Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 23—Patakatifu ni Nini?

  Andiko ambalo juu ya yote mengine limekuwa msingi na nguzo kuu ya imani ya marejeo lilikuwa tamko hili: “Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa” (Danieli 8:14). Haya ni maneno yaliyojulikana sana kwa wote walioamini ujio wa haraka wa Bwana. Katika midomo ya maelfu ya watu unabii huu ulikaririwa kama kauli mbiu ya imani yao. Wote walihisi kuwa juu ya matukio yaliyotabiriwa katika aya hii ndipo kulikuwa na matarajio na matumaini waliyojivunia. Siku hizi za kiunabii zilionekana kuishia wakati wa vuli ya mwaka 1844. Kama ulimwengu wote wa Wakristo ulivyoamini, Waadventista wa wakati ule waliaamini kuwa dunia, au sehemu yake fulani, ilikuwa patakatifu. Walielewa kuwa kutakaswa kwa patakatifu kulikuwa kusafisha dunia kwa moto wa siku kuu ya mwisho, na kuwa hili lingetokea wakati wa ujio wa pili wa Kristo. Ndiyo maana wakafikia hitimisho kuwa Kristo angerudi duniani 1844.PKSw 313.1

  Lakini wakati uliopangwa ulipita, na Bwana hakutokea. Waumini walijua kuwa neno la Mungu halikosei; tafsiri yao ya unabii ndiyo inapaswa kuwa na makosa; lakini ni wapi palikuwa na makosa? Wengi walifanya haraka kukata fundo la matatizo kwa kukataa kuwa siku 2300 hazikuishia mwaka 1844. Hakuna sababu ambayo ilitolewa kwa ajili ya hili isipokuwa kwamba Kristo hakuja kwa wakati waliomtarajia. Walitoa hoja kuwa kama siku za kiunabii ziliishia mwaka 1844, Kristo angekuja kutakasa patakatifu kwa kuisafisha dunia kwa moto; na kwamba kwa kuwa hakuja, siku zilikuwa bado hazijaisha.PKSw 313.2

  Kukubali hitimisho hili kulimaanisha kukanusha ukokotoaji wa awali wa vipindi vya kiunabii. Siku 2300 zilionekana kuanzia wakati amri ya Artashasta ya kuujenga upya Yerusalemu ilipotekelezwa wakati wa vuli ya mwaka 457 K.K. Kwa kuchukua wakati huu kama mahali pa kuanzia, kulikuwa na mwafaka kamili katika kutumia matukio yaliyotabiriwa katika maelezo ya kipindi kinachotajwa katika Danieli 9:25-27. Majuma sitini na tisa, miaka 483 ya kwanza katika kipindi cha miaka 2300, yalipaswa kuishia kwa Masihi, Mpakwa Mafuta; na ubatizo wa Kristo na kupakwa mafuta na Roho Mtakatifu, mwaka, 27 B.K, vilitimiza kikamilifu unabii. Katikati ya juma la saba, Masihi alipaswa kukatiliwa mbali. Miaka mitatu na nusu baada ya ubatizo Wake, Kristo alisulubishwa, wakati wa masika wa mwaka 31 B.K. Majuma sabini, au miaka 490, ilitengwa kwa ajili ya Wayahudi. Mwishoni mwa kipindi hiki taifa lilitia muhuri kumkataa kwao Kristo kwa kuwatesa wanafunzi Wake, na mitume waliwageukia Mataifa, mwaka 34 B.K. Miaka 490 ya kwanza kati ya miaka 2300 ikiwa imekwisha, miaka 1810 ilikuwa imebaki. Tangu mwaka 34 B.K. miaka 1810 inaishia mwaka 1844. “Ndipo,” alisema malaika, “patakatifu patakapotakaswa.” Vipengele vyote vinavyotangulia vya unabii vilitimizwa pasipo shaka yo yote kwa wakati uliopangwa.PKSw 313.3

  Kwa ukokotoaji huu, yote yalikuwa wazi na yaliafikiana, isipokuwa halikuonekana tukio lo lote lililotimiza utakaswaji wa patakatifu likitokea mwaka 1844. Kukataa kuwa siku ziliishia wakati ule ilikuwa kuingiza unabii wote katika machafuko, na kukanusha hadharani misimamo yote iliyokuwa imewekwa kwa utimizo usio na mashaka wa matukio mbalimbali ya kiunabii.PKSw 314.1

  Lakini Mungu aliwaongoza watu Wake katika vuguvugu la marejeo; nguvu na utukufu Wake viliambatana na kazi, na asingeruhusu iishie gizani na kukata tamaa, idhihakiwe kama msisimko wa uongo na ushikiliaji sana mambo bila kutumia akili. Asingeruhusu neno Lake libaki katika mashaka na bila mwelekeo. Ingawa wengi waliachana na ukokotoaji wa awali wa vipindi vya kiunabii na kukataa usahihi wa vuguvugu lililojengwa juu yake, wengine hawakuwa tayari kukana vipengele vya imani na uzoefu uliokuwa na ushahidi wa Maandiko na ushuhuda wa Roho wa Mungu. Waliamini kuwa walitumia kanuni sahihi za kutafsiri Maandiko katika kujifunza kwao unabii, na kwamba ilikuwa wajibu wao kuhifadhi ukweli uliokwishapatikana, na kuendelea na jukumu la uchunguzi wa Biblia. Kwa maombi ya dhati walihakiki misimamo yao na walijifunza Maandiko ili wagundue kosa lao. Kwa kushindwa kuona kosa lao katika ukokotoaji wa vipindi vya kiunabii, walivutwa kuchunguza kwa makini somo la patakatifu.PKSw 314.2

  Katika uchunguzi wao waligundua kuwa hakuna ushahidi wa kimaandiko uliounga mkono wazo lililoaminiwa na wengi kuwa dunia ni patakatifu; lakini walipata katika Biblia maelezo kamili kuhusu somo la patakatifu, asili yake, mahali, na huduma zake; ushuhuda wa waandishi watakatifu ukiwa wazi na wa kutosha kiasi cha kuweka suala hilo katika nuru kamili isiyokuwa na swali lo lote. Mtume Paulo, katika Waraka kwa Waebrania, anasema: “Basi hata agano la kwanza lilikuwa na kawaida za ibada, na patakatifu pake, pa kidunia. Maana hema ilitengenezwa, ile ya kwanza, mlimokuwa na kinara cha taa, na meza, na mikate ya Wonyesho; ndipo palipoitwa, Patakatifu. Na nyuma ya pazia la pili, ile hema iitwayo Patakatifu pa patakatifu, yenye chetezo cha dhahabu, na sanduku la agano lililofunikwa kwa dhahabu pande zote, mlimokuwa na kopo la dhahabu lenye ile mana, na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya agano; na juu yake makerubi ya utukufu, yakikitia kivuli kiti cha rehema” (Waebrania 9:1-5).PKSw 314.3

  Patakatifu panaporejelewa na Paulo ilikuwa hema iliyojengwa na Musa kwa amri ya Mungu kama mahali pa makazi ya duniani Yake Yeye Aliye Juu Sana. “Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao” (Kutoka 25:8), likuwa agizo lililotolewa kwa Musa wakati akiwa mlimani na Mungu. Waisraeli walikuwa wakisafiri kupitia jangwani, na hema lilijengwa kwa namna ambayo lingeweza kuhamishwa kutoka sehemu moja kusimikwa sehemu nyingine; lakini lilikuwa banda kubwa lenye utukufu mwingi. Kuta zake zilikuwa mbao zilizosimama wima zilizopakwa dhahabu nyingi na kuchomekwa katika soketi ya fedha, wakati paa lilitengenezwa kwa mfuatano wa mapazia, au vifuniko—vya nje vilikuwa vya ngozi, vya ndani vilikuwa vya kitani safi iliyochorwa picha nzuri za makerubi. Kando ya uwanja wa nje, ambao ulikuwa na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, hema lenyewe ambalo liliundwa na vyumba viwili vilivyoitwa patakatifu na patakatifu pa patakatifu, vilivyotenganishwa kwa pazia la thamani kubwa na zuri, au kifuniko; pazia kama hilo lilifunga lango la kuingilia katika chumba cha kwanza.PKSw 314.4

  Ndani ya patakatifu kulikuwa na kinara cha taa, upande wa kusini, kikiwa na taa saba zilizotoa mwanga kwa ajili ya patakatifu mchana na usiku; upande wa kaskazini kulikuwepo meza ya mikate ya wonyesho; na mbele ya pazia linalogawanya patakatifu na patakatifu pa patakatifu kulikuwa na madhabahu ya dhahabu ya uvumba, ambapo wingu la harufu nzuri likiwa na maombi ya Waisraeli, lilitokea hapo na kupanda kila siku mbele ya Mungu.PKSw 315.1

  Ndani ya patakatifu pa patakatifu lilisimama sanduku la agano, kasha lililotengenezwa kwa mbao za thamani kubwa na kupakwa dhahabu, hifadhi ya mbao mbili za mawe ambazo juu yake Mungu aliandika sheria ya Amri Kumi. Juu ya sanduku, na kikiwa sehemu ya sanduku takatifu, kulikuwa na kiti cha rehema, kilichotengenezwa kwa ufundi wa hali ya juu, kikiwa kimefunikwa na makerubi wawili, mmoja akiwa kila upande, na wote wawili wakiwa wametengenezwa kwa dhahabu ngumu. Katika chumba hiki uwepo wa Kimungu ulidhihirishwa kwa wingu la utukufu katikati ya makerubi.PKSw 315.2

  Baada ya Waebrania kuanza maisha nchini Kanaani, hema liliachwa na badala yake hekalu la Sulemani lilitumika, ambalo, japokuwa lilikuwa jengo la kudumu na kubwa zaidi, lilijengwa kwa uwiano ule ule, na lilikuwa na samani za aina ile ile. Katika muundo huu hekalu lilidumu kuwepo— isipokuwa likiwa limebomolewa wakati wa Danieli—mpaka lilipoharibiwa na Warumi, mwaka 70 B.K.PKSw 315.3

  Tukirudi tena katika kitabu cha Waebrania, watafutaji wa ukweli waligundua kuwa uwepo wa patakatifu pa pili, au patakatifu pa agano jipya, umedokezwa katika maneno ya Paulo yaliyonukuliwa awali: “Basi hata agano la kwanza lilikuwa na kawaida za ibada, na patakatifu pake, pa kidunia“Na matumizi ya neno“pia“kunaashiria kuwa Paulo ameshataja kabla juu ya patakatifu hapa. Tukirudi nyuma mwanzoni mwa sura inayotangulia, tunasoma: “Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu” (Waebrania 8:1, 2).PKSw 315.4

  Hapa pamefunuliwa patakatifu pa agano jipya. Patakatifu pa agano la kwanza paliwekwa na mwanadamu; palijengwa na Musa; lakini patakatifu pa agano jipya pamewekwa na Bwana, siyo mwanadamu. Katika patakatifu pa duniani makuhani wa kibinadamu waliendesha huduma zake; katika patakatifu pa agano jipya, Kristo, Kuhani wetu Mkuu, anahudumu akiwa mkono wa kulia wa Mungu. Patakatifu pa kwanza palikuwa duniani, patakatifu pa pili pako mbinguni.PKSw 316.1

  Zaidi ya hapo, hema lililojengwa na Musa liliundwa kwa kufuata mfano. Bwana alimwelekeza Musa: “Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyovifanya.” Na tena agizo lilitolewa, “Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, ulioonyeshwa mlimani” (Kutoka 25:9, 40). Na Paulo anasema kuwa hema ya kwanza “ndiyo mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa,” lakini mahali pake patakatifu palikuwa “nakala za mambo yaliyo mbinguni;” kwamba makuhani waliotoa zawadi kulingana na sheria walihudumu kama “mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni,” na kuwa “Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu” (Waebrania 9:9, 23; 8:5; 9:24).PKSw 316.2

  Patakatifu pa mbinguni, ambapo Yesu anahudumu kwa ajili yetu, ndipo patakatifu pakuu halisi, ambapo patakatifu palipojengwa na Musa palikuwa nakala. Mungu aliweka Roho Wake juu ya wajenzi wa hekalu la duniani. Stadi za kisanaa zilizooneshwa katika ujenzi wake zilikuwa udhihirisho wa hekima ya Kimungu. Kuta zilikuwa na mwonekano wa bonge kubwa la dhahabu, zikiakisi kila upande mwanga wa taa saba za kinara cha dhahabu cha taa. Meza ya mikate ya wonyesho na madhabahu ya uvumba vilimeremeta kama dhahabu safi. Pazia la kifahari lililofanya kazi kama dari, lililokuwa limechorwa picha za malaika kwa rangi ya bluu na zambarau na nyekundu liliongezea uzuri wa mandhari. Na ng'ambo ya pazia la pili kulikuwa na Shekina takatifu, udhihirisho unaoonekana wa utukufu wa Mungu, ambapo ni kuhani mkuu peke yake angeweza kuingia na kuendelea kuishi.PKSw 316.3

  Utukufu usiokuwa na mfano wa hema ya duniani ulimwonesha mwanadamu utukufu wa hekalu la mbinguni ambapo Kristo mtangulizi wetu anahudumu kwa ajili yetu mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Mahali pa kudumu pa Mfalme wa wafalme, mahali ambapo maelfu mara elfu wanamhudumia, na kumi elfu mara kumi elfu wanasimama mbele Zake (Danieli 7:10); hekalu lile, likiwa limejazwa kwa utukufu wa kiti cha enzi cha milele, mahali ambapo maserafi, walinzi wake wanaong'aa, hufunika nyuso zao katika kicho, ndipo lilipo, jengo lenye utukufu wa juu sana ambalo halijawahi kutengenezwa na mikono ya wanadamu, bali nuru yake iliyoakisiwa kwa uhafifu ya ukubwa na utukufu wake. Pamoja na hayo ukweli muhimu kuhusu patakatifu pa mbinguni na kazi inayoendeshwa pale kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu vilifundishwa kupitia patakatifu pa duniani na huduma zake. Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu,PKSw 317.1

  Sehemu mbili za patakatifu pa mbinguni zimewakilishwa na vyumba viwili katika patakatifu pa duniani. Wakati Yohana alipopewa fursa ya kuona hekalu la Mungu la mbinguni katika njozi, aliona pale “taa saba za moto zikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi” (Ufunuo 4:5). Alimwona malaika “mwenye chetezo cha dhahabu, akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi” (Ufunuo 8:3). Hapa nabii aliruhusiwa kuona chumba cha kwanza cha patakatifu mbinguni; na aliona pale “taa saba za moto” na “madhabahu ya dhahabu,“vilivyowakilishwa na kinara cha taa cha dhahabu na madhabahu ya uvumba katika patakatifu pa duniani. Tena, “hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa” (Ufunuo 11:19), na akatazama ndani ya pazia, ndani ya patakatifu pa patakatifu. Hapa aliona “sanduku la Agano Lake,” lililowakilishwa na sanduku takatifu lililojengwa na Musa ili kuhifadhia sheria ya Mungu.PKSw 317.2

  Hivyo, wale waliokuwa wakijifunza somo hili walipata uthibitisho usiopingika wa uwepo wa patakatifu pa mbinguni. Musa alijenga patakatifu pa duniani kwa kufuta mfano aliooneshwa. Paulo anafundisha kuwa mfano ule ulikuwa patakatifu halisi pa mbinguni. Na Yohana anashuhudia kuwa aliliona mbinguni.PKSw 317.3

  Ndani ya hekalu la mbinguni, makazi ya Mungu, kiti Chake cha rehema kimeimarishwa katika haki na hukumu. Ndani ya patakatifu pa patakatifu sheria Yake, mwongozo mkuu wa haki ambao kwa huo binadamu wote wanapaswa kupimwa. Sanduku linalohifadhi mbao za sheria limefunikwa kwa kiti cha rehema, ambacho mbele yake Kristo anasihi kwa njia ya damu Yake kwa niaba ya mwenye dhambi. Kwa njia hiyo umewakilishwa muungano wa haki na rehema katika mpango wa ukombozi wa mwanadamu. Muungano huu, hekima isiyo na kikomo pekee ndiyo ingeweza kuubuni na nguvu isiyokuwa na kikomo pekee ndiyo ingeweza kuutekeleza; ni muungano unaojaza mbingu yote kwa mshangao na kuabudu. Makerubi wa patakatifu pa duniani, kwa kutazama chini kwa kicho juu ya kiti cha rehema, huwakilisha shauku ambayo malaika wa mbinguni huwa wanakuwa nayo wanapotafakari kuhusu kazi ya ukombozi. Hii ndiyo siri ambayo malaika wanatamani kuielewa—kwamba Mungu anaweza kuwa mwenye haki na wakati huo huo amhesabie haki mwenye dhambi anayetubu na kurudisha uhusiano Wake na jamii ya wanadamu walioanguka; kwamba Kristo aliweza kushuka chini kuinua idadi ya watu isiyo na hesabu kutoka katika shimo la uharibifu na kuwavika mavazi yasiyokuwa na doa ya haki Yake ili awaunganishe na malaika ambao hawakuwahi kuanguka na wanaoishi daima mbele za Mungu.PKSw 317.4

  Kazi ya Kristo kama mwombezi wa mwanadamu imewakilishwa katika ule unabii mzuri wa Zekaria kumhusu Kristo “ambaye jina lake ni Chipukizi.” Nabii anasema: “Yeye atalijenga hekalu la Bwana; naye atauchukua huo utukufu; ataketi akimiliki katika kiti chake cha enzi; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi; na shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili” (Zekaria 6:12, 13).PKSw 318.1

  “Yeye atalijenga hekalu la Bwana.” Kwa njia ya kafara Yake na upatanisho Wake, Kristo ni msingi na mjenzi wa kanisa la Mungu. Mtume Paulo anamwelezea kama “jiwe kuu la pembeni; Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana: Katika yeye ninyi,” anasema, “mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho” (Waefeso 2:20-22).PKSw 318.2

  “Atauchukua huo utukufu.” Kwa Kristo kuna utukufu wa ukombozi kwa jamii ya binadamu iliyoanguka. Katika zama zote za milele, wimbo wa walionunuliwa utakuwa: “Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, ... utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele” (Ufunuo 1:5, 6).PKSw 318.3

  Yeye “ataketi na kutawala juu ya kiti Chake cha enzi; na atakuwa kuhani juu ya kiti Chake cha enzi.” Siyo sasa “juu ya kiti cha enzi cha utukufu Wake;” ufalme wa utukufu bado haujawadia. Ni mpaka kazi Yake kama Mpatanishi ifike mwisho ndipo Mungu “atampa kiti cha enzi cha Daudi baba Yake,” ufalme ambao “hautakuwa na mwisho” (Luka 1:32, 33). Kama kuhani, Kristo ameketi na Baba Yake katika kiti Chake cha enzi (Ufunuo 3:21). Juu ya kiti cha enzi pamoja na Yule ambaye ni wa milele, aliye na uwepo Wake Mwenyewe Ndiye “aliyachukua masikitiko yetu, na kuzibeba huzuni zetu,” ambaye “alijaribiwa katika mambo yote kama tujaribiwavyo, lakini hakutenda dhambi,” ili aweze “kuwasaidia wanaojaribiwa.” “Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba” (Isaya 53:4; Waebrania 4:15; 2:18; 1 Yohana 2:1). Maombezi Yake ni yale ya mwili uliochomwa mikuki na uliovunjika, ya maisha yasiyokuwa na doa. Mikono iliyochubuliwa, ubavu uliochomwa mkuki, nyayo zilizoharibiwa, vinasihi kwa ajili ya mwanadamu aliyeanguka, ambaye ukombozi wake ulinunuliwa kwa gharama isiyokadirika. Na siku ile mtaomba kwa jina langu, kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba.PKSw 318.4

  “Na shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili.” Upendo wa Baba, kadhalika na wa Mwana, ni msingi wa wokovu wa kizazi kilichopotea. Yesu aliwaambia wanafunzi Wake kabla hajapaa kwenda mbinguni: “wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda” (Yohana 16:26, 27). Mungu alikuwa “akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake” (2 Wakorintho 5:19). Na katika huduma ya patakatifu pa mbinguni, “shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili.” “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16).PKSw 319.1

  Swali, Patakatifu ni nini? limejibibiwa kikamilifu katika Maandiko. Neno “patakatifu,” kama linavyotumika katika Biblia, linahusu, kwanza, hema lililojengwa na Musa, kama nakala ya mambo ya mbinguni; na, pili, linahusu “hema la kweli” la mbinguni, ambalo patakatifu pa duniani palielekeza. Wakati wa kifo cha Kristo huduma ya mfano ilikoma.PKSw 319.2

  “Hema la kweli” la mbinguni ni patakatifu pa agano jipya. Na unabii wa Danieli 8:14 unapotimizwa katika kipindi hiki, patakatifu panapohusishwa na unabii huu ni lazima pawe patakatifu pa agano jipya. Mwishoni mwa siku 2300, mwaka 1844, kulikuwa hakuna patakatifu pa duniani kwa karne nyingi. Kwa hiyo unabii, “Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa,” unahusu, bila swali lo lote, patakatifu pa mbinguni.PKSw 319.3

  Lakini swali muhimu ambacho linahitaji kujibiwa: Kutakaswa kwa patakatifu ni nini? Kwamba kulikuwepo na huduma kama hiyo iliyohusu patakatifu imeelezwa katika Maandiko ya Agano la Kale. Lakini kunaweza kuwepo cho chote cha kutakaswa mbinguni? Katika Waebrania 9 kutakaswa kwa patakatifu pa duniani na patakatifu pa mbinguni kumefundishwa kwa uwazi kabisa. “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo, lakini mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa dhabihu zilizo bora kuliko hizo” (Waebrania 9:22, 23), ambayo ni damu ya thamani ya Kristo.PKSw 319.4

  Utakaso, katika huduma ya mfano na huduma halisi, lazima ufanywe kwa njia ya damu: katika huduma ya awali, kwa damu ya wanyama; katika huduma ya pili, kwa damu ya Kristo. Paulo anasema, sababu kwa nini utakaso ni lazima utekelezwe kwa damu, ni kuwa, pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo la dhambi. Ondoleo la dhambi, au kuweka mbali dhambi, ni kazi inayopaswa kutekelezwa. Lakini ni kwa jinsi gani dhambi imeshikamana na patakatifu, ama pa mbinguni au pa duniani? Hili linaweza kueleweka kwa kuchunguza huduma ya mfano; kwa kuwa makuhani waliohudumu duniani, walihudumu kama “mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni” (Waebrania 8:5).PKSw 319.5

  Huduma ya patakatifu pa mbinguni ilikuwa na sehemu mbili; makuhani walihudumu kila siku katika mahali patakatifu, wakati ambapo mara moja kwa mwaka kuhani mkuu alifanya kazi maalumu ya upatanisho katika patakatifu pa patakatifu, kwa ajili ya kutakasa patakatifu. Siku kwa siku mwenye dhambi aliyetubu alileta sadaka yake kwenye mlango wa hema na, akiweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama wa sadaka, aliungama dhambi zake, kwa njia hiyo, kwa mfano, alihamisha dhambi zake kutoka nafsi yake na kuziweka juu ya kafara asiyekuwa na hatia. Mnyama alichinjwa. “Pasipo kumwaga damu,” anasema mtume, “hakuna ondoleo la dhambi.” “Uhai wa mwili u katika hiyo damu” (Walawi 17:11). Sheria iliyovunjwa ilidai uhai wa mkosaji. Damu, ikiwakilisha uhai alionyang'anywa mwenye dhambi, ambaye hatia yake ilibebeshwa mnyama wa kafara, ilichukuliwa na kuhani, naye kuhani alienda nayo katika chumba cha patakatifu na aliinyunyiza mbele ya pazia, ambalo nyuma yake kulikuwa na sanduku lililohifadhi sheria ambayo mwenye dhambi alikuwa ameivunja. Kwa sherehe hii dhambi ilikuwa, kwa njia ya damu, imehamishiwa kwa mfano katika patakatifu. Katika matukio mengine damu haikupelekwa ndani ya patakatifu; badala yake nyama ilipaswa kuliwa na kuhani, kama Musa alivyowaelekeza watoto wa Haruni, akisema: “naye amewapa ninyi ili kuuchukua uovu wa mkutano” (Walawi 10:17). Huduma zote mbili ziliashiria kuhamishwa kwa dhambi kutoka kwa mwenye dhambi aliyetubu na kuiingiza ndani ya patakatifu.PKSw 320.1

  Hiyo ndiyo kazi iliyoendelea, siku kwa siku, katika mwaka mzima. Dhambi za Israeli zilihamishwa kutoka kwao kwa njia hiyo na kuingizwa ndani ya patakatifu, na kazi maalumu ilikuwa lazima ifanywe ili kuziondoa. Mungu aliagiza kuwa upatanisho ufanywe kwa kila chumba kitakatifu. “Naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao” Upatanisho ulipaswa pia kufanywa kwa ajili ya madhabahu, “kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke” (Walawi 16:16, 19).PKSw 320.2

  Mara moja kwa mwaka, katika Siku kuu ya Upatanisho, kuhani aliingia ndani ya patakatifu pa patakatifu kwa ajili ya kupatakasa patakatifu. Kazi iliyofanywa pale ilikamilisha mzungumko wa mwaka wa huduma. Siku ya Upatanisho watoto wawili wa mbuzi waliletwa mlangoni pa hema, na kura zilipigwa juu yao, “kura moja kwa ajili ya Bwana; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli” (Aya ya 8). Mbuzi ambaye aliangukiwa na kura kwa ajili ya Bwana alichinjwa kama sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu. Na kuhani alitakiwa kupeleka damu yake ndani ya pazia na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema na mbele ya kiti cha rehema. Damu ilitakiwa pia kunyunyizwa juu ya madhabahu ya uvumba iliyokuwa mbele ya pazia.PKSw 321.1

  “Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari. Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu” (Aya ya 21, 22). Kamwe mbuzi wa azazeli hakurejea tena katika kambi ya Israeli, na mtu aliyempeleka jangwani alitakiwa kuoga na kufua nguo zake kwa maji kabla ya kurejea kambini.PKSw 321.2

  Sherehe yote ilipangwa kuwapa picha ya utakatifu wa Mungu na chuki Yake dhidi ya dhambi; na, zaidi ya hapo, kuwaonesha kuwa wasingeweza kushiriki dhambi bila kunajisika. Kila mtu alitakiwa kutesa nafsi yake wakati kazi hii ya upatanisho ilipokuwa ikiendelea. Shughuli zote zilipaswa kuwekwa kando, na mkutano wote wa wana wa Israeli ulipaswa kutumia siku hiyo katika unyenyekevu mwingi mbele za Mungu, kwa maombi, kufunga, na kujichunguza moyoni.PKSw 321.3

  Ukweli muhimu kuhusu upatanisho ulifundishwa kwa njia ya huduma ya mifano. Kafara ilikubaliwa badala ya mwenye dhambi; lakini dhambi haikufutwa kwa damu ya mnyama. Njia iliwekwa ambayo kwayo dhambi ilihamishiwa ndani ya patakatifu. Kwa njia ya sadaka ya damu mwenye dhambi alikiri mamlaka ya sheria, alikiri hatia yake ya kosa alilolifanya, na alionesha shauku yake kwa ajili ya msamaha kwa njia ya imani kwa Mkombozi ajaye; lakini hakuondolewa kabisa katika hukumu ya sheria. Siku ya Upatanisho kuhani mkuu, akiwa amechukua sadaka kutoka katika mkutano, aliingia ndani ya patakatifu pa patakatifu akiwa na damu ya sadaka hii, na alinyunyizia juu ya kiti cha rehema, juu ya sheria moja kwa moja, kuridhisha madai yake. Halafu, kwa cheo chake kama mpatanishi, alizichukua dhambi juu yake mwenyewe na kuziondoa ndani ya patakatifu. Akiweka mikono yake juu ya kichwa cha mbuzi wa Azazeli, aliungama dhambi zote hizi, hivyo kwa njia ya kielelezo alizihamisha kutoka juu ya nafsi yake na kuziweka juu ya mbuzi. Ndipo mbuzi alizibeba na kuondoka nazo, na zilichukuliwa kuwa zimetenganishwa na watu milele.PKSw 321.4

  Hiyo ndiyo huduma iliyofanywa kama “mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni.” Na kile kilichofanywa kama mfano katika huduma ya patakatifu pa duniani kinafanywa katika uhalisia wake katika huduma ya patakatifu pa mbinguni. Baada ya kupaa Kwake Mwokozi wetu alianza kazi Yake kama kuhani wetu mkuu. Paulo anasema: “Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu Kristo hakuingia katika patakatifu palipotengenezwa kwa mikono ya wanadamu” (Waebrania 9:24).PKSw 322.1

  Huduma ya kuhani ya mwaka mzima katika chumba cha kwanza cha patakatifu, “ndani ya pazia” ambalo lilikuwa mlango na lililotenga patakatifu na uwanja wa nje, huwakilisha kazi ya huduma ambayo Kristo alianza nayo mara tu baada ya kupaa. Ilikuwa kazi ya kuhani katika huduma ya kila siku kuwakilisha mbele ya Mungu damu ya sadaka ya dhambi, kadhalika uvumba ambao ulipanda na maombi ya watakatifu. Hivyo ndivyo Kristo alitumia damu Yake kumsihi Baba kwa niaba ya wenye dhambi, na kuwasilisha mbele Yake pia, pamoja na harufu nzuri na ya thamani ya haki Yake Mwenyewe, na maombi ya waaminio waliotubu dhambi zao. Hiyo ndiyo ilikuwa kazi ya huduma katika chumba cha kwanza cha patakatifu pa mbinguni.PKSw 322.2

  Pale imani ya wanafunzi wa Kristo ilipomfuata alipopaa kutoka machoni pao. Hapa ndipo matumaini yao yalikuwa yamewekwa. “Matumaini yale yawekwayo mbele yetu,“Paulo alisema, “kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia, alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele.” “Wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele kwa ajili yetu” (Waebrania 6:18, 19, 20; 9:12).PKSw 322.3

  Kwa karne kumi na nane, kazi ya huduma iliendelea katika chumba cha kwanza cha patakatifu. Damu ya Kristo, ilisihi kwa niaba ya waaminio waliotubu, ilipata msamaha na kukubaliwa na Baba, lakini bado dhambi zao zilibaki katika vitabu vya kumbukumbu. Kama ilivyokuwa katika huduma ya mfano kulikuwa na kazi ya upatanisho mwishoni mwa mwaka, hivyo kabla kazi kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu haijakamilika kutakuwa na kazi ya upatanisho kwa ajili ya kuondoa dhambi ndani ya patakatifu. Hii ni huduma ambayo ilianza wakati siku 2300 zilipoisha. Wakati huo, kama ilivyotabiriwa na nabii Danieli, Kuhani wetu Mkuu aliingia ndani ya patakatifu pa patakatifu, kufanya sehemu ya mwisho ya kazi Yake kubwa— ya kutakasa patakatifu.PKSw 322.4

  Kama ilivyokuwa zamani, ambapo dhambi za watu ziliwekwa kwa imani juu ya mnyama wa sadaka ya dhambi na kwa njia ya damu yake dhambi zilihamishiwa, kwa mfano, ndani ya patakatifu, hivyo katika agano jipya dhambi za wanaotubu zinawekwa, kwa imani, juu ya Kristo na kuhamishiwa, kiuhalisia, ndani ya patakatifu pa mbinguni. Na kama utakaso wa mfano wa patakatifu pa duniani ulivyotekelezwa kwa kuondoa dhambi ambazo zilikuwa zimepachafua, kadhalika utakaso halisi wa patakatifu pa mbinguni utatekelezwa kwa kuondoa, au kufuta, dhambi ambazo zimerekodiwa katika kitabu cha kumbukumbu. Lakini kabla hili halijafanyika, inapasa kuwepo uchunguzi wa vitabu vya kumbukumbu ili kubaini wale ambao, kwa njia ya toba ya dhambi na imani kwa Kristo, wana haki ya kupata manufaa ya upatanisho wake. Utakaso wa patakatifu, hivyo basi, unahusisha kazi ya upelelezi—kazi ya hukumu. Kazi hii inapaswa ifanyike kabla ya ujio wa Kristo kuwakomboa watu Wake; kwa kuwa atakapokuja, ujira Wake utakuwa mkononi Mwake kumlipa kila mtu sawasawa na matendo yake (Ufunuo 22:12).PKSw 323.1

  Hivyo wale waliofuata katika nuru ya neno la unabii ambalo, badala ya kuja duniani mwishoni mwa siku 2300 mwaka 1844, Kristo aliingia ndani ya patakatifu pa patakatifu pa hekalu la mbinguni kufanya kazi ya mwisho ya upatanisho na kujiandaa kwa ajili ya ujio Wake wa pili duniani.PKSw 323.2

  Ilionekana, pia, kuwa, wakati mnyama wa sadaka ya dhambi alimwakilisha Kristo kama kafara, na kuhani alimwakilisha Kristo kama mpatanishi, mbuzi wa Azazeli alikuwa mfano wa Shetani, mwasisi wa dhambi, ambaye juu yake dhambi za waliotubu kikamilifu zitawekwa hatimaye. Wakati kuhani mkuu, kwa njia ya damu ya mnyama wa sadaka ya dhambi, alipoondoa dhambi kutoka ndani ya hekalu, aliziweka juu ya mbuzi wa Azazeli. Wakati Kristo, kwa njia ya damu Yake Mwenyewe, ataondoa dhambi za watu Wake kutoka ndani ya hekalu la mbinguni mwishoni mwa huduma Yake, ataziweka juu ya Shetani, ambaye, wakati wa utekelezaji wa hukumu, atawajibika kwa ajili ya adhabu ya mwisho. Mbuzi wa Azazeli alipelekwa mbali katika nchi isiyokaliwa na watu, na hakutakiwa kurudi katika mkutano wa wana wa Israeli tena. Kadhalika Shetani atafukuzwa milele atoke mbele za Mungu na mbele za watu Wake, na atafutiliwa mbali asiwepo tena katika uangamizaji wa mwisho wa dhambi na wa wenye dhambi. PKSw 323.3

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents