Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 26—Kazi ya Matengenezo

  Kazi ya matengenezo ya Sabato inayofanywa katika siku za mwisho ilitabiriwa katika unabii wa Isaya: “Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wo wote.” “Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote” (Isaya 56:1, 2, 6, 7).PKSw 345.1

  Maneno yanaelezea uhalisia wa zama za Ukristo, kama muktadha unavyoonesha: “Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa” (Aya ya 8). Hapa pametabiriwa ukusanyaji wa watu wa Mataifa kwa njia ya injili. Na kwa wale wanaoiheshimu Sabato, mbaraka umetangazwa. Kwa hiyo madai ya amri ya nne yanadumu kuwepo hata baada ya kusulubishwa, kufufuka, na kupaa kwa Kristo, hadi wakati watumishi Wake watakapokuwa wamehubiri injili kwa mataifa yote ujumbe wa habari njema.PKSw 345.2

  Bwana anaagiza kupitia kwa nabii huyo huyo: “Ufunge huo ushuhuda, ukaitie muhuri sheria kati ya wanafunzi wangu” (Isaya 8:16). Muhuri wa sheria ya Mungu unapatikana katika amri ya nne. Hii peke yake, miongoni mwa zote kumi, hudhihirisha jina na cheo cha Mtoa sheria. Inamtangaza kuwa Yeye ni Muumbaji wa mbingu na nchi, na hivyo, huonesha dai Lake la kuheshimiwa na kuabudiwa juu ya miungu yo yote mingine. Kando ya amri hii, hakuna kitu kingine katika Amri Kumi kinachoonesha ni kwa mamlaka ya nani sheria imetolewa. Wakati Sabato ilipobadilishwa na mamlaka ya upapa, muhuri uliondolewa katika sheria. Wanafunzi wa Yesu wameitwa kurudisha muhuri kwa kuinua Sabato ya amri ya nne na kuirudisha mahali pake sahihi kama kumbukumbu ya Muumbaji na ishara ya mamlaka Yake.PKSw 345.3

  “Na waende kwa sheria na ushuhuda.” Ingawa mafundisho na nadharia zinazopingana zipo nyingi, sheria ya Mungu ndiyo mwongozo usiokosea ambapo maoni, mafundisho, na nadharia zote vinapaswa vipimwe. Nabii anasema: “Ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi” (Aya ya 20).PKSw 345.4

  Kwa mara nyingine tena, amri imetolewa: “Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.” Siyo ulimwengu wa waovu, lakini wale ambao Bwana anawaita “watu wangu,” ambao inapasa waambiwe makosa yao. Anaeleza zaidi: “Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu” (Isaya 58:1, 2). Hapa limedhihirishwa tabaka la watu wanaojiona wenyewe kuwa wenye haki na wanaoonekana kuwa na shauku ya kufanya kazi ya Mungu; lakini onyo kali na zito la Mchunguzaji wa mioyo anawaona kuwa wavunjaji wa amri za Mungu.PKSw 345.5

  Kwa hiyo nabii anataja amri ambayo imeachwa: “Utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu wako usihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana” (Aya ya 12-14). Unabii huu unahusu pia wakati wetu. Upotoshaji wa sheria ya Mungu ulifanywa wakati Sabato ilipobadilishwa na mamlaka ya Kiroma. Lakini wakati umefika ambapo amri hiyo ya Mungu inapaswa irudishwe. Upotoshwaji unapaswa urekebishwe na msingi wa vizazi vingi uinuliwe.PKSw 346.1

  Ikiwa imetakaswa kwa pumziko na mbaraka wa Muumbaji, Sabato ilitunzwa na Adamu katika hali yake ya kutokuwa na hatia katika Edeni takatifu; ilitunzwa na Adamu, aliyeanguka lakini aliyetubu, na ilitunzwa na Adamu baada ya kufukuzwa kutoka Edeni. Sabato ilitunzwa na wazee wote, tangu Habili hadi Nuhu mwenye haki, Ibrahimu, hadi Yakobo. Wakati wateule walipokuwa utumwani Misri, wengi, katikati ya ibada ya sanamu ya wakati ule, waliisahau sheria ya Mungu; lakini Bwana alipowakomboa Israeli, aliitangaza sheria Yake katika utukufu wa kutisha kwa makutano waliokusanyika pamoja, wapate kujua mapenzi Yake na kumcha na kumtii milele.PKSw 346.2

  Tangu siku hiyo hadi leo maarifa ya sheria ya Mungu yamehifadhiwa duniani, na Sabato ya amri ya nne imekuwa ikitunzwa. Ingawa “mtu wa kuasi” alifanikiwa kuikanyaga siku takatifu ya Mungu, lakini hata katika kipindi cha utawala wake walikuwepo, wakiwa wamejificha katika maeneo ya siri, watu waaminifu walioiheshimu. Tangu wakati wa Matengenezo, wamekuwepo watu katika kila kizazi waliodumu kuitunza. Ingawa mara nyingi katikati ya dhihaka na mateso, ushuhuda wa kudumu umetolewa juu ya uendelevu wa sheria ya Mungu na wajibu mtakatifu wa kuitunza Sabato ya uumbaji.PKSw 346.3

  Ukweli huu, kama unavyowakilishwa katika Ufunuo 14 kuhusiana na “injili ya milele,” utalitambulisha kanisa la Kristo wakati wa ujio Wake wa pili. Kwa kuwa kama matokeo ya ujumbe wenye sehemu tatu imetangazwa: “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Na ujumbe huu ni wa mwisho kutolewa kabla ya ujio wa pili wa Bwana. Muda mfupi baada ya utangazaji wake Mwana wa Adamu anaonwa na nabii, akija katika utukufu kuvuna mavuno ya dunia.PKSw 346.4

  Wale waliopokea nuru kuhusiana na patakatifu na kutobadilika kwa sheria ya Mungu walijaa furaha na mshangao walipoona uzuri na mwafaka wa mfumo wa ukweli uliofunuliwa katika ufahamu wao. Walitamani kuwa nuru ambayo ilionekana kwao kuwa ya thamani sana ipelekwe kwa Wakristo wote; na waliamini kabisa kuwa ungepokelewa kwa furaha. Lakini ukweli ambao ungewafanya watofautiane na ulimwengu haukupokelewa na wengi waliodai kuwa wafuasi wa Kristo. Utii kwa amri ya nne ulihitaji kafara ambayo walio wengi walishindwa kuitoa.PKSw 347.1

  Madai ya Sabato yalipowasilishwa, wengi walitoa hoja kwa mtazamo wa kidunia. Walisema: “Siku zote tumetunza Jumapili, baba zetu waliitunza, na watu wengi wema na wacha Mungu wamekufa kwa furaha huku wakiitunza. Ikiwa walikuwa sahihi, na sisi tuko sahihi. Utunzaji wa Sabato hii mpya utatutoa nje ya mwafaka na ulimwengu, na tutapoteza mvuto wetu kwa ulimwengu. Kundi dogo la wanaotunza siku ya saba linaweza kuwa na tumaini la kufanya nini dhidi ya ulimwengu wote unaotunza Jumapili?” Ilikuwa kwa hoja kama hizo ambapo Wayahudi walijaribu kujihesabia haki kwa kumkataa kwao Kristo. Baba zao walikuwa wakikubaliwa na Mungu kwa kutoa sadaka za kuteketezwa, na kwa nini watoto wasipate wokovu kwa kufuata njia ile ile waliyopita baba zao?PKSw 347.2

  Kwa hiyo, wakati wa Luther, waumini wa upapa walitoa hoja kuwa Wakristo wa kweli wamefia katika imani ya Kikatoliki, na hivyo dini ile ilitosha kwa ajili ya wokovu. Hoja kama hiyo ni kikwazo kikubwa dhidi ya ukuaji katika imani au maisha ya kidini.PKSw 347.3

  Wengi walidai kuwa Utunzaji wa Jumapili ulikuwa fundisho kamili na desturi ya kanisa iliyojulikana mahali pengi na iliyodumu kwa karne nyingi. Dhidi ya hoja hii ilioneshwa kuwa Sabato na utunzaji wake vilikuwa vya zamani na ulioenea sehemu nyingi zaidi, hata ilikuwa na umri sawa na umri wa dunia yenyewe, na ilikuwa na idhini ya malaika na Mungu. Wakati misingi ya dunia ilipowekwa, wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, na wana wa Mungu wote walipopiga kelele za shangwe, ndipo msingi wa Sabato uliwekwa (Ayubu 38:6, 7; Mwanzo 2:1-3). Ni halali kabisa amri hii inastahili heshima yetu; haikuanzishwa na mamlaka ya kibinadamu na wala haikujengwa juu ya mapokeo ya kibinadamu; ilianzishwa na Mzee wa Siku na iliamriwa kwa neno Lake la milele.PKSw 347.4

  Wakati akili za watu zilipovutwa kutafakari juu ya mada ya matengenezo ya Sabato, wachungaji mashuhuri walipotosha neno la Mungu, wakitoa tafsiri kuhusu ushuhuda wa Sabato kwa namna ambayo ilinyamazisha akili zilizokuwa zikitafuta kuujua ukweli. Na wale ambao hawakuchunguza Maandiko wao wenyewe binafsi waliridhika kupokea mahitimisho ambayo yalipatana na matakwa yao. Kwa njia ya hoja, hila, mapokeo ya mababa, na mamlaka ya kanisa, wengi walijitahidi kuupindua ukweli. Mawakala wa ukweli walisukumwa kusoma zaidi Biblia ili waweze kutetea uhalali wa amri ya nne. Watu wanyenyekevu, wakiwa na neno la ukweli peke yake, walistahimili mashambulizi ya wasomi, ambao, kwa mshangao na hasira, maneno yao fasaha ya uongo yakiwa hayana nguvu dhidi ya hoja sahili, za moja kwa moja za watu waliokuwa na ujuzi wa kina wa Maandiko badala ya mafundisho ya uongo ya vyuoni.PKSw 347.5

  Kwa kukosa ushahidi wa Biblia unaounga mkono hoja zao, wengi kwa juhudi zisizochoka walisisitiza—wakisahau jinsi ambavyo hoja kama hiyo ilitumiwa dhidi ya Kristo na mitume Wake: “Kwa nini watu wetu mashuhuri hawajui lolote kuhusu suala la Sabato? Lakini wachache ndio huamini kama mnavyoamini. Haiwezekani ninyi muwe sahihi na wasomi wengine wote ulimwenguni wasiwe sahihi.”PKSw 348.1

  Kukanusha hoja kama hizo ilikuwa muhimu kutumia Maandiko na historia ya jinsi Bwana alivyoshughulika na watu Wake katika zama zote. Mungu hufanya kazi kupitia wale wanaosikia na kutii sautiYake, wale ambao, ikiwa lazima, watasema ukweli usiokuwa mtamu, wale ambao hawaogopi kukemea dhambi zinazopendwa. Sababu za Bwana mara nyingi kutotumia watu walio na elimu ya juu na wenye vyeo vikubwa kuongoza katika harakati za matengenezo ni kwamba wanatumainia imani zao, nadharia, na mifumo yao ya kiteolojia, na hawaoni haja ya kufundishwa na Mungu. Wale tu walio na uhusiano binafsi na Chanzo cha hekima ndio wanaweza kuelewa au kueleza Maandiko. Watu walio na elimu ndogo ya shuleni nyakati zingine wanaitwa kutangaza ukweli, sio kwa sababu hawajasoma, bali kwa sababu ni watu wanaohisi kuwa na hitaji la kufundishwa na Mungu. Wanajifunza katika shule ya Kristo, na unyenyekevu na utii wao unawafanya kuwa wakuu. Kwa kuwapatia maarifa ya ukweli Wake, Mungu anawapa heshima kubwa ukilinganisha na heshima ya kidunia na ukuu wa kibinadamu ambao baada ya muda mfupi hupoteza uzito na umuhimu wake.PKSw 348.2

  Waadventista walio wengi waliukataa ukweli kuhusu hekalu na sheria ya Mungu, na wengi pia waliikana imani yao kuhusiana na vuguvugu la kiadventista na badala yake waliamini mawazo yasiyo ya kweli na yaliyopingana kuhusiana na unabii uliozungumzia vuguvugu lile. Baadhi walioongozwa kufanya kosa la kurudia-rudia kupanga wakati maalumu wa ujio wa Kristo. Nuru ambayo sasa ilikuwa iking'aa juu ya somo la patakatifu ingeweza kuwaonesha kuwa hakuna kipindi cha kiunabii ambacho kilifika hadi wakati wa ujio wa pili; ambacho wakati mahsusi wa ujio huo haukutabiriwa. Lakini, wakiwa wameiacha nuru, waliendelea kupanga wakati baada ya wakati kwa ajili ya kuja kwa Bwana mara ya pili, kwa kadiri walivyoendelea kukatishwa tamaa.; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifuPKSw 348.3

  Wakati kanisa la Wathesalonike lilipopokea mawazo potofu kuhusu ujio wa Kristo, mtume Paulo aliwashauri wapime matumaini na matarajio yao kwa uangalifu kwa njia ya neno la Mungu. Alichukua dondoo kutoka katika unabii ulioonesha matukio ambayo yangetokea kabla Kristo hajaja mara ya pili, na alionesha kuwa hawakuwa na sababu ya kutegemea ujio Wake katika siku zake. “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote” (2 Wathesalonike 2:3), ni maneno yake ya onyo. Ikiwa wangeendelea kuwa na matarajio ambayo hayana msingi katika Maandiko, wangeongozwa kupita katika njia isiyokuwa sahihi; kutokupata kile walichotarajia kungewapa nafasi wasioamini kuwadhihaki na kuwacheka, na wangekuwa katika hatari ya kusalimu amri kwa ukatishwaji tamaa huo na wangejaribiwa kutilia mashaka ukweli ulio muhimu kwa ajili ya wokovu wao. Onyo la mtume kwa Wathesalonike limebeba somo kwa watu wanaoishi katika siku za mwisho. Waadventista wengi walihisi kuwa ikiwa wasingeweka imani yao kwenye siku mahsusi ya ujio wa Bwana, wasingeweza kuwa na bidii na juhudi katika maandalizi. Lakini matumaini yao yanaposisimuliwa tena na tena, na wakati wote wakiishia kukatishwa tamaa, imani yao inapata mshtuko mkubwa kiasi kwamba wanakaribia sana kupoteza uwezo wa kuamini ukweli mkuu wa unabii.PKSw 348.4

  Kuhubiri wakati mahsusi kwa ajili ya hukumu, katika utangazaji wa ujumbe wa malaika wa kwanza, kuliagizwa na Mungu. Ukokotoaji wa vipindi vya kiunabii vilivyokuwa msingi wa ujumbe ule, ukiweka mwisho wa siku 2300 katika msimu wa vuli ya mwaka 1844, hauna dosari. Juhudi za mara kwa mara za kutafuta tarehe mpya kwa ajili ya mwanzo na mwisho wa vipindi vya kiunabii, na hoja zisizo na msingi zinazotumiwa kuunga mkono misimamo hiyo, siyo tu kuwa zinapeleka akili mbali na ukweli wa leo, bali pia zinasababisha dharau kwa juhudi zote za kuelezea unabii. Kwa kadiri upangaji wa siku mahsusi wa ujio wa pili wa Bwana unavyofanywa mara kwa mara, na kwa kadiri unavyofundishwa katika maeneo mengi, ndivyo unavyotimiza makusudi ya Shetani kwa ufanisi zaidi. Baada ya muda kupita, Shetani huchochea dhihaka na dharau dhidi ya mawakala wa siku hizo mahsusi za ujio wa Kristo, na kwa njia hiyo analeta aibu juu ya vuguvugu kuu la ujio wa pili wa Kristo la mwaka 1843 na mwaka1844. Wale wanaodumu katika kufanya kosa hili mwishowe wataweka tarehe ya baadaye sana kwa ajili ya ujo wa Kristo. Kwa njia hiyo wataongozwa kupumzika katika usalama bandia, na wengi hawataachana na uongo huo mpaka wajikute wamechelewa.PKSw 349.1

  Historia ya Israeli ya zamani ni mfano mzuri wa uzoefu uliopita wa Waadventista. Mungu aliwaongoza watu Wake katika vuguvugu la ujio wa pili, wakati alipowaongoza wana wa Israeli kutoka Misri. Katika kukatishwa tamaa huku kwao, imani yao ilijaribiwa kama vile imani ya Waebrania ilipojaribiwa kwenye Bahari ya Shamu. Ikiwa wangeendelea kuutumaini mkono unaoongoza uliokuwa nao katika uzoefu wao wa nyuma, wangeuona wokuvu wa Mungu. Ikiwa watu wote waliohusika kwa umoja wao katika vuguvugu la marejeo la mwaka 1844, wangepokea ujumbe wa malaika wa tatu na kuutangaza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, Bwana angetenda matendo makuu pamoja na juhudi zao. Mafuriko ya nuru yangeangazia ulimwengu wote. Miaka mingi iliyopita wakazi wa dunia wangekuwa wameonywa, kazi ya kufungia historia ya ulimwengu ingekuwa imekamilika, na Kristo angekuwa amerudi kwa ajili ya ukombozi wa watu Wake.PKSw 349.2

  Haikuwa mapenzi ya Mungu kuwa Israeli watange-tange jangwani kwa miaka arobaini; Alitamani waende moja kwa moja hadi katika nchi ya Kanaani na kuwastawisha pale, na kuwafanya kuwa watu watakatifu, wenye furaha. Lakini “hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao” (Waebrania 3:19). Kwa sababu ya kurudi nyuma kwao na uasi wao waliangamia jangwani, wengine waliinuliwa ili waingie katika Nchi ya Ahadi. Kwa misingi hiyo hiyo, haikuwa mapenzi ya Mungu kuwa Kristo akawie sana kwa kiasi hicho na watu Wake wabaki kwa miaka mingi katika ulimwengu huu wa dhambi na huzuni. Lakini kutokuamini kuliwatenga na Mungu. Walipokataa kufanya kazi aliyokuwa amewapangia, wengine waliinuliwa kuutangaza ujumbe. Kwa sababu ya rehema Yake kwa ulimwengu, Yesu amechelewesha ujio Wake, ili wenye dhambi wapate fursa ya kusikiliza onyo na kupata hifadhi ndani Yake kabla ghadhabu ya Mungu haijamwagwa.PKSw 350.1

  Sasa kama ilivyokuwa katika zama zilizopita, wasilisho la ukweli linalokemea dhambi na makosa ya wakati huu litaamsha upinzani. “Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa” (Yohana 3:20). Watu wanapoona kuwa hawawezi kuthibitisha hoja zao kwa Maandiko, wengi wanadhamiria kushikilia kwa gharama zote, na kwa roho mbaya wanashambulia tabia na nia za wale wanaotetea ukweli usiopendwa sana. Ni sera hiyo hiyo ambayo imetumiwa katika zama zote. Eliya alitangazwa kuwa mtaabishaji wa Israeli, Yeremia aliitwa msaliti, Paulo aliitwa mchafuzi wa hekalu. Tangu siku ile mpaka siku hii ya leo, wote wanaochagua kuwa watiifu kwa ukweli wanahukumiwa kuwa wachochezi, wazushi, au wanaogawa watu. Watu wengi wasioamini kiasi cha kulipokea neno la hakika la unabii watapokea kwa wepesi usio na swali shitaka dhidi ya wale wanaothubutu kukemea dhambi zinazopendwa na watu. Roho hii itaongezeka zaidi na zaidi. Na Biblia inafundisha wazi wazi kuwa wakati unakaribia ambapo sheria ya nchi itapingana na sheria ya Mungu kiasi ambacho yeyote ambaye atazitii amri zote za Mungu itampasa kukabiliana na adhabu kama mkosaji.PKSw 350.2

  Katika mazingira kama haya, wajibu wa mjumbe wa ukweli ni nini? Ahitimishe kuwa ukweli usihubiriwe, kwa kuwa mara nyingi matokeo yake ni kuwafanya watu wakwepe au wapinge madai yake? Hapa; hana sababu zaidi ya kutokutoa ushuhuda wa neno la Mungu, kwa sababu unaamsha upinzani, kuliko ilivyokuwa kwa Wanamatengenezo wa awali. Kuikiri imani kulikofanywa na watakatifu na wafia dini wa zamani kuliandikwa na kuwekwa katika kumbukumbu kwa manufaa ya vizazi vilivyofuata. Mifano ile hai ya utakatifu na uaminifu usioyumba imehifadhiwa ili kuchochea ujasiri kwa wale ambao sasa wanaitwa kusimama kama mashahidi kwa ajili ya Mungu. Walipokea neema na ukweli, siyo kwa ajili yao peke yao, bali ili, kupitia kwao, maarifa ya Mungu yaangazie dunia. Je, Mungu ametoa nuru kwa ajili ya watumishi Wake katika kizazi hiki? Ikiwa hivyo, inapasa waiache iangaze ulimwenguni.PKSw 350.3

  Zamani Bwana alimwambia mtu mmoja aliyesema katika jina Lake: “Bali nyumba ya Israeli hawatakusikiliza wewe; kwa kuwa hawanisikilizi mimi.” Hata hivyo alisema: “Nawe utawaambia maneno yangu, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia” (Ezekieli 3:7; 2:7). Kwa mtumishi wa Mungu wakati huu amri inatolewa: “Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao” (Isaya 58:1).PKSw 351.1

  Kwa kadiri fursa zake zinavyopanuka, kila mmoja ambaye amepokea nuru ya ukweli yuko chini ya wajibu ule ule mzito na kutisha kama aliokuwa nabii Ezekieli, ambaye kwake neno la Bwana lilimjia, likisema: “Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu. Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako” (Ezekieli 33:7-9).PKSw 351.2

  Kikwazo kikuu katika kuukubali na kuutangaza ukweli ni ukweli kuwa unajumuisha usumbufu na aibu. Hii ndiyo hoja pekee dhidi ya ukweli ambao mawakala wake hawajawahi kukanusha. Lakini hili haliwazuii wafuasi wa kweli wa Kristo. Hawa hawasubiri mpaka ukweli upendwe na watu wengi. Wakishawishika kuhusu wajibu wao, wanakubali kwa hiari yao wenyewe kubeba msalaba, wakihesabu pamoja na Paulo kuwa “dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;” pamoja na yule wa zamani, “akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri” (2 Wakorintho 4:17; Waebrania 11:26).PKSw 351.3

  Bila kujali taaluma zao ni zipi, ni wale tu wanaoutumikia ulimwengu kwa moyo wa dhati wanaotenda kazi kwa sera zaidi kuliko kwa maoni binafsi katika masuala ya dini. Inatupasa kuchagua ukweli kwa sababu ni ukweli, na kuacha matokeo kwa Mungu. Ulimwengu unapaswa kuwashukuru watu wa kanuni, imani, na uthubutu kwa ajili ya mabadiliko yake.PKSw 351.4

  Hivyo ndivyo asemavyo Bwana: “Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao. Maana nondo itawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote” (Isaiah 51:7, 8).PKSw 351.5

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents