Sura Ya 11 - Upinzani Wa Wakuu
Mojawapo ya shuhuda zenye kuvutia zilizowahi kutolewa kwa ajili ya Matengenezo; ni upinzani walioutoa wakuu wa waliokuwa Wakristo nchini Ujerumani kwenye mkutano mkuu wa dini uliofanyika Spires mnamo mwaka 1529. Ujasiri na uimara wa watu hao wa Mungu, ulivipatia vizazi vilivyofuata-uhuru wa dhamiri, na kulipatia kanisa la Wanamatengenezo jina-Uprotestanti.TK 128.1
Uwezo wa Mungu ulikuwa umezuia nguvu zilizokuwa zinapinga ukweli. Charles V alikuwa amekamia kuponda ponda Matengenezo, lakini mara alipokuwa akinyanyua mkono wake kufanya hivyo, Mungu alikuwa akimlazimisha kuligeuzia pigo lake upande mwingine. Mara kwa mara katika wakati wa hatari, majeshi ya Waturuki yalionekana mpakani, au mfalme wa Ufaransa, ama Papa mwenyewe, alifanya vita naye. Katikati ya machafuko na ghasia za mataifa, Matengenezo yaliendelea kuimarika na kupanuka.TK 128.2
Hata hivyo mwishowe, watawala wa ngazi za juu wa mamlaka ya Papa walifanya makubaliano na Wanamatengenezo. Mfalme aliitisha Mkutano Mkuu wa kidini kule Spires mnamo mwaka 1529 kwa kusudi la kuuangamiza “uasi wa kidini”. Endapo njia za amani zingeshindwa, Charles alikuwa amejiandaa kutumia upanga.TK 128.3
Kule Spires, wafuasi wa Kanisa la Papa walionesha waziwazi chuki yao dhidi ya Wanamatengenezo. Melanchthon alisema: “Sisi ni watu tunaochukiwa mno na tunaonekana kuwa takataka za ulimwengu; lakini Kristo atawaangalia watu wake walio maskini na kuwatunza.” Watu wa Spires walikuwa na kiu ya Neno la Mungu, bila kujali marufuku iliyokuwepo, maelfu walimiminika kwenye huduma zilizokuwa zikiendeshwa katika kanisa la mbunge wa Saksoni. Jambo hili liliiharakisha hali ya hatari. Taratibu juu ya uvumilivu wa kidini zilikuwa zimewekwa kisheria, na mataifa ya Kilnjili yaliamua kupinga kuingiliwa kwa haki zao. Luther hakuruhusiwa kuwepo kule Spires, lakini nafasi yake ilikuwa imejazwa na watendakazi wenzake pamoja na wakuu ambao Mungu alikuwa amewasimamisha ili kulinda kusudio Lake. Kifo kilikuwa kimemwondoa Frederick wa Saxony, lakini mrithi wake aliyekuwa anaitwa John alikuwa ameyakaribisha Matengenezo kwa moyo wa furaha na kwa ujasiri mkubwa.TK 128.4
Mapadre waliyataka mataifa yaliyokuwa yameyapokea Matengenezo kujisalimisha kwenye sheria za Kanisa la Roma. Kwa upande wao, Wanamatengenezo hawakuridhia kuwa Kanisa la Roma, liyatawale tena mataifa yaliyokuwa yamepokea Neno la Mungu.TK 129.1
Hatimaye ilipendekezwa kuwa kwenye maeneo ambayo Matengenezo yalikuwa hayajaanzishwa, Sheria ya Worms ingeendelea kutumika; na ya kwamba “endapo watu hawangekubaliana na sheria hiyo pasipo hatari za kutokea uasi, wasifanye mageuzi hata kidogo, ... wasipinge kuadhimishwa kwa misa, wasimruhusu Mkatoliki kuwa Mlutheri ” Uamuzi uliofanywa na mkutano huo, uliwaridhisha sana mapadre na maaskofu.TK 129.2
Endapo amri hii ingetekelezwa, “Matengenezo yasingeenea... na wala yasingeweza kujengwa kwenye misingi imara... ambamo tayari yalikuwa.” Uhuru ungepigwa marufuku. Kubadili dini kusingeruhusiwa. Matumaini ya ulimwengu yalionekana kutaka kuzimwa.TK 129.3
Upande wa Waprotestanti walitazamana kwa hofu wasijue la kufanya. “Nini kifanyike?” “Je, viongozi wa Matengenezo wajisalimishe na kukubaliana na agizo hilo?”...Wakuu wa Walutheri walikuwa wamehakikishiwa uhuru kwa shughuli za dini yao. Upendeleo wa aina hiyo hiyo ulikuwa umetolewa kwa watu wao, ambao kabla ya kupitishwa kwa uamuzi huo, walikuwa wamepokea ujumbe wa Matengenezo. “Je, jambo hili si la kuridhisha?”...TK 129.4
“Kwa furaha waliangalia kanuni iliyotumika kufikia mpango huu na walitenda kwa imani. Je, kanuni hiyo ilikuwa ni ipi? Ilikuwa ni haki ya Kanisa la Roma kushurutisha dhamiri na kuzuia maswali. Lakini je, haikuwa haki yao na watu wao waliokuwa Waprotestanti kuufurahia uhuru wa kidini? Ndiyo, ulikuwa upendeleo kama ilivyokuwa imesisitizwa katika mapatano, lakini si kama haki...Kukubaliwa kwa mapendekezo ya mapatano hayo ilikuwa ni kukiri ukweli kwa shingo upande ya kuwa uhuru wa dini ulikuwa unapaswa kuishia tu kwa Wanamatengenezo wa Saxony; lakini kwenye maeneo mengine yote ya Himaya ya Kikristo; kuuliza maswali kwa uhuru na kukiri imani ya Wanamatengenezo yalikuwa ni makosa ya jinai ambayo adhabu yake ilikuwa kutupwa kwenye gereza la chini ya ardhi ama kufungwa kwenye nguzo na kuchomwa moto. Je, wangeridhia kuwa uhuru wa dini uwe wa sehemu fulani tu?...Je, Wanamatengenezo wangekiri kwamba watu hawa hawakuwa na hatia ya damu za watu mamia kwa maelfu, ambao kwa kutaka kufikia makubliano haya walilazimika kutoa uhai wao katika nchi zilizokuwa chini ya mamlaka ya Papa?” TK 129.5
Viongozi hao walisema “Tulikatae agizo hili, katika masuala ya dhamiri uwingi hauna nguvu.” Kulinda uhuru wa dhamiri ni wajibu wa serikali, na huu ni mpaka wa mamlaka yake katika masuala ya dini.TK 130.1
Wakatoliki walikuwa wamedhamiria kukomesha kile walichokiita “ukaidi wa makusudi.” Wawakilishi wa miji iliyokuwa huru walitakiwa kutangaza ikiwa wangekubaliana na masharti yaliyokuwa yamependekezwa. Bila mafanikio waliomba jambo hili licheleweshwe. Karibu nusu nzima walikuwa upande wa Wanamatengenezo, wakifahamu kwamba msimamo wao huo ulikuwa unawaandaa kwa ajili ya mateso na shutuma za siku za usoni. Mmoja wao alisema, “Tunalazimika kulikana Neno la Mungu, ama- tuchomwe moto.” TK 130.2