Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Sura ya 28—Kukabiliana na Kumbukumbu za Maisha

  “Nikatazama,” anasema nabii Danieli, “hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa” (Daniel 7:9, 10).PKSw 366.1

  Hivyo ndivyo nabii Danieli alivyooneshwa katika njozi siku kuu na ya kutisha wakati tabia na maisha ya watu vitakapochunguzwa na Jaji Mkuu wa dunia yote, na kila mtu kulipwa “sawasawa na matendo yake.” Mzee wa Siku ni Mungu Baba. Anasema mwandishi wa Zaburi: “Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu” (Zaburi 90:2). Ni Yeye, aliye chanzo cha uhai, na chemchemi ya sheria, atakayekalia kiti cha hukumu. Na malaika kama wahudumu na mashahidi ambao idadi yao ni “maelfu elfu ..., na elfu kumi mara elfu kumi,” wanahudhuria mahakama kuu hii.PKSw 366.2

  “Na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe” (Danieli 7:13, 14). Ujio wa Kristo unaoelezwa hapa siyo ujio Wake wa pili duniani. Anakuja kwa Mzee wa Siku mbinguni apewe mamlaka na utukufu na ufalme, ambao atapewa mwisho wa kazi Yake kama mpatanishi. Ni ujio huu, ule uliotabiriwa katika unabii kuwa utatimizwa mwishoni mwa siku 2300 mwaka 1844, na siyo ujio Wake wa pili duniani. Akisindikizwa na malaika wa mbinguni, Kuhani wetu Mkuu anaingia patakatifu pa patakatifu na pale anakwenda mbele ya Mungu afanye kazi ya huduma Yake kwa ajili ya mwanadamu—kufanya kazi ya hukumu ya upelelezi na kufanya upatanisho kwa ajili ya wote wanaoonekana kuwa wanastahili kupata manufaa ya upatanisho.PKSw 366.3

  Katika huduma ya mfano wale tu waliokuja mbele ya Mungu wakiungama na kutubu, na ambao dhambi zao, kwa njia ya sadaka ya dhambi, zilihamishiwa katika chumba cha patakatifu, walikuwa na sehemu katika huduma ya Siku ya Upatanisho. Kwa hiyo, katika siku kuu ya upatanisho wa mwisho na hukumu ya upepelezi kesi zitakazoshughulikiwa zitakuwa zile tu za wanaodai kuwa watu wa Mungu. Hukumu ya waovu ni kazi ya pekee na inayojitegemea, na hutokea kipindi cha baadaye. “Kwa maana wakati umefika wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii injili ya Mungu utakuwaje?” (1 Petro 4:17).PKSw 366.4

  Vitabu vya kumbukumbu mbinguni, ambamo majina na matendo ya wanadamu yameandikwa, vitatumiwa kufanyia maamuzi ya hukumu. Nabii Danieli anasema: “Hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa.” Nabii wa Ufunuo, akieleza mandhari hiyo hiyo, anaongezea: “na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao” (Ufunuo 20:12).PKSw 367.1

  Kitabu cha uzima kina majina ya wote waliowahi kuingia katika huduma ya Mungu. Yesu aliwaagiza wanafunzi Wake: “Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni” (Luka 10:20). Paulo anazungumzia juu ya watenda kazi wenzake waaminifu, “ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima” (Wafilipi 4:3). Danieli, akitazama kwa mbali hata “wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo,” anaeleza kuwa watu wa Mungu wataokolewa, “kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.” Na nabii wa Ufunuo anasema kuwa wataingia katika jiji la Mungu wale tu ambao majina yao yameandikwa “katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo” (Danieli 12:1; Ufunuo 21:27).PKSw 367.2

  “Kitabu cha ukumbusho” kimeandikwa mbele ya Mungu, ambamo yameandikwa matendo mema “ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake” (Malaki 3:16). Maneno yao ya imani, matendo yao ya upendo, yameandikwa mbinguni. Nehemia anaeleza jambo hili anaposema: “Unikumbukie hayo, Ee Mungu wangu, wala usifute fadhili zangu nilizozitenda kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu” (Nehemia 13:14). Katika kitabu cha Mungu cha kumbukumbu kila tendo la haki limeandikwa. Pale, kila jaribu lililopingwa, kila uovu ulioshindwa, kila neno la huruma na upendo lililotamkwa, linaandikwa kwa uaminifu. Na kila tendo la kujitoa kafara, kila teso na huzuni iliyopitiwa kwa ajili ya Kristo, linaandikwa. Mwandishi wa zaburi anasema: “Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?)” (Zaburi 56:8).PKSw 367.3

  Kuna kumbukumbu pia ya dhambi za watu. “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.” “Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.” Mwokozi anasema: “Kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa” (Mhubiri 12:14; Mathayo 12:36, 37). Makusudi na nia ya siri vinaonekana katika kitabu cha kumbukumbu kisichokosea; kwa kuwa Mungu “atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo” (1 Wakorintho 4:5). “Tazama, neno hili limeandikwa mbele zangu....maovu yenu na maovu ya baba zenu pamoja, asema Bwana” (Isaya 65:6, 7).PKSw 367.4

  Kila kazi ya mtu inachunguzwa na Mungu na inaandikwa ama kama ni ya uaminifu au sio ya uaminifu. Mbele ya kila jina katika vitabu vya mbinguni pameandikwa kwa usahihi wa kutisha kila neno lisilo sahihi, kila tendo la ubinafsi, kila wajibu ambao haukutimizwa, na kila dhambi ya siri, na kila aina ya udanganyifu uliofichika. Maonyo yaliyotumwa kutoka mbinguni yakapuuzwa, muda uliopotezwa, fursa ambazo hazikufanyiwa kazi, mvuto uliohamasisha wema au uliochochea uovu, pamoja na matokeo yake mapana, yote yameandikwa na malaika anayetunza kumbukumbu.PKSw 368.1

  Sheria ya Mungu ndicho kiwango kitakachotumika kupima tabia na maisha ya watu katika hukumu. Alisema mtu mwenye hekima: “Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu; Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi” (Mhubiri 12:13, 14). Mtume Yakobo anawaonya ndugu zake: “Semeni ninyi, na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ya uhuru” (Yakobo 2:12).PKSw 368.2

  Wale ambao katika hukumu wanahesabiwa “kuwa wamestahili” watakuwa na sehemu katika ufufuo wa wenye haki. Yesu alisema: “Wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, ... huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo” (Luka 20:35, 36). Na tena anasema kuwa “wale waliofanya mema” watatoka “kwa ufufuo wa uzima” (Yohana 5:29). Wenye haki waliokufa hawatafufuliwa mpaka baada ya hukumu ambayo kwayo wamehesabiwa kuwa wamestahili “ufufuo wa uzima.” Kwa hiyo hawatakuwepo mahakamani kimwili wakati kumbukumbu zao zikichunguzwa na kesi zao zikiamriwa.PKSw 368.3

  Yesu atakuwepo kama wakili wao, akiomba na kusihi kwa ajili yao mbele za Mungu. “Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki” (1 Yohana 2:1). “Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu.” “Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee” (Waebrania 9:24; 7:25).PKSw 368.4

  Vitabu vya kumbukumbu vilifunguliwa katika hukumu, maisha ya wote waliomwamini Yesu vilichunguzwa mbele za Mungu. Uchunguzi ukianza na watu wa kwanza kuishi duniani, Wakili wetu anawasilisha kesi za kizazi baada ya kizazi, na anamalizia na walio hai. Kila jina linatajwa, kila kesi inachunguzwa kwa makini. Majina mengine yanakubaliwa, na majina mengine yanakataliwa. Ikiwa jina lo lote lina dhambi ambazo bado zimebaki katika vitabu vya kumbukumbu, ambazo mhusika hajazitubu na kusamehewa, majina yao yanafutwa kutoka katika kitabu cha uzima, na kumbukumbu ya matendo mema yanafutwa kutoka katika kitabu cha ukumbusho. Bwana alimwambia Musa: “Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu” (Kutoka 32:33). Na anasema nabii Ezekieli: “Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, .... matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo” (Ezekieli 18:24).PKSw 368.5

  Wote ambao wametubu dhambi kweli kweli, na kwa imani wakadai damu ya Kristo kuwa kafara yao ya upatanisho, msamaha huingizwa mbele ya majina yao katika vitabu vya mbinguni; kwa kuwa wamekuwa washirika wa haki ya Kristo, na tabia zao zinaonekana kupatana na sheria ya Mungu, dhambi zao zitafutwa kutoka katika vitabu, na wao watahesabiwa kuwa wanastahili uzima wa milele. Bwana anasema, kupitia kwa nabii Isaya: “Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako” (Isaya 43:25). Yesu alisema: “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.” “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni” (Ufunuo 3:5; Mathayo 10:32, 33).PKSw 369.1

  Shauku kubwa inayooneshwa miongoni mwa wanadamu katika maamuzi ya mahakama za kidunia inawakilisha japo kwa uhafifu shauku inayodhihirishwa katika mahakama ya mbinguni wakati majina yaliyoingizwa katika kitabu cha uzima yanapoletwa kuchunguzwa na Jaji Mkuu wa dunia yote. Mwombezi wa Kimungu anawasilisha ombi kuwa wote walioshinda kwa njia ya imani katika damu Yake wasamehewe dhambi zao, kuwa warudishwe katika nyumba yao ya Edeni, na wavikwe taji kama warithi pamoja Naye wa “mamlaka ya kwanza” (Mika 4:8). Shetani katika juhudi zake za kudanganya na kujaribu wanadamu alikusudia kuharibu mpango wa Kimungu wa kumuumba mwanadamu; lakini Kristo sasa anaomba kuwa mpango huu utekelezwe kana kwamba mwanadamu hajawahi kuanguka. Anaomba kwa ajili ya watu Wake siyo tu msamaha na kuhesabiwa haki, kuliko kamili na kamilifu, bali pia wapewe sehemu ya utukufu Wake na waketishwe katika kiti Chake cha enzi.PKSw 369.2

  Wakati Yesu akiwaombea wanufaikaji wa neema yake, Shetani anawashitaki mbele za Mungu kama wakosaji. Mdanganyaji mkuu alitafuta kuwaingiza katika mashaka, kuwafanya wamshuku Mungu, ili wajitenge na upendo Wake, na wavunje sheria Yake. Sasa anaonesha kumbukumbu za maisha yao, anawaonesha dosari katika tabia zao, jinsi wasivyofanana na Kristo, ambako kumemwaibisha Mkombozi wao, anawaonesha dhambi zote alizowashawishi kuzitenda, na kwa sababu ya hizo dhambi anadai kuwa ni watu wake.PKSw 369.3

  Yesu hatoi udhuru kwa ajili ya dhambi zao, bali anaonesha toba na imani yao, na, anadai msamaha kwa ajili yao, ananyosha juu mikono Yake iliyojeruhiwa mbele ya Baba na malaika, akisema: nawajua kwa majina yao. Nimewachora juu ya viganja vya mikono Yangu. “Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau” (Zaburi 51:17). Na kwa mshitaki wa watu Wake anasema: “Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni?” (Zekaria 3:2). Kristo aliwavika watu Wake waaminifu kwa haki Yake, ili awawasilishe kwa Baba Yake kama “Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa” (Waefeso 5:27). Majina yao yamebaki yakiwa yameandikwa katika kitabu cha uzima, na kuhusiana nao imeandikwa: “Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili” (Ufunuo 3:4).PKSw 370.1

  Kwa njia hiyo itatimia kikamilifu ahadi ya agano: “Nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.” “Katika siku hizo na wakati huo, asema Bwana, uovu wa Israeli utatafutwa, wala uovu hapana; na dhambi za Yuda zitatafutwa, wala hazitaonekana” (Yeremia 31:34; 50:20). “Siku hiyo chipukizi la Bwana litakuwa zuri, lenye utukufu, na matunda ya nchi yatakuwa mema sana, na kupendeza, kwa ajili ya Waisraeli wale waliookoka. Tena itakuwa ya kwamba yeye aliyebaki katika Sayuni, na yeye aliyeachwa ndani ya Yerusalemu, ataitwa mtakatifu; yaani, kila mmoja aliyeandikwa miongoni mwa hao walio hai ndani ya Yerusalemu” (Isaya 4:2, 3).PKSw 370.2

  Kazi ya hukumu ya upelelezi na utakasaji wa dhambi inapaswa kutekelezwa kabla ya ujio wa pili wa Bwana. Kwa kuwa watu waliokufa wanahukumiwa kutokana na mambo yaliyoandikwa katika vitabu, haiwezekani kuwa dhambi zao zifutwe mpaka baada ya hukumu ambapo kesi zao zinachunguzwa. Lakini mtume Petro anasema wazi kuwa dhambi za waaminio zitafutwa “nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo” (Matendo 3:19, 20). Wakati hukumu ya upelelezi itakapofungwa, Kristo atakuja, na ujira Wake utakuwa pamoja Naye kumlipa kila mmoja sawasawa na matendo yake.PKSw 370.3

  Katika huduma ya mfano kuhani mkuu, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli, alitoka nje kuwabariki watu. Kadhalika Kristo, mwishoni mwa kazi Yake kama mwombezi, atatokea, “pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu” (Waebrania 9:28), kuwabariki watu Wake kwa uzima wa milele. Kama kuhani, kwa kuondoa dhambi kutoka katika hema, aliziungama juu ya kichwa cha mbuzi wa Azazeli, kadhalika Kristo ataweka dhambi zote juu ya Shetani, mwanzilishi na mchochezi wa dhambi. Mbuzi wa Azazeli, akiwa amebeba dhambi za Israeli, alipelekwa mbali “mpaka nchi isiyo watu” (Walawi 16:22); kadhalika Shetani, akiwa amebeba hatia ya dhambi zote alizosababisha watu kuzitenda, atafungwa kwa miaka elfu moja duniani, ambayo wakati huo itakuwa ukiwa, bila watu, na mwishowe atapewa adhabu ya mwisho ya dhambi katika moto ambao utawaangamiza waovu wote. Hivyo, mpango mkuu wa ukombozi utafikia ukamilifu wake kwa kuondoa kabisa dhambi na kwa wokovu wa wote waliochagua kuachana na uovu.PKSw 370.4

  Wakati uliopangwa wa hukumu—mwishoni mwa siku 2300, mwaka 1844—ilianza kazi ya upepelezi na utakaso wa dhambi. Wote waliowahi kubeba jina la Kristo itawapasa kupita katika uchunguzi wa kina wa hukumu ya upelelezi. Walio hai na waliokufa watapaswa kuhukumiwa “katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.”PKSw 371.1

  Dhambi ambazo hazikuungamwa na kuachwa hazitasamehewa wala kufutwa katika vitabu vya kumbukumbu, lakini zitasimama na kutoa ushuhuda dhidi ya mwenye dhambi katika siku ya Mungu. Anaweza kuwa alizitenda wakati wa nuru ya mchana au katika giza la usiku; lakini zilikuwa wazi na dhahiri mbele Yake Yeye tunayewajibika Kwake. Malaika wa Mungu walishuhudia kila dhambi na waliiandika katika kumbukumbu zisizokosea. Dhambi inaweza kufichwa, kukanwa, kufunikwa isionwe na baba, mama, mke, watoto, na marafiki; hakuna mtu mmoja isipokuwa mwenye hatia anayeweza kuwa na mashaka kuhusu dhambi hiyo; lakini iko wazi mbele za wenye akili wa mbinguni. Giza la usiku wenye giza totoro, usiri wa sanaa zote za udanganyifu, halitoshi kuficha wazo hata moja lisijulikane kwa Yule aliyepo milele zote. Mungu anayo kumbukumbu sahihi ya kila taarifa isiyo ya haki na kila tendo la uonevu. Hadanganywi na mwonekano wa utakatifu. Hafanyi makosa katika tathmini Yake ya tabia. Watu wanaweza kudanganywa na wale walio mioyo miovu, lakini Mungu anapenya mionekano yote na kusoma maisha ya ndani.PKSw 371.2

  Wazo hilo linatisha kiasi gani! Siku baada ya siku, hadi katika umilele, linabeba mzigo wake wa kumbukumbu za mbinguni. Maneno yanapotamkwa mara moja, matendo yakitendwa mara moja, hayawezi kukumbukwa. Malaika wameandika mema na mabaya. Mshindi mwenye nguvu kuliko wote duniani hawezi kurudisha kumbukumbu hata za siku moja. Matendo yetu, maneno yetu, hata nia zetu za sirini kabisa, yote yana uzito katika kuamua hatima yetu kwa wema kwa ubaya. Hata kama tutakuwa tumeyasahau, yatatoa ushahidi wao kututhibitisha au kutuhukumu.PKSw 371.3

  Kama vile alama za usoni zinavyonakiliwa kwa usahihi usiokosea kwenye bamba lililong'arishwa la mchoraji, kadhalika tabia imenakiliwa kwa uaminifu katika vitabu vya mbinguni. Ni kujali kidogo kiasi gani kunahisiwa kuhusiana na kumbukumbu ambazo inapasa zichunguzwe na wenye uhai wa mbinguni. Ikiwa pazia linalotenganisha ulimwengu unaoonekana na usioonekana lingeondolewa, na wanadamu wamwone malaika akiandika kila neno na tendo, ambalo itawapasa kukutana nalo katika hukumu, ni maneno mangapi ambayo yanasemwa kila siku yangebaki bila kusemwa, na ni matendo mangapi yangebaki bila kutendwa.PKSw 372.1

  Katika hukumu, uchunguzi utafanywa kuhusiana na jinsi kila talanta ilivyotumika. Tumetumiaje mtaji tuliokopeshwa na Mbingu? Bwana atakaporudi atapata iliyo yake pamoja na faida? Tumeboresha uwezo tuliodhaminiwa, katika mkono na moyo na akili, kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kwa ajili ya kuubariki ulimwengu? Tumetumiaje muda wetu, kalamu zetu, sauti zetu, pesa zetu, na mvuto wetu? Tumemfanyia nini Kristo, katika kuwahudumia maskini, yatima na wajane? Mungu ametufanya kuwa wahifadhi wa neno Lake takatifu; tumefanya nini na nuru na ukweli tuliopewa kuwafanya watu wawe na hekima kwa ajili ya wokovu? Hakuna thamani yo yote imeambatanishwa na madai ya mdomo ya kuwa na imani katika Kristo peke yake; upendo ambao unadhihirishwa kwa vitendo ndio pekee unahesabiwa kuwa wa dhati. Lakini ni upendo pekee mbele za Mbingu ambao unafanya tendo lolote liwe na thamani. Lo lote ambalo linatendwa kutokana na upendo, hata kama lingekuwa dogo kiasi gani katika tathmini ya kibinadamu, linakubaliwa na kuzawadiwa na Mungu.PKSw 372.2

  Uchoyo uliofichika wa wanadamu umefunuliwa katika vitabu vya mbinguni. Pale kuna kumbukumbu ya wajibu ambao haukutimizwa kwa wanadamu wenzao, ya usahaulifu wa madai ya Mwokozi. Pale wataona ni mara ngapi wakati, fikra, na nguvu ambazo ni mali ya Kristo vilitolewa kwa Shetani. Kumbukumbu ambazo malaika wanapeleka mbinguni ni za kuhuzunisha kiasi gani. Wenye uhai wenye akili, wanaotangaza kuwa wafuasi wa Kristo, wanajishughulisha zaidi na kukusanya mali za kidunia au kufurahia anasa za dunia. Pesa, wakati, na nguvu vinatolewa kafara kwa ajili ya kujionesha na kukidhi tamaa binafsi; lakini ni nyakati chache sana zinatumiwa kwa ajili ya maombi, kwa ajili ya kuchunguza Maandiko, kujinyenyekesha na kuungama dhambi.PKSw 372.3

  Shetani anagundua mipango isiyokuwa na idadi ya kushikilia akili zetu, ili zisijishughulishe na kazi ambayo tulipaswa kuifahamu vizuri kuliko kitu kingine cho chote. Mdanganyaji mkuu anachukia vipengele muhimu vya ukweli vinavyodhihirisha kafara ya upatanisho na mwombezi mwenye nguvu zote. Anajua kuwa kwake yeye kila kitu hutegemea kuelekeza akili za watu mbali na Yesu na ukweli Wake.PKSw 372.4

  Wale ambao wanapaswa kuwaeleza wengine manufaa ya upatanisho wa Mwokozi hawapaswi kuruhusu kitu chochote kuingilia wajibu wao wa kuwa na utakatifu kamili katika kicho cha Mungu. Saa za thamani, badala ya kutumiwa katika anasa, kujionesha, kutafuta mapato, zinapaswa kutumiwa usomaji wa neno la kweli kwa moyo wa dhati na kwa maombi mengi. Somo la patakatifu na hukumu ya upelelezi inapasa lieleweke kikamilifu kwa watu wa Mungu. Wote wanahitaji kujua wenyewe nafasi na kazi ya kuhani wao Mkuu. Vinginevyo haitawezekana kwao kufanyia mazoezi imani ambayo ni ya muhimu kwa wakati huu au kujaza nafasi ambayo Mungu amepanga waijaze. Kila mtu ana nafsi ya kuokoa au kupoteza. Kila mtu ana kesi inayomngoja katika mahakama ya Mungu. Kila mmoja inampasa kukutana na Jaji Mkuu uso kwa uso. Ni muhimu kiasi gani, hivyo basi, kuwa kila akili itafakari mara kwa mara mandhari ya kutisha wakati hukumu itakapokaa na vitabu vitakapofunguliwa, wakati, pamoja na Danieli, kila mtu atapaswa asimame katika kizimba chake, mwishoni mwa siku.PKSw 373.1

  Wote ambao wamepokea nuru juu ya masomo haya inawapasa kutoa ushuhuda wa ukweli mkuu ambao Mungu amewakabidhi. Patakatifu pa mbinguni ndiyo kituo mahsusi cha kazi ya Kristo kwa ajili ya wanadamu. Panaihusu kila nafsi inayoishi duniani. Panafunua mpango wa ukombozi, pakituleta karibu kabisa na mwisho wa wakati na pakifunua suala la ushindi wa pambano kati ya haki na dhambi. Ni suala muhimu sana kuwa wote wajifunze masomo haya na waweze kumjibu kila mtu awaulizaye sababu ya tumaini lililoko ndani yao.PKSw 373.2

  Maombezi ya Kristo kwa ajili ya mwanadamu ndani ya patakatifu pa mbinguni ni muhimu sana kwa ajili ya mpango wa wokovu kama kifo Chake msalabani kilivyo muhimu. Kwa kifo Chake alianza kazi ambayo baada ya ufufuo Wake alipaa kumalizia mbinguni. Inatupasa kwa imani kuingia ndani ya pazia, “alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu” (Waebrania 6:20). Mle nuru kutoka kwenye msalaba wa Kalwari inaakisiwa. Mle tunaweza kupata uelewa wa wazi zaidi kuhusu siri za ukombozi. Wokovu wa mwanadamu unatekelezwa kwa gharama isiyokuwa na kikomo ya mbinguni; kafara iliyotolewa ni sawasawa na madai mapana ya sheria ya Mungu iliyovunjwa. Yesu amefungua njia ya kwenda kwenye kiti cha enzi cha Baba, na kwa njia ya upatanisho Wake, shauku ya dhati ya wote wanaokwenda Kwake kwa imani wanaweza kuwasilishwa kwa Mungu.PKSw 373.3

  “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema” (Mithali 28:13). Ikiwa wale wanaoficha na kutoa udhuru kwa ajili ya makosa yao wangeona jinsi Shetani anavyofurahia kwa ajili yao, jinsi anavyomsuta Kristo na malaika watakatifu kwa sababu ya ufichaji na udhuru wao huo, wangeharakisha kuungama dhambi zao na kuziacha. Kwa njia ya dosari katika tabia zao, Shetani anatenda kazi kutawala akili yote, na anajua kuwa ikiwa dosari hizi zitapaliliwa, atafaulu. Kwa hiyo anatafuta daima kuwadanganya wafuasi wa Kristo kwa hila zake zinazofisha kiasi ambacho haiwezekani wao wenyewe kushinda. Lakini Yesu anasihi kwa ajili yao kwa njia ya mikono Yake iliyojeruhiwa, mwili Wake uliochubuliwa; na anawaambia wafusi Wake: “Neema yangu yakutosha” (2 Wakorintho 12:9). “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:29, 30). Hivyo basi, asiwepo mtu anayechukulia kuwa dosari zake hazitibiki. Mungu atatoa imani na neema ili kuzishinda.PKSw 373.4

  Tunaishi sasa katika siku kuu ya upatanisho. Katika huduma ya mfano, wakati kuhani mkuu alipokuwa akifanya upatanisho kwa ajili ya Israeli, wote walitakiwa kutesa nafsi zao kwa toba na kujinyenyekesha mbele za Bwana, ili wasije wakaondolewa kutoka miongoni mwa watu. Hali kadhalika, wale wote ambao wanapenda kudumisha majina yao katika kitabu cha uzima inawapasa sasa, katika siku chache zilizosalia za rehema, kutesa nafsi zao mbele za Mungu kwa kuhuzunikia dhambi zao na kufanya toba ya kweli. Inapasa kujichunguza moyoni kwa kina na kwa uaminifu. Roho ya kurahisisha mambo ya kejeli inayoendekezwa na wengi wanaodai kuwa Wakristo inapaswa kuachwa. Kuna vita kali kabisa inayowakabili wote wanaojitahidi kudhibiti mielekeo ya uovu inayotaka kutawala nafsi. Kazi ya matayarisho ni kazi ya mtu mmoja mmoja binafsi. Hatuokolewi katika makundi. Usafi na uaminifu wa mtu mmoja hautafidia upungufu wa sifa hizi kwa mtu mwingine. Ingawa inapasa mataifa yote kupita katika hukumu ya Mungu, pamoja na hayo, atachunguza kesi ya mtu mmoja mmoja kwa karibu na kwa kina kana kwamba hakuna mtu mwingine duniani. Kila mmoja inapasa ajaribiwe na aonekane kuwa hana doa au kunyanzi au chochote cha aina hiyo.PKSw 374.1

  Mandhari zinazoambatana na kazi ya mwisho ya upatanisho zinatisha sana. Maslahi makubwa yanahusishwa na kazi hiyo. Hukumu inapita sasa katika patakatifu pa mbinguni. Kwa miaka mingi kazi hii imekuwa ikiendelea. Muda mfupi—hakuna anayejua ni muda mfupi kiasi gani— itahamia kwa kesi za walio hai. Mbele ya uwepo wa kutisha wa Mungu maisha yetu yanapaswa kupelekwa kwa ajili ya uchunguzi. Wakati huu juu ya nyakati zingine zote inapasa kila nafsi kuzingatia onyo la Yesu: “Angalieni, kesheni, ombeni, kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo” (Marko 13:33). “Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako” (Ufunuo 3:3).PKSw 374.2

  Wakati kazi ya hukumu ya upelelezi itakapofungwa, hatima ya wote itakuwa imeamriwa kwa ajili ya uzima au mauti. Rehema inafungwa muda mfupi kabla ya kuonekana kwa Bwana katika mawingu ya mbinguni. Kristo katika Ufunuo, akitazama mbele na kuuona wakati huu, alisema: “Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa. Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo” (Ufunuo 22:11, 12).PKSw 375.1

  Wenye haki na waovu watakuwa bado wakiishi duniani katika hali ya kufa—watu watakuwa wakipanda na kujenga, wakila na kunywa, wote bila kujua kuwa uamuzi wa mwisho, usiotenguliwa umekwisha kutangazwa katika patakatifu pa mbinguni. Kabla ya Gharika, baada ya Nuhu kuingia katika safina, Mungu alimfungia ndani na kuwafungia nje wasiomcha Mungu; lakini kwa siku saba watu, bila kujua kuwa maangamizi yao yamekwisha kupangwa, waliendelea na maisha yao ya kutokujali, ya kupenda anasa na waliendelea kudhihaki hukumu iliyokuwa mbele yao. “Ndivyo,” anasema Mwokozi, “kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu” (Mathayo 24:39). Kimya kimya, bila taarifa, kama mwizi wa usiku wa manane, itafika saa ile ya uamuzi ambayo itapanga hatima ya kila mtu, saa ya kuondolewa kabisa kwa fursa ya rehema kwa mwanadamu mwenye hatia.PKSw 375.2

  “Kesheni basi, ... asije akawasili ghafula akawakuta mmelala” (Marko 13:35, 36). Hali ya hatari inawakabili wale wote ambao, kwa kuchoka kukesha, wanageukia vivutio vilivyopo ulimwenguni. Wakati mfanya biashara amemezwa na utafutaji wa mapato, wakati mtafutaji wa anasa amezama katika tamaa zake, na wakati binti wa mitindo anapangilia mapambo yake—inawezekana katika saa ile Jaji Mkuu wa dunia yote akatangaza hukumu: “Umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka” (Daniel 5:27).PKSw 375.3

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents