Vijana Waliofundishwa Kuwa Wamisionari
Wakristo wa Kiwaldensia waliona kuwa walikuwa na wajibu nyeti wa kuangaza nuru yao. Kwa nguvu ya Neno la Mungu walitafuta njia ya kuondoa utumwa uliokuwa umeletwa na Kanisa la Roma. Iliwapasa wachungaji wa Wawaldensia kutumika kwa miaka mitatu katika maeneo ya kimisionari kabla ya kushika uongozi wa kanisa nyumbani. Hili lilikuwa zoezi murua kwa maisha ya wachungaji katika wakati ambapo roho za watu zilikuwa zinajaribiwa. Vijana hawakuwa wanaona utajiri na heshima ya kidunia mbele yao, bali walikuwa wanaona hatari na pengine kuuawa kwa ajili ya imani. Wamisionari walikuwa wanakwenda wawili wawili, kama Yesu alivyokuwa amewatuma wanafunzi wake.TK 48.2
Kutangaza kusudi lao kungefanya lisifanikiwe. Kila mchungaji alikuwa na ujuzi wa kazi au fani fulani, na wamisionari walifanya kazi zao kwa siri huku wakijulikana kama wafanyabiashara au wachuuzi.“Walibeba nguo za hariri, vito, na bidhaa nyingine, ... Na kule ambapo wangekataliwa kuingia kama wamisionari, walikuwa wanakaribishwa kama wafanyabiashara.” Walibeba nakala za Biblia kwa siri, wakati fulani Biblia yote au nusu yake. Mara kwa mara shauku ya kusoma Neno la Mungu ilikuwa inaamshwa, na sehemu za Biblia ziliachwa pamona na watu waliokuwa na nia. Wamisionari hawa, huku wakiwa pekupeku na mavazi yao yakiwa yamechakaa na kuchafuka safarini , walipita katika miji mikubwa na kupenya hadi nchi za mbali. Makanisa yalianzishwa njiani walimokuwa wakipita, na damu ya wafia dini ilikuwa inaushuhudia ukweli. Likiwa limefichwa na kimya kimya, Neno la Mungu lilikuwa likipokelewa kwa furaha katika nyumba na mioyo ya watu.TK 48.3
Wawaldensia walikuwa wanaamini kuwa mwisho wa mambo yote ulikuwa hauko mbali sana. Kadiri walivyoendelea kusoma Biblia waliifurahia sana kazi yao ya kuufanya wa Biblia ukweli unaookoa ujulikane kwa wengine. Walipata faraja, tumaini na amani katika kumwamini Yesu. Mioyo yao ilipoangaziwa nuru hii, walitamani kuiangaza miali yake kwa wale waliokuwa katika giza la uongo wa utawala wa Papa.TK 49.1
Chini ya uongozi wa Papa na mapadre, watu wengi walifundishwa kutegemea matendo yao kuwaokoa. Siku zote walikuwa wanajitumainia wenyewe, akili zao zikiwa zimezama katika hali yao ya dhambi, wakitaabisha roho na miili, lakini walikuwa hawapati nafuu. Maelfu walikuwa wanaishi maisha yao yote katika vyumba vya watawa. Kwa kufunga mara kwa mara na mapigo, kwa kukesha usiku, kwa kulala kifudifudi kwenye mawe ya baridi yaliyomwagiwa maji, kwa safari ndefu za hija—wakisumbuliwa na hofu juu ya ghadhabu ya Mungu ya kulipiza kisasi—wengi waliteseka, mpaka mwili uliochoka uliposhindwa kustahimili. Waliingia kaburini bila hata chembe ya matumaini.TK 49.2