Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 7—Luther Ajitenga na Rumi

  Miongoni mwa wale walioitwa kuliongoza kanisa kutoka katika giza la upapa na kulipeleka katika nuru ya imani safi, aliyekuwa maarufu zaidi kuliko wote alikuwa Martin Luther. Akiwa mwenye, juhudi, umakini, na uaminifu, asiyeogopa kitu cho chote isipokuwa Mungu, na asiyetambua msingi mwingine wa imani ya kidini isipokuwa Maandiko Matakatifu, Luther alikuwa mtu maalumu kwa wakati wake; kupitia kwake Mungu alitimiza kazi kubwa ya matengenezo ya kanisa na kutoa mwangaza kwa ulimwengu.PKSw 88.1

  Kama walivyokuwa wajumbe wa awali wa injili, Luther alizaliwa katika mazingira ya kimaskini. Miaka yake ya awali ilitumika akiishi katika nyumba ya kimaskini ya mkulima wa Kijerumani. Kwa kutoa jasho kila siku kama mfanya kazi katika mgodi wa baba yake alipata pesa kwa ajili ya elimu yake. Alidhamiria awe mwanasheria; lakini Mungu alikusudia kumfanya awe mjenzi wa hekalu kuu lililokuwa likiinuka pole pole katika karne zote. Ugumu, kujinyima, na nidhamu kali vilikuwa shule ambayo Hekima ya Milele ilimwandaa Luther kwa ajili ya utume muhimu wa maisha yake.PKSw 88.2

  Baba yake Luther alikuwa mtu mwenye akili sana na utendaji na msukumo mkubwa wa tabia, mwaminifu, mwenye msimamo, na mnyoofu. Alisimamia kile alichokiamini kuwa ni wajibu wake, bila kujali kile ambacho kingetokea. Nia yake njema ilimwongoza kutilia mashaka mfumo wa kitawa. Alichukizwa sana wakati Luther alipoingia, bila ridhaa yake, nyumba ya watawa; na ilichukua miaka miwili kabla baba yake hajapatanishwa na mwanawe, na hata hivyo maoni yake yalibaki vile vile.PKSw 88.3

  Wazazi wa Luther waliwekeza kwa umakini mkubwa katika elimu na mafunzo ya watoto wao. Walijitahidi sana kuwafundisha neno la Mungu na kanuni njema za maisha ya Kikristo. Ombi la baba daima lilitolewa huku mwanae akisikia kwamba mtoto akumbuke jina la Bwana na siku moja asaidie katika kuendeleza ukweli Wake. Kila fursa kwa ajili ya makuzi ya kimaadili na kiakili ambayo maisha yao ya kimaskini yalimudu kuwapatia ilitumiwa vizuri kwa furaha na wazazi hawa. Juhudi zao zilikuwa za dhati na zilizojali kuwaandaa watoto wao kwa ajili ya maisha yanayomcha Mungu na yenye manufaa maishani. Kwa uimara na nguvu ya tabia yao walitumia ukali mwingi kupita kiasi; lakini Mwanamatengenzo mwenyewe, japokuwa alifahamu kuwa walikosea, aliiona nidhamu yao kuwa ni ya kusifiwa zaidi kuliko kulaumiwa.PKSw 88.4

  Shuleni, ambako alipelekwa akiwa bado na umri mdogo, Luther alitendewa kwa ukali na hata ukatili. Umaskini wa wazazi wake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba alipokwenda shule iliyokuwa katika mji mwingine alilazimika kwa muda fulani kupata chakula kwa kuimba nyimbo kutoka mlango mmoja hadi mwingine, na mara kwa mara aliteseka kwa njaa. Mawazo dhaifu, ya kishirikina ya dini yaliyokuwepo wakati ule yalimjaza hofu. Mara kwa mara alilala usiku akiwa na moyo uliojazwa huzuni, akitazamia wakati ujao wenye giza huku akitetemeka na akiwa katika hofu ya kudumu inayotokana na wazo kuwa Mungu ni mkali, jaji asiyekuwa na huruma, na jitu katili, badala ya Baba wa mbinguni aliye mwema.PKSw 88.5

  Lakini chini ya mambo mengi na makubwa yanayokatisha tamaa Luther alisonga mbele kwa nguvu zaidi kuelekea kiwango cha juu cha ubora wa uadilifu na akili kilichovuta roho yake. Alikuwa na kiu kubwa ya maarifa, na tabia ya dhati na utendaji ya kitabia ya akili yake ilimwongoza kutamani kitu thabiti na chenye kina.PKSw 89.1

  Akiwa na umri wa miaka kumi na minane, alijiunga na Chuo Kikuu cha Erfurt, hali yake ilikuwa nzuri zaidi na mustakabali wake ulikuwa na matumaini makubwa kuliko katika miaka yake ya mwanzoni. Wazazi wake kwa mikono yao hodari ya kazi walipata uwezo mkubwa, waliweza kumpa msaada wote aliohitaji. Na mvuto wa marafiki wenye busara kwa kiasi fulani ulipunguza madhara ya uzoefu wake wa awali. Alisoma sana vitabu vya waandishi wazuri, akihifadhi kwa bidii mawazo yao muhimu na kufanya hekima ya watu wenye busara kuwa yake. Hata chini ya nidhamu kali ya wakufunzi wa awali tangu mwanzo alionesha dalili ya uwezo mkubwa, na chini ya mivuto mizuri akili yake ilikua haraka. Akili inayoshika, yenye tafakari kubwa, nguvu kubwa ya hoja, na matumizi yasiyochoka mara moja vilimfanya kuwa katika nafasi ya mbele miongoni mwa wenzake. Nidhamu ya kiakili ilikomaza uelewa wake na iliamsha utendaji wa akili na umakini wa ufahamu uliokuwa unamwandaa kwa ajili ya migogoro ya maisha yake.PKSw 89.2

  Hofu ya Mungu ilikaa ndani ya moyo wa Luther, ikimwezesha kudumisha uimara wake wa kusudi na kumwongoza kuwa na unyenyekevu mbele ya Mungu. Alikuwa na hitaji la kudumu la kutegemea msaada wa Mungu, na hakushindwa kuanza kila siku kwa maombi, wakati moyo wake ulikuwa daima ukipumua ombi kwa ajili ya mwongozo na msaada. “Kuomba vizuri,” alisema daima, “ni sehemu kubwa ya mafunzo.”—D'Aubigne, b. 2, ch. 2.PKSw 89.3

  Siku moja, wakati akisoma-soma vitabu katika maktaba ya chuo kikuu, Luther aligundua Biblia ya Kilatini. Kitabu kama hicho alikuwa hajakiona kabla. Alikuwa hata hajui kuwa kuna kitabu kama hicho. Alikuwa amesikia sehemu za Injili na Nyaraka, ambazo zilikuwa zimesomwa katika mikutano ya ibada za hadhara, na alidhani kuwa hizo ndizo zilikuwa Biblia yote. Sasa, kwa mara ya kwanza, aliliona Neno lote la Mungu. Akiwa na mchanganyiko wa kicho na mshangao alifungua kurasa zake; wakati mapigo ya moyo yakiongezeka kasi na huku akiwa anatetemeka, yeye mwenyewe alijisomea maneno ya uzima, akipumzika mara kwa mara na kutamka kwa mshangao: “Yaani Mungu anaweza kunipatia kitabu hiki!”—Ibid., b. 2, sura ya 2. Malaika wa mbinguni walikuwa kando yake, na miale ya nuru kutoka katika kiti cha enzi cha Mungu ilimfunulia hazina ya ukweli ili aweze kuelewa. Daima siku zote alikuwa mwoga wa kumkosea Mungu, lakini sasa usadikisho wa kina kuwa yeye ni mwenye dhambi ulimshika zaidi kuliko wakati wowote uliopita.PKSw 89.4

  Shauku ya dhati ya kuondokana na dhambi na kupata amani mbele za Mungu vilimwongoza kujiunga na nyumba ya watawa na kujiweka wakfu kwa ajili ya maisha ya utawa. Alitakiwa kufanya kazi za chini kabisa na kuwa omba omba nyumba kwa nyumba. Alikuwa katika umri ambao kwa kawaida heshima na kutambuliwa ndipo huhitajiwa sana, na kazi hizi dhalili zilimuaibisha sana kulingana na hisia zake; lakini kwa uvumilivu mkubwa alistahimili sana kunyenyekeshwa huko, akiamini kuwa ilikuwa lazima kwa sababu ya dhambi zake.PKSw 90.1

  Kila wakati alioweza kuupata baada ya kazi zake za kila siku aliutumia kusoma, akijinyima usingizi na akisikitika hata kwa muda alioutumia kula chakula chake kidogo sana. Kuliko vyote, Luther alifurahia kusoma neno la Mungu. Alikuwa ameona Biblia iliyokuwa imefungwa kwa mnyororo kwenye ukuta wa nyumba ya watawa, na alipenda kukaa hapo mara nyingi. Kwa kadiri alivyozidi kushawishika kuwa yeye ni mwenye dhambi, alizidi kutafuta kwa njia ya matendo yake mwenyewe kupata msamaha na amani. Aliishi maisha ya kujitesa sana, akijitahidi kwa kufunga, kukesha, na vipigo kudhibiti maovu katika silika yake, ambayo maisha ya utawa yalishindwa kumsaidia kuachana nayo. Hakusita kutoa kafara yo yote ambayo kwayo angeweza kupata usafi wa moyo ambao ungemwezesha kupata kibali mbele ya Mungu. “Hakika nilikuwa mtawa kamili,” alikuja kusema baadaye, “na nilifuata kanuni za maisha ya kitawa kikamilifu kuliko ninavyoweza kueleza. Ikiwa mtawa angeweza kupata mbingu kwa kazi za kitawa, hakika nilipaswa kuistahili.... Ikiwa ningeendelea zaidi, ningejitesa hadi kufa.”— Ibid., b. 2, sura 3. Kama matokeo ya udhibiti huu wenye maumivu makali aliishiwa nguvu na nyakati zingine alizimia, ambapo madhara yake hayakwisha kabisa katika maisha yake yote. Lakini pamoja na juhudi zake zote roho yake yenye mizigo haikupata nafuu yo yote. Hatimaye alifikia karibu kukata tamaa.PKSw 90.2

  Ilipoonekana kana kwamba mambo yote yalikuwa yameharibika, Mungu alimwinua rafiki na msaidizi kwa ajili yake. Mtu mwadilifu Staupitz alimfunulia Luther na alimwagiza aache kujiangalia, aache kutafakari juu ya adhabu ya milele kwa kuvunja sheria ya Mungu, na amwangalie Yesu, Mwokozi anayesamehe dhambi zake. “Badala ya kujitesa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zako, jitupe katika mikono ya Mkombozi. Mtegemee Yeye, tegemea haki ya maisha Yake, tegemea upatanisho wa kifo Chake.... Msikilize Mwana wa Mungu. Alifanyika mtu ili akupatie uhakika wa upendeleo wa Kimungu.” “Mpende Yeye aliyekupenda kwanza.”—Ibid., b. 2, ch. 4. Hivyo ndivyo alivyosema huyu mjumbe wa rehema. Maneno yake yaligusa sana akili ya Luther. Baada ya mapambano mengi dhidi ya makosa yaliyojengeka kwa muda mrefu, aliwezeshwa kuushika ukweli, na amani ikaja katika roho yake iliyokuwa ikisumbuka.PKSw 90.3

  Luther aliwekewa mikono ya upadiri na aliitwa atoke katika makazi ya watawa ili awe profesa katika Chuo Kikuu cha Wittenberg. Hapa alitumia muda mwingi kujifunza Maandiko katika lugha za asili. Alianza kutoa mihadhara juu ya Biblia; na kitabu cha Zaburi, Injili, na Nyaraka zilifunguliwa na kufafanuliwa kwa makundi ya wasikilizaji wenye kiu na furaha ya kusikiliza. Staupitz, rafiki yake na mkubwa wake, alimsihi sana apande mimbarani ili ahubiri neno la Mungu. Luther alisita-sita, akijihisi kutostahili kuzungumza na watu kwa niaba ya Kristo. Ilikuwa baada ya pambano refu ndipo alipokubali ushawishi wa rafiki zake. Tayari alikuwa ameshakuwa hodari katika Maandiko, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Ufasaha wake uliwateka wasikilizaji wake, uwazi na uwezo ambao uliandamana na mawasilisho yake ya ukweli ulishawishi uelewa wao, na umakini wake uligusa mioyo yao.PKSw 91.1

  Luther alikuwa bado mtoto halisi wa kanisa la upapa na hakuwa na wazo lolote kuwa angebadilika cho chote na kuwa mtu mwingine. Kwa uongozi wa Mungu alikwenda kutembelea Roma. Alienda safari hiyo kwa mguu, akiwa analala katika nyumba za watawa njiani. Katika nyumba moja ya watawa huko Italia alishangazwa kwa utajiri, fahari, na anasa alivyovishuhudia. Wakiwa na kipato cha juu, watawa waliishi katika nyumba za kifahari, wakivaa majoho ya kitajiri na yenye gharama kubwa, na walikula katika meza zilizojaa vyakula vya kila aina. Kwa uchungu mkubwa Luther alilinganisha mandhari hii na ile ya maisha yake ya kujikana nafsi na ugumu wa maisha yake. Akili yake ilianza kuingiwa na mashaka.PKSw 91.2

  Hatimaye aliona kwa mbali mji wenye vilima saba. Kwa hisia kubwa alianguka na kulala kifudifudi juu ya ardhi, akitamka kwa nguvu: “Mji Mtakatifu wa Roma, ninakusalimia!”—Ibid., b. 2, ch. 6. Aliingia mjini, alitembelea makanisa, alisikiliza maelezo ya ajabu yaliyotolewa na makasisi na watawa kwa kurudia-rudia, na alitekeleza kaida zote zilizotakiwa. Kila mahali aliona mandhari zilizomshangaza na kumjaza hofu. Aliona kuwa uovu ulijaa miongoni mwa matabaka yote ya viongozi wa kanisa. Alisikia mizaha michafu kutoka kwa maaskofu, na alijawa hofu kwa kuona kufuru zao za ajabu, hata katika misa. Alipojichanganya na watawa na wakazi alikutana na ubadhirifu na ufisadi. Kila mahali alipokwenda, iwe katika maeneo matakatifu alikutana na kufuru.” Hakuna awezaye kufikiria,“aliandika,“dhambi na mambo machafu yanayotendwa Roma; inapaswa yaonwe na yasikiwe ili yaaminiwe. Hivyo wamejenga tabia ambayo inaendana na msemo kuwa, ‘Ikiwa kuna jehanamu, Roma imejengwa juu yake: ni shimo ambalo linatapika kila aina ya dhambi.'”—Ibid., b. 2, ch. 6.PKSw 91.3

  Kutokana na amri iliyokuwa imetolewa karibuni cheti cha msamaha kilikuwa kimeahidiwa na papa kwa watu wote ambao wangeweza kupanda kwa magoti yao “Ngazi ya Pilato,” iliyosemwa kuwa Mwokozi wetu alitelemkia alipotoka katika ukumbi wa mahakama ya Kirumi na kuwa ngazi hiyo ilihamishwa kimiujiza kutoka Yerusalemu hadi Roma. Siku moja Luther kwa kicho cha dhati alikuwa akipanda ngazi hii, ambapo kwa ghafla sauti kama radi ilimwambia: “Mwenye haki ataishi kwa imani” (Warumi 1:17). Alisimama mara moja na kuondoka mahali pale kwa aibu na hofu. Kamwe, aya ile haikupoteza nguvu yake moyoni mwake. Tangu wakati ule alielewa wazi zaidi kuliko wakati wowote uliopita udanganyifu uliomo katika kutumainia matendo ya kibinadamu kwa ajili ya wokovu, na umuhimu wa imani ya kudumu katika rehema za Kristo. Macho yake yalifunguliwa, na yasingeweza kufungwa tena, yasibaini udanganyifu wa upapa. Alipogeuza uso wake kutoka Roma alikuwa amegeuza moyo wake pia kutoka Roma, na tangu wakati huo kujitenga kwake kulizidi kuwa kukubwa, hadi alipokata kabisa mshikamano wake na kanisa la kipapa.PKSw 92.1

  Baada ya kurudi kwake kutoka Roma, Luther alipokea kutoka Chuo Kikuu cha Wittenberg shahada ya uzamivu ya eliungu. Sasa alikuwa na uhuru wa kutumia muda wake mwingi, kuliko alivyoweza kufanya kabla ya hapo, kusoma Maandiko aliyoyapenda. Alikuwa ameapa kujifunza kwa uangalifu na kuhubiri kwa uaminifu neno la Mungu, siyo matamko na mafundisho ya mapapa, siku zote za maisha yake. Hakuwa tena mtawa au profesa tu, bali mjumbe wa Biblia mwenye mamlaka. Aliitwa kuwa mchungaji wa kuwalisha kondoo wa Mungu, ambao walikuwa na njaa na kiu kwa ajili ya ukweli. Alieleza kwa mkazo kuwa Wakristo hawapaswi kupokea mafundisho mengine zaidi ya yale yaliyojengwa juu ya mamlaka ya Maandiko Matakatifu. Maneno haya yaligonga kwenye msingi wa ukuu wa upapa. Yalikuwa na kanuni kuu za Matengenezo.PKSw 92.2

  Luther aliona hatari ya kuinua nadharia za kibinadamu juu ya neno la Mungu. Bila hofu alishambulia mafundisho ya uongo wa wasomi na alipinga falsafa na theolojia ambayo kwa muda mrefu ilikuwa na mvuto mkubwa juu ya watu. Aliyapinga mafundisho ambayo siyo tu kuwa hayakuwa na faida yo yote bali pia yalikuwa maovu, na alitafuta kugeuza akili za wasikilizaji wake kutoka kwa mafundisho ya uongo ya wanafalsafa na wanatheolojia na kuzielekeza kwa ukweli uliofundishwa na manabii na mitume.PKSw 92.3

  Ujumbe alioupeleka kwa makundi ya watu waliokuwa na shauku ya kusikiliza maneno yake ulikuwa wa thamani. Kabla ya hapo mafundisho kama hayo hayakuwahi kuingia katika masikio yao. Habari njema ya upendo wa Mwokozi, uhakika wa msamaha na amani kwa njia ya damu Yake ya upatanisho, vilifurahisha mioyo yao na vilihamasisha ndani yao tumaini la kudumu. Pale katika Chuo Kikuu cha Wittenberg nuru ilikuwa imewashwa ambayo miale yake ilikuwa inaenda kuenea mpaka sehemu za mwisho za dunia, na ambayo ilikuwa inaenda kuongezeka katika mwangaza wake hadi mwisho wa wakati.PKSw 92.4

  Lakini nuru na giza haviwezi kupatana. Kati ya ukweli na makosa kuna mgogoro usiosuluhishika. Kuinua na kutetea kimojawapo ni kushambulia na kushinda kingine. Mkombozi wetu Mwenyewe alitangaza: “Sikuja kuleta amani, bali upanga” (Mathayo 10:34). Alisema Luther, miaka michache baada ya kuanzisha Matengenezo: “Mungu haniongozi, ananisukuma kwenda mbele. Ananibeba na kunipeleka mbele. Mimi siyo mtawala wa nafsi yangu. Ninatamani kuishi kwa amani; lakini nimetupwa katikati ya misukosuko na mapinduzi.”—D'Aubigne, b. 5, ch. 2. Alikuwa sasa karibu kuingizwa katika mashindano.PKSw 93.1

  Kanisa la Rumi lilifanyia biashara neema ya Mungu. Meza za wabadilishao fedha (Mathayo 21:12) zilipangwa kando ya madhabahu zake, na hewa ilijazwa makelele ya wanunuzi na wauzaji. Kwa kisingizio cha kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Petro kule Roma, vyeti vya msamaha wa dhambi viliuzwa hadharani na mamlaka ya papa. Kwa gharama ya uhalifu hekalu lilipaswa lijengwe kwa ajili ya kumwabudu Mungu—jiwe kuu la pembeni liliwekwa kwa njia ya uovu! Lakini njia zile zile zilizotumiwa kwa ajili ya utukufu wa Roma zilichochea pigo dhidi ya nguvu na ukuu wake. Ni jambo hili hili ndilo lililochochea azimio na mafanikio ya maadui wa upapa, na ndilo lililosababisha vita iliyotikisa kiti cha enzi cha upapa na kukumba taji ya ngazi tatu juu ya kichwa cha papa.PKSw 93.2

  Afisa aliyeteuliwa kuuza vyeti vya msamaha katika nchi ya Ujermani— Tetzel kwa jina—alikuwa ametiwa hatiani kwa uhalifu dhalili kabisa dhidi ya jamii na kinyume na sheria ya Mungu; lakini baada ya kuponyoka kwenye adhabu kwa ajili ya uhalifu wake, alitumiwa kuendeleza zaidi miradi ya umamluki na ufisadi ya papa. Bila chembe ya aibu alisema kwa kurudia-rudia uongo mkubwa wa wazi na kusema maneno ya kuwadanganya wajinga, wasiojua kitu, na washirikina. Wangekuwa na neno la Mungu mioyoni mwao wasingedanganywa kwa njia hiyo. Ilikuwa ni kwa kusudi la kuwaweka daima chini ya utawala wa upapa, ili kulimbikiza madaraka na mali za viongozi wake wenye tamaa, ndiyo maana Biblia ilifichwa wasiweze kuiona. (Tazama John C. L. Gieseler, A Compendium of Ecclesiastical History, per. 4, sec. 1, par. 5.)PKSw 93.3

  Wakati Twetzel alipoingia mji fulani, mjumbe alimtangulia, na kutangaza: “Neema ya Mungu na ya baba mtakatifu iko malangoni mwako.”—D'Aubigne, b. 3, ch. 1. Na watu walimkaribisha msanii mwenye makufuru kana kwamba alikuwa Mungu Mwenyewe ambaye ameshuka kutoka mbainguni. Biashara haramu iliwekwa ndani ya kanisa, na Tetzel, akiwa madhabahuni, alisifia vyeti vya msamaha kuwa ndiyo zawadi ya thamani kutoka kwa Mungu kuliko zawadi zingine zote. Alitangaza kuwa kwa njia ya vyeti vyake vya msamaha dhambi zote ambazo mnunuzi wa vyeti angeweza baadaye kutamani kuzitenda angesamehewa, na kwamba “hata msamaha usingekuwa muhimu.”—Ibid., b. 3, ch. 1. Zaidi ya hapo, aliwahakikishia wasikilizaji wake kuwa vyeti vya msamaha vilikuwa na nguvu ya kuokoa siyo tu walio hai bali pia waliokufa; kwamba muda huo huo ambao fedha ingegusa sakafu ya sanduku lake, roho ambayo fedha ilikuwa imetolewa kwa ajili yake ingetoka mara moja katika purgatori na kuingia mbinguni. (Tazama K. R. Hagenbach, History of the Reformation, vol. 1, uk. 96.)PKSw 93.4

  Wakati Simoni Magusi alipotaka kununua nguvu ya kutenda miujiza kutoka kwa mitume, Petro alimjibu: “Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali” (Matendo 8:20). Lakini biashara ya Tetzel ilikumbatiwa na maelfu ya watu kwa shauku kubwa. Dhahabu na fedha ilitiririka na kuingia katika hazina yake. Wokovu uliopatikana kwa kununuliwa kwa fedha ulipatikana kirahisi zaidi kuliko wokovu unaohitaji toba, imani, na juhudi kubwa ya kupinga na kushinda dhambi. (Tazama maelezo katika Kiambatisho 59.)PKSw 94.1

  Fundisho la msamaha wa dhambi kwa njia ya vyeti limekuwa likipingwa na wasomi na wacha Mungu katika Kanisa la Roma, na watu wengi wamekuwepo ambao hawaamini mambo ya kuigiza yaliyo kinyume kabisa na busara ya kawaida na Maandiko Matakatifu. Hakuna askofu ye yote aliyethubutu kuinua sauti yake dhidi ya biashara hii haramu; lakini akili za watu zilikuwa zikisumbuliwa na kutaabishwa, na wengi waliomba kwa dhati ili Mungu alitakase kanisa Lake kwa njia fulani.PKSw 94.2

  Luther, japokuwa alikuwa bado ni muumini mwaminifu wa upapa, alijazwa na hofu kutokana na madai yenye kufuru ya wauzaji wa vyeti vya msamaha. Wengi wa waumini wa kanisa lake mwenyewe walikuwa wamenunua vyeti vya msamaha, na walianza kuja kwa mchungaji wao, wakiungama dhambi zao za aina mbalimbali, na walitarajia kutakaswa, siyo kwa sababu walikuwa wametubu na walitamani kufanya matengenezo, bali kwa msingi wa vyeti vya msamaha. Luther aliwanyima utakaso, na aliwaonya kuwa ikiwa hawatatubu na kutengeneza maisha yao, lazima wangeangamia katika dhambi zao. Kwa wasiwasi mkubwa walirudi kwa Tetzel wakiwa na malalamiko kuwa mwungamishaji wao alikataa vyeti vyake; na wengine kwa ujasiri walidai warudishiwe fedha yao. Mtawa alijazwa na ghadhabu. Alitamka maneno mazito ya laana ya kutisha, aliagiza moto uwashwe katika maeneo ya wazi, na alitangaza kuwa alikuwa “amepokea amri kutoka kwa papa kuwachoma moto wazushi wote waliojaribu kupinga vyeti vyake vya msamaha.”—D'Aubigne, b. 3, ch. 4.PKSw 94.3

  Luther sasa aliingia kwa ujasiri katika kazi yake kama shujaa wa ile kweli. Sauti yake ilisikika kutoka mimbarani ikitoa onyo kali na la dhati. Aliwaeleza watu uhalisia wa ubaya wa dhambi, na aliwafundisha kuwa haiwezekani mtu, kwa matendo yake mwenyewe, kupunguza hatia yake au kuepuka adhabu. Hakuna cho chote bali toba kwa Mungu na imani katika Kristo kinachoweza kumwokoa mwenye dhambi. Neema ya Kristo haiwezi kununuliwa; ni zawadi inayotolewa bure. Aliwashauri watu wasinunue vyeti vya msamaha, bali wamtazame kwa imani Mkombozi aliyesulubiwa. Alisimulia uzoefu wake binafsi wa maumivu alivyojaribu kupata wokovu kwa kujidhili na kujitesa bila mafanikio, na aliwahakikishia wasikilizaji wake kuwa ilikuwa kwa njia ya kutokujiangalia mwenyewe na kumwamini Kristo ndivyo vilimpatia amani na furaha.PKSw 94.4

  Kwa kadiri Tetzel alivyoendelea na biashara yake na maigizo yake machafu, Luther alidhamiria kuchukua hatua kubwa zaidi kupinga uonevu huu wa kutisha. Haikuchukua muda fursa ikajitokeza. Kanisa kuu la Wittenberg lilikuwa na mifupa mingi, ambayo katika siku fulani fulani takatifu ilioneshwa kwa watu, na msamaha kamili wa dhambi ulitolewa kwa wote waliotembelea kanisa lile na kuungama. Kwa hiyo katika siku hizo idadi kubwa ya watu walienda pale. Moja ya siku muhimu sana kama hizo, sikukuu ya Watakatifu Wote, ilikuwa imekaribia. Siku moja kabla, Luther, akiungana na makundi makubwa ya watu waliokuwa wakienda kuelekea kwenye kanisa lile, alibandika kwenye mlango wake karatasi iliyoandikwa matamko tisini na tano dhidi ya fundisho la vyeti vya msamaha. Alitangaza utayari wake wa kutetea matamko haya siku iliyofuata pale katika chuo kikuu, dhidi ya watu wote ambao wangeona vema kuyashambulia.PKSw 95.1

  Matamko yake yaliwavuta watu wote. Yalisomwa na kusomwa tena, na yalikaririwa na watu kila upande. Msisimko mkubwa uliibuka katika chuo kikuu na katika jiji zima. Kwa njia ya matamko hayo ilioneshwa kuwa mamlaka ya kutoa msamaha wa dhambi, na kufuta adhabu yake, haijawahi kutolewa kwa papa au kwa mwanadamu mwingine ye yote. Mpango mzima ulikuwa ni ulaghai mtupu,—ujanja wa kujipatia pesa kwa kucheza na imani za kishirikina za watu,—mbinu ya Shetani ya kuangamiza roho za wote wanaotumainia maigizo yake ya uongo. Ilioneshwa wazi pia kuwa injili ya Kristo ni hazina ya thamani ya kanisa, na kuwa neema ya Mungu, iliyofunuliwa ndani yake, imetolewa bure kwa wote wanaoitafuta kwa toba na imani.PKSw 95.2

  Matamko ya Luther yaliamsha mjadala; lakini hakuna aliyethubutu kusema cho chote. Maswali aliyoyaibua siku chache yalienea katika nchi yote ya Ujerumani, na ndani ya wiki chache yalikuwa yamesikika katika ulimwengu wote wa Kikristo. Wafuasi wengi waaminifu wa Kanisa la Roma, waliokuwa wameona na kuomboleza kwa ajili ya uovu uliokuwemo kanisani, lakini hawakujua jinsi ya kuuzuia usiendelee, waliyasoma matamko kwa furaha kubwa, wakiitambua sauti ya Mungu ndani ya matamko hayo. Walihisi kuwa Bwana alikuwa amenyosha mkono Wake kuzuia wimbi lililokuwa likipanuka kwa kasi la ufisadi uliokuwa ukitokea katika ofisi ya upapa wa Roma. Wafalme na mahakimu walifurahia kwa siri kuwa udhibiti ulikuwa umekuja juu ya mamlaka yenye kiburi iliyokataa haki ya kukata rufaa dhidi ya maamuzi yake.PKSw 95.3

  Lakini watu wengi waliopenda dhambi na ushirikina waliogopeshwa wakati imani za uongo zilizowafariji na kuwaondolea hofu zao zilipofagiliwa mbali kwa matamko ya Luther. Makasisi wajanja, kwa kuingiliwa katika kazi yao ya kuhalalisha uhalifu, na kwa kuona kuwa mapato yao yalikuwa hatarini, walighadhibika sana, na walicharuka kutetea ulaghai wao. Mwanamatengenezo alikabiliana na washitaki wao. Baadhi walimshitaki kwa kwenda haraka na kufanya kazi kwa mihemko. Wengine walimshitaki kwa kiburi, wakidai kuwa hakuongozwa na Mungu, bali alifanya kazi kwa kiburi na majivuno. “Nani hajui,” alijibu, “kuwa mtu mara chache hatoi mawazo mapya bila kuwa na mwonekano wa kiburi, na bila kushitakiwa kwa kuamsha migogoro? ... Kwa nini Kristo na wafia dini wote waliuawa? Kwa sababu walionekana kuwa wapinzani wenye kiburi dhidi ya hekima ya wakati wao, na kwa sababu walisimamia mawazo mapya bila kunyenyekea na kupata ushauri wa hekima na maoni ya wazee wa zamani.”PKSw 96.1

  Alisema tena: “Chochote ninachokifanya kitafanyika, siyo kwa busara ya kibinadamu, bali kwa uongozi wa Mungu. Ikiwa kazi ni ya Mungu, ni nani ataisimamisha? Ikiwa siyo kazi Yake, ni nani anaweza kuiendeleza mbele? Siyo mapenzi yangu, wala siyo mapenzi yao, wala mapenzi yetu; lakini mapenzi Yako, Ee Baba Mtakatifu, uliye mbinguni.”—Ibid., b. 3, ch. 6.PKSw 96.2

  Ingawa Luther aliongozwa na Roho wa Mungu kuanza kazi yake, asingeendelea nayo bila kukabiliana na migogoro mikubwa. Kejeli za maadui zake, tafsiri potofu za makusudi yake, na maelezo ya uchonganishi kuhusu tabia na nia yake, vilimwangukia kama mafuriko ya maji mengi; na mambo hayo yalikuwa na madhara. Alikuwa na ujasiri wa kuamini kuwa viongozi wa watu, katika kanisa na mashuleni, wangeungana naye kwa furaha katika juhudi za kufanya matengenezo. Maneno ya kutia moyo kutoka kwa watu waliokuwa katika nafasi za juu yalimtia moyo kwa furaha na kumpatia matumaini. Kwa matazamio tayari alikuwa ameona siku njema ikianza kupambazuka kwa ajili ya kanisa. Lakini kutiwa moyo kulibadilika kukaja kukejeliwa na kulaumiwa. Waheshimiwa wengi, wa kanisa na dola, waliguswa na ukweli wa matamko haya; lakini wakagundua mara moja kuwa kukubali kweli hizi kungeleta mabadiliko makubwa. Kuwaeleza watu ukweli na kufanya matengenezo kungedhoofisha mamlaka ya Roma kwa kiasi kikubwa, na kungefunga maelfu ya mifereji iliyotiririshia maji yake katika hazina yake, na hivyo kukata kwa kiasi kikubwa ufujaji wa pesa na anasa za viongozi wa upapa. Zaidi ya hapo, kuwafundisha watu kufikiri na kutenda kama viumbe wanaowajibika, wakimwangalia Kristo pekee kwa ajili ya wokovu, wangepindua kiti cha enzi cha papa na hatimaye kuondoa mamlaka yao wenyewe. Kwa sababu hii walikataa ujumbe waliopewa kutoka kwa Mungu na wakajipanga dhidi ya Kristo na ukweli kwa upinzani wao dhidi ya mtu ambaye Mungu alimtuma kuwaangazia.PKSw 96.3

  Luther alipojiangalia mwenyewe alitetemeka—mtu mmoja akisimama kinyume dhidi ya mamlaka kuu kabisa za ulimwengu. Nyakati zingine aliingiwa na mashaka ikiwa kweli aliongozwa na Mungu kusimama dhidi ya mamlaka ya kanisa. “Mimi nilikuwa nani,” aliandika, “kupingana na mheshimiwa papa, ambaye... wafalme wa dunia na watu wote ulimwenguni kote walitetemeka mbele yake? ... Hakuna mtu hata mmoja awezaye kujua mateso ambayo moyo wangu uliyapata katika hii miaka miwili ya kwanza, na ninaweza kusema, ukataji tamaa, uvunjikaji moyo ulionipata.”—Ibid., b. 3, ch. 6. Lakini hakuachwa akate tamaa kabisa. Wakati msaada wa kibinadamu ulipokosekana, alimwangalia Mungu pekee na alijifunza kuwa angeweza kutegemea kikamilifu na kuwa salama juu ya mkono wenye nguvu zote.PKSw 97.1

  Kwa rafiki wa Matengenezo Luther aliandika: “Hatuwezi kuelewa Maandiko ama kwa kujifunza au kwa akili. Wajibu wako wa kwanza ni kuanza kwa maombi. Msihi Bwana akupatie, rehema zake kubwa, uelewa wa kweli wa neno Lake. Hakuna mfasiri mwingine wa neno la Mungu zaidi ya Mwasisi wa neno la Mungu, kama alivyosema Mwenyewe, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Usitumainie kabisa kazi zako mwenyewe, kutoka kwa uelewa wako mwenyewe binafsi: mtumainie Mungu pekee, na katika mvuto wa Roho Mtakatifu. Amini hili kwa sababu ya neno la mtu ambaye amewahi kupata uzoefu.”—Ibid., b. 3, ch. 7. Hapa kuna somo muhimu sana kwa wale wanaohisi kuwa Mungu amewaita kuwapelekea wengine kweli muhimu kwa ajili ya wakati huu. Kweli hizi zitaamsha uadui wa Shetani na wa watu wanaopenda hadithi za uongo ambazo zimebuniwa na Shetani. Katika pambano dhidi ya nguvu za uovu kuna hitaji la jambo fulani muhimu kuliko nguvu za akili na hekima za kibinadamu.PKSw 97.2

  Wakati adui walipotumainia desturi na mapokeo, au walipotegemea madai na mamlaka ya papa, Luther alikabiliana nao kwa kutumia Biblia na Biblia pekee. Hapa kulikuwa na maswali ambayo wasingeweza kuyajibu; kwa hiyo watumwa wa mazoea na ushirikina walitamani damu yake, kama Wayahudi walivyokuwa na kiu ya damu ya Kristo. “Ni mzushi,” walipiga kelele wakereketwa wa Kanisa la Kiroma. “Ni uhaini dhidi ya kanisa kuruhusu mzushi wa kutisha kama huyu kuishi hata saa moja zaidi. Hebu jukwaa la kunyongea wahalifu lijengwe haraka kwa ajili yake!”—Ibid., b. 3, ch. 9. Lakini Luther hakuweza kuwa mhanga wa ghadhabu yao. Mungu alikuwa bado ana kazi ambayo alitaka Luther aifanye, na malaika wa mbinguni walitumwa kumlinda. Hata hivyo, wengi, ambao walikuwa wamepokea nuru ya thamani kutoka kwa Luther walifanywa kuwa lengo la ghadhabu ya Shetani na kwa ajili ya ukweli waliteswa na kuuawa.PKSw 97.3

  Mafundisho ya Luther yalivuta usikivu wa akili zenye tafakari katika nchi yote ya Ujerumani. Kutoka katika mahubiri na machapisho yake miale ya nuru iliangazia na kuamsha maelfu ya watu. Imani hai ilikuwa inachukua nafasi ya mazoea mafu ambayo kanisa lilikuwa limeghubikwa ndani yake. Watu walikuwa wakipoteza imani katika ushirikina wa Uroma. Vizuizi vya chuki zisizokuwa na sababu vilikuwa vikiyeyuka. Neno la Mungu, ambalo kwalo Luther alipima kila fundisho na kila dai, lilikuwa kama upanga unaokata kuwili, likikata njia yake na kufikia mioyo ya watu. Kila mahali kulikuwepo maendeleo ya kiroho. Kila mahali kulikuwepo njaa na kiu ya haki kuliko ilivyowahi kutokea miaka mingi kabla ya hapo. Macho ya watu, ambayo kwa muda mrefu yalielekezwa kwa kaida za kibinadamu na wapatanishaji wa kidunia, walikuwa sasa wakigeukia toba na imani katika Kristo na Yeye aliyesulubiwa.PKSw 98.1

  Shauku hii kubwa iliyoenea sana iliamsha zaidi hofu za mamlaka za upapa. Luther alipokea wito wa mahakama ukimtaka aende Roma kujibu mashtaka ya uzushi. Wito huu ulijaza hofu mioyoni mwa marafiki zake. Walijua vizuri hatari iliyomkabili katika jiji lile la kifisadi, ambalo tayari lilikuwa limeshalewa damu ya mashahidi wa Yesu. Walipinga kwenda kwake Roma na kuomba ahojiwe akiwa nchini Ujerumani.PKSw 98.2

  Mpango huu hatimaye ulitekelezwa, na mwakilishi wa papa aliteuliwa asikilize kesi hii. Katika maelekezo yaliyoletwa na papa kwa ofisa huyu, ilielezwa kuwa Luther alikuwa ameshatangazwa tayari kuwa mzushi. Hivyo basi, mwakilishi huyu alikuwa ameagizwa, “kumshitaki na kumzuia mara moja.” Ikiwa angedumu kuwa na msimamo wake, na mwakilishi akishindwa kumkamata, alipewa mamlaka ya“kumpiga marufuku asionekane katika nchi yote ya Ujerumani; kumfukuza, kumlaani, na kuwafuta ushirika watu wote walioshikamana naye.”— Ibid., b. 4, ch. 2. Na, zaidi ya hapo, papa alimwelekeza mwakilishi wake, ili kung'oa kabisa ugonjwa wa uzushi, kuwafuta ushirika wa kanisa wote, hata kama wana hadhi kubwa kiasi gani katika kanisa au serikali, isipokuwa mfalme, watakaopuuza kumkamata Luther na wafuasi wake, na kuwapatiliza kisasi cha Roma.PKSw 98.3

  Hapa pameoneshwa roho halisi ya upapa. Hakuna hata chembe ya kanuni ya Ukristo, au hata haki tu ya kawaida, haiwezi kuonekana katika waraka wote. Luther alikuwa umbali mkubwa kutoka Roma; hakuna na fursa ya kujieleza au kutetea msimamo wake; lakini kabla ya kesi yake kusikilizwa, alitangazwa kuwa mzushi moja kwa moja, na katika siku hiyo hiyo, alishauriwa, alishitakiwa, alihukumiwa, na alipewa adhabu; na haya yote yakifanywa na baba mtakatifu wa kujiweka mwenyewe, mamlaka iliyo kuu, isiyokosea katika kanisa au dola!PKSw 98.4

  Wakati huu, Luther alipohitaji sana huruma na ushauri wa rafiki wa kweli, Mungu katika Majaliwa yake alimtuma Melanchthon aende Wittenberg. Akiwa kijana kiumri, mpole na mtulivu, busara za Melanchthon, ujuzi wake mwingi, na umbuji usio na mshindani, vikichanganywa na usafi na uadilifu wa tabia yake, vilimfanya apate kibali na heshima machoni pa watu wote. Uwezo wa talanta zake haukuwa wa wazi sana zaidi ya uungwana na utu wake. Ghafla alitokea kuwa mwanafunzi mzuri wa injili, na rafiki mwaminifu na msaadizi wa Luther mwenye thamani kubwa; uungwana wake, tahadhari, na usahihi vikitumika kama nyongeza kwa ujasiri na nguvu ya Luther. Muungano wao katika kazi uliongeza nguvu katika Matengenezo na ilikuwa chanzo kikubwa cha hamasa kwa Luther.PKSw 98.5

  Mji wa Augsburg ulikuwa umechaguliwa kuwa mahali pa mahakama, na Mwanamatengenezo alisafiri kwa miguu kwenda huko. Hofu kubwa ilijengeka kwa ajili yake. Vitisho vilikuwa vimetangazwa wazi wazi kuwa angekamatwa na kuuawa akiwa njiani, na marafiki zake walimwomba asiende huko. Hata walimsihi aondoke Wittenberg kwa muda na kutafuta hifadhi na wale ambao wangefurahia kumlinda. Lakini hakutaka kuondoka mahali ambapo Mungu alikuwa amemweka. Ilimpasa aendelee kudumisha kwa uaminifu ukweli, licha ya dhoruba zilizokuwa zikimpiga. Lugha yake ilikuwa: “Mimi ni kama Yeremia, mtu wa migogoro na malumbano; lakini vitisho vyao vinapoongezeka, ndivyo furaha yangu inavyoongezeka.... Tayari wameshanivunjia heshima na kuniharibia sifa. Jambo moja tu limebaki; ni mwili wangu dhaifu: acheni tu wauchukue; kwa kufanya hivyo watafupisha maisha yangu kwa saa chache tu. Lakini kadiri roho yangu inavyohusika, hawawezi kuichukua kamwe. Yeyote anayetamani kutangaza neno la Mungu ulimwenguni, inampasa kutegemea kifo kila wakati.”—Ibid., b. 4, ch. 4.PKSw 99.1

  Habari za kufika kwa Luther jijini Augsburg kulimpa mwakilishi wa papa kuridhika kukubwa. Mzushi msumbufu aliyekuwa akiteka usikivu wa ulimwengu wote alionekana sasa kuwa katika mamlaka ya Roma, na mwakilishi wa papa aliazimia kuwa asiweze kuponyoka kutoka katika mikono yake. Mwanamatengenezo hakuwa na cheti cha uhakika wa usalama wake. Marafiki zake walimsihi asiende mbele ya mwakilishi wa papa bila cheti cha uhakika wa usalama wake, na wao wenyewe walikusudia kuwa wamtafutie cheti hicho kutoka kwa mfalme. Mwakilishi wa papa alikusudia kumlazimisha Luther, ikiwezekana, akanushe mafundisho yake, la sivyo asipokanusha, afanye mpango wa kumpeleka Roma, akakutane na yaliyowakuta akina Huss na Jerome. Hivyo basi, kwa njia ya mawakala wake alijitahidi kumshawishi Luther aje kwake bila cheti maalumu cha uhakika wa usalama, akimwahidi kuwa hatamfanyia madhara yo yote. Mwanamatengenezo alikataa kufanya hivyo. Ni mpaka pale alipopata waraka uliomwahidi ulinzi wa mfalme, ndipo alipotokea mbele ya mwakilishi wa papa.PKSw 99.2

  Kama suala la kisera, viongozi wa kanisa la Roma waliamua kujaribu kumshawishi Luther kwa mwonekano wa uungwana. Mwakilishi wa papa, katika mahojiano na Luther, alijifanya kuonesha urafiki mkubwa; lakini alidai kuwa Luther ajisalimishe kabisa kwa mamlaka ya kanisa, na asalimishe kila kipengele bila ubishi au swali. Hakuwa amejua kiwango cha tabia ya mtu aliyekuwa akishughulika naye. Luther, katika kujibu, alieleza heshima aliyokuwa nayo kwa hakika, shauku yake kwa ajili ya ukweli, utayari wake wa kujibu hoja zote zinazopingana na kile ambacho alikuwa amekifundisha, na kusalimisha mafundisho yake kwa uamuzi wa baadhi ya vyuo vikuu mashuhuri. Lakini wakati huo huo alipinga wazo la kadinali la kumtaka akanushe mafundisho yake bila kumwonesha makosa yake. Jibu pekee lilikuwa: “Kanusha, kanusha!” Mwanamatengenezo alisema kuwa msimamo wake ulikuwa umejengwa juu ya Maandiko na alieleza kwa mkazo kuwa asingeweza kukanusha ukweli. Mwakilishi wa papa, kwa kushindwa kujibu hoja za Luther, alimshambulia kwa dhoruba ya kejeli, mizaha, na sifa za uongo, na huku akiingiza dondoo kutoka katika mapokeo na misemo ya Mababa, bila kumpa Mwana matengenezo nafasi ya kusema. Baada ya kuona kuwa mkutano, kama ungeendelea vile, asingefanikiwa kusudi lake, hatimaye Luther alipata ruhusa ya kuwasilisha jibu lake kwa maandishi. “Kwa kufanya hivyo,” alisema, akimwandikia rafiki yake, “wanaokandamizwa wanapata faida mbili; kwanza, kilichoandikwa kinaweza kuhukumiwa na wengine; na pili, mtu ana nafasi nzuri zaidi ya kushughulikia hofu, siyo katika dhamiri ya mtu katili mwenye kiburi na mpayukaji, anayeshinda kwa lugha yake ya kiimla.”—Martyn, The Life and Times of Luther, kurasa 271, 272.PKSw 100.1

  Katika mahojiano yaliyofuata, Luther aliwasilisha maelezo ya wazi, mafupi, na yenye nguvu ya maoni yake, yakiwa yamesheheni dondoo nyingi za Maandiko. Baada ya kulisoma kabrasha hilo kwa sauti, alimpatia kadinali, ambaye, hata hivyo, kwa dharau alilitupa pembeni, akisema kuwa lilijaa maneno ya upuuzi na dondoo zisizohusika. Luther, akiwa ameamshwa kikamilifu, sasa alimkabili kasisi mwenye kiburi pale pale—mapokeo na mafundisho ya kanisa—na kushinda madai yake yote.PKSw 100.2

  Kadinali alipoona kuwa hoja za Luther haziwezi kujibiwa, alishindwa kujizuia kabisa, na kwa ghadhabu kubwa alipiga kelele: “Kanusha! au nitakupeleka Roma, ili utokee mbele ya majaji waliotumwa wasikilize suala lako. Nitakuondoa katika ushirika wa kanisa na wafuasi wako wote, na wale wote ambao wakati wowote watakuona, na tutawatupa nje ya kanisa.” Na mwishoni alitangaza, kwa sauti ya kiburi na hasira: “Kanusha, au usirudi tena.”—D'Aubigne, London ed., b. 4, ch. 8.PKSw 100.3

  Mwanamatengenezo na marafiki zake waliondoka, na kwa njia hiyo walitangaza wazi kuwa hakuna kukanusha ambako kungetegemewa kutoka kwake. Hili siyo jambo ambalo kadinali alikusudia. Alikuwa amejidanganya kuwa kwa kutumia ukatili angeweza kumfanya Luther ajisalimishe. Sasa, akiwa ameachwa peke yake na wasaidizi wake, alimwangalia mtu mmoja mmoja akiwa na hasira kali kutokana na kushindwa kwa hila zake ambako hakukutegemea.PKSw 100.4

  Juhudi za Luther katika tukio hili hazikwenda bila matokeo mazuri. Umati mkubwa wa watu waliokuwepo pale walipata fursa ya kuwalinganisha watu hawa wawili, na kuamua wenyewe kuhusu roho iliyooneshwa na watu hao wawili, ikiwa ni pamoja na nguvu na ukweli wa nafasi zao. Tofauti kati yao ilikuwa kubwa sana! Mwanamatengenezo, sahili, mnyenyekevu, imara, alisimama katika nguvu ya Mungu, akiwa na ukweli kando yake; mwakilishi wa papa, mwenye majivuno, katili, mwenye kiburi, na asiyekuwa na busara, hakuwa na hoja hata moja kutoka katika Maandiko, lakini kwa hasira alipiga kelele akisema: “Kanusha, la sivyo upelekwe Roma uadhibiwe.”PKSw 101.1

  Pamoja na kuwa Luther alikuwa amepewa cheti cha hakikisho la usalama, viongozi wa kanisa la Roma walikuwa wakipanga kumkamata na kumweka gerezani. Marafiki zake walisisitiza kuwa ilikuwa siyo salama kuendelea kukaa kule, alipaswa kurudi Wittenberg bila kukawia, na kuwa tahadhari kubwa ingechukuliwa ili kuficha makusudi yake. Kwa kuzingatia hayo aliondoka Augsburg alfajiri, kwa punda, akiwa na mwongoza njia aliyepewa na hakimu. Kwa hofu kubwa aliondoka gizani akipita katika mitaa ya jiji iliyokuwa kimya. Maadui, wakiwa macho na katili, walikuwa wakipanga jinsi ya kumwangamiza. Je, angeweza kuepuka mitego iliyotegwa kwa ajili yake? Hizo zilikuwa nyakati za wasiwasi na maombi ya dhati. Alifika kwenye lango dogo la ukuta wa jiji. Lilifunguliwa na mwongoza njia kwa ajili yake, na akiwa na mwongozaji wake aliweza kupita bila kikwazo. Walipofaulu kutoka salama, wakimbizi waliongeza kasi ya mwendo wao, na kabla mwakilishi wa papa hajajua kuwa Luther ameondoka, alikuwa ameshakwenda ng'ambo ya uwezekano wa kukamatwa na watesaji wake. Shetani na vibaraka wake walikuwa wameshindwa. Mtu ambaye walifikiri kuwa alikuwa katika uwezo wao alikuwa ameondoka, aliponyoka kama ndege anavyoponyoka kutoka katika mtego wa mtegaji.PKSw 101.2

  Baada ya kupokea taarifa za kuondoka kwa Luther, mwakilishi wa papa alishangaa na kukasirika sana. Alitarajia kuwa angepata heshima kubwa kwa hekima yake na uimara wake katika kumshughulikia huyu msumbufu wa kanisa; lakini tumaini lake lilikuwa limepotea. Alionesha hasira yake katika barua aliyomwandikia Frederiko, aliyekuwa mtawala wa jimbo la Saxony, kwa uchungu akimshtumu Luther na akimwamuru Frederiko ampeleke Mwanamatengenezo Roma au afukuzwe Saxony.PKSw 101.3

  Katika kujitetea, Luther alisihi kuwa mwakilishi wa papa amwoneshe makosa katika Maandiko, na aliapa kwa nguvu kuwa angekanusha mafundisho yake kama angeoneshwa mahali yanapopingana na neno la Mungu. Na alieleza shukurani zake kwa Mungu kuwa alistahili kuteswa kwa ajili ya kazi takatifu. Mtawala wa Saxony, mpaka wakati ule, alikuwa na ufahamu mdogo wa mafundisho ya Mwanamatengenezo, lakini aliguswa sana na uwazi, nguvu, na ufasaha wa maneno ya Luther; na mpaka Mwanamatengenezo aonekane kuwa na makosa, Frederiko aliamua kusimama kama mlinzi wa wake. Katika kujibu madai ya mwakilishi wa papa aliandika: “Kwa kuwa Dkt. Martin amesimama mbele yake huko Augsburg, unapaswa kuridhika. Hatukutarajia ujaribu kumtaka akane mafundisho yake bila kwanza kumwonesha makosa yake. Hakuna mtu msomi katika eneo letu la utawala ambaye ameniambia kuwa mafundisho ya Martin ni maovu, yanapinga Ukristo, au yana uzushi.’ Elekta wa Saxony alikataa pia kumpeleka Luther Roma, au kumfukuza kutoka katika majimbo yake.”—D'Aubigne, b. 4, ch. 10.PKSw 101.4

  Elekta aliona kuwa kulikuwa na uvunjifu wa jumla wa kanuni za kimaadili za jamii. Kazi kubwa ya matengenezo ilihitajika. Michakato tata na ya gharama ya kusimamia na kuadhibu uhalifu isingekuwa ya muhimu ikiwa watu wangeyatii matakwa ya Mungu na maagizo Yake kwa dhamiri iliyoangaziwa. Aliona kuwa Luther alikuwa akifanya kazi ili kutimiza lengo hili, na kwa siri alifurahia kuona kuwa mvuto bora zaidi ulikuwa ukijitokeza ndani ya kanisa.PKSw 102.1

  Aliona pia kuwa profesa katika chuo kikuu Luther alikuwa amefanikiwa sana. Mwaka mmoja pekee ulikuwa umepita tangu Mwanamatengenezo alipobandika matamko yake kwenye mlango wa kanisa, hata hivyo kulikuwa tayari na kupungua kukubwa kwa idadi ya mahujaji waliotembelea kanisa wakati wa siku kuu ya Watakatifu Wote. Roma ilikuwa imenyimwa waabuduji na sadaka, lakini mahali pake palijazwa na tabaka jingine, la watu waliokuja Wittenberg, siyo mahujaji waliokuja kuabudu mifupa yake, bali wanafunzi waliokuja kujaza kumbi zake za kujifunzia. Maandishi ya Luther yalikuwa yameasha shauku mpya katika Maandiko Matakatifu, na siyo tu kutoka sehemu zote za Ujerumani, bali pia kutoka katika nchi zingine, wanafunzi walifurika katika chuo kikuu. Vijana, walioliona jiji la Wittenberg kwa mara ya kwanza, “waliinua mikono yao mbinguni, na walimtukuza Mungu kwa kuwezesha nuru iangaze kutoka katika jiji lile, kama ilivyomulika kutoka Sayuni ya nyakati za kale, na kutokea hapo ilisambaa hadi nchi za mbali.”— Ibid., b. 4, ch. 10.PKSw 102.2

  Luther alikuwa bado ameongoka nusu kutoka katika makosa ya Uroma. Lakini alivyolinganisha Maandiko Matakatifu na amri na katiba za upapa, alijazwa na mshangao. “Ninasoma,” aliandika, “amri za mapapa, na ... sijui ikiwa papa ni mpinga Kristo mwenyewe, au mtume wake, kwa kuwa Kristo amewakilishwa vibaya na kusulubishwa sana ndani yao.”—Ibid., b. 5, ch. 1. Hata hivyo kwa wakati huo Luther alikuwa bado anaunga mkono Kanisa la Roma, na hakuwa na wazo lo lote kuwa angejitenga na ushirika wake. Maandishi ya Mwanamatengenezo na mafundisho yake yalikuwa yakienea katika kila taifa la Kikristo. Kazi yake iliendelea katika nchi za Uswisi na Uholanzi. Nakala za maandishi yake zilifika Ufaransa na Uhispania. Katika nchi ya uingereza mafundisho yake yalipokelewa kama maneno ya uzima. Ukweli ulifika pia Ubeligiji na Italia. Maelfu ya watu waliamshwa kutoka katika usingizi wa kiroho na kuingizwa katika furaha na matumaini ya maisha ya imani.PKSw 102.3

  Roma ilizidi kuudhiwa zaidi na zaidi kwa mashambulio ya Luther, na ilitangazwa na baadhi ya wapinzani wake wakereketwa, hata na baadhi ya wasomi katika vyuo vikuu vya Kikatoliki, kuwa ye yote ambaye angemwua huyo mtawa angekuwa hana dhambi. Siku moja mgeni, akiwa na bastola iliyofichwa katika joho lake, alimkaribia Mwanamatengenezo na kumwuliza kwa nini alitembea peke yake. “Niko katika mikono ya Mungu,” Luther alijibu. “Yeye ni nguvu na ngao yangu. Mwanadamu ataweza kunifanya nini?”— Ibid., b. 6, ch. 2. Alipoyasikia maneno hayo, mgeni alibadilika sura na kuwa mweupe na akakimbia kutoka mbele ya uwepo wa malaika wa mbinguni.PKSw 103.1

  Roma ilikuwa imejielekeza kumwua Luther; lakini Mungu alikuwa ulinzi wake. Mafundisho yake yalisikika kila mahali—“katika nyumba za wananchi na katika nyumba za watawa, ... katika majumba ya wakuu, katika vyuo vikuu, na katika majumba ya wafalme;” na watu waungwana walikuwa wakitokea kila upande kuunga mkono juhudi zake.—Ibid., b. 6,ch. 2.PKSw 103.2

  Ilikuwa karibu na wakati huu ambapo Luther, kwa kusoma maandishi ya Huss, aligundua kuwa ukweli mkuu wa kuhesabiwa haki kwa imani, ambao yeye mwenyewe alikuwa akiupigania na kuufundisha, ulikuwa ukiaminiwa na kufundishwa na Mwanamatengenezo wa Bohemia. “Sisi sote,” alisema Luther, “Paulo, Agustino, na mimi mwenyewe, tumekuwa wafuasi wa Huss bila kujua !” “Hakika Mungu atauwajibisha ulimwengu kwa ujumbe huu,” aliendelea kusema, “kwamba ukweli ulihubiriwa ulimwenguni karne moja iliyopita, na kuchomwa moto!”—Wylie, b. 6, ch. 1PKSw 103.3

  Katika wito kwa mfalme na kwa wakuu wengine katika ufalme wa Ujerumani kwa niaba ya matengenezo ya Ukristo, Luther aliandika kuhusiana na upapa: “Ni jambo la kutisha kumwona mtu anayejiita mwenyewe mwakilishi wa Kristo, akionekana kuwa na utukufu ambao hakuna mfalme mwingine anayelingana naye. Je, huku ndiko sawa na Yesu maskini, au Petro mnyenyekevu? Wanasema yeye ni bwana wa ulimwengu! Lakini Kristo, ambaye anadai kumwakilisha, alisema, ‘Ufalme wangu si wa ulimwengu huu.’ Je, eneo la utawala wa mwakilishi linazidi la mkubwa wake?”—D'Aubigne, b. 6, ch. 3.PKSw 103.4

  Aliandika ifuatavyo kuhusu vyuo vikuu: “Ninaogopa kuwa vyuo vikuu vinaweza kuwa malango makuu ya jehanamu, visipofanya kazi kwa bidii kueleza Maandiko Matakatifu, na kuyaweka katika mioyo ya vijana. Ninashauri mtoto asipelekwe mahali ambapo Maandiko hayapewi kipaumbele. Kila taasisi ambapo watu hawajishughulishi daima kujifunza neno la Mungu lazima ufisadi utatawala.”—Ibid., b. 6, ch. 3.PKSw 103.5

  Wito huu ulisambazwa haraka katika nchi nzima ya Ujerumani na kuleta mvuto mkubwa kwa watu. Taifa zima lilitikiswa, na watu wengi waliamshwa na kuunga mkono bendera ya matengenezo. Wapinzani wa Luther, wakiwaka shauku ya kulipiza kisasi, walimsihi sana papa achukue hatua za haraza na kali dhidi yake. Iliamuriwa kuwa mafundisho yake yapigwe marufuku mara moja. Siku sitini zilitolewa kwa Mwanamatengenezo na wafuasi wake, ambapo baada ya siku hizo, ikiwa wasingekana mafundisho yake, wote wangeondolewa katika ushirika wa kanisa.PKSw 104.1

  Hilo lilikuwa janga kwa Matengenezo. Kwa karne nyingi hukumu ya Roma ya kufutwa ushirika wa kanisa ilileta hofu kwa wafalme wenye nguvu; ilijaza uchungu na ukiwa katika himaya kuu ulimwenguni. Wale ambao walikumbwa na hukumu hiyo waliangaliwa na watu wote kwa hofu na simanzi; walikatazwa kuongea na marafiki zao na walichukuliwa kama watu waliolaaniwa, na walipaswa kuwindwa na kuuawa. Luther hakuwa kipofu wa kuona dhoruba iliyokuwa karibu kumpasukia; lakini alisimama imara, akimtegemea Kristo kama msaada na ngao yake. Akiwa na imani na ujasiri wa mfia dini aliandika: “Kinachoenda kutokea sikijui, wala sihitaji kukijua.... Acha kinachokuja kije, sina hofu kabisa. Hakuna hata jani linaloanguka chini bila mapenzi ya Baba yetu. Ni kwa kiasi gani basi Mungu anatujali! Ni jambo dogo sana kufa kwa ajili ya Neno, kwa kuwa Neno aliyefanyika mwili Mwenyewe alikufa. Tukifa Naye, tutaishi pamoja Naye; na tukipitia kile alichopitia kabla yetu, tutakuwa mahali alipo na kuishi Naye milele na milele.”—Ibid., 3d London ed., Walther, 1840, b. 6, ch. 9.PKSw 104.2

  Wakati barua ya papa ilipomfikia Luther, alisema: “Ninaidharau na kuishambulia, kwa kuwa ni barua ovu, ya uongo.... Ni Kristo Mwenyewe anayeshutumiwa nayo.... Ninafurahia kupata maumivu kama haya kwa kazi njema kuliko zote. Tayari ninahisi uhuru zaidi moyoni mwangu; kwa kuwa hatimaye nimejua kuwa papa ni mpinga Kristo, na kuwa kiti chake cha enzi ni cha Shetani mwenyewe.”—D'Aubigne, b. 6, ch. 9.PKSw 104.3

  Hata hivyo amri ya Roma haikupita bure—ilileta madhara. Gereza, mateso, na upanga zilikuwa silaha zilizotumiwa kushinikiza utii. Watu dhaifu na washirikina walitetemeka mbele ya amri ya papa; na ingawa kulikuwa huruma kwa ajili ya Luther, wengi walihisi kuwa ilikuwa gharama kubwa mno kuhatarisha maisha katika vuguvugu la matengenezo. Kila kitu kilionesha kuwa kazi ya Mwanamatengenezo ilikuwa karibu kufungwa.PKSw 104.4

  Lakini Luther hakuwa na hofu bado. Roma ilikuwa imemwaga laana zake dhidi yake, na ulimwengu uliangalia kinachoendelea, wakitarajia bila shaka kuwa atauawa au atalazimishwa kujisalimisha. Lakini kwa nguvu ya kutisha alirusha hukumu juu ya kanisa na kutangaza hadharani azimio lake la kuliacha kanisa milele. Akiwa mbele ya umati wa wanafunzi madaktari, na wakazi wa matabaka yote Luther aliichoma barua ya papa, iliyokuwa na sheria za kanisa, maagizo, na maandishi mengine yaliyohalalisha mamlaka ya upapa. “Maadui zangu wameweza, kwa kuchoma vitabu vyangu,” alisema, “kudhuru kazi ya ukweli katika akili za watu wa kawaida, na kuangamiza roho zao; kwa sababu hiyo nimechoma vitabu vyao. Mgogoro mkubwa ulikuwa umeanza. Mpaka wakati huo nilikuwa nikishughulika na papa. Nilianza kazi hii katika jina la Mungu; itaisha bila mimi, na kwa nguvu zake.”—Ibid., b. 6, ch. 10.PKSw 104.5

  Luther alijibu shutuma za maadui zake ambapo walidai kuwa mwelekeo aliouchagua ulikuwa dhaifu, akisema: “Nani ajuaye ikiwa Mungu amenichagua na kuniita, na ikiwa hawapaswi kuliogopa hilo, kwa kunidhihaki, wanamdhihaki Mungu Mwenyewe? Musa alikuwa peke yake alipoondoka Misri; Eliya alikuwa peke yake katika utawala wa Mfalme Ahabu; Isaya peke yake katika mji wa Yerusalemu; Ezekieli pake yake Babeli.... Mungu hakuchagua nabii aliyekuwa kuhani mkuu au mtu ye yote mwingine mwenye cheo cha juu; bali alichagua watu wa chini na waliodharauliwa, ikiwa ni pamoja na mchungaji Amosi. Katika kila zama, watakatifu wamewakosoa wakuu, wafalme, maliwali, makuhani, na watu wenye hekima, kwa kuhatarisha maisha yao Sisemi kuwa mimi ni nabii; lakini nasema kuwa inawapasa kuogopa hasa kwa sababu niko peke yangu na wao ni wengi. Ni hakika na jambo hili, kuwa neno la Mungu liko pamoja na mimi, na kwamba haliko pamoja nao.”—Ibid., b. 6, ch. 10.PKSw 105.1

  Hata hivyo siyo kweli kuwa Luther hakuwa na pambano kubwa ndani ya moyo wake wakatiLuther alipotoa uamuzi wake wa kujitenga na kanisa. Ilikuwa ni karibu na wakati huu ambapo aliandika: “Ninahisi zaidi na zaidi kila siku jinsi ilivyo vigumu kwa mtu kuacha uelewa ambao ameujenga tangu utotoni. Ee, ni maumivu makubwa kiasi gani niliyapata kutokana na uhalisia huo, ingawa nilikuwa na Maandiko kando yangu, kujiridhisha kuwa nilipaswa kuthubutu kusimama peke yangu kinyume na papa, na kumtangaza hadharani kuwa ni mpinga Kristo! Mateso ya moyo wangu yamekuwa makubwa kiasi gani! Mara ngapi nimejiuliza kwa uchungu maswali ambayo wafuasi wa upapa wamekuwa wakiniuliza mara nyingi: ‘Wewe peke yako ndiye uliye na busara? Je, mtu mwingine ye yote anaweza kukosea? Je, itakuwaje, ikiwa, hata hivyo, ni wewe mwenyewe umekosea, na ambaye unawajumuisha wengine katika makosa yako, ambao wataangamia milele?’ ‘Ndivyo nilivyopigana na nafsi yangu na Shetani, mpaka Kristo, kwa maneno Yake yasiyokosea, yalipoimarisha moyo wangu dhidi ya mashaka haya.”—Martyn, kurasa 372, 373.PKSw 105.2

  Papa alimtishia Luther kuwa atamfuta ushirika wa kanisa ikiwa asingekana, na tishio lilikuwa sasa limetekelezwa. Amri mpya ilitokea, ikitangaza hatua ya mwisho ya kutengwa kwa Mwanamatengenezo kutoka katika Kanisa la Roma, ikimhukumu kuwa mtu aliyelaaniwa na Mbingu, na ikiwajumuisha katika hukumu hiyo watu wote ambao wangepokea mafundisho yake. Pambano kuu lilikuwa limeingiwa kikamilifu.PKSw 105.3

  Upinzani ni sehemu ya maisha ya wote ambao Mungu anawatumia kuwasilisha ukweli wa leo mahsusi unaofaa kwa ajili ya wakati wao. Kulikuwepo ukweli wa leo katika siku za Luther,—ukweli wenye umuhimu maalumu ambao kwa wakati huo; kuna ukweli wa leo kwa ajili ya kanisa leo. Ye yote anayefanya mambo kulingana na mashauri na mapenzi ya Mungu amependezwa kuwaweka watu chini ya mazingira ya aina mbalimbali na kuweka majukumu maalumu kwa nyakati walizoishi na mazingira ambayo wamewekwa. Ikiwa wangethamini nuru waliyopewa, mitazamo mipana zaidi ya ukweli ingefunguka mbele yao. Lakini siyo kweli kuwa watu wengi leo wanaupenda ukweli zaidi kuliko wafuasi wa upapa waliompinga Luther. Kuna mwelekeo ule ule wa kukubali nadharia na mapokeo ya watu badala ya neno la Mungu kama ilivyokuwa katika zama za kale. Wanaowakilisha ukweli kwa ajili ya wakati huu wasitegemee kupokelewa kwa furaha kubwa zaidi kuliko wanamatengenezo wa zama zilizopita. Pambano kuu kati ya ukweli na makosa, kati ya Kristo na Shetani, litazidi kuongezeka katika ukali wake hadi mwisho wa historia ya ulimwengu.PKSw 106.1

  Yesu aliwaambia wanafunzi Wake: “Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu” (Yohana 15:19, 20). Na kwa upande mwingine Bwana wetu alisema wazi: “Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo” (Luka 6:26). Roho ya kidunia haipatani na Roho ya Kristo leo kama ilivyokuwa nyakati za kale, na wale wanaohubiri neno la Mungu katika usafi wake hawawezi kupokelewa kirahisi zaidi sasa kuliko ilivyokwa nyakati zile. Miundo ya upinzani dhidi ya ukweli inaweza kubadilika, uadui unaweza usiwe wa wazi sana kwa sababu unaweza kuwa wa hila zaidi; lakini uhasama huo bado upo na utaendelea kuwepo mpaka mwisho wa wakati.PKSw 106.2

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents