Udanganyifu Mkuu
Aliyeahidi uzima pasipo utii alikuwa ndiye mdanganyifu mkuu. Na tamko la nyoka pale Edeni kuwa, “Hakika hamtakufa.”- Ilikuwa ndiyo hotuba ya kwanza kuwahi kuhubiriwa juu ya hali ya kutokufa kwa roho. Lakini tamko hili, likiwa na msingi wake katika mamlaka ya Shetani pekee, linasikika kutoka majukwaani na kupokelewa haraka na wanadamu wengi kama walivyofanya wazazi wetu wa kwanza. Kauli ya Mungu, “Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa” (Ezekieli 18:20), imegeuzwa kumaanisha kuwa, Roho itendayo dhambi, haitakufa, bali itaishi milele. Endapo mwanadamu baada ya anguko, angepewa uhuru wa kula kutoka kwenye mti wa uzima, dhambi ingekuwa imepata hali ya kutokufa. Lakini hakuna hata mmoja kutoka kwenye familia ya Adamu aliyeruhusiwa kula tunda liletalo uzima. Kwa hiyo hakuna mdhambi mwenye hali ya kutokufa.TK 328.2
Baada ya anguko, Shetani aliwataka malaika zake kufundisha imani juu ya hali ya asili ya mwanadamu ya kutokufa. Baada ya kuwashawishi watu kuupokea upotovu huu; walitakiwa kuwaongoza kwenye hitimisho kuwa mwenye dhambi angeishi milele katika mateso. Sasa mkuu wa giza anamwelezea Mungu kuwa ni dikteta mwenye kulipa kisasi, akitangaza kuwa Mungu, huwatumbukiza ndani ya jahannamu wote wasiompendeza na kwamba wanapoungua kwenye moto wa milele, Mwumbaji wao huwachungulia na kuridhika. Hivyo mdhalimu huyu mkuu, anamvisha mfadhili wa wanadamu tabia zake. Ukatili ni tabia ya kishetani. Mungu ni upendo. Shetani ni adui ambaye anawashawishi wanadamu kutenda dhambi na kisha akiweza, anawaangamiza. Ni Mgongano ulioje kati ya upendo, rehema, na haki; na fundisho linalodai kuwa waovu waliokufa wanateseka kwenye moto wa milele na kwamba kwa dhambi walizotenda katika maisha haya mafupi hapa duniani, wataendelea kuteseka kwa kadiri Mungu aishivyo!TK 328.3
Je, fundisho hili linapatikana wapi ndani ya Neno la Mungu? Je, hisia za ubinadamu wa kawaida zigeuke kuwa ukatili na ushenzi? Hasha, hilo siyo fundisho la kitabu cha Mungu. “Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa.” Ezekieli 33:11TK 329.1
Je, Mungu anafurahia kuyaangalia mateso yasiyokoma? Je, anaburudishwana sauti za maumivu na vilio vya viumbe wanaoteseka ambao anawashikilia katika miali ya moto? Je, sauti hizi za kuchukiza zaweza kuwa wimbo katika sikio la Mungu mwenye upendo usio na mwisho? Oh! kufuru ya kutisha! Utukufu wa Mungu hauongezwi kwa kudumisha dhambi katika muda usio na mwisho.TK 329.2