Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 38—Onyo la Mwisho

  “Naliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake. Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza.” “Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake” (Ufunuo 18:1, 2, 4).PKSw 460.1

  Andiko hili huonesha mbele kwa wakati ambapo tangazo la anguko la Babeli, kama lilivyotolewa na malaika wa pili wa Ufunuo 14 (aya 8), litarudiwa, likiwa na nyongeza ya orodha ya matendo ya kifisadi ambayo yamekuwa yakiingia katika mashirika mbalimbali yanayounda Babeli, kwa kuwa ujumbe huo ulitolewa kwanza, wakati wa kiangazi cha mwaka 1844. Hali ya kutisha ya ulimwengu wa kidini imeelezwa hapa. Kwa kila tukio la kuukataa ukweli, akili za watu zinaingiwa na giza zaidi, mioyo yao inazidi kuwa migumu zaidi, mpaka wananaswa katika ugumu wa ukafiri. Kwa kupuuza maonyo ambayo Mungu ameyatoa, wataendelea kukanyaga moja ya kanuni za Amri Kumi, mpaka wanawatesa wale wanaoitakasa. Kristo anaonekana kuwa si kitu kwa sababu ya dharau ambayo imewekwa juu ya neno Lake na watu Wake. Mafundisho ya imani ya kuongea na wafu yanapokelewa na makanisa, kizuizi kilichowekwa kudhibiti moyo usiozaliwa upya kimeondolewa, na kukiri kuwa mtu wa dini kutakuwa joho la kuficha uovu uliokithiri. Imani katika maonesho ya kiroho inafungua mlango kwa roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani, na kwa njia hiyo mvuto wa malaika waovu utahisiwa katika makanisa.PKSw 460.2

  Kuhusu Babeli, wakati ikioneshwa katika unabii huu, imeelezwa: “Dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake” (Ufunuo 18:5). Babeli imejaza kikombe cha hatia yake, na maangamizi yanakaribia kuiangukia. Lakini Mungu bado ana watu ndani ya Babeli; na kabla ya kutekelezwa kwa hukumu Zake, hawa watu waaminifu inapasa waitwe na watoke nje, ili wasishiriki dhambi zake na “wasipokee mapigo yake.” Ndiyo maana kuna vuguvugu linawakilishwa na malaika anayeshuka kutoka mbinguni, akiangazia dunia yote kwa utukufu wake, akilia kwa sauti kuu, kutangaza dhambi za Babeli. Pamoja na ujumbe wake sauti inasikika: “Tokeni kwake, enyi watu wangu.” Matangazo haya, yakiungana na ujumbe wa malaika wa tatu, huunda onyo la mwisho litakalotolewa kwa wakazi wa dunia.PKSw 460.3

  Tukio linaloukabili ulimwengu ni la kutisha. Mamlaka za dunia, zikiungana pamoja kupigana vita dhidi ya amri za Mungu, zitatoa agizo kuwa “wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa” (Ufunuo 13:16), wafuate desturi za kanisa kwa utunzaji wa sabato ya uongo. Wote wanaokataa kutii agizo hilo watapata adhabu za kiserikali, na hatimaye watatangazwa kuwa wanastahili kifo. Kwa upande mwingine, sheria ya Mungu inayoagiza pumziko la siku ya Muumbaji inadai utii na inatishia ghadhabu dhidi ya wale wote wanaovunja kanuni zake.PKSw 460.4

  Baada ya agizo kuletwa kwa uwazi mbele ya mtu, yeyote atakayekanyaga sheria ya Mungu ili kutii agizo la mwanadamu anapokea alama ya mnyama; anapokea ishara ya utii kwa mamlaka anayochagua kuitii badala ya Mungu. Onyo kutoka mbinguni ni: “Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake, yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake” (Ufunuo 14:9, 10).PKSw 461.1

  Lakini hakuna mtu hata mmoja ambaye atakutana na hasira ya Mungu mpaka ukweli umeingia katika akili yake na dhamiri yake, na umekataliwa. Kuna watu wengi ambao hawajapata fursa ya kusikia ukweli maalumu wa wakati huu. Ulazima wa amri ya nne haujawasilishwa mbele yao katika nuru yake halisi. Yeye anayesoma kila moyo na kupima kila nia hatamwacha mtu hata mmoja aliye na shauku ya kuujua ukweli, adanganywe kuhusu masuala ya msingi katika pambano. Amri haitashinikizwa juu ya watu katika hali ya upofu. Kila mtu atapewa nuru ya kutosha ili afanye uamuzi kwa akili.PKSw 461.2

  Sabato itakuwa kipimo kikuu cha utiifu, kwa sababu ni kipengele cha ukweli ambacho kinabishaniwa sana kwa namna ya pekee. Wakati jaribio la mwisho litakapofika, mstari unaoonesha tofauti utachorwa kati ya wale wanaomtumikia Mungu na wale wasiomtumikia. Wakati ambapo utunzaji wa sabato ya uongo katika kutii sheria ya nchi, kinyume na amri ya nne, utakuwa uthibitisho wa kuitii mamlaka inayompinga Mungu, utunzaji wa Sabato ya kweli, katika kuitii sheria ya Mungu, ni ushahidi wa utii kwa Muumbaji. Wakati tabaka moja, kwa kukubali alama ya kujisalimisha kwa mamlaka za kidunia, wanapokea alama ya mnyama, tabaka jingine likichagua ishara ya utii kwa mamlaka ya Kimungu, wanapokea muhuri wa Mungu.PKSw 461.3

  Tangu wakati huo na kurudi nyuma watu waliohubiri ukweli wa ujumbe wa malaika wa tatu, mara nyingi walionekana kama wavumishaji wa mambo ya kutisha. Utabiri wao kuwa kukosa uvumilivu wa kidini utatawala nchini Marekani, kuwa kanisa na serikali vitaungana na kuwatesa wale wanaotunza amri za Mungu, umetangazwa kuwa usio na msingi na imetangazwa kwa uhakika kuwa nchi hii haiwezi kuwa tofauti na jinsi ambavyo imekuwa siku zote—mtetezi wa uhuru wa kidini. Lakini suala la ulazimishaji wa utunzaji wa Jumapili linahamasishwa kila mahali, tukio ambalo limetiliwa mashaka na kutoaminiwa kwa muda mrefu linaonekana kama linakaribia, na ujumbe wa tatu utaleta matokeo ambayo hayajawahi kuletwa kabla ya hapo.PKSw 461.4

  Katika kila kizazi Mungu ametuma watumishi wakemee dhambi, ulimwenguni na kanisani. Lakini watu wanatamani kuambiwa mambo laini, na ukweli ulio safi usiopakwa vanishi haukubaliki. Wanamatengenezo wengi, walipoanza kazi yao, waliazimia kutumia busara kubwa katika kushambulia dhambi za kanisa na za taifa. Walitumaini, kwa njia ya mfano wa maisha safi ya Kikristo, wangewaongoza watu kwenye mafundisho ya Biblia. Lakini Roho wa Mungu alikuja juu yao kama alivyokuja kwa Eliya, akamsukuma kukemea dhambi za mfalme mwovu na watu walioasi; hawakuweza kujizuia kuhubiri matamko ya wazi ya Biblia—mafundisho ambayo walikuwa wazito kuyahubiri. Walisukumwa kutangaza kwa bidii ukweli na hatari iliyotishia roho. Maneno waliyopewa na Bwana waliyasema, bila kuogopa matokeo, na watu walilazimishwa kusikia onyo.PKSw 462.1

  Hivyo ndivyo ujumbe wa malaika wa tatu utakavyohubiriwa. Wakati ukifika wa kuutangaza kwa nguvu nyingi zaidi kuliko wakati mwingine wo wote, Bwana atatenda kazi kwa njia ya vyombo vinyenyekevu, akiongoza akili za wale ambao wamejiweka wakfu kwa ajili ya huduma ya Bwana. Watendakazi watawezeshwa hususani kwa upako wa Roho Mtakatifu kuliko kwa njia ya mafunzo katika vyuo vya elimu. Watu wenye imani na maombi watabidishwa kutoka kwa juhudi takatifu, wakitangaza maneno ambayo Mungu atawapa. Dhambi za Babeli zitawekwa wazi. Matokeo ya kutisha ya kushinikiza uadhimishaji wa siku kuu za kikanisa kwa njia ya mamlaka za kiserikali, madhara ya imani ya kuongea na wafu, maendeleo ya kimya lakini ya kasi ya mamlaka ya upapa—vyote vitawekwa wazi. Kwa njia ya maonyo haya watu wataamshwa. Maelfu kwa maelfu watasikia ambao hawajawahi kusikia maneno kama haya. Kwa mshangao watasikia ushuhuda kuwa Babeli ni kanisa, lililoanguka kwa sababu ya makosa yake na dhambi zake, kwa sababu liliukataa ukweli liliotumiwa na Mbingu. Watu watakapowaendea walimu wao wa zamani wakiwa na swali la dhati, Je, mambo haya yako hivyo? Wachungaji watawasimulia hadithi za kutunga, watatoa unabii wa mambo laini, ili kupoza hofu zao na kunyamazisha dhamiri zao zilizoamshwa. Lakini, kwa kuwa wengi watakataa kuridhishwa na mamlaka za watu na kudai tamko la wazi la “Hivi ndivyo Bwana asemavyo,” viongozi wa kanisa, sawa na Mafarisayo wa zamani, wakiwa wamekasirika kwa kuwa mamlaka yao imehojiwa, watakemea ujumbe huo wakisema kuwa ni ujumbe wa Shetani na watawachochea wapenda dhambi wawatukane na kuwatesa wale wanaoutangaza.PKSw 462.2

  Pambano litakapopanuka na kuingia katika maeneo mapya na akili za watu kuvutwa na kugundua sheria ya Mungu iliyokanyagwa, Shetani ataamka. Nguvu iliyomo katika ujumbe itawakasirisha zaidi wale wanaoupinga ujumbe. Viongozi wa kidini watatumia nguvu nyingi sana kuizima nuru isije ikawamulikia waumini wao. Kwa kila njia iliyoko katika uwezo wao watajitahidi kukomesha mjadala wa masuala haya muhimu. Kanisa litaomba msaada wa mkono wenye nguvu wa serikali, na, katika kazi hii wafuasi wa upapa na Waprotestanti wataungana. Vuguvugu la ulazimishaji wa Jumapili litakuwa na ujasiri mkubwa zaidi na litawekewa mikakati ya makusudi, sheria itatungwa dhidi ya watunzaji wa amri kumi. Watatishiwa kutozwa faini na kupelekwa kifungoni, na baadhi watapewa vyeo vikubwa, na zawadi na fursa zingine, kama vishawishi vya kuwafanya wakane imani zao. Lakini jibu lao lisilobadilika ni: “Mtuoneshe kosa letu katika neno la Mungu”—ombi ambalo liliwahi kutolewa na Luther katika mazingira yanayofanana na hayo. Wanaofikishwa mahakamani wanatoa ushuhuda thabiti wenye nguvu kwa ajili ya ukweli, na baadhi ya wale wanaousikia wanachukua uamuzi wa kusimama pamoja na wale wanaotunza amri za Mungu. Kwa njia hiyo, nuru itapelekwa kwa maelfu ambao, kama isingekuwa kwa njia hiyo, wasingepata fursa ya kuujua ukweli huu.PKSw 462.3

  Utii uliojengwa juu ya uelewa wa neno la Mungu utachukuliwa kuwa uasi. Kwa kufumbwa macho na Shetani, mzazi atatumia ukali na ukatili dhidi ya mtoto wake atakayeuamini ukweli. Upendo utatoweka; watoto watanyang'anywa urithi wao na watafukuzwa nyumbani. Maneno ya Paulo yatatimizwa kama yanavyosomeka: “Wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa” (2 Timotheo 3:12). Watetezi wa ukweli watakapokataa kuiheshimu sabato ya Jumapili, baadhi watatupwa gerezani, baadhi yao watakimbia nchi zao, badhi watafanywa kuwa watuma. Kwa hekima ya kibinadamu yote haya kwa sasa yanaonekana kama mambo yasiyowezekana; lakini Roho wa Mungu anayezuia atakapoondolewa kwa watu, wabaki wakiwa chini ya utawala wa Shetani, ambaye anachukia kanuni za Kiungu, kutakuwepo matukio ya ajabu. Moyo unaweza kuwa mkatili wakati hofu ya Mungu na upendo Wake vinapokuwa vimeondolewa.PKSw 463.1

  Dhoruba inapokaribia, tabaka kubwa la wale ambao wameuamini ujumbe wa malaika wa tatu, lakini hawakutakaswa kwa njia ya kuutii ukweli, watatupilia mbali msimamo wao na watajiunga na kundi la wapinzani. Kwa kuungana na ulimwengu na kushiriki roho yake, watakuwa na mtazamo wa mambo unaofanana sana na wa ulimwengu; na wakati jaribu litakapokuja, watakuwa tayari kuchagua upande ulio rahisi, upande unaopendwa na wengi. Watu wenye talanta na wenye nafasi katika jamii, ambao awali walifurahia ukweli, watatumia mivuto yao kudanganya na kupoteza. Wanatokea kuwa maadui wakuu wa ndugu zao wa zamani. Wakati watunza Sabato watakapoletwa mbele ya mahakama kujibu maswali kuhusu imani yao, hawa waasi watakuwa mawakala makini wa Shetani katika kuwawakilisha vibaya na kuwashitaki, na kwa njia ya taarifa za uongo na kauli zisizokuwa za kweli watawachochea watawala dhidi yao.PKSw 463.2

  Katika kipindi hiki cha mateso imani ya watumishi wa Bwana itajaribiwa. Watakuwa wametoa onyo kwa uaminifu, wakimwangalia Mungu na neno Lake pekee. Roho wa Mungu, akigusa mioyo yao, amewabidisha kusema. Wakisukumwa na bidii takatifu, na nguvu ya Mungu ikiwa juu yao, wataingia katika utekelezaji wa majukumu yao bila ya kuhofia matokeo ya kuwahubiria watu neno ambalo Bwana atawapa. Hawatajali maslahi yao ya muda, wala hawatajali heshima yao, au maisha yao. Hata hivyo, wakati dhoruba ya upinzani na dhihaka itakapopasukia juu yao, baadhi yao, kwa hofu na mshangao, watafikia hatua ya kusema: “Ikiwa tungejua mapema matokeo ya maneno yetu, tungenyamaza kabisa.” Watazingirwa na matatizo makubwa. Shetani atawashambulia kwa majaribu makali. Kazi ambayo walikuwa wamejaribu kuifanya inaonekana kana kwamba iko nje ya uwezo wao kuikamilisha. Watatishiwa kuuawa. Hamasa watakayoanza nayo itatoweka; lakini hawatakuwa na uwezo wa kurudi nyuma. Ndipo, kwa kuhisi kutokuwa na msaada kabisa, watamkimbilia Yeye aliye na nguvu zote awape nguvu. Watakumbuka kuwa maneno waliyoyasema hayakuwa maneno yao, bali Yake Yeye aliyekuwa amewaagiza kutoa onyo. Mungu aliweka ukweli katika mioyo yao, na wasingeweza kujizuia kuutangaza.PKSw 463.3

  Majaribu kama hayo yalishawapata watu wa Mungu zama zilizopita. Wycliffe, Huss, Luther, Tyndale, Baxter, Wesley, walisisitiza kuwa mafundisho yote lazima yapimwe kwa kuyalinganisha na Biblia na walitangaza kuwa wangekataa kila kitu ambacho Biblia ilikitaa. Dhidi ya hawa mateso yalirindima kwa hasira kali; hata hivyo hawakuacha kutangaza ukweli. Vipindi mbalimbali na tofauti katika historia ya kanisa vina alama na kila kipindi kikiwa na alama yake ya ukweli fulani maalumu ulioibuliwa na kufundishwa kukidhi mahitaji maalumu ya watu wa Mungu kwa wakati huo. Kila ukweli mpya ulisonga mbele dhidi ya chuki na upinzani; wale waliobarikiwa na nuru ya ukweli huo walijaribiwa na kuteswa. Bwana hutoa ukweli maalumu kwa watu wakati wa dharura. Ni nani wanaothubutu kukataa kuutangaza? Anawaagiza watumishi wake kutangaza wito wa mwisho wa rehema kwa ulimwengu. Hawawezi kukaa kimya, isipokuwa kwa kuhatarisha roho zao. Mabalozi wa Kristo hawapaswi kufikiria juu ya matokeo ya kutekeleza agizo la Mungu. Inawapasa kutekeleza wajibu wao na kumwachia Mungu matokeo.PKSw 464.1

  Upinzani unapoinuka juu katika kilele cha ukali wake, watumishi wa Mungu wanatatizika; hii ni kwa sababu inaonekana kana kwamba wao ndio wamesababisha mgogoro huo. Lakini dhamiri na neno la Mungu vinawathibitishia kuwa wapo katika njia sahihi; na japokuwa majaribu yanaendelea, wanapewa nguvu ya kukabiliana nayo. Shindano hukua na kuwa karibu yao zaidi na kuwa kali zaidi, lakini imani na ujasiri huongezeka na kupanda kukabiliana na dharura iliyopo. Ushuhuda wao ni: “Hatuwezi kuthubutu kuchezea neno la Mungu, kuigawa sheria Yake takatifu; tukisema sehemu hii ni muhimu na sehemu hii siyo muhimu, ili tupendwe na ulimwengu. Bwana tunayemtumikia aweza kutuokoa. Kristo amezishinda mamlaka za dunia; sisi tuogope ulimwengu ambao tayari umeshashindwa?”PKSw 464.2

  Mateso katika miundo yake mbalimbali ni mwendelezo wa kanuni ambayo itadumu kuwepo kwa kadiri Shetani atakavyodumu kuwepo na kwa kadiri Ukristo utakavyodumu kuwa na nguvu. Hakuna mtu anayeweza kumtumikia Mungu bila kujiletea upinzani wa majeshi ya giza dhidi yake mwenyewe. Malaika waovu watamshambulia, wakiogopa kuwa mvuto wake utawapokonya mateka wao kutoka katika mikono yao. Watu waovu, kwa kukemewa na mfano wake, wataungana pamoja wakitafuta kumtenga na Mungu kwa majaribu yanayovutia. Haya yasipofaulu kumwangusha, ndipo mamlaka yenye nguvu inatumika kumlazisha aende kinyume na dhamiri yake.PKSw 465.1

  Lakini kwa kadiri Yesu anaendelea kuwa mwombezi wa mwanadamu katika patakatifu pa mbinguni, nguvu inayozuia ya Roho Mtakatifu inahisiwa na Watawala na watu. Kwa kiasi fulani bado nguvu hii inatawala sheria za nchi. Isingekuwa kwa njia ya sheria hizi, hali ya ulimwengu ingekuwa mbaya zaidi ya ilivyo sasa. Wakati wengi wa watawala wetu ni mawakala hai wa Shetani, Mungu pia anao mawakala Wake miongoni mwa watu wakuu wa nchi. Adui anawasukuma watumishi wake wapendekeze hatua ambazo zingeweza kuzuia kazi ya Mungu; lakini viongozi wa serikali wanaomcha Bwana wanashawishiwa na malaika watakatifu wapinge mapendekezo kama hayo kwa hoja zisizoweza kujibiwa. Kwa njia hiyo watu wachace wanadhibiti mkondo wenye nguvu wa uovu. Upinzani wa maadui wa ukweli utadhibitiwa ili ujumbe wa malaika wa tatu uweze kufanya kazi yake. Wakati onyo la mwisho litakapotolewa, litavuta usikivu wa hawa viongozi wa umma ambao kwa njia yao Bwana anatenda kazi, na baadhi yao watakubali kuonya, na watasimama na watu wa Mungu katika kipindi cha taabu.PKSw 465.2

  Malaika anayejiunga katika utangazaji wa ujumbe wa malaika ataangazia dunia yote kwa utukufu wake. Kazi inayoenea duniani kote na ambayo ina nguvu isiyokuwa ya kawaida imetabiriwa hapa. Vuguvugu la ujio wa pili la miaka ya 1840-44 lilikuwa udhihirisho wenye utukufu wa mamlaka ya Mungu; ujumbe wa malaika wa kwanza ulipelekwa kwa kituo cha umishenari ulimwenguni kote, na katika baadhi ya nchi kulikuwepo shauku ya kidini kubwa kuliko ilivyowahi kushuhudiwa katika nchi yoyote tangu wakati wa Matengenezo ya karne ya kumi na sita; lakini haya yote yatazidiwa na vuguvugu kuu litakalotokea chini ya onyo la mwisho la malaika wa tatu.PKSw 465.3

  Kazi itakuwa kama ile ya Siku ya Pentekoste. Kama “mvua ya vuli” ilivyotolewa, kwa kumwagwa kwa Roho Mtakatifu wakati wa ufunguzi wa injili, kuwezesha kuchipuka kwa mbegu za thamani, kadhalika “mvua ya masika” itatolewa wakati wa kufunga injili kwa ajili ya kukomaza mavuno. “Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi” (Hosea 6:3). “Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie Bwana, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na mvua ya vuli, kama kwanza” (Yoeli 2:23). “Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu.” “Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa” (Matendo 2:17, 21).PKSw 465.4

  Kazi kubwa ya injili itafungwa kwa udhihirisho wa nguvu ya Mungu ambayo siyo chini zaidi ya ile iliyoonekana wakati wa kuifungua. Unabii uliotimizwa katika umwagwaji wa mvua ya vuli wakati wa kufungua injili utatimizwa tena katika umwagwaji wa mvua vya masika wakati wa kufunga injili. Hapa kuna“nyakati za kuburudishwa“ambazo Petro alikuwa akizifikiria aliposema:“Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu” (Matendo 3:19, 20).PKSw 466.1

  Watumishi wa Mungu, nyuso zao zote zikiwa zimeangazwa na kung'arishwa kwa mbaraka wa utakatifu, wataharakisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakiwa na ujumbe kutoka mbinguni. Kwa maelfu ya sauti duniani kote, onyo litatolewa. Miujiza itafanywa, wagonjwa wataponywa, na ishara na maajabu vitaandamana na waaminio. Shetani pia atatenda, kwa maajabu ya uwongo, hata akishusha moto kutoka mbinguni mbele ya watu (Ufunuo 13:13). Hivyo wakazi wa duniani watatakiwa kutoa msimamo wao.PKSw 466.2

  Ujumbe utahubiriwa siyo kwa njia ya kutumia hoja sana bali kwa njia ya ushawishi wa kina wa Roho wa Mungu. Hoja zimekwishawasilishwa. Mbegu zimeshapandwa, na sasa zitachipuka na kuzaa matunda. Machapisho yaliyotawanywa na watenda kazi wa kimishenari yametoa mvuto wake, lakini wengi ambao akili zao ziliguswa walizuiwa kuelewa vizuri ukweli au walizuiwa kuutii ukweli. Sasa miale ya nuru inapenya kila mahali, ukweli unaonekana katika uwazi wake na watoto waaminifu wa Mungu wanakata kamba zilizokuwa zimewashika. Mishikamano ya kifamilia, mahusiano ya kikanisa, havina nguvu ya kuwazuia sasa. Ukweli una thamani kubwa zaidi kuliko mambo yote mengine. Licha ya mawakala ambao wataungana kusimama dhidi ya ukweli, watu wengi watakata shauri kusimama upande wa Bwana.PKSw 466.3

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents