Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 20—Mwamko Mkuu wa Kidini

  Mwamko mkuu wa kidini wakati wa utangazaji wa ujio wa haraka wa Kristo umetabiriwa katika unabii wa ujumbe wa malaika wa kwanza wa Ufunuo 14. Malaika anaonekana akiruka “katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa.” “Kwa sauti kuu” anatangaza ujumbe: “Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji” (Aya ya 6, 7).PKSw 272.1

  Ukweli kuwa malaika anatajwa kuwa ndiye anayetangaza onyo hili ni wa muhimu. Kwa njia ya usafi, utukufu, na nguvu ya mjumbe wa mbinguni, hekima ya Kiungu iliona vema kuwakilisha tabia iliyoinuliwa ya kazi iliyopaswa kutekelezwa kwa ujumbe na nguvu na utukufu ulioandamana nao. Na urukaji wa malaika “katikati ya mbingu,” na “sauti kuu” ambayo kwayo onyo linatolewa, na utangazaji wake kwa wote “wakaao juu ya nchi,“—“kwa kila taifa, na kabila, na lugha na jamaa”—hutoa ushahidi wa uharaka na ueneaji wa vuguvugu hilo ulimwenguni kote.PKSw 272.2

  Ujumbe wenyewe unadokeza kuhusiana na wakati mahsusi ambapo vuguvugu hilo hutokea. Unaelezwa kuwa sehemu ya “injili ya milele;” na unatangaza kuanza kwa hukumu. Ujumbe wa wokovu umehubiriwa katika zama zote; lakini ujumbe huu ni sehemu ya injili ambayo inahubiriwa wakati wa siku za mwisho peke yake, kwani wakati wa mwisho pekee ndiyo unaendana na tamko kuwa saa ya hukumu imekuja. Unabii huwasilisha mfululizo wa matukio yanayoongozana hadi wakati wa kuanza kwa hukumu. Jambo hili ni la kweli hususani katika kitabu cha Danieli. Lakini sehemu ile ya unabii wake unaohusiana na siku za mwisho, Danieli aliagizwa kuufunga na kuutia muhuri “hata wakati wa mwisho.” Ni mpaka tufikie wakati huu ndipo ujumbe kuhusiana na hukumu ungehubiriwa, ukiwa umejengwa juu ya utimizwaji wa unabii huu. Lakini wakati wa mwisho, nabii anasema, “wengi watakimbia huko na huko, na maarifa yataongozeka” (Danieli 12:4).PKSw 272.3

  Mtume Paulo alilionya kanisa lisitazamie ujio wa Kristo katika siku zake. “Siku ile haiji,” anasema, “usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu” (2 Wathesalonike 2:3). Mpaka baada ya uasi mkuu, na kipindi kirefu cha utawala wa “mtu wa kuasi,” ndipo pekee tunaweza kutazamia ujio wa pili wa Bwana. “Mtu wa kuasi,” ambaye pia anajulikana kama “siri ya uasi,” “mwana wa uharibifu,” na “yule mwovu,” huwakilisha upapa, ambao, kama ulivyotabiriwa katika unabii, ulipaswa kudumu kuwa mamlaka yenye nguvu kwa miaka 1260. Kipindi hicho kilikomea mwaka 1798. Ujio wa Kristo usingetokea kabla ya wakati huo. Paulo anaelezea kwa tahadhari kipindi chote cha Ukristo hadi mwaka 1798. Upande huu wa wakati huo ambapo ujumbe wa ujio wa Kristo unapaswa kuhubiriwa.PKSw 272.4

  Hakuna ujumbe kama huo uliowahi kuhubiriwa katika zama zilizopita. Paulo, kama tulivyokwisha kuona, hakuhubiri ujumbe huo; aliwaelekeza ndugu zake kwa wakati ujao uliokuwa bado mbali wa ujio wa Bwana. Wanamatengenezo hawakuhubiri ujumbe huo. Martin Luther aliweka siku ya hukumu kama miaka mia tatu katika wakati ujao tangu wakati wake. Lakini tangu mwaka 1798 kitabu cha Danieli kilifunguliwa, maarifa ya unabii yameongezeka, na wengi wamehubiri ujumbe mkuu wa ukaribu wa hukumu.PKSw 273.1

  Kama ilivyokuwa kwa Matengenezo ya karne ya kumi na sita, vuguvugu la ujio wa pili lilitokea katika nchi tofauti za Ukristo. Katika nchi za Ulaya na Amerika watu wa imani na maombi waliongozwa kujifunza unabii, na, wakifuatilia kumbukumbu ya Maandiko yaliyovuvia, waliona ushahidi unaoshawishi kuwa mwisho wa mambo yote ulikuwa karibu. Katika nchi tofauti kulikuwepo hapa na pale makundi ya Wakristo ambao, kwa kujifunza Maandiko peke yake, walijenga imani kuwa ujio wa Mwokozi ulikuwa karibu.PKSw 273.2

  Mwaka 1821, miaka mitatu baada ya Miller kufikia ufafanuzi wake wa unabii ulioonesha wakati wa hukumu, Dkt. Joseph Wolff, “mmishenari kwa ulimwengu,” alianza kutangaza ujio wa Bwana wa haraka. Wolff alizaliwa katika nchi ya Ujerumani, wazazi wake walikuwa Wayahudi, na baba yake alikuwa rabi wa Kiyahudi. Akiwa bado mdogo aliuamini ukweli wa dini ya Kikristo. Akiwa na akili inayojishughulisha, inayohoji, alikuwa msikilizaji makini wa maongezi yaliyofanyika katika nyumba ya baba yao kama Waebrania wacha Mungu wakisimulia matumaini na matarajio ya taifa lao, utukufu wa Masihi ajaye, na urejeshwaji wa Israeli. Siku moja aliposikia Yesu wa Nazareti akitajwa, kijana aliuliza akitaka kujua Yesu wa Nazareti alikuwa nani hasa. “Alikuwa Myahudi mwenye talanta kubwa sana,” ndilo lilikuwa jibu; “lakini alipojifanya kuwa Masihi, mahakama ya Kiyahudi ilimhukumu kifo” “Kwa nini,” aliongeza swali, “Yerusalemu iliangamizwa, na kwa nini tupo utumwani?” “Ala, ala!” baba yake alijibu, “kwa sababu Wayahudi waliwaua manabii.” Wazo lilijengeka mara moja kwa mtoto: “Labda Yesu pia alikuwa nabii, na Wayahudi walimwua wakati alikuwa hana hatia.”—Travels and Adventures of the Rev. Joseph Wolff, vol. 1, uk. 6. Hisia zilikuwa kali sana kiasi kwamba, ingawa alikatazwa kuingia katika Kanisa la Kikristo, alikaa nje ya kanisa kusikiliza mahubiri.PKSw 273.3

  Alipokuwa tu miaka saba alikuwa akitamba mbele ya jirani Mkristo mzee juu ya ushindi ujao wa Israeli wakati wa ujio wa Masihi, ambapo mzee alisema kwa utulivu: “Kijana mpendwa, nitakuambia Masihi wa kweli alikuwa nani: Alikuwa Yesu wa Nazareti, ... ambaye mababu zenu walimsulubisha, kama walivyowaua manabii wa zamani. Nenda nyumbani kasome sura ya hamsini na tatu ya Isaya, na utashawishika kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”—Ibid., vol. 1, uk. 7. Imani ilijengeka mara moja. Alienda nyumbani na kusoma maandiko, akiwa na shauku ya kuona jinsi maandiko yalivyotimia kikamilifu kupitia kwa Yesu wa Nazareti. Inawezekana kuwa maneno ya Mkristo yakawa ya kweli? Kijana alimwuliza baba yake ampe maelezo ya unabii, lakini alikutana na ukimya uliokuwa na hasira nyingi kiasi kwamba hakurudia tena kuzungumzia suala hilo siku zilizofuata. Lakini jambo hili, hata hivyo, liliongeza shauku yake ya kutaka kujua zaidi kuhusu dini ya Kikristo.PKSw 273.4

  Maarifa aliyoyatafuta yalifichwa kwa makini katika nyumba yake ya Kiyahudi; lakini, alipofika umri wa miaka kumi na moja, aliondoka nyumbani kwa baba yake na kwenda ulimwenguni kujipatia elimu, kuchagua dini yake mwenyewe na kazi yake ya maisha. Alikaribishwa kwa muda kuishi na jamaa zake wa karibu, lakini muda si mrefu alifukuzwa kutoka kwao kama mtu mwasi, na akiwa mpweke na bila pesa alilazimika kwenda kuishi miongoni mwa watu asiowajua. Alitangatanga huku na huko, akijifunza kwa bidii na kujipatia kipato kwa kufundisha Kiebrania. Kwa njia ya msaada wa mwalimu wa Kikatoliki aliongozwa kupokea imani ya Kirumi na alikusudia kuwa mmishenari kwa watu wake. Akiwa na kusudi hili, miaka michache baadaye, alienda kusoma katika Chuo cha Propaganda cha Rumi. Hapa, tabia yake ya mawazo huru na usemaji wa wazi vilimpa sifa mbaya ya uzushi. Alishambulia wazi wazi makosa ya kanisa na kudai umuhimu wa matengenezo. Ingawa mwanzoni alishughulikiwa kwa upendeleo na viongozi wa kipapa, baada ya muda si mrefu alifukuzwa Rumi. Chini ya ufuatiliwaji wa kanisa alihama kutoka mahali kwenda mahali kwingine, mpaka ilipothibitika kuwa asingewezekana kujisalimisha kwa utumwa wa Urumi. Alitangazwa kuwa mtu asiyewezekana aliachwa aende kokote alikopenda kwenda. Sasa alisafiri kwenda Uingereza na, akitangaza kuwa na imani ya Kiprotestanti, alijiunga na Kanisa la Kianglikana. Baada ya mafunzo ya miaka miwili aliondoka, mwaka 1821, na kwenda katika kazi yake ya umishenari.PKSw 274.1

  Wakati ambapo Wolff aliupokea ukweli mkuu wa ujio wa kwanza wa Kristo kama “Mtu wa huzuni, ajuaye sikitiko,” aliona kuwa unabii unafunua kwa uwazi ule ule ujio Wake wa pili katika nguvu na utukufu. Na wakati akitafuta kuwaongoza watu wake kwa Yesu wa Nazareti kama Yeye aliyeahidiwa, na kuwaonesha ujio Wake wa kwanza katika hali ya unyenyekevu kama kafara ya dhambi za wanadamu, aliwafundisha pia kuhusu ujio Wake wa pili kama mfalme na mkombozi.PKSw 274.2

  “Yesu wa Nazareti, Masihi wa kweli,” alisema, “ambaye mikono na nyayo Zake zilitobolewa, aliyepelekwa kama mwakondoo apelekwavyo machinjioni, aliyekuwa Mtu mwenye huzuni ajuaye sikitiko, ambaye baada ya fimbo ya ufalme kuondolewa kwa Yuda, na nguvu ya utungaji wa sheria kuondolewa kutoka katikati ya nyayo zake, alikuja kwa mara ya kwanza; atakuja kwa mara ya pili katika mawingu ya mbinguni, pamoja na tarumbeta ya Malaika Mkuu” (Joseph Wolff, Researches and Missionary Labors, ukurasa 62) “na atasimama juu ya Mlima wa Mizeituni; na kwamba utawala, ambao wakati mmoja alipewa Adamu juu ya uumbaji, halafu akanyang'anywa (Mwanzo 1:26; 3:17), atapewa Yesu. Atakuwa mfalme juu ya dunia yote. Maumivu na maombolezo ya viumbe yatakoma, bali nyimbo za sifa na shukurani zitasikika. ... Wakati Yesu anapokuja katika utukufu wa Baba Yake, pamoja na malaika watakatifu,... waaminio waliokufa watafufuka kwanza (1Wathesalonike 4:16; 1 Wakorintho 15:23). Huu ndio ambao sisi Wakristo tunauita ufufuo wa kwanza. Ndipo ufalme wa wanyama utabadilisha silika yake (Isaya 11:6-9), na kusalimishwa kwa Yesu (Zaburi 8). Amani itatawala katika Ulimwengu wote.”—Journal of the Rev. Joseph Wolff, kurasa 378, 379. “Bwana tena ataitazama dunia, na kusema, ‘Tazama, ni njema sana.'”— Ibid., ukurasa 294.PKSw 274.3

  Wolff aliamini ujio wa Bwana ulikuwa karibu, tafsiri yake ya vipindi vya kiunabii ikiweka hitimisho kuu hilo ndani ya miaka michache sana ya muda ulioelezwa na Miller. Kwa wale waliodai kutoka katika Maandiko, “Kuhusu siku na saa ile hakuna ajuaye,” kwamba watu hawapaswi kujua chochote kuhusu ukaribu wa ujio Wake wa pili, Wolff alijibu: “Kwani Bwana wetu alisema kuwa siku na saa ile haitajulikana kamwe? Kwani hakutueleza dalili za nyakati, zitusaidie kujua angalau ukaribu wa ujio Wake, kama vile mtu anavyojua ukaribu wa msimu wa kiangazi kwa mtini kupukutisha majani yake? (Mathayo 24:32). Je hatupaswi kamwe kujua kuwa kipindi kile, wakati Yeye Mwenyewe alituhimiza siyo tu kusoma kitabu cha nabii Danieli, bali pia kukielewa? Na katika kitabu hicho hicho cha Danieli, ambacho kinasema kuwa maneno yake yalifungwa mpaka wakati wa mwisho (ambapo ufungwaji wa maneno yake ulikuwa kwa wakati wa Danieli), na kuwa ‘wengi wataenda huko na huko’ (usemi wa lugha ya Kiebrania kwa ajili ya kuchunguza na kufikiri juu ya wakati), ‘na maarifa’ (kuhusu wakati) ‘yataongezeka’ (Danieli 12:4). Kando ya hili, Bwana wetu hakusudii kusema kwa kauli hii, kuwa ukaribu wa wakati hautajulikana, bali kuwa ‘siku na saa mahsusi hakuna mtu ajuaye.’ Inatosha, Yesu alisema, kuwa itajulikana kwa dalili za nyakati, kutuhimiza tujiandae kwa ajili ya ujio Wake, kama Nuhu alivyoandaa safina.”—Wolff, Researches and Missionary Labors, ukurasa 404, 405.PKSw 275.1

  Kuhusu mfumo maarufu wa kutafsiri, au kukosea kutafsiri Maandiko, Wolff aliandika: “Sehemu kubwa ya kanisa la Kikristo wameacha maana ya wazi ya Maandiko, na wamegeukia mfumo wa kufikirika wa Wabudha, wanaoamini kuwa furaha ya baadaye ya wanadamu itatokana na kutembea tembea hewani, na kudhani kuwa palipoandikwa Wayahudi ni lazima wapaelewe kumaanisha Mataifa; na wanaposoma Yerusalemu ni lazima wapafahamu kama kanisa; na ikiwa imesemwa nchi, inamaanisha anga; na kwa ajili ya ujio wa Bwana ni lazima wafahamu maendeleo ya vyama vya wamishenari; na kwenda juu ya mlima wa nyumba ya Bwana, humaanisha tabaka kubwa linalokutana na Wamethodisti.”—Journal of the Rev. Joseph Wolff, ukurasa 96.PKSw 275.2

  Kwa kipindi cha miaka ishirini na nne tangu 1821 hadi 1845, Wolff alisafiri sana: katika Bara la Afrika, alitembelea Misri na Ethiopia; katika Bara la Asia alizunguka katika nchi za Palestina, Siria, Uajemi, Bokhara, na India. Alitembelea pia Marekani, akiwa safarini kuelekea huko alihubiri katika kisiwa cha Mtakatifu Helena. Alifika New York mwezi wa Agosti, 1837; na, baada ya kuhubiri katika jiji lile, alihubiri katika jiji la Philadelphia na Baltimore, na mwisho alikwenda katika jiji la Washington. Hapa, alisema, “kwa njia ya hoja iliyotolewa na Rais mstaafu, John Quincy Adams, katika moja ya vikao vya Kongresi, Bunge lilipitisha kwa kauli moja azimio la kunipatia ukumbi wa Bunge la Kongresi kwa ajili yangu mimi kutoa mhadhara, ambao niliutoa siku ya Jumamosi, nikiheshimiwa kwa uwepo wa wabunge wote wa Kongresi, na pia kwa uwepo wa askofu wa Virginia, na uwepo wa viongozi wa dini na wakazi wa jiji la Washington. Heshima hiyo hiyo nilipewa na maofisa wa serikali wa majimbo ya New Jersey na Pennsylvania, ambapo na wao wakiwepo niliwasilisha mihadhara juu ya utafiti wangu nilioufanya katika Bara la Asia, na pia juu ya utawala binafsi wa Yesu Kristo.”—Ibid., ukurasa 398, 399.PKSw 276.1

  Dkt. Wolff alisafiri katika nchi za watu katili sana bila ulinzi wa serikali yo yote ya Ulaya, akistahimili shida nyingi na akiwa amezungukwa na hatari zisizokuwa na idadi. Aliteswa kwa kupigwa viboko kwenye visigino na kunyimwa chakula, aliuzwa kama mtumwa, na mara tatu alihukumiwa kifo. Alishambuliwa na majambazi, na mara kadhaa alikuwa karibu kufa kwa sababu ya kiu. Mara moja alinyang'anywa kila kitu alichokuwa nacho na aliachwa kutembea kwa miguu umbali mamia ya maili katika milima, barafu ikimpiga usoni na miguu yake isiyokuwa na viatu ikipoteza hisia kwa kukanyaga ardhi iliyoganda.PKSw 276.2

  Alipoonywa dhidi ya kwenda kwake bila silaha miongoni mwa makabila katili na pinzani, alisema kuwa “alikuwa na silaha”—“maombi, juhudi kwa ajili ya Kristo, na uhakika wa kupata msaada wa Mungu.” “Mimi pia,” alisema, “nina upendo kwa Mungu na kwa jirani yangu katika moyo wangu, na Biblia ipo mikononi mwangu.”—W.H.D. Adams, In Perils Oft, ukurasa 192. Alibeba Biblia ya Kiebrania na Kiingereza kila alipokwenda. Kuhusiana na moja ya safari zake alisema: “Nilidumu kuwa na Biblia iliyo wazi mikononi mwangu. Nilihisi kuwa nguvu yangu ilikuwa katika Kitabu, na kuwa nguvu ya Kitabu ilinipatia nguvu ya kusonga mbele.”—Ibid., ukurasa 201.PKSw 276.3

  Alidumu kushiriki katika kazi yake mpaka ujumbe wa hukumu ulipopelekwa katika sehemu kubwa ya dunia iliyokaliwa na wakati huo. Miongoni mwa Wayahudi, Waturuki Waparsi, Wahindu, na kwa watu wengine wengi wa mataifa na makabila mengine alihubiri neno la Mungu katika lugha mbalimbali na kila mahali alitangaza ukaribu wa Masihi.PKSw 277.1

  Katika safari zake katika nchi ya Bokhara alikuta fundisho la ujio wa karibu wa Bwana likishikiliwa na watu walioishi mbali na miji katika maeneo ya vijijini. Waarabu wa Yemeni, alisema, “wana kitabu kinachoitwa Seera, ambacho kinatoa tangazo la ujio wa pili wa Kristo na utawala Wake wa utukufu; na wanatarajia matukio makubwa yatokee katika mwaka 1840.”—Journal of the Rev. Joseph Wolff, ukurasa 377. “Katika nchi ya Yemeni... nilitumia siku sita nikiwa na watoto wa Rekabu. Hawanywi pombe, hawalimi mizabibu, hawapandi mbegu, na wanaishi katika mahema, na wanamkumbuka mzee mwema Yonadabu, mwana wa Rekabu; na nilikuta miongoni mwao wana wa Israeli, wa kabila ya Dani, ... wanaotarajia, pamoja na wana wa Rekabu, ujio wa haraka wa Masihi katika mawingu ya mbinguni.”—Ibid., ukurasa 389.PKSw 277.2

  Imani kama hiyo ilikutwa na mmishenari mwingine katika eneo la Tataria. Padri wa Kitataria alimwuliza mmishenari kuhusiana na lini Kristo angerudi mara ya pili. Mmishenari alipojibu kuwa hakujua chochote kuhusiana na lini Kristo angerudi, padri alishangaa sana kuhusiana na ujinga huo kwa mtu ambaye alidai kuwa mwalimu wa Biblia, na alieleza imani yake binafsi, iliyojengwa juu ya unabii, kuwa Kristo angekuja takribani mwaka 1844.PKSw 277.3

  Takribani mwanzoni mwa mwaka 1826 ujumbe wa ujio wa pili ulianza kuhubiriwa katika nchi ya Uingereza. Vuguvugu halikukua sana kama ilivyokuwa katika Bara la Amerika; wakati mahsusi wa ujio wa pili kwa jumla haukufundishwa, lakini ukweli mkuu wa ujio wa haraka wa Kristo katika nguvu na utukufu ulitangazwa maeneo mengi sana. Na ulitangazwa siyo miongoni mwa wapinzani au waungaji mkono peke yao. Mourant Brock, mwandishi wa Kiingereza, anasema kuwa takribani wachungaji mia saba wa Kanisa la Anglikana walijishughulisha na kuhubiri “injili hii ya ufalme” Ujumbe unaoeleza mwaka 1844 kama wakati wa kurudi kwa Bwana ulitolewa katika Uingereza Kuu. Machapisho ya Kiadventista kutoka Marekani yalisambazwa maeneo mengi sana. Vitabu na majarida vilichapishwa Uingereza. Na mwaka 1842 Robert Winter, Mwingereza kwa kuzaliwa, aliyekuwa amepokea imani ya marejeo katika Bara ya Amerika, alirudi katika nchi yake alikozaliwa kutangaza ujio wa Bwana. Wengi waliungana naye katika kazi, na ujumbe wa hukumu ulitangazwa katika sehemu mbalimbali na Uingereza.PKSw 277.4

  Katika Amerika ya Kusini, katikati ya ukatili na udanganyifu wa kidini, Lakunza, Mhispinia na Mjesuti, alijifunza Maandiko na kwa njia hiyo alipokea ukweli wa marejeo ya haraka ya Kristo. Akisukumwa kutoa onyo, lakini akitamani kuepuka makaripio ya Rumi, alichapisha mawazo yake kwa kutumia jina tofauti na lake la “Rabbi Ben-Ezra,” akijifanya kuwa Myahudi aliyeongoka. Lakunza aliishi katika karne ya kumi na nane, lakini ilikuwa takribani mwaka 1825 ambapo kitabu chake, ambacho baada ya kufika London, kilitafsiriwa katika lugha ya Kiingereza. Kuchapishwa kwake kulisaidia kukuza shauku iliyokuwa ikiamka katika nchi ya Uingereza kuhusu mada ya ujio wa pili wa Kristo.PKSw 278.1

  Katika nchi ya Ujerumani fundisho hili lilifundishwa katika karne ya kumi na nane na Bengeli, mchungaji wa Kanisa la Lutherani na msomi mashuhuri na mkosoaji wa Biblia. Baada ya kuhitimu elimu yake, Bengeli“alijikita katika kujifunza teolojia, ambayo uwezo wake mkubwa wa kiakili na wa kidini uliokuzwa na mafunzo na nidhamu yake ya awali, vilimwongoza kufanya. Kama vijana wengine wenye tabia ya kutafakari mambo kwa kina, kabla na tangu hapo, alianza kupambana na mashaka na matatizo ya asili ya kidini, na anagusia, kwa hisia kubwa, ‘mishale mingi ambayo ilichoma moyo wake, na kusababisha ugumu katika maisha ya ujana wake.’” Akiwa mjumbe wa Baraza la Kanisa la Wurttemberg, alitetea uhuru wa dini. “Huku akidumisha haki na fursa za kanisa, alikuwa mtetezi wa uhuru wa msingi uliotolewa kwa wale waliohisi kuwa wamefungwa, kwa misingi ya dhamiri, kujitoa katika ushirika wa kanisa.”—Encyclopaedia Britannica, 9th ed., art. “Bengel.” Athari chanya za sera hii bado zinahisiwa katika jimbo lake la kuzaliwa.PKSw 278.2

  Ilikuwa wakati akihubiri kutoka Ufunuo 21 kwa ajili ya Jumapili ya majilio ambapo nuru ya ujio wa pili wa Kristo ilimulika katika akili ya Bengeli. Unabii wa Ufunuo ulifunuliwa katika ufahamu wake zaidi kuliko hapo awali. Akiwa amegubikwa na hisia ya umuhimu wa kushangaza na utukufu mwingi wa matukio yaliyowasilishwa na nabii, alilazimishwa kuacha kwa muda kutafakari juu ya mada hiyo. Katika mimbari lilijitokeza tena kwa uwazi wake wote na nguvu zake zote. Tangu wakati huo alielekeza nguvu zake zote katika kujifunza unabii, hususani ule uliohusu kitabu cha Ufunuo, na kwa muda mfupi alifikia hatima ya kuamini kuwa ulielezea juu ya ujio wa karibu wa Kristo. Tarehe aliyoiweka kama wakati wa ujio wa pili wa Kristo ilikuwa ndani ya miaka michache baada ya ile iliyowekwa na Miller.PKSw 278.3

  Maandishi ya Bengeli yalisambazwa katika ulimwengu wote wa Kikristo. Mawazo yake ya unabii yalipokelewa kwa jumla katika jimbo lake la Wurttemberg, na kwa kiasi fulani katika maeneo mengi ya Ujerumani. Vuguvugu liliendelea baada ya kifo chake, na ujumbe wa marejeo ulisikika katika nchi ya Ujerumani kwa wakati huo huo ulipokuwa ukipata mvuto katika nchi zingine. Tarehe za mwanzoni baadhi ya waumini walienda Urusi na kule waliunda makoloni, na imani ya ujio wa haraka wa Kristo bado inashikiliwa na makanisa ya Ujerumani katika nchi ya Urusi.PKSw 278.4

  Nuru iliangaza pia katika nchi ya Ufaransa na Uswisi. Katika jiji la Geneva ambapo Fareli na Kalvini walieneza ukweli wa Matengenezo, Gaussen alihubiri ujumbe wa ujio wa pili. Wakati akiwa mwanafunzi shuleni, Gaussen alikutana na roho ya mantiki iliyoenea katika nchi zote za Ulaya katika sehemu ya mwisho ya karne ya kumi na nane na sehemu ya mwanzo wa karne ya kumi na tisa; na alipojiunga na uchungaji alikuwa haelewi imani ya kweli, bali alikuwa na mwelekeo wa kutokuwa na imani. Katika ujana wake alipata shauku ya kujifunza unabii. Baada ya kusoma kitabu cha Rollin’s Ancient History, fikra zake zilielekezwa katika sura ya pili ya Danieli, na aliguswa na usahihi wa kushangaza wa unabii uliotimizwa, kama ulivyoonekana katika kumbukumbu za kihistoria. Hapa kulikuwa na ushuhuda wa uvuvio wa Maandiko, uliotumika kama nanga kwake katikati ya hatari za miaka ya baadaye. Hakuridhishwa na mafundisho ya mantiki, na katika kujifunza Biblia na kutafuta nuru kubwa, baada ya muda, aliongozwa kujenga imani chanya.PKSw 279.1

  Alipokuwa akifanya utafiti wake wa unabii alifikia hatua ya kuwa na imani kuwa ujio wa Bwana ulikuwa umekaribia. Kwa kuguswa na utukufu na umuhimu wa ukweli huu mkuu, alitamani kuuleta mbele ya watu; lakini imani iliyozoeleka kuwa unabii wa Danieli ni siri na hauwezi kueleweka kilikuwa kikwazo kikubwa katika njia yake. Hatimaye aliazimia—kama Fareli alivyofanya kabla yake katika kuihubiri Geneva—kuanza na watoto, kupitia kwao alitumaini kuwafurahisha wazazi wake.PKSw 279.2

  “Natamani kueleweka,“alisema baadaye, akizungumzia lengo lake katika kazi hii, “siyo kwa sababu ya umuhimu wake mdogo, lakini kinyume chake, kwa sababu ya thamani yake kubwa, kwamba nilitamani kuuwasilisha katika muundo wake unaoeleweka, na kwamba niliuwasilisha kwa watoto kwanza. Nilitamani kusikiwa, na niliogopa nisingesikiwa ikiwa ningeanza na watu wazima kwanza.” “Niliazimia, hivyo basi, niwaendee watoto wadogo kwanza. Nilikusanya wasikilizaji ambao ni watoto wadogo; ikiwa kundi likiongozeka, ikiwa inaonekana kuwa wanasikiliza, wamefurahishwa, wanatamani, kuwa wanafahamu na kueleza mada, nina hakika ya kuwa na duara la pili, na katika zamu yao, watu wazima wataona kuwa ni muhimu kutumia muda wao kukaa chini na kujifunza. Jambo hili likitendeka, kazi itakuwa imekamilika.”—L. Gaussen, Daniel the Prophet, vol. 2, Preface.PKSw 279.3

  Juhudi zilifanikiwa. Alipowafundisha watoto, watu wazima walikuja kusikiliza. Korido za kanisa lake zilijaa wasikilizaji wenye usikivu mzuri. Miongoni mwao walikuwemo watu wenye vyeo na wasomi, na wageni na wasafiri kutoka nchi za nje waliotembelea jiji la Geneva; na hivyo ujumbe ulipelekwa sehemu zingine.PKSw 279.4

  Kwa kutiwa moyo na mafanikio haya, Gaussen alichapisha masomo yake, kwa matumaini ya kuhamasisha ujifunzaji wa vitabu vya unabii katika makanisa ya watu wanaoongea Kifaransa. “Kuchapisha mafundisho yanayotolewa kwa watoto,” Gaussen alisema, “ni kuwaambia watu wazima, ambao mara nyingi pia hupuuza vitabu kama hivyo kwa kisingizio cha uongo kuwa havieleweki, ‘Vinawezaje kutoeleweka, wakati watoto wenu wanavielewa?’” “Nilikuwa na shauku kubwa,” aliongeza, “ya kutoa elimu ya unabii unaopendwa na watu wetu, kama ikiwezekana” “Hakuna ujifunzaji, kwa kweli, ambao unaonekana kwangu kuwa unakidhi mahitaji zaidi.” “Ni kwa sababu ya jambo hili ambalo kwalo inatupasa kujiandaa kwa ajili ya mateso yaliyo karibu, na kukesha na kumngoja Yesu Kristo.”PKSw 280.1

  Ingawa alikuwa mmoja wa wahubiri mashuhuri na waliokuwa wanapendwa katika lugha ya Kifaransa, Gaussen baada ya muda mfupi aliondolewa katika uchungaji, kosa lake kubwa likiwa kwamba badala ya katekisimu ya kanisa, mwongozo baridi na razini, unaokaribia kukosa kabisa imani chanya, alikuwa anatumia Biblia kuwafundisha vijana. Baadaye alifanya kazi ya kufundisha katika shule ya theolojia, wakati huo huo siku ya Jumapili aliendelea na kazi yake kama katekista, akiongea na watoto na kuwafundisha Maandiko. Kazi yake kuhusu unabii iliamsha shauku kubwa. Kutoka katika kiti cha profesa, kwa njia ya mitambo ya uchapishaji, na katika kazi yake aliyoipenda kama mwalimu wa watoto aliendelea kwa miaka mingi kuwa na mvuto mkubwa na mwezeshaji katika kujifunza unabii ulioonesha kuwa ujio wa Bwana ulikuwa karibu.PKSw 280.2

  Katika nchi ya Scandinavia pia ujumbe wa marejeo ulitangazwa, na shauku ya watu mahali pengi iliamshwa. Wengi waliamshwa kutoka katika hali yao ya kutojali usalama wao wakaungama na kuziacha dhambi zao, na waliomba msamaha katika jina la Kristo. Lakini viongozi wa kanisa la dola walipinga vuguvugu, na kwa njia ya mvuto wao baadhi ya waliohubiri ujumbe walitupwa gerezani. Katika maeneo mengi ambapo wahubiri wa ujio wa haraka wa Bwana walinyamazishwa, Mungu alipendezwa kutuma ujumbe, kwa njia ya kimuujiza, kupitia watoto wadogo. Kwa kuwa walikuwa na umri mdogo, sheria ya nchi isingewazuia, na waliruhusiwa kusema bila kubughudhiwa.PKSw 280.3

  Vuguvugu lilikuwa zaidi miongoni mwa watu wa tabaka la watu wa chini, na lilipamba moto katika nyumba za kawaida za vibarua ambamo watu walikusanyika kusikiliza onyo. Wahubiri watoto wenyewe walikuwa maskini wakazi wa vibanda hivyo. Baadhi yao walikuwa na umri usiozidi miaka sita au nane; na wakati ambapo maisha yao yalishuhudia kuwa walimpenda Mwokozi, na walijaribu kuishi maisha ya utii kwa matakwa matakatifu ya Mungu, wakionesha akili na uwezo wa kawaida tu ambao huonekana kwa watoto wa umri huo. Waliposimama mbele ya watu, hata hivyo, ilishuhudiwa kuwa walisukumwa na nguvu iliyokuwa kubwa zaidi ya karama zao za asili. Mwelekeo na tabia vilibadilika, na kwa nguvu kubwa walitoa onyo la hukumu, wakitumia maneno mahsusi ya Maandiko: “Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja.” Walikemea dhambi za watu, siyo tu kwa kushutumu ufisadi na uovu, bali pia kwa kukemea kuipenda dunia na kurudi nyuma kiroho, na wakiwaonya wasikilizaji wao wafanye haraka kuikimbia hasira inayokuja.PKSw 280.4

  Watu walisikiliza kwa kutetemeka. Roho wa Mungu anayeshawishi aliongea na mioyo yao. Wengi waliongozwa kuchunguza Maandiko kwa shauku mpya na ya kina, wasio na kiasi na wasio waadilifu walifanya matengenezo, wengine waliacha matendo yao ya dhuluma, na kazi ilifanyika kwa namna ambayo hata wachungaji wa kanisa la dola walilazimika kukiri kuwa mkono wa Mungu ulikuwa katika vuguvugu hilo.PKSw 281.1

  Ilikuwa mapenzi ya Mungu kuwa habari za ujio wa Mwokozi zihubiriwe katika nchi za Skandinavia; na sauti za watumishi Wake ziliponyamazishwa, Mungu aliweka Roho Wake juu ya watoto, ili kwamba kazi itekelezwe. Yesu alipokuwa karibu na Yerusalemu akikaribishwa na makundi ya watu wenye furaha kuwa, kwa kelele za ushindi na upeperushaji wa matawi ya mitende, walimtangaza kama Mwana wa Daudi, Mafarisayo na Masadukayo walimwagiza awanyamazishe; lakini Yesu aliwajibu kuwa yote yale yalikuwa hivyo ili kutimiza unabii, na ikiwa hawa watanyamaza, mawe yatapiga kelele. Watu, wakiwa wametishiwa kwa vitisho vya makuhani na watawala, walisitisha utangazaji wao wa furaha walipokuwa wakiingia malango ya Yerusalemu; lakini watoto katika ukumbi wa hekalu baadaye walilidaka pambio hilo, na, wakipeperusha matawi yao ya mitende, walipiga kelele: “Hosana Mwana wa Daudi!” (Mathayo 21:8-16). Mafarisayo, wakiwa wamechukizwa sana, walimwambia Yesu, “Wasikia hawa wasemavyo?” Yesu alijibu, “Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa?” Mungu alitekeleza kwa njia ya watoto wakati wa ujio wa kwanza wa Kristo, kadhalika aliwatumia watoto kutoa ujumbe wa ujio wa pili wa Kristo. Neno la Mungu inapasa litimizwe, kuwa utangazaji wa ujio wa Mwokozi ilipaswa utolewe kwa kila jamaa, lugha, na kabila za watu.PKSw 281.2

  Kwa William Miller na washirika wake lilitolewa agizo la kuhubiri onyo kwa watu wa Amerika. Nchi ya Marekani ilikuja kuwa kitovu vuguvugu kuu la marejeo. Ilikuwa hapa ambapo unabii wa ujumbe wa malaika wa kwanza ulipata utimizwaji wake wa moja kwa moja. Maandishi ya Miller na wenzake yalisambazwa hadi nchi za mbali. Kila mahali ambapo wamishenari walipenya mahali pote ulimwenguni, ilipelekwa habari njema ya marejeo ya haraka ya Kristo. Maeneo ya mbali na mengi ulienea ujumbe wa injili ya milele: “Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja.”PKSw 281.3

  Ushuhuda wa unabii ulioonekana kueleza kuwa ujio wa Kristo katika msimu wa masika wa mwaka 1844 ulishika akili za watu. Ujumbe ulipoenea kutoka jimbo moja hadi jimbo, kila mahali kulikuwepo mwamko mkubwa kwa watu wengi. Wengi walishawishika kuwa hoja zilizotokana na vipindi vya kiunabii zilikuwa sahihi, na, wakiacha kiburi cha maoni yao, waliupokea ukweli kwa furaha. Baadhi ya wachungaji waliweka kando mawazo yao na hisia zao za kimadhehebu, waliacha mishahara na makanisa yao, na waliungana katika kutangaza ujio wa Yesu. Walikuwepo wachungaji wachache, hata hivyo, ambao walikuwa tayari kuupokea ujumbe huu; hivyo basi uliachiwa zaidi walei wa kawaida. Wakulima waliacha mashamba yao, mafundi waliweka chini zana zao, wafanya biashara waliacha bidhaa zao, wanataaluma waliacha vyeo vyao; na bado idadi ya wafanya kazi ilikuwa ndogo kulinganisha na kazi iliyotekelezwa. Hali ya kanisa la watu wasiomcha Mungu na ulimwengu uliolala katika uovu, ilizilemea roho za walinzi wa kweli, na walikabiliana na kazi za suluba kwa hiari yao wenyewe, kujinyima, na mateso, ili wawaite watu kutubu ili wapate wokovu. Japokuwa walimpinga Shetani, kazi ilisonga mbele hatua kwa hatua, na ukweli wa marejeo ulipokelewa na watu maelfu.PKSw 282.1

  Kila mahali ushuhuda unaogusa ulisikika, ukiwaonya wenye dhambi, watu wa dunia na washiriki wa kanisa, kuikimbia hasira inayokuja. Kama alivyokuwa Yohana Mbatizaji, mtangulizi wa Kristo, wahubiri waliweka shoka katika shina la mti na waliwahimiza watu wote wazae matunda yaletayo toba. Miito yao yenye mguso ilikuwa na tofauti kubwa ukilinganisha na uhakikisho wa amani na usalama uliosikika ukitolewa katika mimbari mashuhuri; na kila mahali ambapo ujumbe ulitolewa, uliteka fikra za watu. Ushududa sahili, wa moja kwa moja wa Maandiko, ulieleweka kwa njia ya nguvu ya Roho Mtakatifu, ulileta uzito katika ushawishi ambao wachache waliweza kupinga kabisa. Maprofesa wa dini waliamshwa kutoka katika usalama wa uongo. Waliona kurudi nyuma kwao, udunia wao na kutokuamini kwao, kiburi chao na ubinafsi wao. Wengi walimtafuta Bwana kwa toba na unyenyekevu. Mshikamano ambao kwa muda mrefu walikuwa nao na vitu vya kidunia ulielekezwa kwa mambo ya mbinguni. Roho wa Mungu alikaa juu yao, na kwa mioyo iliyolainishwa na kutiishwa waliungana na kupiga kelele kwa pamoja: “Mcheni Mungu, na kumtukuza; kwa kuwa hukumu Yake imekuja.”PKSw 282.2

  Wenye dhambi waliuliza kwa machozi: “Nifanye nini nipate kuokoka?” Wale ambao maisha yao yalisifika kwa kukosa uaminifu walikuwa na shauku ya kurudisha vitu walivyovipata kwa dhuluma. Wote waliopata amani katika Kristo walitamani kuwaona wengine pia wakipata mbaraka huo. Mioyo ya wazazi iliwarudia watoto wao, na mioyo ya watoto iliwarudia wazazi wao. Vizuizi vya kiburi na kujiamini vilifutiliwa mbali. Maungamo ya dhati yalifanywa, na watu wa nyumbani walifanya kazi sana kwa ajili ya wokovu wa wale walio karibu yao na wale waliowapenda. Mara nyingi ilisikika sauti ya kuombeana kwa dhati. Kila mahali kulikuwepo na roho zilizokuwa katika kumsihi Mungu kwa dhati. Wengi walipambana usiku kucha ili kupata uhakikisho wa msamaha wa dhambi zao, au kwa ajili ya kuongoka kwa ndugu zao wa karibu au majirani zao.PKSw 282.3

  Tabaka zote za watu walifurika katika mikutano ya Waadventista. Matajiri kwa masikini, walio juu na walio chini, waliokuwa na kazi za aina mbalimbali, wakiwa na shauku ya kusikia wao wenyewe, fundisho la ujio wa pili. Bwana alidhibiti roho ya upinzani wakati watumishi Wake walipofafanua sababu za imani yao. Nyakati zingine chombo kilikuwa dhaifu; lakini Roho wa Mungu alitoa nguvu kwa ajili ya ukweli Wake. Uwepo wa malaika watakatifu ulihisiwa katikati ya mikutano hii, na waongofu wengi waliongezwa kila siku kwa wale waliokuwa wameamini. Kwa kadiri ushahidi wa ujio wa haraka wa Kristo ulivyorudiwa mara kwa mara, makundi makubwa ya watu walisikiliza maneno mazito kwa ukimya mkubwa. Mbingu na nchi vilionekana kukaribiana. Nguvu ya Mungu ilihisiwa na wazee na vijana na watu wa umri wa kati. Watu walirudi majumbani mwao wakiwa na sifa midomoni mwao, na sauti ya furaha ilisikika katika hewa tulivu ya usiku. Hakuna aliyehudhuria mikutano hiyo ambaye anaweza kusahau mandhari zile zinazosisimua.PKSw 283.1

  Utangazaji wa wakati mahsusi wa ujio wa Kristo uliamsha upinzani mkali kutoka kwa watu wengi tabaka zote, tangu kwa mchungaji katika mimbari hadi kwa mwenye dhambi asiyejali, wa kutupwa. Maneno ya unabii yalitimizwa: “Katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa” (2 Petro 3:3, 4). Wengi wa waliodai kumpenda Mwokozi, walitangaza kuwa hawakuwa na upinzani dhidi ya fundisho la ujio wa pili; walidai kuwa walipinga tu utangazaji wa wakati mahsusi. Lakini jicho la Mungu linaloona kila kitu lilisoma mioyo yao. Hawakupenda kusikia habari za ujio wa Kristo kuuhukumu ulimwengu katika haki. Hawakuwa watumishi waaminifu, kazi zao zisingeweza kustahimili ukaguzi wa Mungu anayechunguza mioyo, na waliogopa kukutana na Bwana wao. Kama Wayahudi wakati wa ujio wa kwanza wa Kristo hawakuwa tayari kumkaribisha Yesu. Siyo tu kuwa walikataa kusikiliza hoja za wazi za Biblia, bali pia waliwadhihaki watu waliomtarajia Bwana. Shetani na malaika zake walishangilia, na walirusha dhihaka kwa Kristo na malaika watakatifu kuwa watu Wake walimpenda kidogo sana na kuwa hawakuwa na shauku ya kuja Kwake.PKSw 283.2

  “Hakuna ajuaye siku wala saa” ilikuwa hoja ambayo ilitolewa mara nyingi na watu waliokataa imani ya marejeo. Maandiko yanasema: “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake” (Mathayo 24:36). Maelezo ya wazi na yanayopatana ya aya hii yalitolewa na wale waliomtarajia Bwana, na matumizi mabaya yaliyofanywa wapinzani wao yalioneshwa wazi wazi. Maneno yalisemwa na Kristo katika yale maongezi yanayokumbukwa na wanafunzi Wake juu ya mlima wa Mizetuini baada kutoka hekaluni kwa mara ya mwisho. Wanafunzi walikuwa wameuliza swali: “Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?” Yesu aliwapa dalili, na alisema: “Nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni” (Aya 3, 33). Kauli moja ya Mwokozi isitumiwe kuharibu kauli yake nyingine. Ingawa hakuna mtu anayejua siku wala saa ya ujio Wake, tumeelekezwa na tumetakiwa kujua wakati unapokaribia. Tumefundishwa pia kuwa kupuuza onyo Lake, na kukataa au kupuuza kujua wakati marejeo Yake yanapokaribia, tutaangamia kama walivyoangamia watu walioishi wakati wa Nuhu kwa kukataa kujua wakati gharika ilipokuwa inakuja. Na mfano katika sura hiyo hiyo, inayoonesha matokeo tofauti kwa mtumishi mwaminifu na asiyekuwa mwaminifu, na kutoa fursa kwa mtu aliyesema moyoni mwake, “Bwana wangu anachelewa kuja,” inaonesha nuru ambayo kwayo Kristo aliwachukulia na kuwazawadia wale anaowakuta wakikesha, na wakifundisha ujio Wake, na wale wanaoukataa. “Kesheni basi,” alisema. “Heri mtumwa yule, ambaye Bwana wake akija atamkuta akifanya hivyo” (Aya 42, 46). “Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako” (Ufunuo 3:3).PKSw 284.1

  Paulo anaongelea juu ya tabaka la watu ambao kwao kuja kwa Bwana kutakuwa jambo la kushtukiza. “Siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, ....wala hakika hawataokolewa” Lakini anaongozea, kwa wale ambao watakuwa wamesikiliza onyo la Mwokozi: “Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza” (1 Wathesalonike 5:2-5).PKSw 284.2

  Hivyo ilioneshwa kuwa Maandiko hayatoi idhini kwa watu kubaki katika ujinga kuhusiana na ukaribu wa ujio wa Kristo. Lakini wale waliokuwa na shauku ya kupata kisingizio cha kuukataa ukweli waliziba masikio yao wasisikilize maelezo haya, na maneno “Hakuna mtu ajuaye siku wala saa” yaliendelea kurudiwa na watu wenye dhihaka na hata watu waliodai kuwa wachugaji wa Kiristo. Watu walipoamshwa, na kuanza kuulizia juu ya njia ya wokovu, walimu wa dini waliingia kati yao na ukweli, wakitafuta kunyamazisha hofu zao kwa kutoa tafsiri za uongo za neno la Mungu. Walinzi wasiokuwa waaminifu waliungana katika kazi ya mdanganyaji mkuu, wakipiga kelele, Amani, amani, wakati Mungu hakusema amani. Kama Mafarisayo katika siku za Kristo, wengi walikataa kuingia katika ufalme wa mbinguni, na wale waliokuwa wakiingia waliwazuia. Damu ya roho hizi itatakiwa mikononi mwao.PKSw 284.3

  Watu wanyenyekevu na waaminifu kabisa katika makanisa ndio ambao mara nyingi walikuwa wa kwanza kupokea ujumbe. Waliojisomea Biblia wenyewe waliona jinsi ambavyo tafsiri za unabii zilizofundishwa na kuaminiwa na watu wengi wakati huo hazikuwa na msingi wowote wa kimaandiko; na mahali popote pale ambapo watu hawakutawaliwa na mvuto wa viongozi wa makanisa, popote pale ambapo watu waliweza kuchunguza maandiko wenyewe, fundisho la marejeo lilihitaji tu kulinganishwa na Maandiko kulipatia mamlaka ya Kiungu.PKSw 285.1

  Wengi waliteswa na ndugu zao wasioamini. Ili wabaki katika nafasi zao kanisani, baadhi walikubali kubaki kimya juu ya tumaini lao; lakini wengine walihisi kuwa utii wao kwa Mungu uliwakataza kuficha ukweli ambao Mungu alikuwa amewakabidhi kama dhamana. Sio wachache walioondolewa katika ushirika wa kanisa sio kwa sababu nyingine isipokuwa tu ile ya kueleza imani yao kuhusu ujio wa Kristo. Maneno ya nabii yalikuwa ya thamani kubwa sana kwa wale waliostahimili majaribu ya imani yao: “Ndugu zenu wawachukiao ninyi, waliowatupa kwa ajili ya jina langu, wamesema, Na atukuzwe Bwana, tupate kuiona furaha yenu; lakini watatahayarika” (Isaya 66:5).PKSw 285.2

  Malaika wa Mungu walikuwa wakiangalia kwa shauku kubwa matokeo ya onyo. Wakati makanisa mengi yalipokataa ujumbe, malaika waligeukia upande mwingine kwa huzuni. Lakini walikuwepo watu wengi ambao walikuwa hawajajaribiwa kuhusiana na ukweli wa marejeo. Wengi walipotoshwa na waume zao, wake zao, wazazi wao, au watoto wao, walisukumwa kuaminishwa kuwa ni dhambi hata kusikiliza uzushi kama huo uliofundishwa na Waadventista. Malaika waliagizwa kuwalinda kwa uaminifu watu hawa, kwa kuwa nuru nyingi ilipaswa ing'ae tena juu yao kutoka katika kiti cha enzi cha Mungu.PKSw 285.3

  Kwa shauku isiyoelezeka wale waliopokea ujumbe walikesha wakingoja ujio wa Mwokozi wao. Wakati ambao walitarajia kukutana Naye ulikuwa karibu. Walikaribia saa hii kwa utulivu mkubwa. Walibaki katika tafakari nzuri kuhusu Mungu, na uhalisia wa amani ambayo wangeipata katika muda mfupi angavu baada ya wakati huo. Hakuna ye yote aliyepata uzoefu wa tumaini hili anayeweza kusahau saa zile za thamani za kungoja. Kwa majuma kadhaa kabla ya wakati huo, shughuli za ulimwengu ziliwekwa pembeni kwa muda kwa walio wengi. Waaminio waaminifu walichunguza kwa makini kila wazo na mhemko wa mioyo yao kana kwamba wapo juu ya vitanda vya kifo chao na katika saa chache wafumbe macho yao na kuachana na mandhari za kidunia. Kulikuwa hakuna ushonaji wa “majoho ya kupaalia” (tazama Kiambatisho); lakini wote walihisi hitaji la ushahidi wa ndani kuwa walikuwa tayari kukutana na Mwokozi; majoho yao meupe yalikuwa usafi wa roho zao—tabia zilizotakaswa dhambi kwa damu ya upatanisho ya Kristo. Heri kama kungekuwa bado miongoni mwa watu wanaodai kuwa wa Mungu roho ile ile ya kujichunguza mioyo, imani ile ile ya dhati, na iliyo thabiti. Ikiwa wangeendelea kujinyenyekesha mbele ya Bwana na kupeleka maombi yao mbele ya kiti cha rehema wangeweza kuwa na uzoefu mkubwa zaidi kuliko walio nao sasa. Kuna maombi machache sana, kushawishika kudogo sana kuhusiana na dhambi, na ukosefu wa imani iliyo hai unawaacha wengi bila neema itolewayo kwa wingi na Mkombozi wetu.PKSw 285.4

  Mungu alipanga kuwahakiki watu Wake. Mkono Wake ulifunika kosa katika ukokotoaji wao wa vipindi vya kiunabii.Waadventista hawakugundua kosa, wala halikugunduliwa na wasomi wa hali ya juu kabisa miongoni mwa wapinzani wao. Wapinzani wao wasomi walisema: “Ukokotoaji wenu wa vipindi vya kiunabii ni sahihi. Tukio kubwa la aina fulani liko karibu kutokea; lakini siyo hilo ambalo Bwana Miller analitabiri; ni uongofu wa ulimwengu, na siyo ujio wa pili wa Kristo” (Tazama Kiambatisho.)PKSw 286.1

  Wakati wa matarajio ulipita, na Kristo hakuoonekana na kuwakomboa watu Wake. Wale ambao kwa imani ya dhati na upendo wa kweli walikuwa wametarajia kumwona Mwokozi wao, walihisi maumivu makali sana. Lakini makusudi ya Mungu yalitimizwa; alikuwa akihakiki mioyo ya watu waliodai kuwa wanangojea ujio Wake. Walikuwepo miongoni mwao wengi waliokuwa wamesukumwa kungoja siyo kwa sababu ya makusudi sahihi bila hofu tu. Kutangaza imani yao kulikuwa hakujabadilisha mioyo yao wala maisha yao. Wakati tukio lililotarajiwa lilipoacha kutokea watu hawa, walitangaza kuwa hawakuumia kwa namna yo yote ile; hawakuwa na imani yo yote kuwa Kristo angekuja. Walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kudhihaki huzuni ya walioamini kwa dhati.PKSw 286.2

  Lakini Yesu na jeshi lote la mbinguni waliwaangalia kwa upendo na huruma wale waliokuwa wamejaribiwa na waaminifu lakini waliokuwa wameumizwa. Ikiwa pazia linalogawa ulimwengu unaoonekana na usioonekana lingefunguliwa, malaika wangeweza kuonekana wakiwakaribia watu hawa waaminifu wakiwakinga dhidi ya mishale ya Shetani.PKSw 286.3

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents