Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 31—Wakala wa Pepo

  Mshikamano wa ulimwengu unaoonekana na usioonekana, huduma za malaika wa Mungu, na ya wakala wa pepo, umefunuliwa katika Maandiko, na umeshikamana na historia ya mwanadamu. Kuna mwelekeo unaokua wa kutokuamini katika uwepo wa pepo wachafu, wakati malaika watakatifu “watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu” (Waebrania 1:14) wanachukuliwa kama roho za watu waliokufa. Lakini Maandiko yanafundisha siyo tu juu ya uwepo wa malaika, wema na wabaya, bali pia huwasilisha uthibitisho usio na mashaka kuwa malaika hawa sio roho za watu waliokufa.PKSw 391.1

  Kabla ya uumbaji wa mwanadamu, malaika walikuwepo; kwa kuwa wakati misingi ya dunia ilipowekwa, “nyota za asubuhi ziliimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipiga kelele kwa furaha” (Ayubu 38:7). Baada ya anguko la mwanadamu, malaika walitumwa kuulinda mti wa uzima, na hili lilitokea kabla mwanadamu hajafa. Malaika katika asili yao wako juu zaidi kuliko wanadamu, kwani mtunga zaburi anasema mwanadamu aliumbwa “akiwa mdogo punde kuliko malaika” (Zaburi 8:5).PKSw 391.2

  Tumefahamishwa katika Maandiko kuhusu idadi, na nguvu, na utukufu, wa malaika, na mshikamano wao na serikali ya Mungu, na pia kuhusu uhusiano wao na kazi ya ukombozi. “Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.” Na nabii anasema, “Nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi.” Mbele ya uwepo wa Mfalme wa wafalme wanahudumu—“malaika zake ... hodari,” “watumishi wake wafanyao mapenzi yake,” “Wakiisikiliza sauti ya neno lake” (Zaburi 103:19-21; Ufunuo 5:11). Kumi elfu mara kumi elfu na maelfu kwa maelfu, walikuwa wajumbe walioonwa na nabii Danieli. Mtume Paulo alitangaza kuwa wao ni “majeshi ya malaika elfu nyingi” (Danieli 7:10; Waebrania 12:22). Kama wajumbe wa Mungu wanasafiri kama “kuonekana kwa kumulika kwa umeme,” (Ezekieli 1:14), ndivyo ulivyo mng'ao wa utukufu wao, na ndivyo ilivyo kasi ya urukaji wao. Malaika aliyetokea kwenye kaburi la Mwokozi, sura yake iliyokuwa “kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji,” iliwafanya walinzi kutetemeka kwa hofu, na “wakawa kama wafu” (Mathayo 28:3, 4). Senakeribu, Mwashuri mwenye kiburi, alipomtukana na kumkufuru Mungu, na kutishia kuwaangamiza Israeli, “Ikawa usiku uo huo malaika wa Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini na tano elfu.” “Naye Bwana akatuma malaika aliyewakatilia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida,” wa jeshi la Senakeribu. “Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso” (2 Wafalme 19:35; 2 Nyakati 32:21).PKSw 391.3

  Malaika wanatumwa kwa ajili ya utume wa rehema kwa watoto wa Mungu. Kwa Ibrahimu, walikwenda wakiwa na ahadi ya baraka; kwenye malango ya Sodoma, walikwenda kumwokoa Lutu mwenye haki kutoka katika maangamizi ya moto; kwa Eliya, alipokuwa karibu kufa kwa sababu ya uchovu na njaa katika jangwa, alimpelekea chakula; kwa Elisha, walikwenda wakiwa na magari na farasi wa moto wakauzunguka mji mdogo uliokuwa umezingirwa na adui zake; kwa Danieli, wakati akitafuta hekima ya Kimungu katika ikulu ya mfalme mpagani, au akiwa ameachwa aliwe na simba walikwenda kumwokoa; alikwenda kwa Petro, akikabiliwa na kifo katika gereza la Herode, na kumtoa gerezani; alikwenda kwa wafungwa pale Filipi; alikwenda kwa Paulo na wenzake katikati ya usiku wa dhoruba baharini; alitumwa kufungua akili ya Kornelio ili apokee injili; alimtuma Petro na ujumbe wa wokovu kwa mgeni Mmataifa—hivyo malaika watakatifu, katika zama zote, wamewahudumia watu wa Mungu.PKSw 392.1

  Malaika mlinzi amepangwa kwa ajili ya kila mfuasi wa Kristo. Walinzi hawa wa mbinguni wanakinga wenye haki dhidi ya nguvu za yule mwovu. Shetani alilitambua hili aliposema: “Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukingo pande zote?” (Ayubu 1:9, 10). Wakala anayetumiwa na Mungu kuwalinda watu Wake ameelezwa katika maneno ya mtunga zaburi: “Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa” (Zaburi 34:7). Mwokozi alisema, akiongea juu ya wale wanaomwamini: “Angalieni msidharau mmojawapo wa wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu” (Mathayo 18:10). Malaika waliopangwa kuwahudumia watoto wa Mungu wakati wote wanakwenda mbele za Mungu.PKSw 392.2

  Hivyo watu wa Mungu, kwa sababu ya kukabiliwa na nguvu ya udanganyifu na uovu usiokoma wa mfalme wa giza, na kwa sababu ya kukabiliwa na mapambano dhidi ya nguvu za uovu wakati wote, wamehakikishiwa ulinzi usiokoma wa malaika wa mbinguni. Wala uhakika hautolewi bila hitaji. Mungu amewapa watoto Wake ahadi ya neema na ulinzi, kwa sababu kuna mawakala wenye nguvu wa uovu wa kukabiliana nao—mawakala wengi, waliodhamiria, na wasiochoka, ambao ubaya na nguvu yake hakuna hata mtu mmoja anaweza kuwa salama kutokujua na kutokujali.PKSw 392.3

  Pepo wabaya, mwanzoni waliumbwa wakiwa hawana na dhambi, wakiwa sawa na malaika watakatifu, ambao kwa sasa ni wajumbe wa Mungu, katika asili, nguvu, na utukufu. Lakini wakiwa wameanguka dhambini, wameungana pamoja ili kumvunjia heshima Mungu na kuwaangamiza wanadamu. Wakiwa wameungana na Shetani katika uasi wake, wakifukuzwa mbinguni pamoja naye, katika zama zote mfululizo, wameshirikiana naye katika vita yake dhidi ya mamlaka ya Mungu. Tumeambiwa katika Maandiko kuhusu shirikisho lao na serikali yao, kuhusu makundi yao mbalimbali, kuhusu akili na hila zao, na kuhusu mipango yao mibaya dhidi ya amani na furaha ya wanadamu.PKSw 392.4

  Historia ya Agano la Kale hutaja mara chache uwepo wao na mawakala wao; lakini wakati Kristo alipokuwa duniani pepo wabaya walidhihirisha nguvu zao kwa namna iliyokuwa wazi zaidi. Kristo alikuwa ameingia katika mpango uliobuniwa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, na Shetani alidhamiria kuonesha haki yake ya kuutawala ulimwengu. Alikuwa amefanikiwa kuanzisha ibada ya sanamu kila sehemu ya dunia isipokuwa katika nchi ya Palestina. Katika nchi pekee ambayo ilikuwa haijajisalimisha kikamilifu chini ya himaya ya mjaribu, Kristo alikuja kuwaangazia watu nuru ya mbinguni. Hapa, nguvu mbili hasimu zilidai ukuu. Yesu alikuwa akinyosha mikono Yake ya upendo, akiwaalika wote wanaotafuta msamaha na amani ndani Yake. Majeshi ya giza yaliona kuwa hayakuwa na utawala usio na ukomo, na yalielewa kuwa ikiwa utume wa Kristo ungefaulu, utawala wao ungekoma ndani ya muda mfupi. Shetani alikasirika kama simba aliyefungwa mnyororo na alionesha nguvu zake kwa ukali katika miili na roho za watu.PKSw 393.1

  Ukweli kuwa watu walipagawa na pepo wachafu, umeelezwa wazi wazi katika Agano Jipya. Watu walioteswa hivyo hawakuwa wanaumwa ugonjwa uliotokana na sababu za kawaida. Kristo alikuwa na uelewa kamili wa kile alichokuwa akishughulika nacho, na alitambua uwepo wa moja kwa moja na wakala wa pepo.PKSw 393.2

  Mfano wa wazi wa idadi, nguvu, na ubaya wao, na pia nguvu na rehema ya Kristo, umetolewa katika maelezo ya Maandiko juu ya watu waliopagawa na pepo katika nchi ya Wagerasi. Wale wendawazimu maskini, wakivunja kila kizuizi, wakigaragara na kujitupa huku na huku, wakitokwa povu mdomoni, wakionesha hasira, waliijaza hewa kwa kelele zao, wakiifanyia ukatili miili yao, na kuhatarisha wote waliowakaribia. Miili yao iliyokuwa ikivuja damu na iliyokuwa imeharibika; na akili zao zilizopotezwa mwelekeo, viliwasilisha kituko ambacho kilimfurahisha sana mfalme wa giza. Mmoja wa pepo waliopagaa wagonjwa wale alisema: “Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi” (Marko 5:9). Katika jeshi la Kirumi, legioni inaundwa na watu kuanzia elfu tatu hadi elfu tano. Majeshi ya Shetani nayo pia yamepangwa katika makundi, na kundi moja ambalo hawa pepo walikuwa sehemu yake walikuwa siyo chini ya legioni moja.PKSw 393.3

  Kwa amri yaYesu pepo waliwaacha wahanga wao, wakiwaacha wamekaa kwa utulivu karibu na miguu ya Mwokozi, wakiwa katika hali ya kujitawala, wakiwa na akili timamu, na wapole. Lakini pepo waliruhusiwa kufagia kundi la nguruwe na kuwatosa baharini; na kwa wakazi wa Wagerasi hasara ya hawa nguruwe ilikuwa kubwa zaidi kuliko mibaraka ambayo Kristo alikuwa ameileta, na Mponyaji wa Kiungu alisihiwa aondoke. Hili lilikuwa matokeo ya mipango ya Shetani. Kwa kurushia lawama ya hasara yao kwa Yesu, alichochea hofu za kibinafsi za watu na aliwazuia wasisikilize maneno Yake. Daima Shetani huwashitaki Wakristo kama chimbuko la hasara, balaa, na mateso, badala ya kuruhusu shutuma ziende mahali pake—juu yake mwenyewe na mawakala wake.PKSw 394.1

  Lakini makusudi ya Yesu hayakukwamishwa. Aliruhusu pepo waangamize nguruwe kama kemeo kwa wale Wayahudi waliofuga wanyama hawa najisi kwa ajili ya mapato. Ikiwa Kristo asingewazuia hawa pepo, wangewatosa baharini, siyo tu nguruwe, bali pia wafugaji na wamiliki wa nguruwe. Utunzaji wa wafugaji na wa wamiliki wa nguruwe ulitokana na mamlaka Yake, ambayo ilitumiwa kwa ajili ya wokovu wao. Zaidi ya hapo, tukio hili liliruhusiwa ili wanafunzi washuhudie nguvu ya kikatili ya Shetani kwa wanadamu na wanyama. Mwokozi alitamani wafuasi Wake wamwelewe adui ambaye wangekabiliana naye, ili wasidanganywe na kushindwa na hila zake. Ilikuwa pia mapenzi Yake pia kuwa watu wa eneo lile wauone uwezo Wake wa kuvunja utumwa wa Shetani na kuwaachilia mateka wake. Na ingawa Yesu Mwenyewe aliondoka, watu ambao kwa njia ya miujiza walikuwa wameachiliwa, walibaki kutangaza rehema ya Mfadhili wao.PKSw 394.2

  Matukio mengine yenye sura hiyo yamerekodiwa katika Maandiko. Binti wa mwanamke Myunani, Msirofoenike aliteswa sana na pepo, ambaye Yesu alimtoa kwa neno Lake (Marko 7:26-30). “Mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu” (Mathayo 12:22); kijana aliyekuwa na pepo bubu, ambaye mara nyingi “amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize” (Marko 9:1727); mtu ambaye, kwa kuteswa na “roho wa pepo mchafu” (Luka 4:33-36), alivuruga utulivu wa Sabato wa sinagogi Kapernaumu—wote waliponywa na Mwokozi mwenye huruma. Katika kila tukio, Kristo alizungumza na pepo kama nafsi yenye akili, akimwamru amtoke mhanga wake na asimtese tena. Waabudu wa Kapernaumu, baada ya kuona uwezo Wake mkuu, “Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, Ni neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka” (Luka 4:36).PKSw 394.3

  Waliopagawa na pepo wanaoneshwa kuwa katika hali ya mateso makubwa; lakini kulikuwepo na tofauti katika matukio mengine ya kupagawa. Kwa ajili ya kupata nguvu zisizokuwa za kawaida baadhi ya watu walikaribisha nguvu ya pepo. Lakini hawa hawakuwa na mgogoro na pepo. Katika kundi hili walikuwemo wale waliokuwa na pepo la uaguzi,—Simoni Magus, Elima mchawi, na binti aliyemfuata Paulo na Sila kule Filipi.PKSw 394.4

  Hakuna mtu aliye katika hatari zaidi ya mvuto wa pepo kuliko wale ambao, licha ya ushahidi maridhawa wa Maandiko, wanakana uwepo na wakala wa Shetani na malaika zake. Kwa kadiri tunavyokosa ufahamu wa hila zao, ndivyo wanavyopata faida kubwa ajabu; wengi wanafuata mapendekezo yao wakidhani kuwa wanafuata maagizo ya hekima zao. Hii ndiyo sababu, kwa kadiri tunavyokaribia mwisho wa wakati, wakati Shetani anapofanya kazi kwa nguvu kubwa zaidi ya kudanganya na kuangamiza, anaeneza kila mahali imani kuwa hayupo. Ni sera yake kujificha na kuficha mbinu anazotumia kufanya kazi yake.PKSw 395.1

  Hakuna kitu mdanganyaji mkuu anachoogopa zaidi kuliko sisi kujua mbinu zake. Ili kuficha tabia na makusudi yake halisi, amejifanya mwenyewe awasilishwe kwa namna ambayo inawafanya watu wamdhihaki na kumdharau. Anafurahi sana anapochorwa akiwa na umbo la kuchekesha au kuchukiza, lisilo la kawaida, nusu mnyama nusu mwanadamu. Anafurahi sana anaposikia jina lake lilikitumiwa katika michezo na dhihaka na wale wanaofikiri kuwa wao ni wenye akili nyingi na wasomi.PKSw 395.2

  Ni kwa sababu amejifunika kwa barakoa ya udanganyifu wa stadi za juu sana swali linaulizwa kila mahali: “Kiumbe wa aina hii yupo kweli?”PKSw 395.3

  Ushahidi wa mafanikio yake ni nadharia za uongo zilizo kinyume na ushahidi wa wazi wa Maandiko zinavyopokelewa na watu wengi katika ulimwengu wa kidini. Na ni kwa sababu Shetani anaweza kutawala kwa urahisi zaidi akili za wale ambao hawana habari za nguvu zake, neno la Mungu linatupatia mifano mingi ya kazi yake mbaya, likitufunulia nguvu zake za siri, na hivyo kutupatia tahadhari dhidi ya mashambulizi yake.PKSw 395.4

  Nguvu na ubaya wa Shetani na jeshi lake hutuweka katika hali ya tahadhari kwa haki kabisa ili tutafute hifadhi na wokovu katika nguvu kubwa zaidi ya Mwokozi wetu. Sisi tunafunga nyumba zetu kwa komeo na kufuli kulinda mali zetu na maisha yetu dhidi ya watu wabaya; lakini ni mara chache sana tunafikiria juu ya malaika waovu wanatutafuta daima, na ambao mashambulizi yao, katika nguvu zetu sisi wenyewe, hatuna mbinu ya kujilinda dhidi yake. Wakiruhusiwa, wanaweza kupotosha akili zetu, kuharibu na kutesa miili yetu, wanaweza kuharibu mali zetu na kuangamiza maisha yetu. Furaha yao pekee ni taabu na maangamizi. Hali ya kuogofya inawakabili wanaopinga madai ya Mungu na kujisalimisha kwa majaribu ya Shetani, mpaka Mungu anawaachia kwa utawala wa pepo. Lakini wale wanaomfuta Kristo daima wako salama chini ya ulinzi Wake. Malaika wenye nguvu nyingi wanatumwa kutoka mbinguni kuwalinda. Shetani hawezi kupenya ulinzi ambao Mungu amewazungushia watu Wake.PKSw 395.5

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents