Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 1—Kuharibiwa kwa Yerusalemu

  “Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako” (Luka 19:42-44).PKSw 11.1

  Akiwa katika kilele cha Mlima wa Mizeituni, Yesu aliutazama mji wa Yerusalemu. Mji uliokuwa na mwonekano mzuri na uliojaa amani ulitanda mbele Yake. Ilikuwa majira ya Pasaka, na kutoka nchi zote wana wa Yakobo walikuwa wamekusanyika hapo kusherehekea siku kuu hiyo kubwa ya kitaifa. Katikati ya bustani na mashamba ya mizababu, na miteremko ya kijani iliyokuwa imepambwa kwa mahema ya mahujaji, viliinuka vilima, majengo ya kifalme, na kuta kubwa za mji mkuu wa Israeli. Ni kama vile binti Sayuni alionekana kwa kiburi chake akisema, nimeketi malkia na sitaona huzuni; akijiona mzuri, na akidhani kuwa yuko salama kwa sababu ya kupendelewa na Mbingu, sawa na wakati, zama nyingi zilizopita, mwimbaji wa nyumba ya mfalme alipoimba: “Kuinuka kwake ni mzuri sana, Ni furaha ya dunia yote. Mlima Sayuni,...Mji wa Mfalme mkuu” (Zaburi 48:2). Majengo mazuri ya hekalu yalikuwa yakionekana vizuri sana. Miale ya jua lililokuwa likizama iliakisiwa na weupe uliofanana na theluji wa marumaru za kuta zake na kuifanya rangi ya dhahabu ya lango na mnara na ncha ya mnara, kung'ara. “Ukamilifu wa uzuri” ulisimama, kiburi cha taifa la Wayahudi. Ni mtoto gani wa Israeli ambaye angetazama mwonekano wa mji ule asipate msisimko wa furaha na kupigwa butwaa! Lakini fikra za Yesu zilijazwa na mawazo mengine. “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia” (Luka 19:41). Katikati ya shangwe na furaha kuu ya Yesu kuingia mji wa Yerusalemu, wakati matawi ya mitende yalipokuwa yakipeperushwa hewani kwa madaha, wakati hosana zenye nderemo na bashasha zilipoamsha miangwi ya milima, na maelfu ya sauti yalipomtangaza kuwa Mfalme, Mkombozi wa ulimwengu aligubikwa na huzuni iliyofichika. Yeye, Mwana wa Mungu, Ahadi ya Israeli, ambaye nguvu zake zilishinda mauti na kuwaita mateka wa mauti kutoka kaburini, alibubujikwa machozi, siyo machozi ya kawaida, bali machozi yaliyotokana na uchungu mzito, yaliyotokana na maumivu makali yasiyovumilika.PKSw 11.2

  Machozi Yake hayakuwa kwa ajili Yake Mwenyewe, japokuwa alijua vema kule nyayo Zake zilikokuwa zikielekea. Mbele Yake kulikuwa na Gethsemane, mahali pa maumivu Yake yaliyokuwa yanakaribia. Mlango wa kondoo ulikuwa mbele Yake pia, mlango ambao kwa karne nyingi wanyama wa kafara walipitishiwa, ambao ulikuwa tayari umeshafunguliwa kwa ajili Yake ili “apelekwe machinjoni” (Isaya 53:7). Kalwari, mahali aliposulubiwa, hapakuwa mbali. Kwenye njia ambayo Kristo angepita muda si mrefu ilipasa pajae hofu ya giza kuu wakati alipotoa roho Yake kuwa sadaka kwa ajili ya dhambi. Pamoja na hayo, tafakari juu ya matukio hayo haikuwa sababu ya giza lililokuwa juu Yake wakati wa saa ya furaha. Hakuna tishio lo lote la maumivu dhidi ya mwili Wake lilifunika roho Yake isiyokuwa na ubinafsi. Alililia maelfu ya watu wa Yerusalemu waliokuwa wanaelekea kuangamia—kwa sababu ya upofu na ugumu wa mioyo ya wale aliokuja kuwabariki na kuwaokoa.PKSw 11.3

  Historia ya zaidi ya miaka elfu moja ya upendeleo wa kipekee na utunzaji makini, uliooneshwa kwa watu waliochaguliwa, ilifunuliwa mbele ya Yesu. Kulikuwa na Mlima Moria, mahali ambapo mwana wa ahadi, kafara asiye na ubishi, alifungwa juu ya madhabahu—ishara ya sadaka ya Mwana wa Mungu. Pale, agano la baraka, ahadi tukufu ya Masihi, ilithibitishwa kwa baba yao watu walio waaminifu (Mwanzo 22:9, 16-18). Pale, ndimi za moto wa kafara zilizopanda juu mbinguni kutoka katika sakafu ya kupuria nafaka ya Ornani ziliweka kando upanga wa malaika anayeangamiza (1 Nyakati 21)—alama stahiki ya kafara ya Mwokozi na upatanisho kwa ajili ya wanadamu wenye hatia. Yerusalemu iliheshimiwa na Mungu kuliko miji mingine yote duniani. Bwana “aliuchagua Sayuni,” “Alitaka uwe makao Yake” (Zaburi 132:13). Pale, kwa miaka mingi, manabii watakatifu walitangaza ujumbe wao wa onyo. Pale, makuhani walipepea vyetezo vyao, na wingu la uvumba, pamoja na maombi ya watu waliokuja kuabudu, lilipaa juu hadi mbele za Mungu. Pale, kila siku damu ya wanakondoo waliochinjwa ilitolewa, ikielekeza kwa Mwanakondoo wa Mungu ajaye. Pale, Yehova alifunua uwepo Wake katika wingu la utukufu juu ya kiti cha rehema. Pale, palikaliwa na ncha ya ngazi ya kimuujiza iliyounganisha nchi na mbingu (Mwanzo 28:12; Yohana 1:51)—ngazi ile ambayo juu yake malaika wa Mungu walishuka na kupanda, na ambayo ilifungulia ulimwengu njia ya kuingia mahali patakatifu mno. Ikiwa taifa la Israeli lingedumisha utii wake kwa Mbingu, Yerusalemu ungedumu kuwa mji mteule wa Mungu milele zote (Yeremia 17:21-25). Lakini historia ya wale watu waliopata upendeleo ilikuwa kumbukumbu ya kurudi nyuma na kuasi. Walipinga neema ya Mbingu, walitumia vibaya nafasi zao za upendeleo, na walichezea fursa zao.PKSw 12.1

  Ingawa Israeli “waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno Yake, na kuwacheka manabii wake” (2 Nyakati 36:16), bado Mungu alijifunua kwao kuwa “Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli” (Kutoka 34:6); licha ya kukataliwa mara nyingi, rehema Yake iliendelea kuwasihi. Kwa upendo na huruma inayozidi ya baba kwa mtoto wake mpendwa, Mungu “akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake” (2 Nyakati 36:15). Wakati hoja, nasaha, na maonyo viliposhindwa, aliwatumia zawadi bora kabisa kuliko zote kutoka mbinguni; ndiyo, alitoa mbingu yote kupitia zawadi hiyo moja.PKSw 12.2

  Mwana wa Mungu mwenyewe alitumwa aubembeleze mji usiotubu. Kristo ndiye aliyewaleta Israeli kama mzabibu kutoka Misri (Zaburi 80:8). Mkono Wake Mwenyewe uliyaondoa mataifa ya kipagani mbele yao. Aliwapanda Israeli “Kilimani penye kuzaa sana.” Ulinzi na utunzaji Wake ulikuwa wigo uliolizunguka shamba pande zote. Watumishi Wake walitumwa kulitunza. “Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu,” alieleza, “nisiyoitenda?” (Isaya 5:1-4). Ingawa alitarajia kuwa lingezaa zabibu, lilizaa zabibu mwitu, lakini bado akiwa na tumaini la kuzaa zabibu alikuja Mwenyewe kushughulikia shamba Lake. Alililima shamba Lake; alilipogolea na kulipalilia. Alikuwa na juhudi zisizochoka za kuliokoa shamba Lake alilolipanda Mwenyewe.PKSw 13.1

  Kwa miaka mitatu Bwana wa nuru na utukufu aliingia na kutoka miongoni mwa watu Wake. Naye “akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi,” kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, viwete waweze kwenda, wenye ukoma watakaswe, viziwi wasikie, wafu wapate kufufuliwa, na maskini wahubiriwe habari njema (Matendo 10:38; Luka 4:18; Mathayo 11:5). Wito wa neema unatolewa kwa makundi yote ya watu: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28).PKSw 13.2

  Ingawa alizawadiwa ubaya kwa wema, na chuki kwa upendo Wake (Zaburi 109:5), aliendelea kutekeleza utume Wake wa rehema. Kamwe hakuwafukuza wale wote waliotafuta rehema Kwake. Msafiri asiyekuwa na makao rasmi, aibu na umaskini vikiwa ndiyo sehemu ya maisha Yake, aliishi kukidhi mahitaji na kupunguza maumivu ya watu, akiwasihi waipokee zawadi ya uzima. Mawimbi ya neema, yaliyorudishwa nyuma na watu wenye mioyo migumu, yalirudi katika mkondo wenye nguvu zaidi wa huruma na upendo usioelezeka. Lakini Israeli walikuwa wamemwacha Rafiki mwema na Msaidizi wao pekee. Wito Wake wa upendo ulipuuzwa, mashauri Yake yalitupiliwa mbali, na maonyo Yake yalidhihakiwa.PKSw 13.3

  Saa ya tumaini na msamaha ilikuwa ikipita haraka; kikombe cha hasira ya Mungu iliyokawizwa kilikuwa karibu sana kujaa. Wingu lililokuwa likijikusanya katika zama zote za uvunjaji wa sheria na uasi, sasa likiwa na weusi wa huzuni, lilikuwa linakaribia kuwapasukia watu wenye hatia; na Yeye ambaye peke Yake angeweza kuwaokoa dhidi ya hatari iliyowakabili alikuwa amepuuzwa, amekejeliwa, amekataliwa, na alikuwa karibu kusulubiwa. Wakati ambao Kristo angening'inizwa juu ya msalaba wa Kalwari, ndiyo siku ambayo Israeli kama taifa lililopendelewa na lililobarikiwa na Mungu lingekoma. Kupotea kwa roho hata moja ni janga kubwa zaidi kuliko faida na hazina za ulimwengu; lakini Kristo alipoutazama Yerusalemu, kuangamia kwa mji wote, taifa lote, kulikuwa mbele Yake—mji ule, taifa lile, ambalo awali lilikuwa taifa teule la Mungu, hazina Yake ya ajabu.PKSw 13.4

  Manabii walilia machozi kwa ajili ya uasi wa Israeli na ukiwa wa kutisha ambao dhambi iliuleta kwa Waisraeli. Yeremia alitamani macho yake yawe chemchemi ya machozi, ili aweze kulia usiku na mchana kwa ajili ya mauaji ya binti wa watu wake, kwa ajili ya kundi la Bwana ambalo lilikuwa limechukuliwa mateka (Yeremia 9:1; 13:17). Kwa misingi hiyo, huzuni ya Yule ambaye mtupo Wake wa jicho la kiunabii ulihusisha siyo miaka tu, bali ulihusisha vizazi vingi, ilikuwa kubwa kiasi gani! Alimwona malaika mwuaji akiwa na upanga ulioinuliwa dhidi ya mji ambao kwa muda mrefu ulikuwa makazi ya Yehova. Kutoka katika mlima wa Mizeituni, mahali ambapo baadaye Tito na jeshi lake walisimama, alitazama ng'ambo ya bonde na kuona ukumbi na malango ya kuingia ukumbini, na kwa macho yaliyojaa machozi aliona, kwa maono ya kutisha, kuta zilizozungukwa na majeshi ya kigeni. Alisikia vishindo vya nyayo za majeshi ikienda vitani. Alisikia sauti za akina mama na watoto wakililia mkate katika mji uliozingirwa. Aliona nyumba nzuri, majengo ya kifalme, na minara ya Yerusalemu, vikiwaka moto, na mahali viliposimama, pakiwa na rundo la mabaki yaliyokuwa yakiungua moto.PKSw 14.1

  Akiangalia matukio ya zama zijazo, aliwaona watu wa agano wakiwa wametawanyika katika kila nchi, “kama mabaki ya ajali katika pwani ya jangwani.” Katika kisasi cha muda mfupi kilichokuwa karibu kuwaangukia watoto wake, aliona mkupuo wa kwanza kutoka katika kikombe cha hasira ya Bwana ambacho wakati wa hukumu ya mwisho itawapasa kukinywa mpaka tone la mwisho. Huruma ya Kimungu, upendo wenye kujali, ulioneshwa katika maneno haya ya huzuni: “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!” Ee Israeli, ambaye ulikuwa taifa lililopendelewa na Mungu zaidi ya mataifa mengine, laiti ungelijua wakati wa kujiliwa kwako, na mambo yapasayo amani yako! Nimemzuia malaika wa haki, nimekuita upate kutubu, lakini bila mafanikio. Siyo tu watumishi, wajumbe, na manabii, ambao umewagomea na kuwakataa, lakini umemkataa pia Mtakatifu wa Israeli, Mkombozi wako. Ikiwa utaangamia, utawajibika peke yako. “Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima” (Mathayo 23:37; Yohana 5:40).PKSw 14.2

  Kristo aliuona mji wa Yerusalemu kama mfano wa ulimwengu uliofanywa kuwa mgumu kwa kutokuamini na uasi, na kuharakisha kukutana na hukumu za adhabu za Mungu. Maumivu ya kizazi kilichoanguka, yakimsonga rohoni Mwake, yalilazimisha kilio chenye uchungu mwingi kutoka katika midomo Yake. Aliona kumbukumbu ya dhambi ikiwa katika mateso, machozi, na damu ya wanadamu; moyo Wake ulijaa huruma isiyokuwa na kikomo kwa ajili ya watu wanaoteseka na wanaoumia duniani; alitamani kuwasaidia wote. Lakini hata kama mkono Wake ungeweza kurudisha nyuma mkondo wa maumivu ya wanadamu; wachache wangetafuta Chanzo chao pekee cha msaada. Alikuwa tayari kumimina roho Yake hadi kifo, kuuleta wokovu mahali ambapo wangeweza kuupata; lakini wachache ambao wangemwendea ili wapate uzima.PKSw 15.1

  Mfalme wa mbinguni anatokwa machozi! Mwana wa Mungu wa milele anaumia moyoni, anainama kwa uchungu! Tukio lile lilileta mshangao mbinguni. Tukio lile linadhihirisha ubaya usio wa kawaida wa dhambi; linaonesha jinsi ambavyo kazi ya kumwokoa mwenye hatia kutoka katika matokeo ya kuasi sheria ya Mungu ilivyo ngumu hata kwa Mungu Mwenyewe. Yesu, akitazama hadi kizazi cha mwisho, aliona ulimwengu utakavyojihusisha na uongo unaofanana na huo uliosababisha uharibifu wa Yerusalemu. Dhambi kubwa ya Wayahudi ilikuwa kumkataa Kristo; dhambi kubwa ya ulimwengu wa Wakristo ni kuikataa sheria ya Mungu, msingi wa serikali Yake mbinguni na duniani. Kanuni za Yehova zitadharauliwa na kuhesabiwa kuwa si kitu. Mamilioni katika utumwa wa dhambi, watumwa wa Shetani, wakikabiliwa na mauti ya pili, wangekataa kusikiliza maneno ya ukweli katika siku ya kujiliwa kwao. Upofu wa kutisha! Kupumbazika kwa ajabu sana!PKSw 15.2

  Siku mbili kabla ya Pasaka, wakati Kristo alipokuwa ameondoka hekaluni kwa mara ya mwisho, baada ya kukemea unafiki wa viongozi wa Wayahudi, alitoka tena na wanafunzi Wake hadi katika Mlima wa Mizeituni na alikaa pamoja nao kwenye mteremko wenye nyasi upande unaotazamana na mji wa Yerusalemu. Kwa mara nyingine tena alizitazama kuta zake, minara yake, na nyumba zake za kifalme. Mara nyingine tena alilitazama hekalu katika mwangaza wake wa kushangaza, taji la uzuri likiufunika mlima matakatifu.PKSw 15.3

  Miaka elfu moja kabla, mwandishi wa Zaburi alieleza vizuri upendeleo wa Mungu kwa Waisraeli kwa kulifanya hekalu lao kuwa mahali Pake pa kukaa:“Kibanda chake pia kiko Salemu, Na maskani yake iko Sayuni.” Bali “aliichagua kabila ya Yuda, Mlima Sayuni alioupenda. Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele” (Zaburi 76:2; 78:68, 69). Hekalu la kwanza lilijengwa wakati wa kipindi cha mafanikio makubwa ya historia ya Israeli. Akiba kubwa ya hazina kwa ajili ya kusudi hili ilikusanywa na Mfalme Daudi, na mipango kwa ajili ya ujenzi wake ilifanywa kwa uongozi wa Mungu (1 Nyakati 28:12, 19). Suleimani, mfalme mwenye hekima kuliko wafalme wote wa Israeli, alitekeleza kazi ya ujenzi. Hekalu hili lilikuwa jengo zuri ajabu ambalo ulimwengu ulikuwa haujawahi kuliona. Pamoja na hayo, Bwana alitangaza kupitia kwa nabii Hagai, kuhusiana na hekalu la pili: “Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza.” “Nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema Bwana wa majeshi” (Hagai 2:9, 7).PKSw 15.4

  Baada ya kuharibiwa kwa hekalu na Nebukadneza lilijengwa upya takribani miaka mia tano kabla ya kuzaliwa kwa Kristo na watu ambao walitoka katika utumwa wa miaka mingi waliorudi katka nchi iliyoharibika na kukaribia kutelekezwa. Wakati huo walikuwepo miongoni mwao wazee walioona utukufu wa hekalu la Sulemani, na ambao walililia kwenye msingi wa jengo jipya, kuwa lilikuwa lazima liwe chini ya viwango vya lile la awali. Hisia zilizokuwepo zinaelezwa vizuri na nabii: “Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu?” (Hagai 2:3; Ezra 3:12). Ndipo ahadi ilipotolewa kuwa utukufu wa hekalu la baadaye utakuwa mkubwa zaidi ya lile la kwanza.PKSw 16.1

  Lakini hekalu la pili halikuwa sawa na la kwanza katika uzuri; wala halikutukuzwa kwa viashiria vinavyoonekana vya uwepo wa Mungu kama vilivyoonekana katika hekalu la kwanza. Hakukuwa na udhihirisho wo wote wa wazi wa nguvu zisizokuwa za kawaida wakati wa uwekaji wakfu wake. Hakuna wingu la utukufu lililoonekana likijaza hekalu jipya. Hakuna moto ulioshuka kutoka mbinguni kuunguza kafara juu ya madhabahu. Shekina haikuwepo tena kati ya makerubi ndani ya patakatifu pa patakatifu; sanduku la agano, kiti cha rehema, na meza za ushuhuda havikuwemo humo. Hakuna sauti iliyotoka mbinguni kumjibu kuhani aliyeuliza kuhusiana na mapenzi ya Yehova.PKSw 16.2

  Kwa karne nyingi Wayahudi walijaribu bila mafanikio kuonesha ni wapi ahadi iliyotolewa na Mungu kwa njia ya Hagai ilikuwa imetimizwa; hata hivyo kiburi na kutokuamini vilipofusha akili zao zisielewe maana halisi ya maneno ya nabii. Hekalu la pili halikuheshimiwa kwa wingu la utukufu wa Yehova, bali kwa uwepo mbashara wa Yule ambaye utimilifu wa Uungu unakaa ndani Yake kwa jinsi ya kimwili— ambaye alikuwa Mungu Mwenyewe aliyejidhihirisha katika mwili. Yeye ambaye ni “Shauku ya mataifa yote” alikuja katika hekalu Lake wakati Mtu wa Nazareti alipofundisha na kuponya katika ukumbi mtakatifu. Kwa uwepo wa Kristo, na kwa njia hii tu, ndiyo utukufu wa hekalu la pili ulizidi utukufu wa lile la kwanza. Lakini Israeli walikuwa wamemkataa Yeye aliyekuwa zawadi kutoka mbinguni. Kwa Mwalimu mnyenyekevu ambaye siku ile alitoka nje kupita lango lake la dhahabu, utukufu ulikuwa umeondoka katika hekalu milele. Tayari maneno ya Mwokozi yalikuwa yametimizwa: “Nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa” (Mathayo 23:38).PKSw 16.3

  Wanafunzi walipata mshtuko na mshangao kwa sababu ya utabiri wa Kristo wa kutekwa kwa hekalu, na walitamani kuelewa kikamilifu zaidi maana ya maneno Yake. Mali, kazi, na stadi za ujenzi zilikuwa zimetumika sana kuboresha uzuri wake. Herode Mkuu alikuwa amewekeza kwenye jengo hili kwa kutumia utajiri wa Kirumi na hazina ya Kiyahudi, na hata mfalme wa ulimwengu alileta zawadi kwa ajili ya uboreshaji wa hekalu. Matofali ya marumaru, yenye ukubwa wa ajabu, yaliyosafirishwa kutoka Rumi kwa kusudi hilo, yalikuwa sehemu ya jengo hilo; na haya ndiyo matofali ambayo wanafunzi walikuwa wamemwonesha Bwana wao, wakisema: “Tazama, yalivyo mawe na majengo haya!” (Marko 13:1).PKSw 17.1

  Kwa maneno haya, Yesu alitoa jibu la kushangaza na kushitua: “Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa” (Mathayo 24:2).PKSw 17.2

  Wanafunzi walihusianisha kuharibiwa kwa Yerusalemu na matukio ya kuja kwa Kristo Mwenyewe katika utukufu wa muda na kuketi kwenye kiti cha enzi cha ufalme wa ulimwengu wote, kuwaadhibu Wayahudi wasiotubu, na kulikomboa taifa kutoka katika kongwa la utumwa wa Kirumi. Bwana aliwaambia kuwa angekuja mara ya pili. Hivyo kwa kutaja hukumu za Yerusalemu, akili zao zilirejelea kuja kule; na walipokuwa wamekusanyika pamoja wakimzunguka Mwokozi juu ya Mlima wa Mizeituni, waliuliza: “Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?” (Aya ya 3).PKSw 17.3

  Wanafunzi walifichwa mambo yajayo kwa kuhurumiwa. Ikiwa wakati ule wangejua kikamilifu mambo mawili ya kutisha ya kweli— mateso na mauti ya Mkombozi, na kuharibiwa kwa mji wao na hekalu lao—wangezidiwa na hofu. Kristo aliwaeleza kwa muhtasari matukio makuu yaliyopaswa kutokea kabla ya mwisho wa wakati. Maneno Yake hayakueleweka kikamilifu wakati ule; lakini maana yake ingefunuliwa kwa kadiri watu Wake walivyohitaji maelekezo yaliyokuwa ndani yake. Unabii alioutoa ulikuwa na maana mbilia; wakati ukieleza kuharibiwa kwa Yerusalemu, uliwakilisha vitisho vya siku ya mwisho.PKSw 17.4

  Yesu aliwaeleza wanafunzi waliokuwa wakimsikiliza hukumu zilizowakabili Waisraeli walioasi, na hususani hukumu ya adhabu iliyowakabili kwa kumkataa na kumsulubisha Masihi. Ishara zisizoweza kukosewa zingetangulia kilele cha kutisha. Saa ya kutisha ingekuja kwa ghafla na haraka. Na Mwokozi aliwaonya wafuasi Wake:“Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani” (Mathayo 24:15, 16; Luka 21:20, 21). Wakati bendera za ibada ya sanamu za Warumi zitakaposimikwa katika uwanja mtakatifu, ambao ulipanuka na kwenda kilomita kadhaa nje ya kuta za mji, ndipo wafuasi wa Kristo iliwapasa kukimbia kwa ajili ya usalama wao. Wakati ishara ya onyo ilipoonekana, wale waliotaka kukimbia iliwapasa wasichelewe. Katika nchi yote ya Yuda, pamoja na mji wa Yerusalemu wenyewe, ishara ya kukimbia ilipaswa kutiiwa mara moja. Mtu aliyekutwa juu ya nyumba hakupaswa kuteremka na kuingia ndani ya nyumba yake, hata kuokoa hazina yake ya thamani kubwa. Watu waliokuwa wakifanya kazi mashambani au wakishughulikia mizabibu hawakupaswa kupoteza muda kwa kurudi kuchukua vazi lao la nje walilolivua wakati wakipambana na kazi kwa ajili ya joto la mchana. Hawakupaswa kusita-sita hata kwa muda mfupi sana, ili wasikumbwe na uharibifu wa jumla.PKSw 17.5

  Wakati wa utawala wa Herode, siyo tu kuwa Yerusalemu ulikuwa umependezeshwa, bali pia kwa kujenga minara, kuta, na ngome, vikiongeza uimara wa asili wa mazingira yake, ulikuwa umefanyiwa uzio usioweza kupenywa kirahisi. Mtu ambaye wakati huu angebashiri hadharani juu ya uangamizaji wake, kama Nuhu katika siku zake, angeitwa mropokaji kichaa atangazaye mambo yaletayo hofu. Lakini Kriso alisema: “Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe” (Mathayo 24:35). Kwa sababu ya dhambi zake, hasira ilikuwa imetangazwa dhidi ya Yerusalemu, na usugu wake wa kutokuwa na imani ulifanya uharibifu wake uwe wa hakika.PKSw 18.1

  Bwana alikuwa ametangaza kupitia kwa nabii Mika: “Sikieni haya, tafadhali, enyi vichwa vya nyumba ya Yakobo, mnaoitawala nyumba ya Israeli, mnaochukia hukumu, na kuipotosha adili. Wanaijenga Sayuni kwa damu, na Yerusalemu kwa uovu. Wakuu wake huhukumu ili wapate rushwa, na makuhani wake hufundisha ili wapate ijara, na manabii wake hubashiri ili wapate fedha; ila hata hivyo watamtegemea Bwana, na kusema, Je! Hayupo Bwana katikati yetu? Hapana neno baya lo lote litakalotufikia” (Mika 3:9-11).PKSw 18.2

  Maneno haya yalieleza kwa uaminifu hali ya wakazi wa Yerusalemu waliojawa na ufisadi na kujihesabia haki. Huku wakidai kutimiza matakwa ya sheria ya Mungu kikamilifu, walikuwa wakivunja kanuni zake. Walimchukia Kristo kwa sababu usafi na utakatifu Wake vilifunua uovu wao; na walimshitaki kuwa Yeye ndiye aliyekuwa chanzo cha taabu zilizowakabili kama matokeo ya dhambi zao. Ingawa walijua kuwa hakuwa na dhambi yo yote, walitangaza kuwa kifo chake kilikuwa cha lazima kwa ajili ya usalama wao kama taifa. “Tukimwacha hivi,” viongozi wa Kiyahudi walisema, “watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu” (Yohana 11:48). Ikiwa Kristo atasulubiwa, wangeweza tena kuwa na nguvu, watu walioungana. Hivyo ndivyo walivyofikiri, na walikubaliana na uamuzi wa kuhani mkuu, kuwa ilikuwa bora kwa mtu mmoja kufa kuliko taifa zima kuangamia.PKSw 18.3

  Hivyo ndivyo viongozi wa Kiyahudi walivyoijenga “Sayuni kwa damu, naYerusalemu kwa uovu” (Mika 3:10). Na bado, wakati walimwua Mwokozi wao kwa sababu ya kukemea dhambi zao, kujihesabia haki kwao kulikuwa kukubwa mno kiasi kwamba walijihesabu kuwa watu waliopendelewa na Mungu na walitarajia awaokoe dhidi ya maadui zao. “Basi,” nabii aliendelea, “kwa ajili yenu, Sayuni utalimwa kama shamba lilimwavyo, na Yerusalemu utakuwa magofu; na mlima wa nyumba utakuwa kama mahali palipoinuka msituni” (Aya ya 12).PKSw 19.1

  Kwa karibu miaka arobaini baada ya uharibifu wa Yerusalemu kutangazwa na Kristo Mwenyewe, Bwana alizuia hukumu Yake juu ya mji na taifa. Uvumilivu wa Mungu ulikuwa wa ajabu kwa watu waliokataa injili Yake na wauaji wa Mwana Wake. Mfano wa mtini usiozaa matunda uliwakilisha jinsi Mungu alivyoshughulika na taifa la Kiyahudi. Amri ilikuwa imetolewa, “Uukate, mbona hata nchi unaiharibu?” (Luka 13:7) lakini rehema ya Mungu iliuacha kwa muda mrefu kidogo zaidi. Kulikuwepo bado wengi miongoni mwa Wayahudi waliokuwa hawajui tabia na kazi ya Kristo. Na watoto walikuwa hawajapata fursa au nuru ambayo wazazi wao walikuwa wameitupilia mbali. Kwa njia ya mahubiri ya mitume na washirika wao, Mungu angewezesha nuru kuwaangazia; wangeweza kuruhusiwa kuona jinsi unabii ulivyokuwa umetimizwa, siyo katika kuzaliwa na maisha ya Kristo, lakini pia katika kifo na ufufuo. Watoto hawakuhukumiwa kwa dhambi za wazazi wao; bali wakati, wakiwa na ujuzi wa nuru yote iliyotolewa kwa wazazi wao, watoto walipokataa nuru ya nyongeza waliyopewa wenyewe, walikuwa washirika wa dhambi za wazazi wao, na walijaza kipimo cha uovu wao.PKSw 19.2

  Uvumilivu wa Mungu kwa wakazi wa Yerusalemu ulizidi kuwafanya wakomaze shingo zao zaidi katika uasi. Kwa chuki na ukatili wao dhidi ya wanafunzi wa Yesu walikataa nafasi yao ya mwisho ya rehema. Ndipo Mungu alipoondoa ulinzi Wake kwao na kuondoa nguvu Yake ya kumzuia Shetani na malaika zake, na taifa likaachwa katika utawala wa kiongozi waliyemchagua. Watoto wao waliitupilia mbali neema ya Kristo, ambayo ingewawezesha kudhibiti misukumo yao ya uovu, na sasa misukumo hii ilipata ushindi. Shetani aliamsha misisimko mikali na hatarishi ndani ya mioyo yao. Watu walipoteza uwezo wao wa kufikiri vizuri; walikuwa kama vichaa—walitawaliwa na mihemko na hasira iliyopofushwa. Walibadilika na kuwa kama mashetani katika ukatili wao. Katika familia na katika taifa, miongoni mwa matabaka ya juu na ya chini sawia, kulikuwa kutoaminiana, kijicho, ugomvi, uasi, na mauaji. Usalama ulitoweka kila mahali. Marafiki na ndugu wa karibu walisalitiana. Wazazi waliwachinja watoto wao, na watoto waliwachinja wazazi wao. Watawala wa watu hawakuwa na uwezo wa kujitawala wenyewe. Misisimko isiyodhibitiwa iliwafanya kuwa wakatili kupindukia. Wayahudi waliukubali ushuhuda wa uongo kumhukumu Mwana wa Mungu aliyekuwa hana hatia yo yote. Sasa mashitaka ya uongo yalifanya maisha yao kuwa ya wasiwasi. Kwa matendo yao walikuwa wakisema kwa muda mrefu: “Mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu” (Isaya 30:11). Sasa hitaji lao lilikidhiwa. Hofu ya Mungu haikuwasumbua tena. Shetani ndiye aliyekuwa kiongozi wa taifa, na mamlaka ya juu kabisa ya kiraia na kidini vilikuwa chini ya utawala wake.PKSw 19.3

  Nyakati zingine, viongozi wa vikundi hasimu waliungana kupora na kutesa wahanga wao wasioweza kujitetea, na tena waliangukiana wao kwa wao kwa majeshi ya kikundi kimoja kuangukia kikundi hasimu na walichinjana bila huruma. Hata utakatifu wa hekalu haukuweza kudhibiti ukatili wao wa kutisha. Waabuduji walipigwa na kuuawa mbele ya madhabahu, na patakatifu palinajisiwa kwa miili ya watu waliochinjwa. Hata hivyo, katika upofu wao na kiburi chenye kufuru wachochezi wa kazi hii ya kuzimu walitangaza hadharani kuwa walikuwa hawana hofu kuwa Yerusalemu ingeangamizwa, kwa kuwa ulikuwa mji wa Mungu Mwenyewe. Kuimarisha zaidi nguvu zao, waliwahonga manabii wa uongo watangaze, hata wakati majeshi ya Kirumi walipokuwa wakilizingira hekalu, kuwa watu walipaswa kusubiri ukombozi kutoka kwa Mungu. Hatimaye, watu wengi walishikilia kwa bidii imani kuwa Mungu Aliye Juu angeingilia kati na kuwashinda maadui zao. Lakini Israeli alikuwa ameshatupilia mbali ulinzi wa Mungu, na sasa hakuwa na ulinzi. Yerusalemu wenye huzuni! Ukiwa umeraruliwa na mipasuko ya ndani, damu ya watoto wake waliochinjwa kwa mikono yao wenyewe mmoja dhidi ya mwenzake ikiweka wekundu kwenye mitaa yake, wakati majeshi ya kigeni yalipoangusha ngome zake na kuwaua watu wake wa vita!PKSw 20.1

  Mambo yote yaliyoelezwa katika utabiri uliotolewa na Kristo kuhusiana na kuharibiwa kwa Yerusalemu yalitimizwa. Wayahudi walishuhudia ukweli wa maneno Yake ya onyo: “Na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa” (Mathayo 7:2).PKSw 20.2

  Ishara na maajabu vilitokea, majanga na matatizo ya kutisha yalitokea. Katikati ya usiku mwangaza usio wa kawaida uliangaza juu ya hekalu na madhabahu. Juu ya mawingu wakati wa jua kuzama zilichorwa picha za magari na watu wa vita wakijikusanya kwa ajili ya vita. Makuhani waliokuwa wakihudumu usiku katika patakatifu walitishwa na sauti za ajabu; dunia ilitetemeka, na sauti nyingi zilisikika zikipiga kelele: “Tuondoke haraka.” Lango la mashariki, ambalo lilikuwa zito sana kiasi kwamba lilifungwa na watu ishirini kwa shida, na ambalo lilikuwa limefungwa kwa nondo kubwa za chuma zilizofungwa kwa uimara katika sakafu yam awe magumu, lilifunguliwa usiku bila mfunguaji ye yote anayeonekana.—Milman, The History of the Jews, book 13.PKSw 20.3

  Kwa miaka saba mtu mmoja aliendelea kuzunguka akienda na kushuka katika mitaa ya Yerusalemu, akitangaza majanga yaliyokuwa yanaujia mji. Mchana na usiku aliimba wimbo wa ajabu: “Sauti kutoka mashariki! Sauti kutoka magharibi! Sauti kutoka pepo nne! Sauti dhidi ya Yerusalemu na dhidi ya hekalu! Sauti dhidi ya mabwana harusi na mabibi harusi! Sauti dhidi ya watu wote!”—Ibid. kiumbe huyu wa ajabu alifungwa na kuchpawa mijeledi, lakini hakuna neno la manung'uniko lilitoka katika midomo yake. Jibu lake kwa matusi na dharau aliyofanyiwa lilikuwa: “Ole, ole wako Yerusalemu!” “ole, ole wenu enyi wakazi wake!” Kilio chake cha onyo hakikukoma mpaka alipochinjwa katika maangamizi ambayo aliyatabiri.PKSw 21.1

  Hakuna Mkristo hata mmoja aliyeangamia katika kuharibiwa kwa Yerusalemu. Kristo alitoa onyo kwa wanafunzi Wake, na wote walioamini maneno Yake na kuzingatia ishara iliyoahidiwa. “Hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi,” alisema Yesu, “ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia. Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie” (Luka 21:20, 21). Baada ya Warumi chini ya Ketio kuuzunguka mji, bila kutarajiwa waliachana na kazi ya utekaji wakati kila kitu kilionekana kuwa tayari kwa ajili ya mashambulizi ya ghafla. Watekwaji, wakiwa katika hali ya kukata tamaa ya kuukabili na kuuzuia utekaji, walikuwa karibu kujisalimisha, wakati jenerali wa Kirumi aliporudisha nyuma majeshi yake bila sababu ya msingi. Lakini uongozi wa Mungu wenye rehema ulikuwa ukielekeza matukio kwa ajili ya mazuri kwa ajili ya watu Wake. Ishara iliyoahidiwa ilikuwa imetolewa kwa Wakristo waliokuwa wakisubiri, na sasa fursa ilitolewa kwa wote ambao wangependa, watii onyo la Mwokozi. Matukio yalidhibitiwa ili kwamba Wayahudi wala Warumi wasizuie Wakristo kukimbia. Kufuatia kurudi nyuma kwa Ketio, Wayahudi, wakishambulia kuanzia Yerusalemu, walilikimbiza jeshi lakei; na wakati majeshi yote mawili yalipokuwa yameumana katika pambano, Wakristo walipata fursa ya kuondoka mjini. Wakati huu mji ulikuwa hauna maadui wo wote ambao wangejaribu kuwazuia. Wakati wa shambulio, Wayahudi walikuwa wamekusanyika kuadhimisha Siku kuu ya Vibanda, na hivyo Wakristo katika nchi nzima waliweza kukimbia bila bughudha yo yote. Bila kuchelewa walikimbilia mahali salama—mji wa Pela, katika nchi ya Perea, ng'ambo ya Yordani.PKSw 21.2

  Majeshi ya Kiyahudi, yaliyokuwa yakimshambulia Ketio na jeshi lake, waliwaangukia upande wao wa nyuma kwa nguvu sana kiasi cha kutishia kuwaangamiza kabisa. Ilikuwa kwa shida kubwa sana Warumi walifaulu kukimbia na kurudi nyuma. Wayahudi walifaulu kukimbia bila kupata hasira kubwa, na wakiwa na mali zao walizoziteka walirudi Yerusalemu kwa ushindi. Hata hivyo, ushindi huu wa juu juu uliwaletea matatizo makubwa. Uliwahamasisha kujenga roho ya upinzani na kiburi dhidi ya Warumi mambo ambayo yalisababisha madhara makubwa kwa mji uliokwisha kuhukumiwa kuharibiwa.PKSw 21.3

  Majanga ya kutisha yaliukumba mji wa Yerusalemu wakati utekaji uliotekelezwa mara ya pili na Tito. Mji ulishambuliwa wakati wa Pasaka, wakati mamilioni ya Wayahudi walipokuwa wamekusanyika ndani ya kuta. Maghala yao ya vyakula, ambayo kama yangetunzwa kwa uangalifu yangeliweza kuhifadhi vyakula vya kuwatosha wakazi wa Yerusalemu kwa miaka mingi, yalikuwa yameharibiwa kwa sababu ya wivu na ulipizaji kisasi wa makundi yaliyohasimiana, na sasa tishio la kufa kwa njaa liliwakabili. Kipimo kimoja cha ngano kiliuzwa kwa talanta moja. Maumivu ya njaa yalikuwa makali sana kiasi kwamba walitafuna ngozi za mikanda na gidamu za viatu vyao na mifuniko ya ngao zao. Idadi kubwa ya watu walitoroka usiku na kwenda kukusanya mimea ya porini iliyoota nje ya kuta za mji, japokuwa wengi wao walikamatwa na kuuliwa kwa mateso makali, na mara nyingi wale walioweza kurudi salama walinyang'anywa kile walichokuwa wamekikusanya katika mazingira mabaya na hatarishi. Mateso yasiyo na ubinadamu kabisa yalitumiwa na wale waliokuwa madarakani, kuwalazimisha walio na mahitaji wasalimishe chakula chochote kidogo ambacho walikuwa wamekificha. Na mambo haya ya ukatili hayakutendwa mara chache na watu ambao wao wenyewe walikuwa na chakula cha kutosha, na ambao lengo lao lilikuwa kujiwekea akiba kwa ajili ya wakati ujao.PKSw 22.1

  Maelfu ya watu walikufa kwa njaa na magonjwa. Upendo wa asili ulionekana kuharibiwa kabisa. Waume waliibia wake zao, na wake waliwaibia waume zao. Watoto waliweza kuonekana wakinyakua chakula kutoka katika midomo ya wazazi wao wazee. Swali la nabii, “Je, mwanamke aweza kumshahu mtoto wake anyonyae?” lilipata jibu ndani ya kuta za mji uliokuwa umezingirwa pande zote: “Mikono ya wanawake wenye huruma Imewatokosa watoto wao wenyewe; Walikuwa ndio chakula chao Katika uharibifu wa binti ya watu wangu” (Isaya 49:15; Maombolezo 4:10). Tena ulitimizwa unabii wa onyo uliotolewa karne kumi na nne kabla: “Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye hangehatarisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu ya binti yake,... na juu ya wanawe atakaowazaa; kwa kuwa atawala kwa siri, kwa uhitaji wa vitu vyote; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako” (Kumbukumbu 28:56, 57).PKSw 22.2

  Viongozi wa Kirumi walijaribu kuwatishia Wayahudi ili kuwafanya wajisalimishe. Wafungwa waliojaribu kupinga walipotekwa, walipigwa, waliteswa, na walisulubishwa mbele ya ukuta wa mji. Mamia waliuawa kwa njia hii, na kazi hii ya kuogofya iliendelea kufanywa mpaka, katika bonde lote la Yehoshati na Kalwari, misalaba ilisimikwa kwa wingi kiasi kwamba kulikuwa hakuna nafsi ya kupita katikati yake. Laana ile iliyotamkwa mbele ya kiti cha hukumu cha Pilato ililetelezwa kwa jinsi ya kutisha: “Damu Yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu” (Mathayo 27:25).PKSw 23.1

  Tito alikuwa tayari kusitisha zoezi hili la kutisha, na hivyo kutotekeleza kipimo kamili cha uharibifu wa mji wa Yerusalemu. Alitishika alipoona miili ya watu waliokufa ilivyorundikwa huko na huko katika mabonde. Kama mtu aliyeshikwa na butwaa, kutoka kilele cha mlima wa Mizeituni alitazama hekalu zuri na akatoa amri kuwa hata jiwe lake moja lisiguswe. Kabla ya kujaribu kuteka ngome hii, alitoa wito wa dhati kwa viongozi wa Kiyahudi wasimlazimishe kunajisi mahali patakatifu kwa damu. Ikiwa wangetoka na kupigania mahali pengine po pote, hakuna Mrumi ambaye angeharibu utakatifu wa hekalu. Josephus mwenyewe, kwa wito fasaha kabisa, aliwasihi wajisalimishe, ili wajiokoe wenyewe, mji wao, na mahali pao pa ibada. Lakini maneno yake yalijibiwa kwa laana kali. Mishale ilirushwa kumwelekea, mpatanishi wao wa mwisho wa kibinadamu, aliposimama kuwasihi. Wayahudi walikuwa wamekataa miito ya Mwana wa Mungu, na sasa malalamiko na nasaha viliwafanya wazidi kudhamiria kupinga mpaka mwisho. Juhudi za Tito kuliokoa hekalu hazikufua dafu; Yeye aliyekuwa mkuu kuliko yeye alikuwa ameshatangaza kuwa hakuna jiwe litakalosalia juu ya jiwe.PKSw 23.2

  Ukaidi na upofu wa viongozi wa Kiyahudi, na uhalifu unaotisha uliofanyika ndani ya mji uliozungukwa, vilichochea chuki na hasira ya Warumi, na Tito hatimaye aliamua kuliteka hekalu kwa nguvu. Aliazimia, hata hivyo, kuwa ikiwezekana hekalu lisiharibiwe. Lakini amri zake zilipuuzwa. Baada ya kupumzika katika hema lake usiku, Wayahudi, wakitokea katika hekalu waliwashambulia maaskari wa Kirumi kwa nje. Katika pambano, kijinga cha moto kilirushwa na askari kupitia uwazi wa lango, na kwa ghafla, vyumba vilivyonakshiwa kwa mierezi kando kando ya nyumba takatifu viliwaka moto. Tito alifanya haraka kwenda eneo la tukio, akiwa amefuatana na majenerali na majeshi yake, na aliwaamuru maskari wauzime moto. Maneno yake hayakusikilizwa. Kwa hasira maaskari walirusha vijinga vya moto katika vyumba vilivyoshikamana na hekalu, na ndipo kwa mapanga yao waliwachinja watu wengi sana waliokuwa wamejihifadhi katika vyumba hivyo. Damu ilibubujika katika ngazi za hekalu kama maji. Maelfu kwa maelfu ya Wayahudi waliangamia. Juu ya kelele za vita, sauti zilisikika zikisema: “Ikabodi!”—utukufu umeondoka.PKSw 23.3

  “Tito alishindwa kudhibiti hasira za maaskari; aliingia na maofisa wake, na kuchunguza eneo la ndani ya jengo takatifu. Uzuri wake uliwashangaza; na wakati ndimi za moto zilipokuwa bado hazijapenya na kuteketeza mahali patakatifu, alifanya juhudi zake za mwisho kupaokoa, alisogea mbele kwa haraka na kuwaagiza maaskari wasitishe zoezi la uchomaji moto hekalu. Mkuu wa kikosi husika, Liberalisi, alijaribu kuwalazimisha maofisa walio chini yake watii agizo; lakini hata heshima kwa mfalme ilishindwa na kuachia hasira na chuki dhidi ya Wayahudi, msisimko mkali wa vita, na tumaini na tamaa ya kupata nyara, vitawale. Maaskari waliona kila kitu kilichowazunguka kiking'aa kwa dhahabu iliyoakisi mwanga mkali wa ndimi za moto; walidhania kuwa hazina ya dhahabu isiyokuwa na hesabu iliwekwa mahali fulani katika hekalu. Askari mmoja, kwa siri, alichomeka kijinga cha moto katikati za bawaba za mlango: jengo lote liliwaka moto mara moja. Moshi uliopofusha na ukali wa joto la moto viliwalazimisha maaskari kurudi nyuma, na kuliacha jengo zuri likiteketea.PKSw 24.1

  “Lilikuwa tukio la kutisha kwa Mrumi—kwa Myahudi ilikuwaje? Kilele chote cha mlima uliotawala mji, kiliwaka moto kama volkano. Majengo yalianguka moja baada ya jingine, kwa mshindo mkuu, na yalimezwa katika utisho mkubwa wa moto. Mapaa ya mwerezi yalikuwa kama karatasi za ndimi za moto; vilele vya minara ya dhahabu viling'ara kama mikuki ya mwanga mwekundu; ngome za lango zilirusha juu mihimili ya ndimi za moto na moshi. Milima ya jirani ilimulikwa kwa mwanga; na makundi meusi ya watu yalionekana, watu waliangalia kwa wasiwasi na hofu maendeleo ya uharibifu: kando kando ya kuta na kwenye mitaa ya mji kulikuwa na nyuso nyingi, baadhi zikiwa nyeupe kwa uchungu wa kukata tamaa, nyingine zikiwa na mwonekano wa hasira na hitaji la kulipiza kisasi bila mafanikio. Kelele za maaskari wa Kirumi waliokuwa wakikimbia huku na huku, na vilio vya maaskari wa Kiyahudi waliokuwa wakiungua ndani ya ndimi za moto, zilichanganyika na ngurumo za moto na sauti kubwa za mbao zilizokuwa zikidondoka chini. Myangwi ya milima ilijibu au ilirudisha sauti za uchungu za watu waliokuwa juu ya vilele vya milima; kando kando ya kuta zote zilisikika sauti za miguno ya maumivu na vilio; watu waliokuwa wakielekea kukata roho kwa kukosa chakula kwa muda mrefu walijikaza kwa nguvu kidogo zilizobaki kutoa kilio cha uchungu na kukata tamaa.PKSw 24.2

  “Mauaji ya ndani yalikuwa ya kutisha zaidi kuliko mauji yaliyotokana na mashambulizi kutoka nje. Wanaume na wanawake, wazee na vijana, maaskari waasi na makuhani, waliopigana na wale waliosihi kuhurumiwa, wote walichinjwa na kuuliwa bila kuchagua. Idadi ya watu waliochinjwa ilikuwa kubwa kuliko idadi ya watu waliochinja. Majeshi ya Kirumi hayakuwa na budi kukanyaga marundo ya maiti ili waendelee na kazi yao ya kuangamiza.”—Milman, The History of the Jews, book 16.PKSw 24.3

  Baada ya kuharibu hekalu, mara moja mji wote uliangukia mikononi mwa Warumi. Viongozi wa Wayahudi walizikimbia ngome zao zisizopenywa kirahisi, na Tito aliwakuta wakiwa peke yao. Aliwatazama kwa mshangao, na alitangaza kuwa Mungu amewatia mikononi mwake; kwa kuwa hakuna zana yo yote, hata kama ingekuwa na nguvu kubwa kiasi gani, ingeweza kuhimili mapambano yale ya kutisha. Majengo ya mji na hekalu yaliungua hadi misingi yake, na uwanja mahali ambapo nyumba takatifu ilikuwa imesimama ulilimwa “kama shamba lilimwavyo” (Yeremia 26:18). Katika utekaji na uchinjaji uliofuata, zaidi ya watu milioni moja waliuawa; waliopona walichukuliwa mateka, waliuzwa kama watumwa, walikokotwa hadi Rumi kushuhudia ushindi wa mtekaji, walitupwa kwa wanyama wakali wa porini katika viwanja vya michezo, au walitawanywa kama watu wasio na makazi wazururaji duniani kote.PKSw 25.1

  Wayahudi walifua mikatale yao wenyewe; walikijaza kikombe cha kisasi wao wenyewe. Kwa uharibifu mkubwa uliowapata kama taifa, na kwa maumivu yaliyowafuata huko katika utawanyiko wao, walikuwa wakivuna mazao ambayo mikono yao ilikuwa imepanda. Nabii alisema: “Ee Israeli, umejiangamiza mwenyewe;” “maana umeanguka kwa sababu ya uovu wako” (Hosea 13:9; 14:1). Mateso yao mara nyingi yanawakilishwa kama adhabu iliyowasibu kwa agizo la Mungu moja kwa moja. Ndivyo mdanganyaji mkuu anavyojaribu kuficha kazi yake. Kwa kutupilia mbali upendo na neema ya Mungu kwa muda mrefu na kwa kiburi na shingo ngumu, Wayahudi walisababisha ulinzi wa Mungu uondolewe kutoka kwao, na Shetani aliruhusiwa kuwatawala kulingana na mapenzi yake. Ukatili wa kutisha katika kuiharibu Yerusalemu ni kielelezo cha nguvu ya Shetani isiyo na huruma juu ya wale wanaojiweka chini ya utawala wake.PKSw 25.2

  Hatuwezi kujua ni kiasi gani tunawiwa na Kristo kwa ajili ya amani na ulinzi tulio nao. Ni nguvu inayodhibiti ya Mungu inayozuia wanadamu wasiwe chini ya utawala wa Shetani kikamilifu. Wasiokuwa watiifu na wasio na shukurani wana sababu kubwa ya kushukuru rehema na uvumilivu wa Mungu kwa kudhibiti nguvu yenye ukatili na ubaya wa mwovu. Lakini watu wanapopita mipaka ya uvumilivu wa Mungu, udhibiti unaondolewa. Mungu hasimami mbele ya mwenye dhambi kama mtekelezaji wa hukumu dhidi ya makosa yake; lakini huwaacha waliotupilia mbali rehema yake washughulikiane wenyewe kwa wenyewe, wavune walichokipanda. Kila mwale wa nuru uliotupiliwa mbali, kila onyo lililodharauliwa au kutosikilizwa, kila tamaa iliyopaliliwa, kila uvunjaji wa sheria ya Mungu, ni mbegu iliyopandwa ambayo huzaa mavuno bila kukosea. Roho wa Mungu, anapopingwa kwa wakati wote, hatimaye huondolewa kutoka kwa mwenye dhambi, na ndipo haibaki tena nguvu ya kudhibiti tamaa mbaya za moyoni, na haubaki ulinzi dhidi ya ukatili na uadui wa Shetani. Uharibifu wa Yerusalemu ni onyo la kutisha na la dhati kwa wote wanaopuuza fursa za neema na wanaopinga miito ya rehema ya Mungu. Kamwe haujawahi kutolewa ushuhudi mkubwa zaidi kuliko huo juu ya chuki ya Mungu dhidi ya dhambi na adhabu ya hakika itakayowapata wenye hatia.PKSw 25.3

  Unabii wa Mwokozi kuhusu kumwagwa kwa hukumu juu ya Yerusalemu una utimizo mwingine, ambao kwao ukiwa ule wa kutisha ulikuwa kivuli hafifu tu. Katika kile kilichoupata mji mteule tunaweza kuona uharibifu wa ulimwengu ambao umekataa rehema ya Mungu na kuikanyaga sheria Yake. Kumbukumbu za taabu za wanadamu ambazo dunia imezishuhudia katika kipindi chake cha karne ndefu za uhalifu ni nyeusi. Moyo unaugua, na akili inazimia kwa kutafakari. Matokeo ya kukataa mamlaka ya Mbingu ni ya kutisha sana. Lakini tukio la kutisha zaidi limewasilishwa katika ufunuo wa wakati ujao. Kumbukumbu za matukio ya zamani,—mlolongo mrefu wa fujo, migogoro, na mapinduzi, “silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyofingirishwa katika damu” (Isaya 9:5),—haya ni nini, ukilinganisha na vitisho vya siku ile wakati Roho wa Mungu anayedhibiti uovu atakapoondolewa kwa waovu, ili asizuie mlipuko wa misisimko na hasira za kishetani! Ndipo ulimwengu utaona, kuliko ilivyowahi kutokea, matokeo ya utawala wa Shetani.PKSw 26.1

  Lakini katika siku ile, kama ilivyokuwa katika uharibifu wa Yerusalemu, watu wa Mungu watakombolewa, kila mmoja atakayeonekana ameandikwa miongoni mwa walio uzima (Isaya 4:3). Kristo alisema kuwa atakuja mara ya pili kuwakusanya waaminifu Wake awachukue Kwake: “Ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu” (Mathayo 24:30, 31). Ndipo wale ambao hawakuitii injili wataangamizwa kwa pumzi ya kinywa Chake na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo Kwake(2 Wathesalonike 2:8). Kama Israeli ya zamani waovu wanajiangamiza wenyewe; wanaanguka kwa uovu wao wenyewe. Kwa njia ya maisha yao ya dhambi, wanajiweka nje ya upatanifu na Mungu, asili zao zikiwa zimeharibiwa na uovu sana, kiasi ambacho kufunuliwa kwa utukufu Wake kunakuwa moto ulao.PKSw 26.2

  Hebu watu wawe waangalifu wasije wakapuuza somo lililotolewa kwao katika maneno ya Kristo. Kama alivyowaonya wanafunzi Wake kuhusu uharibifu wa Yerusalemu, kwa kuwapa ishara ya maangamizi yaliyokuwa yanakaribia, ili waweze kukimbia na kuponya nafsi zao; kadhalika ameuonya ulimwengu kuhusu siku ya uharibifu wa mwisho na amewapa ishara ya ukaribu wake, ili wale watakaopenda kuokoa nafsi zao waweze kuikimbia hasira inayokuja. Yesu alisema: “Kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa” (Luka 21:25; Mathayo 24:29; Marko 13:24-26; Ufunuo 6:1217). Wanaoziona ishara hizo za ujio Wake inawapasa watambue “kuwa yu karibu, mlangoni” (Mathayo 24:33). “Kesheni basi,” ndiyo maneno Yake ya onyo (Marko 13:35). Watakaotii onyo hawatabaki gizani, hata siku ile iwakute bila maandalizi. Bali kwa wale wasiokesha, “siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku” (1 Wathesalonike 5:2-5).PKSw 26.3

  Ulimwengu uko tayari zaidi kuukubali ujumbe wa wakati huu kuliko Wayahudi walivyokuwa tayari kupokea onyo kuhusu Yerusalemu. Bila kujali ni lini itafika, siku ya Mungu itakuja bila taarifa kwa watu wasiomcha Mungu. Wakati maisha yanaendelea katika hali yake ya kawaida ya siku zote; wakati watu wamemezwa katika starehe, katika biashara, katika usafiri, katika utafutaji wa pesa; wakati viongozi wa dini wanahamasisha maendeleo na elimu ya dunia, na watu wakiwa wanabembelezwa na usalama bandia—ndipo, kama mwizi anavyokuja usiku wa manane katika nyumba ambayo haina mlinzi, ndivyo uharibifu utakavyowajia wasiojali na wasiomcha Mungu, “wala hakika hawataokolewa” (Aya ya 3).PKSw 27.1

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents