pombe, na mafisadi waliacha ufisadi wao. Mitindo ya maisha isiyofaa ya ulimwengu iliwekwa pembeni. Wakristo hawakutafuta“kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali ... utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu” (1 Petro 3:3, 4).PKSw 352.2

    Mikutano ya uamsho ilichochea ari ya kujichunguza mioyo na unyenyekevu. Mikutano hiyo ilihusisha miito mizito na ya dhati kwa mwenye dhambi, kwa kutamani huruma ya upatanisho wa damu ya Kristo. Wanaume na wanawake waliomba na kupigana mieleka na Mungu kwa ajili ya wokovu wa roho. Matunda ya mikutano hiyo ya uamsho ilionekana kwa idadi ya watu ambao hawakusita kujikana nafsi na kujitoa kafara, bali walifurahia kuwa walistahili kupata aibu na majaribu kwa ajili ya Kristo. Watu waliona badiliko katika maisha ya wale walioliamini jina la Yesu. Jamii ilinufaika kwa njia ya mvuto wao. Walikusanya pamoja na Kristo, na kupanda kwa Roho, ili kuvuna uzima wa milele.PKSw 352.3

    Maneno haya yaliweza kusemwa juu yao: “Mlihuzunishwa, hata mkatubu.” “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo” (2 Wakorintho 7:9-11).PKSw 353.1

    Haya ni matokeo ya kazi ya Roho wa Mungu. Hakuna ushahidi wa toba ya kweli ikiwa toba hiyo haileti matengenezo. Hebu aliyetubu atimize ahadi aliyoitoa, arudishe kile alichokiiba, aungame dhambi zake, ampende Mungu na wanadamu wenzake, hapo ndipo mwenye dhambi anaweza kuwa na hakika ya kuwa na amani na Mungu. Wakipimwa kwa matunda yao, walijulikana kuwa wamebarikiwa na Mungu katika wokovu wa wanadamu na kuwainua wanadamu kwa jumla.PKSw 353.2

    Lakini matukio mengi ya uamsho wa siku hizi yameonesha tofauti kubwa na ule udhihirisho wa neema ya Mungu ambao katika siku za awali uliandamana na kazi za watumishi wa Mungu. Ni kweli kuwa shauku ya watu wengi inaamshwa, na wengi wanakiri kuwa wameongoka, na watu wengi wanajiunga na makanisa; hata hivyo matokeo hayathibitishi kwa hakika kabisa kuwa kuna ukuaji wa dhati wa maisha ya kiroho unaowiana na ongezeko la waumini wapya. Nuru inayomulika kwa muda mfupi huzimika, ikiacha giza nene zaidi kuliko lililokuwepo kabla.PKSw 353.3

    Matukio ya uamsho yanayopendwa sana na watu ni yale ambayo huchochea fikra juu ya mambo ya kufikirika lakini yasiyo na uhalisia, ambayo husisimua hisia za watu, na ambayo huchochea tamaa ya kupenda mambo mapya yanayoshtua. Waongofu wanaopatikana kwa njia hizi huwa na hamu ndogo sana ya kusikiliza ukweli wa Biblia, na huwa na shauku kidogo sana ya ushuhuda wa manabii na mitume. Huduma ya kidini isipokuwa na misisimko haina mvuto kwao kabisa. Ujumbe ambao hugusa akili iliyotulia hauamshi mwitikio wo wote kwao. Maonyo ya wazi ya neno la Mungu, yanayohusiana moja kwa moja na maslahi yao ya milele, hayapokelewi.PKSw 353.4

    Kwa kila roho iliyoongoka kikamilifu, uhusiano wake na Mungu na mambo ya milele utakuwa mada kuu ya maisha. Lakini ni wapi, katika makanisa makuu ya leo, kuna roho ya kujiweka wakfu kwa Mungu? Waongofu hawaachi kiburi chao na upendo wao kwa ulimwengu. Hawako tayari kujikana nafsi, wala kubeba msalaba, na kumfuata Yesu aliye mpole na mnyenyekevu, kuliko kabla ya kuongoka kwao. Dini imekuwa kichekesho kwa wasioamini na wenye mashaka kwa sababu wengi wa wale wanaobeba jina la dini hawazijui kanuni zake. Nguvu ya utaua imekaribia kutoweka kabisa katika makanisa yaliyo mengi. Pikiniki, michezo ya kuigiza makanisani, maonesho ya kanisa, nyumba nzuri, maonesho binafsi, vimeondoa mawazo ya watu juu ya Mungu. Ardhi na mali na shughuli za kidunia hujaa akilini mwa watu, na mambo yenye maslahi ya umilele mara chache sana hutupiwa macho.PKSw 353.5

    Pamoja na kushuka kwa imani na utakatifu kulikoenea kila mahali, wapo wafuasi wa kweli wa Kristo katika makanisa haya. Kabla hukumu ya mwisho ya Mungu haijamwagwa juu ya dunia kutakuwepo miongoni mwa watu wa Bwana uamsho wa utauwa wa kweli ambao haujawahi kushuhudiwa tangu nyakati za mitume. Roho na nguvu ya Mungu vitamwagwa juu ya watoto Wake. Wakati ule wengi watajitenga na makanisa ambayo ndani yake kuupenda ulimwengu kumechukua nafasi ya kumpenda Mungu na neno Lake. Wengi, miongoni mwa wachungaji na watu wengine, wataupokea ukweli mkuu ambao Mungu ameagiza utangazwe kwa wakati huu kuwaandaa watu kwa ajili ya ujio wa pili wa Bwana. Adui wa roho anatamani kuzuia kazi hii; na kabla ya wakati wa vuguvugu hilo kufika, atajaribu kuzuia vuguvugu hilo kwa kuleta vuguvugu lake bandia. Katika makanisa yale ambayo ataweza kuyaweka chini ya nguvu yake ya udanganyifu atafanya ionekane kana kwamba mbaraka maalumu wa Mungu umemwagwa; kutakuwepo udhihirisho wa kile kitakachodhaniwa kuwa ni shauku kubwa ya kidini. Watu wengi watafurahia kuwa Mungu anatenda miujiza kwa ajili yao, wakati kazi ile ni ya roho nyingine. Chini ya mwavuli wa dini, Shetani atatafuta kueneza mvuto wake juu ya ulimwengu wa Kikristo.PKSw 354.1

    Katika matukio mengi ya uamsho ambayo yametokea katika nusu karne iliyopita, nguvu ya aina hiyo imekuwa kazini, kwa kiwango kikubwa au kidogo zaidi, nguvu hiyo itatenda kazi kwa upana zaidi katika wakati ujao. Kunakuwepo misisimko na mihemko, mchanganyiko ya mambo ya kweli na ya uongo, vyote hivi vikiwa na kusudi la kupoteza watu. Lakini hakuna hata mtu mmoja anayelazimika kudanganywa. Katika nuru ya neno la Mungu siyo vigumu kugundua asili ya harakati hizi. Mahali popote watu wanapopuuza ushuhuda wa neno la Mungu, wakiuacha ukweli wa wazi, unaopima mioyo, unaotaka kujikana nafsi na kuachana na dunia, hapo tunaweza kujua kuwa mbaraka wa Mungu hauwezi kutolewa. Na kwa mwongozo ambao Kristo Mwenyewe aliutoa, “Mtawatambua kwa matunda yao” (Mathayo 7:16), ni dhahiri kuwa harakati hizi siyo kazi ya Roho wa Mungu.PKSw 355.1

    Katika ukweli wa neno Lake, Mungu amejifunua kwa watu; na watu wote wanaoupokea huo ukweli wanakingwa dhidi ya uongo wa Shetani. Ni kupuuza ukweli huu ambako kumefungua mlango kwa ajili ya maovu ambayo sasa yanazidi kuenea katika ulimwengu wa kidini. Msingi na umuhimu wa sheria ya Mungu, kwa kiasi kikubwa, havipo akilini mwa watu. Uelewa potovu kuhusu sifa, uendelevu, na ulazima wa sheria ya Mungu umesababisha makosa kuhusiana na uongofu na utakaso, na umesababisha kushuka kwa kiwango cha utakatifu katika kanisa. Na hii ndiyo siri ya kutokuwepo kwa Roho na nguvu ya Mungu katika matukio ya uamsho ya nyakati zetu hizi.PKSw 355.2

    Wapo, katika madhehebu mbalimbali, watu mashuhuri kwa uadilifu wao, wanaoukiri na wanaoukataa ukweli huu. Profesa Edwards A. Park, akielezea hatari za sasa za kidini alisema kwa ufasaha: “Chanzo kimoja cha hatari ni uzembe wa mimbari katika kusimamia utekelezaji wa sheria ya Mungu. Katika siku za awali mimbari ilikuwa mwangwi wa sauti ya dhamiri.... Wahubiri wakuu walio wengi waliyapa mahubiri yao utukufu wa ajabu kwa kufuata mfano wa Bwana wao, wakiweka uzito kwa sheria ya Mungu, kanuni zake, na utisho wake. Walirudia misemo miwili ya hekima, kuwa sheria ni nakala ya tabia ya utakatifu wa Mungu, na kuwa mtu asiyeipenda sheria ya Mungu haipendi injili; kwa kuwa sheria na injili ni kioo kinachoakisi tabia ya kweli ya Mungu. Hatari hii inaongozana na hatari nyingine, hatari ya kushindwa kubaini ubaya wa dhambi, ukubwa wake, na madhara yake. Kuna uwiano kati ya kiwango cha uzuri wa kuitii sheria ya Mungu na kiwango cha ubaya wa kutoitii....PKSw 355.3

    “Pamoja na hatari zilizokwisha kutajwa, kuna hatari nyingine ya kushindwa kubaini haki ya Mungu. Mwelekeo wa mimbari za leo ni kutenganisha haki ya Mungu na wema wa Mungu; mimbari za leo kushusha hadhi ya wema wa Mungu na kuuona kama hisia tu badala ya kuupa hadhi ya kanuni. Ufafanuzi wa kiteolojia unatenganisha alivyoviunganisha Mungu. Je, sheria ya Mungu ni njema au ni mbaya? Ni njema. Haki ni njema; kwa kuwa kazi yake ni kutekeleza sheria. Kutokana na tabia ya kushindwa kubaini wema wa sheria na haki ya Mungu, na kushindwa kubaini kiwango na hasara ya uasi wa mwanadamu, wanadamu ni wepesi kuteleza na kujikuta wakipuuza neema ambayo inawezesha upatanisho kwa ajili ya dhambi.” Hivyo injili inapoteza thamani yake na umuhimu wake katika akili za watu, na haichukui muda mrefu wanakuwa tayari kutupilia mbali Biblia yenyewe.PKSw 355.4

    Walimu wa dini wengi wanadai kuwa, Kristo, kwa njia ya kifo Chake, aliitangua sheria, na watu sasa hawabanwi na matakwa yake. Wapo baadhi wanaoiwasilisha sheria ya Mungu kama mzigo mzito, na kinyume na utumwa wa sheria, wanawasilisha uhuru unaopatikana chini ya injili.PKSw 355.5

    Lakini sivyo manabii na mitume walivyoichukulia sheria takatifu ya Mungu. Daudi alisema: “Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako” (Zaburi 119:45). Mtume Yakobo, aliyeandika baada ya kifo cha Kristo, anaeleza Amri Kumi kuwa “sheria ya kifalme” na “sheria kamilifu iliyo ya uhuru” (Yakobo 2:8; 1:25). Na nabii wa ufunuo, nusu ya karne baada ya kusulubishwa kwa Kristo, alitangaza baraka juu yao “wazishikao amri Zake, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake” (Ufunuo 22:14).PKSw 356.1

    Dai kuwa Kristo, kwa njia ya kifo Chake, alitangua sheria ya Baba Yake halina msingi. Kama kungekuwa na uwezekano wa kubadilisha sheria au kuiweka pembeni, Kristo asingelazimika kufa kumwokoa mwanadamu kutoka katika adhabu ya dhambi. Kifo cha Kristo, mbali na kuwa hakikutangua sheria, kinathibitisha kuwa sheria haibadiliki. Mwana wa Mungu alikuja “kuitukuza sheria, na kuiadhimisha” (Isaya 42:21). Alisema: “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati;” “Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka” (Mathayo 5:17, 18). Na Kristo Mwenyewe anaeleza msimamo Wake: “Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu” (Zaburi 40:8).PKSw 356.2

    Sheria ya Mungu, kutokana na ilivyo, haiwezi kubadilika. Ni ufunuo wa mapenzi na tabia ya Mwasisi wake. Mungu ni pendo, na sheria Yake ni pendo. Kanuni zake kuu mbili ni kumpenda Mungu na kumpenda mwanadamu. “Pendo ndilo utimilifu wa sheria” (Warumi 13:10). Tabia ya Mungu ni haki na ukweli; na hiyo ndiyo asili ya sheria Yake. Mwandishi wa zaburi anasema: “Sheria yako ni kweli:” “Sheria yako ni haki ya milele” (Zaburi 119:142, 172). Na mtume Paulo anasema: “Torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema” (Warumi 7:12). Sheria hiyo, kwa kuwa inaeleza kilichomo katika akili na mapenzi ya Mungu, lazima iwe ya milele kama Mwasisi wake alivyo wa milele.PKSw 356.3

    Ni kazi ya uongofu na utakaso kuwapatanisha watu na Mungu kwa kuwapatanisha na kanuni za sheria Yake. Hapo mwanzo, mwanadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu. Alikuwa akiafikiana na asili na sheria ya Mungu; kanuni za haki zilikuwa zimeandikwa ndani ya moyo wake. Lakini dhambi ilimtenga na Muumbaji wake. Hakuweza tena kuakisi sura ya Mungu. Moyo wake ulipigana vita dhidi ya kanuni za sheria ya Mungu. “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii” (Warumi 8:7). Lakini “Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee,” ili mwanadamu apatanishwe na Mungu. Kwa njia ya haki ya Kristo anaweza kurudishwa katika mwafaka na Mwumbaji wake. Moyo wake unapaswa uumbwe upya kwa neema ya Mungu; ni lazima apokee maisha mapya yatokayo mbinguni. Badiliko hili ni uzoefu wa kuzaliwa upya, ambao, mtu asipokuwa nao, Yesu anasema, “hawezi kuuona ufalme wa Mungu.”PKSw 356.4

    Hatua ya kwanza katika upatanisho na Mungu ni mtu kushawishika na kukiri kuwa ni mwenye dhambi. “Dhambi ni uasi wa sheria” “Kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria” (1 Yohana 3:4; Warumi 3:20). Ili aone hatia yake, mwenye dhambi lazima apime tabia yake kwa njia ya kiwango cha Mungu cha haki. Ni kioo kinachoonesha ukamilifu wa tabia ya haki na humwezesha mwenye dhambi kutambua mapungufu yake.PKSw 357.1

    Sheria inamfunulia mtu dhambi zake, lakini sheria haitoi tiba. Wakati ambapo inaahidi uzima kwa mtu mtiifu, inatangaza kuwa kifo ndiyo mshahara wa mkosaji. Injili ya Kristo pekee ndiyo inaweza kumwokoa mwenye dhambi kutoka katika hukumu au uchafu wa dhambi. Inampasa mwenye dhambi kutubu kwa Mungu, ambaye sheria Yake imevunjwa; na imani katika Kristo, kafara yake pekee ya upatanisho. Hivyo anapokea “ondoleo la dhambi zilizopita” na anakuwa mshirika wa asili ya uungu. Yeye ni mwana wa Mungu, akiwa amepokea roho ya kupangwa, ambapo analia: “Aba, Baba!”PKSw 357.2

    Je, sasa yuko huru kuvunja sheria ya Mungu? Paulo anasema: “Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria” “Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” Na Yohana anatangaza: “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito” (Warumi 3:31; 6:2; 1 Yohana 5:3). Katika kuzaliwa mara ya pili moyo unaafikishwa na Mungu, kwa kuwa unapatanishwa na sheria Yake. Wakati badiliko hili kubwa linapokuwa limetokea ndani ya mwenye dhambi, ametoka katika mauti na kuingia katika uzima, kutoka dhambini na kuingia katika utakatifu, kutoka katika makosa na uasi na kuingia katika utii na uaminifu. Maisha ya zamani ya kujitenga na Mungu yamekoma; maisha mapya ya upatanisho, ya imani na upendo, yameanza. Ndipo “maagizo ya torati” yatatimizwa “ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho” (Warumi 8:4). Na lugha ya roho itakuwa: “Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa” (Zaburi 119:97).PKSw 357.3

    “Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi” (Zaburi 19:7). Bila sheria, wanadamu hawana ufahamu wa haki wa usafi na utakatifu wa Mungu au wa hatia yao na uchafu wao. Hawana hisia ya kweli ya hatia ya dhambi na hawahisi hitaji la toba. Kwa kutokuona hali yao ya kupotea kama wavunjaji wa sheria ya Mungu, hawatambui hitaji lao la damu inayopatanisha ya Kristo. Tumaini la wokovu hupokelewa bila badiliko la moyo au matengenezo ya maisha. Kwa njia hiyo waongofu wa juu juu ni wengi, na watu wengi wanaunganishwa na kanisa ambao hawajawahi kamwe kuunganishwa na Kristo.PKSw 357.4

    Nadharia potovu za utakaso, pia, zinazotokana na kupuuza au kukataa sheria ya Mungu, zinashika nafasi ya juu katika harakati za kidini za siku hizi. Nadharia hizi ni za uongo na ni za hatari katika matokeo ya kila siku; na ukweli kuwa zinakubaliwa na wengi kwa jumla, zinafanya iwe muhimu mara mbili kwamba watu wote wawe na uelewa sahihi wa kile kinachofundishwa na Maandiko kuhusu suala hili.PKSw 358.1

    Utakaso wa kweli ni fundisho la Biblia. Mtume Paulo, katika barua yake kwa kanisa la Thesalonike, anasema: “Haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu” Na anaomba kuwa: “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa” (1 Wathesalonike 4:3; 5:23). Biblia inafundisha wazi juu ya utakaso na jinsi unavyopatikana. Mwokozi aliomba kwa ajili ya wanafunzi Wake: “Uwatakase kwa ile kweli, neno Lako ndiyo kweli” (Yohana 17:17). Na Paulo anafundisha kuwa waaminio wanapaswa “kutakaswa na Roho Mtakatifu” (Warumi 15:16). Kazi ya Roho Mtakatifu ni nini? Yesu aliwaambia wanafunzi Wake: “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote” (Yohana 16:13. Na mwandishi wa Zaburi anasema: “Sheria Yako ni kweli“Kwa njia ya neno na Roho wa Mungu kanuni kuu za haki zilizowekwa katika sheria Yake zinafunuliwa. Na kwa kuwa sheria ya Mungu ni“takatifu, na ya haki, na njema,” nakala ya ukamilifu wa Kimungu, ina maana kuwa tabia inayojengwa kwa njia ya kuitii sheria ile itakuwa takatifu. Kristo ni mfano mkamilifu wa tabia hiyo. Anasema: mimi nimezishika “amri za Baba yangu” “Kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo” (Yohana 15:10; 8:29). Wafuasi wa Kristo wanapaswa kuwa kama Yeye alivyo—kwa neema ya Mungu inawapasa wajenge tabia zinazopatana na kanuni za sheria takatifu. Huu ni utakaso wa Biblia.PKSw 358.2

    Kazi hii inaweza kutekelezwa tu kwa njia ya imani katika Kristo, kwa nguvu ya Roho wa Mungu anayekaa ndani yao. Paulo anawahimiza waaminio: “Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Wafilipi 2:12, 13). Mkristo atahisi misukumo ya dhambi, lakini atadumu kuipiga vita dhambi. Hapa ndipo msaada wa Kristo unapohitajika. Udhaifu wa mwanadamu unaungana na nguvu ya Mungu, na imani inasema: “Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo” (1 Wakorintho 15:57).PKSw 358.3

    Maandiko yanaoneshwa wazi kuwa kazi ya utakaso ni endelevu. Wakati wa uzoefu wa uongofu, mwenye dhambi anapopata amani na Mungu kwa njia ya damu ya upatanisho, maisha ya Ukristo ndiyo yameanza tu. Sasa inampasa “akaze mwendo ili aufikilie utimilifu;” akue “hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo” Mtume Paulo anasema: “Natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu” (Wafilipi 3:13, 14). Na Petro anaweka mbele yetu hatua ambazo inampasa mtu kuzifuata ili kupata utakaso wa Biblia: “Mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. ... mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe” (2 Petro 1:5-10).PKSw 358.4

    Watu wanaopata uzoefu wa utakaso wa Biblia watadhihirisha roho ya unyenyekevu. Kama Musa, wamepata udhihirisho wa utukufu wa kutisha wa utakatifu, na wanaona kutokustahili kwao wakijilinganisha na usafi na ukamilifu ulioinuliwa juu wa Yeye asiyekuwa na Kikomo.PKSw 359.1

    Nabii Danieli alikuwa mfano wa utakaso wa kweli. Maisha yake marefu yalijazwa na huduma njema kwa ajili ya Bwana wake. Alikuwa mtu “apendwaye sana” (Danieli 10:11) na Mbingu. Hata hivyo, badala ya kudai kuwa msafi na mtakatifu, nabii huyu aliyeheshimiwa alijitambulisha kuwa mmoja wa wana wa Israeli ambao kwa kweli walikuwa watenda dhambi hasa alipokuwa akimlilia Mungu kwa niaba ya watu: “Hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi.” “Tumefanya dhambi, tumetenda maovu.” Anasema: “Nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu.” Na wakati wa baadaye Mwana wa Mungu alitokea, kumpa maelekezo, Danieli anasema: “Uzuri wangu uligeuzwa ndani yangu kuwa uharibifu, wala sikusaziwa nguvu” (Danieli 9:18, 15, 20; 10:8).PKSw 359.2

    Ayubu aliposikia sauti ya Bwana ikitoka katika upepo wa kisulisuli, alisema kwa huzuni: “Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu katika mavumbi na majivu” (Ayubu 42:6). Ilikuwa wakati Isaya alipouona utukufu wa Bwana, na alipomsikia kerubi akipiga kelele, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi,” ambapo alipiga kelele ya hofu, “Ole wangu! Kwa maana nimepotea” (Isaya 6:3, 5). Paulo, baada ya kuchukuliwa mpaka mbingu ya tatu na kusikia mambo ambayo yalikuwa hayawezekani kwa mwanadamu kuyatamka, anaeleza uzoefu wake kuwa alijona kuwa “mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote” (2 Wakorintho 12:24; Waefeso 3:8). Ilikuwa Yohana mpendwa, ambaye aliegemea kwenye kifua cha Yesu na kuuona utukufu Wake, ambaye alianguka chini kama mtu aliyekufa mbele ya miguu ya malaika (Ufunuo 1:17).PKSw 359.3

    Haiwezekani kuwepo kujiinua, madai ya majivuno ya kutokuwa na dhambi, kwa wanaotembea katika kivuli cha msalaba wa Kalwari. Wanatambua kuwa dhambi zao ndizo zilizosababisha uchungu uliovunja moyo wa Mwana wa Mungu, na wazo hili linawafanya wajishushe. Wanaoishi karibu kabisa na Yesu wanatambua kwa uwazi zaidi udhaifu na udhambi wa mwanadamu, na tumaini lao pekee linapatikana katika haki ya Mwokozi aliyesulubiwa na aliyefufuka.PKSw 359.4

    Utakaso ambao sasa unashika kasi sana katika ulimwengu wa kidini unabeba pamoja nao roho ya kujiinua na kupuuza sheria ya Mungu ambayo inaupinga kama jambo geni katika dini ya Biblia. Watetezi wa utakaso huo wanafundisha kuwa utakaso ni kazi ya kufumba na kufumbua, ambao kwa njia yake, kwa njia ya imani peke yake, wanafikia utakatifu kamili. “Amini peke yake,” wanasema, “na mbaraka ni wako.” Hakuna juhudi zaidi kwa upande wa mpokeaji inayohitajika. Kwa wakati huo huo wanakataa mamlaka ya sheria ya Mungu, wakidai kuwa wameachiliwa kutoka katika ulazima wa kutunza amri. Lakini inawezekanaje kwa wanadamu kuwa watakatifu, kulingana na mapenzi na tabia ya Mungu, pasipokuwa na mwafaka kati yao na kanuni ambazo zinaeleza asili na mapenzi Yake, na ambazo zinaonesha kile kinachompendeza Yeye?PKSw 360.1

    Tamaa ya kuwa na dini rahisi isiyohitaji kujitahidi, isiyohitaji kujikana nafsi, isiyohitaji kuachana na upuuzi wa kiulimwengu, imelifanya fundisho la imani, na imani pekee, kuwa fundisho pendwa; lakini neno la Mungu linasemaje? Mtume Yakobo anasema: “Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa?... Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai? Je! Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu? Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale? ... Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake” (Yakobo 2:14-24).PKSw 360.2

    Ushuhuda wa neno la Mungu uko kinyume cha fundisho hili lenye mtego la imani pasipo matendo. Siyo imani inayodai upendeleo wa Mbingu pasipo utii kwa masharti ambayo ni ya lazima ili rehema itolewe, ni kujidanganya; kwa kuwa imani ya kweli msingi wake ni ahadi na maagizo ya Maandiko.PKSw 360.3

    Mtu yeyote asijidanganye kuwa kuna imani ambayo kwayo mtu anaweza kuwa mtakatifu huku, kwa uchaguzi wake mwenyewe, anavunja moja ya matakwa ya Mungu. Utendaji wa dhambi inayojulikana unanyamazisha sauti inayoshuhudia ya Roho na unaitenga roho na Mungu. “Dhambi ni uasi wa sheria.” Na “kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua” (1 Yohana 3:6). Ingawa Yohana katika nyaraka zake anazungumzia kikamilifu juu ya upendo, lakini hasiti kufunua tabia halisi ya tabaka la watu wanaodai kuwa wametakaswa huku wakiishi katika uasi wa sheria ya Mungu. “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli” (1 Yohana 2:4, 5). Hapa kuna kipimo cha kila imani ya mtu. Hatuwezi kumhesabu mtu kuwa mtakatifu bila kumpima kwa kipimo cha kiwango pekee cha Mungu cha utakatifu mbinguni na duniani. Watu wasipohisi uzito wa sheria ya uadilifu, ikiwa wanapuuza na kudharau kanuni za Mungu, ikiwa wanavunja amri iliyo ndogo kabisa miongoni mwa amri Zake, na kuwafundisha watu hivyo, wanajidhalilisha wenyewe mbele za Mbingu, na tunaweza kutambua kuwa madai yao hayana msingi.PKSw 360.4

    Na dai la kutokuwa na dhambi, kwa lenyewe, ni ushahidi kuwa yeye anayetoa dai hilo yuko mbali kabisa na utakatifu. Ni kwa sababu hana uelewa sahihi wa usafi na utakatifu usio na kikomo wa Mungu au hana uelewa sahihi wa jinsi anavyopaswa kuwa yule ambaye atapatana na tabia Yake; kwa sababu hana uelewa sahihi wa usafi na uzuri ulioinuliwa juu wa Yesu, na hana uelewa sahihi wa madhara na madhila ya dhambi, ambapo mwanadamu anaweza kujidhania kuwa yeye ni mtakatifu. Kwa kadiri umbali kati yake na Kristo unavyokuwa mkubwa zaidi, na kwa kadiri uelewa wake wa tabia ya Mungu na matakwa Yake unavyokuwa mdogo zaidi, ndivyo anavyojiona kuwa yeye ni mwenye haki mbele ya macho yake mwenyewe.PKSw 361.1

    Utakaso ulioelezwa katika Maandiko hujumuisha uhai wote—roho, akili, na mwili. Paulo aliwaombea Wathesalonike kuwa nafsi zao na roho zao na miili yao wahifadhiwe wawe “kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo” (1 Wathesalonike 5:23). Tena aliwaandikia waaminio: “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu” (Warumi 12:1). Nyakati za Israeli ya zamani kila sadaka iliyoletwa kama kafara kwa Mungu ilipimwa kwa auangalifu. Ikiwa kasoro yo yote iligundulika katika mnyama aliyeletwa, mnyama yule alikataliwa; kwa sababu Mungu alikuwa ameagiza sadaka “asiyekuwa na mawaa.” Kwa hiyo Wakristo wameagizwa kutoa miili yao, “dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu.” Ili kufanya hivyo, nguvu zao zote inapasa zitunzwe katika hali nzuri kabisa kwa kadiri inavyowezekana. Kila tendo linalodhoofisha nguvu za mwili au za akili linamfanya mtu asifae kwa ajili ya huduma ya Muumbaji wake. Na je, Mungu atapendezwa na kitu chochote kilicho chini ya kiwango tunachoweza kutoa? Kristo alisema: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote.” Wale wanaompenda Mungu kwa moyo wao wote watakuwa na shauku ya kumpa huduma bora kabisa ya maisha yao, na watatafuta daima kuleta kila nguvu ya maisha yao katika mwafaka na sheria zitakazokuza uwezo wao wa kutenda mapenzi Yake. Hawatadhoofisha au kuchafua, kwa kuendekeza uchu au tamaa, sadaka ambayo wanaitoa kwa Baba yao wa mbinguni.PKSw 361.2

    Petro anasema: “Ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho” (1 Petro 2:11). Kila dhambi inayotendwa inatia ganzi fahamu na kuua utambuzi wa kiakili na kiroho, na neno au Roho huwa na mguso hafifu katika moyo wa mhusika. Paulo aliwaandikia Wakorintho: “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu” (2 Wakorintho 7:1). Na pamoja matunda ya Roho—“upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole”—anajumuisha “kiasi” (Wagalatia 5:22, 23).PKSw 362.1

    Licha ya matamko haya yaliyovuviwa, ni Wakristo wangapi hudhoofisha nguvu zao katika kutafuta faida ibada ya mitindo; ni wangapi hudhalilisha utu wao wenye sura ya Mungu kwa ulafi, unywaji wa pombe, na anasa zilizokatazwa. Na kanisa, badala ya kukemea, mara nyingi huhamasisha uovu kwa kuchochea uchu, tamaa ya mapato au kupenda anasa, ili kujaza hazina ya kanisa, ambayo upendo wa Kristo umeshindwa kuijaza kwa sababu ni dhaifu mno. Ikiwa Yesu angeingia makanisa ya leo na kuona sherehe na biashara najisi zinazoendeshwa humo kwa jina la dini, je, si angewatoa nje hao watu wanaonajisi makanisa, kama alivyotoa nje wabadilishao fedha kutoka hekaluni?PKSw 362.2

    Mtume Yakobo anasema kuwa hekima itokayo juu “kwanza ni safi.” Ikiwa angekutana na watu wanaolikiri jina la Yesu kwa midomo iliyochafuliwa na sigara, wale ambao pumzi na miili yao imechafuliwa kwa harufu yake mbaya, na huchafua hewa ya angani na kuwalazimisha wote wanaomzunguka kuvuta sumu—ikiwa mtume angekutana na tabia hii ambayo ni kinyume na usafi wa injili, si angeikemea na kuiita “ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani”? Watumwa wa tumbaku, wakidai kuwa wamepata mbaraka wa utakaso kamili, wanazungumzia tumaini lao la mbinguni; lakini neno la Mungu linasema waziwazi kuwa “ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge” (Ufunuo 21:27).PKSw 362.3

    “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu, na katika roho zenu, ambayo ni ya Mungu” (1 Wakorintho 6:19, 20). Yeye ambaye mwili wake ni hekalu la Roho Mtakatifu hatakuwa mtumwa wa tabia inayomdhuru. Nguvu zake ni mali ya Kristo, ambaye amemnunua kwa ghrama ya damu. Mali yake ni mali ya Bwana. Atakosaje kuwa na hatia kwa kufuja mtaji aliopewa dhamana kuusimamia? Wanaojiita Wakristo hutumia kiasi kikubwa cha pesa kununulia vitu visivyo na manufaa na vyenye madhara, wakati roho zinaangamia kwa kukosa neno la uzima. Mungu anaibiwa zaka na sadaka, huku wakiteketeza juu ya madhabahu ya tamaa zinazoangamiza kiasi kikubwa zaidi kuliko kile wanachotoa kusaidia maskini au kwa ajili ya kutegemeza injili. Ikiwa wale wanaodai kuwa wafuasi wa Kristo wangekuwa wametakaswa kikamilifu, mali zao, badala ya kutumika kwa ajili ya matumizi yasiyo ya lazima na hata yenye madhara, zingepaswa kuletwa katika hazina ya Bwana, na Wakristo inawapasa kuonesha mfano kiasi, kujikana nafsi, na kutoa kafara. Ndipo watakuwa nuru ya ulimwengu.PKSw 362.4

    Ulimwengu umejitumbukiza katika anasa. “Tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima” vinatawala idadi kubwa ya watu. “Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu.” Katika nuru ya neno la Mungu tuna haki ya kusema kuwa utakaso hauwezi kuwa wa kweli ikiwa hauwezi kufanya kazi hii ya kuukataa kabisa utafutaji wa dhambi na anasa za dunia.PKSw 363.1

    Kwa wale wanaotimiza masharti, “Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, ... Msiguse kitu kilicho kichafu,” ahadi ya Mungu ni, “Nami nitawakaribisha, na nitakuwa Baba kwenu, nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi” (2 Wakorintho 6:17, 18). Ni fursa na wajibu wa kila Mkristo kuwa na uzoefu mkubwa na mwingi katika mambo ya Mungu. “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu,“Yesu alisema.” Yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima” (Yohana 8:12). “Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu” (Mithali 4:18). Kila hatua ya imani na utii huileta roho katika mshikamano wa karibu zaidi na Nuru ya ulimwengu, ambamo ndani Yake “giza lo lote hamna.” Miale inayong'ara ya Jua la Haki inawamulika watumishi wa Mungu, na wao wanaakisi miale ya nuru Yake. Kama vile nyota zinavyotuambia kuwa kuna nuru kubwa mbinguni ambayo inazifanya zinang'are, kadhalika Wakristo wanapaswa kudhihirisha kuwa kuna Mungu juu ya kiti cha enzi cha Ulimwengu ambaye anastahili sifa na kuigwa. Neema za Roho, usafi na utakatifu wa tabia Yake, vitaonekana miongoni mwa mashahidi Wake.PKSw 363.2

    Paulo katika barua yake kwa Wakolosai anataja mibaraka mikubwa inayotolewa kwa watoto wa Mungu. Anasema: “Hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha” (Wakolosai 1:9-11).PKSw 363.3

    Kadhalika anaandika kuhusu shauku yake kuwa ndugu walioko Efeso wajue kimo cha upendeleo wa Mkristo. Anawaeleza, kwa lugha fasaha kabisa, nguvu na maarifa ya ajabu ambayo wanaweza kuwa nayo kama wana na binti za Yeye Aliye Juu sana. Ilikuwa stahiki yao “kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani,” kuwa “na shina na msingi katika upendo ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu” Lakini ombi la mtume linafikia kilele cha upendeleo anapoomba kuwa “mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Waefeso 3:16-19).PKSw 363.4

    Hapa kuna kimo cha mafanikio ambacho tunaweza kukifikia kwa njia ya imani katika ahadi za Baba yetu wa mbinguni, tunapotimiza matakwa Yake. Kwa njia ya haki ya Kristo tunayo fursa ya kukiendea kiti cha enzi cha Nguvu Isiyokuwa na Mipaka. “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?” (Warumi 8:32). Baba alimtoa Roho Wake kwa Mwana Wake bila kipimo, na sisi pia tunaweza kushiriki ukamilifu Wake. Yesu anasema, “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” (Luka 11:13). “Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” “Ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu” (Yohana 14:14: 16:24).PKSw 364.1

    Ingawa maisha ya Mkristo yatadhihirisha unyenyekevu, hayapaswi kugubikwa na huzuni na kutojithamini. Ni fursa iliyo wazi kila mmoja kuishi kwa jinsi ambayo Mungu atamkubali na kumbariki. Siyo mapenzi ya Baba yetu wa mbinguni kuwa tuwe chini ya hukumu na giza daima. Hakuna ushahidi wa unyenyekevu wa kweli katika kutembea huku kichwa kimeinamishwa chini na moyo ukiwa umejaa mawazo ya ubinafsi. Tunaweza kumwendea Yesu ili tutakaswe, na kusimama mbele ya sheria bila aibu wala hatia. “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu” (Warumi 8:1).PKSw 364.2

    Kwa njia ya Yesu wana wa Adamu walioanguka wanakuwa “wana wa Mungu” “Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake” (Waebrania 2:11). Maisha ya Mkristo yanapaswa kuwa ya imani, ushindi, na furaha ndani ya Mungu. “Kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu” (1 Yohana 5:4). Mtumishi wa Mungu Nehemia alisema ukweli: “Furaha ya Bwana ni nguvu zenu” (Nehemia 8:10). Na Paulo anasema: “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini” “Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” (Wafilipi 4:4; 1 Wathesalonike 5:16-18).PKSw 364.3

    Haya ndiyo matunda ya uongofu na utakaso wa Biblia; na ni kwa sababu kanuni kuu za haki zilizotajwa katika sheria ya Mungu hazipendwi sana na ulimwengu wa Wakristo ndio maana matunda haya hayaonekani sana. Hii ndiyo sababu kuna udhihirisho mdogo sana wa kazi endelevu na ya kina ya Roho wa Mungu iliyokuwepo katika harakati za uamsho za miaka ya awali.PKSw 365.1

    Ni kwa kutazama tunabadilishwa. Na zile kanuni takatifu ambazo ndani yake Mungu amewafunulia watu ukamilifu na utakatifu wa tabia Yake zinapopuuzwa, na akili za watu zikavutwa kutafakari mafundisho na nadharia za kibinadamu, hatupaswi kushangaa kuwa kuna poromoko la utakatifu kanisani. Bwana alisema: “Wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji” (Yeremia 2:13).PKSw 365.2

    “Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki.... Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa” (Zaburi 1:1-3). Ni pale tu sheria ya Mungu inaporudishwa mahali pake stahiki kunaweza kuwepo uamsho wa imani na utauwa wa awali miongoni mwa watu wa Mungu. “Bwana asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, I wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu” (Yeremia 6:16). PKSw 365.3

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents