Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Tumaini la Vizazi Vyote - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    65 — Hekalu Latakaswa Tena

    Mwanzoni mwa huduma yake, Kristo alikuwa amewafukuza hekaluni watu waliokuwa wakifanyia biashara yao batili hekaluni. Ujasiri na mwenendo wake mtakatifu viliwatia hofu wafanya biashara wenye hila.TVV 329.1

    Panapo mwisho wa huduma yake alikuja tena hekaluni akaona hali ya uchafuzi wa hekalu ingalipo kama hapo kwanza. Milio ya wanyama na kelele za ubadilishaji wa, fedha, na fujo ya kila aina vilifanyika humo. Wakuu wa hekalu ndio waliokuwa wenyewe, wakinunua na kuuza. Wao wenyewe ndio walikuwa wachoyo kabisa, wala mbele za Mungu hawakuwa na afadhali kupita watu wezi.TVV 329.2

    Kila wakati wa Pasaka na Sikukuu ya vibanda, wanyama maelfu walichinjwa, damu zao zilichukuliwa na makuhani na kumwagwa madhabahuni. Wayahudi walikuwa wamesahau umuhimu wa kuchinja wanyama hao kwamba ni kwa ajili ya dhambi. Hawakufahamu kwamba kuchinja wanyama ni mfano wa kumchinja Kristo kwa, ajili ya dhambi za ulimwengu.TVV 329.3

    Yesu aliona jinsi Wayahudi walivyofanya mikutano hii kuwa tamasha za kumwaga damu na ukatili. Walikuwa wamezidisha wanyama wa kafara kana kwamba Mungu hupendezwa na huduma za juu juu tu. Makuhani na watawala walizifanya kafara zinazoelekeza kwa Mwana Kondoo wa Mungu kuwa njia za kujipatia mapato. Kwa hiyo utakatifu wa kafara kwa kiasi kikubwa uliharibiwa kabisa. Yesu alijua kuwa damu yake ambayo karibu itamwagwa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, nayo ingehafifishwa na makuhani na wazee kama walivyofanya damu ya wanyama!TVV 329.4

    Kristo alikuwa amepinga matendo ya jinsi hii kupitia kwa manabii. Isaya, akiona kwa njozi Wayahudi walioasi aliwaambia. “Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? asema Bwana. Nimejaa mafuta ya kafara ya kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona, mimi siifurahii damu ya ng’ombe wala ya wana kondoo wala ya mbuzi waume. Jiosheni, jitakaseni, ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu.” Isaya 1:11-16.TVV 329.5

    Yeye aliyetoa unabii huu, sasa kwa mara ya mwisho anarudia maonyo haya. Katika utimizo wa unabii huu watu walikuwa wamemtangaza Yesu kuwa mfalme wa Israeli. Alikuwa amekubali heshima yao, na kukubali uteuzi wa kuwa mfalme. Katika tabia hii lazima atende. Alifahamu kuwa katika kujitahidi kuwarekebisha makuhani itakuwa kazi bure; Hata hivyo ushahidi wa utume wake mtakatifu lazima utolewe kwa taifa lisiloamini.TVV 330.1

    Mara hii tena mtazamo wa kutisha wa Yesu ulieneza ukumbi wote wa hekalu. Watu wote walimtazama. Uungu uliwaka kama umeme katika ubinadamu na kumwangaza, Kristo, kwa utukufu na heshima, ambavyo hakupatwa kuwa navyo kabla ya hapo. Watu waliokuwa karibu naye walisogea mbali kadiri ilivyowezekana. Alisimama peke yake isipokuwa wanafunzi wake wachache. Kukawa kimya kabisa. Kristo alizungumza kwa uwezo mkuu uliotikisa watu kama tufani; Akisema: “Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa ya sala, lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.” Sauti yake ilitoka kama tarumbeta ndani ya hekalu. “Yaondoeni haya ...” Yohana 2:16.TVV 330.2

    Miaka mitatu iliyopita wakuu wa hekalu walikuwa wameaibishwa na kukimbia kwao mbele ya agizo la Yesu. Hawakutaka tena hali yao ya kudhalilishwa kurudiwa tena mara ya pili. Walakini hata hivyo wakati huu waliogofishwa zaidi kuliko hapo kwanza, na wakaharakisha kutii amri yake. Makuhani na wenye biashara walikimbia na wakiwaswaga ng’ombe wao.TVV 330.3

    Walipokuwa njiani kutoka hekaluni, walikutana na watu wengi wakileta wagonjwa wao kwa Mganga Mkuu. Habari walizoambiwa na watu waliokimbizwa hekaluni ziliwaogopesha, hata wengine wakarudi, lakini kundi kubwa zaidi walisonga mbele wakitamani kumfikia. Mara ukumbi wa hekalu ulijaa watu wenye maradhi, na waliokuwa karibu kufa na Yesu akawahudumia wote.TVV 330.4

    Baada ya muda, makuhani na wakuu walithubutu tena kurudi hekaluni. Walikuwa wakidhani kuwa Yesu atatawazwa kuwa mfalme na kuchukua kiti cha Daudi. Walipoingia hekaluni walisimama hali wakiduwaa. Waliwaona wagonjwa wa kila aina wakiponywa, vipofu wakiona, vilema wakiruka kwa furaha, viziwi wakisikia na kadhalika. Watoto ndio waliokuwa wakishangilia zaidi. Yesu alikuwa amewaponya maradhi yao; na kuwakumbatia mikononi mwake. Na sasa wanamsifu kwa sauti zao za shangwe. Walirudia kuimba Hosana na kupunga matawi, kama walivyofanya siku ya jana yake.TVV 330.5

    Sauti za hawa wenye shangwe ziliwachukiza wakuu na waangalizi wa hekalu. Wakawaambia watu kuwa nyumba ya Mungu inadharauliwa sana kwa kelele za shangwe na mirukoruko ya furaha za watoto. Wakuu wakamwambia Kristo: “Husikii hayo yote?” Yesu akawaambia: “Je, hamjasoma kwamba: Kwa midomo ya watoto na kwa midomo ya wanyonyao utakamilisha sifa?” Unabii ulitabiri kuwa Kristo atatangazwa kama mfalme, na Mungu aliwainua watoto hawa wawe mashahidi wake. Kama sauti za watoto zingenyamaza kimya, nguzo za hekaluni zingemsifu Mwokozi.TVV 331.1

    Mafarisayo walifadhaishwa kabisa. Yesu alikuwa hajajichukulia mamlaka ya kifalme jinsi hivyo. Alikuwa ametenda maajabu, lakini kamwe, alikuwa hajatukuzwa kama wakati huo. Ingawa alikuwa amewachukiza na kuwafedhehesha makuhani na wakuu, lakini hawakufanya lo lote siku ile. Kesho yake tena baraza la Sanhedrin lilikutana ili lione nini cha kumtendea Yesu. Kwa miaka mitatu wakuu walishuhudia kuwa Yesu ni Masihi. Sasa hawakuwa na haja kutaka ishara, ila walitaka akiri au kutamka ili wapate sababu ya kumkamata na kumhukumu.TVV 331.2

    Ndani ya hekalu walimwuliza: “Unafanya haya yote kwa uwezo gani? Nani amekuruhusu?” Yesu aliwakabili na majibu yenye masharti ya kujibu swali lake: “Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi, mbinguni au kwa wanadamu?”TVV 331.3

    Makuhani waliona kuwa wamo mtegoni. Kama wakisema kuwa ulitoka mbinguni, Yesu atawaambia: Mbona hamkumwamini? Yohana alishuhudia akisema: “Tazama Mwana Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” Yohana 1:29. Kama makuhani waliukubali ujumbe wa Yohana kwa hiyo wangewezaje kuukataa Umasihi wa Kristo?TVV 331.4

    Kama wangekubali kuwa ubatizo wa Yohana ulikuwa wa wanadamu, watajiamshia fujo na vita kutoka kwa makutano. Maana waliamini kuwa Yohana ni nabii. Watu walijua kuwa makuhani walimkiri Yohana kuwa nabii, na kukubali kuwa alitumwa na Mungu. Lakini baada ya kushauriana kwa siri, walikata shauri kujitosa wenyewe. Kwa unafiki wakidai hawafahamu, walisema “Hatujui.” Kristo naye alisema: “Hata mimi siwaambii kwamba kwa uwezo gani ninatenda haya.”TVV 331.5

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents