Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 40—Watu wa Mungu Wakombolewa

  Wakati ulinzi wa sheria za kibinadamu utakapoondolewa kwa wale wanaoheshimu sheria ya Mungu, zitakuwepo, katika nchi mbalimbali, harakati za wakati uleule za kuwaua. Wakati uliopangwa utakapokaribia, watu watapatana kuangamiza kikundi cha watu wanaochukiwa. Itaazimiwa kuwapiga pigo moja la uhakika, ambalo litanyamazisha kabisa sauti ya mfarakano wa mawazo na onyo.PKSw 484.1

  Watu wa Mungu—baadhi yao wakiwa katika vyumba vya gereza, baadhi wakiwa wamejificha katika maeneo ya siri misituni na milimani—wakingali katika kuomba kwa ajili ya ulinzi wa Mungu, wakati kila mahali makundi ya watu wenye silaha, wakishawishiwa na majeshi ya malaika waovu, wanajiandaa kwa ajili ya kazi ya mauji. Ni sasa, katika saa ya uhitaji, ambapo Mungu wa Israeli ataingilia kati kuwaokoa wateule Wake. Bwana anasema; “Mtakuwa na wimbo kama vile wakati wa usiku, ishikwapo sikukuu takatifu, mtakuwa na furaha ya moyo kama vile mtu aendapo ... katika mlima wa Bwana, aliye Mwamba wa Israeli. Naye Bwana atawasikizisha watu sauti yake ya utukufu, naye atawaonyesha jinsi mkono wake ushukavyo, na ghadhabu ya hasira yake, na mwako wa moto ulao, pamoja na dhoruba, na tufani, na mvua ya mawe ya barafu” (Isaya 30:29, 30).PKSw 484.2

  Katikati ya kelele za ushindi, dhihaka, na laana, makundi ya watu waovu wanavamia mawindo yao, ambapo, tazama, giza nene, giza totoro kuliko usiku, linaifunika dunia. Ndipo upinde wa mvua, uking'aa kwa utukufu utokao katika kiti cha enzi cha Mungu, unaonekana mbinguni na unaonekana kuwazunguka kila kundi la watu wanaoomba. Makundi ya watu wenye hasira yanashtuka. Kelele zao za dhihaka zinakoma. Walengwa wa hasira zao za uuaji wanasahauliwa. Kwa hisia zenye hofu wanaona ishara ya agano la Mungu na wanatamani wakingwe dhidi ya mwangaza mkali unaowazidi nguvu.PKSw 484.3

  Kwa upande wa watu wa Mungu sauti, ya wazi na tamu, inasikika, ikisema, “Tazameni juu,” na wanapoinua macho yao kutazama mbinguni, wanaona upinde wa ahadi. Mawingu meusi, yenye hasira yaliyokuwa yamefunika anga yanatawanyika, na, kama Stefano, wanatazama juu mbinguni kwa bidii, na wanauona utukufu wa Mungu na wa Mwana wa Adamu wakiwa wamekaa juu ya kiti Chake cha enzi. Katika umbo Lake la Kimungu wanatambua unyenyekevu Wake; na kutoka katika midomo Yake wanasikia ombi likiwasilishwa mbele ya Baba Yake na malaika watakatifu: “Hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo” (Yohana 17:24). Tena sauti, nzuri na ya ushindi, inasikika, ikisema: “Waje! waje! watakatifu, hawana madhara, na ni safi. Wamelitunza neno la subira Yangu; watembee miongoni mwa malaika;” na midomo mikavu, inayotetemeka ya wale walioishika sana imani yao inapiga kelele ya ushindi.PKSw 484.4

  Ni wakati wa usiku wa manane ambapo Mungu anadhihirisha nguvu Yake kwa ajili ya ukombozi wa watu Wake. Jua linatokea, liking'aa katika nguvu yake. Ishara na maajabu vinatokea mfululizo na haraka haraka. Waovu wanayaona matukio hayo kwa hofu na mshangao, wakati wenye haki wanatazama kwa furaha kuu viashiria vya ukombozi wao. Kila kitu miongoni mwa vitu vya asili kinaonekana kuondoka katika utaratibu wake. Vijito vinaacha kutiririka. Mawingu meusi, mazito yanaibuka na yanagongana. Katikati ya mbingu zenye giza totoro kunaonekana mwanya mmoja wenye utukufu usioelezeka, ambamo kunatokea sauti ya Mungu kama sauti ya maji mengi, Ikisema: “Imekwisha kuwa” (Ufunuo 16:17).PKSw 485.1

  Sauti ile inatetemesha mbingu na dunia. Kunatokea tetemeko kubwa sana, “ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo” (Aya 17, 18). Anga linaonekana kufunguliwa na kufungwa. Utukufu kutoka katika kiti cha enzi cha Mungu unakaribia kupenya anga. Milima inayumbayumba kama tete katika upepo, na mawe yenye sura mbaya yanasambazwa kila upande. Inasikika ngurumo kama ya tufani inayokuja. Bahari inachafuka. Inasikika sauti ya tufani kama sauti ya pepo waliotumwa kwenda kuangamiza. Dunia nzima inanyumbuka ikipanda na kushuka kama mawimbi ya bahari. Uso wa dunia unataka kuchanika. Misingi yake yenyewe inaonekana kama imeng'oka. Vilele vya milima vinazama. Visiwa vyenye wakazi vinatoweka. Bandari ambazo zimekuwa kama Sodoma kwa uovu zinamezwa na maji yenye dhoruba kali. Babeli mkuu unakumbukwa mbele za Mungu, “kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake.” Mvua ya mawe kubwa sana, kila moja “kama uzito wa talanta,” inafanya kazi yake ya kuangamiza (Aya 19, 21). Miji yenye kiburi ya dunia inashushwa chini. Maeneo ya kifahari, ambayo wakuu wa dunia hii wameteketezea mali zao ili kujitukuza, yanaanguka na kuwa magofu mbele ya macho yao. Magereza yanapasuliwa, na watu wa Mungu, walioko mahabusu kwa sababu ya imani yao, wanaachiwa huru.PKSw 485.2

  Makaburi yanafunguka, na “wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele” (Danieli 12:2). Wote ambao wamekufa katika imani ya ujumbe wa malaika wa tatu wanatoka makaburini wakiwa na utukufu, kusikia agano la Mungu la amani na wale ambao wameishika sheria Yake. “Na hao waliomchoma” (Ufunuo 1:7), wale waliodhihaki na kukejeli maumivu ya kifo cha Kristo, na wapinzani wakuu wa ukweli Wake na watu Wake, wanafufuliwa washuhudie heshima ikitolewa kwa wale waaminifu na watiifu.PKSw 485.3

  Mawingu mazito bado yamelifunika anga; lakini jua linapenya mawingu na kuonekana kila baada ya muda fulani kupita, likionekana kama jicho la Yehova linalolipiza kisasi. Radi kali zinapiga kutoka mbinguni, zikiifunika dunia kwa shuka la ndimi za moto. Juu ya ngurumo za kutisha za radi, sauti, zisizojulikana na za kutisha, zinatangaza kifo kwa ajili ya waovu. Maneno yaliyosemwa hayaeleweki kwa wote; lakini yanaeleweka kikamilifu kwa walimu wa uongo. Wale waliokuwa kabla wakiwa wakorofi, waliokuwa wakijivuna na wasiojali, waliokuwa wakifurahia ukatili wao kwa watu watunzao amri za Mungu, sasa wanazidi kuwa na wasiwasi na wanatetemeka kwa hofu. Vilio vyao vinasikika juu ya sauti ya vitu vya asili. Mashetani yanakiri uungu wa Kristo na yanatetemeka mbele ya nguvu Yake, wakati watu wakiomba kwa ajili ya rehema na kubembeleza katika hofu iliyokithiri.PKSw 486.1

  Manabii wa zamani walisema, walipoiona siku ya Mungu katika njozi takatifu: “Pigeni kelele za hofu; maana siku ya Bwana i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu” (Isaya 13:6). “Ingia ndani ya jabali; ukajifiche mavumbini mbele za utisho wa Bwana, mbele za utukufu wa enzi yake. Macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye Bwana, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo. Kwa maana kutakuwa siku ya Bwana wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini.” “Siku hiyo kila mtu atazitupilia mbali sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, walizojifanyia ili kuziabudu, kwa fuko na popo; ili aingie ndani ya pango za majabali, na ndani ya tundu za miamba iliyopasuka, mbele za utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia” (Isaya 2:10-12, 20, 21).PKSw 486.2

  Kupitia ufa uliopo katikati ya mawingu nyota inamulika ambayo ukali wa mwanga wake umeongezwa mara nne kinyume na giza lililokuwepo. Inatangaza tumaini na furaha kwa waaminifu, lakini ukali na hasira kwa wavunjaji wa sheria ya Mungu. Wale ambao wameteseka kwa ajili ya Kristo sasa wako salama, wamefichwa katika hema la siri la Bwana. Wamejaribiwa, na mbele ya ulimwengu na mbele ya wenye dhihaka dhidi ya ukweli wameonesha uaminifu wao Kwake Yeye aliyekufa kwa ajili yao. Badiliko la ajabu limetokea kwa wale ambao wamedumisha uaminifu wao mbele ya kifo. Wamekombolewa kutoka katika ukatili wa giza na wa kutisha wa watu waliogeuzwa kuwa kama mashetani. Nyuso zao, ambazo mpaka wakati mfupi uliopita zilikuwa zimekauka, zikiwa na wasiwasi, na zikisumbuka, sasa zinang'aa kwa mshangao, imani, na upendo. Sauti zao zinapaa juu kwa wimbo wa ushindi: “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake” (Zaburi 46:1-3).PKSw 486.3

  Wakati maneno haya ya dhamana takatifu yanapanda kwa Mungu, mawingu yanarudi nyuma, na mbingu zenye nyota zinaonekana, zikiwa na utukufu usioelezeka kinyume na anga jeusi totoro upande huu na upande huu. Utukufu wa jiji la mbinguni unatiririka kutoka katika malango yaliyo wazi. Ndipo kunatokea angani mkono ulioshikilia mbao mbili za mawe pamoja. Nabii anasema: “Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu” (Zaburi 50:6). Sheria takatifu, haki ya Mungu, ambayo katikati ya radi na ndimi za moto ilitangazwa kutoka Mlima Sinai kama mwongozo wa maisha, sasa inafunuliwa kwa watu kama kanuni ya hukumu. Mkono unafungua mbao zile, na zinaonekana Amri Kumi kama vile zimeandikwa kwa kalamu ya moto. Maneno ni ya wazi sana kiasi ambacho wote wanaweza kuyasoma. Kumbukumbu inaamshwa, giza la ushirikina na uzushi vinafutwa kutoka akilini, na kauli kumi za Mungu, fupi, za kina, zenye mamlaka, zinawasilishwa machoni pa wakazi wa dunia.PKSw 487.1

  Haiwezekani kueleza hofu na kukata tamaa kwa wale ambao wamekanyaga matakwa matakatifu ya Mungu. Mungu aliwapa sheria Yake; wangeweza kulinganisha na tabia zao na sheria hiyo na kurekebisha dosari zao wakati bado fursa ya kutubu na kufanya matengenezo ilipokuwepo; lakini ili kupata ukubali wa ulimwengu, waliweka pembeni kanuni zake na kuwafundisha wengine kuzivunja. Walijaribu kuwalazimisha watu wa Mungu kuinajisi Sabato Yake. Sasa wanaadhibiwa kwa sheria waliyoidharau. Kwa uwazi wa kutisha wanaona kuwa hawana udhuru. Walichagua yule ambaye walimtumikia na kumwabudu. “Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia” (Malaki 3:18).PKSw 487.2

  Maadui wa sheria ya Mungu, kutoka kwa wachungaji hadi kwa yule mdogo wao kabisa miongoni mwao, wanapata uelewa mpya wa ukweli na wajibu. Kwa kuchelewa sana wanaona kuwa Sabato ya amri ya nne ni muhuri wa Mungu aliye hai. Kwa kuchelewa sana wanaona asili ya kweli ya sabato yao bandia na msingi wa mchanga ambao wamekuwa wakijenga juu yake. Wanagundua kuwa wamekuwa wakipambana dhidi ya Mungu. Walimu wa dini wameongoza roho upotevuni huku wakifikiri kuwa waliwaongoza kwenda katika malango ya Paradiso. Ni mpaka siku ya hukumu ya mwisho ndipo utakapojulikana ukubwa wa wajibu wa watu walioko katika kazi takatifu na jinsi yalivyo ya kutisha matokeo ya kukosa uaminifu. Ni katika umilele peke yake ndipo tunaweza kukisia kwa usahihi hasara ya roho moja. Maangamizi yatakuwa ya kutisha ya mtu ambaye Mungu atamwambia: Ondoka, wewe mtumwa mwovu.PKSw 487.3

  Sauti ya Mungu inasikika mbinguni, ikitangaza siku na saa ya kuja kwa Yesu, na inatoa agano la milele kwa watu Wake. Kama milio ya radi yenye sauti kubwa sana maneno Yake yanabiringika na kuenea duniani kote. Israeli wa Mungu wanasimama wakisikiliza, macho yao yakiwa yametazama juu. Nyuso zao zinang'aa kwa utukufu Wake, na wanang'aa kama uso wa Musa ulivyong'aa aliposhuka kutoka Mlima wa Sinai. Waovu hawawezi kuwaangalia. Na mbaraka unapotangazwa kwa wale waliomheshimu Mungu kwa kutunza Sabato Yake takatifu na kuitakasa, kuna sauti kubwa ya ushindi.PKSw 488.1

  Muda si mrefu kunatokea upande wa mashariki wingu dogo jeusi, takribani ukubwa wa kiganja cha mtu. Ni wingu linalomzunguka Mwokozi na ambalo linaonekana kwa mbali kuzungukwa na giza. Watu wa Mungu wanatambua kuwa hii ni ishara ya Mwana wa Adamu. Kwa ukimya mkubwa wanalitazama linapokaribia duniani, likiwa jepesi na lenye utukufu zaidi, mpaka linakuwa wingu kubwa jeupe, chini kuna utukufu kama wa moto unaoteketeza, na juu yake kuna upinde wa mvua wa agano. Yesu anatokea kama mshindi mkuu. Sasa siyo “Mtu wa huzuni,” ili kunywa kikombe kichungu cha aibu na mateso, anakuja, akiwa mshindi wa mbingu na nchi, awahukumu walio hai na waliokufa. “Mwaminifu na Wa-kweli,” “kwa haki ahukumu na kufanya vita.” Na “majeshi yaliyo mbinguni” (Ufunuo 19:11, 14) wakamfuata. Pamoja na nyimbo za sauti ya mbinguni malaika, wengi, wasiokuwa na idadi, wanamsindikiza katika safari Yake. Anga lilionekana kujazwa na maumbo yanayong'aa—“elfu kumi mara elfu kumi, na elfu mara elfu.” Hakuna kalamu inayoweza kueleza mandhari hiyo; hakuna akili yenye uwezo wa kuelewa utukufu wake. “Utukufu wake ukazifunika mbingu, Nayo dunia ikajaa sifa yake. Mwangaza wake ulikuwa kama nuru” (Habakuki 3:3, 4) . Wakati wingu lililo hai liliposogea zaidi, kila jicho lilimwona Mfalme wa uzima. Hakuna taji ya miiba inayoharibu kile kichwa kitakatifu; lakini utepe wa utukufu unatulia juu ya uso Wake mtakatifu. Uso Wake unang'aa zaidi kuliko mwangaza mkali wa jua la mchana.” Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA” (Ufunuo 19:16).PKSw 488.2

  Mbele Yake “nyuso zote zimegeuka rangi;” hofu ya kukata tamaa milele inaanguka juu ya wakataaji wa rehema ya Mungu. “Moyo unayeyuka, na magoti yanagongana-gongana; ... na nyuso za wote zimekuwa nyeupe kwa hofu” (Yeremia 30:6; Nahumu 2:10). Kilio cha haki na kutetemeka: “Ni nani awezaye kusimama?” Wimbo wa malaika ulisitishwa, na kinatokea kipindi cha ukimya mkubwa. Ndipo sauti ya Yesu inasikika, ikisema: “Neema Yangu inakutosha.” Nyuso za wenye haki zinang'aa, na furaha inajaa ndani ya kila moyo. Na malaika wanapiga noti iliyo juu zaidi na kuimba tena wanavyosogea karibu na dunia.PKSw 488.3

  Mfalme na wafalme anashuka juu ya wingu, akiwa amezingirwa na ndimi za moto. Mbingu zinakunjwa kama karatasi, dunia inatetemeka mbele Yake, na kila mlima na kisiwa kinaondoka mahali pake. “Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza, Moto utakula mbele zake, na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote. Ataziita mbingu zilizo juu, Na nchi pia awahukumu watu wake” (Zaburi 50:3, 4).PKSw 489.1

  “Na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi. Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake. Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho” (Ufunuo 6:15-17).PKSw 489.2

  Kejeli na dharau vinakoma. Midomo ya waongo inanyamazishwa. Mgongano wa silaha, ghasia za vita, “wakati wa mshindo na mavazi yaliyofingirishwa katika damu” (Isaya 9:5), vinasitishwa. Hakuna sasa kinachosikika zaidi ya sauti ya maombi na sauti ya kilio na maombolezo. Kilio kinalipuka kutoka katika midomo ambayo muda mfupi uliopita ilikuwa ikidhihaki: “Siku kuu ya hasira Yake imekuja; ni nani awezaye kusimama?” Waovu wanaomba wafunikwe chini ya miamba na milima kuliko kukutana na uso wa Yeye ambaye wamekuwa wakimdhihaki na kumkataa.PKSw 489.3

  Sauti ile ipenyayo sikio la wafu, wanaijua. Mara ngapi sauti inayosihi, ya upole imekuwa ikiwaita watubu. Mara ngapi sauti hiyo imesikika katika miito inayogusa ya rafiki, kaka, na Mkombozi. Kwa wanaokataa neema Yake hakuna sauti nyingine ambayo ilikabiliwa na lawama, kulemewa na shutuma sana, kama sauti ile ambayo kwa muda mrefu ilitoa wito: “Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa?” (Ezekieli 33:11). O, laiti ingekuwa sauti ya mgeni kwao! Yesu anasema: “Nimeita, nanyi mkakataa; Nimeunyosha mkono wangu, asiangalie mtu; Bali mmebatilisha shauri langu, Wala hamkutaka maonyo yangu” (Mithali 1:24, 25). Sauti inaamsha kumbukumbu ambazo walitamani zingekuwa zimefutwa— maonyo yaliyodhihakiwa, miito iliyokataliwa, fursa zilizopuuzwa.PKSw 489.4

  Wapo wale waliomdhihaki Kristo wakati wa kudhalilishwa Kwake. Kwa nguvu na msisimko mkubwa wanayakumbuka maneno ya Yesu, alipoagizwa kwa kiapo na kuhani mkuu, alisema kwa mkazo: “Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni” (Mathayo 26:64). Sasa wanautazama utukufu Wake, na bado hawajamwona akiwa ameketi mkono wa kuume wa nguvu.PKSw 489.5

  Waliodharau dai Lake la kuwa Mwana wa Mungu hawana cha kusema sasa. Yupo Herode mwenye kiburi aliyekejeli cheo Chake cha kifalme na kuwaagiza askari wenye dhihaka kumvika taji kama Mfalme. Kuna watu ambao kwa mikono yao najisi waliweka juu ya mwili Wake joho la zambarau, juu ya paji la uso Wake mtakatifu taji ya miiba, na katika mkono Wake usiokuwa na ubishi fimbo ya kifalme ya kuigiza, na kuinama mbele Yake kwa dhihaka yenye kufuru. Watu waliompiga na kumtemea mate Mfalme wa uzima sasa wanageuka pembeni wasiyatazame macho Yake na kutafuta kukimbia waende mbali na utukufu wa uwepo Wake. Waliopigilia misumari katika mikono Yake na nyayo Zake, askari aliyechoma mkuki ubavuni Mwake, wanaziona alama hizi kwa aibu.PKSw 490.1

  Kwa uwazi wa kutisha makuhani na wandishi wanayakumbuka matukio ya Kalwari. Kwa hofu kubwa wanakumbuka sasa jinsi, wakitikisa vichwa vyao kwa furaha ya kishetani, walivyodai:“Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu” (Mathayo 27:42, 43).PKSw 490.2

  Wanakumbuka wazi wazi mfano wa Mwokozi wa mpanzi aliyekataa kumpa bwana wao matunda ya shamba la mizabibu, aliyewadhihaki watumwa wake na kumwua mwanae. Wanakumbuka, pia, sentensi ambayo wao wenyewe waliitamka: Bwana wa shamba la mizabibu “atawaua wale watu waovu.” Katika dhambi na adhabu ya wale wasiokuwa waaminifu makuhani na wazee wanaona njia yao na hatima yao. Na sasa kinainuka kilio cha uchungu wa kufa. Kikiwa cha sauti ya juu zaidi kuliko kelele za “Msulubishe, Msulubishe” zilizosikika katika mitaa yote ya Yerusalemu, kinageuka kuwa maombolezo ya kutisha, na kukata tamaa, “Ni Mwana wa Mungu! Ni Masihi wa kweli!” Wanatafuta kukimbia na kuondoka katika uwepo wa Mfalme wa wafalme. Katika mashimo yenye kina kirefu ardhini, yaliyochimbwa na migongano ya vitu vya asili, wanajaribu kujificha bila mafanikio.PKSw 490.3

  Katika maisha ya wote wanaoukataa ukweli kuna nyakati ambapo dhamiri inaamshwa, wakati kumbukumbu zinapoleta mambo ya zamani yanayotesa ya maisha ya unafiki na roho inaumia na kuwa na masikitiko yasiyosaidia cho chote. Lakini masikitiko haya ni nini ukilinganisha na huzuni ya siku ile wakati “hofu ... ifikapo kama tufani,” wakati “msiba ... ufikapo kama kisulisuli”! (Mithali 1:27). Wale ambao walimwua Kristo na watu Wake waaminifu sasa wanashuhudia utukufu ukiwa juu yao. Katikati ya hofu yao wanasikia sauti za watakatifu wakiimba nyimbo za furaha wakishangilia: “Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie” (Isaya 25:9).PKSw 490.4

  Katikati ya kuwayawaya kwa dunia, mwangaza wa radi, na ngurumo za radi, sauti ya Mwana wa Mungu inawaita watakatifu waliolala usingizi wa mauti. Anayatazama makaburi ya wenye haki, ndipo, akiinua mikono yake juu mbinguni, anapiga kelele: “Amkeni, amkeni, amkeni, ninyi mnaolala katika mavumbi, na msimame!” Katika marefu na mapana ya dunia yote waliokufa wataisikia sauti ile, na watakaoisikia wataishi. Na dunia nzima itarindima kwa vishindo vya jeshi kubwa sana la watu wa kila taifa, jamaa, lugha, na kabila. Kutoka katika gereza la makaburi wanatoka, wakiwa wamevikwa utukufu usiokufa, wakisema: “Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?” (1 Wakorintho 15:55). Na wenye haki walio hai na watakatifu waliofufuliwa wanaunganisha sauti zao pamoja katika kelele za furaha na ushindi kwa muda mrefu.PKSw 491.1

  Wote wanatoka katika makaburi yao wakiwa na kimo kilekile walichoingia nacho kaburini. Adamu, ambaye anasimama miongoni mwa watu waliofufuliwa, ana kimo kikubwa na umbo adhimu. Anaonekana kuwa na tofauti kubwa sana na watu wa vizazi vya baadaye; katika kipengere hiki kimoja kunaonekana poromoko katika ubora wa maisha ya mwanadamu. Lakini wote wanaamka wakiwa na upya na uhai wa ujana wa milele. Hapo mwanzo, mtu aliumbwa katika mfano wa Mungu, siyo tu katika tabia, bali pia katika umbo na mwonekano. Dhambi iliharibu na kufuta karibu kila mfano wa Kimungu; lakini Kristo alikuja kurudisha kile kilichopotea. Atabadilisha miili yetu michafu na kuiumba upya ifanane na mwili Wake wa utukufu. Mwili unaokufa, ulioharibika, usiokuwa na uzuri, uliochafuliwa na dhambi, unakuwa kamili, mzuri, na usiokufa. Kasoro zote na ulemavu wa aina yo yote vinaachwa kaburini. Wakiwa wamerudishwa mahali palipo na mti wa uzima katika Edeni iliyopotea kwa miaka mingi, waliokombolewa “watakua” (Malaki 4:2) hadi wafikie kimo cha kizazi cha mwanadamu katika utukufu wake wa awali. Viashiria vya mwisho-mwisho vya laana ya dhambi vitaondolewa, na watu waaminifu wa Kristo watatokea katika “uzuri wa Bwana Mungu wetu,” katika akili na roho na mwili, wakiakisi sura takatifu ya Bwana wao. Ndiyo, ukombozi wa ajabu! Ulioongelewa kwa muda mrefu, uliotumainiwa kwa muda mrefu, uliofikiriwa kwa matarajio na shauku kubwa, lakini bila kueleweka kikamilifu.PKSw 491.2

  Wenye haki walio hai wanabadilishwa “dakika moja, kufumba na kufumbua” Kwa sauti ya Mungu walitukuzwa; sasa wanafanywa kuwa wasiokufa na watakatifu waliofufuliwa wanachukuliwa kumlaki Bwana wao hewani. Malaika “wanawakusanya pamoja wateule Wake kutoka pepo nne, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.” Watoto wadogo wanabebwa na malaika watakatifu na kuwapeleka kwa mama zao na kuwakabidhi katika mikono yao. Marafiki waliotenganishwa kwa kifo wanaunganishwa, wasitenganishwe tena, na wakiimba nyimbo za furaha wanapaa kwenda pamoja kuelekea katika mji wa Mungu.PKSw 491.3

  Kila upande wa gari la wingu kuna mabawa, na chini yake kuna magurudumu hai; na magari yanapopaa kwenda juu, magurudumu yanapiga kelele, “Mtakatifu,” na mabawa, yanaporuka, yanapiga kelele, “Mtakatifu,” na msafara wa malaika wanapiga kelele, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mwenyezi.” Na waliokombolewa wanapiga kelele, “Haleluya!” wakati gari linapoondoka kuelekea Yerusalemu.PKSw 492.1

  Kabla ya kuingia Mji wa Mungu, Mwokozi anawapa wafuasi Wake nishani za ushindi na anawavalisha tepe za hadhi zao za kifalme. Waliokombolewa wakiwa wanang'aa wanapangwa katika umbo la mraba wenye nafasi katikati kumzunguka Mfalme wao, ambaye umbo Lake limepanda juu ya kila malaika na kila mtakatifu, ambaye uso Wake unaonekana kujaa upendo na wema. Kutoka kwa jeshi la watu wasiokuwa na idadi kila jicho limekazwa Kwake, kila jicho linauona utukufu Wake Yeye ambaye “Uso Wake uliharibiwa zaidi kuliko mtu mwingine ye yote, na umbo Lake liliharibiwa zaidi kuliko wanadamu wengine wote.” Juu ya vichwa vya washindi, Yesu kwa mkono Wake wa kulia anaweka taji ya utukufu. Kwa kila mmoja kuna taji, iliyoandikwa “jina jipya” lake mwenyewe (Ufunuo 2:17), na maandishi, “Utakatifu kwa Bwana.” Katika kila mkono kunawekwa tawi la mtende la ushindi na kinubi kinachong'aa. Ndipo, wakati malaika waongozaji wanapopiga noti, kila mkono unafagia nyuzi za kinubi kwa mguso wenye stadi, ukiamsha muziki mtamu wenye sauti zenye melodi nzuri. Furaha isiyoelezeka inachemka ndani ya kila moyo, na kila sauti inainuliwa katika sifa na shukurani: “Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele” (Ufunuo 1:5, 6).PKSw 492.2

  Mbele ya mkutano wa watu waliokombolewa kuna Mji Mtakatifu. Yesu anafungua malango ya lulu, na mataifa walioutunza ukweli wanaingia ndani. Pale wanaiona Paradiso ya Mungu, nyumba ya Adamu katika utakatifu wake. Ndipo sauti, iliyo nzuri kuliko muziki wo wote uliowahi kuingia sikio la mtu anayekufa, inasikika ikisema: “Pambano lenu limekwisha.” “Njooni, nyinyi mliobarikiwa na Baba Yangu, urithini ufalme mlioandaliwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.”PKSw 492.3

  Sasa ombi la Mwokozi kwa wanafunzi Wake: “Hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo.” “Mbele ya utukufu Wake bila mawaa katika furaha kuu” (Yuda 24), Kristo anawasilisha kwa Baba watu walionuliliwa kwa damu Yake, akitangaza:“Nipo hapa, na watoto ulionipa.” “Wote ulionipa nimewatunza.” Ndiyo, maajabu ya upendo unaokomboa! Furaha ya saa ile wakati Baba wa milele, akiwaangalia waliokombolewa, ataiona sura Yake, misuguano ya dhambi ikiwa imeondolewa, uozo wake ukiwa umefutiliwa mbali, na wanadamu wakiwa wamerudishwa tena katika mwafaka na Mungu!PKSw 492.4

  Kwa upendo usioelezeka, Yesu anawakaribisha watu Wake waaminifu katika furaha ya Bwana wao. Furaha ya Mwokozi ni katika kuona, katika ufalme wa utukufu, roho zilizookolewa kwa mateso Yake na kudharauliwa Kwake. Na waliokombolewa watakuwa washiriki katika furaha Yake, wanapowaona, miongoni mwa waliokombolewa, wale waliowaleta kwa Kristo kupitia maombi yao, kazi zao, na upendo wao wa kujitoa kafara. Wanapokusanyika kando kando ya kiti cha enzi cheupe, furaha isiyoelezeka inajaza mioyo yao, wanapoona wale waliowaleta kwa Kristo, na kugundua kuwa mmoja aliwapata wengine, na bado hawa waliwapata wengine, wote wakiwa wameletwa katika bandari ya pumziko, pale kuweka taji zao kwenye miguu ya Yesu na kumsifu Yeye katika mizunguko isiyokoma ya umilele.PKSw 493.1

  Wakati waliokombolewa walipokaribishwa katika Mji wa Mungu, kunatokea mlipuko wa furaha hewani kelele za furaha. Akina Adamu wawili wanakaribia kukutana. Mwana wa Mungu anasimama mikono Yake ikiwa imenyooshwa kumpokea baba wa kizazi chetu—mwenye uhai aliyemuumba Mwenyewe, aliyetenda dhambi dhidi ya Muumbaji wake, na ambaye kwa ajili ya dhambi yake alama za kuslubishwa zinaonekana katika mwili wa Mwokozi. Wakati Adamu anapotambua alama za misumari ya kikatili, haanguki katika kifua cha Bwana wake, lakini kwa unyenyekevu anajitupa chini kwenye nyayo Zake na kupiga kelele: “Anastahili, anastahili Mwanakondoo aliyechinjwa!” Kwa huruma Mwokozi anamwinua na kumwambia aitazame tena nyumba ya Edeni ambayo aliondolewa muda mrefu uliopita.PKSw 493.2

  Baada ya kufukuzwa Edeni, maisha ya Adamu duniani yalijaa huzuni. Kila jani lililokauka, kila mnyama wa kafara, kila dosari katika uso mzuri wa uumbaji wa asili, kila doa katika usafi wa mwanadamu, ilikuwa ukumbusho wa dhambi yake. Ulikuwa wa kutisha uchungu wake alipoona ongezeko la uovu kila mahali, na, kama jibu kwa maonyo yake, alikutana na aibu iliyorushwa kwake kama msababishaji wa dhambi. Kwa uvumilivu na unyenyekevu alibeba, kwa takribani miaka elfu moja, adhabu ya makosa yake. Kwa uaminifu alitubu dhambi yake na kutumainia huruma za Mwokozi aliyeahidiwa, na alikufa katika tumaini la ufufuo. Mwana wa Mungu alikomboa kushindwa na kuanguka kwa mwanadamu; na sasa, kwa njia ya kazi ya upatanisho, Adamu anarudishwa katika utawala wake wa kwanza.PKSw 493.3

  Akiwa amebebwa na furaha, anatazama miti ambayo ilikuwa furaha yake kuiona mwanzoni—miti ile ile ambayo yeye mwenyewe alikuwa akikusanya matunda yake siku za maisha yake yasiyokuwa na hatia na nyakati ambazo alikuwa na furaha daima. Anaiona mizabibu ambayo mikono yake mwenyewe iliifundisha, na miti ile ile ya maua aliyofurahia kuitunza. Akili yake inaelewa uhalisia wa mandhari; anaelewa kuwa Edeni hii iliyorejeshwa upya, ni nzuri zaidi sasa kuliko ilivyokuwa wakati alipofukuzwa kutoka ndani yake. Mwokozi anamwongoza kwenda mahali ulipo mti wa uzima na anachuma tunda lenye utukufu na anamwagiza alile. Anawatazama waliomzunguka na anaona umati wa familia yake waliokombolewa, wakisimama katika Paradiso ya Mungu. Ndipo anatupa taji yake inayong'aa kwenye nyayo za Yesu na, akiangukia katika kifua cha Yesu, anamkumbatia Mwokozi. Anagusa kinubi cha dhahabu, na makuba ya mbinguni yanarudisha mwangwi wa wimbo wa ushindi: “Astahiliye, astahiliye, astahiliye ni Mwakondoo aliyechinjwa, na yuko hai tena!” Familia ya Adamu wanadaka wimbo na kutupa taji zao kwenye nyayo za Mwokozi na wanainama mbele yake kwa heshima na kicho.PKSw 493.4

  Muungano huu wa watu waliokuwa pamoja wakati fulani unashuhudiwa na malaika waliolia machozi wakati wa anguko la Adamu na kufurahia wakati Yesu, baada ya ufufuko, alipopaa mbinguni, baada ya kufungua kaburi kwa ajili ya wote ambao wangeliliamini jina Lake. Sasa wanatazama kazi ya ukombozi ikiwa imekamilika, na wanaunganisha sauti zao kuimba wimbo wa sifa.PKSw 494.1

  Panapo bahari ya fuwele mbele ya kiti cha enzi, bahari ile ya kioo iliyonekana kana kwamba ilikuwa imechanganywa na moto,—kwa kung'arishwa na utukufu wa Mungu,—umesimama mkutano wa wale walioshinda “watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake.” Pamoja na Mwanakondoo juu ya Mlima Sayuni, “wenye vinubi vya Mungu,” wanasimama, watu mia moja arobaini na nne elfu waliokombolewa kutoka miongoni mwa watu; na inasikika sauti kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu, “sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao.” Na wanaimba “wimbo mpya” mbele ya kiti cha enzi, wimbo ambao hakuna anayeweza kuujifunza isipokuwa wale mia arobaini na nne elfu. Ni wimbo wa Musa na Mwanakondoo—wimbo wa ukombozi. Hakuna mtu hata mmoja anayeweza kujifunza wimbo ule isipokuwa wale mia arobaini na nne peke yao; kwa kuwa ni wimbo wa uzoefu wao— uzoefu ambao hakuna kundi jingine lolote liliwahi kuwa nao. “Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako.” Hawa, wakiwa wamehamishwa kutoka duniani, kutoka miongoni mwa walio hai, wanachukuliwa kuwa “malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo” (Ufunuo 15:2, 3; 14:1 5) . “Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu;” wamepita katika wakati wa taabu ambayo haijawahi kuwepo tangu kuwepo kwa taifa lo lote; wamevumilia maumivu ya wakati wa taabu ya Yakobo; wamesimama bila mwombezi wakati wote mpaka umwagaji wa mwisho wa hukumu za Mungu. Lakini wamekombolewa, kwa kuwa “wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.” “Katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa” mbele za Mungu. “Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao.” Wameiona dunia ikiharibiwa kwa njaa na magonjwa, jua likipewa nguvu ya kuwaunguza watu kwa joto kubwa, na wao wenyewe wamekabiliana na mateso, njaa, na kiu. Lakini “hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote. Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao” (Ufunuo 7:14-17).PKSw 494.2

  Katika zama zote wateule wa Mwokozi wamelelewa katika shule ya majaribu. Wametembea katika njia nyembamba duniani; wamesafishwa katika tanuru la mateso. Kwa ajili ya Kristo wamevumilia upinzani, chuki, na kusingiziwa. Walimfuata katikati ya mapambano makali; walivumilia kujikana nafsi na walipata uchungu wa kukatishwa tamaa. Kwa njia ya uzoefu wa maumivu waligundua ubaya wa dhambi, nguvu yake, na madhara yake; na wanaichukia. Utambuzi wa kafara kubwa iliyotolewa ili kuitibu unawanyenyekesha machoni pao wao wenyewe na unajaza mioyo yao kwa shukrani na sifa ambazo wale ambao hawakuanguka hawawezi kuelewa. Wanapenda zaidi kwa kuwa wamesamehewa mno. Wakiwa washiriki wa mateso ya Kristo, wanafaa kuwa washirika wa utukufu Wake.PKSw 495.1

  Warithi wa Mungu wametoka katika upenu, kutoka katika vibanda vibovu, kutoka katika magereza ya chini ya ardhi, kutoka katika majukwaa ya kunyongea watu, kutoka milimani, kutoka majangwani, kutoka katika mapango ya ardhini, kutoka katika mapango ya baharini. Duniani walikuwa “maskini, watu wa kuteseka, watu wa kuudhiwa.” Mamilioni walikwenda makaburini wakiwa hawana sifa njema kwa sababu walikataa daima kukubali madai ya uongo ya Shetani. Kwa njia ya mahakama za kibinadamu walihukumiwa kama wahalifu wakubwa zaidi kuliko wahalifu wengine wote. Lakini sasa “Mungu ndiye aliye hakimu” (Zaburi 50:6). Sasa maamuzi ya dunia yanageuzwa. “Aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote” (Isaya 25:8). “Nao watawaita, Watu watakatifu, Waliokombolewa na Bwana.” Mungu amepanga “wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito” (Isaya 62:12; 61:3). Wao sio watu dhaifu tena, wanaoteswa, waliosambaa, na wanaoudhiwa. Tangu hapo wanakuwa na Bwana milele zote. Wanasimama mbele ya kiti cha enzi wakiwa katika majoho mazuri zaidi kuliko majoho yote yaliyowahi kuvaliwa na waheshimiwa na wakuu wa duniani.PKSw 495.2

  Wamevalishwa vilemba vyenye utukufu mwingi zaidi kuliko vilemba vyote vilivyowahi kuvaliwa na wafalme wa kidunia. Siku za maumivu na kutoa machozi zimekoma milele. Mfalme wa utukufu amefuta kutoka katika nyuso zao kila kitu kinacholeta huzuni. Katikati ya matawi ya mitende inayopepea wanaimba wimbo wa sifa, unaosikika vizuri, mtamu, na wenye upatanifu; kila sauti inajiunga katika uimbaji mpaka wimbo unapanda na kujaa katika makuba ya mbinguni: “Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo.” Na wakazi wote wa mbinguni wanaitikia kwa kuimba kibwagizo cha kukiri: “Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele” (Ufunuo 7:10, 12).PKSw 496.1

  Katika maisha haya tunaweza tu kuanza kuelewa mada ya ajabu ya ukombozi. Kwa uelewe wetu wenye kikomo tunaweza kufikiria kwa bidii sana juu ya aibu na utukufu, uzima na mauti, haki na rehema, ambavyo hukutana msalabani; pamoja na hayo, hata kwa kupanua sana uwezo wetu wa kiakili bado tunashindwa kuelewa uzito wake kikamilifu. Urefu na mapana, kina na kimo, cha upendo unakomboa vinaeleweka kidogo sana. Mpango wa ukombozi hautaeleweka kikamilifu, hata wakati waliokombolewa watakapoona kama wanavyoonwa na kujua kama wanavyojulikana; bali katika zama zote ukweli mpya utafunuliwa daima kwa akili zinazoshangaa na kufurahia. Ingawa huzuni na maumivu na majaribu ya duniani yamekoma na chimbuko lake kuondolewa, watu wa Mungu watadumu kuwa na uelewa wa wazi, akilini mwao wa gharama ya wokovu wao.PKSw 496.2

  Msalaba wa Kristo utakuwa sayansi na wimbo wa waliokombolewa milele zote. Ndani ya Kristo aliyetukuzwa watamwona Kristo aliyesulibiwa. Kamwe haitasahaulika kuwa Yeye ambaye uwezo Wake uliumba na kushikilia sayari zisizo na idadi katika anga lisilokuwa na kikomo, Mpendwa wa Mungu, Mfalme wa mbinguni, Yeye ambaye makerubi na maserafi wanaong'aa wanafurahia kumwabudu—alijinyenyekesha Mwenyewe ili amwinue mwanadamu aliyeanguka; kuwa alibeba hatia na aibu ya dhamgi, na akificha uso wa Baba Yake, mpaka misiba ya ulimwengu uliopotea ilipopasua moyo Wake na kuondoa uhai Wake juu ya msalaba wa Kalwari. Kwamba Mwumbaji wa sayari zote, Mwamuzi wa miisho ya watu wote, aliweka kando utukufu Wake na kujinyenyekesha kwa sababu ya upendo Wake kwa mwanadamu— daima yote haya yataamsha mshangao na kuhamasisha ibada katika sayari zote. Wakati mataifa ya waliookolewa yatakapomtazama Mkombozi wao na kuona utukufu wa milele wa Baba uking'aa katika uso Wake; wanapoangalia kiti Chake cha enzi, ambacho ni cha milele na milele, na kujua kuwa ufalme Wake hautakuwa na mwisho, wanaimba wimbo wa furaha: “Anastahili, anastahili Mwanakondoo aliyechinjwa, na ametukomboa na kutuleta kwa Mungu kwa njia ya damu Yake Mwenyewe yenye thamani kubwa!”PKSw 496.3

  Siri ya msalaba inaeleza mambo mengine yote yasiyoeleweka. Katika nuru inayotiririka kutoka Kalwari sifa za Mungu ambazo zilitujaza hofu na kicho zinaonekana kuvutia na kuwa nzuri. Rehema, upole, na upendo wa mzazi vinaonekana kuungana na utakatifu, haki na nguvu. Wakati tunaona utukufu wa kiti Chake cha enzi, kilichoinuliwa juu, tunaona tabia Yake katika udhihirisho wa neema, na kuelewa, kuliko kabla ya hapo, umuhimu wa cheo kile kinachoashiria upendo, “Baba yetu.”PKSw 497.1

  Itakuja kuonekana kuwa Yeye aliye na hekima isiyokuwa na kikomo hakuweza kubuni mpango mwingine kwa ajili ya wokovu wetu isipokuwa kwa njia ya kafara ya Mwana Wake. Malipo kwa ajili ya kafara hii ni furaha ya kuijaza dunia kwa watu waliokombolewa, watakatifu, wenye furaha, na wasiokufa. Matokeo ya pambano kati ya Mwokozi na nguvu za giza na furaha ya waliokombolewa, vitamletea Mungu utukufu milele zote. Na hii ndiyo thamani ya roho kwamba Baba anaridhishwa na gharama iliyolipwa; na Kristo Mwenyewe, akitazama matunda ya kafara Yake kubwa, anaridhika. PKSw 497.2

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents