Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 42—Mwisho wa Pambano

  Mwishoni mwa miaka elfu moja, Kristo anarudi tena duniani. Anaandamana na jeshi la waliokombolewa na kusindikizwa na msafara wa malaika. Anaposhuka katika utukufu wa kutisha anawaamuru waovu waliokufa waamke ili wapokee adhabu yao. Wanaamka, jeshi kubwa, wasioweza kuhesabika kama mchanga wa bahari. Tofauti iliyoje ukiwalinganisha na wale waliofufuliwa katika ufufuo wa kwanza! Wenye haki walikuwa wamevikwa ujana wenye uzuri na hali ya kutokufa. Waovu wana viashiria vya magonjwa na hali ya kufa.PKSw 505.1

  Kila mmoja katika umati mkubwa wa watu unageuka kuangalia utukufu wa Mwana wa Mungu. Kwa sauti moja waovu wanatamka kwa mshangao: “Amebarikiwa Yeye ajaye katika jina la Bwana!” Siyo upendo kwa ajili ya Yesu unaohamasisha tamko hili. Nguvu ya ukweli ilazimishayo maneno hayo kutoka katika midomo isiyopenda. Wakati waovu walipokwenda katika makaburi yao, wanatoka wakiwa vile vile wakiwa na uadui ule ule dhidi ya Kristo na roho ile ile ya uasi. Hawapewi rehema mpya ili warekebishe kasoro za maisha yao yaliyopita. Hakuna lo lote la maana lingeweza kupatikana kwa njia hii. Maisha yao ya uasi hayakulainisha mioyo yao. Muda wa pili wa rehema, hata kama wangepewa, ungetumiwa kama ulivyotumika ule wa kwanza kwa kukwepa matakwa ya Mungu na kuchochea uasi dhidi Yake.PKSw 505.2

  Kristo anashuka juu ya mlima wa Mizeituni, mahali ambapo, baada ya kufufuka Kwake, kutokea hapo alipaa, na mahali ambapo malaika walirudia kutangaza ahadi ya kurudi Kwake. Nabii anasema: “Bwana, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye.” “Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, ... na litakuwako huko bonde kubwa sana.” “Naye Bwana atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo Bwana atakuwa mmoja, na jina lake moja” (Zekaria 14:5, 4, 9). Wakati Yerusalemu Mpya, katika utukufu wake mwingi, unaposhuka chini kutoka mbinguni, unatua mahali ambapo pamesafishwa na kuandaliwa kuupokea, na Kristo, pamoja na watu Wake na malaika, wanauingia Mji Mtakatifu.PKSw 505.3

  Sasa Shetani anajiandaa kwa ajili ya pambano lake la mwisho kwa ajili ya ukuu. Wakati ameshanyang'anywa nguvu zake na kuachishwa kazi yake ya udanganyifu, mfalme wa uovu akiwa na hali mbaya na akiwa amechoka sana; lakini waovu wanapofufuliwa na yeye akiuona mkutano mkubwa ukiwa upande wake, matumaini yake yanafufuka, na anaazimia kutokuacha pambano kuu. Atawakusanya majeshi ya waliopotea chini ya bendera yake kwa kupitia kwao atajaribu kutekeleza mipango yake. Waovu ni mateka wa Shetani. Katika kumkataa Kristo wameukubali utawala wa kiongozi aliyeasi. Wako tayari kupokea mapendekezo yake na kutii amri zake. Hata hivyo, akishikilia msimamo wake wa tangu awali, hataki kukiri kuwa yeye ni Shetani. Anadai kuwa yeye ni mfalme ambaye ni mmiliki halali wa ulimwengu na ambaye urithi wake umeporwa kutoka kwake kinyume na sheria. Anajinasibu mwenyewe kwa watu wake waliodanganyika kuwa yeye ni mkombozi, akiwahakikishia kuwa uwezo wake umewatoa katika makaburi yao na kuwa anakwenda kuwaokoa kutoka katika utawala wa kikatili. Uwepo wa Kristo ukiwa umeondolewa, Shetani anatenda maajabu kuunga mkono madai yake. Anawafanya walio dhaifu kuwa na nguvu na anavuvia wote kwa roho yake na nguvu yake. Anapendekeza kuwaongoza dhidi ya kambi ya watakatifu na kuuteka Mji wa Mungu. Kwa furaha ya kishetani anaonesha mamilioni yasiyo na idadi ya watu ambao wamefufuliwa kutoka makaburini na anatangaza kuwa kama kiongozi wao anaweza kabisa kuushinda mji na kurudisha kiti chake cha enzi na ufalme wake.PKSw 505.4

  Katika mkutano ule mkubwa wapo watu wengi wa kizazi cha watu waliokuwa na maisha marefu walioishi kabla ya Gharika; watu wenye maumbo marefu na akili nyingi, ambao, kwa kujisalimisha chini ya utawala wa malaika walioanguka, walitumia stadi zao na ujuzi wao kujiinua wenyewe; watu ambao kazi zao za ajabu za sanaa ziliufanya ulimwengu kuabudu uwezo wao wa kiakili, lakini ambao ukatili wao na ugunduzi wao wa uovu, vikiichafua dunia na kuondoa sura ya Mungu duniani, vilimfanya Mungu kuwafutilia mbali kutoka katika uso wa uumbaji Wake. Wapo wafalme na majenerali walioshinda mataifa, watu mashujaa ambao hawakuwahi kushindwa vitani, wenye kiburi, wapiganaji wenye tamaa ya kufanya makubwa ambao ujio wao ulizifanya falme kutetemeka. Mautini hawakupoteza uzoefu wao. Wanapotoka makaburini, wanarudia mkondo wa mawazo yao pale yalipokomea. Wanachochewa na shauku ile ile ya kushinda iliyowatawala walipofariki.PKSw 506.1

  Shetani anashauriana na malaika zake, na ndipo anashauriana na hawa wafalme na washindaji na watu wenye nguvu. Wanatathmini nguvu na idadi ya wapiganaji walio upande wao, na wanatangaza kuwa jeshi lililoko ndani ya mji ni dogo ukilinganisha na jeshi lao, na kuwa wanaweza kulishinda lile jeshi dogo. Wanaweka mipango yao ya kuteka mali na utajiri na utukufu wa Yerusalemu Mpya. Wote mara moja wanaanza kujiandaa kwa ajili ya vita. Mafundi wenye stadi wanaunda zana za vita. Viongozi wa kijeshi, waliotukuka kwa mafanikio yao, wanawapanga watu wa vita katika vikosi na migawanyo mbalimbali.PKSw 506.2

  Hatimaye amri ya kusonga mbele inatolewa, na wapiganaji wasiokuwa na idadi wanatembea kwenda mbele—jeshi ambalo halijawahi kukusanywa na washindi wa kidunia, jeshi ambalo litaunganisha wapiganaji wa zama zote tangu vita ya kwanza kutokea duniani. Shetani, mpiganaji mwenye nguvu nyingi kuliko wapiganaji wengine wote, anaongoza msafara wa kivita, na malaika zake wanaunganisha nguvu zao pamoja kwa ajili ya pambano hili la mwisho. Wafalme na wapiganaji wamo katika msafara wake, na watu wasiokuwa na idadi wanafuata katika vikosi vikubwa, kila kikosi kikiwa chini ya kiongozi aliyeteuliwa. Kwa umahiri mkubwa wa kijeshi askari waliosongamana wanasonga mbele wakitembea juu ya ardhi iliyoharibika wakiuelekea Mji wa Mungu. Kwa amri ya Yesu, malango ya Yerusalemu Mpya yanafungwa, na majeshi ya Shetani yanauzingira mji na wanajiandaa kwa ajili ya mashambulizi.PKSw 506.3

  Sasa Kristo anatokea tena na kusimama mahali ambapo anaonwa na maadui Zake. Juu sana ya mji, juu ya msingi wa dhahabu iliyosafishwa sana, kuna kiti cha enzi, kilicho juu na kilichoinuliwa sana. Juu ya kiti hiki cha enzi anakaa Mwana wa Mungu, na kando kando Yake kuna raia wa ufalme Wake. Nguvu na utukufu wa Kristo hakuna lugha inayoweza kueleza, hakuna kalamu inayoweza kuandika. Utukufu wa Baba wa Milele unamfunika Mwanaye. Utukufu wa uwepo Wake unaujaza Mji wa Mungu, na unatiririka na kutoka nje ya malango ya mji, na kufurika duniani kote kwa mwangaza wake.PKSw 507.1

  Karibu kabisa na kiti cha enzi kuna wale ambao awali walikuwa na bidii sana upande wa Shetani, lakini, ambao baada ya kuopolewa kama kijinga kutoka motoni, walimfuata Mwokozi wao kwa kujitoa kikamilifu. Safu inayofuata ni yale wale waliokamilisha tabia ya Kikristo katikati ya madanganyifu na ufisadi, wale walioiheshimu sheria ya Mungu wakati ulimwengu wa Kikristo ukitangaza kuwa sheria hiyo imebatilishwa, na mamilioni ya watu, wa zama zote, waliouawa kwa ajili ya imani yao. Na baada ya hao kuna “mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, ... mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao” (Ufunuo 7:9). Vita yao imekwisha, ushindi wao umepatikana. Wameshiriki katika shindano na wamepokea tuzo. Tawi la mtende katika mikono yao ni ishara ya ushindi wao, vazi jeupe ni nembo ya haki ya Kristo isiyokuwa na doa ambayo ni yao sasa.PKSw 507.2

  Waliokombolewa wanaimba wimbo wa sifa ambao mwangwi wake unaakisiwa na kuakisiwa katika makuba ya mbinguni: “Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo” (Aya 10). Na malaika na maserafi wanaunganisha sauti zao katika kusifu. Baada ya waliokombolewa kuona nguvu na ubaya wa Shetani, wamethibitisha, kwa uhakika zaidi kuliko kabla ya hapo, kuwa ni nguvu ya Kristo peke yake ingeweza kuwasaidia wapate ushindi. Miongoni mwa wale wote wanaong'aa hakuna mtu hata mmoja ambaye anaweza kujitapa kuwa alipata wokovu kwa uwezo wake mwenyewe, kuwa alishinda kwa nguvu zake na wema wake mwenyewe. Hakuna jambo lo lote linatajwa kuhusiana na kile walichokifanya au mateso waliyoyapata; lakini maudhui ya kila wimbo, wazo kuu la kila wimbo, ni: Wokovu una Mungu wetu na Mwanakondoo.PKSw 507.3

  Mbele ya wakazi wa duniani na mbinguni waliokusanyika pamoja uvalishwaji taji wa Mwana wa Mungu unafanyika. Na sasa, akiwa amekabidhiwa ukuu na mamlaka ya juu kabisa, Mfalme wa wafalme anatangaza hukumu juu ya waasi dhidi ya serikali Yake na anatekeleza haki juu ya wote walioivunja sheria Yake na kuwatesa watu Wake. Nabii wa Mungu anasema: “Nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao” (Ufunuo 20:11, 12).PKSw 508.1

  Mara tu vitabu vya kumbukumbu vinapofunguliwa, na jicho la Yesu kuwatazama waovu, wanatambua kila dhambi waliyowahi kuitenda katika maisha yao. Wanatambua mahali nyayo zao zilipoteleza na kuondoka katika njia ya usafi na utakatifu, kiasi ambacho kiburi na uasi vilipowafikisha katika kuvunja sheria ya Mungu. Majaribu ya udanganyifu waliyopalilia kwa kulea dhambi, mibaraka iliyotumiwa vibaya, wajumbe wa Mungu waliodharauliwa na kupuuzwa, maonyo yaliyotupiliwa mbali, mawimbi ya rehema yaliyorudishwa nyuma na moyo mgumu, usiotubu—vyote vinaonekana kama vilivyoandikwa kwa herufi za moto.PKSw 508.2

  Juu ya kiti cha enzi kunafunuliwa msalaba; na kama onesho la filamu zinatokea mandhari za majaribu na anguko la Adamu, na mfululizo wa hatua katika mpango mkuu wa ukombozi. Kuzaliwa kwa Mwokozi katika mazingira ya kimaskini; maisha Yake ya awali ya usahili na utii; ubatizo Wake katika mto waYordani; mfungo na majaribu katika jangwa; huduma Yake ya hadhara, kuwafunulia wanadamu mibaraka ya mbinguni yenye thamani kubwa; siku zilizojaa matendo ya upendo na rehema, nyakati za usiku zilizotumiwa katika maombi na kukesha katika maeneo ya faragha milimani; mipango ya wivu, chuki, na ubaya iliyopangwa dhidi Yake kama malipo kwa wema Wake; uchungu wa kutisha, wa siri katika Bustani ya Gethsemane chini ya mzigo mzito wa dhambi za ulimwengu wote; kusalitiwa Kwake katika mikono ya kundi la wauaji; matukio ya kutisha ya usiku ule wa hofu—mfungwa asiye na ubishi, aliyekimbiwa na wanafunzi Wake wapendwa, akiburuzwa kikatili katika mitaa ya Yerusalemu; Mwana wa Mungu akioneshwa mbele ya Anasi kwa furaha, akishitakiwa katika nyumba ya kuhani mkuu, katika ukumbi wa hukumu wa Pilato, mbele ya Herode mwoga na katili, akidhihakiwa, akitukanwa, akiteswa, na akihukumiwa kufa—vyote vinaoneshwa wazi wazi.PKSw 508.3

  Na sasa mbele ya umati mkubwa wa watu zinafunuliwa mandhari za mwisho—Mtesekaji mvumilivu akitembea katika njia inayoelekea Kalwari; Mfalme wa mbinguni akining'inia juu ya msalaba; makuhani wenye kiburi na umati wa watu wenye zogo wakikejeli uchungu Wake unaoishia; giza lisilo la kawaida; dunia iliyoumka na kusinyaa, miamba iliyopasuka, makaburi yaliyofunguka, vikiashiria wakati Mkombozi wa ulimwengu alipotoa uhai Wake.PKSw 509.1

  Tukio la kutisha linatokea kama lilivyokuwa. Shetani, malaika zake, na wafuasi wake hawana uwezo wa kugeuka wasiitazame picha ya kazi yao. Kila mhusika anakumbuka sehemu aliyofanya. Herode, aliyewaua watoto wasio na hatia wa Bethlehemu ili amuue Mfalme wa Israeli; Herodia mwovu, ambaye moyoni mwake kuna hatia ya damu ya Yohana Mbatizaji; Pilato dhaifu na kigeukigeu; askari wanaodhihaki; makuhani na wakuu na umati uliofyatuka akili wakipiga kelele, “Damu Yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu!”—wote wanaona ukubwa wa hatia yao. Wanatafuta bila mafanikio kujificha wasionekane mbele ya utukufu wa Kimungu wa uso Wake, ambao unang'aa zaidi kuliko utukufu wa jua, wakati waliokombolewa wakizitupa taji zao kwenye nyayo za Mwokozi, wakisema: “Alikufa kwa ajili yangu!”PKSw 509.2

  Miongoni mwa waliokombolewa wamo mitume wa Kristo, Paulo shujaa, Petro mwenye juhudi, Yohana anayependwa na mwenye upendo, na ndugu zao wa kweli, na pamoja nao jeshi kubwa la wafia dini; wakati nje ya kuta, palipo na kila kitu kichafu na kila kitu kinachochukiza, kuna wale ambao kwa mikono yao watumishi wa Mungu wa kweli waliteswa, walifungwa, na kuuawa. Yupo Nero, jitu lile katili na ovu, likiona furaha ya kuinuliwa kwa wale ambao huko nyuma aliwatesa, na ambao kwa sababu ya uchungu wao mwingi alipata furaha ya kishetani. Mama yake yupo pale akishuhudia matokeo ya kazi yake; aone jinsi mfano wake mbaya wa tabia aliorithisha kwa mwanaye, mihemko iliyochochewa na kukuzwa kwa mvuto na mfano wake, vimezaa matunda ya uhalifu ulioufanya ulimwengu kutetemeka.PKSw 509.3

  Kuna mapadri na makasisi wa kipapa, waliodai kuwa mabalozi wa Kristo, lakini walitumia kitanda cha kutesea, gerezani la ardhini, na nguzo ya kuchomea watu moto kudhibiti dhamiri za watu Wake. Kuna mapapa wenye kiburi waliojiinua juu ya Mungu na kujaribu kubadili sheria ya Yeye Aliye Juu sana. Wale waliojifanya kuwa mababa wa kanisa wanatakiwa kutoa maelezo ambayo wanatamani wasamehewe. Kwa kuchelewa sana wanagundua kuwa Yeye anayejua mambo yote ana wivu juu ya sheria Yake na kuwa hawezi kumhesabia anayeivunja kuwa hana hatia. Wanagundua kuwa Kristo alijali maslahi ya watu Wake wanaoteseka; na wanahisi uzito wa maneno Yake: “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Mathayo 25:40).PKSw 509.4

  Ulimwengu wote mwovu unasimama ukiwa katika kizimba cha Mungu wakishtakiwa kwa kosa la uhaini mkuu dhidi ya serikali ya mbinguni. Hawana wa kuwatetea; hawana udhuru; na hukumu ya mauti ya milele inatangazwa dhidi yao.PKSw 510.1

  Inakuwa dhahiri kwa wote kuwa mshahara wa dhambi siyo uhuru kamili na uzima wa milele, bali utumwa, uharibifu, na kifo. Waovu wanaona kile ambacho wamekipoteza kwa maisha yao ya uasi. Uzito wa milele wa utukufu ulio muhimu zaidi kuliko kitu kingine cho chote ulidhihakiwa ulipotolewa kwao; lakini sasa unaonekana kuhitajika sana. “Yote haya,” roho iliyopotea inalia, “ningekuwa nayo; lakini nilichagua kujitenga nayo. Aa! kupumbazwa kwa ajabu! Nimepoteza amani, furaha, na heshima, na badala yake nimepata umaskini, kudharaulika, na kukata tamaa.” Wote wanaona kuwa kutengwa na mbingu ni haki kabisa. Kwa maisha yao walitangaza kuwa: “Hatumtaki huyu Mtu [Yesu] atutawale.”PKSw 510.2

  Kama watu walio katika maono, waovu wanamwona Mwana wa Mungu akivikwa taji. Wanaona katika mikono Yake mbao za sheria ya Mungu, amri ambazo walizidhihaki na kuzivunja. Wanashuhudia mlipuko wa mshangao, furaha, na sifa kwa waliookolewa; na wakati wimbi la sauti tamu linapopaa juu ya umati watu walioko nje ya mji, wote kwa sauti moja wanashangilia, “Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa” (Ufunuo 15:3); na, wakianguka kifudifudi, wanamwabudu Mfalme wa uzima.PKSw 510.3

  Shetani anaonekana kana kwamba amepigwa kiharusi anapouona utukufu na ukuu wa Kristo. Yeye aliyekuwa kerubi afunikaye anakumbuka ni wapi alipoangukia. Serafi ang'aaye, “mwana wa asubuhi;” amebadilika kiasi gani, ameshuka chini kiasi gani! Kutoka katika baraza alipokuwa akiheshimiwa, ameondolewa milele zote. Anamwona mwingine akisimama karibu na Baba, akifunika utukufu Wake. Ameona taji ikiwekwa juu ya kichwa cha Kristo na malaika mmoja mrefu na mwonekano wenye utukufu mwingi, na anatambua kuwa cheo cha juu cha malaika huyu kilikuwa kiwe chake.PKSw 510.4

  Kumbukumbu zinamrudisha hadi wakati alipokuwa hana hatia na wakati alipokuwa msafi, amani na kuridhika vilikuwa vyake mpaka alipojiingiza katika manung'uniko dhidi ya Mungu, na kumwonea wivu Kristo. Mashtaka yake, uasi wake, madanganyifu yake ili apate huruma na kuungwa mkono na malaika, ukaidi wake na kutofanya juhudi yo yote ya kuungama makosa yake wakati Mungu alipokuwa tayari kumsamehe— yote yanakuja mbele yake kwa uwazi. Anatathmini kazi yake kati ya watu na matokeo yake—uadui wa mwanadamu kwa mwanadamu mwenzake, maangamizi ya kutisha ya wanadamu, kuinuka na kuanguka kwa falme, kupinduliwa kwa viti vya enzi, mfululizo mrefu wa fujo, migogoro, na mapinduzi. Anakumbuka juhudi zake zisizochoka za kupinga kazi ya Kristo na kumdidimiza mwanadamu chini zaidi na zaidi. Anaona kuwa mipango yake ya kuzimu imeshindwa kuwaangamiza wale walioweka tumaini lao kwa Yesu. Shetani anapoangalia ufalme wake, matunda ya kazi zake, anaona tu kushindwa na kuangamizwa. Anawaongoza watu wengi kuamini kuwa Mji wa Mungu ni windo rahisi; lakini anajua kuwa huu ni uongo. Tena na tena, katika mwenendo wa pambano kuu, ameshindwa na kulazimishwa kujisalimisha. Anajua vizuri pia mamlaka na nguvu za Yule Aishie Milele.PKSw 510.5

  Kusudi la mwasi mkuu limekuwa daima kujihesabia haki na kuonesha kuwa serikali ya Mungu ndiyo inawajibika kwa uasi. Ili kufikia azma hii ameelekeza nguvu zote za akili yake kubwa. Amefanya kazi kwa kudhamiria na kwa kupangilia, na kwa mafanikio ya kushangaza, kuwaongoza watu wengi kukubali tafsiri yake hii ya pambano kuu ambalo limedumu kuwepo kwa muda mrefu. Kwa miaka mingi, huyu mkuu wa njama ametawanya uongo badala ya ukweli. Lakini wakati umefika sasa ambapo uasi unapaswa kushindwa na historia na tabia ya Shetani ifunuliwe. Katika juhudi yake kubwa ya mwisho ya kumpindua Kristo na kumwondoa kwenye kiti Chake cha enzi, kuwaangamiza watu Wake, na kuutwaa Mji wa Mungu, mdanganyaji mkuu anajifunua kikamilifu. Wale walioungana naye wanaona kushindwa kwa mipango yake. Wafuasi wa Kristo na malaika waaminifu wanatazama upana wa mikakati yake dhidi ya serikali ya Mungu. Anachukiwa na wenye uhai wote.PKSw 511.1

  Shetani anaona kuwa uasi wake wa kujitolea umemfanya asifae kuishi mbinguni. Amezoeza nguvu zake kufanya vita dhidi ya Mungu; usafi, amani na mwafaka wa mbinguni vingekuwa mateso makubwa kwake. Mashtaka yake dhidi ya rehema na haki ya Mungu sasa yamenyamazishwa. Aibu ambayo amejitahidi kuirundika juu ya Yehova inamrudia yeye kikamilifu. Na sasa Shetani anainama chini na anakiri haki ya hukumu yake.PKSw 511.2

  “Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa” (Aya 4). Kila suala kuhusu ukweli na uongo katika pambano kuu la muda mrefu litakuwa limewekwa wazi. Matokeo ya uasi, matunda ya kuweka pembeni amri za Mungu, yatakuwa yamewekwa wazi na kuonwa na viumbe wote wenye akili. Tofauti ya utendaji kazi wa utawala wa Shetani na serikali ya Mungu umewekwa wazi kwa ulimwengu wote. Kazi za Shetani zimekwisha kumhukumu. Hekima ya Mungu, haki Yake, na wema Wake vimethibitishwa kikamilifu. Imedhihirika kuwa utendaji kazi Wake wote katika pambano kuu umefanyika kwa kuzingatia manufaa ya milele kwa ajili ya watu Wake na kwa maslahi ya sayari zote alizoziumba. “Kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi” (Zaburi 145:10). Historia ya dhambi itabaki milele zote kama ushuhuda kuwa uwepo wa sheria umeshikamana na furaha ya wenye uhai wote walioumbwa na Mungu. Kwa kuzingatia ukweli wote kuhusu pambano kuu, ulimwengu, wa waaminifu na waasi, kwa sauti moja wanatangaza: “Ni za haki na kweli njia Zako, Ee Mfalme wa watakatifu.”PKSw 511.3

  Mbele ya ulimwengu wote imewasilishwa kwa uwazi kafara kuu iliyotolewa na Baba na Mwana kwa ajili ya mwanadamu. Saa imekuja ambapo Kristo anakalia nafasi Yake ya haki anaadhimishwa juu ya mamlaka na nguvu na kila jina linalotajwa. Ilikuwa kwa ajili ya furaha iliyoko mbele Yake—kwamba awaingize watu wengi katika utukufu—kuwa aliustahimili msalaba na kuidharau aibu. Na kwa kadiri huzuni na aibu ilivyokuwa kubwa, ndivyo furaha ilivyokuwa kubwa na utukufu ulivyokuwa mwingi zaidi. Anawaangalia waliokombolewa, wakiwa wameumbwa upya katika sura Yake, kila moyo ukiwa na chapa kamilifu ya sura ya Mungu, kila uso ukiaksi mfano wa Mfalme wao. Anaona ndani yao matokeo ya kazi ya nafsi Yake, na anaridhika. Ndipo, kwa sauti inayosikika kwa wote waliokusanyika, wenye haki na waovu, anatangaza: “Tazama thamani ya damu Yangu! Kwa ajili ya hawa niliteseka, kwa ajili ya hawa nilikufa, ili waweze kuishi mbele Yangu katika zama zote milele na milele.” Na wimbo wa sifa unapanda juu kutoka kwa wale waliova mavazi meupe waliokizunguka kiti cha enzi: “Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka” (Ufunuo 5:12).PKSw 512.1

  Licha ya kuwa Shetani amelazimishwa kukiri haki ya Mungu na kuinama kwa ukuu wa Kristo, tabia yake inabaki bila kubadilika. Roho ya uasi, kama mkondo wa maji wenye nguvu, inainuka tena. Akiwa amejazwa na wazimu, anaazimia kutokujisalimisha katika pambano kuu. Wakati umefika kwa ajili ya pambano la mwisho la kufa na kupona dhidi ya Mfalme wa mbinguni. Anaharakisha kwenda katikati ya wafuasi wake anajaribu kuwachochea kwa hasira zake na kuwahamasisha waingie vitani mara moja. Lakini miongoni mwa mamilioni yote ambao amewadanganya kufanya uasi, hakuna hata mmoja wao anayetambua ukuu wake. Mamlaka yake imefikia mwisho. Waovu wamejazwa na chuki ileile dhidi ya Mungu iliyoko ndani ya Shetani; lakini wanaona kuwa hali yao haina tumaini, kuwa hawawezi kumshinda Yehova. Hasira yao inawaka dhidi ya Shetani na wale ambao walikuwa mawakala wake katika udanganyifu, na kwa ghadhabu ya mashetani wanamshambulia.PKSw 512.2

  Bwana anasema: “Kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu; basi, tazama, nitaleta wageni juu yako, watu wa mataifa wenye kutisha; nao watafuta panga zao juu ya uzuri wa hekima yako, nao watautia uchafu mwangaza wako. Watakushusha hata shimoni.” “Nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto.... Nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.... Nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao.... Umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele” (Ezekieli 28:6-8, 16-19).PKSw 512.3

  “Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyofingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni” “Maana Bwana ana ghadhabu juu ya mataifa yote, na hasira kali juu ya jeshi lao lote; amewaangamiza kabisa, amewatoa waende kuchinjwa” “Awanyeshee wasio haki mitego, Moto na kiberiti na upepo wa hari, Na viwe fungu la kikombe chao” (Isaya 9:5; 34:2; Zaburi 11:6). Moto unashuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Dunia inapasuka. Silaha zilizofichwa katika vina vyake zinatoka nje. Mioto inayoteketeza inalipuka kutoka katika uwazi wa kila shimo ardhini. Miamba yenyewe inawaka moto. Siku imekuja ambayo inaunguza kama tanuru. Vitu vya asili vinayeyuka kwa joto kali, dunia pia, na kazi zote zilizomo zinaunguzwa (Malaki 4:1; 2 Petro 3:10). Uso wa dunia unaonekana kama donge moja kubwa lililoyeyuka— ziwa kubwa la moto. Ni wakati wa hukumu na kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu—“siku ya kisasi cha Bwana, mwaka wa malipo, ili kushindania Sayuni” (Isaya 34:8).PKSw 513.1

  Waovu wanapokea mshahara wao duniani (Mithali 11:31). Waovu “watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi” (Malaki 4:1). Baadhi wanaangamizwa kwa muda mfupi, wakati wengine wanateseka kwa siku nyingi. Wote wanaadhibiwa “kulingana na matendo yao” Kwa dhambi za wenye haki kuhamishiwa kwa Shetani, anawajibika kuteseka siyo tu kwa ajili ya uasi wake peke yake, bali pia kwa ajili ya dhambi alizosababisha watu wa Mungu kuzitenda. Adhabu yake inapaswa kuwa kubwa zaidi kuliko adhabu ya wale aliowadanganya. Baada ya wote walioanguka kwa kudanganywa kuteketea, Shetani ataendelea kuishi na kuteseka zaidi. Katika moto unaosafisha, waovu hatimaye wanaangamizwa, shina na tawi—Shetani ndiye shina, wafuasi wake ni matawi. Adhabu kamili ya sheria imetekelezwa; madai ya haki yametimizwa; na mbingu na dunia, zikiangalia, zinatangaza haki ya Yehova.PKSw 513.2

  Kazi ya Shetani ya uharibifu imefikia kikomo milele. Kwa miaka elfu sita ametekeleza mapenzi yake, akiijaza dunia kwa misiba na kuleta huzuni katika ulimwengu wote. Uumbaji wote umekuwa ukiugua na kutaabika kwa pamoja kwa sababu ya maumivu. Sasa viumbe wa Mungu wamekombolewa milele na kuwa mbali kabisa na uwepo wake na majaribu yake. “Dunia yote inastarehe na kutulia; Hata [wenye haki] huanzilisha kuimba” (Isaya 14:7). Na kelele za sifa na ushindi zinapanda juu kutoka kwa ulimwengu wote mtiifu. “Nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikisema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki” (Ufunuo 19:6).PKSw 513.3

  Wakati dunia itakapokuwa imefunikwa kwa moto wa maangamizi, wenye haki wanaishi katika Mji Mtakatifu. Mauti ya pili haina nguvu juu ya wale walio na sehemu katika ufufuo wa kwanza. Wakati Mungu ni moto ulao kwa waovu, Yeye ni jua na ngao kwa watu Wake (Ufunuo 20:6; Zaburi 84:11).PKSw 514.1

  “Nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita” (Ufunuo 21:1). Moto utateketeza waovu na kusafisha dunia. Kila kiashiria cha laana kinafutiliwa mbali. Hakuna kuzimu inayowaka moto itakayodumu kuwepo milele mbele ya waliokombolewa kama kumbukumbu ya matokeo ya kutisha ya dhambi.PKSw 514.2

  Kumbukumbu moja tu itabaki: Mkombozi wetu atadumu kuwa na alama Zake za kusulubiwa. Katika kichwa Chake kilichojeruhiwa, ubavuni Mwake, mikono na miguu Yake, ndizo alama pekee za kazi ya kikatili iliyofanywa na dhambi. Nabii anasema, akimtazama Kristo katika utukufu Wake: “Mwangaza wake ulikuwa kama nuru; Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake; Ndipo ulipofichwa uweza wake” (Habakuki 3:4). Ubavu ule uliochomwa mkuki ambapo ilitoka damu iliyompatanisha mwanadamu na Mungu—pale ndipo palipo na utukufu wa Mwokozi, pale“Ndipo ulipofichwa uweza wake.” “Uweza wa kuokoa,” kwa njia ya kafara ya ukombozi, alikuwa na nguvu za kutekeleza hukumu juu ya wale waliodhihaki neema ya Mungu. Na ishara za mateso Yake ndiyo heshima Yake ya juu kuliko vitu vyote; katika zama zote, milele na milele, majeraha ya Kalwari yataonesha sifa Yake na kutangaza uweza Wake. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta, kuwa sifa ya utukufu wake.PKSw 514.3

  “Ee mnara wa kundi, kilima cha binti Sayuni, utajiliwa; naam, mamlaka ya kwanza yatakuja” (Mika 4:8). Wakati umefika ambao watu watakatifu wamekuwa wakiutazamia kwa shauku kubwa tangu upanga wa moto ulipowazuia Adamu na Hawa kuingia katika Bustani ya Edeni, wakati kwa ajili ya “ukombozi wa milki yake” (Waefeso 1:14). Dunia ambayo awali ilikabidhiwa kwa mwanadamu kama ufalme wake, ikasalitiwa na mwanadamu na kuwekwa katika mikono ya Shetani, na kwa muda mrefu ikashikiliwa na adui mwenye nguvu, imerudishwa kwa njia ya mpango mkuu wa ukombozi. Kila kitu kilichokuwa kimepotea kwa ajili ya dhambi sasa kinarudishwa. “Maana Bwana, ... asema hivi; ... ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu” (Isaya 45:18). Kusudi la Mungu la awali katika uumbaji wa dunia linatimizwa wakati dunia inapofanywa kuwa makao ya milele ya waliokombolewa. “Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele” (Zaburi 37:29).PKSw 514.4

  Hofu ya kuufanya urithi wa milele kuwa ni wa vitu zaidi imewafanya watu wengi kuona kila kitu ni cha kiroho katika kutafsiri ukweli unaoeleza mahali tutakapoishi mbinguni. Kristo aliwahakikishia wanafunzi Wake kuwa alikwenda kuandaa makao kwa ajili yao katika nyumba ya Baba. Watu wanaoyakubali mafundisho ya neno la Mungu hawatashindwa kuelewa kabisa kuhusiana na makao ya mbinguni. Na bado, “jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao” (1 Wakorintho 2:9). Lugha ya kibinadamu haitoshi kueleza zawadi ya wenye haki. Itaeleweka tu kwa wale watakaoiona. Hakuna akili yenye kikomo inaweza kuelewa utukufu wa Paradiso ya Mungu.PKSw 515.1

  Katika Biblia, urithi wa waliookolewa unaitwa “nchi” (Waebrania 11:14-16). Pale Mchungaji wa mbinguni anawaongoza kondoo Wake hadi kwenye chemchemi ya maji ya uzima. Mti wa uzima unazaa matunda yake kila mwezi, na majani ya mti ni kwa ajili ya kuwahudumia mataifa. Pale kuna mito inayotiririka daima maji, meupe kama bilauri, na kando ya mito kuna miti inayopepea na kuweka kivuli chake juu ya njia zilizoandaliwa kwa ajili ya waliokomobolewa na Bwana. Pale nyika pana na kubwa zinaenea na kupanda katika vilima vizuri, na milima ya Mungu nyuma ya vilele vyake virefu. Kwenye nyanda hizo za amani, kando ya mito hiyo iliyo hai, watu wa Mungu, watu waliosafiri na kutanga-tanga kwa muda mrefu, wataishi humo.PKSw 515.2

  “Watu wangu watakaa katika kao la amani; na katika maskani zilizo salama, na katika mahali pa kupumzikia penye utulivu.” “Jeuri haitasikiwa tena katika nchi yako, Ukiwa na uharibifu hazitakuwa mipakani mwako; Bali utaziita kuta zako, Wokovu, Na malango yako, Sifa.” “Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; ... wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi” (Isaya 32:18; 60:18; Isaya 65:21, 22).PKSw 515.3

  Pale, “nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi.” “Badala ya michongoma utamea msonobari, Na badala ya mibigili, mhadesi.” “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwanakondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ... na mtoto mdogo atawaongoza.” “Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu,” asema Bwana (Isaya 35:1; 55:13; Isaya 11:6, 9).PKSw 515.4

  Maumivu hayawezi kuwepo katika angahewa la mbinguni. Hakutakuwa na machozi tena, hakuna misafara ya mazishi, hakuna alama za maombolezo. “Mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, ... kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.” “Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao” (Ufunuo 21:4; Isaya 33:24).PKSw 515.5

  Pale kuna Yerusalemu Mpya, mji mkuu wa dunia mpya iliyotukuzwa, “taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.” “mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri.” “Mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake.” Bwana anasema: “Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu.” “Maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao” (Isaya 62:3; Ufunuo 21:11, 24; Isaya 65:19; Ufunuo 21:3).PKSw 516.1

  Katika Mji wa Mungu “Usiku hautakuwepo.” Hakuna atakayehitaji au kuwa na shauku ya pumziko. Hakutakuwa na kuchoka kufanya mapenzi ya Mungu na kutoa sifa kwa jina Lake. Daima tutahisi upya wa asubuhi na daima hatutakaribia mwisho wake. “Wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru.” (Ufunuo 22:5). Nafasi ya nuru ya jua itachukuliwa na mwangaza ambao mng'ao wake hauumizi, lakini ambao unaupita mbali mno mwangaza wa adhuhuri. Utukufu wa Mungu na Mwanakondoo unajaza jiji hili takatifu kwa nuru isiyofifia. Watakatifu wanatembea katika utukufu usio na jua wa siku isiyo na ukomo.PKSw 516.2

  “Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake” (Ufunuo 21:22). Watu wa Mungu wanapata fadhila ya kuwa na maongezi ya wazi na Baba na Mwana.PKSw 516.3

  “Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo” (1 Wakorintho 13:12). Tunaiona sura ya Mungu ikiwa imeakisiwa, kama katika kioo, katika kazi za vitu vya asili na katika ushughulikiaji Wake wa watu; lakini wakati huo tunamwona uso kwa uso, bila kiambaza kinachotukinga katikati na kupunguza mwanga. Tutasimama mbele Yake na kuuona utukufu wa uso Wake.PKSw 516.4

  Pale waliokombolewa watajua, kama wanavyojuliwa. Upendo na huruma ambao Mungu ameweka rohoni pale vitapata matumizi ya kweli na mazuri sana. Ushirika safi na wenye uhai mtakatifu, maisha ya kijamii yenye mwafaka na malaika waliobarikiwa na watu waaminifu wa zama zote walioosha mavazi yao na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo “ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa” (Waefeso 3:15), vifungo vitakatifu vinavyowafunga pamoja—hivi vinasaidia kuleta furaha ya waliokombolewa.PKSw 516.5

  Pale, akili zisizokuwa na hali ya kufa zitatafakari kwa furaha isiyo na kikomo maajabu ya uwezo wa uumbaji, siri za upendo na ukombozi. Hakutakuwa na adui katili wa kumjaribu mtu kumsahau Mungu. Kila karama itakuzwa, kila talanta itaongezwa. Matakwa ya kupata maarifa hayatachosha akili wala kudhoofisha uwezo. Pale shughuli muhimu zitaendelezwa, vilele vya juu vya matarajio vitafikiwa, matamanio ya juu kabisa yatapatikana; na bado kutatokea vilele vipya vya kupanda na kupita, maajabu mapya ya kufurahia, na ukweli mpya wa kujifunza, malengo mapya ya kuhitaji nguvu za akili na roho na mwili.PKSw 516.6

  Hazina zote za uumbaji zitakuwa wazi kwa ajili ya mafunzo ya watu wa Mungu waliokombolewa. Bila kukatishwa na hali ya kufa, wanaruka kwa mabawa yao na kwenda katika sayari za mbali—sayari zilizozizima kwa huzuni kwa sababu ya tabu za mwanadamu na kurindima nyimbo za furaha kwa ajili ya roho moja iliyokombolewa. Kwa furaha isiyoelezeka watoto wa duniani wanaingia katika furaha na hekima ya viumbe ambao hawakuanguka. Wanashiriki hazina za ujuzi na ufahamu uliopatikana kwa zama nyingi kwa kutafakari juu ya kazi za mikono ya Mungu. Kwa macho yasiyokuwa na hali ya kufifia wanauona utukufu wa uumbaji—mifumo ya jua na nyota, vyote katika mpangilio wake wa awali vikizunguka kiti cha enzi cha Mungu. Juu ya vitu vyote, kuanzia vitu vidogo kabisa hadi vitu vikubwa kabisa, jina la Muumbaji limeandikwa, na vyote vinadhihirisha utajiri wa nguvu Zake.PKSw 517.1

  Na miaka katika umilele, itakavyoendelea, italeta ufunuo mkubwa na wenye utukufu mwingi zaidi kumhusu Mungu na kumhusu Kristo. Uelewa ni endelevu, kadhalika upendo, kicho, na furaha vinaongezeka siku kwa siku. Kwa kadiri watu wanavyomwelewa Mungu zaidi, ndivyo wanavyoipenda zaidi tabia Yake. Yesu alipofungua mbele yao upana wa ukombozi na mafanikio ya kushangaza katika pambano kuu dhidi ya Shetani, mioyo ya waliokombolewa ilizizima kwa kujiweka wakfu na kumpenda Yesu zaidi, na kwa furaha kubwa wanapiga vinubi vyao vya dhahabu; na sauti kumi elfu mara kumi elfu na maelfu kwa maelfu ya sauti yanafumka na kuimba kibwagizo cha sifa.PKSw 517.2

  “Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele” (Ufunuo 5:13).PKSw 517.3

  Pambano kuu limekwisha. Dhambi na wenye dhambi havipo tena. Ulimwengu wote uko safi. Mdundo wa mwafaka na furaha unapiga katika uumbaji wake wote. Kutoka Kwake Yeye aliyewaumba wote, vinatiririka uzima na nuru na furaha, katika maeneo yote na nafasi isiyokuwa na ukomo. Kutoka kwa atomu ndogo sana hadi ulimwengu mkubwa sana, mambo yote, vyenye uhai na visivyo na uhai, katika uzuri wao usiokuwa na kivuli na furaha kamili, vinakiri kuwa Mungu ni pendo.PKSw 517.4

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents