Hati ya Usalama Kutoka kwa Mfalme
Katika barua aliyowaandikia rafiki zake alisema: “Ndugu zangu,...Ninaondoka nikiwa na hati ya usalama toka kwa mfalme ili nikakutane na maadui zangu walio wengi na ambao ni wanadamu tu....Yesu Kristo aliteseka kwa ajili ya wapendwa wake; kwa hiyo, kwa nini tushangae kwamba ametuachia mfano wake?... Kwa hiyo, wapendwa, kama kifo changu kitaongeza utukufu wake, ombeni ili kije upesi, na pia aniwezeshe kukabili majanga yangu yote nikiwa thabiti.... Hebu tumuombe Mungu...ili nisizuie hata chembe ya ukweli wa Injili, ili niwaachie ndugu zangu mfano ulio bora wa kufuata.” TK 67.2
Katika waraka mwingine, Huss alinena kwa unyenyekevu juu ya makosa yake mwenyewe, akijilaumu “kwa kujisikia fahari katika kuvalia mavazi ya kitajiri na kwa kupoteza saa nyingi kwenye shughuli za kipuuzi.” Kisha aliongezea, “hebu utukufu wa Mungu na wokovu wa roho ujaze mawazo, na wala isiwe kuwa na vyeo na makazi. Jihadhari na upambaji wa nyumba yako kuliko roho yako: na zaidi ya vyote, wekeza ulivyo navyo katika majengo ya kiroho. Uwe mchaji wa Mungu na mnyenyekevu kwa maskini, na usitumie raslimali zako katika karamu.” TK 67.3
Kule Constance, Huss alipewa uhuru kamili. Zaidi ya hati ya usalama aliyopewa na mfalme, aliongezewa uhakika kwake binafsi wa ulinzi kutoka kwa Papa. Lakini, kwa namna iliyokuwa ya kukiuka matamko haya yaliyorudiwa, Mwana matengenezo alikamatwa baada ya muda mfupi kutokana na amri ya Papa na makadinali na akatupwa kwenye gereza la ardhini lenye kuchukiza mno. Baadaye alihamishiwa kwenye ngome iliyokuwa ng’ambo ya mto Rhine na pale akatunzwa kama mfungwa. Muda si mrefu Papa naye alitiwa kwenye gereza hilo hilo. Alikuwa ameonekana kuwa na hatia ya makosa mabaya sana, kando ya mauaji, kuuza vitu vilivyowekwa wakfu na uzinzi, “dhambi ambazo hazikustahili kutajwa.” Hatimaye alinyang’anywa ile taji. Mapapa waliopingana pia waliondoshwa madarakani, na Papa mpya akachaguliwa.TK 68.1
Ingawa Papa mwenyewe alikuwa na hatia ya uhalifu mkubwa zaidi ya ule wa Huss kuwashtaki mapadre, bado baraza lile lile ambalo lilimuondoa Papa liliendelea na kummaliza Mwanamatengenezo. Kufungwa kwa Huss kuliamsha ghadhabu kubwa sana Bohemia. Mfalme, kwa kutotaka kukiuka hati ya usalama, alipinga mashitaka kufanyika dhidi yake. Lakini maadui wa Mwanamatengenezo walileta hoja za kuthibitisha kwamba “sharti imani isitunzwe na wazushi, wala watu wanaoshukiwa kuwa na uzushi, ingawa wamepewa hati za usalama toka kwa watawala na wafalme.” TK 68.2
Kudhoofishwa na ugonjwa-unyevunyevu uliokuwa kwenye gereza la ardhini ulileta homa ambayo ilikaribia kumaliza maisha yake-Hatimaye Huss aliletwa mbele ya baraza. Akiwa na mzigo wa minyororo iliyomfunga, alisimama mbele ya mfalme, ambaye nia yake njema ilikuwa imetumika katika kumlinda. Bila kutetereka alisimamia ukweli na kuonesha upinzani mzito dhidi ya upotovu wa mamlaka ya Kanisa la Roma. Alipohitajika kuchagua kati ya kukana mafundisho yake au kuuawa, alikubali kifo cha ufia dini.TK 68.3
Neema ya Mungu ilimdumisha. Katika majuma ya kuteseka kabla ya kauli yake ya mwisho, amani ya mbinguni iliujaza moyo wake.TK 68.4
“Ninaandika barua hii,” alimwambia rafiki yake, “nikiwa gerezani kwangu, na mikono yangu ikiwa imefungwa, nikitegemea hukumu yangu ya kifo kesho.... Wakati ambapo, nikisaidiwa na Yesu Kristo, tutakutana tena kwenye amani iliyo tamu ya maisha yajayo, utajifunza jinsi ambavyo Mungu mwenye rehema amejionesha kwangu mimi, jinsi ambavyo amenisaidia wakati wa maonjo na majaribu yangu.” TK 69.1