Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 4—Wawaldensia

  Katikati ya utusitusi uliotanda duniani katika kipindi kirefu cha utawala wa upapa, nuru ya ukweli haikuzimika kabisa. Katika kila zama walikuwepo mashahidi wa Mungu—watu waliodumu kumwamini Kristo kama mpatanishi pekee kati ya Mungu na mwanadamu, watu, ambao waliishikilia Biblia kama kanuni pekee ya maisha, na ambao waliitakasa Sabato ya kweli. Ni kiasi gani ulimwengu unadaiwa na watu hawa, vizazi vijavyo haviwezi kujua. Waliitwa wapotoshaji, dhamiri zao zilitiliwa mashaka, sifa zao zilichafuliwa, maandishi yao yalipuuzwa, yalitafsiriwa vibaya, au yalichanwa. Hata hivyo walisimama imara, na kutoka zama moja hadi zama nyingine walishikilia imani yao katika hali yake ya usafi, kama urithi mtakatifu kwa ajili ya vizazi vijavyo.PKSw 44.1

  Historia ya watu wa Mungu katika zama za giza za utawala wa Rumi imeandikwa mbinguni, lakini ina sehemu ndogo sana katika kumbukumbu za wanadamu. Mabaki kidogo ya uwepo wao yanaweza kupatikana, lakini ni katika mashitaka ya watesi wao. Ilikuwa sera ya Rumi kufuta kabisa mabaki yote yaliyohusiana na watu waliopingana nao katika mafundisho au maagizo yao. Kila kitu chenye viashiria vya upinzani wa kimafundisho, kiwe kilihusiana na mtu binafsi au maandishi viliharibiwa. Maneno yaliyoonesha mashaka, au maswali yaliyohoji mamlaka ya imani kuhusu upapa, yalitosha kuondoa uhai wa mtu tajiri au maskini, wa juu au wa chini. Rumi ilijitahidi kuharibu kumbukumbu zote za ukatili waliowafanyia waliotofautiana nao. Mabaraza ya kipapa yaliamuru kuwa vitabu na maandishi yenye kumbukumbu kama hizo yachomwe moto. Kabla ya kugundua mitambo ya uchapishaji, vitabu vilikuwa vichache katika idadi, na vilikuwa katika mfumo ambao siyo mwepesi kuhifadhiwa; kwa hiyo kulikuwa na vitu vichache vya kuwazuia watawala wa Rumi kutekeleza makusudi yao.PKSw 44.2

  Hakuna kanisa ndani ya mipaka ya utawala wa Rumi lililobaki kwa muda mrefu bila uhuru wao wa dhamiri kubughudhiwa. Muda mfupi baada ya kupata mamlaka upapa ulinyosha mikono yake kuwaangamiza wote waliokataa kutambua mamlaka yake, na makanisa yote, moja baada ya jingine yalijisalimisha chini ya utawala wake.PKSw 44.3

  Katika nchi ya Uingereza Ukristo wa awali ulikuwa umeanza kukita mizizi mapema kabisa. Injili iliyopokelewa na Waingereza katika karne za kwanza wakati huo haikuwa imechafuliwa na uasi wa Rumi. Mateso ya wafalme wa kipagani, yaliyosambaa mpaka pwani hizi za mbali, ndiyo zawadi pekee iliyopokelewa na makanisa ya Uingereza kutoka Rumi. Wakristo walio wengi, waliokimbia mateso huko Uingereza, walipata hifadhi katika nchi ya Scotland; kutoka hapo ukweli ulipelekwa Ireland, na katika nchi zote hizi injili ilipokelewa kwa furaha.PKSw 44.4

  Wakati watu wa kabila la Wasaxon walipoivamia Uingereza, upagani ulipata nguvu na kutawala. Watekaji waliona aibu kufundishwa na watumwa wao, na Wakristo walilazimika kujificha milimani na maporini. Hata hivyo nuru, iliyofichwa kwa muda, iliendelea kuwaka. Katika nchi ya Scotland, karne iliyofuata, ilimulika nuru kubwa iliyoenea hadi nchi za mbali. Kutoka Ireland aliibuka Kolumba mcha Mungu na watendakazi wenzake, ambao, wakiwakusanya karibu yao waumini waliokuwa wamesambaa katika kisiwa pweke cha Iona, walipafanya mahali pale kuwa kituo chao cha kazi za umishenari. Miongoni mwa hawa wainjilisti alikuwemo mtunzanji wa Sabato ya Biblia, na kupitia kwake, ukweli huu ulitambulishwa kwa watu wengine. Shule ilianzishwa hapo Iona, ambapo wamishenari waliandaliwa na kutumwa sehemu zingine, siyo Scotland na Uingereza, bali pia Ujerumani, Uswisi, na hata Italia.PKSw 45.1

  Lakini Rumi ilikuwa imeelekeza macho yake kwa Uingereza, na iliazimia kuiweka chini ya himaya yake. Katika karne ya sita wamishenari wake walijaribu kuwaongoa Wasaxon wapagani. Walipokelewa na wapagani wenye kiburi, na waliwashawishi maelfu kuikiri imani ya Kirumi. Kadiri kazi ilivyoendelea, viongozi wa upapa na waongofu wao walikutana na Wakristo wenye msimamo wa Ukristo wa awali. Tofauti kubwa ilijitokeza. Wakristo wa kundi la awali walikuwa sahili, wanyenyekevu, wenye tabia ya Maandiko Matakatifu, wenye kuzingatia mafundisho, na waungwana, wakati Wakristo wa kundi la kwanza walionesha roho ya ushirikina, majivuno, na kiburi cha upapa. Mwakilishi wa Rumi aliyaamrisha haya makanisa ya Kikristo yakiri ukuu wa utawala wa papa. Waingereza walijibu kwa unyenyekevu kuwa walitamani kuwapenda watu wote, lakini kuwa papa hakustahili kuwa na ukuu ndani ya kanisa, na kuwa walikuwa tayari kumpa heshima ambayo anastahili kila mfuasi wa Kristo. Majaribio yalifanywa mara kadhaa ili kupata utii kwa Rumi; lakini hawa Wakristo wanyenyekevu, wakiwa wameshangazwa kwa kiburi kilichooneshwa na mjumbe wa papa, walisimama imara na kundelea kujibu kuwa hakumjua Bwana mwingine zaidi ya Kristo. Sasa roho ya kweli ya upapa ilifunuliwa. Kiongozi wa Kirumi alisema: “Usipowapokea ndugu wanaokuletea amani, utawapokea maadui wanaokuletea vita. Msipoungana nasi ili kwa pamoja tuwaoneshe Wasaxon njia ya uzima, mtapata kutoka kwao pigo la mauti.”—J. H. Merle D'Aubigne, History of the Reformation of the Sixteenth Century, b. 17, ch. 2. Hivi havikuwa vitisho vidogo. Vita, ujanja, na udanganyifu vilitumika dhidi ya mashahidi wa imani ya Biblia, mpaka makanisa ya Uingereza yalipoharibiwa, au yalipojisalimisha kwa mamlaka ya papa.PKSw 45.2

  Katika nchi zilizokuwa nje ya utawala wa Rumi walidumu kuwepo kwa karne nyingi makundi ya Wakristo waliobaki kwa kiasi kikubwa bila kuchafuliwa na ufisadi wa kipapa. Walikuwa wamezungukwa na upagani na baada ya vizazi vingi kupita waliathiriwa na makosa yaliyomo katika upagani; lakini waliendelea kuheshimu Biblia kama kanuni pekee ya imani na walizingatia nyingi ya kweli zake. Wakristo hawa waliamini kuwa sheria ilikuwa ya kudumu na waliitunza Sabato ya amri ya nne. Makanisa yaliyoshikilia imani hii na matendo haya walikuwepo Afrika ya Kati na miogoni mwa Waarmenia wa Asia.PKSw 45.3

  Lakini kati ya wale waliopinga kuburuzwa na mamlaka ya upapa, Wawaldensia walikuwa mbele kulikowa wengine wote. Katika nchi ile ile ambapo upapa ulikuwa umesimika kiti chake, mambo hayo ya uongo na ufisadi yalipingwa kwa nguvu zote. Kwa karne nyingi makanisa ya Piedmont yalidumisha uhuru wao; lakini muda ulifika hatimaye ambapo Rumi ilisisitiza sana na wao wajisalimishe. Baada ya mgogoro ulioonekana kutozaa matunda dhidi ya adui wao katili, viongozi wa makanisa haya bila kuridhika kabisa waliitambua mamlaka ambayo ulimwengu wote uliitambua na kuiabudu. Walikuwepo baadhi, hata hivyo, waliokataa kujisalimisha kwa mamlaka ya upapa au uaskofu. Waliazimia kudumisha utii wao kwa Mungu na kutunza usafi na usahili wa imani yao. Utengano ukatokea. Walioshikilia imani ya zamani sasa walijiondoa; baadhi, wakiyakimbia makazi yao ya asili ya Alps, waliinua bendera ya ukweli katika nchi za ugenini; baadhi walijificha katika maeneo pweke ya mapangoni na kati kati ya mianya ya miamba iliyoko milimani, na huko walidumisha uhuru wao wa kumwabudu Mungu.PKSw 46.1

  Imani ambayo kwa karne nyingi ilishikiliwa na kufundishwa na Wakristo Wawaldensia ilitofautiana sana na mafundisho ya uongo yaliyotolewa na Rumi. Imani yao ya dini ilijengwa juu ya neno la Mungu lililoandikwa, msingi wa kweli wa Ukristo. Lakini wakulima wale wanyenyekevu, katika maficho yao, wakiwa wamejifungia mbali na ulimwengu, na wakiwa wamegubikwa na shughuli zao za kila siku katikati ya mifugo yao na mashamba yao ya mizabibu, walikuwa wao wenyewe hawajaelewa ukweli uliopingana na uongo na upotovu wa kanisa asi. Imani yao haikuwa imani mpya waliyokuwa wameipokea. Imani yao ya dini ilikuwa ile waliyoirithi kutoka kwa baba zao. Waliridhishwa na imani ya kanisa la mitume,—“imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu” (Yuda 3). “Kanisa jangwani,” na siyo mamlaka iliyoketi juu ya kiti cha enzi katika mji mkuu wa dunia, ndilo lilikuwa kanisa la Kristo, mwangalizi wa hazina za ukweli ambao Mungu amewapa watu Wake ili waueneze ulimwenguni.PKSw 46.2

  Miongoni mwa sababu muhimu zilizosababisha kanisa la kweli lijitenge na Rumi ilikuwa ni chuki ya Kanisa la Rumi dhidi ya Sabato ya Biblia. Kama unabii ulivyotabiri, mamlaka ya upapa ilitupa chini ukweli. Sheria ya Mungu ilikanyagwa katika mavumbi ya ardhi, ilhali mapokeo na desturi za wanadamu vikiinuliwa juu. Makanisa yaliyokuwa chini ya utawala wa upapa yalilazimishwa kuiheshimu Jumapili kama siku takatifu mapema kabisa. Katikati ya makosa na ushirikina ulioshamiri, wengi, hata miongoni mwa watu wa kweli wa Mungu, walichanganywa sana kiasi ambacho ingawa waliitunza Sabato, waliacha kufanya kazi siku ya Jumapili. Lakini jambo hili halikuwaridhisha viongozi wa kipapa. Walidai siyo tu kuwa Jumapili itakaswe, bali pia Sabato inajisiwe; na waliwashutumu kwa lugha kali watu waliojaribu kuiheshimu. Ilikuwa tu kwa njia ya kuikimbia mamlaka ya Rumi ndiyo mtu yeyote angeweza kuitii sheria ya Mungu kwa amani (Tazama Kiambatanisho).PKSw 46.3

  Wawaldensia walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza wa Ulaya kupata tafsiri ya Maandiko Matakatifu (Tazama Kiambatisho). Miaka mamia kabla ya Matengenezo walikuwa na Biblia katika muswada katika lugha yao ya asili. Walikuwa na ukweli usiochafuliwa, na jambo hili liliwafanya wawe walengwa wa chuki na mateso. Walilitangaza Kanisa la Rumi kuwa Babeli iliyoasi ya Ufunuo, na kwa kuhatarisha maisha yao walisimama imara kupinga ufisadi wake. Wakati, chini ya shinikizo la mateso yaliyodumu kwa muda mrefu, baadhi walilegeza imani yao, kidogo kidogo wakiacha kanuni zake bainishi, wengine walishikilia ukweli. Katika zama zote za giza na uasi walikuwepo Wawaldensia waliokataa ukuu wa Rumi, waliokataa ibada ya sanamu, na waliotunza Sabato ya kweli. Chini ya dhoruba kali kabisa za upinzani walishikilia imani yao. Wakiwa wamechanwa na mikuki ya kisavoyadi, na kupigwa fimbo za Kirumi, walisimama bila kutetereka kwa ajili ya neno la Mungu na heshima Yake.PKSw 47.1

  Nyuma ya ngome ndefu za milima—katika zama zote maficho ya walioteswa na walioonewa—Wawaldensia walijificha. Hapa nuru ya ukweli ilidumu kuwaka katikati ya giza la Zama za Kati. Hapa, kwa miaka elfu moja, mashaidi wa ukweli walidumisha imani ya zamani.PKSw 47.2

  Mungu aliwatunza watu Wake katika maficho mazuri ajabu—maficho yaliyofaa kuhifadhia ukweli wenye nguvu waliopewa kuutunza kama amana. Kwa watu waaminifu waliokuwa uhamishoni milima ilikuwa ishara ya haki ya Yeshova usiobadilika. Milima iliwaelekeza watoto wao kwa vilele virefu juu yao katika utukufu usiobadilika, na iliwaambia habari za Yule ambaye Kwake hakuna kubadilika wala kivuli cha kugeuka, Yeye ambaye neno Lake linadumu kama milima ya milele. Mungu aliiweka milima na kuivika nguvu; hakuna mkono isipokuwa wa Nguvu ya Milele unaoweza kuihamisha kutoka katika sehemu zao. Kwa jinsi hiyo hiyo, Mungu aliiweka sheria kuwa msingi wa serikali Yake mbinguni na duniani. Mkono wa mwanadamu ungeweza kuwafikia wanadamu wenzake na kuharibu maisha yao; lakini mkono huo huo ungeweza kirahisi pia kuing'oa milima kutoka misingi yake, na kuitupa baharini, kama ungeweza kubadili kanuni moja ya sheria ya Yehova, au kufuta moja ya ahadi Zake kwa wale wanaotenda mapenzi Yake. Katika uaminifu wao kwa sheria ya Mungu, watumishi wa Mungu wanapaswa kutobadilika kama millima isivyobadilika.PKSw 47.3

  Milima iliyozungukwa na mabonde ya chini ilikuwa mashahidi wa kudumu wa nguvu za Mungu za uumbaji, na uhakikisho usiobadilika wa ulinzi na utunzaji Wake. Wasafiri wale walijifunza kupenda alama za kimya za uwepo wa Yehova. Hawakulalamika kwa sababu ya ugumu wa maisha yao; hawakuhisi upweke katika maficho yao ya milimani. Walimshukuru Mungu kwa kuwapa maficho dhidi ya chuki na ukatili wa wanadamu. Walifurahia uhuru wa kuabudu mbele Zake. Mara nyingi walipofuatiliwa na maadui zao, nguvu ya milima ilikuwa ulinzi wa hakika kwao. Katikati ya milima mingi mirefu walimwimbia Mungu nyimbo za sifa, na majeshi ya Rumi hayakuweza kunyamazisha nyimbo zao za shukurani.PKSw 48.1

  Utakatifu wa hawa wafuasi wa Kristo ulikuwa safi, sahili, na wa dhati. Walithamini zaidi kanuni za ukweli zaidi kuliko nyumba na ardhi, marafiki, ndugu, hata maisha yenyewe. Walitafuta kwa bidii kuziweka kanuni hizi katika mioyo ya watoto wao. Tangu watoto wakiwa wachanga vijana walifundishwa Maandiko na walifundishwa kutambua utakatifu wa madai ya sheria ya Mungu. Nakala za Biblia zilikuwa haba; kwa hiyo maneno yake ya thamani yalikaririwa. Wengi waliweza kukariri sehemu kubwa ya Agano la Kale na Agano Jipya. Mawazo ya Mungu yaliambatana sawa sawa na mandhari nzuri ya uumbaji na baraka za kila siku katika maisha. Watoto wadogo walijifunza kumtazama Mungu kwa shukurani kama mruzuku wa fadhili na wa kila jambo jema.PKSw 48.2

  Wazazi, pamoja na wema wao na kujali kwao, waliwapenda watoto wao kwa hekima sana kiasi cha kuwazoezesha maisha ya afya na kiasi. Mbele yao kulikuwa na maisha ya majaribu na ugumu, pengine kifo cha mfia dini. Walielimishwa tokea utotoni kuvumilia ugumu wa maisha, kujitawala, na walijengewa uwezo wa kufikiri na kutenda kwa ajili yao wenyewe. Mapema kabisa walifundishwa kubeba majukumu, uangalifu katika maneno yao, na kuelewa hekima ya ukimya. Neno moja lisilofaa lililoruhusiwa kutoka midomoni mwao na kusikiwa na maadui zao lingeweza kuhatarisha siyo tu maisha ya msemaji, bali pia maisha ya mamia ya ndugu zake; kwani kama vile mbwa mwitu walivyowinda mawindo yao ndivyo maadui wa ukweli walivyowawinda watu waliodai kuwa na uhuru wa imani ya dini.PKSw 48.3

  Wawaldensia walitoa kafara ya mafanikio ya maisha yao ya duniani kwa ajili ya ukweli, na kwa uvumilivu endelevu walipambana kujipatia riziki. Kila sehemu iliyoweza kulimwa katikati ya milima iliweza kuboreshwa; mabonde na miteremko isiyokuwa na rutuba iliwezeshwa kutoa mazao mengi. Kubana matumizi na kujikana nafsi sana vilikuwa sehemu ya elimu waliyopewa watoto kama urithi wao pekee. Walifundishwa kuwa Mungu alipanga maisha yawe kujikana nafsi, na kuwa mahitaji yao yangeweza kukidhiwa kwa kazi binafsi, kwa kupanga, kujali, na imani. Mchakato ulikuwa mgumu na wa kuchosha, lakini ulikuwa mkamilifu, kwani ulikidhi hitaji la mwanadamu katika hali yake ya anguko, shule ambayo Mungu aliipanga kwa ajili ya mafunzo na maendeleo. Wakati vijana walifunzwa kuteseka na kufanya kazi ngumu, maendeleo ya akili hayakuachwa nyuma. Walifundishwa kuwa nguvu zao zote zilikuwa za Mungu, na kuwa zote zilipaswa kuboreshwa na kuendelezwa kwa ajili ya huduma Yake.PKSw 48.4

  Makanisa ya Kivodwa, katika usafi na usahili wake, yalifanana na kanisa la nyakati za mitume. Wakikataa mamlaka ya upapa na uaskofu, walishikilia Biblia kuwa ndiyo mamlaka pekee iliyo juu, isiyokosea. Wachungaji wao, kinyume na waheshimiwa mapadre wa Roma, walifuata mfano wa Bwana wao, ambaye “hakuja kutumikiwa, bali kutumika.” Walilisha kundi la Mungu, wakiliongoza kwenye majani mabichi na chemchemi hai za neno Lake takatifu. Tofauti kabisa na kumbukumbu za majivuno na kiburi, watu walikusanyika, siyo katika makanisa mazuri au katika kathedro kubwa, bali chini ya vivuli vya milima, katika mabonde yaliyoko katika milima ya juu, au, katika nyakati za hatari, katika ngome za miamba, kusikiliza maneno ya ukweli kutoka kwa watumishi wa Kristo. Wachungaji walihubiri siyo tu injili, bali pia walitembelea wagonjwa, waliwafundisha watoto, waliwaonya wakosaji, na walifanya kazi ya kutatua migogoro na kuhamasisha mapatano na upendano wa kindugu. Katika nyakati za amani walitunzwa kwa sadaka za hiari za watu; lakini, kama Paulo mtengeneza ngozi, kila mmoja alijifunza kazi au taaluma fulani ambayo kwayo, ilibidi, aweze kujitegemeza mwenyewe.PKSw 49.1

  Kutoka kwa wachungaji wao vijana walipata mafundisho. Wakati muda mwingi ulitumiwa kujifunza maarifa ya aina mbalimbali za jumla, Biblia ilifanywa kuwa somo kuu. Injili za Mathayo na Yohana zilikaririwa, pamoja na Nyaraka zilizo nyingi. Walitumika pia katika kunakili Maandiko. Baadhi ya nakala zilikuwa na Biblia nzima, zingine zilikuwa na sehemu fupi zilizochaguliwa, zikiambatana na maelezo sahili ya aya husika yaliyoongezwa na wale waliokuwa na uwezo wa kufafanua Maandiko. Kwa njia hiyo hazina za kweli zilizokuwa zimefichwa kwa muda mrefu na wale waliotafuta kujiinua juu ya Mungu ziliwekwa wazi.PKSw 49.2

  Kwa kazi ya uvumilivu, iliyofanywa bila kuchoka, nyakati zingine ikifanyiwa katika mapango yenye giza chini ya ardhi, kwa kutumia mwanga wa mienge, Maandiko Matakatifu yaliandikwa, aya kwa aya, sura kwa sura. Kwa njia hiyo, kazi ilisonga mbele, mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa yaking'aa kama dhahabu safi; kwamba iling'aa zaidi, kwa uwazi zaidi, na kwa nguvu kiasi gani, kwa sababu ya majaribu waliyopitia kwa sababu ya Maandiko, wanaoweza kuelewa ni wale tu waliohusika na kazi hiyo. Malaika wa mbinguni waliwazunguka watendakazi hawa waaminifu.PKSw 49.3

  Shetani aliwafanya makasisi na maaskofu wa kipapa wazike neno la ukweli chini ya takataka za makosa, upotovu, na ushirikina; lakini kwa namna ya ajabu sana neno la Mungu lilihifadhiwa bila kuchafuliwa katika zama zote za giza. Halikutiwa mhuri wa mwanadamu, bali mhuri wa Mungu. Wanadamu hawakuchoka katika juhudi zao za kuficha maana ya wazi, sahili ya Maandiko, na kuyafanya yapingane na ushuhuda wake yenyewe; lakini kama safina juu ya vilindi vya maji, neno la Mungu lilipona dhoruba iliyotishia kuliharibu. Kama vile mgodi unavyokuwa na mishipa ya dhahabu na fedha chini ya uso wa ardhi, ili watu wote walazimike kuchimba ili kugundua maghala yake ya thamani, kadhalika Maandiko Matakatifu yana hazina za ukweli ambazo hufunuliwa tu kwa mtafutaji wa dhati, mnyenyekevu, na mwenye maombi. Mungu alipanga Biblia iwe kitabu cha masomo kwa ajili ya wanadamu wote, wakati wa utoto, utu uzima, na isomwe wakati wote. Aliwapa wanadamu neno Lake kama ufunuo Wake Mwenyewe. Kila ukweli mpya unaogunduliwa ni ufunuo mpya wa tabia ya Mtunzi wake. Kujifunza Maandiko ni njia iliyowekwa na Mungu kuwaleta watu katika mshikamano wa karibu na Muumbaji wao na kuwapa uelewa wa wazi zaidi wa mapenzi Yake. Ni mfereji wa mawasiliano kati ya Mungu na mwanadamu.PKSw 49.4

  Wakati Wawaldensia wakichukulia kicho cha Bwana kuwa mwanzo wa hekima, hawakuwa na upofu wa kushindwa kutambua umuhimu wa kukutana na ulimwengu, kuwaelewa watu na shughuli za maisha yao ya kila siku, ili kupanua akili na kunoa utambuzi. Baada ya shule zao za milimani baadhi ya vijana walipelekwa katika taasisi za elimu katika miji ya Ufaransa au Italia, ambapo palikuwa na uwanja mpana zaidi wa elimu, fikra, na utafiti kuliko katika shule zao za milimani. Vijana waliopelekwa huko walikutana na majaribu, walishuhudia uovu, walikutana na mawakala wa Shetani wenye hila, waliosihi wakubali mafundisho ya uongo uliojificha sana na udanyifu wa hatari sana. Lakini elimu yao ya tangu utotoni ilikuwa imewaandaa kwa ajili ya mambo haya yote.PKSw 50.1

  Katika shule walizokwenda, hawakupaswa kuwa karibu sana na mtu ye yote. Mavazi yao yalikuwa yametengenezwa kwa namna ambayo yangetumiwa kuficha hazina yao yenye thamani kuu—nakala za Maandiko. Nakala hizi, ambazo zilikuwa ni matunda ya miezi na miaka ya kazi ngumu, walizibeba, na kila wakati walipoweza kufanya hivyo bila kutiliwa mashaka na mtu ye yote, kwa tahadhari waliweka baadhi ya nakala hizo katika njia za wale ambao mioyo yao ilionekana kuwa wazi kupokea ukweli. Tangu wakiwa kwenye magoti ya mama zao vijana Wawaldensia walifundishwa kusudi hili likiwa mawazoni; waliijua kazi yao na kwa uaminifu waliifanya. Waongofu wa imani ya kweli, walipatikana katika taasisi hizi za elimu, na mara nyingi kanuni zake zilionekana kupenya na kusambaa katika shule nzima; pamoja na hayo viongozi wa upapa hawakuweza, kwa uchunguzi mkali, kugundua chanzo cha kile ambacho wao walikiita mafundisho ya upotovu yanayoharibu.PKSw 50.2

  Roho ya Kristo ni roho ya kimishenari. Msukumo wa kwanza kabisa wa moyo uliobadilishwa ni kuwaleta wengine pia kwa Mwokozi. Hiyo ndiyo ilikuwa roho ya Wakristo wa Kivodwaa. Waliamini kuwa Mungu alitaka jambo kubwa zaidi kutoka kwao kuliko kuhifadhi tu ukweli katika usafi wake katika makanisa yao; kuwa wajibu mkubwa ulikuwa umewekwa juu yao wa kuwaangazia nuru yao walio gizani; kwa nguvu kubwa ya neno la Mungu walitafuta kuvunja utumwa ambao Rumi ilikuwa imeuleta. Wachungaji wa Kivodwaa walikuwa wamefundishwa kuwa wamishenari, kila mtu aliyetarajia kujiunga na uchungaji akitakiwa kwanza kupata uzoefu wa kuwa mwinjilisti. Kila mmoja alitakiwa kutumika miaka mitatu katika eneo fulani la kimishenari kabla ya kupewa kanisa la kuongoza nyumbani. Huduma hii, ikihitaji tangu mwanzo kujikana nafsi na kujinyima, ulikuwa mwanzo mzuri wa maisha ya kichungaji katika zama hizo zilizojaribu roho za watu. Vijana waliowekewa mikono ya uchungaji waliona mbele yao, siyo mustakabali wa utajiri na utukufu wa dunia, bali maisha ya kazi ngumu na hatari, na pengine hatima ya kuwa mfia dini. Wamishenari walitumwa wawili wawili, kama Yesu alivyowatuma wanafunzi Wake. Kawaida, kila kijana alipangwa kufanya kazi na mtu mwenye umri mkubwa na uzoefu, kijana akiwa chini ya uongozi wa mwenzi wake, aliyewajibika kumfundisha, na ambaye mafundisho yake ilipasa yazingatiwe na kijana. Watendakazi hawa waliofanya kazi pamoja, siyo kwamba waliambatana kila wakati, lakini mara nyingi walikutana kwa ajili ya maombi na kushauriana, hivyo kuimarishana katika imani.PKSw 51.1

  Kueleweka kwa lengo la utume wao ingekuwa ndiyo hakikisho la kushindwa kwa utume; hivyo, kwa uangalifu mkubwa walificha tabia yao halisi. Kila mchungaji alikuwa na ujuzi wa shughuli au taaluma fulani, na wamishenari walitekeleza kazi yao chini ya mwavuli wa shughuli za kawaida za utafutaji zisizokuwa za kidini. Mara nyingi walichagua kazi ya biashara ya jumla au reja reja. “Walibeba hariri, vito vya thamani, na vitu vingine, ambavyo kwa wakati huo havikupatikana maeneo ya karibu isipokuwa tu masoko ya mbali; na walikaribishwa kama wafanyabiashara wakubwa ambapo wangefukuzwa kama wamishenari” (Wylie, b. 1, ch. 7). Wakati wote huo mioyo yao iliinuliwa juu kwa Mungu kupata hekima ya kuwasilisha hazina iliyo ya thamani zaidi kuliko dhahabu au vito vya thamani. Kwa siri walibeba nakala za Biblia, zikiwa nzima au sehemu yake; na fursa ilipojitokeza waliwaeleza wateja wao kuhusu nakala hizo. Mara nyingi hamu ya kusoma neno la Mungu iliamshwa, na sehemu ya Maandiko iliachwa kwa furaha kwa wale waliotamani kuipokea.PKSw 51.2

  Kazi ya wamishenari hawa ilianzia katika maeneo tambarare na mabondeni karibu na milima yao, lakini ilipanuka mbali zaidi ya mipaka ile. Wakitembea kwa miguu isiyovalishwa kitu cho chote na mavazi yaliyochakaa kwa sababu ya safari nyingi kama zilivyokuwa nguo za Bwana wao, walipita katika miji mikuu na walipenya hadi katika nchi za mbali. Kila mahali walisambaza mbegu za thamani. Makanisa yalichipuka katika njia yao, na damu ya wafia dini ilishuhudia kwa ajili ya ukweli. Siku ya Mungu itafunua mavuno makubwa ya roho zilizokusanywa kwa kazi za hawa watu waaminifu. Likiwa limejificha na likiwa kimya, neno la Mungu lilipenya katika ulimwengu wa Ukristo na lilipokelewa kwa furaha katika nyumba na mioyo ya watu.PKSw 51.3

  Kwa Wawaldensia Maandiko hayakuwa tu kumbukumbu za Mungu alivyoshughulikia wanadamu hapo kale, na ufunuo wa wajibu na majukumu ya wakati huu, bali ufunuo wa hatari na utukufu wa wakati ujao. Waliamini kuwa mwisho wa mambo yote haukuwa mbali, na walivyosoma Biblia kwa maombi na machozi waliguswa zaidi na maneno yake ya thamani na wajibu wa kutangaza kwa wengine kweli zake zinazookoa. Waliuona mpango wa wokovu ukiwa umefunuliwa kwa uwazi zaidi katika kurasa zake takatifu, na walipata faraja, tumaini, na amani kwa kumwamini Yesu. Nuru ilivyoangaza ufahamu wao na kuleta furaha mioyoni mwao, walipata shauku ya kuwaangazia miale ya nuru yake kwa wale walio gizani na walio katika makosa ya upapa.PKSw 52.1

  Waliona kuwa chini ya uongozi wa papa na makasisi, watu wengi walikuwa wakijaribu kupata msamaha bila mafanikio kwa kuitesa miili yao kwa ajii ya dhambi za roho zao. Wakiwa wamefundishwa kutumainia kazi zao njema kuwaokoa, walikuwa daima wakijitazama wenyewe, akili zao zikitafakari hali yao ya dhambi, wakiona walivyokabiliwa na hasira ya Mungu, wakiitesa miili na roho zao, lakini bila kupata nafuu. Hivyo roho zenye bidii kubwa zilikuwa zimefungwa kwa mafundisho ya Rumi. Maelfu walitupilia mbali marafiki na ndugu wa karibu, walitumia maisha yao katika vyumba vya watawa. Kwa kufungwa mara kwa mara na vipigo vya kikatili, kwa kukesha mpaka usiku wa manane, kwa kuanguka kifudi-fudi kwa masaa mengi kwenye mawe yaliyolowa maji ya makazi yao yanayokera, kwa kutembea kwa miguu safari ndefu, kwa adhabu za kuaibisha na suluba za kutisha, maelfu walitafuta bila mafanikio amani ya dhamiri. Wakiteswa kwa utambuzi wa dhambi, na kuumizwa kwa hofu ya ghadhabu ya kisasi cha Mungu, wengi waliteseka, mpaka miili yao iliyoishiwa nguvu iliposalimu amri, na bila mwale mmoja wa nuru au tumaini waliingia kaburini.PKSw 52.2

  Wawaldensia walitamani kuwamegea mkate wa uzima watu hawa waliokuwa wakifa kwa njaa ya kiroho, kuwafungulia ujumbe wa amani katika ahadi za Mungu, na kuwaelekeza kwa Kristo kama tumaini lao pekee la wokovu. Fundisho waliloliamini kuwa matendo mema yanaweza kupatanisha uvunjaji wa sheria ya Mungu lilijengwa juu ya uongo. Kutegemea kazi ya mwanadamu kupata wokovu kunapotosha mtazamo wa upendo wa milele wa Kristo. Yesu alikufa kuwa kafara kwa ajili ya mwanadamu kwa sababu mwanadamu aliyeanguka dhambini hawezi kufanya jambo lo lote la kumfanya akubalike mbele za Mungu. Wema wa Mwokozi aliyesulubiwa na kufufuka ni msingi wa imani ya Kikristo. Tegemeo la roho kwa Kristo ni jambo halisi, na uhusiano wake na Yeye lazima uwe wa karibu, kama ule wa mguu na mwili, au tawi na mzabibu.PKSw 52.3

  Mafundisho ya mapapa na makasisi yalikuwa yamewafanya watu kuiona tabia ya Mungu, na hata ya Kristo, kama katili, ya huzuni, na inayotisha. Mwozi aliwakilishwa kama ambaye hana huruma kwa mwanadamu katika hali yake ya kuanguka kiasi kwamba alihitaji upatanisho wa makasisi na watakatifu. Waliokuwa wameangaziwa na neno la Mungu walitamani kuzielekeza roho hizi kwa Yesu kama Mwokozi wao mwenye huruma na upendo, akiwa amesimama na mikono iliyonyooshwa, akiwaalikwa wote wamwendee na mizigo yao ya dhambi, mashaka na uchovu wao. Walitamani kuondoa vikwazo ambavyo Shetani alikuwa amevirundika ili watu wasione ahadi, na kumwendea Mungu moja kwa moja, wakiungama dhambi zao, na kupata msamaha na amani.PKSw 53.1

  Kwa shauku kubwa, mmishenari wa Kivodwaa aliwafunulia kweli za injili watu waliokuwa wanatafuta ukweli. Kwa tahadhari kubwa aliwatolea sehemu za nakala za Maandiko Matakatifu zilizonakiliwa kwa uangalifu. Ilikuwa furaha yake kubwa kuipa tumaini roho iliyokuwa na shauku kubwa, iliyopondeka kwa sababu ya dhambi, iliyomwona Mungu kuwa ni Mungu wa kisasi tu, aliyekuwa akisubiri kutekeleza haki. Kwa midomo iliyotetemeka na macho yaliyojaa machozi, alipiga magoti na kuwafunulia ndugu zake ahadi za thamani zinazofunua tumaini pekee la mwenye dhambi. Kwa njia hiyo nuru ya ukweli ilipenya akili nyingi zilizokuwa gizani, ikaondoa wingu la huzuni, mpaka Jua la Haki lilipoangaza moyoni na miale Yake inayoponya. Mara nyingi sehemu ya Maandiko ilisomwa tena na tena, msikilizaji akiwa na shauku kwamba usomaji urudiwe, kana kwamba alitaka kujiridhisha kuwa amesikia kwa usahihi. Hususani usomaji wa kurudiwa-rudiwa ulitamaniwa sana maneno haya yaliposomwa: “Damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote” (1 Yohana 1:7). “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye” (Yohana 3:14, 15).PKSw 53.2

  Watu wengi hawakudanganyika kuhusiana na madai ya Rumi. Waliona maombi ya wanadamu au malaika kwa niaba ya mwenye dhambi hayakuwa na maana yo yote kwa mwenye dhambi: “Kristo ni kuhani wangu; damu Yake ni kafara Yangu; madhabahu Yake ni ungamo langu.” Walijisalimisha kikamilifu kwa wema wa Yesu, wakikariri maneno, “Pasipo imani haiwezekani kumpendeza” (Waebrania 11:6). “Kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Matendo 4:12).PKSw 53.3

  Hakikisho la upendo wa Mwokozi lilionekana kubwa mno kueleweka kwa baadhi ya roho maskini zilizosukwa-sukwa na dhoruba za uongo. Maneno hayo yalileta furaha kubwa mno, mafuriko ya nuru yaliyowaangazia yaliwafanya kujiona kama wamechukuliwa mbinguni. Mikono yao ilishikiliwa kwa upendo na mkono wa Kristo; nyayo zao zimeoteshwa juu ya Mwamba wa Zama zote. Hofu zote za kifo zilitoweka. Waliweza sasa kutamani gereza na mijeledi ikiwa kwa njia hiyo wangeweza kumheshimu Mkombozi wao.PKSw 53.4

  Katika mahali pa siri neno la Mungu lililetwa hivyo na kusomwa, nyakati zingine kwa roho moja, nyakati zingine kwa kikundi kidogo cha watu waliokuwa wakitamani nuru na ukweli. Mara nyingi usiku kucha ulitumiwa kwa jinsi hiyo. Kwa hiyo hali ya kushangaa na kushtuka ilikuwa kubwa kwa wasikilizaji kiasi ambacho mjumbe wa rehema alilazimishwa mara nyingi kukatisha usomaji mpaka akili ielewe habari njema ya wokovu. Mara nyingi maneno kama haya yalisemwa: “Je, kweli Mungu anaweza kukubali sadaka yangu? Je, Mungu anaweza kutabasamu akiniona? Je, Mungu anaweza kunisamehe?” Jibu lilisomwa: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28). Imani ilishikilia ahadi, na jibu la furaha lilisikika: “Hakuna safari za kwenda mbali; hakuna safari za maumivu za kwenda mahali patakatifu. Naweza kuja kwa Yesu sasa hivi jinsi nilivyo, mwenye dhambi na mchafu, na hatatupilia mbali ombi la toba. ‘Dhambi zako umesamehewa.’ Zangu, hata zangu, zinaweza kusamehewa!”PKSw 54.1

  Wimbi la furaha takatifu lilijaza moyo, na jina la Yesu lingekuzwa kwa sifa na shukurani. Roho zenye furaha zilirudi nyumbani kwao kueneza nuru, kuwasimulia wengine, kwa kadiri walivyoweza, uzoefu wao mpya; kuwa wamepata Njia ya kweli na uzima. Kulikuwa na nguvu ya ajabu na ya dhati katika maneno ya Maandiko yaliyosema na mioyo moja kwa moja ya wale waliokuwa wana shauku kwa ajili ya ukweli. Ilikuwa sauti ya Mungu, na ilikuwa na nguvu ya ushawishi kwa wale walioisikia.PKSw 54.2

  Mjumbe wa ukweli aliendelea na safari yake; lakini mwonekano wake wa unyenyekevu, udhati wake, umakini wake na kujitoa kwake kwa moyo, viliongelewa sana mara nyingi. Katika matukio mengi wasikilizaji wake hawakupata fursa ya kumwuliza alikotoka au alikokwenda. Walikuwa wametekewa, kwanza kwa mshangao, na baadaye kwa shukurani na furaha, kiasi kwamba hawakuwa na muda wa kufikiri juu ya kumwuliza jambo lo lote. Walipomsihi afuatane nao kwenda katika nyumba zao, aliwajibu kuwa ilimpasa kuwatembelea kondoo wa kundi waliopotea. Je, pengine alikuwa malaika kutoka mbinguni? Waliuliza.PKSw 54.3

  Mara nyingi mjumbe wa ukweli hakuonekana tena. Alikuwa ameenda katika nchi zingine, au alikuwa akiteseka katika gereza lisilojulikana, au pengine mifupa yake ilikuwa ikikaukia mahali alipofia kama shahidi wa ukweli. Lakini maneno aliyokuwa ameyaacha nyuma hayakuweza kuharibiwa. Yalikuwa yakifanya kazi katika mioyo ya watu; matokeo yake yaliyobarikiwa yataeleweka kikamilifu tu katika siku ya hukumu.PKSw 54.4

  Wamishenari wa Wawaldensia walikuwa wanavamia ufalme wa Shetani, na nguvu za giza ziliamshwa na kuwa makini zaidi. Kila juhudi ya kueneza ukweli ilichunguzwa na mfalme wa uovu, na aliamsha hofu ya mawakala wake. Viongozi wa upapa waliona dalili za hatari kwa kazi yao kutokana na kazi za hawa waenda kwa miguu wanyenyekevu. Ikiwa nuru itaruhusiwa kuangaza bila kizuizi, ingeweza kufagilia mbali mawingu ya makosa yaliyowafunika watu. Ingeelekeza akili za watu kwa Mungu pekee na ingeweza kuamgamiza ukuu wa Rumi hatimaye.PKSw 55.1

  Uwepo wa watu hawa peke yake, walioshikilia imani ya kanisa la awali, ulikuwa ni ushuhuda wa daima dhidi ya uasi wa Rumi, na hivyo uliamsha chuki na mateso makali. Kukataa kwao kusalimisha Maandiko lilikuwa pia kosa ambalo Rumi isingelivumilia. Rumi ilidhamiria kuwafuta kutoka duniani. Sasa ilianzishwa vita ya kidini ya kutisha dhidi ya watu wa Mungu katika makazi yao ya milimani. Wapelelezi walitumwa kwenda kuwafuatilia, na mandhari ya Habili akianguka mbele ya mwuaji Kaini ilirudiwa mara nyingi.PKSw 55.2

  Tena na tena ardhi zilizokuwa na rutuba zilibaki ukiwa, makazi na makanisa yao yakifagiliwa kabisa, kiasi kwamba mahali palipokuwa na mashamba yaliyostawi vizuri na nyumba za watu wasiokuwa na hatia, wachapa kazi, palibaki jangwa tu. Kama mnyama mkali anavyopandwa na hasira zaidi anapoonja damu, kadhalika hasira ya mapapa iliwasha zaidi mateso ya wahanga wao. Wengi wa mashahidi hawa kwa ajili ya imani safi walifuatiliwa katika milima na waliwindwa katika mabonde walipokuwa wamejificha, wakikingwa na misitu mikubwa na vilele vya miamba. Hakuna shitaka ambalo lingetolewa dhidi ya tabia na uadilifu wa kundi hili la watu waliopigwa vita. Hata maadui zao waliwatangaza kuwa wenye amani, wakimya, watu wacha Mungu. Kosa lao kubwa lilikuwa kutokumwabudu Mungu kulingana na matakwa ya papa. Kwa uhalifu huu kila dharau, tusi, na mateso ambayo watu au mashetani wangeweza kubuni, yalirundikwa juu yao.PKSw 55.3

  Wakati Rumi ilipodhamiria kukiangamiza kikundi kilichochukiwa, barua ilitolewa na papa, ikiwahukumu kuwa waasi dhidi ya mafundisho ya kanisa, na kuamuru wachinjwe (Tazama Kiambatanisho). Hawakushtakiwa kama wazururaji, au wadhulumaji, au wenye fujo; bali ilitangazwa kuwa walikuwa na mwonekano wa uchaji na utakatifu ulioshawishi “kondoo wa kundi la kweli.” Hivyo papa aliamuru “kikundi kiovu na kinachochukiza cha watu waovu,” ikiwa “watakataa kukana, wapondwe-pondwe kama nyoka wenye sumu kali” (Wylie, b. 16, ch. 1). Je, kiongozi huyu alitarajia kukutana na maneno haya tena? Je, alijua kuwa yalikuwa yameandikwa katika vitabu vya mbinguni, akutane nayo siku ya hukumu? “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo,“Yesu alisema, “mlinitendea mimi” (Mathayo 25:40).PKSw 55.4

  Barua hii ilitaka washiriki wote wa kanisa kujiunga na vita vya msalaba dhidi ya wapinzani wa mafundisho ya kanisa. Kama motisha ya kujiunga na kazi hii ya kikatili, barua iliwapa watu wanaojiunga “kinga dhidi ya mateso na adhabu za kanisa, za jumla na mahsusi; kuliwafungua waliojiunga kutoka katika viapo ambavyo walikuwa wamefanya; iliwapa uhalali wa kumiliki mali waliyoipata kwa njia isiyo halali; na kuwapa ahadi ya ondoleo la dhambi zao zote wale ambao wangewaua wapinzani dhidi ya mafundisho yao. Ilifuta mikataba yote iliyowanufaisha Wavodwa (Wafuasi waaminifu wa Kristo), iliwaamrisha waliokuwa katika nyumba zao waende zao, iliwakataza watu wote wasiwape msaada wo wote, na iliwapa mamlaka watu wote kuchukua na kumiliki mali zao” (Wylie, b. 16, ch. 1). Waraka huu unafunua wazi roho kuu iliyo nyuma ya pazia. Ni ngurumo ya joka, na siyo sauti ya Kristo, inayosikika ndani yake.PKSw 56.1

  Viongozi wa upapa hawakujenga tabia zao kulingana na kiwango kikuu cha sheria ya Mungu, bali walisimamisha kiwango kinachoendana na matakwa yao, na waliazimia kuwalazimisha wengine wote wafuate kiwango hicho kwa kuwa tu kimewekwa na Rumi. Uovu wa kutisha sana ulitendwa. Makasisi na mapapa fisadi na wenye kufuru walitenda kazi waliyopewa na Shetani. Rehema haikuwemo katika roho zao. Roho ile ile iliyomsulubisha Kristo na kuwaua mitume, roho ile ile iliyomsukuma Nero mwenye kiu ya damu dhidi ya watu waaminifu wa nyakati zake, ilikuwa kazini kuwafuta duniani watu wanaopendwa na Mungu.PKSw 56.2

  Mateso waliyoyapata kwa karne nyingi watu hawa wanaomcha Mungu waliyavumilia kwa subira kubwa na bila kuyumba ili kumheshimu Mkombozi wao. Licha ya vita vya msalaba dhidi yao, na mauaji ya kinyama yaliyowapata, waliendelea kutuma wamishenari wao kusambaza ukweli wa thamani. Waliwindwa hadi wakauawa; lakini damu yao ilimwagilia mbegu zilizopandwa, na hazikukosa kuzaa matunda. Kwa hiyo Wawaldensia walishuhudia kwa ajili ya Mungu kwa karne nyingi kabla ya kuzaliwa kwa Luther. Wakiwa wametawanyika katika nchi nyingi, walipanda mbegu za Matengenezo yaliyoanza wakati wa Wycliffe, yakapanuka na kupata kina nyakati za Luther, na yanapaswa kuendelezwa mpaka wakati wa mwisho na wale walio tayari kuteseka katika mambo yote kwa ajili ya “neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu Kristo” (Ufunuo 1:9).PKSw 56.3

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents