Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 21—Onyo Lililokataliwa

  Katika kuhubiri fundisho la ujio wa pili wa Kristo, William Miller na wenzake walifanya kazi wakiwa na lengo moja tu kuwaamsha watu wajiandae kwa ajili ya hukumu. Walijitahidi kuwaamsha waliodai kuwa wafuasi wa dini wapate tumaini la kweli na waone hitaji lao la uzoefu wa kina wa Kikristo, na walifanya kazi pia kuamsha watu wasioongoka watambue wajibu wao wa toba na uongofu wa haraka kwa Mungu. “Hawakufanya juhudi yo yote ya kujaribu kuongoa watu wajiunge na kundi au madhehebu yo yote ya dini. Hivyo basi walifanya kazi miongoni mwa vikundi vyote na madhehebu yote, pasipo kuingilia utaratibu wao au nidhamu yao”PKSw 287.1

  “Katika kazi zangu zote,” alisema Miller, “Sikuwahi kuwa na shauku au wazo la kuanzisha kanisa jingine tofauti na madhehebu yaliyokuwepo, au kunufaisha kanisa moja kwa kuliathiri jingine. Nilikusudia kuyanufaisha makanisa yote. Niliamini kuwa Wakristo wote wangefurahia kutarajia ujio wa Kristo, na kuwa wale ambao wasingeweza kuona kama mimi nilivyoona wasingeacha kuwapenda wale wambao wangepokea fundisho hili, sikuwahi kufikiri kuwa kungekuwa na haja ya kuwa na mikutano ya ibada tofauti. Lengo mahsusi lilikuwa shauku ya kuongoa watu wote wamtii Mungu, kuutangazia ulimwengu kuhusu hukumu inayokuja, na kuwashawishi wanadamu wenzagu wafanye matayarisho ya mioyo ambayo yatawawezesha kukutana na Mungu wao kwa amani. Idadi kubwa ya wale walioongoka kupitia kazi zangu walijiunga na makanisa mbalimbali yaliyokuwepo.”—Bliss, uk. 328.PKSw 287.2

  Kwa kuwa kazi yake ilikuwa na matokeo ya kuongeza waumini katika makanisa, kwa muda fulani kazi yake ilikubalika sana. Lakini kwa kuwa wachungaji na viongozi wa dini waliamua kupingana na fundisho la marejeo na shauku ya kuzima msukosuko ulioletwa na mada ya marejeo, siyo tu kuwa waliipinga mada hiyo kutokea mimbarani, bali pia waliwakatalia washiriki wasifike kwenye mikutano ambayo mahubiri ya marejeo yalitolewa, au hata wasizungumzie tumaini lao katika mikutano ya kijamii ya kanisa. Hivyo, walioamini walijikuta katika nafasi ya majaribu na mashaka makubwa. Waliyapenda sana makanisa yao na walichukia sana kutengana nayo; lakini walipoona ushuhuda wa neno la Mungu ukikandamizwa na haki yao ya kuchunguza unabii wakinyimwa walihisi kuwa utii kwa Mungu uliwakataza kujisalimisha. Waliotafuta kufungia nje ushuhuda wa neno la Mungu walishindwa kuwatambua kama sehemu ya kanisa la Kristo, “nguzo na msingi wa ukweli” Kwa hiyo, walijihisi kuwa na haki ya kujitenga na makanisa yao ya awali. Katika msimu wa kiangazi cha mwaka 1844 takribani watu hamsini elfu walijiondoa kutoka katika makanisa yao ya awali.PKSw 287.3

  Karibu na wakati kama huu badiliko kubwa lilionekana katika makanisa yaliyo mengi ya Marekani yote. Kulikuwepo kwa muda mrefu ongezeko la pole pole lakini endelevu kufuata matendo na desturi za kidunia, na poromoko sawia la maisha halisi ya kiroho; lakini katika mwaka ule kulikuwepo ushahidi mwingi wa anguko kubwa na la ghafla la kiroho katika makanisa karibu yote nchini Marekani. Wakati hakuna mtu aliyeonekana kuweza kueleza chanzo cha anguko hilo, ukweli wenyewe ulionekana wazi na ulifafanuliwa na vyombo vya habari na wahubiri mimbarani.PKSw 288.1

  Katika mkutano wa wapresbiteri wa Filadelfia, Bwana Barnes, mwandishi wa kitabu cha ufafanuzi wa Biblia kilichotumiwa na watu wengi na ambaye alikuwa mchungaji wa moja ya makanisa makubwa katika jiji lile, “alisema kuwa alikuwa katika uchungaji kwa miaka ishirini, na kamwe, mpaka Meza ya Bwana ya mwisho, aliiendesha bila kupokea waumini zaidi au waliopo kupungua. Lakini sasa hakukuwa na uamsho, hakukuwa na waongofu wapya, hakuna ukuaji katika neema unaoonekana miongoni mwa wale waliodai kuwa Wakristo, na hakuna anayehudhuria mafundisho yake kuzungumzia juu ya wokovu wa roho zao. Kwa sababu ya ongezeko la shughuli, na mustakabali mzuri wa biashara na viwanda, kuna ongezeko kubwa la watu kuipenda dunia. Hivyo ndivyo ilivyo kwa madhehebu mengine yote.”—Congregational Journal, Mei 23, 1844.PKSw 288.2

  Katika mwezi wa Februari wa mwaka ule ule, Profesa Finney wa Chuo cha Oberlin alisema:“Tuna ukweli mbele ya akili zetu, kuwa, kwa jumla, makanisa ya Kiprotestanti ya nchi hii, kwa kweli, ama hayakujali au yalipinga karibu matengenezo yote ya kimaadili ya kizazi kile. Kuna makanisa machache ambayo yana nafuu, ambayo hata hivyo hayatoshi kubadilisha sana uhalisia wa ukweli huo kwa mtazamo wa jumla. Tunao pia ukweli mwingine wa kuunga mkono hoja hii: kutokuwepo mvuto wa uamsho karibu katika makanisa yote. Kutokujali mambo ya kiroho kunatawala karibu mahali pote, na ni kutokujali mambo ya kiroho ni kukubwa mno; hivyo ndivyo magazeti ya kidini ya nchi nzima yanavyoshuhudia.... Katika ujumla wao, washiriki wa kanisa wanazidi kuwa mateka wa mitindo,—wanashikana mikono na watu wasio wacha Mungu katika sherehe za anasa, katika densi, na matamasha ya anasa, n.k Lakini hatuna haja ya kueleza sana mada hii inayoumiza sana. Itoshe kusema kuwa ushahidi mkubwa na mpana sana juu yetu, unaoonesha kuwa makanisa kwa jumla yanazidi kuporomoka kiroho. Yameenda mbali sana na Bwana, Naye Bwana amejiondoa kutoka katika makanisa hayo.” Na mwandishi katika gazeti la Religious Telescope anashuhudia: “Hatujawahi kushuhudia kurudi nyuma kukubwa katika mambo ya dini kama ilivyo sasa. Kwa kweli, kanisa linapaswa kuamka, na kutafuta chanzo cha tatizo hili; kama tatizo la kila mtu anayeipenda Sayuni anavyoliona. Tunapokumbuka matukio ‘machache na ya kati’ ya uongofu wa kweli, na ukosefu wa toba na ugumu wa moyo usio kifani wa wenye dhambi, tunajikuta bila kupenda tukipiga kelele, ‘Je, Mungu amesahau kuwa mwenye rehema? au, Je, mlango wa rehema umefungwa?’”PKSw 288.3

  Hali kama hiyo haiwezi kutokea isipokuwa chanzo chake kiwe ndani ya kanisa lenyewe. Giza la kiroho linalokalia mataifa, linalokalia makanisa na mtu mmoja mmoja, lipo, sio kwa sababu ya kuondoka kwa misaada ya neema ya Mungu bila sababu, bali kwa sababu ya kupuuza au kukataa nuru ya Kiungu kwa upande wa wanadamu. Mfano mzuri wa ukweli huu umewasilishwa katika historia ya Wayahudi wakati wa Kristo. Kwa njia ya kujiweka wakfu kwa ulimwengu na kumsahau Mungu na neno Lake, ufahamu wao ulitiwa giza, mioyo yao ilijazwa udunia na tamaa za mwili. Hivyo hawakujua lolote kuhusu marejeo ya Masihi, na kwa sababu ya kiburi chao na kutokuamini kwao walimkataa Mkombozi. Mungu hata hivyo hakukatilia mbali taifa la Wayahudi na kuwanyima maarifa ya, au fursa ya kushiriki katika, mibaraka ya wokovu. Lakini wale waliokataa ukweli walipoteza shauku ya zawadi ya Mbinguni. “Walilifanya giza kuwa nuru, na nuru kuwa giza,” mpaka nuru iliyokuwa ndani yao ikawa giza; na giza lilikuwa kubwa sana!PKSw 289.1

  Inapatana na sera ya Shetani kuwa watu wabaki na mwonekano wa dini ili mradi tu roho ya uchaji halisi wa Mungu haipo. Baada ya wao kuikataa injili, Wayahudi waliendelea kutekeleza kwa bidii kaida zao za zamani, walitunza kwa uangalifu sana kujitenga kwao na mataifa, ilhali wao wenyewe hawakuweza kukiri kuwa uwepo wa Mungu haukuwa tena ukionekana miongoni mwao. Unabii wa Danieli ulionesha pasipo kukosea wakati wa ujio wa Masihi, na ulitabiri moja kwa moja kifo Chake, kiasi kwamba waliwakatisha tamaa watu wasijifunze unabii huo, na hatimaye marabi walitangaza laana kwa wale wote ambao wangejaribu kukokotoa huo wakati. Katika upofu na moyo usiokuwa na toba watu wa Israeli katika karne zilizofuata walisimama, wakipuuza fursa za neema ya wokovu, bila kujali mibaraka ya injili, na bila kujali onyo kali na la kuogofya la hatari ya kuikataa nuru kutoka mbinguni.PKSw 289.2

  Mahali popote palipo na kisababishi, matokeo yale yale hufuata. Ye yote ambaye, kwa makusudi, anazima ushawishi kuhusu wajibu wake kwa sababu unaingilia matakwa yake hatimaye atapoteza uwezo wa kutofautisha kati ya ukweli na uongo. Ufahamu hujazwa giza, dhamiri huwa sugu, moyo huwa mgumu, na roho hutengwa na Mungu. Mahali ambapo ujumbe wa ukweli wa Mungu umekataliwa au umepuuzwa, pale kanisa linafunikwa na giza; imani na upendo huwa hupungua sana, na utengano na migawanyiko huingia. Washiriki wa kanisa hupeleka shauku na nguvu zao katika utafutaji wa mambo ya kidunia, na wenye dhambi hufanywa kuwa wagumu zaidi katika uasi wao.PKSw 289.3

  Ujumbe wa malaika wa kwanza wa Ufunuo 14, unaotangaza saa ya hukumu ya Mungu na kuwaita watu wamche Mungu na wamwabudu Yeye, umekusudiwa kuwatenga watu wa Mungu na mivuto ya ulimwengu na kuwaamsha ili watambue hali yao hali ya udunia na kurudi nyuma kwao. Katika ujumbe huu, Mungu ametuma kwa kanisa onyo, ambalo, kama lingekubaliwa, lingesahihisha maovu yaliyowatenga Naye. Ikiwa wangepokea ujumbe kutoka mbinguni, wakanyenyekesha mioyo yao mbele za Bwana na kufanya matayarisho ya dhati ili waweze kusimama katika uwepo Wake, Roho na nguvu ya Mungu vingedhihirika miongoni mwao. Kanisa lingeweza tena kufikia ile hali iliyobarikiwa ya umoja, imani, na upendo ambao ulikuwepo katika siku za mitume, ambapo waaminio “walikuwa na moyo mmoja na roho moja,“na“walihubiri neno la Mungu kwa ujasiri,” wakati “Bwana alipoliongeza kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa” (Matendo 4:32, 31; 2:47).PKSw 289.4

  Ikiwa watu wa Mungu wangeipokea nuru kama inavyowaangazia kutoka katika neno la Mungu, wangefikia ule umoja ambao Kristo aliuombea, ule ambao mtume Paulo anauelezea, “umoja wa roho katika kifungo cha amani.” “Kuna,” anasema, “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja” (Waefeso 4:3-5).PKSw 290.1

  Hayo ndiyo yalikuwa matokeo yaliyobarikiwa waliyoyapata wale walioukubali ujumbe wa marejeo. Walitoka katika madhehebu mbalimbali, na vikwazo vyao vya kimadhehebu viliondolewa; imani zilizopingana zilisawazishwa; tumaini lisilokuwa na msingi wa Biblia la miaka elfu moja ya muda mfupi lilitupiliwa mbali, dhana potofu za ujio wa Yesu zilisahihishwa, kiburi na mshikamano kwa ulimwengu viliondolewa kabisa; makosa yaliungamwa; mioyo iliunganishwa katika ushirika mtamu, na upendo na furaha vilikuwa juu. Ikiwa fundisho hili lilileta mambo haya kwa wachache waliolipokea, lingeweza kufanya jambo hilo hilo kwa wote ambao wangelipokea.PKSw 290.2

  Lakini makanisa kwa jumla hayakupokea onyo hilo. Wachungaji wao, ambao, kama walinzi “katika kuta za nyumba ya Israeli,” walipaswa kuwa wa kwanza kutambua ishara za ujio wa Yesu, walishindwa kujifunza ukweli kutoka katika ushuhuda wa manabii au kutoka katika alama za nyakati. Kwa kadiri matumaini na tamaa ya mafanikio ya kidunia yalivyojaza mioyo yao, upendo kwa Mungu na imani katika neno Lake vilipoa; na wakati fundisho la marejeo lilipowasilishwa, liliamsha tu chuki na kutoamini. Ukweli kuwa ujumbe ulikuwa, kwa kiwango kikubwa, ukihubiriwa na walei, ulitumiwa kama zana dhidi ya ujumbe wenyewe. Kama ilivyokuwa katika siku za kale ushuhuda wa wazi wa neno la Mungu ulikutana na swali: “Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo?” Na baada ya kugundua jinsi ilivyokuwa kazi ngumu kukanusha hoja zilizotokana na vipindi vya kiunabii, walipiga marufuku kujifunza unabii, wakifundisha kuwa vitabu vya kiunabii vilikuwa vimetiwa muhuri na visingeweza kueleweka. Watu wengi, kwa kuwaamini wachungaji wao bila maswali, walikataa kusikiliza onyo; na wengine, ingawa walikuwa wameshawishika na kuuamini ukweli, hawakuthubutu kuukiri, wasije “wakatupwa nje ya sinagogi.” Ujumbe ambao Mungu alikuwa ameutuma kwa ajili ya kulipima na kulisafisha kanisa ulidhihirisha wazi kuwa idadi kubwa ya watu ilikuwa imeweka mioyo yao katika mambo ya kidunia kuliko kwa Kristo. Kamba zilizowafungamanisha na ulimwengu zilikuwa na nguvu zaidi ya mivuto ya mbinguni. Walichagua kusikiliza sauti ya hekima ya kidunia na kuupa kisogo ujumbe wa ukweli unaogusa moyo na kuufanya ujihoji.PKSw 290.3

  Kwa kulikataa onyo la malaika wa kwanza, walikataa njia ambayo Mbingu ilikuwa imeleta kwa ajili ya wokovu wao. Walimkataa mjumbe wa neema ambaye angesahihisha maovu yao ambayo yaliwatenga na Mungu, na kwa shauku kubwa zaidi walirudi kutafuta kushikamana na ulimwengu zaidi. Hiki ndicho kilikuwa chanzo cha hali ya kutisha ya udunia, kurudi nyuma, na kifo cha kiroho iliyokuwepo katika makanisa mwaka 1844.PKSw 291.1

  Katika Ufunuo 14 malaika wa kwanza anafuatwa na malaika wa pili anayetangaza: “Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake” (Ufunuo 14:8). Neno “Babeli” linatokana na neno “Babel,” na linamaanisha machafuko. Linatumika katika Maandiko kuelezea namna mbalimbali za dini ya uongo au dini iliyoasi. Katika Ufunuo 17 Babeli imewasilishwa kama mwanamke—kielelezo kinachotumiwa katika Biblia kama alama ya kanisa, mwanamke safi akiwakilisha kanisa safi, mwanamke kahaba akiwakilisha kanisa lililoasi.PKSw 291.2

  Katika Biblia tabia takatifu na inayostahimili ya uhusiano uliopo kati ya Kristo na kanisa Lake imewakilishwa kwa njia ya muungano wa ndoa. Bwana ameunganisha watu Wake na Yeye Mwenyewe kwa njia ya agano thabiti, Yeye akiahidi kuwa Mungu wao, na wao wakiahidi kuwa watu Wake na Wake peke yake. Anatangaza: “Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema” (Hosea 2:19). Na, tena: “Maana mimi ni mume wenu” (Yeremia 3:14). Naye Paulo anatumia kielelezo hicho hicho katika Agano Jipya anaposema: “Naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi” (2 Wakorintho 11:2).PKSw 291.3

  Kanisa linapokosa uaminifu kwa Kristo na kuruhusu imani na upendo kuondoka Kwake, na kukubali upendo kwa mambo ya dunia uujaze moyo, hufananishwa na uvunjaji wa kiapo cha ndoa. Dhambi ya Israeli ya kumwacha Bwana inawasilishwa kwa kielelezo hiki hiki; na upendo wa ajabu wa Mungu ambao waliupuuza umeoneshwa kwa njia inayogusa sana: “Nalikuapia, nikafanya agano nawe, asema Bwana MUNGU, ukawa wangu.” “Nawe ulikuwa mzuri mno, ukafanikiwa hata kufikilia hali ya kifalme. Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kwa sababu ya uzuri wako; kwa maana ulikuwa mkamilifu, kwa sababu ya utukufu wangu niliokutia .... Lakini uliutumainia uzuri wako, ukafanya mambo ya kikahaba kwa sababu ya sifa zako.” “Hakika kama vile mke amwachavyo mumewe kwa hiana, ndivyo mlivyonitenda mimi kwa hiana, Ee nyumba ya Israeli, asema Bwana;” “Mke wa mtu, aziniye! Akaribishaye wageni badala ya mumewe!” (Ezekieli 16:8, 13-15, 32; Yeremia 3:20).PKSw 291.4

  Katika Agano Jipya, lugha inayofanana na hiyo imetumiwa kuelezea Wakristo wanaotafuta urafiki na dunia zaidi kuliko kutafuta kukubaliwa na Mungu. Mtume Yakobo anasema: “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”PKSw 292.1

  Mwanamke (Babeli) wa Ufunuo 17 anaelezewa kuwa “amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake,PKSw 292.2

  kilichojawa na machukizo, na machafu Na katika kipaji cha uso wakePKSw 292.3

  alikuwa na jina limeandikwa, la siri, Babeli mkuu, mama wa makahaba.” Anasema nabii: “Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu” Babeli umeelezwa zaidi kuwa “ni mji ule mkubwa, wenye ufalme juu ya wafalme wa nchi” (Ufunuo 17:4-6, 18). Mamlaka ambayo kwa karne nyingi iliwatawala kiimla wafalme wa nchi za Kikristo ilikuwa Rumi. Rangi ya zambarau na nyekundu, dhahabu na mawe ya thamani na lulu, huchora picha dhahiri ya utukufu na zaidi ya ukuu wa kifalme uliooneshwa na upapa wa Rumi. Na hakuna mamlaka nyingine ambayo ingeweza kutangazwa kuwa “amelewa kwa damu ya watakatifu” kama kanisa ambalo liliwatesa kikatili wafuasi wa Kristo. Babeli inashitakiwa pia kwa kuwa na uhusiano haramu na “wafalme wa dunia” Ilikuwa kwa njia ya kujitenga na Bwana, na kushikamana na upagani, ambapo kanisa la Kiyahudi lilibadilika na kuwa kahaba; na Rumi, kwa kujinajisi kwa jinsi iyo hiyo kwa kutafuta msaada wa mamlaka za kidunia, inapokea hukumu inayofanana na hiyo hiyo.PKSw 292.4

  Babeli unasemwa kuwa “mama wa makahaba.” Mabinti zake lazima wawakilishe makanisa ambayo yanang'ang'ania mafundisho na mapokeo yake, na yanayofuata mfano wake wa kupuuza ukweli na kukubaliwa na Mungu, ili kuunda ushirika haramu na ulimwengu. Ujumbe wa Ufunuo 14, unaotangaza kuanguka kwa Babeli unahusu mashirika ya kidini ambayo awali yalikuwa safi na sasa yamechafuka. Kwa kuwa ujumbe huu unafuata onyo la hukumu, ni lazima unatolewa katika siku za mwisho; kwa hiyo hauwezi kuhusika na Kanisa la Rumi peke yake, kwani kanisa hilo liko katika hali ya kuanguka kwa karne nyingi. Zaidi ya hapo, katika sura ya kumi na nane ya Ufunuo watu wa Mungu wanaitwa watoke Babeli. Kwa mujibu wa andiko hili, wengi wa watu wa Mungu ni lazima bado wako Babeli. Na ni katika mashirika gani ya kidini ambamo kuna sehemu kubwa ya wafuasi wa Kristo kwa sasa? Bila shaka, ni katika makanisa mbalimbali ya imani ya Kiprotestanti. Wakati wa kuzaliwa kwa makanisa haya yalikuwa na msimamo mzuri kwa ajili ya Mungu na ukweli, na mbaraka Wake ulikuwa pamoja nao. Hata ulimwengu usioamini ulilazimika kukiri matokeo bora yaliyofuata upokeaji wa kanuni za injili. Katika maneno ya nabii kwa Israeli: “Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kwa sababu ya uzuri wako; kwa maana ulikuwa mkamilifu, kwa sababu ya utukufu wangu niliokutia, asema Bwana MUNGU.” Lakini walianguka kwa sababu ya shauku ile ile ambayo ilikuwa laana na maangamizi ya Israeli—shauku ya kuiga na kutafuta urafiki na watu wasiomcha Mungu. “Lakini uliutumainia uzuri wako, ukafanya mambo ya kikahaba kwa sababu ya sifa zako” (Ezekieli 16:14, 15).PKSw 292.5

  Mengi ya makanisa ya Kiprotestanti yanafuata mfano wa Rumi wa mshikamano haramu na “wafalme wa dunia”—makanisa ya dola, kwa uhusiano wao na serikali za kiraia; na madhehebu mengine, kwa kutafuta kukubaliwa na ulimwengu. Na neno “Babeli”—machafuko—linaweza kutumiwa kwa madhehebu haya kwa usahihi kabisa, wote wakidai kupata mafundisho yao kutoka katika Biblia, lakini wakiwa wamegawanyika katika vikundi visivyokuwa na idadi, vikiwa na imani na nadharia zinazotofautiana na kupingana sana.PKSw 293.1

  Pamoja na muungano haramu na ulimwengu, makanisa yaliyojitenga na Rumi yanaonesha baadhi ya tabia za Rumi.PKSw 293.2

  Kitabu cha Kanisa Katoliki la Rumi hutoa hoja kuwa “ikiwa Kanisa la Rumi lina hatia ya ibada ya sanamu kuhusiana na watakatifu, binti yake, Kanisa la Uingereza, lina hatia ile ile, kwa kuwa lina makanisa kumi yaliyowekwa wakfu kwa ajili ya Maria na kanisa moja tu ndilo limewekwa wakfu kwa Kristo.”—Richard Challoner, The Catholic Christian Instructed, Preface, ukurasa 21, 22.PKSw 293.3

  Na Dkt. Hopkins, katika“A Treatise on the Millennium,“anasema:“Hakuna sababu ya kufikiri kuwa roho na matendo ya mpinga Kristo ipo katika kanisa linaloitwa kwa sasa Kanisa la Roma peke yake. Makanisa ya Kiprotestanti yana mambo mengi ya mpinga Kristo, na hayajafanya matengenezo kikamilifu na kuacha kabisa ufisadi na uovu.”— Samuel Hopkins, Works, vol. 2, uk. 328.PKSw 293.4

  Kuhusiana na utengano kati ya kanisa la Wapresbiteri na Roma, Dkt. Guthrie ameandika: “Miaka mia tatu iliyopita, kanisa letu, likiwa na Biblia iliyo wazi katika bendera yake, na tamko la hamasa linalosomeka,'Chunguza Maandiko,’ kwenye waraka ulioviringishwa, lilitoka nje ya malango ya Rumi.” Halafu anauliza swali la msingi: “Walitoka Babeli wakiwa safi?”—Thomas Guthrie, The Gospel in Ezekiel, ukurasa 237.PKSw 293.5

  “Kanisa la Uingereza,” anasema Spurgeon, “linaonekana kutafunwa na mfumo wa sakramenti; lakini maboresho yake nayo pia yanaonekana kuwa yamegubikwa na falsafa za kipagani. Wale tuliowatarajia kuleta mambo mema wanageuka mmoja mmoja na kuacha misingi ya imani. Tena na tena, naamini, moyo wa Uingereza umetobolewa-tobolewa na ukafiri wa kutisha unaodiriki kupanda mimbarani na kujiita Ukristo.” Chanzo cha uasi mkuu kilikuwa ni nini? Kanisa liliachaje kwa mara ya kwanza usahili wa injili? Kwa kuiga matendo ya kipagani, ili kuwawezesha wapagani waupokee Ukristo. Mtume Paulo anaeleza kuwa, hata katika siku zake, “siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi” (2 Wathelanike 2:7). Nyakati za uhai wa mitume kanisa lilibaki safi ukilinganisha na nyakati zingine. Lakini “kuelekea sehemu ya mwisho wa karne ya pili karibu makanisa yote yalikuwa yamejenga tabia na muundo mpya; usahili wa awali ulitoweka, na bila kutambua, kwa kadiri wanafunzi wa zamani walivyopumzika katika makaburi yao, watoto wao, pamoja na waongofu wapya, ... walijitokeza na kuleta mwelekeo mpya wa kanisa.”— Robert Robinson, Ecclesiastical Researches, ch. 6, par. 17, uk. 51. Ili kupata waongofu wapya, kiwango cha juu cha imani ya Kikristo kilishushwa chini, na matokeo yake “mafuriko ya upagani, ukitiririka kuingia kanisani, ulibeba na desturi, matendo, na sanamu zake.”—Gavazzi, Lectures, ukurasa 278. Dini ya Kikristo ilipopata ukubali na msaada wa tawala za kidunia, ilipokelewa na watu wengi kwa jina; lakini wakati kwa mwonekano wa nje walikuwa Wakristo, wengi “kwa ndani walibaki wapagani, hususani wakiabudu kwa siri sanamu zao.”—Ibid., ukurasa 278.PKSw 293.6

  Je, mchakato huo huo si umerudiwa-rudiwa karibu katika kila kanisa linalojiita la Kiprotestanti? Kama waasisi, wale waliokuwa na roho ya dhati ya matengenezo, wanapita, watoto na wao huja na “kubuni upya mwelekeo wa kazi” Wakati katika upofu wanashikilia imani ya baba zao na kukataa kupokea nuru yo yote ya kuendeleza walichokiona, watoto wa wanamatengenezo wanaenda mbali kabisa ya unyenyekevu, kujikana nafsi, na kuukataa ulimwengu. Kwa njia hiyo “ule usahili wa kwanza unatoweka” Mafuriko ya ulimwengu, unaotiririka na kuingia ndani ya kanisa, huja “na desturi, matendo, na sanamu zake.”PKSw 294.1

  Ndiyo, kiwango cha ule urafiki na ulimwengu ambao ni “uadui na Mungu,“unaopaliliwa sasa miongoni mwa wanaodai kuwa wafuasi wa Kristo kinatisha kiasi gani! Ni kwa idadi kubwa kiasi gani makanisa mashuhuri katika ulimwengu wote wa Kikristo yameacha kiwango cha Biblia cha unyenyekevu, kujikana nafsi, usahili, na utauwa! John Wesley alisema, akizungumzia juu ya matumizi mazuri ya pesa: “Usitumie vibaya sehemu yo yote ya talanta yako yenye thamani, kwa ajili ya kuridhisha tamaa yako ya macho, kwa nguo nzuri au bei kubwa kupita kiasi, au kwa mapambo yasiyokuwa ya lazima. Usitumie vibaya sehemu ya pesa yako kwa ajili ya kupamba nyumba zenu; kwa ajili ya samani nzuri au za gharama kupita kiasi; kwa picha za gharama kubwa, mchoro, au mapambo.... Usitoe chochote kwa ajili ya kuridhisha kiburi cha uzima, kuwafanya watu wakuone ni mtu mwenye uwezo mkubwa au ili watu wakusifie....PKSw 294.2

  ' Ili mradi unatenda wema kwa jinsi uanvyoona mwenyewe, watu watasema mema juu yako.’ Ili mradi wewe ‘unavaa nguo za zambarau na kitani safi,’ na unakula ‘vizuri kila siku,’ bila shaka wengi watasifia umaridadi wako, ukarimu na upendo wako. Lakini usikubali sifa zao nzuri. Badala yake ridhika na heshima inayotoka kwa Mungu.”—Wesley, Works, Sermon 50, “The Use of Money.” Lakini katika makanisa mengi ya wakati huu fundisho kama hili linapuuzwa.PKSw 294.3

  Tabia ya watu kukiri kufuata dini imekuwa jambo la kawaida ulimwenguni sasa. Watawala, wanasiasa, wanasheria, madaktari, wafanyabiashara, hujiunga na kanisa kama njia ya kupata heshima na kuaminiwa na jamii, na kupata maslahi yao ya kidunia. Kwa njia hiyo wanatafuta kufunika miamala yao ya udhalimu chini ya mwavuli wa Ukristo. Mashirika mbalimbali ya kidini, kwa msaada wa matajiri na mvuto wa watu dunia waliobatizwa, yanaongeza juhudi zao ili kupata umaarufu na udhamini mkubwa zaidi. Makanisa ya kifahari, yaliyopambwa kwa umaridadi mkubwa sana, yanajengwa kando kando ya barabara mashuhuri. Waabudu wanavalia nguo za gharama kubwa na za mitindo ya kisasa. Mshahara mkubwa unatolewa kwa mchungaji mwenye talanta ili kuwaburudisha na kuwavutia watu. Mahubiri yake hayapaswi kugusa dhambi zinazopendwa na watu, lakini yanapaswa yawe laini na yanayopendeza kwa ajili ya wasikilizaji wa kisasa. Kwa njia hiyo wenye dhambi wa kisasa wanaandikwa majina yao katika kumbukumbu za kanisa, na dhambi za kisasa zinafichwa chini ya vazi la uchaji Mungu wa kuigiza.PKSw 294.4

  Likitoa ufafanuzi juu ya mtazamo wa sasa wa wale wanaodai kuwa Wakristo kwa ulimwengu, jarida mashuhuri lisilokuwa la kidini lilisema: “Bila kujua kanisa linaongozwa na roho ya kizazi hiki, na limeiga mifumo ya kizazi hiki ya ibada ili kukidhi matakwa ya kisasa.” “Mambo yote, kwa kweli, yanayosaidia kuifanya dini ivutie, kanisa sasa linayatumia kama nyenzo zake.” Na mwandishi katika jarida la New York Independent anasema hayo hayo juu ya Umethodisti kama ulivyo: “Msitari unaogawa katikati ya wacha Mungu na wasio na dini unafifia na kuwa kama kivuli cha aina fulani, na watu wenye bidii pande zote wanafanya kazi kwa bidii ili kuondoa tofauti zote katika mbinu zao za kazi na burudani.” “Umashuhuri wa dini una mwelekeo wa kuongeza sana idadi ya wale wanaoweza kupata manufaa yake bila kutekeleza majukumu yake.”PKSw 295.1

  Howard Crosby alisema: “Ni jambo la kusikitisha sana kuwa tunaliona kanisa la Kristo likitekeleza kidogo sana mipango ya Bwana wake. Kama vile Wayahudi wa zamani walivyoruhusu ushirikiano wao wa kawaida na mataifa walioabudu sanamu uibe mioyo yao kutoka kwa Mungu, ... kadhalika, kanisa la Yesu sasa, kwa mahusiano ya uongo na ulimwengu usioamini, linaacha mbinu za Mungu za maisha yake ya kweli, na linafuata tabia za jamii isiyokuwa na Kristo ambazo ni za uovu, japokuwa zinaonekana kuwa za busara, kwa kutumia hoja na kufikia mahitimisho ambayo hayapatani na neno la Mungu, na yakipingana na ukuaji wote katika neema.”—The Healthy Christian: An Appeal to the Church, ukurasa 141, 142.PKSw 295.2

  Katika mkondo huu wa mambo ya kidunia na usakaji wa anasa, kujikana nafsi na kujitolea binafsi kwa ajili ya Kristo vimetoweka kwa kiwango kikubwa. “Baadhi ya wanaume na wanawake sasa wanaojishirikisha katika makanisa yetu walifundishwa, wakiwa watoto, kujinyima ili kuweza kutoa au kufanya kitu fulani kwa ajili ya Kristo.” Lakini “ikiwa fedha zinatakiwa sasa, ... hakuna mtu anayeitwa atoe. La, hapana! Itisha tamasha, maonesho, maigizo, mauzo ya vyakula vya zamani, au kitu fulani cha kula—kitu chochote cha kuwachekesha watu.”PKSw 295.3

  Gavana Washburn wa Wisconsin, katika ujumbe wake wa kila mwaka, wa Januari 9, 1873, alieleza kuwa: “Sheria fulani inaonekana kuhitajika ili kuvunja shule ambazo zinazalisha wacheza kamari. Shule hizi zipo kila mahali. Hata kanisa (bila kujua, bila shaka) nyakati zingine linajikuta likifanya kazi ya Shetani. Maonyesho ya muziki ya zawadi, biashara na kamari za zawadi, nyakati zingine kwa kusudi la kutekeleza malengo ya kidini au msaada, lakini mara nyingi kwa makusudi yasiyofaa sana, bahati nasibu, vifurushi vya zawadi, nk., zote ni nyenzo za kupatia fedha pasipo thamani iliyopatikana. Hakuna jambo linaloharibu maadili au linalolewesha, hususani kwa vijana, kama kupata pesa au mali bila kufanya kazi. Watu wenye hadhi wanaojihusisha katika biashara hizi, na kutuliza dhamiri zao kwa kufikiri kuwa pesa inakwenda kutekeleza kusudi jema, siyo ajabu kuwa vijana wa taifa wanajikuta mara nyingi wakiangukia katika tabia za msisimko wa michezo ya hatari ambayo kwa kiwango kikubwa huisababisha kwa hakika.”PKSw 295.4

  Roho ya kupatana na ulimwengu inapenya ndani ya makanisa yote ya ulimwengu wa Kikristo. Robert Atkins, katika hubiri alilohubiri jijini London, anachora picha ya anguko la kiroho lililoko katika nchi ya Uingereza: “Wacha Mungu wa kweli wanatoweka duniani, na hakuna mtu anayejali, katika kila kanisa, kuna watu wanaopenda ulimwengu, wanaopatana na ulimwengu, wanaopenda faraja ya kiumbe, na wanaotafuta kukubalika. Wameitwa kuteseka na Kristo, lakini wanaogopa kuaibika.... Uasi, uasi, uasi, umechorwa mbele ya kila kanisa; na laiti wangelijua hilo, na laiti wangelihisi hilo, kungekuwa na tumaini; lakini, ala! Wanapiga kelele, ‘Sisi ni matajiri, tumejitajirisha, wala hatuna haja ya kitu.'”—Second Advent Library, tract No. 39.PKSw 296.1

  Dhambi kubwa ambayo Babeli unashitakiwa nayo ni kuwa Babeli uliwanywesha “mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.” Hiki kikombe cha mvinyo ambacho Babeli unawapa watu wa ulimwengu huwakilisha mafundisho ya uongo ambayo ameyapata kama matokeo ya mshikamano haramu na wakuu wa dunia. Urafiki wa kanisa na dunia hunajisi imani ya kanisa, na matokeo yake kanisa huwa na mvuto unaonajisi ulimwengu kwa kufundisha mafundisho yaliyo kinyume na mafundisho ya wazi ya Maandiko Matakatifu.PKSw 296.2

  Rumi ilificha Biblia isisomwe na watu na liliwataka watu wote wayapokee mafundisho yake badala ya Biblia. Ilikuwa kazi ya Matengenezo kuwarudishia watu neno la Mungu; lakini siyo kweli kuwa katika makanisa ya wakati wetu watu wanafundishwa kujenga imani yao katika matamko yao ya imani na mafundisho ya kanisa kuliko Maandiko? Charles Beecher alisema, akizungumza kuhusu makanisa ya Kiprotestanti: “Wanachukia wakati neno baya linaposemwa dhidi ya imani yao kwa hisia kali kama zile za mababa watakatifu wanavyochukia wakati neno linalokosoa lilipotamkwa dhidi ya ibada ya watakatifu na wafia dini.... Madhehebu ya Waprotestanti wa Kiinjiisti yameshikamana sana wao kwa wao kiasi kwamba, mtu ye yote miongoni mwao, hawezi kuwa mhubiri kabisa, mahali popote, asipokubali kitabu fulani kando ya Biblia.... hakuna kitu cha kufikirika katika kauli kuwa nguvu ya mfumo wa imani inaanza kuzuia Biblia kwa hakika kama vile Rumi ilivyofanya, japo kwa njia ya hila zaidi.”—Sermon on “The Bible a Sufficient Creed,” delivered at Fort Wayne, Indiana, Feb. 22, 1846.PKSw 296.3

  Wakati waalimu waaminifu wanapoeleza neno la Mungu, wanainuka watu wasomi, wachungaji wanaojidai kuelewa Maandiko, wanaokataa mafundisho sahihi kama uzushi, na hivyo wanarudisha nyuma juhudi za kuutafuta ukweli. Kama ulimwengu ungekuwa haujanyweshwa mvinyo wa Babeli, watu wengi wangeshawishika na kuongolewa na ukweli ulio wazi, unaokata wa neno la Mungu. Lakini imani ya kidini inaonekana kuwa imechafuka mno na kuwa na mambo mengi yanayopingana kiasi kwamba watu hawajui ni jambo lipi la kuamini kama ukweli. Dhambi ya kutotubu kwa ulimwengu inalala katika mlango wa kanisa.PKSw 297.1

  Ujumbe wa malaika wa pili wa Ufunuo 14 ulihubiriwa kwa mara ya kwanza katika msimu wa kiangazi cha mwaka 1844, na wakati ule ulihusu moja kwa moja zaidi makanisa ya Marekani, ambapo onyo la hukumu lilikuwa limehubiriwa katika maeneo mengi na kukataliwa na watu walio wengi, na mahali ambapo hali ya kurudi nyuma katika makanisa ilikuwa ya haraka zaidi kuliko maeneo mengine. Lakini ujumbe wa malaika wa pili haukufikia utimizwaji wake kikamilifu mwaka 1844. Makanisa wakati ule yalipata anguko la uadilifu, kama matokeo ya kukataa kwao nuru ya ujumbe wa marejeo; lakini anguko lile halikuwa kamili. Na kwa kadiri yalivyoendelea kukataa ukweli maalumu kwa ajili ya wakati huu yameendelea kuanguka chini na chini zaidi. Lakini, hata hivyo, haiwezi kusemwa kuwa “Umeanguka Babeli,... maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.” Bado Babeli hajawafanya mataifa yote yafanye hivyo. Roho ya kushikamana na ulimwengu na kupuuza ukweli unaopima wa wakati wetu ipo na inaendelea kuota mizizi katika makanisa ya imani ya Kiprotestanti katika nchi zote za Ukristo; na makanisa haya yamejumuishwa katika onyo kali na kutisha la malaika wa pili. Lakini kazi ya uasi bado haijafikia kipeo chake.PKSw 297.2

  Biblia inatangaza kuwa kabla ya kuja kwa Bwana, Shetani atatenda “kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu;” na kwamba wale ambao “hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa,” wataachwa wapokee “nguvu ya upotevu, wauamini uongo” (2 Wathesalonike 2:9-11). Ni mpaka hali hii itakapofikiwa, na muungano wa kanisa na ulimwengu utakapokamilika katika ulimwengu wote wa Ukristo, ndipo anguko la Babeli litakapokamilika. Badiliko ni la hatua kwa hatua, na utimizo wa Ufunuo 14:8 bado ni wa wakati ujao.PKSw 297.3

  Licha ya giza la kiroho na utengano na Mungu ulioko katika makanisa yanayounda Babeli, kundi kubwa la wafuasi wa kweli wa Kristo bado wapo katika ushirika wao. Kuna wengi wao ambao hawajaona ukweli maalumu wa wakati huu. Siyo wachache ambao hawajaridhika na hali yao ya sasa na watamani nuru iliyo wazi zaidi. Wanaangalia sura ya Kristo katika makanisa yaliyo na ushirika wao bila mafanikio. Na makanisa haya yanavyozidi kwenda mbali na ukweli zaidi, na kujiungamanisha kwa karibu zaidi na ulimwengu, tofauti kati ya makundi mawili itakuwa kubwa zaidi, na hatimaye watatengana. Wakati utafika ambapo wale wanaompenda Mungu kweli kweli hawataendelea kuwa na mshikamano na wale “wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; walio na mfano wa utauwa, lakini wakiikana nguvu yake.”PKSw 297.4

  Ufunuo 18 huelezea wakati ambapo, kama matokeo ya kukataa onyo lenye sehemu tatu la Ufunuo 14:6-12, kanisa litakuwa limefikia kikamilifu hali iliyotabiriwa na malaika wa pili, na watu wa Mungu ambao watakuwa bado katika Babeli wataitwa watoke katika ushirika wake. Ujumbe huu ni wa mwisho kutolewa ulimwenguni; na utatimiza kazi yake. Wakati wale ambao“hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu” (2 Wathesalonike 2:12), wataachwa wapokee uongo mkubwa zaidi na watauamini uongo, ndipo nuru ya ukweli itawaangazia wale ambao mioyo yao iko wazi kuupokea, na watoto wote wa Bwana ambao bado katika Babeli wataisikia sauti: “Tokeni kwake, Enyi watu wangu” (Ufunuo 18:4). PKSw 298.1

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents