Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Tumaini Kuu - Contents
 • Results
 • Related
 • Featured
No results found for: "".
 • Weighted Relevancy
 • Content Sequence
 • Relevancy
 • Earliest First
 • Latest First
  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents

  Kushuhudia Mtu Akichomwa Moto

  Siku moja alipokuwa ametembelea viwanja vya umma, Calvin alishuhudia “mwasi” mmoja akichomwa moto. Katikati ya mateso na kifo kiie cha kutisha chini ya laana ya kuogofya ya kanisa, mfia dini yule alidhihirisha imani na ujasiri aliokuwa nao. Yule kijana mwanafunzi aliona ukinzani kati ujasiri wa mfiadini na hali yake ya kuishi gizani na kukata tamaa. Alikuwa anafahamu ya kuwa “waasi” walikuwa wamejenga imani yao juu ya Biblia. Alidhamiria kuisoma ili agundue siri ya furaha yao.TK 142.1

  Ndani ya Biblia alikutana na Kristo. “Ooh Baba” alilalama, “Kafara yake imetuliza ghadhabu yako; damu yake imeondoa uchafu wangu; msalaba wake umechukua laana yangu; kifo chake kimefanya upatanisho kwa ajili yangu...Umeugusa moyo wangu ili niyaone mambo mengine kuwa ni machukizo isipokuwa matendo ya Yesu.” 138Martyn, vol. 3, ch. 13.TK 142.2

  Aliamua kuyatoa maisha yake kwa ajili ya Injili. Lakini, yeye kwa asili alikuwa mwoga na alitaka sana kwanza kujitoa kwa masomo. Hata hivyo, juhudi walizozifanya marafiki zake kumsihi, hatimaye zilimfanya kuridhia kuwa mhubiri. Maneno yake yalikuwa kama umande unaoshuka kuiburudisha dunia. Kwa wakati huu alikuwa kwenye mji wa jimbo lililokuwa chini ya uangalizi wa binti mfalme aliyekuwa anaitwa Margaret, huyu akiwa anaipenda Injili, aliwawekea ulinzi waliokuwa wahubiri wa Injili. Calvin alianza kazi yake katika nyumba za watu. Wale waliokuwa wameusikia ujumbe waliwaambia wengine habari njema. Alisonga mbele huku akiweka msingi wa makanisa ambayo yangekuja kuzalisha mashahidi wa ukweli wasioogopa.TK 142.3

  Paris ingepokea mwaliko mwingine wa kuipokea Injili. Mwito wa Lefevre na Farel ulikuwa umekataliwa, lakini ujumbe ungesikika tena kwa madaraja yote ya watu katika mji huo mkuu. Mfalme alikuwa hajajiunga kwa ukamilifu na Kanisa la Roma dhidi ya Matengenezo. Margaret aliamua ya kwamba imani ya matengenezo ihubiriwe kwenye mji wa Paris. Alimwamuru mchungaji wa Kiprotestanti kuhubiri kwenye makanisa. Ijapo jambo hili lilikuwa limekatazwa na wakuu wa utawala wa Papa, binti mfalme alifungua wazi milango ya ikulu. Ilitangazwa ya kuwa kila siku kutakuwepo na mahubiri, watu walialikwa kuhudhuria. Maelfu walikuwa wanakusanyika kila siku.TK 143.1

  Mfalme aliamuru kwamba mawili kati ya makanisa ya mji wa Paris yafunguliwe. Kamwe ilikuwa haijawahi kutokea mji ule kuguswa hivyo kwa Neno la Mungu. Kiasi, usafi wa moyo, utaratibu, na kufanya kazi kwa bidii vilikuwa vinachukua nafasi ya ulevi, uasherati, machafuko, na uvivu. Watu wengi waliipokea Injili, na wengi zaidi waliikataa. Wafuasi wa Kanisa la Roma walifanikiwa kuendelea kutawala. Makanisa yalifungwa tena, na nguzo ya kuchomea watu moto ilirudishwa tena mahali pake.TK 143.2

  Calvin alikuwa bado mjini Paris. Mwishowe watawala walinuia kumkamata ili akateketezwe kwenye moto. Hakuwa anafikiria juu ya hatari iliyokuwa inamjilia wakati marafiki zake walipokuja kwa haraka chumbani mwake na habari ya kuwa wakuu walikuwa njiani kuja kumkamata. Na papo hapo watu walibisha hodi kwa nguvu kwenye lango la kuingilia. Hakukuwa na muda wa kupoteza. Marafiki waliwachelewesha wale wakuu mlangoni, wakati wengine walimsaidia Mwanamatengenezo huyo kutokea dirishani, na aliharakisha kuelekea kwenye kijumba kidogo cha mfanyakazi mmoja aliyekuwa anapenda matengenezo. Alivaa mavazi ya mwenyeji wake ili kujificha asijulikane, akachukua jembe na kuliweka begani na kuanza safari yake. Alisafiri kuelekea upande wa kusini na kupata tena hifadhi kwenye milki ya Margaret.TK 143.3

  Calvin asingekaa bila kazi kwa muda mrefu. Mara tu dhoruba ilipopungua, alitafuta eneo jipya la kazi kule Poitiers, mahali ambapo mawazo mapya yalikuwa yamepokelewa. Watu wa daraja zote waliisikiliza Injili kwa furaha. Kwa kadiri idadi ya wasikilizaji ilivyozidi kuongezeka, ilifikiriwa kwamba ilikuwa salama zaidi kuwa wanakutana nje ya mji. Pango lililokuwa limezungukwa kwa miti na majabali lilikuwa mahali kamili pa faragha na lilichaguliwa kuwa sehemu ya kukutania. Katika eneo hili lililokuwa limejitenga, Biblia ilikuwa inasomwa na kufafanuliwa. Hapa ndipo meza ya Bwana ilipoadhimishwa kwa mara ya kwanza na Waprotestanti nchini Ufaransa. Kutoka kwenye kanisa hili dogo walnjilisti waaminifu kadhaa walitumwa kupeleka Injili.TK 143.4

  Kwa mara nyingine Calvin alirudi Paris, na kukuta karibu milango yote ya kazi imefungwa. Hatimaye aliamua kuondoka kwenda Ujerumani. Muda mfupi tu baada ya kuondoka kwake nchini Ufaransa, ghadhabu kali iliwakumba Waprotestanti. Wanamatengenezo wa Ufaransa waliamua kuupiga pigo mwenendo wa kishirikina wa Kanisa la Roma ambalo lingelishtua taifa lote. Kwa usiku mmoja, mabango yaliyokuwa yanashambulia misa yalibandikwa katika nchi yote ya Ufaransa. Vuguvugu hili lenye ari kubwa ambalo lilikuwa linaeleweka vibaya liliwafanya wafuasi wa Kanisa la Roma watoe sababu za kuhalalisha kuwaangamiza “waasi” kama wachochezi hatari dhidi ya ufalme na amani ya taifa.TK 144.1

  Moja ya mabango hayo lilibandikwa kwenye mlango wa chumba cha mfalme. Kitendo cha ujasiri usiokuwa kifani wa kuingiza matamko ya kushtusha mbele ya mfalme kulichochea ghadhabu yake. Hasira yake ilitamkwa kwenye maneno haya ya kutisha: “Na wakamatwe pasipo kujali hali zao wote wanaoshukiwa kuwa waasi wamfuatao Luther. Wote nitawaangamiza.” 139D’Aubigne, bk. 2, ch. 30. Mfalme alikuwa amedhamiria kujiweka kikamilifu katika upande wa Kanisa la Roma.TK 144.2

  Larger font
  Smaller font
  Copy
  Print
  Contents