Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 10—Maendeleo ya Matengenezo Ujerumani

  Kutoweka kwa siri kwa Luther kulileta wasiwasi katika nchi nzima ya Ujerumani. Maswali kumhusu yalisikika kila mahali. Uvumi mbaya ulisambazwa, na wengi waliamini kuwa alikuwa ameuawa. Kulikuwa na maombolezo makubwa, siyo tu kwa marafiki zake wa karibu, bali pia kwa maelfu ambao hawakuwa wameonesha kwa wazi msimamo wa kuwa upande wa Matengenezo. Wengi waliapa kwa kiapo kizito kuwa wangelipiza kisasi kwa ajili ya kifo chake.PKSw 138.1

  Viongozi wa Roma waliona kwa hofu kiwango cha kuinuka kwa hisia za watu dhidi yao. Ingawa mwanzoni walifurahia kifo cha kudhania cha Luther, siyo muda mrefu walianza kutamani kujificha mbali na chuki ya watu. Maadui zake hawakusumbuliwa na matendo yake ya kijasiri kabisa wakati alipokuwa miongoni mwao kama wakati alipokuwa ameondolewa. Wale ambao katika hasira yao walitafuta kumwangamiza Mwanamatengenezo jasiri walijazwa na hofu wakati huu alipokuwa mateka asiyekuwa na msaada. “Njia pekee iliyobaki ya kujiokoa,” mmoja alisema, “ni kuwasha mienge, na kumwinda Luther ulimwenguni kote, kumrudisha katika taifa ambalo linamwita.”— D'Aubigne, b. 9, ch. 1. Amri ya mfalme ilionekana kutokuwa na nguvu. Wawakilishi wa papa walijazwa na hasira walipoona kuwa tamko hilo lilivuta usikivu mdogo sana kuliko tatizo lililompata Luther.PKSw 138.2

  Habari kuwa alikuwa salama, japokuwa alikuwa mfungwa, zilituliza hofu za watu, wakati huo huo zikiamsha zaidi ari yao kwa ajili yake. Maandishi yake yalisomwa kwa shauku kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote kabla. Idadi iliyokuwa ikiongezeka ya watu ilijiunga na kazi ya shujaa ambaye, wakati wa hatari kama ule, alilitetea neno la Mungu. Matengenezo yalikuwa daima yakipata nguvu. Mbegu aliyokuwa ameipanda Luther ilichipuka kila mahali. Kutokuwepo kwake kulifanya kazi ambayo kuwepo kwake kungeshindwa kuifanya. Watendakazi wengine walihisi wajibu mpya, kwa kuwa kiongozi wao mkuu alikuwa ameondolewa. Kwa imani na ari mpya walisonga mbele kufanya yote yaliyokuwa katika uwezo wao, ili kazi nzuri iliyokwisha kuanza isizuiliwe.PKSw 138.3

  Lakini Shetani hakuwa amekaa kivivu. Sasa alijaribu kile ambacho amekuwa akijaribu kufanya katika kila msukumo wa matengenezo— kudanganya na kuangamiza watu kwa kuwaletea watu kitu bandia mahali pa kazi ya kweli. Kama vile kulivyokuwa na Makristo wa uongo katika karne ya kwanza ya kanisa la Kikristo, kadhalika kuliinuka manabii wa uongo katika karne ya kumi na sita.PKSw 138.4

  Watu wachache, kwa kuathiriwa na msisimko katika ulimwengu wa kidini, walijidhania kuwa wamepokea ufunuo maalumu kutoka Mbinguni, na walidai kuwa walitumwa na Mungu kuendeleza mpaka mwisho Matengenezo ambayo, walisema, yalikuwa yameanzishwa na Luther kwa udhaifu. Kusema ukweli, walikuwa wanaharibu kazi ambayo alikuwa ameifanya. Walikataa kanuni kuu ambayo ilikuwa msingi halisi wa Matengenezo — kwamba neno la Mungu ni kanuni inayojitosheleza ya imani na matendo; na badala ya mwongozo huo usiokosea waliweka kiwango kinachobadilika, kisichokuwa na uhakika cha hisia na mawazo yao. Kwa kitendo hiki cha kuweka kando mgunduzi mkuu wa makosa na uongo walimpa Shetani nafasi ya kutawala akili zao kwa kadiri alivyopenda mwenyewe.PKSw 139.1

  Mmoja wa hawa manabii alidai kuwa alikuwa ameelekezwa na malaika Gabrieli. Mwanafunzi aliyekuwa ameungana naye aliacha masomo, akitangaza kuwa alipewa na Mungu Mwenyewe hekima ya kufafanua neno Lake. Wengine ambao kwa silika yao walikuwa na mwelekeo wa ushikiliaji sana wa jambo bila akili waliungana nao. Shughuli za watu hawa zilianzisha vurugu nyingi. Mahubiri ya Luther yalikuwa yameamsha watu kila mahali wahisi umuhimu wa matengenezo, na sasa baadhi ya watu ambao kwa kweli walikuwa waaminifu walipotoshwa na maagizo ya hawa manabii wapya.PKSw 139.2

  Viongozi wa harakati hii walikwenda hadi Wittenberg ili kushinikiza madai yao kwa Melanchthon na watenda kazi wenzake. Walisema: “Tumetumwa na Mungu kuwafundisha watu. Tumefanya maongezi kwa karibu sana na Bwana; tunajua mambo yanayokuja; kwa kifupi, sisi ni mitume na manabii, na umwambie Dkt. Luther.”—Ibid., b. 9, ch. 7.PKSw 139.3

  Wanamatengenezo walishitushwa na walichanganywa. Hili lilikuwa jambo ambalo walikuwa hawajawahi kukutana nalo, na hawakujua jambo la kufanya. Melanchthon akasema: “Hakika kuna roho zisizokuwa za kawaida ndani ya watu hawa; lakini ni roho gani? ... Upande mmoja, inatupasa tuwe makini tusimzimishe Roho wa Mungu, na upande mwingine, inatupasa tuwe makini tusipotoshwe na roho wa Shetani.”—Ibid., b. 9, ch. 7.PKSw 139.4

  Haikuchukua muda tunda la fundisho jipya lilianza kuonekana. Watu waliongozwa kuipuuza Biblia au kuiacha kabisa. Shule ziliingizwa katika machafuko. Wanafunzi, wakipuuza kila kizuizi, waliacha masomo na kuondoka katika chuo kikuu. Watu waliojifikiria wenyewe kuwa na uwezo wa kuamsha na kuongoza kazi ya Matengenezo walifaulu kuyaleta karibu na ukingo wa kuyaharibu. Wafuasi wa Uroma sasa walirudisha ujasiri wao wakisema kwa furaha: “Pambano moja tu, na wote watakuwa wetu.”—Ibid., b. 9, ch. 7.PKSw 139.5

  Luther akiwa jijini Wartburg, baada ya kusikia kilichokuwa kimetokea, alisema kwa huzuni kubwa: “Daima nilitegemea kuwa Shetani angetuma tauni hii.”—Ibid., b. 9, ch. 7. Alibaini tabia halisi ya watu waliojifanya manabii na sasa aliona hatari iliyohatarisha kazi ya ukweli. Upinzani wa papa na mfalme haukuwa umemletea wasiwasi na hofu kama alivyohisi sasa. Kutoka kwa watu waliojifanya kuwa marafiki wa Matengenezo kuliibuka maadui wake wakuu. Ukweli uliokuwa umemletea furaha kubwa na faraja ulitumiwa kuamsha migogoro na kuleta machafuko katika kanisa.PKSw 140.1

  Katika kazi ya matengenezo, Luther alisukumwa na Roho wa Mungu kusonga mbele, na alipelekwa mbele zaidi ya vile alivyofikiria. Hakuwa amekusudia kuwa na misimamo aliyokuja kuwa nayo hatimaye, au kuleta mabadiliko makubwa. Alikuwa tu chombo katika mkono wa Nguvu usiokuwa na Kikomo. Hata hivyo daima alitetemeka kwa sababu ya matokeo ya kazi yake. Wakati fulani alisema: “Ikiwa ningejua kuwa fundisho lilikuwa limeujeruhi mtu mmoja, mtu mmoja tu, hata kama ni mtu wa chini na asiyejulikana,—jambo ambalo haliwezekani, kwa kuwa ni injili yenyewe,— ingekuwa bora nife mara kumi zaidi kuliko kuikana.”—Ibid., b. 9, ch. 7.PKSw 140.2

  Na sasa Wittenberg wenyewe, ambao ulikuwa kitovu cha Matengenezo, ulikuwa unatekwa na nguvu ya msimamo mkali na uvunjaji wa sheria. Hali hii ya kutisha haikutokana na mafundisho ya Luther; lakini katika nchi ya Ujerumani maadui zake walikuwa wakimlaumu kwa machafuko haya. Katika uchungu wa roho wakati mwingine aliuliza: “Je, inawezekana, hivyo basi, kuwa suala hili litaleta mwisho wa kazi kubwa ya Matengenezo?”—Ibid., b. 9, ch. 7. Hali kadhalika, alipopambana na Mungu katika maombi, amani ilibubujika ndani ya moyo wake. “Kazi siyo yangu, bali ni Yako,” alisema; “Wewe hutaruhusu kazi ya injili iharibiwe na ushirikina na misimamo ya itikadi kali.” Lakini wazo la kuwa mbali na migogoro katika mazingira kama hayo, lilionekana kuwa halifai. Alidhamiria kurudi Wittenberg.PKSw 140.3

  Bila kuchelewa alianza safari yake ya hatari. Alikuwa chini ya marufuku ya mfalme. Maadui walikuwa na uhuru wa kumwua; marafiki walikuwa wamekatazwa kumsaidia au kumlinda. Serikali ya kifalme ilikuwa ikichukua hatua kali sana dhidi ya wafuasi wake. Lakini aliona kuwa kazi ya injili ilikuwa hatarini, na katika jina la Bwana aliondoka bila woga kwenda kupigana vita kwa ajili ya ukweli.PKSw 140.4

  Katika barua kwa elekta, baada ya kueleza kusudi lake la kuondoka Wartburg, Luther alisema: “Ninakujulisha mfalme mkuu kuwa ninaenda Wittenberg chini ya ulinzi mkubwa zaidi kuliko ulinzi wa wakuu na maelekta wa kidunia. Ninafikiri sihitaji msaada wako, na wala sihitaji ulinzi wake, badala yake nitajilinda mwenyewe. Kama ningejua kuwa ungeweza kulinda watu, nisingekwenda kabisa Wittenberg. Hakuna upanga unaoweza kupeleka mbele zaidi kazi hii. Mungu peke Yake lazima afanye kila kitu, bila msaada au ukubali wa mtu. Yeye aliye na imani kubwa kuliko wote ni yeye anayeweza zaidi kulinda.”—Ibid., b. 9, ch. 8.PKSw 141.1

  Katika barua ya pili, iliyoandikwa akiwa njiani kuelekea Wittenberg, Luther aliongeza: “Niko tayari kukukasirisha wewe mfalme na kuukasirisha ulimwengu wote. Kwani wakazi wa Wittenberg siyo kondoo wangu? Kwani si Mungu amewaweka katika utunzaji wangu? Na siwajibiki, ikiwa lazima, kukabiliana na kifo kwa ajili yao? Kando ya hayo, ninaogopa kuona mlipuko wa ugonjwa wa kutisha katika nchi ya Ujerumani, ambao kwao Mungu ataliadhibu taifa letu.”—Ibid., b. 9, ch. 7.PKSw 141.2

  Kwa tahadhari na unyenyekevu mkubwa, lakini kwa uamuzi na uimara, alianza kazi yake. “Kwa neno,” alisema, “ni lazima tushinde na tuharibu kile ambacho kimewekwa kwa ukatili. Sitatumia nguvu dhidi ya washirikina na wasioamini.... Hakuna mtu atakayelazimishwa. Uhuru ni kiini hasa cha imani.”—Ibid., b. 9, ch. 8.PKSw 141.3

  Haukupita muda mrefu taarifa zilienea katika jiji lote la Wittenberg kuwa Luther amerudi na kuwa angehubiri. Watu walifurika kutoka pande zote, na kanisa lilijaa hadi likafurika. Alipopanda mimbarani, kwa hekima na upole mwingi alifundisha, alishauri, na alikosoa. Akigusia njia ya baadhi ambao walikuwa wameanza kutumia vurugu katika kukomesha misa, alisema:PKSw 141.4

  “Misa ni kitu kibaya; Mungu anapingana nayo; inapaswa kukomeshwa; na ningefurahi kuwa katika ulimwengu wote ingebadilishwa na mahali pake iwekwe Meza ya Bwana ya injili. Lakini tafadhali asiwepo mtu ye yote atakayeachanishwa nayo kwa nguvu. Inatupasa kuliacha jambo hilo mikononi mwa Mungu. Inapasa neno lake lifanye kazi, na siyo sisi. Na kwa nini iwe hivyo? Utaniuliza. Kwa sababu sishikilii mioyo ya watu mkononi mwangu, kama vile ambavyo mfinyanzi anavyoshikilia udongo. Tunayo haki ya kusema: hatuna haki ya kutenda. Sisi tuhubiri; yaliyobaki ni ya Mungu. Nikitumia nguvu, ninapata nini? Mkunjo wa uso, urasmi, uigizaji, kanuni za kibinadamu, na unafiki.... Lakini hakutakuwa na udhati wa moyo, wala imani, wala upendo. Mahali ambapo mambo haya matatu yanakosekana, vyote vinakosekana, na siwezi kuwekeza juhudi zangu katika shughuli yenye matokeo kama hayo.... Mungu anatenda zaidi kwa njia ya neno Lake pekee kuliko mimi na wewe na ulimwengu wote kuunganisha nguvu zetu. Mungu anashika moyo; na moyo unapochukuliwa, vyote vimepatikana....PKSw 141.5

  “Nitahubiri, nitajadili, na nitaandika; lakini sitamlazimisha ye yote, kwa kuwa imani ni tendo la hiari. Angalia nilichokifanya. Nilisimama dhidi ya upapa, vyeti vya msamaha, na wafuasi wa upapa, lakini bila fujo au vurugu. Niliwasilisha neno la Mungu; Nilihubiri na niliandika—haya ndiyo niliyoyafanya. Na nilipokuwa nimesinzia, ... neno nililokuwa nimelihubiri liliushinda upapa, na hakuna mkuu au mfalme aliyeliletea madhara makubwa neno la Mungu. Na sikufanya jambo lolote; neno la Mungu lilifanya yote hayo. Ikiwa ningependa kutumia nguvu, nchi yote ya Ujerumani labda pengine ingekuwa imefurika damu. Lakini matokeo yake yangekuwa nini? Uharibifu na ukiwa kwa wa mwili na roho. Kwa hiyo mimi nilikaa kimya, na nikaacha neno litembee ulimwenguni kote peke yake.”—Ibid., b. 9, ch. 8.PKSw 141.6

  Siku baada ya siku, kwa juma lote, Luther aliendelea kuhubiri makundi ya watu wenye shauku kubwa. Neno la Mungu lilivunja hirizi ya msisimko wa ushikiliaji sana mambo bila akili. Nguvu ya injili iliwarudisha watu waliokuwa wamepotoka na kuwaleta katika ukweli. Luther hakuwa na shauku ya kukutana na watu walioshikilia sana mambo bila akili ambao kazi yao ilikuwa imeleta madhara makubwa. Aliwajua kuwa ni watu waliokuwa hawana uamuzi mzuri na mihemko isiyokuwa na nidhamu, ambao, wakati wakidai kuwa na ufunuo maalumu kutoka mbinguni, wasingestahimili kupingwa hata kidogo na wasingepokea onyo au ushauri hata kama ungekuwa mzuri kiasi gani. Wakidai kuwa na mamlaka ya juu kabisa, walimtaka kila mmoja akiri madai yao bila maswali. Lakini, walipodai kuwa na mahojiano naye, alikubali kukutana nao; na alifanikiwa kuanika wazi maagizo yao kiasi kwamba walaghai wale waliondoka mara moja Wittenberg.PKSw 142.1

  Ushikiliaji sana mambo bila akili ulidhibitiwa kwa muda; lakini miaka kadhaa baadaye ulilipuka tena na kuleta vurugu nyingi zaidi na matokeo ya kutisha zaidi: “Kwao Maandiko Matakatifu yalikuwa barua iliyokufa, na wote walianza kupiga kelele, ‘Roho! Roho!’ Lakini kwa hakika sitafuata kule roho yao inapowapeleka. Naomba Mungu kwa rehema Zake anitunze dhidi ya kanisa ambalo ndani yake kuna watakatifu pekee. Ninatamani kuishi na watu wanyenyekevu, wanyonge, wagonjwa, wanaojua na kuhisi dhambi zao, na wanaoumia na kumlilia Mungu daima kwa moyo wa dhati wapate faraja na msaada Wake.”—Ibid., b. 10, ch. 10.PKSw 142.2

  Thomas Munzer, mashuhuri sana kwa itikadi kali, alikuwa mtu mwenye uwezo kiasi fulani, ambao kama ungeelekezwa vizuri, ungemwezesha kutenda mema; lakini hakuwa amejifunza kanuni za kwanza za dini ya kweli. “Alikuwa na shauku ya kuutengeneza ulimwengu, na alisahau, kama watu wote wenye itikadi kali wanavyofanya, kuwa matengenezo yalipaswa yaanze na yeye mwenyewe.”—Ibid., b. 9, ch. 8. Alikuwa na shauku kubwa ya kupata cheo na mvuto, na hakupenda awe wa pili, hata kwa Luther. Alitangaza kuwa Wanamatengenezo, kwa kuweka mamlaka ya Biblia badala ya papa, ilikuwa ni kuanzisha aina tofauti ya upapa. Yeye mwenyewe, alidai, alikuwa ametumwa na Mungu kuanzisha matengenezo ya kweli. “Aliye na roho hii,” Munzer alisema, “ana imani ya kweli, ingawa asingeona Maandiko katika maisha yake.”—Ibid., b. 10, ch. 10.PKSw 142.3

  Walimu walioshikilia sana mambo bila akili walijielekeza kuongozwa na hisia, wakichukulia kila wazo na shauku kama sauti ya Mungu; matokeo yake walienda mbali sana katika imani yao. Baadhi walichoma Biblia, wakipiga kelele: “Neno linaua, lakini Roho inahuisha.” Mafundisho ya Munzer yaliamsha shauku ya kupata mambo ya ajabu, huku yakifurahisha kiburi chao na kuweka mawazo na maoni ya kibanadamu juu ya neno la Mungu. Mafundisho yake yalipokelewa na maelfu ya watu. Alishutumu aina zote za utaratibu katika ibada ya hadhara, na alitangaza kuwa kutii viongozi wa serikali ilikuwa ni kujaribu kumtumikia Mungu na Beliali.PKSw 142.4

  Akili za watu, tayari zikiwa zinaanza kutupilia mbali nira ya upapa, zilikuwa pia vikianza kukosa uvumilivu dhidi ya makatazo ya mamlaka za kiraia. Mafundisho ya kimapinduzi ya Munzer, akidai kuwa yalikuwa na kibali cha Mungu, yaliwaongoza kujitenga na utawala wa aina yo yote na kuruhusu kutawaliwa na chuki na tamaa. Mandhari za kutisha za uchochezi wa uasi na vurugu vilifuata, na maeneo ya Ujerumani yalitapakaa damu.PKSw 143.1

  Maumivu makali ya rohoni ambayo Luther aliwahi kuyapata kabla akiwa katika mji wa Erfurt sasa yalimsonga yakiwa na nguvu iliyoongezeka mara mbili alipoona matokeo ya itikadi kali yakisababisha mashtaka dhidi ya Matengenezo. Viongozi wa upapa walisema—na wengi walikuwa tayari kuamini kauli—kuwa uasi ulikuwa tunda halisi la mafundisho ya Luther. Japokuwa shitaka hili halikuwa na msingi wowote, bado lilimsababishia dhiki kuu Mwanamatengenezo. Kwamba kazi ya ukweli iliaibishwa kwa kulinganishwa na itikadi kali, lilionekana kuwa jambo ambalo asingeweza kulistahimili. Kwa upande mwingine, viongozi wa uasi walimchukia Luther kwa sababu siyo tu kuwa alipinga mafundisho yao na kukana madai yao ya kuwa na uvuvio kutoka kwa Mungu, bali pia aliwaita waasi dhidi ya mamlaka za kiraia. Katika kulipiza kisasi walimshutumu kuwa mwigizaji mwovu. Ilionekana kana kwamba amejitengenezea mwenyewe maadui upande wa viongozi wa serikali na watu wa kawaida.PKSw 143.2

  Wafuasi wa Roma walifurahia, wakitarajia kushuhudia anguko la haraka la Matengenezo; na walimlaumu Luther, hata kwa makosa ambayo yeye alijitahidi sana kuyasahihisha. Kundi la wenye itikadi kali, kwa madai ya uongo kuwa walikuwa wakidhulumiwa sana, walifanikiwa kupata huruma ya tabaka kubwa la watu, na, kama ilivyo mara nyingi kwa wale wanaokuwa upande ambao unashambuliwa, walichukuliwa kuwa kama wafia dini. Hivyo, wale waliokuwa wakifanya kazi kwa nguvu kupinga Matengenezo walihurumiwa na walipongezwa kama wahanga wa ukatili na uonevu. Hii ilikuwa kazi ya Shetani, ikihimizwa na roho ile ile ya uasi iliyooneshwa kwanza mbinguni.PKSw 143.3

  Shetani hutafuta daima kuwadanganya watu na kuwaongoza kuiita dhambi haki, na haki dhambi. Kazi yake imefanikiwa sana! Ni mara ngapi watumishi wa Mungu waaminifu hukosolewa na huaibishwa kwa sababu wanatetea ukweli bila hofu! Watu ambao kimsingi ni mawakala wa Shetani wanasifiwa na wanapongezwa, na hata wanatazamwa kama wafia dini, wakati ambao wangeheshimiwa na kutiwa moyo kwa sababu ya uaminifu wao kwa Mungu, wanaachwa kusimama peke yao, chini ya tuhuma na kutoaminiwa.PKSw 143.4

  Utakatifu bandia, utakaso wa kuigiza, bado unafanya kazi yake ya uongo. Katika mifumo ya aina mbalimbali unaonesha roho ile ile kama ilivyokuwa katika siku za Luther, kuondoa akili za watu kutoka kwenye Maandiko na kuwafanya watu wafuate hisia na shauku zao kuliko kusalimisha utii wao kwa sheria ya Mungu. Hii ni moja ya mbinu za Shetani zenye mafanikio makubwa sana za kuaibisha usafi na ukweli.PKSw 144.1

  Bila hofu Luther aliitetea injili dhidi ya mashambulizi yaliyotoka kila upande. Neno la Mungu lilionekana kuwa silaha yenye nguvu katika kila mgogoro. Kwa neno hilo alipigana dhidi ya mamlaka ya kujipachika ya upapa, na dhidi ya falsafa ya mantiki ya wasomi, wakati alisimama imara kama mwamba dhidi ya ushikiliaji sana wa mambo bila akili uliotafuta kujiambatisha na Matengenezo.PKSw 144.2

  Kila moja ya sekta hizi zinazopingana kila moja kwa njia yake ilikuwa ikiweka pembeni Maandiko Matakatifu na kuinua hekima ya mwanadamu kama chanzo cha ukweli na maarifa ya kidini. Falsafa mantiki huifanya mantiki kuwa sanamu ya kuabudu na huifanya kuwa kipimo cha dini. Uroma, ukidai kwa ajili ya kiongozi wao mkuu uvuvio ulioshuka katika mstari ulioshikamana tangu mitume, na usiobadilika nyakati zote, hutoa fursa maridhawa kwa kila aina ya ubadhirifu na ufisadi kufichwa chini ya utakatifu wa agizo la mitume. Uvuvio ambao Munzer na wenzake walidai kuwa nao ulitoka katika michakato ya fikra, na nguvu yake ilikuwa kinyume na mamlaka zote, za kibinadamu au za Kimungu. Ukristo wa kweli hupokea neno la Mungu kama nyumba kubwa ya hazina ya ukweli uliovuviwa.PKSw 144.3

  Baada ya kurudi kutoka Wartburg, Luther alimaliza tafsiri yake ya Agano Jipya, na muda mfupi baada ya hapo injili ilitolewa kwa watu wa Ujerumani katika lugha yao wenyewe. Tafsiri hii ilipokelewa kwa furaha kubwa na wote walioupenda ukweli; lakini ilikataliwa kwa dharau na wale waliochagua mapokeo ya wanadamu na amri za wanadamu.PKSw 144.4

  Makasisi walihofia wazo kuwa watu wa kawaida wangeweza sasa kubishana nao juu ya kanuni za neno la Mungu, na kuwa ujinga wa makasisi ungeanikwa kwa njia hiyo. Silaha zao za hoja za kimwili hazikuwa na nguvu dhidi ya upanga wa Roho. Roma ilitumia mamlaka zake zote kuzuia usambazaji wa Maandiko; lakini amri, laana, na maumivu vilikuwa bure. Kwa kadiri Roma ilivyozidi kushutumu na kupiga marufuku Biblia, ndivyo watu walivyojenga shauku kubwa zaidi ya kujua Biblia ilifundisha nini. Wote walioweza kusoma walitamani kujifunza neno la Mungu wao wenyewe. Waliibeba kila mahali walikokwenda, na walisoma na kusoma tena, na hakuridhika mpaka walipokariri sehemu kubwa ya Maandiko. Alipoona jinsi watu walivyolipokea Agano Jipya kwa furaha, Luther alianza mara moja kutafsiri Agano la Kale, na alichapisha sehemu zake mara moja alipomaliza.PKSw 144.5

  Maandishi ya Luther yalipokelewa mahali pote, iwe mijini au vijijini. “Kilichoandikwa na Luther na marafiki zake, wengine walisambaza. Watawa, waliposhawishika kuwa matakwa ya maisha ya kitawa hayakuwa halali, kwa kutamani kubadilisha maisha yao ya kivivu ili waishi maisha ya kujishughulisha, lakini wakiwa hawajui jinsi ya kuhubiri neno la Mungu, walisafiri katika majimbo, wakitembelea mitaa na nyumba, ambapo waliuza vitabu vya Luther na marafiki zake. Kwa muda mfupi Ujerumani ilifurika hawa wainjilisti wa vitabu jasiri.”—Ibid., b. 9, ch. 11.PKSw 145.1

  Maandishi haya yalisomwa kwa shauku kubwa na matajiri na maskini, wasomi na wasio kuwa wasomi. Usiku walimu wa shule za vijijini waliwasomea kwa sauti makundi madogo ya watu waliokusanyika kando ya moto. Kwa juhudi zote baadhi ya roho ziliuamini ukweli na, baada ya kupokea ukweli kwa furaha, ilikuwa zamu yao kuwaeleza wengine habari njema.PKSw 145.2

  Maneno yaliyovuviwa yalithibitika: “Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga” (Zaburi 119:130). Kujifunza Maandiko kulileta badiliko kubwa katika akili na mioyo ya watu. Utawala wa kipapa ulikuwa umeweka juu ya wafuasi wake nira ya chuma iliyowafunga pamoja katika ujinga na umaskini. Uzingatiaji wa kishirikina wa taratibu ulisimamiwa kwa uangalifu; lakini katika huduma yao yote moyo na akili vilikuwa na sehemu ndogo sana. Mahubiri ya Luther, yaliyowasilisha ukweli wa wazi wa neno la Mungu, na halafu neno lenyewe, lililowekwa katika mikono ya watu wa kawaida, liliamsha akili zao zilizokuwa zimelala, siyo tu likisafisha na kuimarisha hali ya kiroho, bali pia likileta nguvu na uhai mpya wa akili.PKSw 145.3

  Watu wa matabaka yote walionekana wakiwa na Biblia mikononi mwao, wakilinda mafundisho ya Matengenezo. Viongozi wa upapa waliokuwa wamewaachia mapadri na watawa kujifunza Maandiko waliwaita waje na kukanusha mafundisho hayo mapya. Lakini, kwa kutoyajua Maandiko na nguvu ya Mungu, viongozi wa upapa walishindwa kabisa na wale waliowashutumu kuwa wajinga na wazushi. “Kwa huzuni,” mwandishi wa Kikatoliki alisema, “Luther alikuwa amewashawishi wafuasi wake kutoamini kanuni yoyote kuliko Maandiko Matakatifu.”—D'Aubigne, b. 9, ch. 11. Makundi ya watu walikusanyika kusikia ukweli uliowasilishwa na watu wenye elimu ndogo, na hata walipojadiliana na wasomi na wanateolojia wenye ufasaha. Ujinga wa kuaibisha wa hawa watu wakubwa ulifunuliwa wakati hoja zao zilipokutana na mafundisho sahili ya neno la Mungu. Vibarua, maaskari, wanawake, na hata watoto, waliyajua mafundisho ya Biblia zaidi ya mapadri na madaktari wasomi.PKSw 145.4

  Tofauti kati ya wanafunzi wa injili na wapiga debe wa ushirikina wa kipapa ilikuwa wazi siyo tu miongoni mwa wasomi, bali pia miongoni mwa watu wa kawaida. “Tofauti na mabingwa wa zamani wa upapa, waliopuuza kujifunza lugha na stadi za fasihi, ... walikuwa vijana wenye akili za kiungwana, makini katika kujifunza, wakichunguza Maandiko, na wakijielimisha juu ya mambo ya kale yaliyomo katika vitabu vya watu mashuhuri. Wakiwa na akili ya kiutendaji, roho iliyoinuliwa, na mioyo jasiri, vijana hawa kwa muda mfupi walipata maarifa ambayo kwa muda mrefu hakuna mtu ambaye angeweza kushindana nao.... Kwa mantiki hiyo, wakati vijana hawa watetezi wa Matengenezo walipokutana na madaktari wasomi wa Kiroma katika kongamano lo lote, waliwashambulia kwa urahisi na kujiamini kiasi kwamba hawa watu wasiojua Maandiko walisita, waliudhika, na walidharaulika mbele ya watazamaji wote.”—Ibid., b. 9, ch. 11.PKSw 146.1

  Viongozi wa Kiroma walipoona makanisa yao yalikuwa yakiishiwa watu, walitafuta msaada kwa mahakimu, na kwa kila njia iliyokuwa katika uwezo wao walijaribu kuwarudisha wasikilizaji wao. Lakini watu walikuwa wamepata katika mafundisho mapya kile ambacho kilikidhi mahitaji ya roho zao, na waliachana kabisa na wale ambao kwa muda mrefu waliwalisha pumba zisizofaa za kaida za kishirikina na mapokeo ya wanadamu.PKSw 146.2

  Mateso yalipowashwa dhidi ya walimu wa ukweli, walitii maneno ya Kristo: “Watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine” (Mathayo 10:23). Nuru ilipenya kila mahali. Wakimbizi waliweza kupata mahali fulani mlango wenye ukarimu uliofunguliwa kwa ajili yao, na wakiwepo hapo, walimhubiri Kristo, nyakati zingine kanisani, au, ikiwa walinyimwa fursa hiyo, katika nyumba binafsi au eneo la wazi. Mahali popote walipopata watu wa kuwasikiliza palikuwa hekalu takatifu. Ukweli, ulipotangazwa kwa nguvu na uhakika kama huo, ulienea kwa nguvu isiyopingika.PKSw 146.3

  Bila mafanikio mamlaka za kikanisa na kiraia zilitumika kukomesha uzushi. Bila mafanikio walitumia vifungo magerezani, maumivu, moto, na upanga. Maelfu ya waumini waligonga muhuri imani yao kwa damu yao, na bado kazi iliendelea. Mateso yalikuwa kichocheo cha kuenea kwa ukweli, na unafiki ambao Shetani alijaribu kuungana nao uliishia katika kuleta tofauti kubwa zaidi kati ya kazi ya Shetani na kazi ya Mungu.PKSw 146.4

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents